NILIWEKWA KIMADA NIKIWA NA MIAKA 12
Simulizi Ya Kweli
Chanzo: BBC
Hivi karibuni nilipita sehemu nikakutana na binti, ambaye hajafika umri wangu, anakunywa vinywaji vikali na sigara akiwa na mtoto mdogo hata mwaka mmoja hajatimiza.
Nilipomuita, akaniuliza kwa ukali ‘‘Wewe mbona unaniita hivyo wewe askari’’?, nilimwambia hapana mimi nimekupenda tu.
Nilimuuliza yeye amezaliwa mwaka gani akajibu mwaka 2001
Nilimjibu, ‘Ila haya unayopitia na mimi pia nilipitia ila haya si maisha’
Aliamua kunisikiliza na mara akaniambia ninakuja sasa hivi, nisiondoke ila ndiyo alikuwa amenikimbia.
Ninatamani sana maisha niliyopitia mimi, binti mwingine asipitie…niliumia sana lakini sikuwa na jinsi na katika mitaa yetu hii duni kuna vijana wengi wanapitia maisha haya, elimu niliyoipata ya maisha ya mtaani ninatamani kuitoa ili mtu mwingine asipite nilipopita…
Hayo ni maelezo ya mwanzo ya Elizabeth Paul Chitesya, mwenye umri wa miaka 29, anayeishi na maambukizi ya virusi vya UKIMWI kwa takribani miaka 10 sasa.
Mtu anayejipenda sana na kujivunia alivyo
Mimi ni mtoto wa tatu kuzaliwa katika familia yangu ambayo ilibahatika kupata watoto wanne ila wawili walifariki tumebaki watoto wawili wa kike.
Mimi ninajipenda sana na mtu ambaye ni mcha Mungu ingawa ninaweza kusema nilipotea na kuharibu ndoto zangu.
“Sijibrand ila mimi ni mtu ninajipenda sana na ninajivunia kuwa mimi,”.
Nilikuwa ninapenda sana kusoma na ningefanikiwa kumaliza shule nilikuwa natamani sana niwe mhudumu wa ndege ingawa shida nilikuwa naambiwa mimi ni mfupi sana hivyo hiyo kazi siwezi kuipata.
Uhudumu wa kwenye ndege ni kitu ambacho nilikuwa ninakipenda sana nikiona kwenye filamu, ingawa baba yangu alitamani niwe daktari maana hiyo sio kazi ya kupata pesa nyingi.
Baba yangu hakuwa mchoyo wa kunipeleka shule nzuri tu za gharama, lakini niliishia kidato cha tatu na ndoto zangu hazikutimia.
Kuanza maisha yasiyoeleweka katika umri wa miaka 12
Baba alinichukua nikiwa katika umri mdogo baada ya kuachana na mama yangu, akawa ananilea na mama mwingine.
Akili ya kijinga ilianzia nyumbani kipindi cha kuvunja ungo, ninakumbuka, baba yangu alikuwa mkali sana kuna siku alinipiga na pia akaninyoa nywele.
Nikiwa na umri wa miaka 12, kuna siku nilitumwa chakula katika baa na kuchelewa kurudi, hivyo niliogopa niliamua kurudi kwa muuzaji chips ambaye alikuwa rafiki wa baba anisaidie, ili nisichapwe.
Lakini kumbe yule baba alikuwa ananitamani kimapenzi hivyo badala yake aliniambia nisiende, nibaki palepale na mtu aliyetumwa kuja kuniulizia alimwambia sipo na baada ya hapo aliniambia niende kwenye gari yake anipeleke sehemu salama maana ningerudi nyumbani muda huo ningechapwa na akaniambia angeweza hata kuniua.
Alinipeleka kwa rafiki yake, Mikocheni kule ambako kuna nyumba kubwa ya kifahari alikuwa anakaa peke yake.
Aliniacha hapo akasema atakuja kunichukua baada ya siku mbili maana anatafuta nauli ili anipeleke Tanga, kwa kuwa baba yake anamtafuta na kuna mtu alimwambia alimuona nyumbani kwake.
Aliponipeleka Tanga, tukawa na mahusiano mimi na yeye.
Wakati huo nilikuwa mdogo hata mambo ya mahusiano sikuwa najua lakini niliona yule baba ndiye msaada wangu.
Aliniacha Tanga, nikae na ndugu yake ambapo huyo mdogo wake alikuwa ananitongoza pia. Sikuwa na simu na nilikuwa hata elimu ya msingi sijamaliza, maisha yalianza kuwa magumu tena.
Maisha yalikuwa magumu sana nikiwa Tanga, maana hata akituma pesa inafika kwa mdogo wake, hivyo hata kula yangu ilikuwa ngumu, nikaona bora nirudi nyumbani nikachapwe na baba maisha yaendelee.
Kuna siku niliomba dada mmoja kumpigia yule baba aliyenipeleka Tanga, nikamwambia anitumie pesa kwa namba ya huyo dada, hapo ikawa ndiyo niliponea.
Nilibahatika kutoroka kurejea Dar es Salaam ila nilipofika kituo cha basi nikakutana na jirani yetu aliyeniambia ninatafutwa sana mpaka kituo cha polisi.
Sasa niliposikia kituo cha polisi nikapata hofu, nikaogopa tena kurejea nyumbani.
Ila wakati ninajitafakari, kuna dada alikuja akaniambia, Nakumbuka alikuwa anaitwa Hawa, yeye alikuwa mkubwa kwangu, akaniambia niache ujinga kusoma hakulazimishwi, hivyo niende naye niwe rafiki yake.
Ila kumbe mwenzangu michezo ya kushiriki na wanaume ili kupata pesa alikuwa ameanza muda na nilikuwa sijawahi kufanya hiyo kazi ya kujiuza. Yule baba alikuwa ananishikashika tu ila hakuwahi kulala na mimi.
Ila nikiwa na Hawa, ilinichukua kama miezi mitatu ndiyo wazazi wangu walinipata. Niliporudi nyumbani, nilipelekwa polisi na mwisho nilimuomba baba anipeleke shule ya karibu na kwa mama huku Temeke eneo la Yombo dovya.
Nilifanya mtihani na kufaulu kidato cha kwanza, licha ya kutokuwa na cheti cha darasa la saba.
Hivyo nikaanza maisha mapya ya kukaa kwa mama nikawa nimehama Mbezi kwa baba.
Nilisoma vizuri kidato cha kwanza na cha pili, ila nilivyoingia kidato cha tatu nilianza maisha mengine kabisa ambayo naweza kusema hayakuwa maisha kabisa.
Hakuna mtu wa kumlaumu bali mimi mwenyewe
Nikiwa na umri wa miaka 15, nilijikuta nipo katika jinamizi la uraibu wa dawa za kulevya na kukatisha masomo yangu.
Kuiga ndiyo kunatuponza sana, uhuru na marafiki ndiyo kuliniponza na wakati huo nilikuwa nakaa na mama tu.
Nilianza na sigara, na hata shule yetu ilikuwa haina ukuta, nilikuwa nasifiwa nina akili na nilikaribishwa ili kuwa na marafiki.
Kidogo kidogo nikaanza na mimi nikaanza kuvuta bangi. Ulinzi ulikuwepo ingawa shule hizi za ndani ndani, ni ngumu sana. Mama alianza kuhoji mbona huli, unafifia na nikaanza kuwa mkali.
Juhudi za masomo zilipungua, mama alikuwa anaongea sana na mwisho shule nikaacha.
Baba alipunguza mahusiano na mimi kwa kuwa hakutaka nije kukaa huku Temeke.
Mama mlezi alikuwa mzuri tu tena sana ila ni mimi tu nilikuwa nataka kuja kwa mama yangu ili nipate uhuru. Sababu kubwa ya mimi kuacha shule ilikuwa ni makundi ya marafiki, siwezi kusema mtu yeyote yule kuwa chanzo cha mimi kufikia hapa.
Sijui nani aliniambukiza virusi vya UKIMWI
Niliona shule inanipotezea muda kabisa, bora nifanye mambo yangu.
Kilichonigharimu mimi ni uhuru na ujinga wangu binafsi.
Wengi sana tuliibomoa misingi, yani kama tungekuwa tunapanga maisha vizuri tusingepotea. Sijui hata aliyeniambukiza virusi vya UKIMWI ni nani.
Sijui kama nilipata wakati natumia dawa au wakati niliposhiriki ngono na mtu maana afya yangu ya akili haikuwa sawa.
Nilikuwa najiita ‘sista doo’ natamani kuwa fulani lakini nilianguka, ila pia hata sasa najivunia kuwa mimi na nashukuru nilipofika.
Unyanyapaa ni mwingi sana, mtu akikuona unakunywa dawa huwa watu wanakosesha amani. Mwanzoni nilikuwa natengwa hata nyumbani, hata wakati wa kula ila sasa ninajiamini.
Nimefanya hadi nyumbani sasa wananiona ni mmoja wao, tunaweza kula pamoja na sijihisi vibaya na kujihisi nguvu zaidi ya kusonga mbele kumlea mtoto wangu. Yaani nimefikia kipindi ambacho hata mtu akiongea, siumii kwa kuwa ni mimi na maneno ya watu hayawezi kuninyong’onyeza.
Mtoto wangu amekuwa mkombozi wangu.
Nina mtoto wa miaka minne ambaye, mimi ninafanya jukumu la baba na mama.
Ninashukuru binti yangu mwenye miaka minne ni mzima wa afya na anaendelea vizuri. Nilihakikisha ninafuata muongozo wote wa kumlinda mwanangu tangu nikiwa mjamzito na ninashukuru yuko vizuri.
Baba wa mtoto pia, nilimlinda maana hata sasa nikipata mwenza lazima nimjulishe hali yangu, maana sitaki kumuambukiza mtu yeyote kwa maksudi, mateso niliyopitia sitaki mwingine apitie.
Ila lazima nikiri kuwa mtoto wangu alinipa mwanga mpya wa kuishi maisha mapya na kutaka kufanikiwa kama wengine.
Baba yake alisema ‘tumuite siku ya kuzika’
Kutokana na mazingira aliyokuwa nayo ni kama siamini,
mwanzo kula, kuoga ilikuwa tatizo maana hata baba yake alimsusa alisema sitaki kumuona akifa mniambie nije kuzika.
Nilikuwa nawaza hivi mimi nimezaa nini? Nilikuwa najuta sana sana
Ninamshukuru Mungu tu kwa sasa, naweza kumuachia hata nyumba lakini zamani ilikuwa huwezi kumkaribia kabisa. Ninajiona nimepumzika sana sasa, maana maisha yangu yote ilikuwa ni kukimbizana mitaani na hospitalini, alisema Mama Elizabeth.

