Nilimsomesha Mrembo Chuo, Tazama Kilichotoea
Simulizi Ya Kweli
Siku ya kwanza kabisa nilimuona kanisani. Niseme tu macho yangu hayakutaka kuondoka kutoka kwake. Alikuwa mzuri, yaani kama ulikuwa unajiuliza maana ya uzuri, basi kama ungewahi kumuona hakika ungesema yeye ndiye uzuri wenyewe.
Alikuwa na lipsi nene kidogo, kifua chake kilikuwa saa sita. Alikuwa na makalio fulani ya uchochezi na hakuwa na tumbo kubwa kama lile ambalo wanawake wanaliita tummy.
Alikuwa na macho legevu, ilikuwa ni rahisi sana kusema alikuwa akikukonyeza pale alipokuwa akikuangalia. Hakuwa msichana mkubwa, kwa kukadiria, inawezekana alikuwa na miaka ishirini tu.
Hakika nilimpenda, nilisema ilikuwa bahati sana kumuona kwenye maisha yangu, hasa katika kipindi hiki ambacho nilikuwa natafuta mwanamke wa kuoa, nimuweke ndani, anizalie watoto, nimuite mama, naye aniite baba.
Sikutaka kulaza damu, ningewezaje hasa baada ya kumuona mwanamke kama huyu? Nikajisemea tu kwamba huyu naoa, ndiyo! Hakika nilitaka kumuona, nimueweke ndani, anipikie nile, anifulie, nimpe mapenzi na anipe zawadi nzuri ya mtoto.
Ibada ilikuwa inaendelea lakini mawazo yangu yalikuwa mbali kabisa. Nilikuwa nawaza ndoa na huyu msichana ambaye ndiyo ilikuwa mara ya kwanza kumuona katika maisha yangu. Nikasema sikubali, nitazungumza naye, nimzoee na mwisho wa siku nimwambie kwamba nilimpenda.
Nimwambie namtaka.
Nimwambie nataka awe mke wangu wa wa ndoa.
Muda wa sadaka ulipofika, nilitamani kumwambia nitakutolea mimi sadaka, yaani sikutaka atoe pesa yoyote ile, labda hiyo ingekuwa maana halisi ya kujali, kwamba hakutakiwa kupata shida na wakati mimi nipo. Hakutakiwa kutumia kitu chochote wakati mimi nipo.
Ibada ikaisha, nikasalimiana na watu wengine, nikaamua kumfuata mama yangu na kumwambia ibada ilikuwa imenoga sana na hatimaye Mungu amenionyesha mke wangu.
“Ni nani?”
Hilo swali nililoulizwa na mama ndilo lililonifanya nimuonyeshe. Akafurahi.
“Ooh! Anaitwa Esta.”
Nikamwambia ni kwa namna gani nilimpenda Esta. Kama kila siku alikuwa ananipigia kelele za oa oa oa, sasa nilikuwa tayari kuoa, na sikutaka kumuoa mwanamke yeyote zaidi ya Esta, yaani huyu esta tayari nilimuona akiwa mke wangu.
Kwa furaha mama akawafuata wazazi wa Esta na kuanza kuongea nao, sikujua alikuwa akiongea nao nini ila wote walionekana kuwa na furaha, walicheka mpaka meno ya mwisho kuonekana, mwisho wa siku nikaitwa, nikaenda na kuwasalimia kwa adabu.
Okay!
Kwa jina ninaitwa George. Mimi ni kijana niliyemalia masomo yangu ya biashara pale katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam miaka kadhaa nyuma na kwa kipindi hiki nilikuwa nafanya biashara zangu, nilikuwa na pesa, si pesa nyingi ila kwa maisha yetu haya ya ujanani, nilikuwa na pesa.
Basi hiyo ndiyo ilikuwa siku ya kwanza kumuona Esta. Aliitwa, tukaongea, nilitetemeka kwa hisia kali kama mtu anayepigwa na shoti ya umeme baada ya kumsalimia kwa kumgusa mkono wake.
Ulikuwa lainiiiiiiii.
Yaani kama alitoka kuzaliwa.
Akajitambulisha kwa jina hilo, alimaliza kidato cha sita na alikuwa akienda kujiunga na chuo. Nikajiambia nitasubiri. Kama niliweza kumsubiri mama kunileta duniani kwa miezi tisa, tena nikiwa siongei chochote kile, nitashindwaje kumsubiri Esta kwa miaka mitatu?
Nikasema nitasubiri.
Tena nitasubiri huku nikiwa na furaha.
Nikaanza kuzoeana na Esta, tukabadilishana namba za simu na kuanza kuwasiliana. Kwa kweli nilimpenda sana huyu msichana, niseme tena na tena kwamba nilimpenda sana.
Hakuwa ametoka kwenye familia yenye pesa, kwa maana hiyo hata ada ya chuoni kwao nikajipa jukumu kulipa, nikawa nalipia mpaka matumizi yake, yaani kwangu mimi niliona kama namlipia mke, mwanamke ambaye muda wowote ule baada ya kumaliza masomo basi tungefunga ndoa na kuwa mume na mke.
Penzi likaanza na kushamiri. Tukapendana sana. Nikawa nakwenda chuo kumsalimia, namtoa out na kuendelea kula maisha. Baada ya miezi kama minne hivi nikaamua kwenda kujitambulisha kwao.
Yaaap! Niliamua tu kufanya huo uamuzi wa kifala.
Nikajilipua.
Hakika ulikuwa ni wa kifala sana.
Sijui nilikuwa nimelewa.
Sijui nililogwa.
Labda mapenzi yalinilevya kishenzi.
Kila mmoja akafurahi na kisha nikampeleka Esta chuoni kwao, maisha yakaendelea. Kwa takribani kipindi hicho nadhani nilitumia zaidi ya milioni nane kwenye matumizi yake na mambo mengine.
Sikujali hata kidogo.
Baada ya kubakiza mwaka mmoja kabla ya kumaliza chuo ndipo hapo nilipoanza kuona kulikuwa na mambo hayapo sawa. Huyu Esta ni kama akawa bize sana. Ikawa hatuongei sana kama kipindi cha nyuma.
Nilipokuwa nataka kwenda chuo kumsalimia, akawa ananiambia yupo bize na masomo ya mwaka wa mwisho, hakutaka kupata sup. Nikawa namwambia sawa mama…nimekuelewa….nitakuja siku nyingine.
Sasa siku moja nikaamua kwenda tu chuoni kwao, sikutaka hata kutoa taarifa. Unajua kwa nini? Nilimwambia siku nyingi sana niende kumsalimia, hakutaka kwa kusema alikuwa bize. Sasa na mimi nilimmisi, nilimisi hata kumuona, ningefanya nini? Nikaenda.
Nilifika na kutulia kwenye kibanda fulani hivi cha juisi. Wakati nakunywa, kwa mbali nikamuona Esta akiwa anatembea na rafiki yake wa kike, alipendeza sana, yaani kwa siku hiyo alikuwa mzuri zaidi ya kipindi chote nilichowahi kumuona.
Sijui alikuwa zaidi ya mzuri ama nilikuwa nimemmisi tu. Nikasimama kwa lengo la kumuona, niliamini ingekuwa bonge la sapraizi kuniona mahali hapo.
Wakati nataka kumuita, ghafla nikamuona kijana fulani akiwasogelea, alipomfikia Esta, akamtekenya kwenye mbavu zake, Esta akashtuka, halafu akamgeukia kijana yule, wote wakacheka. Yaani alifurahia kitendo kile.
Moyo wangu ukachoma.
Ulichoma mno.
Nilihisi kama mtu alichukua kaa la mawe na kuliweka. Nikawa siamini nilichokuwa nakiona, baada ya hapo, wakashikana mikono. Walikuwa wakiongea, wakiangaliana kama njiwa waliokuwa wakipendana mno.
Esta alijibebisha kwa yule kijana, walivyoonekana, yaani walikuwa kwenye mapenzi ya kufa na kuzikana. Nikaamua kujikalia chini na kuwaangalia, walikuwa mbali kidogo hivyo hawakuniona.
“Ngoja nimpigie simu.”
Nilijisemea na kufanya hivyo, ikaanza kuita, Esta akaichukua simu yake, akaangalia kioo kisha kuirudisha kwenye mkoba wake. Yaani aliipuuzia simu yangu kuipokea na wakati hata simu aliyokuwa akiitumia ilikuwa yangu.
Nikaamua kuwapiga picha za ushahidi, nilitaka kuwa na kila kitu kukiwa na ushahidi wa kutosha. Nikaondoka zangu.
Miaka ya nyuma nilikuwa nawaashangaa sana watu waliokuwa wakijimaliza kisa mapenzi. Yaani unajimaliza vipi na wakati kulikuwa na wanawake, wanaume kibao? Ukiachwa na huyu si unamfuata mwingine na maisha yanaendelea?
Sasa kwa wakati huo wal watu niliona wakiwa wanafanya mambo sahihi kabisa, nilichokifikiria? Na mimi kujimaliza tu.
Yaani kwa ajili ya mapenzi, nikataka kuitoa roho yangu. Sikutaka kushauriwa na yeyote yule, yaani hata kama Yesu angeshuka, akanipa ushauri wake mwingiiii, ningemsikiliza, halafu baada ya kupoteza dakika zake, ningekwenda kununua kamba na kujimaliza.
Yaani nilidhamiria.
Nilitaka niondokane na aibu hii.
Nirudi kwa Mungu muumba.
Nimwache Esta atanue na mwanaume wake wapendavyo.
Itaendelea.


1 Comment
I would like to thank you for the efforts you’ve put in writing this blog. I’m hoping the same high-grade website post from you in the upcoming also. Actually your creative writing abilities has encouraged me to get my own site now. Really the blogging is spreading its wings fast. Your write up is a great example of it.