𝗠𝗔𝗟𝗜𝗣𝗢 𝗞𝗜𝗧𝗔𝗡𝗗𝗔𝗡𝗜
ONYO: Wakubwa tu, kuanzia Miaka 18, ndio wasome hii Hadithi
EP 7
Zilipita siku kama tano hivi, bado Mr Erick alikuwa haeleweki kutaka kumsaidia mkewe aweze kupata hiyo kazi, Erick alionekana mwenye kuwa na wivu na mkewe, kwa sababu tu alikuwa ameshajua kuwa mke wake alikuwa akitoka na Amidu kwa siri kabla ya Amidu kufariki.
Aneth akiwa amejilaza kitandani alisikia simu yake ikiita, akaitazama, Haidali ndiye alikuwa akimpigia simu, binti akaipokea na kuongea
“Haidali” alisema mwanamke huyo
“Kwema Aneth?”
“Kwema vipi hali yako?”
“Salama kabisa, sasa inakuwaje?”
“Kuhusu nini tena?” aliuliza Aneth
“Tuliongea nini? Naomba kesho jumapili tuonane maana jumatatu ndio tunatoa yale majina, hivyo jitahidi uje ili tuongee kuhusu ule mpango basi” alisema
“Sawa” binti aliongea
“Poa”
Haidali alikata simu yake ndipo binti akafikiria sekunde chache akampigia “Haidali samahani, kwani hatuwezi tu kuongea kwenye simu?”
“Amh,….unajua tatizo hapa nipo mwenyewe na dili hili ni la watu watatu, yaani wale tuliokoufanyia interview wote tunatakiwa tuwepo”
“Sawa…kwani mnahitaji kiasi gani?” aliuliza binti
“Sio pesa nyingi, we njoo najua hatutashindwana”
“No bora uniambie ili kama sitaweza nisiwapotezee muda wenu”
“Usijali kuhusu hilo wee njoo”
“Mh haya poa nitakupa taarifa asubuhi”
“Ok”
Aneth alikata simu akabaki ana mawazo tele, hakuwa na cha kufanya zaidi ya kusubiri kesho. Mkononi alikuwa na laki mbili tu ndiyo alikuwa amejikusanya na hakujua kama itaweza kumtosha yeye kupata kazi, aliogopa.
Erick asingetaka kumsaidia, na vile vile Erick hakutaka mkewe afanye kazi ya kuajiriwa, licha ya kumruhusu yeye kuenda katika interview wiki moja iliyokuwa imepita
Kwa kuwa vijana waliojiajiri wengi na wenye ndoto za kuzidi kushika pesa nyingi huwa hawana mapumziko hata kama ni wikiendi, basi Erick siku ya jumapili aliamka mapema asubuhi, akaenda kanisani misa ya kwanza kabisa..
Kanisani alikuwa na ubavu wake, yaani Aneth, na walipomaliza ibada alimuarakisha “Panda gari nikupeleke nyumbani maana ninataka kuwahi kule ofisini” alisema
“Usijal kama vipi wewe nenda mimi nitapanda tu pikipiki” alisema Aneth, ikiwa nia yake ni kutokurudi nyumbani, yaani aelekee moja kwa moja kuonana na Haidali
“No panda twende, hujui una kiumbe tumboni, ya nini kurushwa rushwa na bodaboda jinsi walivyo na fujo”
“Ah” binti alibetua mdomo na kusogea kwenye gari la mumewe kisha akafungua mlango na kuzama ndani ndipo safari ikaanza ya kuondoka kuelekea nyumbani kwao
Erick aliendesha gari haraka haraka maana alitaka kuwahi, na biashara zake alifanya mbali kidogo na nyumbani, alikuwa amewekeza Kariakoo pamoja na Buguruni.
Walipofika nyumbani hakuwa na haja hata ya kuingia ndani, ila alimbusu mkewe, akashuka na kuingia ndani ya geti, ndipo Aneth akaingia ndani ya nyumba yake.
Erick alichukua safari yake akaelekea kazini kwake, ila upande wa nyuma alikuwa amemuacha mkewe akiwa na ratiba ya kwenda kuonana na Haidali kwa siri ili aweze kumsaidia apate kazi.
Aneth alichukua simu kisha akampigia Haidali na kumuuliza wakutane wapi
“Naomba uje Mbezi Beach”
“Sawa nakuja sasa hivi”
“Hamna tatizo, ukifika utaniambia”
“Okay”
Aneth alikata simu, hakuwa hata na haja ya kubadilisha nguo ambazo alikuwa ametoka nazo ibadani, baada ya dakika kadhaa alichukua pochi iliyokuwa na kile kiasi cha fedha ambacho alikuwa amedhamiria kukipeleka kwa watu hao watatu.
Aneth alitoka akafunga geti lake vizuri ndipo akatembea mpaka katika barabara kuu ya madale akasubiri bajaji.
Alipopata bajaji aliipanda ikampeleka mpaka Mbezi beach, ndipo alipompigia Haidali simu na kumuelewa kwamba ameshafika tayari
“Sawa ninakuja hapo dakika moja”
“Okay”
Baada ya dakika sita Haidali na Aneth walikuwa katika hoteli moja wakiwa wanakunywa juisi huku wakipiga stori mbili tatu na kuwasubiri wenzake, Irene Biseko na Jonas Jonathan ambao walikuwa pia wanafanya kazi kwenye ile kampuni binti aliyoomba kazi ili waje wakubaliane kwa pamoja.
Ni kweli baada ya dakika kadhaa tu walifika pale, walikuwa wanahitaji kupata angalau marupurupu ya kazi yao waliyokuwa wakiifanya.
Wote walikaa wakaagiza vinywaji na kuendelea na mazungumzo, sasa tabu ilitokea pale Jonas alipoanza kuongea
“Sasa jamani mimi ninatakiwa niwahi, so ni vyema tukafanya lililotuleta hapa kwanza”
“Sawa, hamna shida, mwanamke mwenyewe ni huyu hapa” alisema Haidali
“Sawa kwa hiyo unatupa kiasi gani binti?” aliuliza Jonas
“Nyie mnataka kiasi gani?” aliuliza
“Sisi hapa tuko watatu ninaona utupe shilingi million na laki tano”
“Milioni na laki tano????? Binti aliuliza kwa mshangao mkubwa, yaani hata robo ya hiyo pesa hana
“Ndio, ili kila mmoja apate laki tano yake kati ya sisi watatu” alisema Irene
“Mh, hapana kwa kweli hela ni nyingi jamani ndo kwanza natafuta kazi” alisema mtoto wa kike Aneth
“Kwa hiyo wewe una shilingi ngapi?” aliuliza Jonas
“Mh mi kaka zangu nina shilingi laki mbili tu hapa”
“Whaat??” Irene alisema kwa mshangao, huku Jonas akiinuka na kutembea tembea kwa kutokuamini kile alichokisikia
“Ndiyo hivyo” alisema Aneth, alikuwa ameshakata tamaa ya kupata ile kazi
“Duuh” aliinuka Irene akasogea pembeni na kuanza kuongea na Jonas huku chini akimuacha Haidali akiongea na Aneth
Jonas alirudi na kuokota simu yake halafu akaaga “Oya utajuana na mgeni wako bwana, mimi ninaongea” alisema Jonas na kuondoka zake kwa hasira halafu Irene akamfuata nyuma
Haidali alibaki na Aneth wakawa wanaongea “Aneth hiyo ndo pesa uliyo nayo kweli?”
“Ndio….naomba unisaidie kaka yangu” alisema binti huku akimtazama machoni kwa ukaribu wa hali ya juu
Hii ilipelekea Haidali kuwaza mambo mengi, unajua macho ya jinsia mbili yanavyokutana yanakuwaga na hali fulani hivi ya hisia kali za msisimko mwilini
“Nisaidie” alisema binti
Walitazamana kwa muda, Haidali akawaza mengine, halafu kadri binti alivyokuwa anamtazama machoni ndivyo ilivyokuwa ikimjia picha ya marehemu Amidu kwa kasi maana walishawahi kutoka kimapenzi tena kwa kipindi kirefu
“Amidu……aah” alisema binti huku akijisahau na kumsogelea mdomoni
“Wee unafanya nini?” aliuliza Haidali na kuinuka halafu naye akamuaga.
Haidali alijua binti anataka kumtega kimapenzi ili ampe kazi lakini sio kweli ni kwamba binti alikuwa akivuta hisia za mpenzi wake wa zamani ambaye alikuwa anafanana sana na kijana yule. Hii ilipelekea binti kujishtukia hadi akaanza kulia
Baadaye alichukua usafiri akarejea nyumbani, alipofika alimuomba Mungu amuondolee kumbukumbu ya Amidu lakini kabla hata maombi hayajajibiwa. Uliingia ujumbe kwenye simu na ulitoka kwa Haidali
Ulikuwa ukisema hivi “Aneth ni kweli unataka kazi?’
Akajibu “Ndio ninahitaji”
“Sawa, sikiliza nitakusaidia ila kuna kitu nataka kutoka kwako” alisema kitu kilichomshtua binti
“Kitu gani tena Haidali?”
EP 08
“Nikikuomba hicho kitu utakubali?” aliuliza Aneth
“Mh inategemea” alisema binti
“Ah mh unajua tangu siku ya kwanza kukuona pale ofisini nilipata sana tabu maana kila nilipokutazama nilikutana na macho mazuri sana” alisema bwana Haidali
“Weee…acha mambo yako, saa ile ilitokea bahati mbaya tu mimi nikawa nafanya vile, I am sorry” alisema Aneth
“Hamna sio kwamba namaanisha ya saa ile, ila hata kuchukua namba yako ya simu tu ilitokea kwa sababu siku ile nilikuzimia si unakumbuka nilikutafuta mimi mwenyewe”
“Sawa ulinitafuta lakini haiwezekani, mimi ni mke wa mtu, halafu kingine ni kwamba mim hapa nina mimba in the moment, tena ndo kwanza ndoa yangu ni mpya kabisa so samahani kwa hilo”
“Hivi umeolewa?” aliuliza Haidali
“ndio tena hatuna hata miezi sita tangu tulipofunga pingu za maisha” alisema binti
“basi samahani sana kwa kukuambia vile sikujua kama wewe ni mke wa mtu” alisema Haidali
“Ok”
Haidali alikata simu yake akaachana na mke wa mtu lakini alimuhurumia sana kwa jinsi alivyokuwa akihangaika kutafuta kazi Haidali alihisi kwamba alihisi kwamba labda Aneth alikuwa akinyanyaswa sana na mumewe ndo maana siku ya kwanza binti alisema kwamba anataka kutafuta kazi kwa sababu hataki kutegemea pesa ya mwanaume.
Kumbe sio kwamba mumewe alikuwa akimnyanyasa yule mwanamke ila tu ni kiherehere cha binti kujifanya anajua kujituma.
Hali ya huruma za Haidali zilimfanya atamani kumsaidia binti ili aweze kupita na kupata kazi kwenye ile kampuni.
Haidali alimtumia ujumbe Aneth ukiwa unasema hivi “basi usigope nakuahidi utapata hii kazi” alisema
Aneth hakuweza kujibu ule ujumbe maana bado alikuwa anahisi Haidali bado alikuwa akimtaka kimapenzi
Kesho yake ikiwa ni siku ya Jumatatu Haidali alifika katika ofisi yake akiwa ameshikilia karatasi ya majina ya watu watatu ambao walikuwa wamechaguliwa na kampuni kufanya kazi nao, wote wale walitakiwa kwenda kufanya kazi katika tawili lao jipya ambalo walikuwa wamelifungua maeneo ya Bagamoyo mkoani Pwani.
Watu hao walikuwa ni wanaume wawili na mwanamke mmoja ambaye alikuwa ni Aneth. Haidali alimkabidhi Jonas ile karatasi, Jonas akaisoma
“Mh boss” alisema kijana yule
“Nini? Waite hao” alisema kumbe Haidali alikuwa ni boss kuliko wote pale ofisini, hii ni kwa sababu baba yake wa kufikia (yaani mume wa mama yake) alikuwa ndiye mmiliki wa ile kampuni, alikuwa ni mtu wa Zanzibar.
“Huyu si yule binti?” aliuliza Jonas
“Ndio, mpigie simu afike mara moja yeye na wenzake pia” alisema mtaalamu Haidali halafu akapiga hatua ila alipofika mlangoni aligeuka na kusema “Halafu Irene na Levis watahamia Bagamoyo halafu Huyu Aneth na mwenzake aliyechaguliwa naye mmoja wataungana pamoja nasi hapa hapa Dar es Salaam” alisema kwa maringo, siku hiyo alikuwa hataki kabisa utani katika kazi yake, licha ya siku zingine kujiweka kama vile yuko sawa na wale wengine.
Jonas na Irene hawakuwa na la kufanya kwa sababu mkubwa kwao kasema, japo walilingana kielimu lakini alikuwa akitoka kwenye familia ya boss wao hivyo hawakuwa na namna lazima wamsikilize tu.
Jonas aliwapigia hao vijana watatu waliokuwa wamechaguliwa kujiunga na kampuni hiyo kama wanafunzi, Aneth akiwa amekaa nje barazani anachezea simu, hakuamini kupokea simu kutok AB Insurance Company
“Hallo, naongea na Aneth?” alisema Jonas kwenye simu
“Yes”
“Hongera umechaguliwa kuwa mkurugenzi wa AB Insurance, tafadhali fika kesho jumanne asubuhi saa mbili kwa ajili ya maelezo zaidi”
“Asante kaka yangu nitafika” alisema binti kwa furaha, alikuwa akitamani sana kuajiriwa maana alikuwa amesomeshwa na wazazi wake wa Kibosho wakiamini atakuja kuajiriwa, maana hawakuamini katika kujiajiri kwani familia nyingi masikini huwa hazina mitaji ya kuwasaidia watoto.
Binti alilifurahi sana, alijisikia faraja, lakini kwa upande mwingine alikuwa akihofia labda anaweza kuja kuletewa shida na mumewe kwa sababu alikuwa ameshamuambia atamfungulia biashara binafsi.
Akiwa anawaza namna atakavyomuambia mumewe, mara alipokea ujumbe, akaufungua ulikuwa wa Haidali
“Umepigiwa simu nadhani”
Binti alitabasamu kisha akajibu “Ndio, ninashukuru sana”
“Usijali tuko pamoja, nimeamua kukupambania kwa sababu wewe ni kama dada yangu, halafu vipi ungependelea kwenda kufanya Bagamoyo au hapa hapa Dar?” aliuliza Haidali
“duh Bagamoyo mbali na vile hali yangu naomba nifanyie hapa hapa Dar”
“Okay usijali katika hilo”
“Jamani asante ee” alisema binti kwa furaha
“Karibu”
Usiku kama saa nane ndipo aliporudi mtaalam Erick, tena siku hiyo alikuwa akiendeshwa na Dullah maana alikuwa amelewa hasa, alifungua geti maana naye alikuwa na ufunguo wake wa ziada, kisha alitoa vinywaji aina ya wine ndani ya gari na kumuaga Dullah ambaye aliondoka na gari yake.
Erick aliingia ndani ya geti akafungua mlango na kuzama hadi sebuleni ambapo aliweka vinywaji kisha akaingia hadi chumbani alipomkuta binti akiwa amelala fofofo.
“Uko macho?” aliuliza Erick kwa sauti hafifu maana hakutaka kumsumbua mama kijacho
“Nn…..aaaah” binti alijinyoosha, bado macho kafumba akasema kwa sauti dhaifu iliyochanganyika na usingizi “Pole mume wangu” alisema binti
“Asante sana…uko powa?” aliuliza Erick huku akivua fulana
“Niko powa” alisema binti na kufungua macho akamtazama kwa macho yaliyokuwa yanakaribia kufumbika
Erick alitabasamu kisha akasema “Nimekuletea wine ziko sebuleni kama utakunywa usiku huu au asubuhi”
“Nitakunywa asubuhi bhana” alisema binti
Erick alimalizia kuvua nguo akaenda mpaka bafuni akaoga kwa dakika chache sana ndipo akarudi na kujilaza kitandani akapitiwa na usingizi mara moja.
Ilipofika saa kumi na moja asubuhi, Erick aliamka na kumpigia simu Dullah ambaye alikuwa ameondoka na gari yake, halafu akamuambia aanze safari ya kuja kumchukua nyumbani.
Erick alishuka kitandani kisha akaenda tena bafuni, alioga na kuswaki kisha akarudi na kuanza kuvaa nguo zake za kuendea kazini.
“Erick” Aneth ambaye alikuwa kitandani alimuita mumewe
“Nambie mke wangu”
“Unaondoka saa hizi?” aliuliza
“Ndio, kwani kuna tatizo?”
“Hapana, ila nimepata kazi kule kwenye ile kampuni niliyoenda kufanya interview”
“Eeeh??” alishtuka Erick “Umepata kazi?” aliuliza
“Ndio…jana waliniambia niende leo nikaanze training pamoja na kusaini mkataba” alisema binti
Erick alikusanya mikono kifuani halafu akatazama juu kwenye gypsum na kuwaza kwa muda wa dakika moja. Aneth akamuuliza “Unaniruhusu niende au niendelee kukutegemea kila kitu mume wangu?”
Erick alishusha macho, akamtazama na kusikitika akamuuliza “Kwa hiyo hali yako kweli utaweza kufanya kazi kwa amani mke wangu?”
“Nitaweza, sio kazi ngumu halafu isitoshe mimi hii mimba wala hainichoshi sana”
Erick alimtazama kwa sekunde thelathini bila kuzungumza chochote ndipo binti akaongeza swali “Niambie basi au umekasirika?”
Erick akatikisa kichwa na kuuliza “Kwani unapenda kuajiriwa au kujiajiri mwenyewe?”
“Mume wangu napenda kila kazi inayoniingizia pesa, sipendi kukaa hivi hivi tu”
“Kwanini usisubiri nikakujazia ule mtaji halafu ukafungua tena goli lako la miamala?”
“Nitasubiri hadi lini? Ni heri nikafanya, wote tukaunganisha nguvu kwa pamoja, ndo tutapata mtaji kwa haraka zaidi”
Erick alimpenda sana mke wake, hakuwahi kumsaliti licha ya kuishi katika vikundi vya wahuni, aligundua mkewe ana akili fulani ya maisha, alitabasamu kisha akamjibu “Basi usijali we fanya kinachoufurahisha moyo wako, ila please usiteseke, ukiona inakusumbua we acha, nitakopa popote uwe na biashara yako sawa?”
“Sawa mume wangu”
Ghafla simu ya Erick iliita, ni Dullah alikuwa anampigia, alipokea “Oya niko getini hapa” alisema dullah
“Poa” alisema Erick na kukata simu halafu akamtazama mkewe na kumuambia “Haya mi naondoka” alisema Erick na kutoa wallet akamtolea kiasi cha fedha za matumizi halafu akamkabidhi
“Asante” alisema binti baada ya kupokea
Erick aligeuka na kuanza kuondoka, alipofika mlangoni Aneth alimuita “Mume wangu” ndipo Erick akageuka na kumtazama binti akasema “Asante ee”
“Usijali”
Erick alitoka mpaka getini wakapeana tano na Dullah halafu safari ikaanza kuelekea katika kazi zao huko
*
Ilipofika saa moja asubuhi Aneth aliondoka nyumbani kuelekea kule kwenye ile kampuni ambayo alikuwa ameitwa kwa ajili ya mafunzo maalum kabla ya kuanza kazi rasmi.
Alipofika alimkuta Jonas akiwa anacheze taraklishi (compyuta) ya mezani, akamsalimia “Za asubuhi ndugu” alisema mtoto wa kike
“Salama kwema?”
“Kwema kabisa” alisema Jonas huku akiendelea kuchezea compyuta yake taratibu na binti akawa anachezea simu yake taratibu.
Ilipopita kama dakika kumi hivi bila maongezi yoyote, Aneth alianza “Samahani kaka, eti uani ni wapi?”
“Anhaa unataka kwenda uani?” aliuliza Jonas huku akimtazama
“Ndio kaka yangu”
“Okay nenda hivi” alisema Jonas huku akimuonyesha kwa ishara ya mikono “Ukifika mbele utakuta pameandikwa tu ndani ya korido hiyo hapo”
“Sawa” binti alitoa tishu kwenye pochi kisha akainuka na kuanza kutembea, kwa bahati mbaya au nzuri, binti alikuwa na umbo ambalo ni tamanishi kabisa, licha ya kuwa ni mke wa mtu tena mama kijacho lakini kadri alivyokuwa akipiga hatua alikuwa akisababisha majanga kwa kila mwanaume rijali aliyefanikiwa kumuona
Alitembea mtoto wa kike kwa mwendo fulani hivi, Jonas akamkodolea macho kwa kujiiba ndipo moyoni akajisemea “Daah kuna wana wanafaidi” huku akimtazama mpaka alipoishilia huko kwenye veranda
Baada ya dakika kadhaa binti alirudi na kuendelea kuketi pale, ndipo wenzake walifika wawili, alikuwa ashawahi kuwaona kipindi wanafanya interview, walipiga hadithi mbili tatu mpaka pale Haidali alipofika.
“Habarini za asubuhi” alisema Haidali
“Salama” walijibu wale vijana wawili na binti mmoja (Aneth) ambao walikuja tayari kwa ajili ya kupewa mafunzo fulani kulingana na kazi
Macho ya Haidali yalitua moja kwa moja juu ya macho ya Aneth na walitazamana ana kwa ana, damu zikawachemka, Aneth akatabasamu halafu Haidali naye akatabasamu na kumsogelea Jonas na kumpa tano
“Vipi ndugu yangu?” aliuliza Jonas
“Asee fresh, umeshafika?” aliuliza
“Ndio, nimefika mapema leo”
“Hahaha noma, mi niko juu, Biseko yuko wapi?” aliuliza
“Ametoka mara moja anakuja tu muda sio mrefu”
“Poa mfanye uhakika basi”
Haidali aliondoka pale kwenye ile ofisi akaenda kwenye ofisi yake kuu maana kidogo yeye alikuwa ni mkubwa kuliko kina Jonas kikazi lakini.
Alipofika kwenye ofisi, alimtumia ujumbe Aneth, njoo ofisi namba 3 tafadhali” alisema Haidali
Aneth aliisoma ile message akaweka simu kwenye pochi halafu akainuka na kuelekea kwenye ile ofisi
EP 09
Alipofika katika ofisi ya Haidali alimkuta Haidali akiwa ameshika tama, akamtazama na kuonyesha hali fulani hivi ya furaha sana baada tu ya kumuona Aneth pale ofisini kwake. Aneth mwenyewe alitabasamu halafu alisimama na kushikilia pochi yake tumboni kwa mikono yote miwili halafu akawa anamtazama Haidali huku tabasamu pana likimtoka
“Njoo ukae basi” alisema Haidali huku akimuonyesha kwa mkono kiti kilipo
“Sitaki” alisema binti kwa kifupi alikuwa amemzoea kwa haraka sana yule mwanaume
“Mmmh kwani nimekukosea nini?” aliuliza Haidali huku akitabasamu na kutanua mikono kwa mbwembwe
“Umenikosea sana tu” alimtania binti halafu akasogea na kuketi akamuamkia “Shikamoo kaka” alisema kwa utani
“Marahabaa,…mdogo wangu” alisema Haidali kwa furaha kidogo, kila mmoja alionekana kuwa na furaha ya kuwa karibu na mwenzake, japo ni muda mfupi tu wamefahamiana.
Mara ghafla Haidali alijifanya yuko bize anashika shika madocuments yaliyokuwa pale mezani halafu akamuuliza “Vipi uko powa lakini?”
“Niko safi jamani, namshukuru Mungu sana halafu ninakushukuru sana pia wewe umenipigania katika hili, nitakulipa hiyo pesa yako uliyowapa”
“Don’t worry, nimefanya kwa upendo tu kwa sababu ninakuona kama dada yangu”
Aneth hakuweza kumjibu lolote, alibaki akimshangaa yaani alimtazama kwa muda mrefu halafu akaguna na kusema “eeh kweli”
“Vipi mbona umeniangalia halafu ukaguna kuna tatizo?” aliuliza
“Kiukweli kuna watu wanafanana” alisema binti
Haidali alitabasamu maana alijua binti alishawahi kumuambia anamfananisha na kijana mmoja ambaye ni marehemu Amidu.
“Kwanini unasema hivyo?” Haidali aliuliza
“Yaani unanikumbusha mbali sana, yaani unafanana sana na Amidu….kila kitu hadi sauti hadi vituko yaani kila kitu khaaa….mi nahisi nyie ni ndugu”
“Sijui labda upande wa baba…maana nilikuambia kwamba baba yangu mimi simfahamu kabisa” alisema mkali Haidali
“Haya bana” binti alisema “Enhee umeniitia nini?”
“Aneth nimekuita ili nijue kama uko powa tu….” aliongea mtaalam ila ghafla Irene alifungua mlango na kumtazama Haidali akamuwahi kwa kusema “Irene vipo Miss?”
“Boss salama umeamkaje leo?”
“Safi tu…..”
“Okay powa nianze ile kazi sasa hivi au?” aliuliza Irene maana alitakiwa kuwafundisha hao waajiriwa wapya namna kazi itakavyokwenda
“Of course anza sasa hivi maana baadaye unatakiwa uende Bagamoyo ukaangalie ile ofisi nyingine kama imeshakaa sawa”
“Mh mimi tena kazi zote jamani?”
“Yeah, kwa sababu uko attractive, una mvuto wa hali ya juu ndo unaweza kushawishi wateja”
“Hahahahaa…..acha mambo yako wewe” alisema binti kwa furaha halafu akatoka akabamiza mlango kwa lakini akaufungua na kumuuliza “Huyu naye si anafanyiwa training?” hapa alikuwa anamuulizia Aneth ambaye alikuwa ndani ya ofisi ile ya Haidali
“Yeah” alisema Haidali kisha akamtazama Aneth “Nenda kwenye mafunzo tutaongea baadaye”
“Haya powa” Aneth alisema na kuinuka akamfuata Irene
Walifika katika chumba maalumu kwa ajili ya mafunzo, wakaanza kufundishwa kwa masaa kama mawili ndipo wakachukuliwa na kupelekwa hotelini wakanywe chai.
Walikunywa kisha wakarudishwa kwa ajili ya mafunzo mpaka saa saba na nusu ndipo yalipokamilika
“Sasa hivi mnaweza kwenda” alisema Irene
“Kwa hiyo turudi kesho tena?” aliuliza kijana mmoja kati ya wale waliokuja wapya
“Ndio, tutaendelea wiki nzima hii, halafu Jumatatu ijayo ndo kazi itaanza”
“Sawa dada….asante”
“Haya karibuni”
Wale vijana walitoka, ila Aneth aliingia ofisini kwa Haidali, akamkuta akiwa na mteja mmoja hivi, akamuambia “Boss mimi naondoka”
“Okay okay nitakupigia”
“Sawa” Aneth alisema na kuondoka akarudi nyumbani
Mafunzo yaliendelea kila siku kwa wiki nzima, lakini kadri siku zilivyosogea mazoea yalizidi mara dufu kati ya Aneth na boss wake, Haidali japokuwa alikuwa amemzidi umri lakini boss ni boss tu.
Hii ilichangiwa pia na Erick kuwa na ubize uliokithiri, muda mwingi alitumia kufanya biashara zake, ambapo ilimpa fursa ya kuwasiliana na Haidali mara nyingi, na hata kuwa anamrudisha nyumbani na gari kipindi akitoka kazini
Siku moja, Haidali alimpeleka binti wazo, ilikuwa ni mida ya saa 11 jioni, ndipo wakasimama na gari nje ya geti la Aneth. Ndipo Aneth akamtazama Haidali kisha akasema
“Asante mi nashuka ee” alisema binti halafu akashika mlango wa gari na kufungua anataka ashuke, ghafla Haidali akamvuta kwa karibu kitendo kilichofanya midomo ikaribiane, na vile vile macho kutazama kwa karibu
“Aneth” aliita Haidali kwa mahaba
“Abee” binti aliitika kwa hisia
Haidali alimsogezea mdomo taratibu anataka apate hata busu lakini binti alilikwepa kisha akasema “Usifanye hivyo”
“Kwanini jamani?”
“I am sorry….bye” alisema binti kisha akafungua mlango na kushuka kisha akatembea haraka haraka mpaka getini akafungua na kuingia ndani
Huku nje alimuacha Haidali katika hali mbaya, Haidali alikuwa ana hisia sana na binti lakini hakuwahi kumuambia, alijiuliza “Kwa hiyo mpaka nimuambie nampenda ndo ataelewa?” halafu akajijibu “Hapana siwezi kumuambia…naanzaje kumtongoza mke wa mtu” alijiuliuza tena na tena halafu akageuza gari speed sana halafu akaondoka kuelekea zake ofisini maana ilikuwaga ni utamaduni wake kuondoka pale kazini jioni saa moja au saa mbili.
Aneth naye alijilaza kwenye mkeka sebuleni, mara baada ya kuoga akawa anaitazama picha kubwa ya harusi iliyokuwa ukutani na kusema “Hivi huyu Haidali ananitaka nini lakini kwani hajui mimi nina mume na tumetoka mbali? Halafu nina mimba khaa wanaume” alijisema halafu akaendelea kujilaza.
Usiku ilipoingia mida ya saa mbili, Aneth akiwa anapika jikoni huku akicheza muziki uliokuwa ukidunda sebuleni kwenye redio kupitia Bluetooth ya simu yake, alisikia mziki umesita, akasikilizia ndipo akagundua kwamba simu yake inaita.
Huyu binti alienda sebuleni, kulikuwa sio mbali na jikoni, akakuta kuna namba ngeni ninampigia, ndipo akaipokea
“Hallo” alisema yule aliyekuwa anampigia
“Hallo” alijibu binti huku akisikilizia kwamba sauti ni ya nani
“Mzima wewe?” aliuliza huyo mtu
“Mzima”
“Umeshanijua?” aliuliza yule mtu
“Hapana”
“Mimi Jonas Jonathan”
“Ahaa boss nambie” alisema kwa nidhamu Aneth maana yule alikuwa ni mfanyakazi mkongwe kwake, alimkuta na alimfanyia interview siku alipokuja kuhojiwa
“Samahani kidogo uko wapi?” aliuliza Jonas
“Niko nyumbani tu”
“Peke yako?” aliuliza Jonas
“Yes”
“Mumeo hajarudi?”
“Hajarudi vipi kwani?” binti alipoona maswali alijawa na wasiwasi
“kuna ishu natamani kuongea na wewe privately Aneth please”
“Mh ishu gani tena?”
“Aneth naomba tuonane kesho baada ya kutoka kazini”
“Haitawezekana, naomba uniambie tu kwenye simu”
Jonas alikata simu yake, na kusababisha Aneth asonye kidogo maana alijua mwanaume kazi yake ni kutongoza tu, hakuna kingine
Akiendelea kupika, alipata ujumbe mrefu kidogo kutoka kwa Jonas, ule ujumbe ulisema hivi
“ANETH UNAJUA MIMI NINA MKE, NA WEWE UNA MUME, LAKINI KIUKWELI WEWE NI MWANAMKE AMBAYE UNA MVUTO WA HALI YA JUU SANA, NAOMBA PLEASE HATA MARA MOJA MOJA TUWE TUNAONANA, NITAKUWEKEA RATIBA YA KUKUPATIA SHILINGI LAKI TANO KILA MWEZI KWA PENZI TU” alisema mwamba
INAENDELEA

