MAMA AUA MTOTO WAKE KWA KUMCHOMA KWA MAFUTA YA TAA, KWA KUIBA TSH. 1500
Kaunti ya Kisumu ilitumbukia katika maombolezo baada ya mvulana wa umri wa miaka 12 kutoka eneo la Nyamgun kaunti ndogo ya Seme kupoteza maisha katika kisa cha kushangaza kinachodaiwa kufanywa na mamake mzazi.
Kulingana na ripoti za polisi, mtoto huyo aliyetambuliwa kwa jina la B.O, alipata majeraha mabaya ya moto baada ya mamake kumshutumu kwa kuiba Sh150.
Majirani walisema mwanamke huyo alimmiminia mafuta taa mvulana huyo kabla ya kumchoma moto wakati wa makabiliano hayo makali.
Mvulana huyo aliokolewa Jumatatu usiku na wenyeji waliokimbia kuzima moto huo.
Alipelekwa katika Hospitali ya Kata ya Kombewa akiwa katika hali mbaya, lakini licha ya jitihada za kumwokoa, madaktari walithibitisha kuwa ameungua kwa asilimia 90 sehemu ya juu ya mwili, mikono na pajani. Alikufa kutokana na majeraha yake Jumanne asubuhi.
Makachero wa Kituo cha Polisi Kombewa na maofisa wa Kurugenzi ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) Seme walitembelea hospitali hiyo na eneo la tukio. Katika boma hilo, walipata fulana ya buluu iliyoungua kiasi inayoaminika kuwa ya mwathiriwa.
Duru za polisi zilifichua kuwa mama huyo mwenye umri wa miaka 47 alikamatwa mara moja.
Anazuiliwa katika Kituo cha Polisi cha Kombewa na anatarajiwa kukabiliwa na mashtaka ya mauaji siku ya Jumatano.
Chanzo: NYALENDA

