Baba wa watoto watano amehitimu masomo yake chuoni akiwa na umri wa miaka 64.
Baada ya kukamilisha mafunzo ya uuguzi yanayoambatana na kazi ya vitendo (apprenticeship) katika Chuo Kikuu cha West of England (UWE) jijini Bristol, Uingereza, John Adesoye alisherehekea mafanikio ya juhudi zake katika hafla ya mahafali iliyofanyika Jumatano, Julai 15, kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na chuo hicho.
Adesoye alibadili taaluma na kuwa muuguzi baada ya kuanza maisha yake ya kazi kama fundi wa vifaa vya kielektroniki nchini Ugiriki, kabla ya kuhamia Uingereza. Alikulia nchini Nigeria na alianza kuvutiwa na masuala ya vifaa vya kielektroniki akiwa mtoto, wakati alipovutiwa sana na redio.
“Awali, nilikuwa nikishughulikia vifaa vya kielektroniki na nilifurahi nilipoweza kufanya vifaa vilivyoharibika vifanye kazi tena,” alisema, kulingana na taarifa hiyo. “Katika kazi yangu ya huduma za afya, wagonjwa wanapopata nafuu, jambo hilo hunipa furaha na kuridhika sana.”
Wakati akisoma, Adesoye alihudhuria masomo katika chuo cha UWE pamoja na mwanawe, Daniel, ambaye alikuwa akisomea shahada ya teknolojia ya muziki wa ubunifu. Alitumia siku moja kwa wiki chuoni na siku nyingine zilizosalia akipata mafunzo katika Hospitali ya Southmead jijini Bristol.
Awali, Adesoye alibadili taaluma yake mwaka wa 2013 alipoanza kufanya kazi katika Hospitali ya Southmead kama msaidizi wa huduma za afya, kulingana na taarifa iliyotolewa.
Kisha alijiunga na kozi ya usaidizi wa uuguzi kabla ya kukamilisha mafunzo ya kivitendo ya shahada ya uuguzi na kuwa muuguzi aliyesajiliwa msimu huu wa joto.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Adesoye amepata nafasi ya kazi ya uuguzi katika hospitali ya Southmead na hajatupilia mbali uwezekano wa kusomea shahada ya uzamili hapo baadaye.
Amefanya kazi katika idara mbalimbali huko Southmead, zikiwemo idara ya huduma za dharura, magonjwa ya moyo, mifupa na huduma ya wagonjwa mahututi.
Chanzo: PEOPLE

