UNA NINI LAKINI MELISSA
ONYO: Wakubwa tu, kuanzia Miaka 18, ndio wasome hii Hadithi
Sehemu Ya 4
Akamwambia kuna mengi anataka kuteta naye ila yote hayo yapasa yawe ya siri baina wao. Hategemei kumwona mtu yeyote anapata kuyafahamu, na basi kwa kufanya hivyo atakuwa amejiweka shidani.
Maneno hayo yakamfanya Darren awe mtulivu na msikivu sana maana yalimaanisha ni jambo kubwa lenye uzito. Baba yake, Mr Gerald, akanywa kwanza fundo la glasi ya whisky kisha akamtazama mwanaye machoni.
“Sikia, Darren,” akasema kabla hajasafisha koo lake na kujipangusa kwa mgongo wa kiganja. “Kuna mambo ya ajabu ajabu hapa katikati. Najua hauyafahamu na nilipata kumsisitizia sana mama yako akwambie lakini hakuwa tayari. Mpaka kifo kinamkuta hajatekeleza ahadi yake hiyo…”
Akaweka kituo akitazama sakafuni kifikira. “Ulikuwa ni wakati mgumu sana, kwangu na kwake. Tangu yu kwenye usichana mpaka tulipokupata wewe. Nakumbuka, pindi alipokuwa msichana mdogo, alikuwa anapitia mambo ya ajabu sana. Ndoto za ajabu. Na mara kwa mara akinambia anaona watu wa ajabu wakimjia.
Kuna muda tulikuwa tunashindwa kulala. Angesema kuna mtu nyuma ya mlango. Mtu dirishani. Mtu koridoni. Mtu kila sehemu! Hatukuwa na amani, na, Mungu nisamehe, nilishawahi kufikiria kuachana naye maana hayakuwa yanavumilika.”
Akanywa tena fundo la whisky. Kuyaongea hayo aliyokuwa anaongea, ilimpasa apashe kichwa na kujitoa ufahamu.
“… lakini kila nilipokuwa nataka kumwacha, ningalijiuliza, vipi ingekuwa mimi? Ningejisikiaje mtu angeniacha kwasababu ya matatizo yangu? Bila shaka ningehisi nimetupwa na kukomolewa, basi nikapiga moyo konde. Maisha ya taabu, taabu sana.
Tukahama pale tulipokuwa tunakaa kwa kudhani aidha hapafai, lakini bado matatizo yakawa yaleyale. Shida haikuwa nyumba. Shida ilikuwa damu. Damu ya mama yako. Na hata angeenda wapi, basi angelibadilisha jambo.”
Aliposema hayo akanyamaza kana kwamba anapangilia sentensi kichwani. Na kabla hajateta lingine, akanywa tena whisky, tena saa hii mara mbili tofauti na hapo awali kisha akanguruma kama simba kwa kuwakwa na koo.
“Unakumbuka kwenye msiba wa bibi yako?” Akauliza.
“Ndio, nakumbuka,” Darren akajibu.
“Uliona bibi yako alizikwaje?” Baba akauliza, naye Darren alipofikiria kidogo akasema, “Hatukumuaga kama wengine. Na hakukuwa na kiongozi wa dini kuendesha misa!”
“Unadhani kwanini?”
“Sijajua kwanini … lakini … mimi sikuwahi kuona ubaya wowote wa bibi alipokuwa hai!”
“Ni sawa. Na hamna shida yoyote katika hilo. Lakini utakuwa umejifunza kuwa mama yako hakuwa na mahusiano mazuri na bibi yako, japo alikuwa mama yake. Ni aghalabu angeenda kumtembelea na kumjulia hali. Sio?”
“Ndio.”
“Darren, Bibi yako hakuwa mtu wa kawaida. Na alimweka kifungoni mama yako kwa takribani miaka tisa! Sijui nisemeje, sikuwa mtu wa kuamini hayo mambo hapo kabla, ila baada ya kukutana na mama yako ndipo nikaelewa juu ya uwepo wake.
Ni kama kheri, tukiwa tumehamia kwenye makazi mapya, baada ya kukaa hapo kwa miezi mitatu, tukapata jirani ambaye alitokea South Carolina. Jirani huyu baada ya kukaa siku tatu tu kando na sisi, akafahamu yale tuliyokuwa tunapitia.
Nakumbuka siku moja nikiwa natoka kazini, aliniita na kunambia angependa kuongea na mimi mambo kadhaa. Nilisita kidogo ila sikuona haja ya kumkatalia. Nikasonga akanipatia kiti nikae sebuleni mwake. Hapo akaniuliza akiwa amenikodolea macho yake ya kizee, ‘una shida kubwa, sio?’
Mimi nikamkatalia, lakini aliweza kuona ndani yangu. Kwa upole akasema anataka kunisaidia na kama nikiwa tayari kukiri kuwa nina hiyo shida basi atakuwa radhi. Mimi nikakataa. Sikuwa namfahamu hata kidogo na nilihofia asije akaniongezea matatizo mengine zaidi ya yale niliyokuwa nayo.
Basi nikaondoka nikiwaza sana. Kesho yake nilipopita hapo kwake, nikamkuta kibarazani. Nikamsalimu na kwenda. Siku hiyo usiku nikapata tabu sana. Mama yako alinikaba mno na kwa macho yangu nikashuhudia nyayo za damu koridoni! Nikakoma ubishi.
Kesho nilipotoka kazini nikamwendea yule mama na kumwambia nina shida. Naomba anisaidie kwa namna yoyote ile. Na atakapoweza, basi nitajikunja kwa kadiri ya uwezo wangu nimpatie chochote cha thamani.
Kwa wakati huo nilikuwa nimekonda sana. Sitamaniki. Hata nguo zangu nazoendea kazini zikiwa zimefubaa, chafu na kukuu. Sikuwa na raha na maisha haya.
Yule mama akaniambia yu tayari kunisaidia, cha muhimu nimlete mke wangu kwake nikiwa na petali nne za maua zamaridi, mafuta ya ngamia na matumbawe toka baharini.
Japo masharti yalikuwa magumu, nikaridhia. Ugumu wake haukuwa sawa na ule nlokuwa napitia kila siku. Nikatafuta vitu hivyo na ndani ya siku mbili nikavipata vyote. Nikambeba mke wangu na kumpeleka huko.
Basi mama yule akafanya mambo yake. Sikuelewa anachofanya, alikuwa anaongea kwa lugha ya ajabu. Alitengeneza maji na kuchanganya na petali zile za zamaridi kisha akampaka Sarah mafuta yale ya ngamia kwenye paji la uso.
Na kama nakumbuka vema, alichukua unga nisiojua wa nini, akautia kwenye maji yenye zile petali alafu kama haitoshi, akamchanja Sarah kwenye mkono wake wa kushoto, akakinga damu na kuweka humo.
Mwishowe akatengeneza uji mzito ambao akawa anachovyea na kuandikia kwenye kitabu akiwa ananena kwa lugha ya ajabu. Alipomaliza kuandika, akakizungusha kile kitabu kichwani mwa Sarah na kumgusishia kwenye paji la uso kisha akamwambia naye aseme maneno alokuwa anayatamka.
Sarah alipofanya hivyo, akazirai. Mama yule akan’tazama na kunambia, kitabu kile kiende kuhifadhiwa mbali msituni kwani ndiyo roho pekee salama ya Sarah. Kadiri kitabu kitakapokuwa salama, naye atakuwa vivyo. Lakini kitakapoharibika, naye ataenda vivyo hivyo.
Na kwa kadiri ambavyo kitabu hicho kitakuwa hai, hamna mtu yeyote mbaya anaweza kumdhuru, akisisitizia zaidi juu ya majini. Watamwogopa kama ukoma na watamkimbia popote pale atakapokanyaga.”
Basi hapa Darren akajikuta akimkumbuka Melissa. Mbona alikuwa akimkimbia mama yake? Lakini hakuwaza sana, akaendelea kumpatia masikio babaye aliyekuwa na mengi ya kumwambia.
“Na tokea hapo mama yako hakusumbuliwa tena. Na punde bibi yako alipofariki, ni yeye ndiye akashauri kuwa nyumba ile iuzwe. Na hata vile vilivyomo ndani visichukuliwe hata kimoja kwa kuhofia vyaweza kubeba na kusafirisha matatizo!”
Darren akakumbuka kuhusu ile picha ya bibi yake na namna ambavyo mama yake alivyokuwa ameghafirika kuitafuta. Akajikuta akitikisa kichwa kwa masikitiko. Sasa ndiyo alijiona mjinga.
“Mama yako,” baba akaendelea kuteta kwa huzuni, “alikufa kwasababu ya moto uliochoma msitu wa kule California. Kitabu chake kitakuwa kimeungua na basi hivyo maisha yake. Hamna kitu ambacho kingeweza kumwokoa.
Lakini nahofia sana, Darren. Nahofia zaidi kuhusu maisha yako. Sidhani kama yatakuwa sawa na kuondoka kwa mama yako. Hata yangu pia. Naamini uwepo wake ulitufanya tukawa salama zaidi.”
Akashusha pumzi ndefu kisha akahitimisha kwa kusema, “Na kwa usalama wetu Darren, inabidi tuachane kabisa na ile nyumba. Ile ya bibi yako. Usiende tena huko, wala kuhusiana nayo kwa njia yoyote ile. Sawa?”
Darren akatikisa kichwa. “Sawa.” Macho yake yalikuwa mekundu yaliyochoka.
Basi tangu hapo, miaka ikaenda na kwenda. Baba yake Darren akasumbuliwa sana na ugonjwa wa saratani ya koo kwasababu ya uvutaji mkubwa wa sigara hivyo akajifia na kumwacha Darren peke yake.
Baada ya mwaka mmoja, Darren akamwoa mwanamke mrembo aitwaye Josephine, na kuwa na familia. Akaishi mbali kabisa na nyumbani, huko New York. Ndani ya mwaka mmoja wakajaaliwa mtoto wa kiume waliyemwita William.
Lakini …
Darren atabaki vipi salama na ingali damu yake ndi’ ile ile ya mama yake? Kama ametoka kwenye tumbo la aliyetoka kwenye tumbo la asiye binadamu, kivipi anasalimika kwa upesi?
***
“Nadhani leo nitakawia kutoka kazini,” alisema Darren akiwa anakunywa chai. Pembeni yake alikuwapo mkewe akiwa amembebelea mtoto. Darren alikuwa ameshajiandaa kikazi, amevalia suti na tai yake nadhifu.
“Kwanini?” Josephine akauliza akimtazama kwa shaka. Hakuwa kuzoea mambo hayo ya mumewe kukawia hivyo alitarajia kutakuwa na sababu kubwa.
“Nina kazi kubwa sana,” akasema Darren. “Na nisipozimaliza leo basi itaniwia ugumu sana hapo baadae.”
Mkewe akaelewa lakini asisite kumwonyesha mumewe kuwa atamkumbuka. Na basi atakapopata namna, ajitahidi kuwahi.
“Usijali,” Darren akamtoa shaka kisha akambusu kwenye paji la uso kabla hajasimama. “Nitajitahidi mpenzi wangu. Ila ukiona nimekawia zaidi basi usikasirike … unajua namba yangu, utan’pigia nikikawia kufanya hivyo.”
Basi akaenda zake baada pia ya kumwaga mwanaye ambaye sasa alikuwa na mwaka mmoja tangu azaliwe. Akajiweka kwenye gari na kisha akaanza safari ya kwenda kazini.
Akaendesha salama mpaka alipokuja kukuta foleni baada ya kama dakika arobaini na tano akiwa barabarani. Akiwa hapo, kwa kuepuka kuboreka kwa kungoja, akawasha redio na kuskiza habari za asubuhi.
Zikapita habari kadhaa, hakuzijali sana japo alizipa sikio. Kidogo akiwa anaskiza ndipo ikaja habari ya ghalfa juu ya ajali kubwa ilotokea huko kaskazini mwa Marekani, hapa akajikuta akiguswa na kujawa na umakini. Akategea sikio na akili yake yote kwa sauti aliyokuwa anaisikia redioni.
Basi akapata kupashwa kuwa moto mkubwa umetafuna msitu wa Orleans. Bahati hakuna taarifa ya mtu yeyote mpaka muda huo ambaye ameripotiwa kufa au kudhurika.
Habari hii japo ilipita na kuendelea na zingine, bado ikabakia kwenye kichwa cha Darren. Alipata kukumbuka juu ya moto ule uliokula msitu miaka ile ulivyommaliza mama yake katika namna ya ajabu. Alijikuta akimkumbuka mama yake, baba yake, bibi yake na hata Melissa!
Mawazo yake yote yalihama, na kwa muda akawa hana raha. Hata akajisahau kuwa yu barabarani na basi inabidi aweke msisitizo mkubwa asisababishe ajali kama si kuwakwaza wengine.
Alikuja kushtuliwa na honi kali nyuma yake maana foleni ilikuwa inaenda sasa. Naye akatia gari yake moto na kusonga mpaka kazini. Bado alikuwa ndani ya muda. Akajiweka kitini na kuanza kupangilia mambo yake atakayoanza kuyafanya moja baada ya jingine. Lakini kabla hajaanza, mawazo yale ya moto yakamteka tena!
Akabaki hapo kwenye kiti akiwaza sana. Alikuja kustaajabu amekula lisaa lizima na dakika zake tena akishtuka baada ya mhudumu akija kumuuliza kama angependelea chai au kahawa kwa siku hiyo.
“Mungu wangu!” Akalalama akitazama saa ya ukutani. “Nimechele …. Jack, niletee kahawa tu! … sawa? Haraka basi!”
Akaanza fanya kazi zake moja baada ya nyingine. Alipomaliza za makaratasi, basi akaenda ‘lab’ huko nako akahangaika kwa masaa kabla hajaenda kupata chakula cha mchana. Ni ndani ya jengo hilo hilo. Akiwa hapo anakula, naye mfanyakazi mwenzake aitwaye Roby akaja na kujiunga naye.
Alikuwa ni mwanaume ‘blonde’, mwembamba na mwenye kuvalia nguo zilizomzidi. Macho yake yalikuwa yamefunikwa na miwani yenye fremu nyembamba ya chuma. Mdomoni amebana toothpick.
“Hey, Darren!”
“Hey!”
Akaweka sahani yake yenye chakula mezani kisha akavuta kiti na kuketi.
“Unaendeleaje leo?”
“Nimebanwa sana na kazi. Ni siku ngumu.”
“Ooh! Pole, nami ilikuwa hivyo jana yake. Nadhani ni muda wa kufikiriwa kuongezewa mshahara sasa.”
Darren akaendelea kula pasipo kusema kitu.
“Darren, hauniungi mkono kwenye hilo?”
“Hata nikikuunga, itasaidia nini Roby?” Akasema Darren akitafuna. “Hamna cha kufanya. Kama kingekuwepo basi kingeshafanyika kwa muda mrefu tu.”
“Kwahiyo umeridhika na hali?”
“Roby, sina muda wa kuongea sana ndugu yangu. Natazamia nimalize chakula kisha nikamalize viporo vyangu.”
“Sawa. Ila Darren nina wazo …”
Darren akamtazama pasipo kunena kitu.
“Si jipya sana. Ni kuhusu lile wazo lako ulilowahi kunambia hapo kabla.”
“Wazo gani?”
“La kufungua sehemu yetu kule uliponambia.”
“Haiwezekani kwa sasa. Kwa muda ule kulikuwa kuna sponsorship. Haukuniunga mkono kwa woga wako. Sasa unadhani saa hii tutafanya nini? Una pesa hiyo?”
Kabla Roby hajajibu, Darren akanyanyuka na kugonga meza, “baadae, Roby!” Kisha akaenda zake. Akarudi ‘lab’ na kuendelea na kazi zake. Mpaka jioni akawa amemaliza huko. Sasa akawa amebakia na kazi ya kuandika ripoti tu.
Akiwa amejichokea, ila hana namna, akaandika ripoti hizo mpaka majira ya saa nne usiku. Watu waliondoka kazini na sehemu kubwa ya jengo ikawa ipo gizani kutokana na kutokuwa na watu.
Na zaidi kukawa kimya. Hata Darren akawa anasikia sauti ya keyboard ya tarakilishi kana kwamba honi ya gari. Kila alipokuwa anabofya ikawa inatoa mlio wa nguvu. Na ni kwasababu kulikuwa na ukimya tu eneoni.
Akiwa anaandika, mara akasikia jambo. Ilikuwa ni kama sauti ya watu wakiteta kwa umbali mdogo, basi akaacha kuchapa kazi yake na kusimamisha masikio. Punde sauti hiyo ikakoma. Basi naye akaachana nayo na kuendelea kuchapa kazi yake.
Akachapa kidogo, sauti ile ikajirudia tena. Alisikia watu wanateta japo hajui wanazungumzia nini. Na zaidi mmoja wao akaangua kicheko! Kicheko hicho kikavuma kana kwamba mtu huyo alikuwapo karibu kabisa. Na kwa namna kubwa kikamuogofya Darren!
Akatoka kwenye kiti chake na kuujongea mlango, akaufungua na kutazama nje. Hakuona kitu. Akapaza sauti, “helloooooow!” Napo hakusikia kitu isipokuwa mwangwi wa sauti yake kumrudia.
Akanyamaza akisimama hapo askize. Kidogo akasikia tena sauti za watu, zilikuwa zinatokea kulia kwake. Akapaza tena sauti, “Helloooow! Kuna mtu huko?”
Kimya. Mara akasikia kicheko na kilipokoma kukawa kimya kama shimoni. Akastaajabu. Akaanza kupiga hatua kwenda kule aliposikia sauti ile. Alipojongea mpaka mwisho, akaangaza kama ataona kitu. Hola!
Kidogo akasikia, ‘tap!’ Alipogeuza shingo yake kutazama nyuma, akaona taa ya ofisi yake imezimwa! Moyo ukamlipuka. Kabla hajafanya jambo, akasikia sauti kubwa ya kitu kama alarm! Mwili ukamtetemeka kwanguvu!
Alipoweka akili yake sawa ndipo akabaini huo ulikuwa ni mlio wa simu yake. Simu ilikuwa inaita. Basi haraka akaendea ofisi yake na kukamata simu, mkewe alikuwa anampigia. Alipopokea, akajongea ‘switch’ ya kuwashia taa na kuibofya. Hakukuwa na umeme!
“Bado upo kazini?” Mkewe aliuliza.
“Ndio, nipo kazini, ila …” akajaribu tena kwa kubofyabofya switch. Bado matokeo yalikuwa yaleyale. ” … ningoje maana nakuja muda si mrefu!”
Akakata simu na kukusanya kilicho cha kwake. Umeme haukuwapo hivyo asingeweza kuendelea na kazi tena. Akafunga ofisi na kutoka ndani lakini akilaumu kwani alikuwa amebakiza kazi kidogo sana amalize kabisa.
Akatembea kama hatua nane, mara umeme ukarudi! Akasimama na kujiuliza arudi ofisini ama aendelee na safari yake ya kwenda nyumbani? Basi baada ya kujiuliza huko kwa muda mfupi, akaona kheri akamalizie kazi kabisa kesho awe huru.
Akarejea na kuketi kitini kisha akawasha tarakilishi. Akaanza kuchapa na kuchapa. Ila hakudumu sana, akasikia tena sauti ya watu ikiteta na kucheka! Na mara hii, umeme ukamkatikia ndani ya ofisi!
Kidogo, akasikia sasa watu wakiteta ndani ya ofisi. Tena si mbali kabisa na yeye. Kwa kando ya kushoto.
***
Akaogopa sana hata kushikwa na kitete cha hofu kuu. Aliwahi simu yake na kumulika awaone watu hao lakini hakufanikiwa kuona jambo. Alikuwa mwenyewe tu!
Akatwetwa jasho akihema. Moyo nao ukaenda pupa. Akiwa amewasha taa ya simu, akakusanya kila kilicho cha kwake asibake tena hapo. Akauendea mlango na kuufungua, hamaki haukufunguka! Aliuvuta na kuuvuta lakini kazi bure. Mlango ulikuwa mgumu kwenda mbele wala nyuma!
Akastaajabishwa na hili maana hakuwa ameutia loki mlango huo. Akaangaza kushoto na kulia kama ataona ufunguo lakini napo ikawa kazi bure, hakuona kitu. Basi akazidi kupatwa na hofu. Akazidi kuhemkwa akihisi kabisa hayuko mazingira salama.
Akihisi kitu fulani kibaya kitamtokea muda wowote ule. Basi jasho likazidi kummiminika. Akalowana makwapani, mgongoni na kifuani. Paji lake la uso likajawa na maji yatiririkayo ingali macho akiwa ameyakodoa haswa.
_Hakukuwa na mtu wa kumsaidia?_ Akawaza kichwani. Alitazama dirishani asione jambo bali kiza tu. Akapata wazo la kuita. Kweli akaita kwanguvu mara tatu akiomba msaada kwa yeyote aliyekuwapo karibu.
Lakini kuita kwake huko akaja kukuona ni bure. Hakusikia muitikio wala kitu chochote kile. Akajikuta anapoteza matumaini ya kusaidiwa. Akaumwa na kichwa akiwaza afanye nini. _je avunje mlango?_
Ila mlango huo haukuwa mwepesi hata kidogo. Kama ni kuuvunja basi yampasa atumie nguvu kubwa sana maana hakuwa na dhana hata moja mkononi. Na akisha kuuvunja je? Nini atakuja kusema kesho yake kwa mkuu wake wa kazi akamwelewa?
“Darren!” Akasikia sauti ya kike ikimwita kwa kunong’ona. Haraka akageuka na kuangaza akitumia simu yake. Uso wake ulifumwa kwa hofu sana na mkono wake ulioshikilia simu ulikuwa unatetemeka!
“Nani wewe? Unataka nini kwangu?” Darren akafoka. Mara akasikia sauti ya kiume ikimjibu kwa nje, “mimi mlinzi! Wewe nani humo?”
Darren akabaini kuna mtu amekuja kumsaidia. Akachungulia dirishani na kumwona mwanaume aliyevalia zare akiwa amesimama hapo. Akamsihi, “nisaidie kufungua mlango tafadhali!”
Yule mlinzi akabinya komeo na mara mlango ukafunguka! Haukuwa umefungwa kabisa.
“Mbona mlango u’ wazi?” Akauliza mlinzi. Naye Darren hakuwa na majibu, na kwasababu ya kuona vitimbi, hakutaka kustaajabu, akajitoa nje na kufunga mlango huo.
“Nashukuru sana,” akamwambia mlinzi kisha akatupa miguu yake kujiondokea. Mlinzi akamtazama akiishilia kisha akatikisa kichwa na kusema, “ukisoma sana tabu pia.” Alafu akajiendea zake.
Darren akanyookea sehemu ya kuegeshea magari, akajipakia kwenye lile lililo kwake kisha akatimka. Hakuwa sawa kiakili. Na alijitahidi sana kuhakikisha hawazi yale mambo yaliyomtukia ofisini ili asije pata ajali barabarani kwasababu ya msongo.
Alipofika akamkumbatia mkewe kwanguvu na kumbusu kwenye paji lake la uso. Mtoto alikuwa tayari ameshalala.
“Darren,” Josephine akaita. Uso wake ulikuwa hauna furaha. Ulijawa na makunyanzi na macho yake yakiwa mekundu. “Nilikukumbuka sana. Saa tano hii yaelekea saa sita. Hujawahi kuja nyumbani muda huu.”
“Najua, mke wangu,” Darren akampoza. Akamkumbatia na kumwambia, “haitatokea tena. Nakuahidi.”
Basi Josephine hakuteta tena kuhusu hayo, akamwandalia mume wake chakula na kumkaribisha ale. Naye japo alikuwa tayari ameshakula, kwasababu ya kumpa motisha mumewe, akala pamoja naye.
Wakala kwa ukimya kwa kama sekunde kumi na mbili kabla Josephine hajauvunja ukimya kwa kumuuliza mumewe, “Ulisikia zile habari za moto?”
Darren akashtuka. Hata mkewe akatahamaki kwanini mumewe alishtuka vile. Bwana akasema, “sitaki hizo habari!’ Akiwa amekunja uso. “Sitaki kuzisikia hata robo. Sawa?”
Hata Josephine hakujibu. Alikuwa amebanwa na tahamaki. Darren akasimama na kwenda zake ndani akiwa ameacha chakula pale mezani.
_Ana nini huyu?_, Josephine akabaki akiduwaa. Akajiuliza akiwa anatazama kile chakula kilichobakia. Mwishowe akakipeleka jikoni na kisha akazima kila kitu aende kumkuta mumewe chumbani.
Alipofika huko, akamkuta Darren akiwa bafuni anakoga. Basi akamgojea kitandani amuulize kulikoni. Alipotoka akamwomba msamaha kama alimkwaza, halikuwa lengo lake.
Lakini pia akataka kujua nini kilikuwa kinamsumbua mumewe. Kwanini aligeuka na kuwa mbogo upesi hivyo? Tangu ameolewa naye hakuwahi kumwona akiwa vile. Shida kitu gani haswa?
“Josephine, sitaki kusikia habari zile ulizonambia. Huwezi jua zimenisababishia matatizo kiasi gani. Tafadhali nisizisikie tena. Nakuomba.” Huo ukawa usemi wa mwisho kwa Darren kabla hajajilalia. Na siku hiyo hakumkumbatia mkewe kama ilivyo ada.
Alijilaza kando ya kitanda akiwa anatazama ukutani. Mkewe naye akalala, tena haikuchukua muda sana akapitiwa na usingizi akimwacha Darren macho.
Baada ya muda kidogo, Darren akaamua kujigeuza na kumkumbatia mkewe. Hapo baada ya muda kidogo akabebwa na usingizi mzito. Alikuwa amechoka sana. Ni hofu tu ndiyo ilimkawiza.
Yalipotimia majira ya saa tisa ya usiku, muda wa shetani, majira ya malaika mkengemfu, Darren akagutuka toka usingizi asijue nini kimemwamsha! Alitazama kushoto na kulia kwake. Kote kulikuwa salama. Akarejesha kichwa chake kitandani aendelee kulala.
Lakini kabla hajaupata huo usingizi, ghafla ya ajabu akasikia mtoto akilipuka kwa kilio! Akashtuka sana. Mtoto huwa analala chumba cha pili yake hivyo ni ngumu kujua kinachomsumbua. Inamlazimu mtu aende kumtazama.
Basi akajaribu kumwamsha Josephine, ila akawa mzito. Aliishia kugugumia na kuguna. Naye Darren akawaza mwanamke huyo atakuwa amechoka kwa kulelea mtoto siku nzima, hivyo acha amsaidie kwa kwenda kutazama.
Akatoka kitandani na kufungua mlango, alafu akaelekea kule kwenye chumba cha mtoto kwa upesi. Alipoingia humo akamkuta mtoto akilia sana. Mdomo ameutanua na macho yake yanamwaga machozi.
Akamnyanyua na kumbembeleza. Baada ya muda kidogo mtoto akanyamaza lakini asilale. Akambembeleza tena zaidi na zaidi, bado hakuwa anataka kulala. Mpaka kwenye majira ya saa kumi inayoelekea saa kumi na moja, ndipo mtoto akaanza kufumba macho yake kwa usingizi.
Basi akamlaza na yeye kurudi chumbani akajilalie kwa muda mdogo uliobakia. Alichoka sana. Alipojiweka tu kitandani akajikuta akipitiwa na usingizi mkali wa kumlaza fofofo.
Kuja kuamka, ilikuwa ni saa nne ya asubuhi!
“Josephine! Josephine! Mbona hukunamsha lakini?” Akang’aka akiwa amewehuka. Alikuwa nyuma ya muda sana. Saa nne! Kazi gani hiyo ya kwenda muda huo?
“Nilikuamsha Darren!” Akasema Josephine. “Mara ya kwanza ukanambia nikuache ulale maana umechoka. Mara ya pili ukanambia nisikusumbue!”
“Mimi?” Darren akatoa macho akijinyooshea kidole.
“Ndio, wewe Darren!” Josephine akamjibu akimbembeleza mtoto. “Sasa ningefanyaje? Nikaona nikuache!”
Darren akajaribu kufikiria hicho anachomwambia mkewe. Hakuwa anakumbuka hata tone. _Yeye kusema hayo?_
Kama haitoshi, Josephine akamwambia kuwa, “uliamka mara ya tatu wewe mwenyewe. Ukaenda bafuni na kisha ukatoka kutazama dirishani. Nilipokuuliza hauendi kazini leo? Ukanijibu wataka kupumzika. Darren haukumbuki au wataka tu kun’tania?”
Darren akatikisa kichwa. Akajikuna kichwa akijaribu kuwaza lakini hakuwa anakumbuka lolote lile. Akachukua simu yake na kumpigia dada Fiona, secretary, kumuuliza juu ya kazini.
“Sikia Fiona, sijiskii vema. Naomba uniandikie note umpelekee boss.”
“Nimwambieje?” Fiona akauliza. “Muda huu kweli ni wa kutoa taarifa, Darren?”
“Tafadhali Fiona, fanya namna yoyote kunisaidia. Nitashukuru ukifanya hivyo.”
Kukawa kimya kidogo.
“Sawa,” Fiona akajibu na kuongezea, “na vipi kuhusu ofisi yako?”
“Imefanyaje?” Darren akauliza.
“Darren hujui ulichofanya?” Fiona akauliza kwa mshangao.
“Sijakupata, Fiona. Ni nini unaongelea?”
“Ofisi yako iko wazi, kila kitu kimevunjwa na kuchanwa. Nayo pia nimwambieje boss?”
Darren akaachama kwa mshangao.
Si kwamba hakuwa amesikia alichoambiwa na Fiona, lah, ila hakuwa anaamini. Akauliza, “Unasemaje, Fiona?”
Fiona akarudia tena kumwambia alichomwambia hapo awali. Basi Darren akakosa ustahimilivu, akasimama na kujiandaa upesi aende huko tofauti kabisa na alivyokuwa ameshapanga. Ndani ya muda mfupi akawa kwenye gari lake, upesi akatimka.
Akiwa barabarani, akitingwa sana na mawazo, almanusura kumgonga mpita njia. Ni shukrani gari lake liliweza kusimama kwa wepesi kabla ya kumsomba mhanga. Akasimamisha gari na kushusha pumzi ndefu apunguze mihemko na kujiweka sawa kisha akaendesha tena mpaka ofisini.
Huko mtu wa kwanza kuonana naye akawa ni Fiona. Akiwa ametweta, akamwambia, “Tafadhali, Fiona. Nambie kilichojiri.” naye Fiona akamweleza kinaganaga kuwa ofisi yake imekutwa wazi na ikiwa shaghalabaghala!
“Lakini imewezekanaje?” Darren akastaajabu. “Jana nimeondoka baada ya kuifunga!”
Fiona akapandisha mabega. “Darren, nitayajuaje yote hayo?”
Darren akauliza, “Bossi yupo ndani?” Fiona akamjibu kwa kutikisa kichwa. Darren akanyookea huko. Akagonga mara moja na kufungua mlango. Boss alikuwa amejilaza kwenye kiti chake kirefu akiwa amekumbata viganja vyake. Amevalia suti nyeusi na tai nyekundu.
Darren akajieleza kwanini hakuwapo kazini siku hiyo, kuwa anaumwa, na hayo ya ofisi kukutwa wazi na vitu vikiwa hovyo, yeye hana habari nayo. Basi Bossi akamsikiza mpaka alipomaliza kisha asiseme jambo, hata salamu akiwa hajaitikia, akafungua droo ya meza yake na kutoa barua bahashani, akampatia Darren.
Darren akaitazama barua hiyo na kumuuliza, “Ya nini?”
“Utakapoisoma, utajua ya nini?” Mkuu akamwambia na kisha akamwonyeshea mkono mlangoni.
“Tafadhali, mkuu,” Darren akaomba. “Uniskize na kila ninachokuambia toka kwenye kinywa changu ni cha kweli tupu.”
“Darren!” Boss akaita kwa sauti kuu. “Naomba uende!”
“Tafadhali, naomba uniskize,” Darren akaendelea kuomba. Basi Boss akamwambia, “kaniletee hiyo kazi unayonambia uliifanya hiyo jana usiku!”
Upesi Darren akatoka na kwenda ofisi kwake. Huko kweli akakuta vitu vikiwa hovyo sana hata akatahamaki asipate majibu. Akajaribu kutazama tarakilishi yake, nayo ilikuwa imepasuliwa kioo, mashine ilikuwa chini! Akaishiwa na nguvu.
Akajikuta akikaa chini akiwa ameshika kichwa chake. Hakuwa anajua cha kufanya. Hakuwa anajua nini cha kusema. Kwa kama dakika tano akiwa amekaa hapo akapata wazo la kwenda kuonana na mlinzi. Alipoenda kwenye kibanda chake, hakumkuta. Mlinzi huwa anakuja nyakati za jioni na si muda ule.
Basi Darren akajikuta hana cha kujitetea. Akiwa ameinamisha kichwa chake chini akajongea kujiondokea. Kabla hajafika langoni, akaitwa, alipogeuka akamwona Roby.
“Ngoja, Dareen!” Roby alimpungia akikimbia. Alipomfikia akamwomba wakaketi kule mgahawani kwani anataka kuteta naye kidogo. Basi wakaongozana kwenda huko, na walipoagiza chakula, Roby akasema, “Nimesikia habari zako, Darren. Ni nini kimetokea?”
Darren akamweleza yale anayojua. Roby alipoyasikia akashangazwa, lakini hakusita kumpatia moyo. “Yote ni maisha, Darren. Nadhani sasa ni muda wa kuangalia mlango mwingine.”
Akamshika bega na kumwambia, “Ni muda wa kufanyia kazi lile shauri lako hivi sasa.”
“Nitawezaje, Roby?” Darren akasema kwa sauti ya chini. Macho yake yalikuwa yameingia ndani. Mdomo wake umemkauka. “Sina pesa hivi sasa. Nitawezaje kuyafanya hayo?”
Roby akatikisa kichwa. Akafikiri kidogo kisha akamwambia, “Ebu ngoja. Nadhani kuna kitu tunaweza kufanya. Niachie hii siku na kesho yake, nitakutafuta. Sawa?”
Basi Darren alipomaliza kula akajiendea zake. Alikuwa ametingwa sana na mawazo. Hata alipofika nyumbani kwake, mkewe akatambua kuwa mumewe hakuwa sawa. Alipomuuliza nini shida, Darren akampatia barua toka kwa bosi wake. “Nimefukuzwa kazi.”
Josephine akasoma barua hiyo na mpaka alipomaliza, machozi yakawa yamemjaa machoni mwake. Alikuwa amevunjika moyo, lakini akamtia moyo mumewe. “Usijali. Ni changamoto za maisha tu. Litapita.” kisha akambusu na kujilaza kifuani mwake.
Siku hiyo ikaenda Darren akiwa na mkewe na mtoto wake. Hata siku inayofuata wakaamka na kudumu siku nzima nyumbani. Darren akacheza na mwanaye na pia mkewe. Ilikuwa ni siku nzuri. Hakuwahi kukaa na familia yake katika namna ile tangu pale alipoipata. Kwa muda akasahau matatizo yake.
Siku iliyofuata, kama vile Roby alivyomuahidi, akamtafuta kwa njia ya simu. Walipoongea wakapanga kuonana majira ya jioni Roby akitoka kazini. Basi majira hayo yalipofika, Darren akaenda nyumbani kwa Roby kukutana naye.
Wakateta kujuliana hali kabla Roby hajaanza kumwambia Darren lengo la wito wake hapo.
“Lile wazo lako laweza kutimia Darren. Tunachokihitaji hivi sasa ni dhamira ya kweli, na si pesa!”
“Umepata pesa?” Darren akawahi kuuliza akitoa macho.
“Tuliza munkari, Darren,” Roby akasihi. “Sijapata pes yoyote, ila pesa ipo. Tunachotakiwa kufanya ni kuandika muswada wa mipango yetu, muswada mzuri wa kueleweka, alafu kuna mahali tutapeleka na kupata pesa.”
Darren akanywesha uso. “Roby, unadhani ni kitu chepesi namna hiyo?”
“Skiza, Darren. Najua ninachokuambia. Na ninakuambia kwa uhakika wote. Kuna kampuni mimi nimeshaongea nayo, nao wako radhi kusaidia kwa kila namna. Niamini mimi. Najua wewe ni mzuri kwenye maandishi, andika hiyo kazi nami nitakuonyesha namna mambo yanavyokwenda,” alisema Roby kwa kujiamini kisha akanyanyua glasi yake ya kinywaji na kuigongesha na ya Darren.
“Tutafanikiwa, Darren. Amini hivyo.”
Basi Darren akarudi nyumbani akiwa na mwanga wa matumaini. Akamkumbatia mkewe na kumjuza habari hizo, naye mkewe akafurahishwa sana. Akamwombea afanikiwe zaidi na zaidi.
Ulipofika usiku wa saa mbili, akaanza kuandika ule muswada ambao Roby alimtaarifu. Akaandika kwa ustadi akitumia masaa. Alipomaliza akausoma tena upya na upya. Akarekebisha aliyoyaona yanastahili, kisha akajilaza ikiwa ni saa tisa kasoro usiku.
Kesho yake akaonana na Roby na kumpatia ile kazi. Naye Roby akaipitia na kupendezwa nayo sana. Akatabasamu na kumwambia Darren, “Tumeshapata pesa hapa!”
Akamwahidi wataonana mwisho wa juma tena akiwa na majibu ya maana. Na kweli ilipofika mwisho wa juma, Roby akamwambia Darren wakutane kumpatia majibu ya ule muswada, ila si nyumbani tena bali kwenye jengo refu la HIGH TOWERING CONSULTANCY.
Darren akiwa na hamu kubwa, akajongea huko. Akakutana na Darren na mwanamke mrembo aitwaye Isabel. Mwanamke huyo alikuwa amevalia suti ya kijivu ilivyomkaa vema. Uso wake ulikuwa umepambwa na miwani nzuri ya macho. Nywele zake nyeupe na laini.
Kwa makadirio alikuwa na miaka thelathini na tano, sita ama saba. Hakuwa mnyimi wa tabasamu. Tabasamu lake zuri. Na alikuwa mtu mchangamfu, nadhifu mwenye macho ya kuvutia.
Roby akamtambulisha Darren kwa Isabel na kisha Isabel akajitambulisha kwa Darren kama ‘Executive Director’. Waliposalimiana na kutambulishana Isabel akakiri kuvutiwa na ule muswada na basi wao kama kampuni watawekeza takribani dola za kimarekani milioni kumi!
Swala hilo likamgusa sana Darren. Haukuwa uwekezaji mdogo huo kabisa. Aliona sasa ndoto yake inaenda kukamilika. Akashukuru na kisha akauliza ni kivipi uwekezaji huo utakuwa unarejeshwa.
Isabel akatabasamu kwanza kabla hajajibu, “ni mpaka pale mtakapoanza kutengeneza faida. Kampuni itakuwa inachukua gawio la asilimia ishirini tu la faida yenu nzima!”
Darren akaridhia. Akamkumbatia Roby akimwona kama malaika mwokozi kwake. Wakafungua akaunti ya pamoja na pesa ikaingizwa baada ya siku mbili tu. Na pasipo kukawia wakapata eneo na kuanza kulifanyia kazi kutengeneza mazingira mazuri kwa ajili ya huduma za tiba ya wanyama.
Kwa kama mwezi mmoja tu, kila kitu kikawa tayari na huduma zikaanza kutolewa. Isabel naye akatembelea hilo eneo na kuomba kupewa mrejesho wa maendeleo ya huduma kila mwisho wa mwezi, lakini zaidi alikuwa amekuja na mbwa wake kwa ajili ya kumpatia chanjo.
Darren akamshughulikia kikamilifu na Isabel kabla hajaenda, akampatia Darren kadi yake ya biashara.
“Utan’tafuta utakapokuwa na tatizo.”
Kisha akamtazama Darren machoni na kumwambia, “Sawa?”
Darren akajibu, “Sawa.” akitabasamu.
Aliporudi nyumbani alikuwa amechoka sana, lakini kabla hajajilaza akapata kuongea na mkewe juu ya maendeleo yake ya kazi. Mkewe naye akafurahishwa sana na hatua za mumewe, basi zaidi akamtia moyo.
Akamsihi tu kuwa anampenda na kila anapokuwa anakutana na gumu lolote basi akumbuke kuwa familia yake inampenda sana. Usiku ukawa mzuri na hata walipoimalizia kwa kula na kuoga.
Kesho yake kama ilivyo ada, Darren akaamka na kwenda kazini. Akafanya sana kazi pamoja na mwenziwe, kisha jioni ilipoingia Roby akamhasa waende mahali kupata chochote kitu kabla hawajaachana. Naye Darren akapendezwa na hilo wazo.
Wakaenda kwenye moja ya mgahawa wa KFC, hapo wakaagiza chakula na kinywaji. Wakala wakifurahia utamu wake na huku wakipiga soga za hapa na pale.
“Darren,” Roby akaita na kusema, “Nadhani sasa ni wakati wa mimi kuoa!”
Darren akashangazwa. “Kweli?” Akamtazama Roby akikodoa.
“Ndio. Nina mpango huo. Vipi wasemaje?”
“Sina neno. Ni wazo zuri ila sijawahi kumwona mpenzi wako. Huwa unamficha kwa wivu nini?” Darren akasema na kisha wakaangua kicheko.
“Hapana ndugu. Nadhani tunapishana muda ndo’ maana hujapata kumjua. Mwisho huu wa wiki tutakutana wote, nitamvesha pete ya uchumba!”
“Wow! Ni wazo zuri sana. Nami nakuunga mkono, Roby. Bila shaka itakuwa siku nzuri sana baina yetu.”
“Ni kweli. Nampenda sana mchumba wangu. Japo bado mambo hayajakaa vema, naona ni muda stahili wa kumwonyesha mapenzi yangu kwake.”
“Nakupongeza sana kwa hilo. Vipi itakuwa ni surprise ama?”
“Ndio, itakuwa ni surprise. Naomba unipe wazo juu ya hilo, Darren. Sitaki aone kama niliyekuwa nikiyapanga yote haya.”
Basi Darren akampatia mawazo yake naye akayapenda sana. Wakakubaliana cha kufanya na muda wa kuyafanya kisha wakaagana na kila mmoja akaenda na njia yake.
Darren alipofika nyumbani akampasha habari hizo mkewe. Naye akafurahishwa nazo sana. Akakumbuka kipindi Darren anamvesha pete. Ilikuwa ni siku ya ajabu asiyoweza kuisahau maishani mwake.
“Ile siku ilikuwa ya kusisimua sana, Darren. Nami siwezi kusahau tabasamu lako na namna ulivyonipigia magoti. Haki ulifanya moyo wangu ukimbie kwa haraka. Nilijihisi fahari sana.”
Darren akafurahishwa na hayo maneno. Akanyanyuka na kumbeba mkewe kisha akamuuliza, “Na vipi kuhusu siku ile nilipokuwa nawe kanisani?”
Josephine akacheka kidogo akiziba mdomo wake kisha akatazama dari. “Loh! Ile ilikuwa ni siku ya maajabu kwangu, Darren! Nakumbuka kila jambo tangu asubuhi mpaka usiku wake. Nawezaje kusahau?”
Basi Darren akampeleka mkewe chumbani na kumlaza kitandani. “Tazama. Wewe ndiye furaha yangu ya kweli. Upendo wako umejaza ndani ya moyo wangu na mimi nafurahia uwepo wako kila siku.”
Ni kweli Darren alimpenda sana mkewe. Alishamsahau kabisa Melissa na vimbwanga vyake. Hakuwa anamkumbuka tena mdhalimu huyo. Mwanzoni hakuwa anaamini kama atakuja kumsahau Melissa. Alikuwa ameganda sana kwenye kichwa chake. Alimpa sana moyo wake. Ila kwa sasa dunia ilikuwa imegeuka.
Tena imegeuka na kubadili mhimili kabisa.
Lakini kwa Melissa …
Vipi kwa Melissa?
Darren hakuwa anajua. Na natamani asingekuwa analijua kamwe. Melissa alikuwa karibu yake kuliko alivyokuwa anadhani. Melissa alikuwa karibu yake pengine kuliko muda wowote ule.
Melissa alikuwa anafanya kazi yake. Tena taratibu na kwa ustadi wa hali ya juu. Mkono wake ulikuwa unagusa njia. Masikio yake yanaskiza upepo ukitikisa vipande vya majani. Sauti yake inaimbia fukweni mwa bahari.
Machho yake yakitawanyika kila pande. Na ndimi zake zikiwa zinasukutua mdomo kwa kila kona yake.
Melissa alikuwa ni shetani ambaye Darren asingewahi kumwazia kuwa. Ile tamu kwenye chungu. Lile tone la sumu ya mamba kwenye maji yaliyojaza jaba la miamba.
Siku zikapita, tena zikikimbia haswa. Na ile siku ya Roby kumvesha pete mchumba wake ikawadia. Siku hiyo Darren na Roby wakawasili mapema sana. Wakatengeneza mazingira ya kufanya mambo yao, ilikuwa ni pembeni ya fukwe ya bahari, na muda wa mchumba wa Roby kuwasili ulipowadia, Darren akajificha.
Walikuwa wameadhimia punde pale mpenzi wa Roby atakapotokea, basi Darren atajivika barakoa usoni na kuigiza amemkaba Roby na kumchoma kisu. Lakini kwa wakati huo huo atampatia Roby kijumba cha pete, hivyo wakati mchumba wa Roby atakapokuwa anamlilia mpenzi wake anayekufa, Roby atatoa kijumba cha pete na kumwomba akubali kuwa mke wake!
Ulikuwa ni mchezo wa hatari.
Basi Roby akamkumbatia mpenzi wake na kumuuliza kama amefurahia kuwapo hapo mwisho huo wa juma. Naye mpenzi wake akasema amefurahia.
Naye mpenzi wake huyo alikuwa ni Melissa.
Uzuri wake ulikuwa upo palepale. Macho yake mazuri ya kumlaghai nyoka atoke shimoni. Uso wake mtamu na sauti ya kukimbiza mapigo ya moyo.
“Kwanini umeamua kunileta ufukweni, Roby?” Melissa akateta kwa sauti yake tamu.
“Haujapapenda?” Roby akauliza wakiwa wanasonga mbele.
“Nimepapenda,” Melissa akamjibu. “Ila sikuwa nadhani kama utanileta huku. Kama ningelikuwa najua na kujipanga basi ningebeba na nguo za kuogelea. Au wewe umebebelea?”
“Hapana. Nipo kama nilivyo mpenzi.”
Basi wakazidi kusonga mbele zaidi na zaidi Roby akimvuta Melissa eneo la tukio. Ndani ya moyo wake alikuwa ana hamu kubwa ya kumshangaza Melissa. Alitamani kumwambia kuhusu mpango wake ila akajitahidi kujibana. Alitamani kupayuka kwa kupaliwa na furaha lakini akajibana sana.
Wakazidi kusonga.
Walipopiga hatua kama tatu tu ndipo Darren akawa amehakiki kile alichokuwa anakiona. Alimwona Melissa! Mwanamke aliyekuwa amemsahau. Alimwona Melissa, mwanamke mwenye kubebelea kitanzi mkononi mwake!
Akabaki akiduwaa, ameachama mdomo na kung’aza macho yake. Na pasipo kutarajia, Melissa akarusha macho kumtazama pale alipokuwapo. Macho kwa macho wakakutana.
Sehemu Ya 5
“Melissa!” Darren akatamka akitikisa kichwa chake. “Niache Melissa!” akanong’oneza. “Niache Melissa!” kisha akajikusanya na kukimbia sana. Aliliendea gari lake na kuzama ndani akitupia barakoa yake pembeni.
Hakuamini alichotoka kuona. Ni kweli amemwona Melissa! Moyo wake ulimwenda mbio mno. Akahema sana akitokwa na jasho. Akataka kuwasha gari aende lakini mikono ikamtetemeka sana. Akaona ni kheri angoje kwani anaweza pata ajali akilazimisha kwenda.
Kule fukweni Roby akangoja sana. Akatazama kushoto na kulia akiwa anaishiwa na uvumilivu. Darren yuko wapi?
“Mpenzi,” Melissa akaita na kuuliza, “Kuna tatizo?”
“Hapana. Hamna ta–” Roby akateta akitupa macho. “Hamna tatizo!”
Basi baada ya kukaa sana hapo pasipo kuona kitu, akaamua kuondoka zake na mpenzi wake. Moyoni akabeba kinyongo kikubwa juu ya Darren. Akabeba pia na maswali, kwanini Darren amemfanyia hivyo? Kama kungalikuwa na tatizo si angemwambia mapema?
Moyo wake ukawa mzito. Akaghafirika sana.
Walipoenendea mahali ambapo Roby alipakia gari, Melissa akazama ndani lakini Roby akang’aza tena macho kama atamwona Darren. Bahati upande wake wa kulia, kwa mbali, akaona gari la Darren! Basi akalijongea upesi akimwambia Melissa amngojee kwa dakika chache.
Alipolifikia gari hilo, kwa ndani akamwona Darren, basi akaanza kufoka kabla hajafika, “Mambo gani hayo Darren unanifanyia? Ikama ungalikuwa hautaki si ungelinambia?”
Akachngulia dirishani kumtazama Darren. Akamwona akiwa amefumba macho kama mtu aliyemezwa na usingizi. Lakini matundu ya pua yake yakiwa yanachuruza damu kwa wingi!
Akatahamaki! “Darren!” akaita akifungua mlango upesi. Akamtikisa Darren kwanguvu akimwita lakini Darren hakuitikia kabisa. Zaidi damu zikarukia mpaka kwenye mikono ya Roby. Basi upesi Roby akamhamishia Darren kwenye kiti cha abiria na kisha akawasha gari kumwahisha Darren hospitalini upesi awezavyo!
Akiwa njiani, Darren akanong’ona kwa mbali, “Ni jini … Roby, Roby, ni jini … atakuua … ata–”
“Nini unasema Darren?” Roby akapaza sauti kuuliza, akitamani kumtazama Darren, akitamani kutazama barabara. Lakini Darren hakuweza kuongea tena. Macho yakajawa na ukungu na mwishowe akapotelea kabisa gizani.
“Roby …
Walipofika hospitali, Darren akatwaliwa na upesi akapewa msaada wa haraka kabla hajalazwa kupumzika. Roby akampigia simu mke wa Darren kumtaarifu na basi muda si mrefu mwanamke huyo akiambatana na mwanaye wakafika eneo la tukio.
Mwanamke huyo alikuwa amejawa na woga sana. Alipomwona mume wake chozi likamtoka akistaajabu ni nini kitakuwa kimemkumba.
“Sijui!” alisema Roby. “Nilimkuta akiwa ndani ya gari anachuruza damu!”
Basi wakaketi kungoja taarifa ya daktari. Muda kidogo Daktari akaja na kuwatoa hofu kuwa mgonjwa anaendelea vema, na kama hali yake ikitengemaa basi anaweza pia kuondoka ndani ya siku hiyo.
“Hatujaona kingine isipokuwa maumivu makali ya kichwa ambayo husababishwa sana na fatigue na msongo wa mawazo. Kila kitu kitakuwa sawa. Msijali,” alisema Daktari kabla hajaondoka zake.
Roby akawasiliana na Melissa na kumwelekeza ajiondokee atamkuta nyumbani kwani amepata udhuru. Melissa akastaajabu. Akamuuliza Roby ni wapi yupo naye aje kumwona.
“Hapana, Melissa. Hamna haja hiyo. We nenda nami nitakuja na kukueleza kila kitu. Sawa?” Melissa akakubali japo kwa shingo upande.
Roby akakaa hapo na Josephine mpaka majira ya jioni kuelekea usiku. Daktari alikuja na kuwaambia hali ya mgonjwa bado haijakaa sawa kiasi cha kumruhusu. Pengine kwa kesho mambo yatakuwa sawa.
Basi kwa utaratibu ikabidi abakie mtu mmoja na mwingine arejee nyumbani. Josephine akasisitiza yeye abaki, lakini angewezaje na ingali alikuwa na mtoto? Roby akamsihi aende nyumbani na yeye abakie na mgonjwa hapo mpaka jua litakapochomoza tena.
Swala hilo likawa gumu sana kwa Josephine. Aliwaza atalalaje pasipo mumewe? Hakuwahi kufanya vivyo tangu waoane. Lakini zaidi hakuwa anaamini kama mumewe atakuwa salama mbali na mikono yake.
Hakuwa na namna. Ilimpasa tu aende. Basi akaaga lakini akiahidi kuja hapo hospitalini asubuhi na mapema kumwona mumewe.
Alimkumbatia Roby na kumwambia, “Naomba umtazame vema.” macho yake mekundu yalikuwa yanachuruza machozi. Akaaga na kwendaze.
Akiwa anaenda, ndipo Roby akapata wazo la kumpeleka Josephine nyumbani kwake. Akamwita na kumwambia hilo wazo lake lakini Josephine hakuridhia. “Hapana. Baki hapa na Darren. Yeye anakuhitaji kuliko mimi.”
Roby akamsihi sana. Haitachukua muda mrefu kwani atamkimbiza na kurudi ndani ya muda. Asingejisikia vizuri kama angemwacha mwanamke huyo ajiendee mwenyewe. Kishingo upande, Josephine akaridhia. Roby akampakia kwenye gari na kuanza safari ya kuelekea nyumbani.
Wakiwa njiani, Josephine akampa pole Roby kwa yale yote yaliyotokea kwenye siku yake hiyo muhimu. “Ilitakiwa uwe una furaha mua huu. Nahisi hisia zako. Pole, Roby.”
Roby akatabasamu kwa huzuni. “Mambo hubadilika haraka,” akasema akiwa anatazama zake mbele waendapo. “Sikutarajia kama yangekuwa haya. Pengine hii haikuwa siku nzuri.”
“Mpenzi wako amekuelewa lakini?” Jospehine akauliza.
“Yeye hajui kinachoendelea,” Roby akamjibu. “Hakuona kitu. Ni mimi pekee ndiye niliyeshuhudia na kuchukua hatua ya kumkimbiza Darren hospitali!”
“Nashukuru sana Roby.”
“Huna haja ya kunishukuru, Jose. Ni jukumu langu. Darren ni rafiki na mshirika wangu. Kama nisingelifanya hivyo, nani mwingine angelitekeleza?”
Basi wakaendesha mpaka nyumbani kwa Darren, hapo Josephine akashuka na kumshukuru Roby alafu na kumuaga. “Uwe na safari njema. Tutakutana kesho mapema, Roby.”
Roby akatabasamu kuitikia kabla hajawasha gari na kurudi moja kwa moja hospitali. Huko akamkuta bado Darren hajapata ufahamu wa kusema anaweza kuongea. Basi akaketi zake sehemu ya kupumzikia na kutoa simu yake mfukoni kumtumia ujumbe mpenzi wake.
“Hey! Umelala?”
Baada ya muda kidogo ujumbe ukajibiwa, wakawa wanachat.
“Bado. Si umesema nikungoje?”
“Yah! Ila nahofia sitaweza kurudi usiku huu, Melissa.”
“Kwanini? Umeniahidi, Roby.”
“Najua. Ni jambo kubwa sana lilionizuia. Rafiki yangu ameumwa ghafla na kulazwa hospitali, sitaweza kumwacha. Nadhani unaona.”
Kukawa kimya kidogo. Roby akatuma tena ujumbe. “Umelala?”
“Hapana.”
“Umekasirika?”
“Hapana.”
“Usiwe hivyo mpenzi. Sikufanya kwa kudhamiria. Natumai unaelewa.”
“Sawa. Nikutakie usiku mwema, Roby.”
Ujumbe huo ulipoingia kwenye simu ya Roby, mwanaume huyo akatikisa kichwa na kung’ata simu yake kwa mawazo. Alishatambua kuwa Melissa alikuwa amekaraishwa. Basi akawaza kitu cha kufanya, mwishowe akaona ni vema atoke upesi kwenda kumwona Melissa alafu atarejea kwa Darren.
Wazo lake hilo likapitishwa na moyo wake pasipo kushirikisha ubongo. Akatumai akimwona Melissa basi ataweza kusuluhisha mambo. Akaendesha upesi na ndani ya nusu saa akawa yu kwenye makazi ya Melissa. Aligonga mlango na punde mwanamke huyo akamfungulia na kumkaribisha.
“Mbona upo hapa? Haukusema upo hospitali?” Melissa akauliza akiketi kitandani.
“Ndio, nilikuwepo huko,” Roby akajibu na kuongezea, “Niliona nije kukuona kwanza alafu nitarejea huko.”
Melissa akamtazama Roby kabla hajamwambia kwa ufupi, “Pole.”
Basi Roby akambembeleza mpenzi wake huyo na kumsihi awe na furaha kwani anataka awe hivyo kila atakapokuwa na yeye, lakini Melissa akasisitizia kutaka kujua wapi ambapo Roby alimpeleka rafiki yake, naye Roby pasipo kusita, akamjuza.
“ … Amelazwa huko. Nadhani kesho ataruhusiwa.”
Melissa alipojua alichokitaka, akaanza kumrembulia Roby akisaula nguo zake. Akamshawishi Roby alale naye kwani alikuwa ana hamu, naye Roby akashindwa kujizuiza, akalala na Melissa.
Punde tu walipomaliza kufanya tendo hilo, Roby akapitiwa na usingizi mzito sana. Alijikuta akiwa hajielewi. Mwili ulikuwa mzito mno. Hajiwezi.
Basi Melissa akatabasamu kabla hajajitoa kitandani na kujivesha nguoze. Alafu akauendea mlango na kuufungua atoke nje.
**
Kwa mbali alisikia sauti za watu wakiteta, akageuza shingo yake kutazama huko sauti zinapotokea lakini hakuwa amefungua macho.
Darren alikuwa anajihisi mchovu sana. Mwili wake umekuwa mzito na mpungufu wa nguvu. Kabla hajafungua macho akajiuliza kchwani mwake nini kilimtokea. Anajua yu hospitali lakini hakuwa anafahamu alifikaje hapo.
Akiwa anajaribu kukumbuka hilo, akajikuta akijiwa na jina la Melissa kichwani mwake! Akaukunja uso wake na kunong’ona, “Melissa … Melissa …”
Basi akafungua macho taratibu sasa aangaze kule ambapo sauti inatokea. Ilikuwa ni dirishani. Alipotazama huko akamwona Melissa akiwa amesimama kando. Mkono wake ameuweka kwenye kioo cha dirisha na macho yake yanamtazama!
Kinywani akahisi Melissa akiita, “Darren … Darren …” alafu mwanamke huyo akatabasamu na kupunga mkono wake.
***
Darren akajikuta akikodoa zaidi. Bado Melissa yupo palepale. Akafikicha macho yake na kuangaza tena, bado Melissa yupo palepale! Akatahamaki. Mapigo yake ya moyo yakamwenda mbio sana. Mwishowe akapoa tu na kumtazama Melissa kwa macho ya pole.
“Melissa,” Darren akaita kwa kunong’ona. Melissa kule kiooni dirishani akatikisa kichwa chake kuitikia. Ilikuwa ni ajabu ni kwa namna gani amesikia. Na kwa kujibu akasema kwa kupanua mdomo wake pasipo kutoa sauti. Umbo la kinywa chake kikisema, “Nimekumiss Darren. Nakupenda.”
Kisha mwanamke huyo akavujisha machozi na kujiondokea. Darren akaangaza pale kiooni pasipo kuona mtu tena. Akafikicha tena macho yake na kuyatupa. Hakuona jambo! Akabaki akihema na kujiuliza.
Kile alichokiona ni cha kweli ama ni macho yake ndiyo humdanganya? Akajiuliza sana. Kichwa kikaanza kumuuma tena, na damu zikaanza kumtoka puani.
Kidogo maumivu yakawa kama mionzi inayomkata kichwa. Mwishowe akashindwa kustahimili na kujikuta akipoteza fahamu! Baada ya kama dakika nane tangu alipopoteza fahamu, daktari akaja na kumkuta kwenye hali hiyo mbaya. Upesi akamsaidia kitaalamu na kisha akampatia mwanya wa kupumzika.
Ila daktari akapata maswali juu ya hali hiyo. Imekuwaje mgonjwa akarejea tena kwenye hali ya mwanzo na ingali alikuwa anaendelea vema hapo kabla? Hakujua kuwa mgonjwa wake alirejea kwenye rundo la mawazo kwa mara nyingine tena.
Basi asubuhi ilipowadia, ile ya saa kumi na moja. Josephine akarejea hospitali akiwa amebebelea juisi aliyomtengenezea mume wake. Si kwamba juisi hizo hazikuwa zikipatikana hospitali na maeneo ya karibu, lah, alitaka tu mumewe atumie kitu alichotengeneza kwa mikono yake mwenyewe. Alihisi hicho ndicho kitu sahihi. Kitu anachotakiwa kukifanya.
Alipotazama hakumwona Roby. Akamuuliza nesi juu ya uwepo wa bwana huyo, akaambiwa ya kuwa aliondoka usiku wake, hata hakulala hapo. Josephine akaghafirika sana. Hata akajilaumu kwanini hakubaki na mumewe. Alihisi ni yeye peke ndiye anajua umuhimu wa mume wake.
“Kwanini Roby alifanya hivyo?” akajiuliza. “Kama hakuwa anaweza kulala hapa, si angeliniambia nikajua cha kufanya!” ila mwishowe akashukuru tu kwa kumkuta mumewe ni mzima wa afya. Hilo ndilo la muhimu.
Kidogo, kwenye majira ya saa mbili asubuhi, Roby akafika hospitali akiwa ameshika kichwa chake na mkono wa kuume. Mwendo wake ulikuwa wa kasi sana, na uso wake ukiwa mithili ya mtu aliyechanganyikiwa.
Alipomwona Josephine, akasita. Akamtazama mwanamke huyo kwa muda kidogo akijiuliza kisha akaamua kusonga na safari yake. Alipomfikia Josephine akamsalimu, naye Josephine akamuitikia na kunyamaza kimya.
“Mgonjwa anaendeleaje?” akauliza kwa aibu.
“Anaendelea vema,” Josephine akajibu akimtazama mwanaye aliyekuwa amemlaza mapajani.
“Samahani, Josephine. Hai –”
“Usijali, Roby. Wa kuomba msamaha ni mimi kwa kukupatia majukumu makubwa.”
“Usiseme hivyo Josephine. Haikuwa dhamira yangu kufanya hayo. … yani siwezi hata … kuelezea. Nisamehe tu Joephine. Najua nimekukosea. Nimemkosea pia na Darren.”
“Nimekusamehe, Roby. Hamna shida.” baada ya Josephine kusema hayo, hakurudia tena kusema kingine. Akanyamaza akihangaika na mtoto wake. Roby akaenda kumtazama mgonjwa na kisha akarejea tena pale sehemu ya mapumziko. Kidogo Daktari akaja na kuwapa taarifa juu ya kile kilichotokea majira ya usiku, lakini akawapa moyo.
“Sidhani kama kitatokea tena. Kama hali yake itaendelea kuwa kama ilivyo sasa mpaka majira ya jioni, basi tutamruhusu aende nyumbani.”
Basi baada ya muda kidogo, Roby akamuaga Josephine kuwa anaenda kazini kutazama mambo kadhaa lakini baadae atarejea tena kumjulia hali Darren. Alipoondoka hapo akaenda kwanza nyumbani kuonana na Melissa kabla hajaendelea na kazi zake.
Akamlaumu sana Melissa kwa kitendo chake alichofanya usiku kwani amefanya mpaka akashindwa kurudi hospitalini mapema. Melissa hakujali sana kuhusu Roby. Hakuwa anamskiza. Akiwa amejilaza kitandani, alikuwa akitazama dari kwa kujawa na mawazo.
Roby alipomaliza kuongea, akamuaga Melissa kuwa anaenda zake, wataonana baadae. Hapo ndipo Melissa akamtazama na kumuuliza kumhusu mgonjwa. “Ameshatolewa hospitali?”
Roby akaghafirishwa. “Ina maana yote niliyokuwa naongea yalikuwa upuzi?”
“Nani kasema ya kipuzi? Sikukuskiza? Au ulikuwa unataka nifanye nini?”
Roby akashusha pumzi ndefu. “Sitaki kugombana na wewe, Melissa.”
“Nani anataka kugombana nawe, Roby?” Melissa akauliza. Roby asijibu, akauendea mlango aende zake. Lakini kabla hajatoka, Melissa akapaza sauti yake. “Nimeuliza mgonjwa ameshatoka hospitali?”
Roby akamtazama Melissa kwa kama sekunde tano na kisha akajibu, “Hapana.” alafu akajiendea. Huku nyuma Melissa akapaza mlango ukiwa umeshafungwa, “Akitoka utanambia!”
Roby hakujali, akatembea kuendea gari lake. Na alipotia moto akanyoosha mpaka kazini. Huko akakaa kwa kama masaa mawili na alipoona kila kitu kipo sawa, akafungafunga ofisi apate kwenda kumwona Darren hospitalini. Lakini kabla hajajiendea, Isabel akafika hapo akiwa ameongozana na mbwa wake. Baada ya kusalimiana, akamuulizia Darren.
“Darren amelazwa hospitali. Ni siku ya pili hivi sasa,” Roby akaeleza. Basi Isabel akaguswa sana na jambo hilo, naye akataka kuongozana na Roby kwenda huko hospitali kumwona Darren.
Pasi na kipingamizi, wakaongozana kwenda huko. Kila mtu alitumia usafiri wake. Walipofika, Roby akamtambulisha Isabel kwa mke wa Darren, Josephine, na kisha mwanamke huyo akapata fursa ya kumwona mgonjwa.
“Ni nini kilimpata?” akauliza Isabel. Uso wake ulikuwa umejawa na mashaka. Alimtazama Darren kwa uso wa huruma na kuguswa mno. Roby akamweleza kwa kadiri alivyokuwa anajua. Isabel akauliza, “Kuna shida nyingine yoyote?”
“Hapana,” Roby akajibu akitikisa kichwa. Isabel akamtazama na kumwambia, “Kama kutakuwa na shida yoyote, basi naomba mnijuze nijue kwa namna gani naweza kumsaidia, sawa?”
“Sawa, hamna shida.”
Basi Isabel akaendelea kumtazama Darren kwa kitambo kidogo. Mara Darren akafungua macho yake na kumtazama. Isabel akafurahi sana. Akamjulia hali Darren kwa tabasamu kubwa na kumpatia pole. “Utapoa, Darren.” kisha akamuuliza, “Ni nini unawaza hivyo? Kuna shida yoyote naweza kukusaidia?”
Darren akatikisa kichwa. “Hamna,” akajibu kwa kunong’ona. Isabel akamuaga na kumwahidi atakuja kumwona tena, aidha hospitali ama nyumbani.
Tangu alipoondoka, Darren akabakia akiwa amefungua macho. Akateta na kujisogeza. Afya yake ilionekana kuimarika. Basi ilipofika jioni, daktari akamruhusu aende zake nyumbani. Huko mkewe akampikia chakula apendacho kisha akamlisha mpenzi wake kwa mahaba.
Lakini kuna kitu Darren alikuwa anataka kuongea na Roby. Na kitu hicho si kingine bali ni kumhusu Melissa. Alishindwa kabisa kumsahau Melissa. Kila alipotuliiia, picha ya mwanamke huyo ikawa inamjia kichwani!
Alitamani kumpigia Roby aje nyumbani kwake lakini akaona hakuna haja hiyo. Aliamini ataonana naye kesho na basi atamweleza.
Lakini tofauti na matarajio hayo, mara mlango ukagongwa. Na Josephine alipoufungua, Roby akazama ndani pamoja na Melissa. Kitu cha kwanza ambacho Darren alikifanya, ni kukutana macho kwa macho na Melissa.
Akajihisi kutetemeka.
Huu ulikuwa ni ugeni asioutarajia kabisa. Japo ugeni ni baraka, kwa Darren huu ulikuwa ni laana. Alijihisi anakosa amani.
Josephine aliwakaribisha wageni kwa bashasha na kuwapatia chakula pamoja pia na vinywaji, pia akawaambia wageni namna Darren aendeleavyo tangu atoke hospitali.
Kukawa kumejawa na matabasamu hapo sebuleni. Hata Darren alitabasamu lakini moyo wake ukiwa wa zambarau. Alikuwa anajibana sana, mwishowe akashindwa na kuomba ruhusa aende chooni, lakini hakwenda huko na badala yake akaenda chumbani na kujilaza kitandani.
Alikuwa anawaza sana. Alikaa hapo akatafakari yaliyopita kumhusu Melissa. Moyo ukamuuma sana. Macho yakajawa na machozi na hata kulowanisha kitanda. Alishindwa kujizuia kabisa na hakuwa anajua kwanini alishindwa kujizuia.
Kidogo mkewe akaja na kumkuta hapo kitandani. Ndani ya chumba kulikuwa na kiza lakini alimwona mumewe akiwa amejilaza hapo. Akashangaa. Pasipo kuwasha taa akamjongea Darren na kumuuliza, “Darren, shida nini? Mbona umejilaza huku peke yako na kuna wageni wamekuja kukuona?”
Darren hakusema kitu. Hakutaka mkewe ajue kuwa analia au amekubwa na shida au hofu yoyote ile. Akasafisha koo lake na kusema hamna tatizo.
“Lakini mbona ukajilaza?” mkewe akauliza akiweka kiganja chake mgongoni.
“Sikuwa najisikia vizuri kwa muda kidogo,” Darren akalaghai. “Nilitoka ili nipate unafuu alafu nitazamie kurudi.”
Josephine akapata mashaka. “Kuna haja ya kurudi hospitali?”
“Hapana!” Darren akawahi kujibu akitikisa kichwa. “Sijajisikia hovyo kiasi hicho. Siwezi nikakuficha mpenzi.”
“Sawa. Kwahiyo utakuja muda gani?” Josephine akauliza kwa sauti yake ya upole.
“Muda si mrefu,” Darren akajibu akiwa anageuzia uso wake kando. Basi mkewe akanyanyuka na kujiondokea zake. Darren akaendelea kujilaza hapo kitandani kwa muda kidogo kabla hajasimama na kuendea dirisha. Akalifungua na kutazama nje.
Akatazama huko kwa muda akiwa anawaza mambo kadhaa kichwani. Alihisi anahitaji hewa zaidi, akafungua dirisha na kuendelea kusimama na kutazama kwa muda.
Kidogo mkewe akarejea tena chumbani. Mara hii alipoingia tu, akasema, “Darren twende sasa sebuleni. Wageni wanataka kuondoka!” Darren hakusema kitu. Macho yake yaliendelea kuzurura huko nje. Mkewe akamjongea karibu. “Darren, kuna shida yoyote?” akawasha taa na kumtazama mumewe usoni. Akamwona akiwa na macho mekundu yaliyolowana.
Mwanamke huyu akapata shaka. Huenda Darren ana jambo asilotaka kumweleza. Akamtazama ndani ya macho yake na kumuuliza, “Una nini mpenzi?”
Darren akamtazama mkewe kwa sekunde kadhaa pasipo kusema jambo. Alafu akamshika shavu na kumweleza, “Ni bora usifahamu kitu, Josephine.” kisha akambusu shavuni, na mara chozi likamwanguka.
Mkewe akamfuta na kumkumbatia kwanguvu alafu akasema kwa kunong’ona, “Napenda kujua, Darren. Pengine naweza kusaidia.”
Darren asiseme kitu, akamtazama mkewe kisha akashusha macho yake chini.
“Niambie,” Josephine akamsihi. Bado alikuwa ananong’ona. Darren akazidi kudondosha machozi. Akafungua kinywa chake na kumwambia Josephine, “Nakupenda sana. Jua hivyo, sawa?” Josephine akatikisa kichwa chake. “Najua, mpenzi.” Kisha akashauri, “twende kwanza sebuleni, si vema kuwakalisha wageni peke yao. Wakiondoka tutateta.”
Basi Darren akajivuta machozi na kusafisha koo lake asije onekana anaongea kama mtu aliyetoka kubanwa na kilio alafu akaongozana na mkewe mpaka sebuleni.
“Kila kitu kipo sawa?” Roby akauliza.
“Yah!” Josephine akadakia kwa tabasamu la wongo. “Kila kitu kipo sawa. Hamna shida.”
Kwa muda ambao Darren alikuwa amekaa ndani, wageni walishamaliza kula na hata kunywa. Muda huo walikuwa wanajiandaa kuondoka tu.
Melissa akamtazama Darren na kusema, “inabidi upate muda wa kupumzika zaidi, Darren. Nashauri kama ingewezekana, hata kwa juma moja ukae nyumbani pasi na kujishughulisha.”
Roby akamuunga mkono. “Kweli. Usijali kabisa kuhusu kazini. Tulia kwanza urejeshe utimamu wako rafiki yangu.”
Darren akashukuru pasipo kutia neno lingine na basi wageni wakaaga kwenda zao. Wakapeana mikono ya kwaheri, Melissa akamminya Darren mkono.
“Ilikuwa furaha kukutana nanyi,” Melissa akasema kwa tabasamu pana. “Nitakuwa nawatembelea kama hamtojali.”
“Karibu sana,” Josephine akamkarimu, wakaenda zao. Baada ya Josephine kutoa vyombo na kusafisha meza, akaenda kuoga na mumewe na kisha wakajiweka kitandani.
Hapo akambembeleza mumewe amweleze ni nini kinamsumbua, nini haswa ambacho kinamtoa chozi, lakini Darren hakuwa radhi kusema. Alimsihi mkewe kuwa hayupo kwenye ‘mood’ ya kuteta muda huo. Asiijali. Pindi atakapokuwa sawa, atamweleza kila kitu.
Basi Josephine kwa moyo mzito, akaridhia. Akajilaza pembeni ya mumewe na kidogo akapitiwa na usingizi. Alikuwa ana furaha maana siku hiyo hakuwa kitandani mwenyewe. Jana yake kitanda kilikuwa kikubwa na cha baridi, lakini kwa upande wa Darren ilikuwa ni kinyume. Hakupata usingizi kabisa. Alijawa na mashaka.
Sasa Melissa ameshajua wapi yalipo makazi yake, je atasalimika? Mwanamke huyo hatoacha kumsumbua? Na hofu yake kubwa haikuwa kwake bali kwa mke wake na mwanaye.
Basi usiku ukaenda akiwa anakodoa macho darini akilala chali. Akawaza sana na sana na hatimaye naye usingizi ukaanza kumnyemelea. Lakini akiwa bado hajalowea usingizini, akashtusha kusikia kioo cha dirisha kikigongwa kwanguvu, “Tih!” akakodoa kutazama huko na wala hakuona kitu, ila akagundua dirisha lilikuwa wazi. Akaogopa. Ila alipofikiria kidogo ndipo akakumbuka kuwa dirisha hilo alilifungua mwenyewe muda ule na kusahau kulifunga.
Akanyanyuka na kuliendea. Alipofika akatazama kwanza kama ataona jambo nje, kwa chini akaona tawi dogo la mti likiwa limedondokea hapo. Upepo ulikuwa mkali sana. Pasipo shaka tawi hilo lilikuwa limeangushwa na pepo kali.
Basi akafunga dirisha na kurudi kulala. Upepo ulikuwa unaendelea kupuliza sana. Hakujali. Akafunga macho yake akijaribu kuvuta usingizi.
Akiwa ameyafumba kwa kama sekunde kumi, dirisha likagongwa tena. Akatahamaki. Moyo wake ukamlipuka na pumzi yake ikaanza kwenda mbio. Alianza kuhisi kuna tatizo. Akanyanyuka na kuendea dirisha alafu akatazama huko nje.
Chini … juu … kushoto … kul— akaona kitu cheusi kwenye mti! Macho yakamtoka akiachama. Baridi kali likampitia tokea unyayoni mpaka kichwani ghafula!
Alipokaza macho yake kutazama, akaanza kujikosoa. Huenda anachokihisi, sicho! Labda ni matawi, akajisema kifuani. Labda ni matawi yamefungamana. Akajilazimisha aamini vivyo.
Lakini …
Punde kidogo hicho kitu cheusi kikasogea toka chini kupanda juu. Hapo Darren akatingwa na hofu kali. Moyo wake ukaitikika ‘gup!’ kisha ukaanza kwenda mbio sana ‘gup!-gup!-gup!-gup!-gup!’
Haraka akafunga dirisha kwa kushusha pazia alafu akabaki akisimama hapo kama ataona kitu. Na kweli, baada ya muda kidogo akaona kivuli cha mtu dirishani. Kivuli cha mwanamke mwenye nywele ndefu zinazopepezwa na upepo.
Lakini mtu huyo hakubaki hapo kwa muda, akanyooshea kidole chake upande wa kushoto. Darren hakuelewa. Ila punde akapata maana baada ya ghafla mtoto kuanza kulia.
Chumba cha mtoto kilikuwa upande wake wa kushoto!
Akahisi kuwehuka. Upesi akatoka chumba chake na kukimbilia kule kwenye chumba cha mtoto. Alipofika huko akamkuta mtoto akiwa chini na ingali kitanda chake kidogo kikiwa kitupu na kinachocheza kwa upweke.
Akamnyanyua mwanaye na kumbembeleza, lakini akiwa anaangaza akitaka kujua ni wapi alipo mtu ambaye alimweka mwanaye chini toka kitandani.
Alitazama na kutazama lakini hakuona jambo. Hakukuwa na mtu humo. Alipotazama vema ndipo akagundua ya kwamba dirisha lilikuwa wazi. Basi akajongea taratibu na kulitazama dirisha hilo. Hapo, alipotazana vema, akapata kuona mabaki ya damu!
Akamkagua mwanaye kama kuna mahali popote ameumia lakini hakuona jambo. Hakuwa na jeraha wala mchubuko. Sasa ile damu ilitokea wapi? Akatazama nje ya dirisha, kushoto na kulia. Kulikuwa kimya tu zaidi ya upepo uliokuwa unapuliza kwa fujo kiasi.
Basi akafunga dirisha lile na kisha akamrejesha mwanaye kitandani. Alikuwa anaelekea kulala sasa. Alikuwa salama. Ila kwa upande wa Darren bado alikuwa mtu aliyejawa na mashaka sana. Alisita kuondoka katika chumba hicho akimwacha mwanaye papo.
Akangoja akiskizia kama kuna lolote litakalotokea. Hakukuwapo na kitu. Dakika ya kwanza mpaka ya kumi. Bado kulikuwa na kimya. Je pashakuwa salama? Akasema na nafsi yake. Japo mazingita yalionyesha kupo salama, bado bwana Darren hakuwa anaafki.
Kuna hisi fulani alikuwa nayo. Ushawahi kuhisi kuna mtu anakutazama mahali? Yaani umekaa ama umesimama lakini unahisi haupo mwenyewe? Ndivyo Darren alivyokuwa anahisi.
Alihisi chumba kina uzito fulani hivi. Ule uzito wa kutokuwa mwenyewe, japo macho yake hayakuweza kuthibitisha hilo jambo.
“Tafadhali,” Darren akasema kana kwamba kuna mtu anazungumza naye. “Naomba uiache familia yangu katika hili! Si mke wangu wala mtoto wangu wenye makosa. Naomba muwaache! Tafadhali naomba.”
Kukawa kimya. Kidogo upepo ukapuliza sana mpaka kutikisa kioo ha dirishani. Darren akatazama huko upesi, kwa woga. Akahisi huyo mtu azungumzaye naye atakuwapo huko.
Akasonga kwenda akiendelea kusema, “Naomba umwache mwanangu. Yeye hana makosa!”
Alipofika kiooni akagundua mabaki yale ya damu yalikuwa yameongezeka. Na si tu kuongezeka, bali yalikuwa yamepanda kwa matonetone kuchafua kioo. Mwanzo Darren hakuwa anaelewa, ila alipotazama vema matone hayo akabaini yalikuwa yameandika ujumbe.
‘WEWE NI WETU. NA YEYE HUYO MTOTO NI WETU PIA.’
Alipomaliza tu kusoma huo ujumbe, ghafla mtoto akalia kwanguvu! Darren akashtuka sana na kujikuta yu kitandani kando kidogo ya mkewe.
“Darren, una shida gani?” mkewe akakurupuka kwa hofu. Macho alikuwa ameyatoa na mdomo wake ameachama. Kwa kumtazama tu ungelijua mwanamke huyo alikuwa amepaliwa vipi na woga.
Darren akahema sana. Mpaka anakuja kutambua kwamba alikuwa ndotoni tayari ameshapitia shida sana, hata kwa mkewe pia. Kitu cha kwanza alichokifanya ikawa ni kutoka kitandani na kwenda moja kwa moja kwenye chumba cha mwanaye.
Alipomkuta yu salama, akashusha pumzi ndefu na kushika kichwa chake akiweka tama. Kidogo mkewe akaingia ndani ya chumba hicho.
“Darren unaweza kunambia kuna nini?” mwanamke akafoka. Alikuwa amechoshwa sasa na vitimbwanga vya mumewe. Darren, pasipo kutoa maelezo, akamnyanyua mtoto na kumpatia mkewe kisha akabeba kitanda cha mtoto na kusema, “tutakuwa tunalala na mtoto chumba kimoja!”
Akanyookea chumbani kwake na kukiweka kitanda cha mtoto pembeni na cha kwao.
Josephine akamwita, “Darren.” kisha akamtazama na kumuuliza kwa ustaarabu, “Nini kinakusumbua?”
“Mtoto hayupo salama, Jose!” Darren akabwatuka. Akashika kichwa chake na kukiacha, alafu akakishika tena. “Inabidi tuwe tunalala naye. Tutafanya hivyo kuanzia leo hii!” alikuwa kama mtu aliyewehuka. Mkewe alipatwa na hofu sana juu yake.
Akamweka mtoto ndani ya kitanda na kisha akamfuata mumewe na kumuuliza nini kinamsibu. Mbona amekuwa si mtu wa kueleweka hivi karibuni?
Basi Darren akanyamaza kwanza kwa muda wa kama dakika moja kabla hajasema kuwa hawapo salama. Hakuelezea sana. Alichomwambia mkewe ni kuwa hawapo salama na basi inawalazimu kuwa makini.
“Sasa si tutoe taarifa polisi?” Josephine akashauri. Alikuwa anamtazama mumewe kana kwamba mama anayemtazama mtoto ampendaye akiwa anamkanya,
“Polisi hawatasaidia kitu,” akasema Darren kwa sauti ya chini. Macho yake yalionyesha kukata tamaa. Yalionyesha hofu ndani yake. Mkewe alipomuuliza kwanini hawawezi kutoa taarifa polisi, Darren akasita kusema. Hakutaka kumtengenezea mkewe hofu zaidi. Alidhani kwa kumweleza mkewe zaidi na zaidi kungefanya apatwe na woga na hivyo kuharibu kabisa maisha yake.
Alitumai huenda akapata suluhisho la matatizo yake pasipo kumhusisha mkewe kwenye shida zake. Ila alikuwa sahihi? Alijikuta akijiuliza hilo swali mwenyewe pasipo kupatia majibu. Kichwa kilikuwa kinamuuma.
Kesho yake asubuhi na mapema, kinyume kabisa na alivyokuwa amekubaliana na Roby, akajiandaa na kwenda kazini. Altumai kwa kufanya kazi kungemfanya awe ‘busy’ na kujisahaulisha matatizo yake.
Alipofika akamweleza Roby kuwa hajiskii vema anapokuwa nyumbani. Mwili umekuwa wa kizembe sana na angependa kujishughulisha zaidi. Basi Roby akakosa maneno mengine ya kusema zaidi ya kumkaribisha Darren kazini, lakini akimpa angalizo, “Utakapoona hali inabadilika, basi utanambia. Sawa?”
Darren akachapa kazi kama kawaida mpaka majira ya saa sita mchana. Akiwa anapata mapumziko, ndipo akamwona Melissa, toka kwenye ghorofa ya pili aliyomo, akiwa anaingizana eneo hilo.
Mwanamke huyo alikuwa amevalia shati jeupe na sketi nyeusi ya kitambaa. Kabana nywele zake na shingoni amevalia skafu ya zambarau. Alikuwa na miadi na Roby. Na amini usiamini, mwanamke huyo hakuwa anafahamu kama Darren yu kazini.
Lakini uwepo wake huo ukamfanya Darren akose amani. Upesi alinyanyuka na kwenda kufunga mlango wa ofisi yake kwa ufunguo kisha akaketi kitini akitazama mlango kana kwamba anataraji kuna majambazi wanaweza kuuvunja.
Zikapita kama dakika ishirini. Dakika zote hizo Darren akiwa hafanyi kitu bali kutazama mlangoni na dirishani kama Melissa amekwenda zake. Ikiwa inaelekea dakika ya ishirini na moja, Darren akaanza kusikia sauti za watu zajongea mlangoni.
Kidogo hodi ikabishwa na sauti ya Roby ikapaza, “Hey Darren, una mgeni!” kisha kicheko kikafuatia kidogo. Darren akanyamaza kimya kama hajasikia.
Kidogo tena hodi ikagongwa, “Darren!” sauti ya Roby ikaita. Darren kimya. Kidogo, Roby akasikika akisema, “Ukute amepatwa na matatizo!” wakajaribu kufungua kwa kitasa, mlango haukufunguka. Wakajaribu tena na tena, majibu hamna. Kidogo Darren akasikia Melissa akishauri, “Tuvunje mlango, Roby!” kisha akalalama, “Kwanini ulimruhusu afanye kazi na unajua si mzima?”
Hapa Darren akapata mashaka. Mlango ukivunjwa itakuwa si jambo jema tena haswa akikutwa ni mzima wa afya. Basi upesi akanyanyuka na kuuendea mlango, akaufungua.
“Darren, vipi?” Roby akatahamaki kumwona mwanaume huyo. “Kuna shida? Mzima?”
Darren akawaondoa hofu kabisa kwa kusema yu mzima. Alikawia tu kufungua mlango sababu ya kutingwa na kazi fulani. Lakini ni wazi wageni wake walitilia shaka hilo jibu japo hawakutaka kulisema.
“Melissa hapa alikuwa anataka kukusalimu,” Roby akasema kwa tabasamu. Melissa na Roby wakapeana mikono. “Unaendeleaje Darren?”
“Niko vizuri, nashukuru. Karibu.”
“Ahsante. Nimefurahi kusikia upo vizuri. Ni habari njema.”
“Nashukuru, Melissa.”
Basi Melissa na Roby wakaaga waende zao. Na ni punde tu damu ikamchuruza Darren puani na kuchafua shati lake jeupe. Bahati damu hiyo haikuvuja zaidi. Ilikata. Darren akaketi na kuwaza afanyeje.
Akiwa anawaza ndipo akakumbuka kuhusu habari za yule jamaa aliyemsaidia mama yake toka kwenye shida za kuandamwa na mambo ya ajabu. Habari ambazo baba yake alimweleza muda mfupi baada ya mamaye kufariki.
Hapo Darren akaanza kuona kuna haja ya kumtafuta mtu huyo kwa udi na uvumba.
Atampatia wapi?
Baada ya kufikiri kidogo, akaona kuna haja ya kwenda kule kwenye makazi ya wazazi wake marehemu, huenda akabahatika kupata chochote kitu huko cha kumpa angalau mwanga.
Akaaga na kujiendea zake akiwa amemaliza kazi. Alipofika akatafuta sana kila mahali mwishowe akaishia kushika simu ya baba yake na kuanza kukagua majina yalokuwemo humo aone kama atabahatisha.
Akasaka pasipo mafanikio, hatimaye akakata tamaa. Akarejesha simu ya baba yake na kujilaza kochini akiwa anawaza afanye nini zaidi.
Lakini akiwa hapo, kama ajali tu, akawa anapepesa macho yake ndani ya nyumba hiyo pweke. Aliporusha macho yake kule jikoni, akagundua kuna mabaki ya chakula yalikuwapo chini. Akakunja uso wake kwa kufikiri. Akanyanyuka na kuendea huko akatazame ni nini kilikuwapo.
Basi alipofika akakuta ni kweli kuna mabaki ya chakula hapo chini. Na si kidogo, mengi tu. Mabaki hayo yalikuwa yametokea kwenye sufuria iliyokuwapo kwenye kitako cha jiko.
Akashangazwa kidogo. Kitu pekee anachokumbuka kuhusu nyumba hii ni kwamba aliiacha ikiwa safi kabla hajajiondokea hapo na kutokurudi tena mpaka siku hiyo. Sasa nani alimwaga mabaki yale ya chakula?
Akafunua na sufuria. Alipotazama ndani, akaona chakula kikiwa kimejaa kede. Na ajabu ni kwamba chakula hicho bado kilikuwa cha moto. Na hata kitako kile cha jiko bado kilikuwa na vuguvugu la joto kumaanisha kimetoka kutumika muda si mrefu.
Hapa Darren akapata shaka sana. Akakagua tena nyumba kwa undani zaidi na kuja kugundua kuwa nyumba ile haikuwa pweke kama alivyokuwa anadhani. Kulikuwa na ishara za mtu humo.
Bafu lenye maji sakafuni. Vyombo vimehamishwa eneo. Makabati yapo wazi. Vitanda vimeezuliwa. Maana yake nini?
Alihofu huenda mwizi aliingia na kuiba, lakini alipotazama kila kitu humo ndani hakuhisi kama kuna lolote lililopungua. Kila kitu kilikuwapo ila kikiwa kimehamishwa ama kuvurugwa. Akahofu sana. Hata akaona inabidi atoke humo ndani upesi awezavyo.
Akakusanya vitu vyake na kuuendea mlango. Alipoufungua, ukagoma. Akajaribu tena na tena, mlango ukagoma. Akajipapasa mfukoni atoe ufunguo, alipoupata akauchomeka kwenye kitasa na kujaribu kufungua japo alikuwa anaamini hakuwa ameufunga mlango huo kwa ufunguo.
Alipotekenya ufunguo, mlango ukatoa mlio kidogo, na mara ukafunguka! Akashusha pumzi ndefu. Upesi akatoka na kuurejesha mlango kama alivyoukuta. Haraka akashuka ngazi na kuendea gari lake na kujitia humo.
Kabla hajaliwasha, akafikiri kwanza yale aliyoyaona kule. Kwa kama dakika mbili kichwa chake kikiwa kinavuruga. Hakujua ni nini kinatokea, na pengine hakuwa anataka kujua. Akawasha gari na kuadhimia kutorudi tena hapo.
Lakini ngoja. Akasimamisha gari lake baada ya kukumbuka jambo – simu za wazazi wake! Yampasa aende nazo! Basi akazima gari na kurudi kule ndani upesi ili abebe simu hizo na asiwe na sababu nyingine tena ya kurejea hapo.
Bado alitumai akiwa na simu zile huenda akapata majibu ya maswali yake.
Akafungua mlango na kuzama ndani akitupa macho. Akatazama sebuleni, hazikuwapo. Sasa aliziweka wapi? Akawaza. Kidogo akakumbuka ni jikoni alipokuwa anashangaa mabaki yale ya chakula. Haraka akaenda huko akatazame, lakini alipofika huko hakuona kitu chochote kile.
Sasa wapi? Akajikuta anajiuliza mwenyewe kwanguvu. Akiwa anaangaza hapo jikoni, akagundua mabaki yale ya chakula aliyoyaona muda ule, hayakuwapo tena! Akastaajabu.
Akafungua sufuria ile nayo aitazame kama ina chakula, hamaki akaikuta ni tupu! Hapo moyo wake ukaanza kusikika masikioni ukikimbia. Upesi akatoka humo jikoni na kwenda chumbani kuangaza kama ataona simu hiyo, na basi atakapoziona azikwapue na kuondoka upesi.
Akafika huko na kuangaza, akakuta vitanda vikiwa vimetandikwa kwa usafi! Macho yakamtoka na moyo ukamkimbia zaidi. Akatazama aone kama kuna simu, hamna! Hakukuwa na alama yoyote ile ya simu.
Sasa zimeenda wapi?
Akiwa anawaza, mara akasikia mlio wa simu! Akatega sikio akikodoa. Inalia wapi? Akadhani sauti hiyo itakuwa inatokea sebuleni. Haraka akaenda huko na kusaka, akafunua makochi na kusaka. Hakuona simu.
Simu ikaendelea kuita. Alipotega sikio vema, akahisi inalilia jikoni, upesi akaenda huko akaone. Napo alipofika akasaka sana pasipo mafanikio. Ila bado simu inaita.
Alipotega tena sikio kwa kadiri awezavyo, akabaini sauti hiyo inatokea chumbani. Hapa sasa ndiyo akaona huu ni mchezo tu. Huko chumbani ndipo alitoka, mbona hakuisikia sauti hiyo akaisikia sebuleni?
Akaona aondoke hapa upesi, hata simu hiyo aiache. Akaachana na kila kitu na kuuendea mlango. Alipoufungua ukagoma. Akachomeka ufunguo na kutekenya kitasa, napo pia mlango ukagoma!
Hapa akatoa macho kana kwamba kitenesi. Akavuta mlango kwanguvu sana lakini haukutii amri. Akavuta tena kwanguvu zake zote, mwishowe kitasa kikang’oka akadondoka chini, Puh!
Aligonga kichwa kwanguvu na kujisababishia maumivu makali. Akadaka kichwa akiugulia. Aaaaghhshhhh! Akajizungushia kushoto na kulia akigugumia.
Alipofungua macho yake kutazama kwa kuyafinya, akaona miguu ya mtu nyuma ya kochi. Miguu hiyo ilikuwa meusi na mipana. Basi upesi Darren akaketi kitako na kutazama nyuma ya kochi kama kuna mtu. Hakumwona!
Akasimama akiwa ameshika kichwa chake. Akatazama sebuleni na hata koridoni, hakumwona mtu. Kote kulikuwa kupweke. Na pia kimyaa kwani simu zilikuwa zimezima.
Lakini aliposkiza zaidi akagundua hakukuwa kimya kama alivyokuwa anawaza. Kwa mbali kulikuwa na sauti za vishindo vya mtu. Kwa mbali vishindo hivyo vilikuwa vinapapasa sakafu.
“Wewe ni nani?” akapaza sauti kuuliza.
Hakuna aliyemjibu. Ni sauti yake tu ndiyo ilimrejea. Akauliza tena, “Unataka nini kwangu? Unataka nini hapa?”
Napo hakuna aliyemjibu. Kadiri alivyokuwa anakaa hapo, moyo wake ukawa unazidi kumwenda mbio.
**
“Una uhakika uliipenda?” aliuliza mwanaume mmoja aliyekuwa anakatiza na mwanamke wakiwa wameshika mkono. Wote walikuwa wamevaa makoti ya kujikinga na baridi na nyuso zao zikiwa na furaha.
Uso wa mwanamke ulikuwa na miwani ya kumsaidia kuona, na ule wa mwanaume ulikuwa mrefu ukipambwa na tabasamu.
“Nimependa sana,” akajibu mwanamke akimtazama yule mwanaume, na kisha wote wakacheka. Wakatembea zaidi kwa kama hatua kumi, kidogo mwanamke akapaza sauti akimvuta mkono huyo mwanaume, “Tazama!” Alinyooshea kidole juu ghorofani. Macho yake yalikuwa yamekodoa haswa!
Mwanaume yule akatazama upesi kule alipolekezewa, na hamaki akamwona mtu akiwa amejishkiza dirishani, ananing’inia!
“Anataka kujitupa!” akaropoka yule mwanamke.
‘Inabidi tumsaidie!” akasema mwanaume kisha akatazama kushoto na kulia kwake aone ni namna gani anaweza kutoa msaada.
Mtu yule aliyekuwa ananing’inia dirishani alikuwa ni Darren! Mikono yake ilikuwa inavuja damu.
Upesi watu wakaongezeka na kufanya namna za kumsaidia Darren. Walikuwa ni wanaume watano wenye nguvu, wakakinga mikono yao kumdaka. Na kheri Darren akajiachia na kudakwa.
Alikuwa amechoka sana. Mikono yake ilikuwa imechanjika viganjani kwa kung’ang’ania kingo za dirisha. Basi kwa kumpatia huduma ya kwanza, wakamwahisha hospitali kupata huduma.
Huko Darren akatiwa dawa kwenye majeraha na kufungwa bandeji kisha akaondoka zake kurudi nyumbani. Alipofika mkewe akastaajabu kumwona mumewe yu kwenye hali ile ya kuchoka na majeraha. Alipomuuliza nini kimetokea, Darren akasihi ni ajali.
“Haukutakiwa kwenda kazini, Darren,” mkewe akalalamika. “Muda mwingine uwe unasikia.”
Darren hakusema jambo. Alipopata chakula akajiendea chumbani na kujilaza. Akawaza sana. Nini kile alichokiona kwenye nyumba ya wazazi wake? Ni nani yule ambaye hakumfahamu?
Akiwa anawaza, simu yake ikaita. Akatazama na kukuta ni namba mpya. Ni nani? Akapokea na kuweka simu yake sikioni. Akasikia sauti ya kike ikimwita kwa sauti ya chini, “Darren!”
“Yes,” akaitikia kwa tahadhari. “Ni nani mwenzangu?”
“Melissa,” sauti ikajibu. Mara kukawa kimya kwa sekunde tatu kabla Darren hajasema, “Melissa, tafadhali naomba uachane na maisha yangu. Sawa?” kisha akakata simu.
“Ni nini mwanamke huyu anataka kwangu?” Darren akauliza akitoa chozi. “Ni nini nilimkosea? Kumpenda kwangu?”
Hakupata majibu. Mara ujumbe ukaingia kwenye simu. Akanyanyua simu yake kuutazama, ‘Darren, tafadhali naomba tukutane tuongee. Usiwe mwepesi wa jazba,’ ujumbe ulisomeka vivyo,
Darren hakujali, akazima simu na kuiweka kando akijilalia. Alijilaza hhapo kitandani mpaka mke wake alipokuja na kumwita kumwamsha. Japokuwa Darren alisikia sauti ya mke wake, hakuitika. Alinyamaza kimya kwani alifahamu kuwa mkewe atamuuliza maswali mengi ambayo yeye hakuwa radhi kuyajibu.
Basi mkewe baada ya kudhani mumewe amelala, akaachana naye kwenda sebuleni. Kidogo akarejea na kuzima taa, kisha akalala.
Baada ya kama masaa manne ya mwanamke huyo kulala, akiwa tayari ameshalowea usingizini, Darren akafungua macho na kutoka kitandani. Alielekea sebuleni akakaa hapo akiwa anawaza sana. Nini haswa afanye? Akawasha simu yake na punde jumbe kama nne zikaingia kwa mkupuo.
Zilikuwa ni jumbe za Melissa.
‘Darren, najua unaniwazia mabaya. Biado nakupenda. Kuna siku utalifahamu hilo,’ ujumbe wa kwanza ulisomeka vivyo.
‘Nina mengi ya kuongea nawe Darren. Tafadhali fanya jitihada tukutane,’ huo ulikuwa ni ujumbe wa pili.
‘Unajua wapi pa kunipata Darren kama ukinihitaji,’ ujumbe wa tatu na wa mwisho ukasema, ‘Kwaheri.’
Darren akasonya na kufuta jumbe zote hizo, na kabla ya kufungia namba ya Melissa akamwandikia ujumbe mwepesi, ‘Sitaki kukutana na wewe kamwe!’ kisha akalaza kichwa chake kwenye kiti akiendelea kuwaza na kuwazua. Mwishowe usingizi ukampitia na akalala fofofo hapohapo.
Hakujielewa mpaka majira aliyokuja kushtuliwa na mkewe. “Darren! Wewe Darren!”
Alipofungua macho akabaini ni asubuhi sasa. Aliwezaje kulala hapo mpaka asubuhi? Alifikicha macho yake, akapiga mihayo na kujinyoosha kisha akamsalimu mkewe.
Lakini,
“Mbona umelala hapa na ulikuwa chumbani?” Josephine akamuuliza.
“Aaahm …” Darren akajiuma, “niliamka usiku wa manane baada ya usingizi kukata. Nilipoketi hapa, sijui nini kilitokea, nikapitiwa na usingizi.”
Josephine hakumuuliza tena mumewe badala yake akampa pole na kumuuliza hali yake, “Auhisi kuumwa viungo vya mwili?”
“Kidogo,” Darren akajibu na kuongezea, “Mgongo na shingo vyauma kwa mbali. Nadhani vitakuwa sawa kadiri muda utakavyoenda.”
“Na vipi kuhusu majeraha yako?” Josephine akaongezea swali.
“Nayo yapo sawa,” Darren akajibu na kusema, “Baadae nitabadili bandeji na kutia dawa.” kisha naye akauliza, “Mtoto anaendeleaje?”
“Yupo sawa,” Josephine akamjibu kwa tabasamu alafu akaenda zake jikoni akapate kuandaa chai kwa ajili ya familia. Wakanywa na kukaa pamoja mpaka majira ya saa saba mchana ambapo walipata ugeni. Alikuwa ni bibie Isabel akija kumjulia hali Darren.
Mwanamke huyo alikuja na gari la thamani akiendeshwa na mwanaume mzee ndani ya suti nyeusi. Akiwa amevalia suti rangi ya ugoro na viatu mchuchumio, alikuwa amependeza haswa. Nywele zake alizozilazia pembeni zikipeperushwa na upepo.
Japo mwanamke huyu alikuwa mtu mzima kidogo, narudia tena, alikuwa na mvuto wa ajabu kwa mwonekano wake. Alijua kupendeza na kujivesha kutokana na mwili wake.
Alipoonana na familia ya Darren akatabasamu sana ingali aliteta nao machache na alipotimiza haja ya kumuulizia hali mgonjwa, akaomba aonane na Darren faragha, kwenye gari. Darren pasipo kusita akaongozana naye mpaka ndani ya gari, huko akiwa yeye, Isabel na dereva.
Dereva ambaye hakuonekana kujali kama nyuma yake kuna watu wanateta.
“Darren,” Isabel akaita akisonga karibu na mwanaume huyo. “Niambie kama kuna tatizo lolote linalokusumbua.”
Kidogo Darren akashtushwa na swali hilo. Aliwaza pengine Isabel anajua anachokipitia ama? Lakini hapana, akasema na nafsi yake. Haiwezekani!
“Sina tatizo, Isabel,” Darren akasema akitikisa kichwa chake.
“Kweli?” Isabel akauliza akimtazama Darren machoni. Macho yake yalikuwa ni makali, Darren akashindwa kuvumilia, akatazama chini.
“Ni kweli. Sina tatizo, Isabel.”
“Sawa,” mwanamke akajibu na kuweka mkono wake kwenye paja la Darren. “Basi mimi nina tatizo.”
Darren akautazama mkono wa Isabel kabla hajauliza, “Tatizo gani?”
Isabel akanyamaza kwanza akingoja Darren amtazame usoni. Darren alipofanya hivyo, Isabel akasema, “Nataka kuwa karibu na wewe zaidi, Darren.”
Sehemu Ya 6
Darren akashtushwa na kauli hiyo. “Una maana gani, Madam Isabel?”
Isabel akatabasamu. “Nini ambacho hujaelewa, Darren? Anyway, hii nyumba unayokaa sasa, sijapendezwa nayo. Umeona nyumba ya mwenzio Roby?”
Kabla Darren hajajibu, Isabel akaendeleza maneno, “Nataka na wewe uwe na nyumba kama ile. Kubwa na ina nafasi kidogo. Sawa?”
“Lakini sina tatizo na nyumba yangu hii,” Darren akajitetea.
“Najua, najua, Darren. Hauna tatizo kabisa na nyumba yako hii, lakini nimekuomba tu uhame hapa. Tafuta nyumba kubwa zaidi. Usijali, nitasimamia kila kitu. Sawa?”
Darren hakujibu, badala yake akatazama chini. Hakuwa ameafiki wazo hilo. Isabel akafungua pochi yake ndogo na kutoa kipande cha gazeti lenye picha kisha akamkabidhi Darren. Ilikuwa ni picha ya jengo la bibi yake kule kijijini.
Akamuuliza, “Unajua nyumba hiyo?”
“Ndio,” Darren akawahi kujibu. “Ni nyumba ya marehemu bibi yangu.”
“Roby aliniambia hivyo,” Isabel akamhusia na kumuuliza, “Je, naweza nikaiununua?”
“Nani alikwambia inauzwa?” Darren akauliza.
“Kwenye gazeti ilikuwa inasema hivyo. Wamekosea?”
Darren akafikiri. Pengine wazazi wake waliweka matangazo hayo wakiwa hai. Sasa vipi? Akawaza. Aibakize ile nyumba ama aiuze tu?
“Ngoja ntakujibu,” akamwambia Isabel.
“Sawa. Utakapokuwa tayari utaniambia,” Isabel akasema akifunga pochi yake. “Nitakulipa pesa taslimu, Darren.”
“Sawa.”
“Kwaheri. Nitakuja kukuona siku nyingine.”
Kabla Darren hajatoka ndani ya gari, Isabel akambusu shavuni na kumuaga kwa kumnong’oneza, “Kwaheri, Darren.”
Darren hakusema kitu akatoka zake na kwenda ndani. Alipoketi sebuleni, mkewe akatokea chumbani akiwa amembebelea mtoto. Macho yake yalikuwa yanatiririsha machozi.
“Darren,” Josephine akaita na kuuliza, “Unaniletea mwanamke wako nyumbani kwangu. Kweli?”
Darren akakodoa.
Kidogo mkewe akajigeuza na kwenda zake ndani pasipo hata kuaga na huku akiwa anamwaga machozi. Hali hiyo ikamfanya Darren ajisikie vibaya sana. Moyo ukamnyong’onyea akiwa anajiuliza nini kimemsibu mkewe?
Hakuwa anajua kwamba mkewe alimwona wakati Isabel akimbusu kwenye gari, kioo cha gari kilikuwa chini hivyo ikapeleka kuonekana kwa urahisi na mkewe akiwa chumbani.
Akaketi pale sebuleni kwa kama sekunde tano kabla hajanyanyuka na kumfuata mkewe ndani kumjulia hali lakini kumuuliza nini shida. Alipofika, akamkuta mkewe akiwa amejilaza kitandani analia. Mtoto alikuwa amelala kwenye kitanda chake.
Akamwita, “Josephine!” mwanamke hakuitika. Akarudia kuita tena na tena lakini bado kukiwa kimya. Akaketi kitandani na kumshika bega.
“Mke wangu,” akaita kwa upole. Mwanamke bado akawa kimya. Ni sauti ya mafua tu ndiyo ilikuwa inasikika na miguno ya kilio.
“Nimekufanya nini?” Darren akauliza. “Niambie basi nini tatizo?” Darren akahisi huenda mkewe aliumizwa na kile kitendo cha mkewe kwenda kuonana na Isabel kando, basi akaomba msamaha huku akimhakikishia kuwa hakufanya jambo baya, lakini bado tu. Josephine aliendelea kulia asiseme jambo.
Zikapita kama dakika tano … sita … saba … bado Josephine kimya. Mwishowe Darren akaona ni staha akimwacha mwanamke huyo yeye aende sebuleni kutulia alafu baadae mwanamke huyo atakapokuwa sawa, aongee naye.
Akaketi sebuleni kwa kama lisaa. Kimya. Akawasha runinga na kutazama lakini akili yake yote ikiwa kwa mkewe. Akaitazama kwa kama nusu saa, bado kimya. He! Akashangazwa na hali hiyo. Akapatwa pia na mkanganyiko wa nafsi, je aende tena kumbembeleza mkewe au atulie hapo mpaka atakapokuja mwenyewe?
Akiwa anawaza, mara akasikia mlango ukifunguliwa na kisha vishindo vya mtu. Kidogo akamwona mkewe akifika sebuleni lakini akipitiliza moja kwa moja kwenda jikoni.
Akarusha macho kumtazama. Kidogo akahofu mkewe asije akawa ameenda kujidhuru. Akakodoa mpaka pale Josephine alipotoka huko jikoni na kutembea kudaka korido. Akamwita tena, mara hii Josephine akaitika kwa kumtazama.
Macho yake yalikuwa yamekauka machozi lakini yakiwa bado mekundu. Uso wake ulikuwa umesinyaa kwa huzuni na mdomo wake umevimba.
“Una nini Josephine?” swali hilo likafungua tena mifereji ya machozi. Josephine akabubujikwa na machozi na mdomo wake ukatetemeka akiumauma meno. Hakuwa anaweza kuongea. Kuna kitu alikuwa anahisi kinamkaba kooni. Mdomo ulikuwa ni mzito na kichwa chake kilikuwa kinagonga.
Hakuwahi kuwaza … hakuwahi kuwaza kabisa kama Darren anaweza kumsaliti kwa kuwa na mwanamke mwingine.
Kila alipotaka kuongea akajikuta taya zinagongagonga. Mdomo unajawa na uchungu usio wa kawaida. Akaamua tu kuondoka zake. Mumewe akamsindikiza kwa macho yenye itilafu mpaka alipozama ndani ya chumba kabisa, akaufunga mlango.
“Eh!” Darren akahema akijilaza kitini. “Kazi nnayo.”
Akabaki hapohapo akitazama runinga na kurudi mawazoni, akitazama runinga na kurudi mawazoni mpaka mwishowe akabebwa na usingizi kabisa. Ulikuwa ni usingizi mwepesi lakini uliomfanya akapata kidogo afueni ya rundo la mawazo alokuwa anapitia.
Lakini katika namna ya ajabu, ya ajabu kabisa, usingizi huo ukageuka kuwa mzito kupita kiasi! Darren akajikuta analala akikoroma kabisa, hata kumwaga udenda akiachama kinywa. Ni kama vile hakuwa amelala kwa juma zima, au amefanya kazi kubwa sana na hakupata muda wa kupumzika.
Akiwa ndani ya usingizi huo akazamia ndotoni ambapo alijiona yu ndani ya nyumba ya bibi yake, kule kijijini. Alikuwa sebuleni akifanya usafi akiwa anangojea ugeni muda si mrefu.
Kidogo akiwa anaendelea na kazi hiyo, mkewe akaja akiwa amembebelea mtoto. Mtoto alikuwa analia lakini punde akanyamaza. Josephine akaketi kwenye kiti na kumtazama Darren.
“Ungesogea kando kidogo na mtoto kwani kuna vumbi!” Darren akamwonya mkewe kisha akaendelea na kazi yake akijua mkewe atafanyia kazi ushauri wake. Lakini baadae alipokuja kutazama, akatahamaki mkewe alikuwa bado amekaa kwenye kiti!
“Josephine!” Darren akaita. Mkewe alikuwa bado anamtazama. “Si nimekwambia utoke hapo lakini? Huoni vumbi?”
Josephine akaendelea kumtazama tu. Hakuonyesha dalili yoyote ya kusikia anachoambiwa. Kidogo, mbele ya macho ya Darren, Josephine akachomoa kisu toka nyuma ya mgongo wake. Kilikuwa ni kisu kipana na kirefu. Kisu kinachometa kwa upya. Na ndani ya sekunde moja tu, kufumba na kufumbua, Josephine akamdidimizia mtoto kisu chote kifuani!
Darren akatoa macho haswa. “Mungu wang – Josephine! Nini unafanya?”
Josephine akamweka mtoto kando na kisha akanyanyuka kumfuata Darren akiwa amebebelea kisu chake mkononi. Darren akapiga yowe kali. Akashuka toka alipokuwa amekwa na kuanza kupambana kujiweka mbali na Josephine kwasababu za usalama wake.
Josephine akazidi kumjongea na kisu kinachochuruza damu. Uso wake ulikuwa umekengeuka kuwa wa ajabu. Macho yake yamekuwa ya kijani na mdomo wake unaapa kifo.
Hakuwa Josephine uliyemzoea, mkarimu, mpole na mwenye kutenda yaliyo mema. Alikuwa ni Josephine kutoka kuzimu. Josephine mwenye umbo la binadamu lakini roho ya shetani!
“Josephine! Hapana! Tafadhali usifanye hivyo!” Darren aliwaka kwa woga. “Tafadhali, Josephine. Mimi ni mume- ” hajamalizia, Josephine akamrukia na kunyanyua mkono wake wenye kisu.
Hapo ndipo Darren akaamka toka kwenye lindi zito la usingizi! Akiwa anahema kama mbwa, akatazama kushoto na kulia kwake. Macho yamemtoka na mdomo ameachama!
Kidogo tu, akasikia sauti kali ya mtoto ikilia. Haraka akanyanyuka na kukimbilia chumbani. Upesi akamwangalia mtoto, alikuwa yu kwenye kitanda chake analia haswa. Basi akamnyanyua na kujaribu kumbembeleza. Kitandani Josephine alikuwa amelala.
“Josephine,” Darrena kaita na kuuliza, “Hausikii mtoto analia?”
Kimya.
Darren akaita tena na kuuliza. Bado kimya. Basi akadhani bado Josephine ameendeleza mgomo wake. Lakini ndiyo mpaka kwa mtoto? Akajiuliza. Akatoka chumbani humo na kwenda mpaka sebuleni akiwa anambembeleza mtoto wake, hatimaye mtoto akalala.
Basi akaona ni vema akamlaze mtoto kitandani chumbani. Alipofanya hivyo, kabla hajatoka chumbani akamwita tena Josephine. Bado kimya. Saa hii akaamua kutoondoka mpaka pale atakapotimiza adhma yake, kuongea na mkewe.
Akamgusagusa na kumshtua. Akamsogezasogeza na kumwita. Kidogo ndipo akabaini ya kuwa mkewe alikuwa amemeza vidonge vingi, kumbe pale hakuwa mzima. Povu lilikuwa linamtoka mdomoni na macho yake yamekwisha panda juu!
Akachanganyikiwa haswa.
Uopesi akambeba mkewe na kumkimbizia kwenye gari, na pasipo kufunga mlango akatia moto gari na kuendesha kwa haraka amwahishe hospitali. Lakini kufika mbele ndipo akabaini hata na mtoto alikuwa amemwacha ndani!
“Mungu wangu!” akajikuta anatoka na maneno. Akarudi nyuma upesi na kujitengenezea vema kwenye barabara kisha akarudi nyumbani kwa kasi ya ajabu.
Alipofika akakimbilia ndani na kumbemba mtoto, akamweka ndani ya gari na kutimka kama kimbunga!
Laiti askari angemwona namna alivyokuwa anaendesha, asingeshani hata kama mwanaume huyo amembembelea mtoto na mwanamke ndani. Akili yote ya Darren ilikuwa imeruka! Alikuwa anamuwaza mkewe tu. Lakini pia akidhani huenda akawa amempoteza, au atampoteza akiwa njiani.
Kheri akafika hospitalini salama. Akamtua mke wake na kumwahisha kupatiwa huduma. Yeye na mwanaye wakakaa kitini kungoja taarifa ya daktari.
Darren akiwa amekaa hapo akawa anaomba kila aina ya sala mkewe anusurike.
Kama baada ya dakika tatu, Isabel akampigia simu.
Akaitazama simu hiyo na kusonya, hakutaka kupokea, lakini ikaita pasipo kukoma, hatimaye, kwa kuepusha usumbufu, akapokea na kuiweka sikioni.
“Hey Darren,” Sauti ya Isabel ikasalimu na kisha kuuliza, “Kuna shida?”
Swali hili likamshtua kidogo Darren. Alijiuliza kama Isabel amemwona ama? Mbona ni mara ya pili hii akimuuliza swali hilohilo?
“Isabel,” Darren akaita na kuuliza, “Una maanisha nini kuniuliza hivyo?”
“Najua una matatizo, Darren,” Isabel akasema kwa kujiamini.
“Umejuaje kama nina matatizo?”
“Uso wako tu unaonyesha. Niambie ukweli Darren, hauna shida?”
Darren akawa kimya kidogo.
“Ni sawa, Darren. Kama utakuwa una shida basi unajua pa kunipata.” kisha Isabel akakata simu na kumwacha Darren akiwa kwenye lindi la mawazo. Ni kweli Isabel anayajua anayoyapitia ama anahisi tu? Je ni sahihi kwake kumshirikisha mwanamke huyo ama akaze kifua tu?
Alijiuliza pasipo na kikomo. Daktari akaja na kumshtua amwitaji ofisini. Alipoenda huko Daktari akamweleza maendeleo ya mkewe kuwa ameathirika sana na madawa aliyoyatumia. Kurudi kwenye hali yake itawachukua muda kidogo.
“Laiti ungemuwahisha, kazi ingekuwa nyepesi zaidi,” Daktari alisema vivyo na kisha kumpatia moyo bwana Darren, “Usijali, atapona tu. Japo yatupasa tuchukue muda kwa mwili wake kurejea kwenye hali ya kawaida.”
Basi Darren baada ya habari hizo, akajiendea kwenye benchi kuketi zaidi. Hapo akawa na mwanaye aliyekuwa anambembeleza. Mwanaye aliyekuwa anamwonea huruma kwa mama yake kuwa hoi kwa ugonjwa.
Alikaa hapo kwa masaa mawili kabla hajaona ni vema kumjuza Roby ili aje kumjulia hali. Punde kidogo, Roby akaja na angalau Darren akapata muda wa kutoa yaliyo kifuani mwake. Angalau akajihisi mwepesi kwa kunena yanayomsibu.
Kuongea napo ni tiba.
Roby akampa pole sana na kumfariji. Akakaa naye kwa muda mrefu kabla hajamuaga aende kupumzika nyumbani.
“Utaniambia kitakachotokea, Darren. Lakini nakushauri kwanza uende nyumbani ukapumzike na kumpatia mahitaji huyo mtoto,” alishauri Roby kabla hajajiendea zake. Darren akamsindikiza kwa macho akitamani kumwambia mwanaume huyo asimwambie Melissa chochote kile.
Alijua fika angemwambia hivyo Melissa basi mwanamke huyo angefika hapo ndani ya masaa machache. Hakutaka kabisa kuwa karibu na mwanamke huyo. Lakini angemwelezaje hivyo Roby?
Roby akaenda zake. Darren akajikusanya na kwenda nyumbani kumlisha mtoto na kuweka mambo mengine sawa. Alipohakikisha kila kitu kipo kwenye utaratibu, akaenda kuoga aondoe uchovu.
Alipotoka bafuni na kutazama simu yake akakuta ‘missed calls’ toka namba ya Roby. Baada ya kujiuliza kidogo akapiga na kupachika simu yake sikioni. Baada ya kuita kidogo, ikapokelewa. Ajabu likuwa ni sauti ya kike. Sauti ambayo si ngeni masikioni mwa Darren.
“Hujambo?”
“Sijambo. Nani?”
“Umeshanitambua, Darren. Najua namba yangu umeifunga.”
“Unataka nini Melissa?”
“Nimesikia una matatizo. Vipi upo sawa?”
“Ndio, nipo sawa. Kuna lingine?”
“Pole sana, Darren. Najua matatizo unayoyapitia hivi sasa. Usi–”
“Melissa! Naomba niskize vema, sawa? Sitaki kuwasiliana na wewe. Naomba uachane na mimi. Tafadhali. Na kama ukiendelea kunisumbua basi nitamwambia Roby juu yako.”
Melissa akaangua kicheko.
“Huoni utakuwa umenirahisishia kazi, Darren?” akauliza. “Kama ukimwambia Roby kuhusu mimi na wewe, nami nitamkubalia kila kitu na kumwongezea taarifa zaidi. Mosi, urafiki na ubia wenu utakuwa hatihati, pili, utakuwa umenisafishia njia ya mimi kurudi kwa–”
Darren akakata simu. “Shenzi!” akatupia simu kochini na kudaka kichwa chake kwa mawazo.
Melissa akasonya akitazama simu yake, kisha akamtazama Roby aliyekuwa amelala kitandani fofofo. Akanyanyuka na kujiondokea zake akimwacha mwanaume huyo hajielewi A wala Z.
Akashuka mpaka chini na huko akapanda gari la Roby na kutimka akienda tusipopajua.
Baada ya muda kidogo, Darren akamwona akiwa anasinzia. Alikuwa tayari ameshakula na ni usiku sasa. Aliwaza kumlaza mtoto huyo alafu aende mwenyewe hospitali, lakini akasita. Atamwachaje mtoto hapo? Akafikiri afanye nini.
Baada ya muda kidogo akaona ni kheri tu kama ataenda na mtoto huyo hospitali. Asingekuwa na amani kama mtoto huyo angelibaki mwenyewe nyumbani. Hakuwa na budi. Akajifungia mwanaye kifuani kwa kibebeo maalum kisha akabeba chupa ya maziwa endapo kama mtoto atahitaji hapo baadae.
Akajiweka kwenye gari na safari ya kwenda hospitali ikaanza. Alifikiri sana alipokuwa njiani. Maisha yalikuwa yamebadilika pasipo mkewe, inabidi atafute namna, hawezi akawa anaongozana na mtoto muda wote. Vipi akihitaji kwenda kazini?
Akiwa kwenye foleni la mataa, akakubali na nafsi yake kuwa kwa kipindi hiki ambacho mkewe anaumwa, inabidi amtafute ‘babysitter’ atakayemtazama mtoto na kumpa mahitaji yake. Na pale mkewe atakaporejea kwenye hali yake basi mhudumu huyo atajiendea zake.
Ila akapata tena wazo jingine, vipi kama akiwa anampeleka mtoto huyo mahali pa kutunzia watoto, ‘daycare’, huko awe anampitia akitoka kwenye mihangaiko yake?
Kidogo wazo hili likawa gumu. Aliona ni kama kumtupa mtoto wake kwa kufanya hivyo. Hapana, siwezi, akawaza. Hakuwa na imani sana na hiyo njia hivyo akachagua ile ya kwanza, amtafute dada atakayekuwa anamsaidia.
Akaendesha gari mpaka hospitali. Alipofika huko akazima gari lake na kukwea kwenda juu. Aliposonga kuendea pale ambapo mkewe alikuwa amepumzishiwa, akastaajabu kumwona Melissa!
Mwanamke huyo alikuwa amesimama akitazamatazama huku na huko, mkononi mwake ana simu kubwa nyeusi anayoipigapiga kiganjani. Alikuwa ni kama mtu aliyepotea.
Darren akamfuata kwa hasira na kusimama mbele yake akimuuliza, “Umekuja kufanya nini hapa Melissa?”
“Kukuona,” Melissa akajibu kwa tabasamu. “Kwani kuna ubaya?”
“Melissa, nikuambie mara ngapi wewe?”
“Kwani Darren mimi nimekuambia mara ngapi? Ushawahi kunielewa?”
“Hivi hauogopi hata Roby akijua upo hapa.”
Melissa akaguna kwa cheko. “Roby?” akauliza na kisha akatabasamu. “Hawezi jua. Amejilalia hajiwezi!”
“Melissa, nikuombeje uachane na maisha yangu? Nikuombeje, ebu niambie. Melissa achana na maisha yangu. Naku–” Mara nesi akapita na kuzama ndani ya chumba alicholazwa Josephine. Kidogo tena, mlinzi aliyekuwa amevalia sare zake akajongea eneo hilo na kuuliza, “Kuna tatizo hapa?”
Darren akamtazama Melissa, Melissa akamjibu mlinzi, “Hamna tatizo, bwana. Waweza tu kuendelea na majukumu yako mengine.”
Lakini kabla mlinzi hajaondoka hapo, mara nesi akatoka chumba cha mgonjwa akiwa anatembea kwa kasi sana. Darren akapatwa na hofu. Kidogo tu, nesi akarejea na daktari wakazama mule chumbani.
Kama baada ya robo saa, daktari akatoka na kumwambia Darren kuwa mke wake amefariki.
Darren alihisi daktari anamtania. Aliuliza mara nne kama alichoambiwa ni kweli na daktari asibadilishe maneno akarejelea kauli yake ile ile na kisha kumpa pole Darren kwa kumpoteza mtu wake wa karibu.
Darren akalia kama mtoto mdogo. Msalaba huu ulikuwa ni mkubwa sana kwake. Hakujiona kama anaweza kuubeba. Bado alikuwa anamhitaji mke wake haswa kipindi hiki ambacho mtoto ni mdogo.
Ataishije? Alijiuliza akiwa anamwaga machozi kwenye benchi. Melissa alijaribu kumtuliza lakini asifanikiwe. Bwana huyo aliendelea kulia kwa uchungu kwa kumpoteza mpendwa wake. Mwishowe hata machozi na sauti ikawa imemkauka.
**
Baada ya watu wote kuondoka na kumwacha makaburini, Darren aliijipangusa mdomo wake na kutazama kaburi la mkewe. Bado halikuwa limesimikwa jina wala maelezo yoyote yale. Macho yake yalikuwa makavu na meupe, hakulia siku hiyo.
Alichuchumaa na kusema mwenyewe akiamini anateta na mkewe, “Nakupenda sana, mke wangu. Umeondoka tukiwa hatujamaliza tofauti zetu. Roho inaniuma sana kwa hilo lakini sina cha kufanya. Nisamehe sana mpenzi.”
Aliposema maneno hayo akanyamaza kwanza. Macho yakaanza kujawa na machozi. Akajipangusa na kuendelea kusema, mara hii sauti yake ikiwa inatetemeka. “Sijui nitaishi vipi pasipo wewe. Sijajua …” akajipangusa chozi. Alikuwa anahisi kifua chake kinawaka moto. Moyo umekuwa mzito sana. Alikuwa anajihisi hovyo, hovyo ambayo haiwezi kuelezeka.
“Umekuwa mwanamke wangu wa kujivunia kwa muda wote huo. Siwezi kueleza ni kwa namna gani ulijaza upendo na furaha ndani ya nyumba yangu. Hakika hakuna wa kuziba pengo lako. Maisha yangu hayatakuwa sawa tena pasipo na wewe.”
Kisha akanyanyuka na kuendea gari, akajipakia kwenye viti vya nyuma na kufunga mlango, gari likaondoka. Dereva alikuwa Roby, pembeni yake akiwa amekaa Melissa.
Japo watu walikuwa wawili kwenye gari, Darren hakuongea chochote. Alikuwa kwenye ulimwengu wake wa pekee kabisa. Akiwa amelaza kichwa chake kwenye kiti, alikuwa anatazama nje. Uso wake ulikuwa umepooza na kupwaya. Alikuwa mbali sana kimawazo.
Gari lilisimama mbele ya nyumba yake, Roby akamgeukia na kumuuliza kama yuko sawa, lakini hakuwa anasikia kitu. Ilimbidi Roby arejelee swali lake mara tatu ndipo Darren akamtazama na kumjibu. “Niko sawa, nashukuru.”
Na kabla halijaongezewa neno lingine, akafungua mlango na kutoka ndani ya gari. “Kwaheri!” akapunga mkono wake mara moja kwa Roby kisha akajigeuza na kuelekea ndani kwake.
Basi baada ya hapo maisha ya Darren yakabadilika kabisa. Hakuwa mtu wa kuzungumza bali kukaa kimya na kujitenga. Mara nyingi alikuwa ni mtu wa mawazo sana na hata kulia. Ndani ya juma moja tu akapungua uzito kwa kiasi kikubwa sana. Alikuwa ni kana kwamba mtu anayeliwa na kansa hatua ya nne.
Hakuwa na raha. Ilikuwa ni nadra kwake kutabasamu ama kucheka. Roby akajitahidi sana kukaa naye na kumhasa lakini haikusaidia. Naye Isabel akajaribu sana kujiweka karibu na Darren, lakini bado jitihada zake zikagonga mwamba. Darren hakuwa anataka kukaa karibu na mtu. Alikuwa anataka kukaa mwenyewe tu.
Akirudi nyumbani humuuliza dada wa kazi juu ya maendeleo ya mtoto kisha anamwona mwanaye kwa muda mfupi na kwenda kujilaza. Siku nyingine akawa anarudi nyumbani akiwa na chupa za vinywaji vikali. Anakunywa pasipo kujionea huruma na kisha analala kama mfu.
Siku nyingine hata kazini akawa haendi. Anakunywa tu siku nzima. Afya yake ikaendelea kuzorota.
Ikiwa ni mwezi mmoja umepita tangu Josephine afariki, Darren akajiona sasa anahitaji msaada. Alionana na mwanasaikolojia na kumweleza shida yake kwa ajili ya ‘counselling’. bwana huyo mwanasaikolojia, bwana Hamlet, akajitahidi kadiri ya uwezo wake kumsaidia Darren kwa kumpatia ushauri, lakini Darren akaenda mbele zaidi kwa kumwambia na yale mengine yakutisha. Mambo anayoona usiku na viumbe wa ajabu.
Hapo bwana Hamlet akasita kumshauri. Mwanzo alihisi Darren atakuwa amekanganyikiwa kutokana na kumpoteza mtu wake wa karibu lakini baadae akaja kuelewa baada ya Darren kumwambia alishawahi kuyaona mambo hayo hata kabla ya mkewe kufariki.
“Tafadhali, unaweza kunisaidia?” Darren alilia. Bwana Hamlet akamtazama kwanza mwanaume huyo kwa mafikirio kisha akamsihi apate muda wa kupumzika zaidi, pia kama itakuwa inawezekana basi akatafute mahali pengine pa kuishi mbali na hapo alipo. Pengine yaweza kumsaidia.
Darren akashukuru kwa ushauri na kwenda zake. Alipojiweka kwenye gari akafikiria kwanza maneno aliyoambiwa na bwana Hamlet.
Akiwa fikirani humo, mara upepo wa wastani ukapuliza kiasi na kupeperusha gazeti fulani lililokuwa chini mpaka kwenye kioo cha gari lake. Gazeti hilo lilikuwa la kale kidogo. Upande ambao ulijipachika kiooni ulikuwa na picha ndogo tatu na maelezo kadha wa kadha.
Katika maelezo hayo, mojawapo ilisomeka; *“MWANAMKE ANAYESUMBULIWA NA VIUMBE WA AJABU, APOTEA.”*
Habari hiyo ilikamata fahamu za Darren. Kidogo upepo ukalisomba gazeti hilo na kulitupia kando na kuliburuza zaidi na zaidi. Darren akatoka kwenye gari na kulikimbilia. Akalinyaka na kurudi ndani ya gari. Akatulia na kusoma taratibu habari ile ambayo ilimkamata hisia.
Alipomaliza kusoma akaliweka gazeti hilo kando na kutazama akiwa amejawa na mawazo. Kidogo akawasha gari na kuendea anwani ya nyumba ambayo ameona taarifaze kwenye gazeti.
Alitembea barabarani kwa masaa matano. Ilimlazimu aweke mafuta ili akamilishe safari yake. Alipofika, ilikuwa ni nyumba ya mbao yenye ukubwa wa wastani, akagonga na punde akafunguliwa na binti mwenye makamo ya miaka ishirini, akaeleza shida yake anataka kuonana na wazazi.
Binti akamkaribisha ndani na kidogo akaja mwanamke mnene kidogo mwenye nywele fupi nyeusi. Mwanamke huyo alikuwa ana macho makali na mkononi mwake alikuwa amebebelea kitambaa alichokuwa anatumia kukaushia vyombo. Yule binti aliyemkarimu mgeni akaenda zake chumbani.
“Habari, naitwa Darren.”
“Karibu, naweza kukusaidia,” aliuliza yule mwanamke akiwa anatazama kwa mashaka. Hakuwa na imani machoni. Darren akaeleza shida yake akionyesha lile gazeti. Alikuwa anataka kusikia habari zaidi za yule mwanamke aliyepotea. Kwa namna moja ama nyingine alikuwa anaona habari hiyo na ile ya maisha yake zinawiana.
Baada ya kusema hivyo yule mwanamke mwenyeji akatazama chini na kisha akarudi alipotokea, jikoni, kisha baada ta muda kidogo akarudi akiwa hana kile kitambaa bali ana kisu. Kidogo Darren akahofia. Mwanamke yule akaketi kiti kitazamanacho na Darren alafu akaweka kisu chake mezani.
Kisu kilikuwa kina mpini wa bluu, na kama ungekitazama vema ungeona maandishi yasomekayo ‘stainless steel’ kwenye shina la makali yake. Kilikuwa ni kisu kirefu chenye ncha kali. Darren alishindwa kujizuia kutokutazama kisu hicho.
“Upo tayari na utasadiki?” akauliza mwanamke yule akiwa anamtazama Darren machoni.
“Ndio, nipo tayari,” Darren akajibu. Basi mwanamke yule akanyanyua kisu kile na kukichomeka kwanguvu mezani. Kisu kikachimba meza na kusimama dede. Darren akazidi kuhofu.
Basi mwanamke yule akaanza kusimulia kwa sauti yake inayofanana na kasuku. Akiwa ameongea sentensi mbili tu, upepo ukapuliza dirishani na kupeperusha pazia kama bendera. Darren akatazama huko upesi akiwa mjawa wa mashaka.
Mwanamke yule akiwa anamtazama Darren machoni akasema ya kwamba yeye hana majibu ambayo Darren alikuwa anayauliza, ila tu amefurahishwa sana na uwepo wa Darren hapo. Lakini inawezekanaje hilo na ingali Darren hajuani na mwanamke huyo?
Darren alipouliza, akatahamaki mwanamke yule anabadili rangi ya macho yake na kuwa nyeusi kama bendera. Alafu mwanamke huyo akachomoa kisu chake toka mezani na kumrukia Darren akitaka kumchoma.
Ilikuwa ni swala la kufumba na kufumbua tu, nyumba ile ikawa ghofu kabisa. Paa lake lilijawa na tando za buibui na madirisha yakiwa yamepotea yasionekane. Kulikuwa giza, mwanga hafifu rangi nyekundu ikiwa inatambaza kwa mbali.
Ilikuwa ni ajabu namna gani ambavyo mambo yalbadilika kwa upesi namna ile! Nyumba iliyokuwa ni nzuri ikageuka na kuwa nyumba ya mizimu, nyumba ya majini! Harufu ya damu ilitawala na mifupa huku na kule.
Kwa Darren yalikuwa ni kama mazingaombwe ama maigizo! Hakuwa anaelewa kinachoendelea hapa. Kila kitu kwake kilikuwa ni kama amerukwa na akili. Kitu pekee alichokuwa ana kijua na kupambana nacho ni kuokoa nafsi yake dhidi ya umauti uliokuwa unataka kumkumba.
Hakujua alikuwa amezama. Tena amezama kwenye lindi zito la kifo. Ameshikwa kwenye tego kali la kummaliza.
Akapambana kumzuia mwanamke yule asimkite na kisu, na alipofanikiwa kufanya hivyo baada ya kumtwanga mwanamke huyo kichwa cha puani, akakimbilia mlango afungue na kwenda, lakini alipofika mlango haukufunguka abadani! Haikujalisha ni nguvu kiasi gani alitumia, mlango ukamtazama kodo pasipo mafanikio.
Yule mwanamke akacheka sana. Akanyanyuka toka chini huku akijitoboatoboa na ncha ya kisu kana kwamba godoro. Ilikuwa ni ajabu kwamba ahisi maumivu? Akavuja damu na kujichafua haswa lakini hakuwa anajali hata kidogo.
Alimtazama Darren kwa macho ya matamanio, alafu akalamba kisu chake kana kwamba mtoto na mche wa ‘ice-cream’, alafu kufumba na kufumbua akamkimbilia mwanaume huyo akammalize. Mwendo wake ulikuwa wa kasi sana, lakini kabla hajafika aendapo, kumbe Darren alikuwa ameshakamata stuli kwa mikono yake miwili, akamkandika kwanguvu mno! Puuh!!! Mwanamke huyo akasombwa na kubwagwa ukutani, kisha kukawa kimya!
Darren, akiwa anahema kwa hofu, akamtazama mwanamke yule kwa jicho la tahadhari. Bado mikononi akiwa ameshikilia ile stuli yake endapo lolote litajiri. Ikapita dakika ya kwanza kukiwa kimya. Dakika ya pi… akasikia mlango unafunguliwa! Akatupa macho yake kupambana na kiza kilichopo apate kuona.
Hakuona kitu!
Moyo wake ulikuwa unamwenda mbio sana. Kwasababu kulikuwa na ukimya wa kufanya masikio yawe kiziwi, Darren alikuwa anaweza kusikia mapigo yake ya moyo kwa uzuri kabisa. Angeliweza kuyahesabu pasipo matatizo kabisa.
Kidogo, akapata wazo la kutumia stuli ile kubomolea mlango. Akabondea hapo mara kadha wa kadha. Akaponda na kubonda lakini mlango haukufunguka. Ulikuwa ni migumu kama ile ya kasri ya mfalme. Ulikuwa ni mgumu kana kwamba malighafi yake ni chuma na metali! Badala ya mlango kukongoroka, ni stuli ndiyo ikaanza kuwa dhoofu na kuanza kumomonyoka!
Mwishowe Darren akabakiwa na vipande tu vya stuli mkononi mwake ingali mlango ukiwa madhubuti.
Akainama kwa kuchoka. Akahema sana akivuja jasho. … lakini nyuma yake kule kulipotoka sauti ya mlango kulikuwa na nini? Kama ungetazama vema, kwa kuyafinya macho na kusisitiza maono yako basi ungeliona kuna kiumbe kilikuwa kinatembea gizani kumjongea.
Miguu ya kiumbe huyu ilikuwa inakanyaga sakafu taratibu. Kwasababu ya kiza, hakikuwa kinaonekana vema.
Kilisonga kwa hatua ya karibu lakini harakaharaka.
Darren alihisi kitu, upesi akageuka na kuangaza koridoni, kizani. Hakuwa anaweza kuona kitu. Japo alikodoa bado hakuwa na uwezo wa kuona jambo. Alipomtazaa yule mwanamke aliyemsomba kwa kumkita awali, akamwona bado amelala palepale. Sasa ni nini hicho anahisi? Akajiuliza.
Kufumba na kufumbua, Darren akastaajabu kuona kitu juu ya paa. Hajakaa vema wala kujitengenezea, kiumbe hicho kikamvamia na kumwangusha chini kikimkaba na kumng’ata shingoni!
Mdomo wake ulikuwa wa baridi sana. Meno yake yaliyochongoka yalikita kwenye mishipa ya shingo ya Darren na kisha koo lake likawa linamnyonya damu!
Kwa ubaridi wa kinywa hicho, Darren akahisi mwili wake umezamishwa kwenye dimbwi la barafu. Alihisi baridi toka kwenye nyayo yake mpaka utosini. Lakini baridi hili likiwa linakera! Baridi linalotisha.
Pumzi ya kiumbe hicho ilisabahi shingo yake na kuzidi kumtia hofu na kimuhemuhe.
Kheri Darren bado alikuwa na vipande vile vya stuli mkononi. Kama mtu aliyepandwa na kichaa, akatumia vipande hivyo kwanguvu na pasipo mafikirio kumshabulia kile kiumbe kilichomshikilia.
Akamtoboatoboa kiasi kwamba hata yeye akajiumiza. Kile kiumbe kikapiga kelele na kuangukia chini. Kabla Darren hajamtazama mvamizi wake huyo akagundua kuwa shingoni alikuwa anachuruzwa na kimiminika cha moto. Alipojipapasa akagundua ni damu! Alikuwa anchuruzwa na damu nyingi na akihisi maumivu makali.
Alimtazama kiumbe kile alichoadhibu na kubaini alikuwa ni yule mtoto aliyemkaribisha na kumfungulia. Alikuwa amejilaza akiwa ametulia na kuvuja damu. Alipotazama kule ambapo alikuwa amelala yule mwanamke aliyemwadhibu mwanzoni, ajabu hakuona kitu!
Akiwa ameweka kiganja chake shingoni kuzuiza damu zinazotiririka, akajongea na kuangaza pale alipokuwa amemwona mwanamke yule mwanzoni. Lah! Hakuwapo. Hapo akapata hofu sana. Kutokuwapo kwa mtu huyo kulikuwa ni ishara mbaya kwa usalama wake.
Akatazama kushoto na kulia, juu na chini asione kitu! Moyo wake bado ulikuwa unadunda kwa kasi, na damu bado zamchuruza kufurika vidole vyake. Ni wazi alikuwa ana muda mfupi wa kuwa hai kama jeraha hilo lisingepata huduma ya upesi.
Aliendelea kuangaza na kuangaza. Kidogo akahisi upande wake wa kulikuwa na kiumbe. Alirusha macho yake upesi akikodoa. Mkono wake wa kuume alikuwa amebebelea kipande cha stuli na ule wa kushoto ukiwa umehifadhi jeraha.
Baada ya muda kidogo, akaona kuna kitu chenye rangi nyeupe ya kufifia mule kizani. Alipojaribu kukaza macho yake atazame, akashindwa. Alikuwa ameanza kuishiwa na nguvu na macho yake yakijawa na ukungu.
Aliona kiza kimeongezeka maradufu … Mkono uliobebelea silaha nao ukaanza kupwaya.
Kidogo akaona kitu kile chenye rangi nyeupe kikisogea zaidi karibu yake. Alikuwa ni mtu lakini alishindwa akumtambua kutokana na macho yake kudhoofu. Na hata alipotaka kumshambulia mtu huyo kwa kutumia silaha yake, hakuweza. Hakuwa na nguvu hiyo tena. Jeraha lilishamzidi nguvu.
Akazabwa kofi shavu lake la kulia na kudondoka chini. Hata hakuhisi maumivu tena. Kitu pekee ambacho kilikuwa hai kwenye mwili wake ni macho yake yaliyokuwa yamekodoa na kuoa ukungu. Aliona tu kiza, kiza na yeye.
Na jambo la mwisho ambalo alilielewa ni kushikwa shati lake na kuburuzwa. Kidogo tu akapoteza fahamu kabisa.
Yalikuwa yamekwisha.
Hakuelewa kinachoendelea hata kidogo. Alikuja kupata ufahamu wake akiwa kwenye gari, viti vya nyuma. Alikuwa amechoka mno, kichwa kinamuuma. Mwili wake anauhisi dhaifu viungio vyote vikiwa vinapwita.
Alijaribu kunyanyuka, akashika kiuno kwa kulalama. Alijikaza akanyanyuka vivyo hivyo na kisha akatupa macho yake kwenye kioo cha mbele cha gari. Ajabu alipotazama hapo akaona kipande kile cha gazeti chenye taarifa juu ya mwanamke yule aliyekumbwa na mikasa kama yake. Kipande kilekile cha gazeti ambacho kilimwelekeza kwenda kule kwa watu wa ajabu.
Akashtuka baada ya kukumbuka mkasa alopitia. Hakika haukufaa kusimulia. Kidogo gazeti lile likapeperushwa na upepo na punde akaonekana mtu akiwa amekaa kwenye kiti cha pembeni ya dereva. Mtu huyo ametulia tuli akitazama mbele.
Darren akashtuka kumwona mtu huyo maana hakumwona hapo awali. Hakujua wapi ametokea. Akaita kwa woga na kuuliza ni nani? Kidogo mtu huyo akageuka na kumwangazia Darren. Kumbe alikuwa ni Melissa.
“Melissa!” Darren akafoka. “Kumbe ni wewe?”
Alipandwa na hasira sana. Alijikuta ananyanyuka toka kwenye kiti chake na kumvamia Melissa. Akamkaba na kumtwanga ngumi mfululizo kwa hasira akiwa anafoka, “Niache na maisha yangu! Niache wewe mpuuzi! Niache! Niache!”
Melissa akajikinga na mashambulizi makali ya Darren, lakini alipoona yanamzidia, akamtupia mwanaume huyo nyuma ya gari! Alimnyanyua kana kwamba usufi. Na Darren, kama mfuko wa saruji, akadondokea vitini na kulalamikia maumivu ya kiuno chake.
“Niskize Darren!” Melissa akapaza sauti yake kali. Vioo vikachipua nyufa. “Kwanini hautaki kunielewa?” akauliza akiwa anamtazama mwanaume huyo kwa macho mekundu. “Kwanini unakuwa na moyo mzito na kichwa kigumu?”
Akaongea sana lakini Darren asijali. Alikuwa anagugumia maumivu ya kiuno huku akiwa anamtazama Melissa kwa jicho la mbali. Melissa alipomaliza kujichosha kwa kuongea, Darren akamwambia kwa sauti ya chini akiwa anachuruza chozi jicho lake la kushoto, “Toka kwenye gari langu. Ondoka mbele yangu Melissa.”
Melissa akamtazama Darren kwa sekunde nne pasipo kusema jambo. Macho yake yalidondosha machozi. Alifungua mlango wa gari na kujiondokea, Darren akashusha pumzi ndefu. Alikuwa anazidi kumwaga machozi aking’ata meno. Mwishowe alishindwa kabisa kujizuia, akalia kilio kikuu.
Akalia sana akiwa anajiona yupo kwenye lindi kubwa la matatizo. Akalia haswa akihitaji kusafisha kifua na kichwa chake. Mwishowe alipojiona kuwa yu sawa, akasonga kwenye kiti cha dereva na kuwasha gari lake aondoke.
Akiwa njiani akawaza sana namna gani aenende. Aliwaza sana nini afanye kujiondokea na matatizo, hata akawaza kujiua, lakini akifanya vivyo nani atakaye mwangalia mtoto wake? Mkewe alishafariki.
Aliendesha akiwa anamwaga tu machozi. Alipofika nyumbani akajilaza kitandani kwake pasipo kumtazama mwanaye. Alikuwa anawaza sana. Ilipofika majira ya usiku, Isabel alimpigia na kumwomba waonane.
**
Usiku wa saa tatu ….
Kulikuwa kumetulia kabisa, ungeweza kusikia mdomo wa Isabel ukitafuna. Mwanamke huyo aliyekuwa amevalia suti rangi ya zambarau alikuwa ameshikilia sambusa mkononi mwake na glasi ya sharubati ikiwa mezani.
Mbele yake alikuwa ameketi Darren akiwa na glasi ya mvinyo mwekundu pekee. Hakutaka kula maana hakuwa na hamu wala kujisikia kufanya hivyo, uso wake ulikuwa umepoa, mara nyingi akitazama watu wanaoingia na kutoka eneo hilo walilopo. Hakuwa sawa.
Kidogo Isabel akamshtua na kumuuliza, “Utakuwa kwenye hali hiyo mpaka lini, Darren?”
Darren akaminya lips zake asiseme kitu. Alitazama glasi yake ya kinywaji kwa mawazo.
“Inabidi uniruhusu nikusaidie Darren. Tafadhali.”
Bado Darren hakusema jambo. Isabel akanywa sharubati yake na kisha akajifuta mdomo kwa ‘tissue’.
“Darren ukiendelea hivi utashindwa kufanya kazi zako. Maisha yako yatapotea. Serious, inabidi ubadilike. Niambie nini tatizo.”
Darren akanywa kwanza mafundo mawili alafu akashusha pumzi ndefu kabla hajasema, “Unajua hapa karibuni nimepitia mambo makubwa sana. Nadhani badi sijapata muda wa kutulia. Bado akili yangu haijakaa sawa.”
“Najua, Darren,” akasema Isabel. “Najua umepitia milima na mabonde hapa karibuni. Lakini inabidi uache vitu viende, sawa? Hauwezi kuishi hivi milele? Hauoni namna unavypungua kwa mawazo? Inatosha Darren. Mfikirie mwanao. Vipi kama ukipatwa na tatizo, atakuwa kwenye hali gani?”
Darren akakosa majibu. Alifikicha macho yake akashika tama.
“Sikia, Darren. Ningependa niwe karibu zaidi na wewe. Naomba uniruhusu,” Isabel akapendekeza.
“Ukaribu kiasi gani, Isabel?” Darren akauliza. “Kwani hapa hatuko karibu?”
“Tuko karibu lakini nataka kuwa karibu zaidi. Naomba uniruhusu Darren. Nataka kuwa karibu na wewe zaidi.”
Wakatazamana kwa kama sekunde tano. Kulikuwa na kitu machoni mwa Isabel.
“Unaweza ukaja kuishi kwangu,” Isabel akapendekeza. “Naishi mwenyewe pamoja na wafanyakazi. Nadhani nitakuwa na wigo mpana wa kukusaidia. Mtoto wako pia hatapata shida. Unasemaje Darren?”
Darren akabinua mdomo wake. Akanyanyua glasi ya kinywaji na kupiga mafundo mawili tena kisha akamtazama Isabel machoni.
“Hapana, Isabel. Haiwezi kuwa haraka kiasi hicho.”
“Nini tatizo?” Isabel akauliza kwa kujiamini. Macho yake makali yalikuwa yanamtazama Darren barabara.
“Si kwamba kuna shida,” Darren akajibu. “Ila tu sijajiandaa kufanya hivyo. Hauoni kama ni hatari?” Isabel akatikisa kichwa.
“Kwa upande wangu, sioni kama kuna shida. Sijajua kwako.”
“Nipe muda nifikirie zaidi juu ya hilo. Siwezi harakisha.”
“Sawa. Muda gani unakutosha kufanya vivyo?”
“Nitakutaarifu, usijali.”
Lakini jibu hilo halikumridhisha Isabel. Alipokunywa fundo moja kumalizia kinywaji chake akauliza, “Kwanini usinipe muda halisia, Darren. Huoni unaweza kuningojesha milele kwa kauli hiyo?”
Basi Darren kwa kulazimika, akasema mpaka juma lijalo atakuwa tayari ameshampatia jibu. Angalau Isabel akafurahi. Wakamalizia maongezi yao kwa kuongea biashara juu ya ile nyumba ya bibi yake Darren kule ‘countryside’, wakaafikiana mpaka bei, ambapo ilikuwa pesa kubwa sana.
Kwa mawazo ya Darren aliona ni kheri akamuuzia Isabel nyumba hiyo kwani haikuwa na faida tena kwake, lakini zaidi apate kiasi cha pesa kitakachomwezesha kuwa na makazi mapya, makazi ambayo yatakuwa salama kwake na familia yake. Aliwaza pengine akihama, anaweza akapata pumziko la kichwa chake.
“Kwahiyo utaingiza lini hiyo pesa?” Akauliza.
“Kesho mchana,” Isabel akamjibu. Kidogo Darren akashangazwa, kilikuwa ni kiasi kikubwa cha pesa kupatikana haraka namna hiyo!
“Kuna shida, Darren?”
“Hapana. Hamna tatizo kabisa.”
“Sawa. Kesho tazama akaunti yako kuanzia majira ya saa sita mchana.”
Wakakubaliana hilo na basi kama alivyomleta, Isabel akamrejesha Darren nyumbani kwake, lakini kabla hajashuka, akamshika mwanaume huyo mkono wake wa kushoto na kumtazama kidogo.
“Kama kutakuwa na tatizo nijulishe Darren.”
Darren akatikisa kichwa chake kuafiki alafu akashuka toka kwenye gari na kwenda ndani. Kulikuwa ni kimya. Alishangaa kukuta hali hiyo. Akamwita dada wa kazi mara tatu pasipo majibu. Akapata shaka kidogo. Akanyanyuka na kwenda vyumbani, akakagua kila chumba lakini hakumwona dada wa kazi wala mtoto wake. Hapa shaka lake likakua zaidi.
Akajaribu kupiga simu ya dada wa kazi, ikaita, ila alipotulia na kuskiza vema akagundua simu hiyo inaitia ndani. Alipoenda chumbani kwa dada huyo akabaini simu ilikuwa imefunikwa na shuka. Sasa ameenda wapi na mtoto?
Tumbo likaanza kumsokota.
Alitoka ndani kwake akaenda kuuliza majirani kama wamemwona msichana huyo na mtoto wake lakini hakupata kitu. Alihisi kuchanganyikiwa. Alirejea ndani akaketi akiwaza na kuwazua. Muda ukaenda mpaka majira ya saa tatu usiku.
Sasa akaona ni vema atoe taarifa polisi kwa uchunguzi zaidi. Akatoa kila taarifa aliyoifahamu na polisi wakaanza kazi yao. Lakini kwenye majira ya saa nne usiku, dada wa kazi akarejea akiwa na mtoto.
Dada huyo mkononi alikuwa amebebelea vitu vya mtoto na kwa kutumia kibebeo maaulum alikuwa amembelea mtoto kifuani mwake. Darren akafurahi sana kumwona mwanae. Akamkumbatia kwanguvu na kumuuliza dada wa kazi wapi alikwenda kwa muda wote huo.
“Nilienda kumchukulia mtoto mahitaji yake,” dada akajitetea. “Lakini nilikutana na msongamano mkubwa wa magari sababu ya ajali. Samahani sana.”
Baada ya maelezo hayo, dada huyo akaenda chumbani kwake akimwacha Darren na mwanaye pale sebuleni. Darren akatoa taarifa polisi juu ya kumpata mwanaye.
“… Nashukuru sana, nitakuwa mwangalifu zaidi siku nyingine.”
Alipokata simu ndipo akagundua kuna kitu kwa mwanaye.
Nyuma ya mgongo wa mwanaye, chini kidogo ya bega la kushoto, aligundua kuna chapa fulani ndogo. Chapa hiyo ilikuwa nyeusi yenye ishara kama ya msalaba lakini ikiwa na mikono miwili.
Hakujua maana ya chapa hiyo lakini alijikuta akiwa na wasiwasi nayo. Alijaribu kuifuta kwa kutumia kidole chake, haikufutika. Akajaribu kumfuta na kitambaa bado napo haikufutika, ilikuwa ni alama ya kudumu!
Upesi akamuuliza dada wa kazi apate kujua nini kimemtokea mtoto. Lakini dada, akiwa ameparamiwa na uso wa hofu, akajitetea sana. Hakuwa anafahamu lolote. Hakuwa anajua hata kama mtoto ana chapa hiyo? Amemwogesha jana yake na hata siku hiyo asubuhi lakini hakuona alama kama hiyo.
Darren akatingwa na maswali lakini pia na hofu. Hakuhisi kama mwanaye yuko salama. Kila mara alitazama alama hiyo na kujiuliza maswali mengi kichwani. Mwishowe aliona ni kheri akafanya jitihada zaidi kung’amua chapa hiyo na hapo ndipo akazama kwenye mtandao na kusaka alama ile baada ya kuiweka kwenye mashine yake.
Baada ya muda kidogo akapata kuona taarifa chache juu ya chapa hiyo ikiwa inahusishwa na habari za zamani sana kuhusu huko Uajemi tena ni ishara aghalabu ya majini!
Alipotafuta sana akabaini kuwa mwanawe hakuwa mtu wa kwanza kuwa nayo, takribani watu watatu walikuwa nayo, ila mwisho wao wote ilikuwa ni kifo! Alipohangaika zaidi kutafuta mengineyo, akapata kukutana na mwanamke mmoja ambaye mwanaye alikuwa na chapa hiyo. Alituma hilo swala mtandaoni kuomba ushauri.
Basi hilo likawa kama neema kwa Darren. Alitafuta zaidi taarifa za mwanamke huyo akafanikiwa kupata anwani yake, akapanga kesho yake akamtafute amwambie zaidi kuhusu hiyo chapa.
Alihofia sana juu ya mwanaye. Na kwa hofu hiyo akataka alalae nae ndani ya chumba chake.
Ulipofika usiku wa manane, Darren akiwa amelowea kwenye usingizi mzito, na pia nyumba ikiwa imetulia tuli sawa sawa na mtaa mzima, taratibu mlango wa chumba alalacho dada wa kazi, ulifunguliwa na kisha ukatuama pasipo lolote kutokea.
Kulikuwa kimya.
Zilipopita kama sekunde tano, ndipo mkono uliobebelea kisu ukatoka kwenye mlango huo. Bada ya punde, ukafuatia na mguu na kisha mtu mzima kabisa. Alikuwa ni yule dada wa kazi.
Aliyatoa macho yake akikodoa. Alitazama kushoto na kisha kulia, alafu akauendea ule mlango wa chumba cha Darren. Alipoufikia, hakugonga, lah! Akapindua kitasa taratibu na mlango huo ukafunguka. Alipousogeza vya kutosha, akatulia hapo akisimama.
Zikapita kama sekunde nne. Basi taratibu akazamisha mguu wake ndani ya chumba, na taratibu sana, akaweka nyayo zake sakafuni akisonga. Alimwendea mtoto na kumpakua toka kwenye kitanda chake. Lakini mikono yake ilikuwa ya baridi sana. Alipomshika mtoto tu, akaanza kulia.
Akakodoa kumtazama Darren. Darren alikuwa amelala bado fofofo. Lakini sauti ya mtoto iliyokuwa inaendelea kupaza na kupaza ilimshtua sasa akaamka na kuangaza.
alipotazama kwenye kitanda cha mtoto, hakukuwa na kitu. Kitanda kilikuwa tupu kikianza kujenga ubaridi! Akachanganyikiwa sana. Alitazama kushoto na kulia kwake asione kitu, mlango ulikuwa umefungwa, ila sauti ya mtoto bado akiisikia!
Sauti hiyo ilikuwa ikiishilia!
Haraka akatoka kitandani na kudaka korido. Akatazama na kupekua kwa macho yake, kidogo, masikio yake yakamwambia kuwa sauti ya mtoto inatokea kwenye chumba cha dada yake wa kazi!
Akauendea mlango huo na kubisha kwa kuutwanga ngumi. Akaukandika na kuukandika lakini haukufunguliwa. Mtoto bado aliendelea kulia!
Akiwa amepandwa na akili za ukichaa, Darren akaubamiza teke kali mlango huo na kuuvunjia mbali. Alipotazama, akamwona dada wa kazi akiwa amemkabia mtoto kitandani kwa kutumia mkono wa kushoto na ule wa kulia ukiwa umeshikilia kisu akitaka kumchoma.
“Tafadhali, usimuue mwanangu!” Darren akapaza sauti akimtazama dada wa kazi kwa imani. Dada akatabasamu na kusema, “Lazima afe, Darren. Hata kama nisipomuua mimi!”
“Kwanini?” Darren akalia. “Kwanini afe? Sina kitu kingine mbali na huyo mtoto. Nambie unataka nini nitakupatia!”
Dada akatabasamu almanusura kucheka. Alimtazama mtoto kisha akayarudisha macho yake kwa Darren na kusema, “Sitaki chochote Darren. Kama ningekuwa nataka chochote kile basi ningekitafuta na kukichukua mwenyewe. Kwa sasa ninachotaka ni roho ya huyu kiumbe tu, si kingine!”
“Lakini amekukosea nini?” Darren akauliza. Macho yake yalikuwa mekundu yakikaribia kudondosha chozi.
“Hajafanya kitu,” Dada akajibu akitikisa kichwa. “ila si mali yako tena. Huyu ni mali ya majini, na ni wa kufa tu!”
Dada aliposema hayo akamkandika mtoto kisu cha kifuani, chote kikazama na kutosha kumfanya mtoto mfu. Darren akalia sana. Akakurupuka toka kitandani mwake na kumtazama mwanaye pembeni. Nalikuwa ni ndoto. Mtoto alikuwa yu kwenye kitanda chake ila akilia sana.
Upesi akamnyanyua na kujitahidi kumbembeleza … sh!-sh!-sh!-sh!-sh!-sh! … lakini alipotazama dirishani akabaini kuwa li wazi. Akalisongea na kutazama nje kama kuna lolote lile, hakuona jambo. Mtaa ulikuwa umetulia sana. Ni upepo wa baridi ndio ulikuwa ukipuliza tena kwa mbali.
Akalifunga dirisha hilo, bado mtoto akilia, alipomaliza akasikia hodi mlangoni mwake. Kidogo mapigo yake yakaruka. Akiwa amemshikilia mtoto wake vema, akapaza sauti kuuliza,
“Nani?”
“Dada wa kazi!” sauti ikamjibu toka mlangoni. Kidogo akajawa na mashaka.
“Unataka nini?”
“Nimemsikia mtoto analia. Vipi kuna shida?”
“Hapana. Hamna shida.”
“Naweza kukusaidia kumbembeleza?”
Darren akasita kwanza.
“Hapana, ahsante. Nitambembeleza mwenyewe.”
Sehemu Ya 7
Baada ya hapo sauti ya dada haikusikika tena bali mtoto akiwa analia tu. Darren akaendelea kumbembeleza mwanaye akimsihi anyamaze kwani usiku umekuwa mkubwa na yeye amechoka sana. Kwa kama lisaa limoja, mtoto akaendelea kulia tu, akipunguza sauti na kurudi tena upya.
Darren akachoka sana kumbembeleza, mikono ikawa inamuuma, macho yanamsaliti kwa kuwa mazito, kichwa nacho kinachoshwa na sauti kali ya mtoto.
Mlango ukagongwa tena.
“Nani?” akauliza kwa sauti ya uchovu.
“Dada wa kazi!” sauti ikamjibu toka mlangoni.
“Unataka nini?”
“Mtoto ana shida gani?”
“Amekurupuka tu toka usingizini, usijali. Unaweza kulala.”
“Naweza kukusaidia?”
“Hapana! Usijali, nitambembeleza mwenyewe mpaka alale.”
Basi baada ya hapo sauti ya dada wa kazi haikusikika tena, Darren akaendelea kumbembeleza mtoto. Kwa kama nusu saa akawa anafanya zoezi hilohilo tu. Kila alipojaribu kumweka mtoto kitandani ambembelezee hapo, ikawa tabu zaidi, mtoto aliongeza kilio.
Hakujua sasa cha kufanya. Kila mtindo alitumia lakini haikusaidia. Ilifikia kipindi akawa anapitiwa na usingizi ingali amesimama. Alimweka mtoto kitandani kwa kulazimisha akaendelea kumbembeleza hapohapo, kidogo akapitiwa na usingizi.
Kama baada ya dakika mbili akakurupushwa na hodi ya tatu mlangoni mwake. Akauliza, “Nani?”
“Dada wa kazi!”
“Unataka nini?”
“Mtoto anasumbuliwa na nini?” dada akauliza.
“Si nilishakwambia!” Darren akafoka kidogo.
“Naomba nimbembeleze,” sauti ya dada ikaomba.
“Nimesema nambembeleza mwenyewe. Hukunielewa?”
Kukawa kimya kidogo.
Punde sauti ya dada ikasema tokea mlangoni, “Utanipa nimbembeleze ama nije nimchukue mwenyewe?” mara hii sauti ilikuwa na amri ndani yake.
.
Darren akajawa na hofu. Akamnyakua upesi mtoto wake na kumfichama kwenye mikono yake akiwa anatazama mlango kwa hofu. Punde mlango ukaanza kubamizwa kwa nguvu na kwanguvu! Darren akajaribu kuteka simu yake atoe taarifa polisi lakini hakuiona. Kwa muda alikuwa kama mtu aliyechanganyikiwa. Hakujua cha kufanya.
Mlango ukaendelea kubamizwa na kubamizwa. Mwishowe ukaanza kudhoofu na kubomoka. Vipande vyake viliruka huku na huko. Ilikuwa ni ajabu mbomoaji alikuwa anatumia nyenzo gani kufanyia zoezi lake hilo.
Darren alichofanya ni kutwaa kipande kidogo cha mbao ya mlango na kubebelea kama silaha. Ni ajabu kama mtu ameweza kubomoa mlango atamzuiaje kwa kipande cha mbao, lakini alikuwa na imani.
Mkono wake uliobebelea kipande hicho cha mbao ulikuwa unatetemeka. Macho yamemtoka na paji lake la uso linatiririsha jasho.
“Ni nani wewe?” Darren akauliza kwa sauti yenye kusita. Hakujibiwa. Kilichokuwa kinafanyika ni mlango kubamizwa tu! Tena kubamizwa kwanguvu mno.
Kidogo, kwasababu ya hofu na kukurupushwa usingizini, mtoto naye akaanza kulia. Alikuwa analia kwanguvu haswa kiasi cha kumchanganya Darren. Ingawa Darren alimsihi anyamaze, haikusaidia kitu.
Mwisho wa siku mlango wote ukawa upo chini na mlangoni akiwa amesimama mwaname anayechuruza damu mikononi. Mwanamke huyo si mwingine bali dada wa kazi. Mikono yake ilikuwa imejeruhiwa vibaya mno kwa kubamiza mlango hata kuvunjika. Macho yake yalikuwa makubwa yanayong’aa, uso wake umepauka kuwa mweupe.
Alimtazama Darren kisha akainamisha shingo yake kwenda kushoto na kulia, kisha kulia na kushoto. Akamnyooshea kidole Darren pasipo kusema jambo. Alafu kama mtu aliyegandishwa na barafu, akaanza kupiga hatua kumwendea Darren.
Darren akamtisha na kipande chake cha mbao, “Kaa mbali!” akafoka. “Kaa mbali na mimi!” lakini mwanamke yule hakuwa anasikia wala kujali, akaendelea kusonga kumfuata Darren, na alipomkaribia akanyoosha mikono yake yote miwili na kisha akasimama.
Kukawa kimya kidogo. Darren akamtazama mwanamke huyo kwa hofu na maulizo. Naye mwanamke huyo akawa anamtazama Darren kwa macho ya kumpembua. Kidogo akashusha macho yake kwa mtoto na kumtazama kwa sekunde kadhaa, alafu akasema kwa sauti ya kukoroma, sauti ya chini, “namtaka huyo mtoto.” alafu akahema kwanguvu na kusema kwa sauti ya hewa, “Nipatie, nami nitaenda nisirudi nyuma!”
“Wewe ni nani?” Darren akauliza akiwa anamshikilia vema mwanaye. Alikuwa amejiminyia kwenye kona akitamani kutoboa ukuta atokee nje.
Yule kiumbe akamtazama Darren alafu akapindishia shingo yake kushoto. Aliporejesha shingo yake kulia, akasema, “Mimi Melissa.”
“Melissa!” Darren akastaajabu. Hakujua alipata wapi nguvu ila alijikuta akisimama huku akitusi na kulaani. “nimekwambia kaa mbali na mimi Melissa!” punde akazabwa kofi lililomtupia ukutani yeye na mwanaye. Kwa muda kidogo akashindwa kuelewa kinachoendelea. Kwa mbali alisikia sauti ya mwanae ikilia sana lakini hakuwa anaweza kufanya kitu.
Kama baada ya dakika tano, akiwa ameanza kupata nguvu, akasikia sauti yaita,
“Hey! Helloooow!” kidogo mwanga ukatua kwenye macho yake yalofumba, akayafinya na kuyafumbua akiwa anajikinga na mkono wake wa kuume.
“Upo sawa?” alisikia sauti inauliza. Kidogo akabaini sauti hiyo inatokea dirishani. Walikuwa ni majirani, wanaume wawili. Mmoja alikuwa amebebelea bunduki kubwa na mwingine amebebelea gongo kubwa na kurunzi. Walikuwa wamesikia zile kelele na walikuja kutazama jirani yao amepatwa na nini.
Kabla Darren hajajibu kitu, alitazama kwanza kando yake kumtafuta mwanaye. Akamwona akiwa amelala kama hatua tatu tokea alipo. Alikuwa kwenye ukimya wa mbao. Na dada wa kazi alikuwa amelala kwa pembeni yake naye akiwa kimya.
Upesi akamfuata mwanaye na kumtazama. Hakuwa na dalili ya uhai. Alimwita na kumwita lakini ikiwa bure, mtoto hakuitika kwa kucheka wala kulia. Darren akapatwa na hofu kubwa sana ya kumpoteza mwanaye. Alimtikisatikisa aone kama ataamka lakini napo haikusaidia. Mtoto alikuwa amenyamaza. Alikuwa amenyazama milele.
Darren akapiga magoti na kugugumia kwa kilio. Alipata hasira sana. Alinyanyuka kama mbogo akamwendea dada wake wa kazi na kumvuta kwanguvu akimuuliza amemfanya nini mtoto wake, lakini dada naye alikuwa kimya. Hakuweza kuongea wala kujitetea kwa njia yoyote ile.
Darren asijali, akaanza kumuadhibu dada huyo kwa kumkandika mateke. “Shetani! Shetani! Shetani mkubwa wewe! Nitakuua!”
Kama si majirani kuvunja mlango na kuja kumshika, sijui hatma ilikuwa ni nini. Waligundua dada wa kazi alikuwa yu mzima, ila kama mtu aliyekuwa kwenye ‘coma’, hali mfu ya kupoteza fahamu, ila mtoto alikuwa amekwishafariki.
Basi dada wa kazi akawahishwa hospitali kwa matibabu zaidi. Mtoto naye akapelekwa huko kuhifadhiwa kwa ajili ya mazishi, na Darren pia, kwakuwa alihisiwa anaweza akawa si mzima, naye akapelekwa hospitali.
**
Baada ya juma moja …
Darren alikuwa ameketi kwenye kingo ya bahari. Alikuwa amevalia bukta na miguu yake ikiwa tupu pasi na viatu.
Upepo ukimpuliza taratibu, alikuwa anatazama bahari kwa umakini. Kuna kitu alikuwa anawaza kichwani ingawa macho yake yalikuwa yanatazama mawimbi ya bahari. Mkono wake wa kuume ulikuwa umebebelea mchanga, ila akiwa ameuminya kana kwamba anataka kuukosesha hewa.
Macho yake mekundu yalitazama mbali na karibu ya bahari. Yalitazama kushoto na kisha kulia ya bahari alafu akashusha pumzi ndefu. Akanyanyuka na kuanza kurandaranda.
Alitembea akiwa anawaza na kuwazua kichwani mwake. Kila alipofunga macho alimwona mwanae, alimwona mkewe. Ilikuwa ni ajabu na ghafla kwake. Kuna muda hakuwa anaamini kama Josephine hakuwapo naye, wala mtoto wao. Ilikuwa inamuwia ugumu sana kuamini kuwa yu mwenyewe hatimaye.
Alihisi maisha yake yanaparanganyika kama kioo kilichobondwa na jabali. Alikuwa anahisi hana umuhimu wowote maishani hivi sasa. Alikuwa anajihisi mfu anayetembea.
Alikunja ngumi yake akiendelea kutembea. Aling’ata meno yake na kutazama bahari tena, alafu punde akasema, “Melissa!” kwa sauti ya kufifia. Akarudia tena, “Melissa. Melissa. Melissa!” alafu akaapa, “Nitakumaliza kwa mkono wangu mwenyewe. Nitakumaliza Melissa!” alipomaliza kusema maneno hayo macho yake yakawa yanamwaga machozi. Alishindwa kujizuia kuumia. Moyo wake ulikuwa unavuja damu.
Jua likiwa linaanza kuwa kali kumaliza asubuhi, Darren akajirejesha kwenye gari lake na kutimka kuelekea upande wa magharibi. Alitembea kwenye gari kwa takribani masaa matatu kabla ya kuja kukomea kwenye nyumba kubwa namba 4089 kibaoni. Nyumba ya mwanamke yule aliyemwona mtandaoni kwa swala la mtoto wake kuwa na chapa mwilini.
Kabla hajashuka na kuzama humo, akalipekua kwanza jengo hilo kwa macho yake mepesi, kisha akashuka na kuliendea. Alipogonga kidogo akafunguliwa na mlinzi, akajitambulisha na mlinzi akamruhusu kuingia ndani maana alikuwa na miadi na mwenye nyumba.
“Nilipata shida sana. Nilitafuta kila namna lakini haikusaidia. Na nakumbuka vema ikiwa ni usiku wa manane, nikampoteza mwanangu wa pekee!”
Darren akataka kujua zaidi kumhusu mwanamke huyo. Mbali na mtoto je yeye alishawahi kukumbwa na kadhia yoyote ile? Basi mwanamke yule akaeleza kuwa kwa kitambo kifupi baada ya mama na baba yake kufariki, ndipo alipoanza kuona mambo fulani ya ajabu ndani ya mji wao. Mwanzoni alikuwa anadhani anawehuka na labda ana laana na ule mji, hivyo akafanya kuhama aende mbali.
Alipoenda huko, akatuama na kuanzisha familia ambayo iliishi kwa amani mpaka pale mambo yalipokuja kuibukia katika namna ambayo hakuwa anaweza kuelewa vema.
“Ninachokumbuka ni kwamba, baada ya tetemeko kubwa la ardhi lilitokea miaka mitano nyuma, maisha yangu yakaanza kubadilika kwa wepesi sana. Sikuwa tena mtu wa amani bali kuona vituko na viroja. Mtu wa kuona mambo ya ajabu yasiyokuwa na mithili. Ajabu ni kwamba, baada ya mtoto wangu kufariki, mambo hayo yalipotea mpaka sasa.”
“Na vipi kuhusu mume wako?” Darren akadadisi. Charlie akatabasamu kwanza ila macho yake yakiwa kinyume. Alitazama chini kwa sekunde chache kabla hajabinua kinywa chake na kusema, “Alikuwa mwanaume niliyekuwa namhitaji. Mwenye kujali na kujua kupenda. Nilijihisi nimekamilika nilipokuwa naye. Alinifanya nisahau kifo cha wazazi wangu kwa muda kwani alikalia sehemu tupu ambayo iliachwa wazi.”
Akadondosha chozi. Akalifuta kwa kidole chake onyeshi kabla hajaendelea kuongea, “nilimpoteza kwenye ajali!” akapandisha mabega yake akisema, “sijui nini kilitokea lakini aliacga daraja na kutumbukia baharini. Waokozi walipokuja kumtazama, hakuwa hai tena.”
“Gari lake lilipata hitilafu?” Darren akauliza.
“Sidhani,” Charlie akajibu. “Gari lake lilikuwa sawa kabisa isipokuwa tu sehemu ambayo iligonga daraja. Sijajua kumhusu yeye. Sijajua alikuwa kwenye hali gani. Ila kwa mujibu wa shuhuda wa tukio, mume wangu alibamiza kioo chake cha pembeni kwanguvu kabla gari halijapoteza mwelekeo na kudumbukia.”
Kwa namna moja Darren akaona simulizi ya huyo mwanamke inawiana na ya kwake. Kwa kutaka kuhakikisha zaidi, akamuuliza Charlie, “Kuna mtu yeyote ambaye ulikuwa naye kwenye mahusiano kabla ya mumeo? Namaanisha mpenzi wako wa kwanza?”
Charlie akafikiri kidogo kabla hajasema, “Niliwahi kuwa naye. Ila ni kipindi cha zamani za utotoni. Sichukulii mahusiano yale kama yalikuwa serious.”
“Je haujawahi kumwona mwanaume huyo uliyewahi kuwa naye kwenye mahusiano? Yaani baada ya kuoana na mumeo? Au kipindi chochote kwa namna yoyote?”
“Hapana,” Charlie akakataa. “Sijawahi kuonana naye tangu kipindi hicho.”
Hapa kidogo Darren akajiona ni wa tofauti na Charlie. Mbona yeye anasumbuliwa na Melissa? Basi akaamua naye kumshirikisha Charlie kuhusu habari zake. Alipomaliza kumweleza kila kitu, Charlie akamuuliza Darren, “Unapajua anapokaa huyo Melissa?”
“Ndio, napajua,” Charlie akajibu.
“Naweza nikaonana naye?” Charlie akauliza akiwa ametoa macho kidogo.
“Unahitaji kuonana naye?”
“Ndio, kama itawezekana.”
Darren akanyamaza kidogo kisha akasema, “Si mtu mzuri kama unavyoweza kudhani.”
“Najua,” Charlie akamkatiza. “Sitegemei awe mtu mzuri, ila ningependa kuonana naye.”
“Kwanini? Huoni utakuwa umejiweka kwenye hatari?”
“Hatari ipi, Darren? Nimepoteza mume na mtoto wangu, kuna hatari nyingine zaidi ya hiyo?”
Kimya kidogo. Charlie akaendelea kuzungumza, “Nadhani kuna maswali yangu atakuwa na majibu nayo.”
“Yapi hayo?”
Hapa Charlie akamweleza Darren kuwa anahisi mama yake alikuwa ni mtu mwenye agano tokea nyuma. Mara kwa mara mama yake alikuwa anamwambia kuwa maisha yake hayatakuwa ya furaha kwakuwa yeye ni kizazi cha shetani. Damu yake inachembechembe za majini. Alipotaka kujua zaidi, mama yake hakumweleza kwa kumwambia muda bado mpaka pale utakapowadia na basi atajua.
“Una picha ya mama yako?” Darren akauliza. Charlie akafungua simu yake na kumwonyesha Darren picha ya mama yake, “huyu hapa wa kwanza upande wa kulia.” darren alipotazama vema, akagundua sura ya mama huyo haikuwa ngeni. Ilikuwa ni sura anayoijua. Aliionea wapi? Akajiuliza akirusha macho huku na kule.
“Vipi, Darren?” Charlie akamuuliza.
“Nahisi namjua huyu mtu,” Darren akajibu akiendelea kufikiri na punde akakumbuka. Sura hiyo aliionea kwenye ile picha ambayo aliipata kwenye jengo la bibi yake! Akamweleza Charlie habari hiyo.
“Kweli?” Charlie akastaajabu.
“Ndio, ni kweli!” Darren akaapa. Basi Charlie akafikiria kwa udogo na kusema, “Darren, nadhani sasa utakuwa unaona kuna haja gani ya kuonana na Melissa. Yeye anaweza kutueleza mambo haya kwa undani.”
Darren akashika kichwa, “Lakini Melissa si mtu mzuri hata kidogo. Ameyfanya maisha yangu yawe magumu kupita kiasi. Sikutaka kabisa kuhusiana naye.”
Charlie akauweka mkono wake begani mwa Darren, “sikia, Darren. Hatuna machaguzi hapa. Na kati ya wewe na mimi, hakuna mwenye maelezo ya kumtosha mwenzake isipokuwa huyo Melissa. Hima twende tukamwone!”
Darren akafikiri kidogo kabla hajanyanyuka na kumpakia Charlie kwenye gari yake, safari ikaanza. Walitembea kwa muda wa kama nusu saa pasipo kuzungumza. Charlie ndiye alikuja kuuvunja ukimya kwa kumuuliza Darren, “Ulimpenda Melissa?”
Darren akanyamaza kwanza kama mtu anayepangilia jibu kichwani kisha akasema kwa ufupi, “Ndio.”
“Na yeye alikupenda?” Charlie akauliza akimtazama Darren anayatazama mbele.
“Sidhani,” Darren akajibu.
“Haudhani?”
“Ndio. Kama angekuwa ananipenda basi angeniweka bayana kila kitu,”
“Kila kitu kama kipi Darren? Kuwa yeye ni jini aliyeishi na bibi zetu tuokea huko nyuma? … ungemwelewa? Ungeendelea kuwa naye?”
“Charlie, sijui haya mambo yaendavyo. Ila nisingeweza kuishi na Melissa zaidi. Unawezaje kufanya hivyo punde unapohisi kuwa uliyenaye si binadamu?”
Charlie akanyamaza asinene tena. Wakaumaliza huo mjadala. Kwenye majira ya saa tano za usiku wakawa wamewasili kwenye makazi ya Robson. Hapo waliposhuka, Charlie akauliza, “Hapa ndipo kwake?”
“Hapana, bali kwa mpenzi wake! Nadhani atakuwapo hapa,” Darren akaji bu wakisonga.
“Na vipi kama hatokuwapo?” Charlie akauliza.
“Basi mpenzi wake atakuwa anajua alipo,” Darren akamalizia kauli na kubisha hodi mara tatu. Punde akafunguliwa na Robson ambaye alishangaa kumwona Darren hapo wakati huo.
“Vipi, Darren?”
“Naweza kuonana na Melissa?” Darren akaenda moja kwa moja kwenye lengo lililomleta.
“Vipi, kuna tatizo?” Robson akauliza.
“Ndio, lipo,” Darren akajibu na kisha akarudia tena kauli yake, “Naweza kuonana na Melissa?”
Robson akawafungulia mlango wakaingia ndani. Ila walipoketi, simu ya Darren ikaingiwa na ujumbe. Alipoutazama kuusoma, ulikuwa unatokea kwa Melissa.
“Sipo hapo. Nikuteni fukweni,” ujumbe ulisoma.
Upesi Darren na Charlie wakaelekea huko ufukweni ambapo Melissa alikuwapo, na kweli wakamkuta akiwa ameketi mchangani akitazama maji ya bahari. Mbali na hivyo kulikuwa kimya sana isipokuwa upepo.
Darren akamwita Melissa akiwa anamtazama, naye Melissa akamtazama na kumkaribisha, “Nadhani hapa ni eneo zuri la kufanyia maongezi.” Darren na Charlie wakaketi wakimweka Melissa katikati yao.
“Ulimwambia Robson kama nipo huku?” Melissa akauliza.
“Hapana, hajui hilo,” Darren akajibu kisha akamuuliza Melissa kama anamjua mwanamke yule aliyekuja naye, yaani Charlie. Pasi na kumtazama, Melissa akasema anamfahamu hata kabla hajaja hapo.
Aliposema hayo akamtazama Darren. Macho yake yalikuwa tayari yameelekea kuwa mekundu. Akamshika mkono na kumuuliza kwa upole, “Darren, utasadiki nitakayokuambia?”
Darren alipojibu swali hilo, Melissa akamuuliza na Charlie swali hilohilo. Alipolijbiwa ndipo akaanza kunena. Darren na Charlie wakawa wametega masikio yao vema kabisa. Japokuwa upepo ulikuwa unapuliza, bado sauti ya Melissa ilisikika vema.
“Pengine mimi naweza nikawa mtu mbaya sana kwenye vichwa vyenu. Hamtaki kuniona na sifai kuwa hai wala kuwa mbele yenu hapa nilipo. Ila …” alipokomea hapo akamtazama Darren, “Kama si upendo wangu kwako, Darren. Basi usingalikuwa hai mpaka sasa. Haujui ni makovu mangapi umenisababishia kwa maneno yako lakini sikuwahi kuacha kukupenda.”
Aliweka kituo na kutazama bahari kwa sekunde kama sita akiwa kimya. Kuna kitu alikuwa anawaza kichwani mwake. Na basi alipojiona yu tayari ndipo akaendelea kunena ya kuwa hapo zamani kabisa ya miaka takribani mia tatu iliyopita, walikuwa kwenye familia kubwa ya bwana Roddeth. Bwana huyo alikuwa ni mtu mwenye nguvu kubwa na mwenye kuhofiwa sana.
Alikuwa na nguvu za ajabu. Watu wangekusanyika kwake awasaidie matatizo mbalimbali lakini kwa sharti la kutoa sadaka. Alikuwa si mtu wa kawaida bali jini, lakini alistahimili kuishi miongoni mwa binadamu. Na kwa uzao wake basi akapata watoto watano wa kike ambao kwa mujibu wa maelezo ya Melissa, mmoja wa hao watoto alikuwa ni yeye, na wengine ni pamoja na bibi yake Darren na Charlie na wengineo wawili.
Walikuwa ni watu wapendanao mpaka pale siku moja baba yao alipokufa na kugawa mali zao pasi na usawa. Walichukiana na kila mmoja akaelekea upande wake. Lakini kwasababu Melissa alikuwa ni kipenzi kikubwa wa baba yao basi ingali baba yupo kwenye kitanda chake cha kifo alimkabidhi mwanaye huyo kito cha moja ya mkufu wake akimwambia, “Utaishi milele, mimi safari yangu naona ikomee hapa.”
Alificha kito hicho kwa namna zote ili ndugu zake wasije kukiona na kumpokonya. Na kwake haikuwa ngumu sana kwani walikuwa tayari wameshatengana na kila mmoja akaenda njia yake binafsi.
Basi miaka ikapita kila mmoja akiwa na chuki na mwenzake na uadui pia. Kila mmoja akapata kuishi kwa namna ajuavyo huko mbali. Wengine wakafikia kuanzisha maisha kwa kuwa na mahusiano na binadamu.
“Halikuwa jambo jema. Baba yetu wakati yu hai alikuwa akitusisitiza juu ya hilo. Endapo tutakapokuwa kwenye mahusiano na binadamu basi si kwamba tutawafanya watoto waingie kwenye damu yetu isiyo ya kawaida, bali damu hiyo itawawinda na kuwaangusha,” alisema Melissa.
Lakini kwasababu za mapenzi, wenzao wawili walizaa na binadamu. Na kama ilivyokuwa neno la baba yao, watoto hao wakawa wanasumbuliwa kwa kutokewa na mambo ya ajabu wasiyoweza kuyaeleza. Mengine hata yakitishia uhai wao.
Kutokana na hayo ndipo binadamu hao wakawa wanatafuta tiba ya kujikinga dhidi ya maajabu waliyokumbana nayo. Na kila tiba walipoipata wakaifungia kwenye vitabu walivyovihifadhi maeneo ya mbali kabisa na makazi yao. Maeneo salama ambayo hayafikiwi na binadamu.
Vitabu hivyo vilikuwa ni vifungo vya kufunga yale yote yaliyokuwa yanawasumbua, na wakafanikiwa kufanya vivyo kwa muda.
“Shida ni kwamba, vitabu hivyo vinakuwa si vifungo tu bali hubeba roho za wale vinavyowalinda. Hivyo pale vinapopata madhara, basi na wale waliokuwa wanavimiliki hufa kwa aina hiyohiyo ya kifo,” maneno hayo ya Melissa ndiyo yakamkumbusha Darren kifo cha mama yake kilivyorandana na moto wa msitu. Akamuuliza naye Charlie akasema kuwa mama yake alikufa kwa kuzama maji ingali alikuwa chumbani mwake! Ikiwa ni muda mfupi baada ya tetemeko la ardhi kutokea.
“Baada ya hapo basi ndipo matatizo yenu yakaanza upya,” Melissa akaendelea soga, “Kwakuwa vifungo vilikuwa vimeenda basi ndiyo maana mambo ya ajabu yakaanza kuwatokea upya kwenye familia zenu, na itakuwa vivyo mpaka pale damu mliyobeba itakapotulizwa.”
Darren akamuuliza Melissa, “Mbona maisha yangu yalikuwa yametulia kabla ya kuja kukutana na wewe? Mbona kila mara ninapoonana na wewe huwa nakutana na jambo baya?”
Melissa akamtazama Darren akiwa anadondosha chozi, “Darren kamwe hautokuja kuelewa ni mangapi nilikuwa nayapitia kwasababu yako. Maisha yako kutuama kabla ya kuja kukutana na mimi haikuwa inamaanisha kuwa utakuwa sawa, lah! Na hilo halikuwa kwako peke yako bali pia kwa Charlie.
Mambo yalianza kubadilika si kwasababu ulikutana na mimi bali kwasababu ulikuwa umepata mtoto. Kama vilevile ilivyokuwa kwa Charlie. Mlikuwa mmefufua upya agano lenu, Darren,” Melissa alisema kwa sauti ya chini alafu akatazama chini kabla hajaendelea kunena, “Kila ulipokuwa unakutana na baya lolote, nami nilikuwapo pembeni, na ndiyo maana ulikuwa unatoka ama kushinda hai. Isingalikuwa hivyo, ungeshakufa muda mrefu Darren.”
“Na vipi kuhusu ile siku nilipoenda kwenye ile nyumba iliyotangazwa kwenye gazeti? Ilikuwa ni kweli ama ndoto kukuona pembeni ya gari yangu?” Darren akauliza. Melissa, bado akiwa anamtazama mwanaume huyo, akamjibu, “Yote yalikuwa ni uhalisia, Darren. Na ni mimi ndiye nilikurudisha pale kwenye gari lako upesi baada ya kuzidiwa na wale wadhalimu. Lakini uliponiona pembeni yako haukunipa muda nikajitetea, bali ukanijaza shutma na kunifukuza!”
“Kwanini hukuniambia yote hayo, Melissa?” Darren akauliza.
“Kwasababu haukunipa muda huo Darren. Maisha yako yote umekuwa ukinichukulia kama adui yako. Mtu ninayekusababishia mabaya na nuksi,” Melissa akieleza hayo machozi yakamtiririka zaidi. Na Charlie akagundua kuwa mwanamke huyo alikuwa akimomonyoka miguu yake kuwa udongo.
Akamshtua Darren atazame. Darren akapayuka kuuliza, “Melissa, nini kinatokea?” akiwa amemshika mkono mwanamke huyo. Melissa akatazama miguu yake inayomomonyoka na kisha akamtazama Darren na kusema, “Hii ndiyo gharama yangu kwa kusema haya. Yanipasa niende Darren. Maisha yangu yamekwisha hapa duniani.”
“Hapana Melissa, si una kito cha kuishi milele?” Darren akauliza.
“Sina kitu chochote Darren,” Melissa akasema akilaza kichwa chake kifuani mwa Darren, “Yote nimeyatoa kwa ndugu zangu kama sadaka ya kukubakiza wewe hai.” kisha akamtazama Darren na kumwambia, “lakini haikusaidia na wamenigeuka. Wanataka maisha yako, wanataka maisha yenu. Wanataka kila ambacho bibi yako alikuwa anamiliki. Siwezi kuwazuia tena, Darren. Sina nguvu hiyo.”
Melissa alipomaliza kauli hiyo, mwili wake ukawa umeshapukutika mpaka kufikia tumboni. Mwili uwake ulikuwa kichuguu cha mchanga. Akamwaga Darren, “Kwaheri, mpenzi”
“Melissa!” Darren akaita akimshika Melissa vema. “Usiondoke, Melissa! Tutawezaje kupambana wenyewe? Tafadhali usituache!” Lakini tayari sasa mwili wa Melissa ulikuwa umepukutika zaidi mpaka kifuani. Maneno pekee ambayo aliyasema kabla hajamalizika kabisa ni haya,
“Kuna kitu kwenye jeneza la bibi yako,” alipotaka kunena zaidi, kichwa chake kikamomonyoka na hatimaye akawa mchanga kabisa. Darren na Charlie wasiamini macho yao wakautazama mchanga ule wa bahari.
“Amejitoa sadaka kwa ajili yetu,” akasema Charlie akimtazama Darren kisha akauliza, “sasa tunafanyaje?” Darren alipohakikisha kuwa kweli Melissa ameenda, akamwambia Charlie waende kule kwa bibi yake. Lakini muda ulikuwa umeenda sana.
“Vipi tukadamka asubuhi?” Charlie akapendekeza.
“Hapana,” Darren akatikisa kichwa. “Huoni ni hatari zaidi tukiendelea kungoja?” kweli Charlie akaafiki, lakini sasa wangefanyaje na muda ulikuwa umewatupa mkono?
Wakiwa wanafikiri namna ya kufanya, simu ya Darren ikaita, alikuwa ni Isabel. Alipokea na kumjulia hali mwanamke huyo.
“Upo wapi, Darren?” Isabel akauliza. Darren akamtazama Charlie na kujibu, “Nipo mbali.”
“Wapi? Tafadhali waweza kuniambia?” Isabel akasisitiza, lakini kabla Darren hajajibu akamtazama kwanza Charlie, mwanamke huyo akamtikisia kichwa. Darren akakata simu.
“Darren, usimwamini mtu yeyote kwa sasa hivi,” Charlie akamwambia akiwa amemkazia macho.
“Kwanini? Huyu nafahamiana na–”
“Hapana!”
Punde simu ikaita tena, Darren akamtazama Charlie. Ajabu mwanamke huyo akampoka simu hiyo na kisha akaikata na kuizima. “Tuondoke, Darren!”
Basi upesi wakalifuata gari lao na kujikwea. Charlie akamwambia Darren waelekee kwake alafu ndiyo waende huko waendako, Darren akatii. Walipofika kwa Charlie wakapakia silaha kadhaa ndani ya gari, Charlie akabeba na pesa, wakaanza safari ya kwenda kwenye nyumba ya marehemu bibi yake Darren.
Wakatembea kwa muda mrefu sana mpaka pale ambapo usiku sasa ukawa mkubwa. Wakiwa kwenye majira ya saa tano usiku, wamebakiza kama kilomita ishirini kuwasili wanapoelekea, Charlie akahisi kuna gari linawafuatilia. Alimshtua Darren na kumtaka aongeze mwendokasi.
Darren alipojaribu kutazama kwa kutumia vioo akaliona gari hilo wanalolishukia. Halikuwa ngeni machoni mwake. Alipoenda mbele zaidi na kulitazama vema, akagundua kitu,
“Isabel!” alijikuta akinena mwenyewe.
“Unamaanisha yule mwanamke?” Charlie akauliza. “Yule aliyekuwa anakupigia simu?”
“Ndio!” Darren akajibu. “Ndiye yeye!”
Charlie akatazama nyuma kuliangazia gari hilo. Lilikuwa linakuja kwa kasi. Alihofia sana.
“Darren, sasa tunafanya nini?”
“Sijui!” Darren akatikisa kichwa akiwa ametoa macho kukodolea kioo cha juu ya kichwa chake. Alikanyaga pedeli ya mafuta zaidi, gari likakimbia. Punde lile gari linalowafuata likatokomea wasijue limeenda wapi!
“Unaliona?” Darren akamuuliza Charlie.
“Hapana, silioni!” Charlie akajibu akiwa anaendelea kukagua. Kwa muda kidogo akaendelea kutazama asilione tena gari lile linalowafukuza, basi wakaendelea na safari yao mpaka waelekeapo. Walipofika wakajitua toka kwenye gari na kabla hawajaenda mbali sana, wakatupa macho yao kukagua.
Ilikuwa ni nyumba iliyomezwa na kiza. Kulikuwa kimya sana. Kwa namna moja ama nyingine kulikuwa kunatisha.
Wakiwa wanaendelea kutazama, Charlie akagundua kitu. Akamwita Darren na kumuuliza, “Nini kile? Ni gari ama macho yangu?” Darren alipotazama akaona gari kwa mbali upande wao wa kulia. Gari hilo lilikuwa limeegeshwa kwa ukimya. Lilikuwa ni lile gari waliloliacha barabarani. Gari ambalo Darren hudhania ni la Isabel.
“Umeliona likiingia muda huu?” Darren akauliza.
“Hapana,” Charlie akajibu na kuongezea, “Nimeliona likiwa tayari limeegeshwa.” kisha akauliza, “atakuwa amefika kabla yetu?”
Darren hakuwa na majibu, upesi akamwamuru Charlie wachukue kila kinachohitajika kwenye gari na waelekee eneo la kaburi upesi. Walipofanya hivyo, mara gari lile likawasha taa zote kwa pamoja, pap! likawamulika na kuwaumiza macho!
Upesi wakakimbia kule kaburini na kuanza kuchimba kwa maelezo ya Darren. Wakiwa wanaendelea kuchimba, Charlie akamwona mtu kwa mbali akija kwenye mwelekeo wao. Hakuweza kumwona vema maana alikuwa yu mbali, kitu pekee alichoweza kubaini ni kuwa mtu huyo ni mwanamke kutokana na umbo lake na mwendo pia.
Mikono yake iliyokuwa tupu ilikuwa ikienda mbele na kurudi nyuma sababu ya mwendo.
“Chimba, Charlie! Chimba!” Darren akabweka. Wakafukua kana kwamba sungura udongoni na mtu yule alipokaribia, Darren akamsihi Charlie aendelee na zoezi ilhali yeye akamkabili mtu huyo anayekuja.
“Darren, una uhakika?” Charlie akauliza kwa mashaka.
“Usijali, endelea,” Darren akasema akitoka shimoni na kupiga hatua kadhaa kusonga mbele. Alipomfikia mtu yule ndipo akabaini kweli alikuwa ni Isabel.
“Isabel,” Darren akaita na kuuliza, “Ni nini unataka hapa?”
Isabel akatabasamu na kuuliza, “Darren mbona haupokei simu yangu?” kabla Darren hajajibu, akauliza tena, “Kwani kuna tatizo lolote baina yetu?”
Darren akamtazama kwanza Isabel kwa namna ya kumtilia mashaka. Alikuwa anahisi kuna kitu hakipo sawa.
“Isabel, unataka nini hapa?”
Isabel akatazama nyumba kubwa iliyokuwa kando yao, “Ni nyumba kubwa. Nimeipenda sana Darren. Vipi ile ofa yangu, waweza kuniuzia?”
“Siuzi tena!” Darren akajibu.
“Kwanini? Auhitaji pesa tena?”
“Sihitaji pesa zako, Isabel.”
Isabel akamtazama Darren na kumsogelea karibu zaidi.
“Tangu lini umeanza kukataa pesa zangu, Darren?”
“Kuanzia leo. Sihitaji tena. Na pia sihitaji kukuona pia!”
Isabel akakunja shingo yake kutazama kule shimoni. “Naona umepata mwanamke mpya.”
“Hayakuhusu, Isabel. Hicho ndicho kimekuleta?”
“Hapana, Darren,” Isabel akajibu akiweka mkono wake begani mwa Darren. “Kilichonileta hapa ni kuchukua kilicho changu tu.”
“Kipi chako hapa?” Darren akauliza.
“Vyote unavyoviona hapa,” Isabel akajibu na kuongezea, “Vyote ni urithi wangu. Na kwakuwa haukutaka niuchukue kwa amani, basi nitatumia nguvu!”
“Ebu tumia nione!” Darren akasema akimkazia Isabel macho.
“Una uhakika?” Isabel akauliza akipandisha nyusi yake moja. Punde Darren akaanza kuhisi maumivu makali ya kichwa.
“Darren nisingependa nitumie nguvu dhidi yako. Nitakumaliza. Kwahiyo kwa kunusuru maisha yako, songa kando nifanye kilichonileta.”
Japo Darren alikuwa anasikia maumivu makali bado hakuwa radhi kumruhusu Isabel atende kile alichokuwa amekusudia. Basi akamvamia akimtupia maneno makali lakini alichoambulia hakikuwa kinasimulika vema. Alitupiwa mbali tena kwa mkono mmoja tu. Akaangukia tumbo na kulalama kwa maumivu makali!
Isabel akapiga hatua nzito kumfuata Charlie. Alipomfikia akanyoosha mkono wake kumnyaka mwanamke huyo, ila upesi Charlie akatumia kifaa alichokuwa anachimbia kumwadhibia Isabel! Alimchana na kumvujisha damu!
Isabel akautazama mkono wake unaovuja damu kisha akakunja ndita akimtazama Charlie. “Umekwisha!” akafoka na kujitupia ndani ya shimo. Charlie alipotaka kumwadhibu tena Isabel, nyenzo yake ikadakwa na mkono wa Isabel wenye nguvu.
“Kamwe usijaribu!”
Isabel akampokonya Charlie dhana hiyo na kisha akataka kumbamiza nayo kichwa. Kheri kabla hajatimiza adhma yake hiyo, nyenzo ikadakwa na mtu nyuma. Isabel alipogeuka kutazama, alikuwa ni Darren. Na kabla hajafanya jambo, mwanaume huyo akamwadhibu kwa kumzamishia ncha za reki usoni mwake! Kilikuwa ni kitendo cha kinyama ambacho Darren amewahi kufanya tangu azaliwe.
Hata wakati Isabel anaanguka chini, Darreb alikuwa ameachana asiamini kama amelitenda hilo. Basi upesi, wakishirikiana, wakamtoa Isabel ndani ya shimo na Darren akamburuza kwa hatua kadhaa mbali na shimo kisha wakaendelea kuchimba kaburi.
Walipofanya hivyo kwa takribani dakika sita, mara Isabel akanyanyuka akiwa na reki lake usoni. Si Darren wala Charlie aliyemwona. Mwanamke huyo akachomoa reki usoni na kulitupia kando. Alikuwa anachuruza damu lakini hakuwa anajali. Upande wake wa kushoto ulikuwa umefunikwa na damu inayotiririka kama bomba.
Alipotupia reki kando ndipo Darren na Charlie wakasikia na kuhisi. Darren alipotazama na kubaini hilo akahofia sana. Hata Charlie vilevile. Ni mtu wa aina gani angenyanyuka baada ya kadhia ile? Lakini kwa ujasiri Darren akatoka ndani ya shimo baada ya kumwambia Charlie aendelee kufukua.
“Darren!” Charlie akaita kwa hofu. Aliogopa. Aliona Darren angeenda kufa. Lakini Darren asijali akajiendea kifua mbele. Alipomfikia Isabel akasema, “Nitakuua!” naye Isabel akamwambia, “Karibu tena!” kisha akamnyaka shingo yake kwa nguvu na kumnyanyua juu juu!
“Ndiyo kwanza tupo kwenye moja, Darren. Unadhani binadamu kama wewe anaweza kuniua?” Darren akarusharusha miguu akijitahisi kujinasua toka kwenye mikono ya Isabel. Hakika asingeweza kwani mikono ya mwanamke huyo ilikuwa imeshiba nguvu haswa. Ilikuwa inaminya uhai toka kwenye mwili wa Darren.
Darren akapapatika sana pasipo mafanikio. Akarusha na mateke ambayo mengine yalikwenda hewa na mengine kumkita Isabel lakini haikusaidia, mwanamke huyo alikuwa mithili ya gogo kavu!
Basi Darren aliyekuwa anaelekea kufa alipoona amefanya kila jambo pasipo mafanikio na sasa anaelekea kufa, akamtazama Isabela akilenga kumtusi ama kumlaani. Ni kheri katika hilo akabaini jeraha alilokuwa nalo Isabel mkononi, lile jeraha ambalo Charlie alimsababishia. Basi kama simba aliye na njaa, Darren akadaka kwa mikono yote jeraha hilo na kuliparua sana. Isabel akashindwa kuvumilia na hatimaye akamwachia Darren aliyejidondokea chini akikohoa.
Darren alikuwa anahisi kifua kinambana, shingo nayo imeziba. Alikuwa anahema kwa tabu. Koo lake bado halikuachia. Alikohoa mara kadhaa akiwa anahangaika kumeza mate.
Hakukaa sana akamwona Isabel akimfuata kwa hasira. Alipotaka kuamka akimbie, Isabel akamwendea kwa kasi sana na kumdaka. Darren akajitahidi kurusha ngumi na kutumia nguvu zake za kibinadamu lakini akashindwa kabisa! Isabel alikuwa ana nguvu mno!
Mwanamke huyo pasipo kujiuliza mara mbilimbili, akadidimizia kucha za mkono wake wa kushoto kwenye tumbo la Darren, na hakufanya vivyo mara moja bali mara tatu! Darren akalalamika sana kwa maumivu. Isabel akamtupia mbali akiwa amemalizana naye.
Darren, akiwa amelala kama mtu anayengoja kifo akiwa ameshika tumbo lake linalovuja, akamtazama Isabel. Akamwona mwanamke huyo akiwa anaenda kumfuata Charlie kule shimoni. Basi akapaza sauti kuu kumwita Isabel. Halikuwa zoezi rahisi, alikuwa anahisi maumivu makali sana lakini alifanikisha adhma yake hiyo.
Isabel alipogeuka kumtazama, Darren akapaza sauti kumtusi na kumkebehi mwanamke huyo. Kitendo hicho kikamkasirisha sana Isabel, akaamua kuachana na Charlie akammalize mwanaume huyo kabisa. Basi akamjongea kwa madaha akiwa anamwambia ni kwa namna gani atakapofurahi akiona roho yake inaenda.
“Kama bibi na mama yako, nawe utaenda hukohuko!” akasema Isabel. “Mwana usiwe na haya ukatembea na bibi yako. Hujui Melissa ni sawa na bibi yako, ati Darren?”
“Na mbona na wewe ulikuwa unanitaka?” Darren akaguguma kuuliza. Saa hii kinywa chake kilikuwa kinachuruza damu pia. Isabel akacheka akiwa anazidi kujongea, “Mimi? Darren mpenzi nilikuwa nataka tu kukumaliza na si kingine. Unadhani mimi ni kama yule mpofu Melissa? Mjinga kama yule?”
“Ni wewe ndiye mjinga, si Melissa!” Darren akafoka.
“Pole sana, Daren,” Isabel akasema akiwa anamalizia hatua yake moja kumfikia Darren. “Mpumbavu wako ameenda, nani atakulinda sasa?” akauliza na kucheka. “Kwa akili yake amejitoa uhai kwa ajili yako. Wewe binadamu. Kwa sababu tu ya kukwambia yote yale ambayo hupaswi kuyajua. Shenzi kabisa!”
Alipomaliza kusema hayo akamnyakua Darren na kisha anyanyue mkono wake ili apate kumkita tena tumboni kama alivyofanya hapo awali. Lakini mara hii kabla hajafanya vivyo, akastaajabu kuona mpini wa reki ukitokezea tumboni mwake! Hamaki alikuwa ni Charlie nyuma yake!
Basi akamwacha Darren na kisha akapiga magoti akiwa anatazama chuma kile kilichomtoboa tokea mgongoni mpaka tumboni na kisha akadondoka puh! Na kutulia tuli,
Charlie akamjulia hali Darren.
“Niko sawa,” Darren akamjibu na kisha akamuuliza, “Umefanikiwa?”
“Bado kidogo!” Charlie akajibu. Akatazama tumboni mwa Darren, kulikuwa kunamwaga damu sana. Akashikwa na imani, “Darren, nikuwahishe hospitali!” alisema akitaka kunyanyuka akaendee gari lakini Darren akamdaka mkono na kumwambia, “Hapana, Charlie. Nenda kamalizie kwanza ile kazi!”
“Darren, nitaendeleaje na upo kwenye hali hii?” Charlie akauliza.
“Hapana! Hapana! Nenda kwanza, tafadhali nenda!” Darren alisisitiza na basi kwa shingo upande, Charlie akaenda zake. Akazama shimoni na kufukua zaidi na zaidi, ndani ya dakika tano akawa amefikia jeneza, akafunua na humo ndani akakuta maiti ya bibi yake Darren ikiwa mifupa.
Alipotazama vema akabaini kulikuwa na kito rangi ya asamawati, basi akakibeba na kupaza sauti, “Darren, nimekipataaaa!”
Haraka akatoka ndani ya shimo na kumkimbilia Darren. Lakini alipofika akabaini Darren hakuwa anasogea wala kuashiria kama mzima. Alipotazama vema akabaini pia mwili wa Isabel ulikuwa umesogea kidogo toka pale alipouacha, na kama haitoshi, reki halikuwa tumboni, bali kwenye kichwa likiwa limemtoboa!
Hapo Charlie akabaini ya kuwa Darren na Isabel walipambana kwa mara nyingine. Akapata hofu zaidi juu ya uhai wa Darren. Akamwita sana na kumtikisa, kwa mbali Darren akafungua macho yake kumtazama. Alikuwa ana mjeraha kooni na kifuani. Karibia mwili wake wote ulijawa damu.
“Umepata?” Darren akauliza kwa kunong’ona.
“Ndio, nimepata!” Charlie akajibu kwa kitete. Macho yake yalikuwa mekundu yakitaka kumwaga machozi. “Twende nyumbani, sasa!” akasema akijaribu kumnyanyua Darren.
“Hapana, Charlie,” Charlie akasema na kuongezea, “Hapa ndiyo nyumbani kwangu, sina pengine. We nenda mimi utaniacha hapa.”
“Nitakuachaje Darren? Tumekuja wote hapa! Nyanyuka tafadhali twende!”
Charlie alipoona ni ngumu kumnyanyua Darren basi akaenda zake asogeze gari karibu. Alipojipaki kwenye gari, akaendesha upesi sana kumrudia Darren. Alipoliweka gari tenge akashuka na kumwendea Darren, ila kwa muda huo hakuwa Darren tena bali mwili tu.
Akapambana kumweka kwenye gari, lakini kabla hajawasha gari Isabel akanyanyuka na reki lake kichwani! Mwanamke huyo akakaa mbele ya gari akimtazama Charlie kwa macho ya kukodoa.
Charlie akastajabu sana. Akahangaika kuwasha gari, kabla hajafanikiwa, Isabel akawa tayari amezama ndani na kumkaba shingo kwanguvu! Charlie akaweweseka sana kujiokoa.
Ajabu wakiwa kwenye zoezi hilo, wakasikia mtu akigonga kwenye kioo cha dirisha. Isabel alipotazama, akabaini ni Melissa! Akastaajabu akiwa ameachama mdomo!
“Ina — inawezekanaje?”
“Unadhani nilikuwa mjinga, sio?” Melissa akauliza.
Kufumba na kufumbua akafungua mlango wa gari na kumnyaka Isabel. Kwa mikono yake akamnyofoa mwanamke huyo koo na kisha akamtupia mbali kana kwamba kitenesi!
“Melissa!” Charlie akaita kwa kustaajabu. Akamkumbatia Melissa kwanguvu na kisha akamwambia kumhusu Darren. Walipomtazama wakabaini mwanaume huyo alikuwa amekwisha kufa.
Basi Melissa akachukua kile kito ambacho Charlie alikipata kwenye jeneza la bibi yake Darren kisha akakitazama na kusema, “Nilikuwa nayajua yaliyo mbele yangu hata kuhifadhi sehemu ya maisha yangu kwenye jeneza lile.” aliposema hayo, akamtazama Charlie na kumwambia, “Utakapokutana na Darren mwambie nampenda sana. Hatimaye amekuwa huru. Hatimaye mmekuwa huru.”
Aliposema hayo akaingiza kile kito kinywani mwa Darren na kisha kumfumba mdomo. Charlie akamuuliza, “vipi kuhusu yule Isabel, hatarejea tena?”
Melissa akamjibu hatorejea tena kwa roho zake zimekwisha. Ndani yake alikuwa na roho kadhaa na kadiri walivyokuwa wanamuua ndivyo walivyozimaliza mpaka kubakia moja aliyoimaliza yeye muda si mrefu.
“Umejuaje?” Charlie akamuuliza.
“Kwasababu isingekuwa rahisi kummaliza kama nilivyofanya,” Melissa akamjibu na kisha akamuaga. Moja kwa moja akaenda kwenye shimo la kaburi na kudmbukia humo. Punde, Darren akaamka. Alikuwa mzima wa afya kabisa asiye na jeraha.
Charlie alipomweleza kila lililotokea, upesi akakimbilia kwenye kaburi kumtazama Melissa. Akamkuta mwanamke huyo akiwa ana uhai amekwishakufa. Akamwita na kumwita pasipo mafanikio, Melissa alikuwa ameenda.
Melissa hakuwapo tena.
Basi wakamfukia kwenye kaburi hilo na kwenda zao.
MWISHO

