DESTURI YA KUTAFUTA WACHAWI, NA JINSI YA KUWAADHIBU
Hapo zamani mtu akifariki, akiwa mwanamume au mwanamke, wenye ndugu baada ya kumaliza kilio tu huenda sehemu mbali mbali kutafuta ni kisa gani kimemwua yule ndugu yao. Basi safari hiyo hufungwa kwa kuambatana kwa ndugu wote wa pande zote mbili: kwa baba, na kwa upande wa mama. Basi baada ya kumtambua kuwa fulani ndiye mchawi (maana hutafuta kwa kila mganga mpaka wamehakikisha mara tatu au zaidi, wakisikia kuwa ni yeye yule tu anayetajwa ndipo wanapoamini).
Hapo wanarudi majumbani kwao na kufanya mashauri ya kuthibitisha mbele za wote. Yakisha hudhihirishwa kwa Mtemi wa nchi ile kwa kweli wakiisha kupeleka habari zile kwa Mtemi naye wanampelekea ng’ombe mmoja jike. Ng’ombe huyo anaitwa: “IKUTU LYA MUTEMI” yaani sikio la Mtemi asikie yanayotokea nchini mwake. Yakisha hayo huitwa wazee wengi wa kutosha. Wanafika kwa yule mchawi (anayedhaniwa). Wakimkuta, kwanza watawatoa watu wote ndani ya nyumba yao na halafu atapigwa kidogo kwa mjeledi mdogo hivi, anaambiwa: “Wewe FULANI BIN FULANI umemwua ndugu yetu FULANI, kwa kisa fulani”.
Pale pale inakuwa kama vita kwa ghadhabu ya wote wa pande zote mbili, lakini wazee ndio wanaamua kwa wale waliotumwa na Mtemi wa nchi ile. Lakini yule aliyeambiwa mchawi haondoki mpaka atakapopimwa kama kweli mchawi au si mchawi, kama si mchawi ataachiliwa. Hivyo huletwa Mganga kumpima. Watapika chungu, huweka maji ndani yake na ndani huwekwa jiwe moja dogo, na maji ya chungu huchemka.
Basi yule anayedhaniwa kuwa ni mchawi hulazimishwa kutia mkono wake ndani ya chungu kile ili ihakikishwe kama ameua kweli, au hapana. Wenye ndugu wa marehemu hunuizia kwa sauti kuu wakisema: “KOBO, KOBO, KOBO” maana yake: “Chubuka, chubuka, chubuka, wewe ndiwe uliyemloga ndugu yetu bila sababu, sasa chubuka.” Na ndugu za yule anayedhaniwa ni mchawi nao hunuizia kwa sauti kuu vile vile wakisema: “SWE, SWE, SWEE, Ku Nghuku nzeru”, maana, “Kweupe, kweupe, kweupe, kama kuku mweupe.” Basi mchawi hutia mkono wake ndani ya chungu.
Kwa kweli ilikuwa kama ni ajabu, kama yeye aliua akisogeza mkono tu tayari maji yanamsonga mkono mpaka kwapani na kumchubua chubua (wanavyohadithia wao); na kama kweli hakuloga ingawa atatia mkono mpaka ndani ya chungu lakini hawezi kuchubuka hata kidogo (wanavyohadithia). Basi hapo aliyepona anaachiliwa kwenda zake.
Lakini aliyeungua lazima auawe siku ile ile, au ya pili yake kwa kupigwa na mchi kichwani, au kupigiliwa msumari (isemwavyo: mambo) ya mti toka kichwani mpaka chini na kumwacha pale pale, hazikwi, aliwe na ndege au fisi. Kiisha hayo ndugu za yule mchawi hulipa ng’ombe 36 kwa ndugu za marehemu na ng’ombe mmoja zaidi wa ‘Mulamu’ (Kupeana mkono).