𝗠𝗔𝗟𝗜𝗣𝗢 𝗞𝗜𝗧𝗔𝗡𝗗𝗔𝗡𝗜
ONYO: Wakubwa tu, kuanzia Miaka 18, ndio wasome hii Hadithi
EP 04
“Vipi?” Dullah alisema baada ya kumuona Elisha akitokwa na jasho mara tu baada ya kusoma ile barua, aliipokea halafu akaketi kitandani naye akaanza kusoma, huku wenzake pia wakikaa kando yake na kuichungulia. Barua ilikuwa inasema hivi
“Ninajua nitawakera ndugu zangu, wazazi pamoja na marafiki zangu ambao walikuwa pamoja na mimi katika maisha na katika kusapotiana kwenye lile na hili, lakini naamini hata nisipokufa leo basi ipo siku nitakuja kufa tu baadaye
Niwaambie tu marafiki zangu, kwa maumivu ninayosikia kiukweli sitoweza kuendelea kuwa hai, sitoweza kuendelea kuwaona watu wakifurahi wakati mimi ninahuzunika katika moyo wangu
Nimepitia mengi mpaka kufika hapa, nimeumizwa na wanawake wengi lakini Aneth amekuwa mwanamke ambaye amenipa maumivu makali sana katika moyo wangu. Najua wengi walijiuliza kwanini niliamua kuondoka kwenye sherehe ya Aneth pamoja na kaka yangu Erick ambaye amekuwa kama mzazi wangu tangu nilipokuja jijini Dar es salaam
Kiukweli nilimpenda Aneth na nilianza kuwa naye katika mahusiano kabla hata ya Erick, kwani mimi ndiye niliyemleta mjini na hata kunisaliti kwa sababu alikutana na mwanaume ambaye ana pesa nyingi kuliko mimi
Mara kadhaa nimekuwa nikimuomba Aneth aachane na Erick ili nibaki naye mimi lakini kamwe hakuwahi kunisikia kwa sababu alikuwa amenizidi kielimu, kiumri na hata kiuchumi pia
Nakubali kwamba mimi ni dhaifu na hii acha iendelee kuwa historia, siwezi kuendelea kuishi na maumivu haya ninayoyapata katika mapenzi, nimehuzunika na nimejikuta namchukia sana mwanamke Aneth, ili kuishi kwa amani lazima moja kati yangu au Aneth afariki, nimechagua nife mimi
Haya yoten nitayafanya kwa sababu ya mapenzi, naandika barua hii kwa uchungu, machozi yakinitoka kwani ni muda mfupi tu umepita tangu Aneth aliponiahidi kwamba mimi ndiye nitamuoa lakini kamwe hakufanya hivyo
Nimejisikia sana uchungu kushuhudia harusi ya mwanamke ambaye nilimpenda sana sana sana na nilikuwa ndoto naye
Ni uchaguzi tu, nimeamua kufa kuliko kuendelea kuishi na maumivu, nimeumia sana
Kwa herini washikaji zangu nimekuwa na nyie pamoja, naombeni muendelee kumtunza mama yangu maana alinitegemea mimi
GOOD BYE”
Hii ilikuwa ni barua iliyokuwa imejaa maumivu makali, iliyoumiza moyo wa marafiki wa marehemu Amidu na kujikuta wote wanalia, na kushindwa kufanya kile kilichokuwa kimewapeleka pale ndani.
Kila nafsi kati ya zile ziligeuzia kisasi kwa Aneth na kujikuta wanamchukia kabisa na hata kutamani naye afe kabisa.
Hakukuwa na namna, Dullah, Elisha na marafiki wengine waliondoka jijini Dar es Salaam saa sita mchana na hawakutaka kumsubiri Aneth na Erick ili nao waje kuzika kwani waligundua kuwa hao ndio maadui wakubwa waliopelekea kijana mwenzao kufariki mapema akiwa na umri mdogo wa miaka 24 tu.
Marehemu alifikishwa salama na kuzikwa siku ile ile. Kikao cha marafiki kikawekwa chini, kila mmoja akitamani Aneth alipe kwa lile lililotokea
Vile vile kule Zanzibar, Aneth alikuwa akigombana na mume wake kwani ilikuwa ni siku nzima imepita, Erick anang’ang’ania simu ya mkewe na hataki kumpatia kwa sababu hakutaka binti ajue Amidu amefariki.
“Nipe simu yangu umeing’ang’ania ya nini??” binti alisema huku akimshika mumewe na kujaribu kumpora simu ambayo alikuwa ameishikilia kwa nguvu mkononi
Ghafla Aneth alianza kulia, na hii ilipelekea Erick kujisikia vibaya na kumpatia simu yake huku akimpa onyo kali “Tafadhali, mara baada ya kushika tu simu yako naomba usiendelee kulia tena” alisema Erick kisha akatoka nje ya pale ndani alipokuwa
Aneth aliwasha simu yake ambayo muda wote ilikuwa imezimika, halafu akawasha data, kitendo cha kuwasha data tu kilimpelekea kupata jumbe nyingi sana za kusikitisha sana.
Binti alizama WhatsApp kwenye group lake na marafiki wengine, alichokikuta hakuamini, jumbe zilikuwepo zaidi ya 2000 watu walikuwa wamechati sana, walikuwa wakiongelea kifo cha Amidu,
Alipita kwenye status, asilimia sabini zilihusiana na kifo cha Amidu
“Whaaat??? Amidu amejiua??” alijiuliza halafu akainuka na kutoka nje akamkuta mumewe amesimama kaweka mikono mfukoni halafu anaangalia mbali “Erick….ina maana ulikuwa unanificha? Kumbe Amidu amejiua??” alisema kwa hasira halafu ghafla akaanza kulia “Mungu wangu, kwanini lakini umeamua kufanya hivi
“Aneth” Erick aliita akiwa bado amekodolea mbali
“Kwanini umenificha??” alisema huku akizidi kulia “Kumbe ndo maana umenibania simu yangu tangu asubuhi, hukutaka niujue ukweli? Au wewe ndo umemuua??” aliuliza
“Nyamaza bwana khaa” alisema kwa hasira “Nilikuambia ukishaishika hiyo simu usiendelee kulia”
Aneth alimtazama kwa uchungu Erick, ni kwamba huyu mwanamke alikuwa anampenda sana Amidu lakini aliingia kimaslahi kwa Erick kwani Erick alikuwa na pesa nyingi sana, na aliamini kwamba atapata mafanikio makubwa kupitia yeye.
Aneth aliamini kwamba akishaoana na Erick basi wataendelea kuwa pamoja na Amidu lakini kumbe Amidu hakuwa na uwezo wa kuzuia maumivu kwani alikuwa ameshajitoa sadaka katika penzi la msichana huyo wa Kibosho.
Aneth aliumia sana, nguvu zilimuishia, aliingia ndani akaketi kitandani akalia, akaona haitoshi, aliketi chini kwa uchungu machozi yalimtiririka kama maji ya Mtoni, alilia sanaaa, hakujua afanye nini kuyamaliza maumivu
Alianza kujilaumu “Itakuwa mimi ndio nimesababisha wewe ukafa, naomba unisamehe…..aaaaagh sikujua kama nitakufanya hivi….maumivu ni makali sana kwangu. Naomba urudi Amiduuuuu aaaaan auwiiii auwiii” alilia kama mtoto kule chumbani
Erick alianza kuhisi kitu cha tofauti kwa mkewe, lakini hakuongea lolote kuhusiana na lile, alirudi tu ndani na kumuambia Aneth ajiandae kwani walitakiwa waondoke kwa ndege kesho yake asubuhi kwa ajili ya kuwahi mazishi
“Mazishi gani wakati mtu ameshazikwa?” aliuliza Aneth
“Ameshazikwa?”
“Ndio, we hujaona kilichopostiwa kwenye group la WhatsApp?” aliuliza kwa hasira binti
“Hata kama, lazima tuende Dar, sihitaji kuendelea kubaki hapa”
“Sawa”
Baada ya siku moja Aneth pamoja na mumewe, Erick waliingia jijini Dar es Salaam katika uwanja wa ndege wa Julius Kambarage Nyerere na walipofika walichukua taxi hadi nyumbani, nyumbani waliweka vitu kisha wakapanda gari yao na kuelekea mkoani Morogoro ili kuweza kuwasalimu wafiwa na kuwatia moyo
Walipofika walikuta bado marafiki zao wapo pale, cha kushangaza wote walikuwa wakiwatenga Aneth pamoja na Erick, wao hawakujua sababu ni nini lakini kiukweli, ile harusi ya Aneth na Erick ndo chanzo cha kifo cha Amidu.
Ghafla Dullah, Elisha na marafiki zao wengine walitoweka usiku sana kule mkoani Morogoro, hawakumuaga mtu yeyote, si Erick wala si Aneth. Walikuwa na magari yao na waliingia Dar es salaam usiku saa saba
Ilipofika asubuhi saa kumi na mbili kasoro, Aneth alipokea simu kutoka kwa mtu ambaye alikuwa amepanga fremu ya jirani na yake pale alipokuwa akifanyia biashara ya miamala huko Wazo, Tegeta
“Maggie” alimuita baada ya kupokea simu
“Vipi shoga uko wapi na hauna habari?”
“Habari gani?”
“Mlinzi ameuawa, na fremu yako imevunjwa”
“Imevunjwa? Lini?”
“usiku huu, ndo napigiwa simu sasa hivi”
“Weee”
“Ndio please njoo haraka”
Aneth alikata simu kwa uoga halafu akamtazama Erick, umesikia habari hiyo? Eti fremu imevunjwa”
“Imevunjwa?” Erick alishangaa”
“Ndio, please naomba turudi Dar es Salaam” alisema kwa uchungu “Kulikuwa na hela kule, na kuna vitu vya thamani twende mume wangu”
Kwa kuwa walikuwa wamelala hotelini usiku ule, basi walioga haraka na safari ikapamba moto kuelekea jijini Dar es Salaam haraka sana.
Ni kweli walipofika Wazo walikuta fremu imevunjwa na watu wasiojulikana halafu watu hao walikuwa na makusudi hawakuchukua pesa wala chochote ila walizichana chana vipande vdogo vidogo, wakachukua computer iliyokuwa ndani wakaipasua pasua na laptop kisha wakavunja vioo na droo zote wakaziacha nyang’anyang’a
Nia ilikuwa ni kumkomoa tu binti huyo pamoja na mumewe
“Sasa kwanini wamefanya hivi? Kwanini napitia majaribu mengi hivi?” alisema Aneth akiwa anakagua ndani ya fremu ile, ndipo akakumbana na barua ikiwa imebanwa kwenye compyuta iliyopasuliwa pasuliwa
Aliinyayua na kuifungua akaitazama, alipouona tu ule mwandiko alishtuka na kuificha kwenye sidiria haraka, ili akasome baadaye akiwa nyumbani kwake
Muda huo Erick alikuwa nje ya fremu anaongea na baba mwenye nyumba, maumivu yalikuwa makubwa, hakika alikuwa na balaa wiki ile
Wakati Erick akiwaza namna ya kutatua tatizo ambalo hakujua chanzo ni nini, kumbe Aneth yeye alikuwa anawaza kinyume chake, Aneth alikuwa akijisememea moyoni
‘Hakika hii ndoa ni ya maumivu kwangu, ni ya balaa najuta kuingia, tangu niingie kwenye ndoa napitia mambo mengi magumu, sina hata wiki mbili lakini nimepata hasara kubwa, simu imepasuka, nimepoteza mtu wangu wa kariabu, nimepoteza mlinzi, nimepoteza biashara na vifaa vya thamani, hakika huyu mwanaume sio wa type yangu, kwa kifupi hana nyotan amimi, najuta sana sana sana’
Baadaye waliondoka kuelekea nyumbani, na walipofika nyumbani, Aneth aliingia chooni akajifungia kama vile anajisaidia, ndipo akaitoa ile barua kwenye maziwa na kuamua kuisoma.
Ilikuwa ni ile barua ambayo Amidu aliiandika kabla ya kufariki, ilikuwa na maneno machungu na aliyeileta pale kwenye biashara ya binti wala hakujulikana ni nani, lakini mara ya mwisho ile barua alikuwa nayo Dullah wakati walipoenda chumbani kwa marehemu Amidu kuchukua vitu wapeleke Morogoro, Aneth hakulijua hili.
Aliisoma ikamuumiza sana, alijikuta naye anaketi katika chumba choo chini kabisa bila kujali kama ni kusafi au la, alikumbuka mbali, alikumbuka jinsi ambayo alishawahi kupitia mambo mengi, ahadi nyingi sana kipindi alipokuwa na Amidu
Kiukweli Amidu alikuwa ni mdogo kwa Aneth, kwani Aneth alimzidi miaka miwili na miezi kadhaa, lakini wakati Aneth anasoma chuo cha Dar es Salaam, Amidu alishawahi kumsaidia mambo mengi sana, maana binti yule hakuwa na mkopo, hakuwa na uwezo wa kujisomesha, lakini kwa biashara ambazo Amidu alishirikiana na Erick zilimfanya akapata uwezo wa kumsaidia mambo mengi sana akiwa chuo, licha ya kwamba hayakuwa mambo yote, na hata baada ya kumaliza chuo, Amidu alimtafutia Aneth kazi ya kufanya miamala ya Erick ambayo baadaye iligeuka kuwa ya kwake mara tu baada ya kumkubalia Erick penzi akampa ile biashara kama zawadi.
Hapo ndipo ulikuwa mwanzo wa mvurugano wa mapenzi ya Amidu na Aneth, na kamwe asingeweza kumuacha Erick maana Erick alikuwa na kila kigezo ambacho mwanamke mjanja anatamani kukipata, ubaya mmoja alioufanya Aneth ni kuendelea kumdanganya Amidu kwamba ipo siku ambayo ataoana naye, hii ilikuwa ni zaidi ya maumivu kwani alikuja kuolewa na mwanaume Erick kwa sababu ya masilahi tu
Haya yalifanya Aneth kupoteza fahamu kule chooni na hata Erick alipoona mkewe harudi ilibdi amgongee, bado mke hakushtuka mpaka Erick akachungulia kwa dirishani akakuta mkewe kazimia
Erick alirudi mbio akavunja mlango wa chooni na kumtoa binti ambaye alikuwa na barua mkono ameishikilia.
Erick aliichukua ile barua akaisoma, ndipo akagundua chanzo cha tatizo kimeanzia wapi
EP 05
Erick aliikunja barua akaiingiza mfukoni halafu alimchukua mkewe na kumpeleka sebuleni akamuwashia feni huku akipiga simu aweze kupata msaada kwa marafiki.
Kabla msaada haujaja binti alizinduka. Akatazama kwa macho makali kisha akamuita Erick ambaye alikuwa kando yake “Erick”
“Naam…umeamka?” aliuliza Erick
“Kwani ilikuwaje?” Binti alitaka kujua
“Ulipata tu mshtuko, nikupeleke hospitali?” aliuliza Erick
“Hapana, niko vizuri, kama nikijisikia vibaya basi nitakueleza”
Kuanzia siku ile Erick aligundua kitu ambacho hakuwahi kukijua kabla, alijua kumbe Amidu alikuwa na mapenzi mazito kwa Aneth, tena alijua kuwa amemuumiza sana kijana mpaka akaamua kujiua, alijilaumu lakini baadaye akajisemea moyoni kwamba dodogo Amidu ndiye mwenye makosa kwani hakuwahi kumuambia ukweli kwamba anatoka na binti, na hata alipoona process zote za kuoana, wala hakutaka kutoa mawazo yake.
Ilikuwa ni purukushani katika moyo wa Erick aliumia ila mwishowe alikubali kwamba hakuna ambacho ataweza kukibadilisha kwani ana ndoa na Aneth na vile vile mtu ameshakufa hivyo hatoweza kumfufua, halafu kingine marehemu hawezi tena kutoka na mkewe, acha ajilie vyake
Kwa hiyo kulingana na lile, ilipelekea Aneth kupoteza kibarua maana biashara yake ilivunjwa kwa visa vikali, urafiki kati yake na mashemeji, kina Dullah ulipungua maana walijua yeye ndiye chanzo cha kifo cha mwenzao.
Aneth aligeuka kuwa mama wa nyumbani kwani hakuwahi kuomba ajira popote licha ya kuwa na elimu kubwa ya shahada ya kwanza. Aliendelea kuwa mama wa nyumbani kwa zaidi ya miezi sita na alikuwa ana ujauzito wa miezi miwili tayari.
Siku moja binti akiwa mtandaoni, alikutana na tangazo la ajira katika kampuni moja iliyokuwa ikihusika na masuala ya bima za vyombo vya moto kama vile pikipiki, magari na bajaji, ndipo ikamuingia akilini kwani alihitajika meneja ambaye alikuwa angalau na elimu ya degree moja.
Hii ilimfanya kujaribu kuwasiliana na kampuni hiyo na hata akaambiwa aende kufanya mahojiano (interview) nao siku mbili baadaye.
Aneth aliongea na mumewe kumuomba amruhusu kwenda kwenye hayo mahojiano
“Upo katika hali hii ya ujauzito, kweli utaweza kwenda kufanya interview?” Erick alihoji
“Hamna shida, hata hivyo hii mimba wala hainisumbui sana, naomba niende mume wangu sipendi mimi kukaa tu nyumbani hivi”
“Sawa, nakuruhusu mke wangu”
“Asante mume wangu kipenzi” walikumbatiana wapendanao hao wawili.
Siku ya interview ilipofika Erick alimpatia pesa mkewe ikiwa ni ya nauli, na matumizi na ya ziada pia ejapo lolote likitokea
Aneth aliondoka zake akaenda kwenye kampuni hiyo maeneo ya Tanki Bovu, ndipo akakuta kuna watu wengi waliokuja kwa ajili ya kufanya interview na viongozi wa kampuni.
Mahojiano yalianza baina ya wale watu mpaka ilipofika zamu ya Aneth. Aneth aliingia ndani ya chumba cha mahojiano akiwa anatetemeka, moyo unamuenda mbio, hakujua anaenda kuulizwa maswali ya aina gani. Ila alishangaa kidogo. Taswira ya Amidu ilimjia machoni mara baada ya kumuona muhoji mmoja kati ya watatu waliokuwepo pale ndani akiwa amefanana sana na marehemu Amidu.
Aneth alishtuka na kubaki anamshangaa, yule kijana alifanana sana na Amidu, kuanzia umbo, rangi na hata macho yaliyokuwa kidogo ni makubwa
“Karibu” mmoja katiki ya mhoji aliyekuwa pale ndani “Wewe ni Janeth, Right??”
“Hapana ni Aneth”
“Oh sawa, ni Aneth, karibu ukae” alisema yule muhoji akinyoosha mkono kuonyesha kiti kilipo
Aneth alisogea na kuketi kwenye kiti, macho yote yako kwa yule mhoji aliyekuwa akifanana na marehemu Amidu
Waliongea kwa kiingereza lakini maneno yalikuwa yakimaanisha Kiswahili hiki hapa
“Karibu sana katika AB Insurance Company” alikuwa anaongea yule mhoji wa kwanza kabisa “Tutakuuliza maswali kadhaa ili kujua kama una vigezo vya kufanya kazi katika kampuni yetu hii ya bima….mimi ninaitwa Jonas Jonathan” alisema yule mhoji kisha akamshika yule mwingine anayefanana na Amidu akasema “huyu anaitwa Mr Haidali Mwasingo na huyo hapo mwisho ni Miss Biseko Irene”
Aneth alitikisa kichwa kukubaliana “Je uko tayari kwa mahojiano?”
“Ndiyo”
Wahoji waliuliza maswali yao mengi sana, lakini binti alionekana kuwa wa kiasi kuwajibu, kwa sababu hakusoma kwa muda mrefu kidogo. Aliondoka pale akaambiwa atapigiwa simu kama akihitajika, akaenda nyumbani
Huku nyuma baada ya interview, mhoji mmoja aitwaye Haidali alichukua namba ya Aneth kwa sababu mara nyingi alishuhudia Aneth akiwa anamshangaa sana pale kwenye interview kama vile alikuwa anamfahamu hivi. Hii ilifanya aamue kuchua namba labda angeweza kumuelezea kama alishawahi kumuona popote kabla.
Aneth akiwa amejilaza kwenye mkeka saa kumi na moja jioni, alipokea simu kutoka kwa Haidali lakini hakujua ni yeye maana ile namba ilikuwa ni mpya kabisa kwake.
EP 06
“Hallo” ilisikika sauti ya Haidali upande wa pili
“Hallo habari” alisema Aneth
“Salama kwema?” aliuliza Haidali
“Kwema” binti alijibu halafu akasikilizia maana alikuwa hajajua kuwa ni Haidali anaongea
“Samahani, bila shaka naongea na Aneth Massawe” alisema mtaalam Haidali
“kwani wewe ni nani ndugu?” aliuliza binti
“mimi ninaitwa Haidali”
“Haidali?” binti aliuliza
“ndio”
“wa wapi tena?” binti alizidi kuchunguza
“samahani sana, mimi nilikuwa ni mmoja wa watu waliokufanyia interview katika kampuni ya AB Insurance” alisema maneno ambayo yalimshtua binti akijua labda ndo ameshafaulu interview lakini kumbe Haidali alikuwa amekuja kwa sababu alikuwa anahisi yeye na binti wanafahamiana
“ndio” alisema kwa nidhamu Aneth
“samahani sana, nimeamua kuchukua namba yako kwa ajili ya maongezi binafsi naomba unisamehe katika hili”
“mh” binti aliguna kisha akamuuliza “kwani wewe ni yupi kati ya wale waliokuwa pale maana nakumbuka wanaume walikuwa wawili”
“mimi niliyekuwa katikati”
“aaaaah” alisema binti kwa mshangao maana alikumbuka mtu huyo alikuwa anafanana sana na marehemu Amidu “We mwenye kamwili kadogo dogo” alisema huku akijichekesha mtoto wa kike
“yeah…..naitwa Haidali”
“okay ni Haidali nambie, kwanini ulichukua namba yangu kuna tatizo?” aliuliza mtoto wa kike
“naam, nilikuwa na wasiwasi maana kila nilipokutazama nilihisi nilishawahi kukuona mahali”
“hahaha….wapi ulishaniona?”
“sikumbuki, ndo maana nikasema nikutafute ili nijue kama wewe unanifahamu”
“Hahaaa….wanaume bwana” alisema binti halafu akavuta pumzi na kusema “Kiukweli sijawahi kukuona kabla, lakini nilipokuona nilikufananisha na mtu fulani hivi”
“Haah…huenda ikawa hujanifananisha, inawezekana ni mimi maana yake hata mimi ninahisi nilishawahi kukuona kabla”
“Hahaa tatizo ni kwamba mtu huyo tayari alishafariki” alisema Aneth
“ahaha….haya bwana, kumbe unanifananisha na marehemu, basi anyway sio mbaya, huenda ikawa nimezaliwa tena”
“hahha…hapana. Lakini nikuulize swali, wewe ni mzawa wa wapi?” aliuliza
“Mimi mama yangu ni mkurya lakini nimezaliwa Dar”
“je baba?” aliuliza binti
“baba simfahamu ila mama alishawahi kuniambia kwamba baba yangu ni mtu wa morogoro huko alinikataa”
“Mhhhhh” binti kusikia ishu ya Morogoro kidogo aliguna maana katika historia ni kwamba Amidu ambaye alikuwa akimfananisha na kijana huyo pia ni mtu wa Moro.
“mbona umeguna?” aliuliza mtaalam
“hamna sijaguna kwa ubaya, ila basi tu,…nafikiri uliponiona nakushangaa pale kwenye interview ndo ulihisi labda nimekufahamu, lakini ni kwamba tu nilikufananisha na rafiki yangu mmoja ambaye alifariki kipindi cha miezi kama mitatu hivi iliyopita”
“Ok pole sana”
“Asante sana” alisema binti halafu akajikoholesha na kusema “Halafu samahani kidogo, vipi interview nilifanya vizuri kweli?” aliuliza mtoto wa kike
“aammmh sio mbaya, lakini nafikiri utasubiri tu utapigiwa simu”
“Sasa sikiliza kaka angu, naomba unisaidia kidogo na mimi nipite, hata kama ni kiasi cha fedha basi mim nitakupatia ili niweze kupita ninahitaji kazi, ninateseka sana bila kuwa na kazi yaani muda wote ninategemea pesa ya mwanaume tu, ninapata taabu sana” alisema mtoto wa kike
“Okay hamna shida tutaongea”
“Sawa, ila please usinisahau katika hili”
“Hakuna tatizo cha muhimu unikumbushe kesho ili nikifika kazini niweze kuwapanga marafiki zangu” alisema Haidali
“Sawa”
Ilipofika usiku kama saa nne hivi ndipo Erick aliporejea nyumbani, alimkuta mkewe amejilaza anaangalia tamthiliya sebuleni.
“Mke wangu” alisema Erick
“Karibu mume wangu…”
“Umeshindaje mke wangu?”
“Salama tu…..nimechoka tu”
“Umechoka na ni…” kabla hajamaliza sentensi alikumbuka kwamba mkewe alienda kwenye interviewe akasema “Anha ulienda kwenye interview asubuhi, vipi iliendaje?” aliuliza
“Ilienda salama tu….ila walinipigia wanataka kitu kidogo kinisaidie nipate kazi”
“Kitu gani?” aliuliza Erick
“Pesa kidogo kama laki tano hivi”
“Laki tano? Hapana laki tano ni nyingi, achana na hiyo kazi mimi nitakufungulia biashara, kwanza sihitaji uajiriwe” alisema Erick kwa hasira, kuna mambo alikuwa ameshayafikiria akagundua kuwa hataki mkewe aajiriwe alitaka mkewe ajiajiri yeye mwenyewe
“Mh Erick!!” alisema kwa mshangao
INAENDELEA

