MALIPO KITANDANI
ONYO: Wakubwa tu, kuanzia Miaka 18, ndio wasome hii Hadithi
EP 01
Ilikuwa ni shamra shamra zilizofanyika katika kanisa la Anglican Tegeta ambapo kulikuwa na sherehe madhubuti ya harusi iliyofanyika kati ya Erick Jackson Makoti Temu pamoja na binti Janeth Williamson Massawe ambao walifunga ndoa yao takatifu katika kanisa hilo takatifu zaidi
Viapo vya kutokuachana hadi kifo kiwatenganishe zilitaradadi, machozi yakamtoka binti wakati anavishwa pete na mwenzake huyo Erick kwani walikuwa wametoka mbali sana mpaka kuamua kuoana.
Sherehe kubwa ilienda kufanyika katika maeneo ya Mlimani City, Mwenge Jijini hapo hapo Dar es Salaam na hata ilipomalizika walikuwa na furaha tele.
Ndoa hii ilikuwa ni furaha kwa watu wengi, kwani Erick alikuwa na pesa nyingi sana huku akijihusisha na biashara ya kuuza mchele kutoka Mbeya na kusambaza jijini Dar es Salaam na mikoa mingine ya pwani. Huku Aneth akiwa na biashara ya miamala ya simu na benki, zote alifunguliwa na Erick mara tu baada ya kumaliza elimu yake ya Shahada ya Kwanza katika chuo kikuu cha Dar es Salaam miaka mitatu iliyokuwa imepita.
Familia zao zilifurahi watoto hao kuungana na kuwa mwili mmoja, waliwapa zawadi nyingi sana ziwasaidie katika maisha yao.
Hata hivyo licha ya furaha kuwepo upande wa Aneth na familia yake, na upande wa Erick na familia yake, kuna upande wa tatu ,wa kijana mmoja aliyefahamika kwa jina la Amidu, alikuwa katika mawazo na stress zisizopingika.
Amidu alikuwa ni mmoja kati ya vijana ambao walikuwa wamehudhuria sherehe zile tena kwa mwaliko rasmi, kwani alikuwa karibu sana na watu hao wawili ambao walimsapoti katika vitu vingi sana licha ya kutokuwa na elimu kubwa lakini walimpenda maana alijituma na alifanya kazi za Erick kwa zaidi ya miaka saba.
Amidu aliondoka pale kwenye sherehe ya harusi, Mlimani City akavua koti lake lake na kubaki na shati jeupe lililolowa jasho, akalegeza tai shingoni kisha akatoka akiwa na mawazo tele tele kwani alionekana kuna jambo lililokuwa likimsibu kijana yule
Marafiki ambao pia walikuwa karibu na Amidu walimuona akitoka kwenye sherehe wakati sherehe bado haijaisha, tena alikuwa speed, macho yalikuwa mekundu sana.
“Oya wapi mzee?” Aliuliza kijana mmoja aliyekuwa akiitwa Elisha Michael lakini Erick alipita bila kujibu lolote na kutoka kupitia mlango mdogo mpaka nje
Huku ndani aliacha mawazo upande wa marafiki zake wale walibaki wakiulizana vipi, au amepata tatizo gani mbona anaondoka hata sherehe haijaisha, hakuna chakula chochote kilicholiwa, walijua labda kapatwa na tatizo
Elisha alihisi vibaya, akaondoka eneo lile, akaenda chooni na kutoa simu mfukoni akampigia ili angalau amuulize kama kuna tatizo lolote lakini Amidu alipoiona simu aliikatilia mbali halafu akazima simu hakutaka mawasiliano kabisa.
Kwa miguu Amidu alitembea mpaka akafika mawasiliano, alipofika aliingia katika mtaa moja pembeni kidogo mwa stendi, kuna kamto fulani, aliketi kando ya ule mto akaanza kulia huku akilaumu
“Nimekukosea nini??? Mimi nimekosea nini mpaka ninyanyasike hivi?? Alisema huku machozi yakimtiririka kwani alionekana kuna jambo zito sana lililokuwa limemkumba kijana yule
Licha ya watu wa ulinzi kumfuata pale kando ya mto na kumuambia aondoke lakini Amidu alikesha paleplae Mtoni, mbu wakimuuma baridi ikimtafuna, bila kuogopa vibaka waliokuja na kumpora simu yake alikuwa analia sana kijana Amidu.
Upande wa kwenye sherehe Bwana harusi, Erick alikuwa na wanafamilia, na marafiki ndipo akamuita Elisha na kumuuliza “Amidu yuko wapi??”
Elisha alimtazama kisha akasema “Aliondoka kwa hasira hapa hatujui kapatwa na nini”
Aneth kusikia maneno yale alishtuka na kumtazama Elisha kisha akamuuliza “Kaondoka akiwa na hasira?”
“Ndio, alikuwa na hasira sana…..alionekana mwenye stress, nilimuongelesha wala hakunijibu chochote, alionekana kukwazwa na kitu fulani kizito sana”
“Duuh itakuwa tatizo nini?” Erick aliuliza
“Hatujui sasa” alijibu Elisha
*
Saa kumi na moja alfajiri, Amidu aliinuka pale mtoni alipokuwa akatembea mpaka barabara kuu, akalipia pikipiki na kupelekwa nyumbani kwake alipokuwa amepanga maeneo ya Shekilango, ndipo akavua nguo na kuingia ndani ya bafu akajifungia na kufungulia maji ya bomba la mvua yakammiminikia mwilini halafu akaketi chini sakafuni huku akizidi kutokwa na machozi ambayo yalibebwa na maji na kutiririshwa moja kwa moja mpaka kwenye chemba ya serikali
EP 02
Siku saba zilipita bila Amidu kuonekana mtaani, simu ilikuwa haipatikani kabisa, na hata walipoenda nyumbani kwao hawakumkuta kabisa kijana yule, walipata mawazo teletele.
Kizaazaa kilianza pale Zanzibar, kwenye fungate lililokuwa likifanyika na wanandoa wawili wapya, Erick na mkewe Aneth Massawe. Hii ni baada ya Aneth kujaribu kuwasiliana na Elisha na kumuuliza kama wamefanikiwa kumuona Amidu ambaye alikuwa mtu mwenye ukaribu mkubwa sana na watu hao hasa kibiashara, alikuwa na nyota ya biashara hasa.
“Shem huyu Amidu hajapatikana, hayupo kule nyumbani kwake, vile vile hayupo kwao mkoani morogoro, kamwe hawakujua kaelekea wapi” ilikuwa ni sauti ya Elisha ikisikika katika tundu la sikio la kushoto la Aneth masawe ambaye alikuwa nje ya hoteli ya kifahari mjini Zanzibar akiwa ameegemea baraza ya hoteli hiyo waliyokuwa wamekodisha vyumba kadhaa kwa ajili ya fungate lao.
Erick akiwa amejifunga taulo kiunoni alitoka, barazani, akamkuta mkewe amesimama anaangalia mbali, huku akiwa na mawazo tele, akamkumbatia kwa nyuma kitendo kilichomshtua binti hadi akadondosha simu
“Ah wewe” aliongea kwa mshtuko mwanamke yule kwa mshtuko “Umenishtua”
“Oh I am sorry baby….kwani vipi mbona umeniacha ndani peke yangu?” aliuliza Erick huku akiokota simu ilikuwa imepata kreki kwenye kioo kilindi (protector)
“Imepasuka???” Binti badala ajibu swali, naye alipachika swali juu juu
“Usijali hii ni protector tu…anyway tutaweka nyingine kesho usijali”
“Sawa”
Erick alimpatia simu mkewe kisha akamshika “embu twende ndani bwana”
Waliingia ndani lakini Aneth hakuwa na furaha hata chembe. Waliketi kwenye sofa kisha binti akasema “Hivi unajua Amidu hajapatikana?”
“Usijali atapatikana tu, ndo uwe na mawazo hivi mke wangu?” aliuliza Erick
Aneth alitabasamu kwa kujilazimisha kisha akasema “Sio hivyo, nilijua atakuwa kule nyumbani atusaidie biashara zetu kipindi tuko huku honeymoon”
“Ah tunarudi siku si nyingi, usijali kuhusu hili atakuwa sawa tu”
“Kweli unasema hivi? Ni mambo mangapi ameshawahi kutusaidia katika maisha? Ni kwanini aondoke tena siku ya harusi yetu? Au ulimkwaza Erick? Nambie nina wasiwasi, yule nimeshamfanya kama mdogo wangu eti”
“Usijali kuhusu hilo tutafuatilia, acha niongee na Elisha halafu atalimaliza hili, sawa??” aliuliza kijana Erick
“Sawa mume wangu”
Erick kwa haraka hakuelewa, alijua ni undugu uliojengeka kati ya familia yao pamoja na kijana Amidu pamoja na marafiki wengine kama kina Elisha na kadhalika.
Ilikuwa ni usiku uliojaa kiza kinene, walikuwa wanafanya mambo yao kitandani, binti alikuwa hajaridhika lakini hakutaka kuendelea, ghafla tu moto ulimkata na kujikuta anamuomba mumewe aahirishe tendo lile walilokuwa wakilifanya
“Why? Kwanini tuache kufanya?”
“Erick, nimechoka, unajua kabisa tumefanya mara nyingi sana tangu tuje hapa, leo hata hamu sina, naomba nipumzike tu” alisema binti
“Okay sawa” Erick hakujali sana, maana alikuwa amefanya mara nyingi na binti yule na vile vile alikuwa sio mgeni kwake.
Saa nane na nusu, simu ya Erick iliita na alipoitazama alikuwa ni Elisha anampigia, ndipo akamtazama mkewe ambaye alikuwa amelala kando kisha akapokea na kuongea kwa sauti ndogo kabisa ambayo anajua haitamsumbua mkewe aliyekuwa fofofo
“Hallo”
Elisha naye akasema “Hallo kaka, najua nakusumbua katika muda wako huu wa kupumzika” aliongea Elisha kwa masham sham halafu akakohoa na kuonyesha ana huzuni kubwa
“hamna tatizo, uko powa wewe?”
“Siko powa kaka”
“Tatizo nini Elisha?”
“Kaka, mwili wa Amidu umekutwa baharini alishakufa”
“Alishakufa???? Kivipi???” Erick aliuliza kwa mshangao mkubwa sana huku akiketi kitandani bila kutarajia.
“Ndio kaka”
“We embu acha masihara bwana” alisema huku akiinuka na kutembea kuelekea mlangoni akafungua mlango taratibu mpaka nje akasimama barazani”
Elisha alilia sana, machozi yalimtiririka kule alipokuwa ndipo akasema “Ndio kaka, ninaumia sana”
“Aliuawa au imekuwaje?”
“Daaah” Elisha alizidi kuongea kwa uchungu, “Inavyosemekana alijirusha mwenye baharini, lakini polisi wanaendelea na uchunguzi” Elisha aliongea akizidi kulia, machozi yalimshinda akashindwa kuongea kabisa
Ulikuwa ni uchungu wa hali ya juu, hakukuwa na namna kabisa, hata hivyo alijikuta anakata simu na kumuacha njiapanda Erick
Erick alibaki na mawazo tele, ndoa imeanza na visirani, ile furaha iliyokuwa imemjaa baada ya kuoa, ilitoweka na kugeuka kuwa huzuni kubwa. Erick aliwasha data, akaingia katika mtandao wa Instagram, ilikuwa hata haijapita dakika nyingi, alikuwa amepost Millard Ayo akiandika kichwa cha habari
“MWILI WAKUTWA BAHARINI, YASEMEKANA ALIJIUA KWA MSONGO WA MAWAZO, huku ikifuatiwa na maelezo
Kijana mmoja ambaye alifahamika kwa jina la Amidu Hassani, miaka 24 amepatikana mwili wake baharini maeneo ya Mbezi beach akiwa amekufa, inasemekana alijirusha baharini kwa lengo la kujiua kwa sababu alikuwa na msongo wa mawazo, polisi kanda maalum ya Dar es Salaam wanaendelea na uchunguzi kuhusiana na tukio hilo”
Hii habari ilimdhirishia Erick kwamba kweli Amidu amefariki, alijiuliza maswali kedekede, kwamba ‘Kwanni ajiue? Kwani alikuwa na stress gani mpaka ashindwe kuniambia? Kwani aliona siwezi kumsaidia? Au alipima akakutwa na ngoma nini?”
Yote haya yalikuwa ni maswali kichwani mwa Erick, ndipo akapita mtandao wa WhatsApp na kuchungulia status, aliona marafiki zake wengi wakiwa wamechapisha hadhi zao huku wakiandika R.I.P MWANANGU HASSAN, ILA UMEONDOKA MAPEMA SANA na maneno mengine kama hayo.
Erick taratibu aliingia katika kitanda chake, akajilaza na kumkumbatia mkewe ambaye alikuwa hajapata taarifa maana alikuwa usingizini..
EP O3
Usiku kucha Erick hakulala, aliwaza mambo mengi ambayo alishawahi kufanya na Amidu, machozi yalimtiririk lakini hakuthubutu kumuamsha mkewe.
Taratibu aliamka kutoka kitandani akaenda kulilia nje, alikuwa anapata uchungu hasa, alijua kabisa mazishi ya Amidu hayatachukua muda mrefu, alijua atazikwa siku itakayofuata.
Saa kumi na mbili asubuhi, usingizi ulimuisha Aneth, na tena bila kufumbua macho alinyoosha mkono na kuuweka juu ya meza ndogo iliyokuwa karibu na kitanda akaanza kupapasa ili kuitafuta simu yake ambayo aliamini ameiweka pale usiku kabla ya kulala.
Alipopasa alishangaa kutokuigusa, akafumbua jicho moja na kuitazama ile meza, akagundua hakuna simu yake, alishtuka na kugeuka huku akiita “Erick” lakini cha kushangaza Erick hakuwepo pale ndani.
“Mh” aliguna halafu akatazama mlangoni, bado ulirudishiwa “We Erick” alisema kwa sauti kubwa na kuinuka akaketi kitandani na kujinyoosha huku akipiga miayo, ndipo akaangaza kule na huku lakini hakufanikiwa kuiona simu yake vile vile.
“Khaa kaondoka nayo?” Aliwaza na kushuka kitandani akasimama halafu akaita “Erick” huku akichungulia dirishani ndipo akamuona Erick akiwa amegemea vyuma vya baraza.
Kwa kuwa binti alikuwa hajavaa, ilibidi ajifunge kitenge hadi kifuani halafu akafungua mlango na kuchungulia. Bado Erick hakumtazama, aliendelea kuwaza huku akiangalia mbali.
“We Erick. Mume wangu” alisema binti na kufungua mlango akatazama, kulikuwa ni ghorofani
Erick aligeuza macho na kumtazama mwanamke wake bila kuongea chochote. Aneth alipomuangalia machoni, aliona macho ni mekundu, yanaonekana yamelia sana, uso umemkakamaa mtaalam, na alionekana hajalala.
Wasiwasi ulimjaa binti, hasa pale alipotazama mikono ya Erick alikuwa ameshikilia simu zote mbili ya kwake na ya mke wake. Hili lilimfanya mkewe akahisi labda Erick amekuta message au kitu chochote kibaya katika simu yake.
Aliwaza haraka haraka lakini akagundua kuwa hakuna chochote kibaya mbona, aliogopa na kuuliza
“Mume wangu uko sawa?”
Aneth alishaanza kutetemeka kwa wasiwasi, lakini Erick alisikitika na kufyonza kidogo kisha akasema “Kaoge uvae vizuri usikae hapa uchi” aliongea kwa hasira kidogo
“Lakini mbona kama hauko s…..”
“Kaogee”
Binti alitetemeka na kuingia ndani akiwa na wasiwasi zaidi, kwanini jamaa amfokee wakati ndoa ndo kabisa ni changa mno haina hata wiki moja.
Aneth alirudi ndani bado kichwani alijiuliza kwanini mumewe anakosa raha kiasi kile, alijua labda kuna kitu amemkosea, lakini kumbe Erick alikuwa na huzuni kisa amepata taarifa juu ya kifo cha kijana wake wa nguvu aliyefahamika kwa jina la Amidu Hassani kijana wa kiluguru halisi na rasmi.
Pia Erick alikuwa amechukua simu ya mkewe wakati akiwa amelala ili akiamka asiingie mtandaoni maana aliamini mkewe akiingia tu, lazima atakutana na ile habari kwamba Amidu amefariki na ataianza siku vibaya.
Aneth akiwa anaoga bafuni, basi huku nje Erick alipata simu kutoka kwa kijana mmoja aitwaye Dullah, pia wote hao walikuwa ni crew moja na kina Elisha pamoja na marehemu Amidu.
Erick aliipokea kwa sauti hafifu ili mkewe akiwa ndani asisikie
“Niambie kaka”
Dullah akamuambia “naamini una taarifa za kifo cha Amidu”
“Ndio kaka”
“Anapelekwa leo, mapema sana akazikwe, embu tuambie unafika?”
“Duuh kaka ni ngumu sana, kumbuka hatujakata tiketi ya ndege, tafadhali chelewesheni maiti tutakuja kesho asubuhi sana”
“Pamoja kaka, nitajitahidi”
“Sawa”
Erick alikata simu haraka baada ya kusikia mlango wa bafu umefunguliwa na mkewe.
Aneth alipofika pale, Erick alitabasamu ili kumuonyesha furaha lakini binti alipomtazama aligundua mumewe hayuko sawa.
“Erick niambie ukweli” alisema binti
“Ukweli wa nini?”
“Umekutana na kitu kibaya kwenye simu yangu? Mbona ulikuwa nayo na macho yameonekana yamekasirika na hata kulia”
“Hahahaaa…..hapana mpenzi, sijapata usingizi kabisa leo, nilikuwa na mawazo tele kuhusu biashara hasa baada ya kutompata tena Amidu…..anyway nimepata furaha ghafla baada ya Dullah kunipigia simu na kuniambia Amidu alikamatwa na polisi ndio maana tulikuwa hatumpati, hata hivyo yuko kituo cha polisi tutaenda kesho tukalishughulikie atoke maana biashara zitakwama” alisema Erick lakini ni dhahiri kwamba alikuwa anamdanganya mkewe, hakutaka mkewe ajue kwamba Amidu kafariki maana alijua binti atapaniki na anaweza kumletea matatizo makubwa zaidi ni heri akamficha ili warudi kwanza bara
“Mh kweli?” aliuliza binti
“Ndio”
“Kwani alikamatwa kwa kosa gani Amidu?”
“Nasikia alimgonga mtu na pikipiki”
Kidogo hili jibu lilimpa faraja mtoto wa kike maana nia yake alikuwa anataka tu Amidu awe na afya njema. Hakujua kwamba mumewe anamdanganya
Kule bara, Shekilango, Ubungo, Dar es Salaam kina Elisha, Dullah na marafiki wengine walikuwa wameingia katika chumba cha marehemu Amidu na walikuwa wanataka kuchukua vitu vyake ili wasafirishe pamoja na mwili kuelekea mkoani Morogoro
Katika kupekua pekua ndani, Elisha alikutana na barua mezani, akaichukua ile barua ambayo ilikuwa imeandikwa siku moja kabla ya kujiua kwa marehemu Amidu.
Elisha alianza kuisoma ile barua, ikamfanya akatoka jasho mwili mzima maana maneno yaliyokuwa yameandikwa kule ndani yalikuwa ni maneno mazito kweli kweli..
JE BARUA ILIKUWA IMEHUSIANA NA NINI?
INAENDELEA

