Mume Wangu Anachukua Mshara Wangu Kumjengea Ex Wake!
Kaka naomba ushauri wako, mimi nimeolewa, ninafanya kazi ni mwalimu na mume wangu naye ni mwalimu. Kabla ya kunioa mume wangu alikua na mahusiano na mwanamke mwingine ambaye ana mtoto mmoja naye, sikua najua mpaka siku ya harusi yangu, yule mwanamke alinitumia picha kesho yake na kuniambia kuwa naringa lakini yeye ndiyo anapendwa na mtoto kashamzalia. Niliumia sana lakini nilimuuliza mume wangu akakubali kuwa ni kweli ana mtoto aliogopa kuniambia kwani alihisi kama naweza kukataa kuolewa. Sikua na namna nilimsame.
Lakini baada tu ya kuingia kwenye ndoa mume wangu aliniambia nimpe ATM card yangu, kwamba msahara tuchanganye tupange matumizi kwa pamoja, nilikubali kishingo upande lakini kaka ni mwaka wanne sasa hivi sijawahi kugusa kabisa pesa yangu ya mshahara, yaani kila kitu ni lazima nimuombe yeye na anakua anasema hana, nikimuuliza pesa anapeleka wapi ananitukana na kunipi*ga akiniambia mimi sina akili mbona nakula nakunywa na siulizi pesa zinatoka wapi. Niliamua kujiongeza baada ya kusoma kitabu chako cha Biashara, nikachukua mkopo kwa mtu nikaanza kuuza mashuka na vitenge.
Alipoona nina pesa akaacha kabisa kutoa pesa ya chakula nikimuuliza anaseme toa kwenye Biashara, wakati mwingine anakuja na kuniomba elfu kumi na harudishi hivyo mtaji ukafa, nikawa sina tena pesa ya mtaji na bado nina deni. Nimekua nikiumia sana nikiteseka kwani huyo mwanamke mwingine alozaa naye kutwa kucha kunipigia simu kunitukana na kuniambia kuwa mimi natafuta yeye anatumia.
Nikimuuliza mume wangu anakua ananiambia kelele za nini wakati wewe umeolewa umewekwa ndani, ananipi*ga naishia kuomba msamaha. Sasa sababu ya kuja kwako Kaka.
Juzi nimeona huyo mwanamke kapost status nyumba kubwa imeisha, ameandika watu na nyota zetu wengine wanafanya kazi sisi tunajengewa. Nimemuuliza mume wangu hata hakubisha ananiambia kuwa, yule mwanamke wana mtoto naye amemjengea mwanae si mwanamke, kaka mimi nina watoto wawili lakini hata kiwanja hakuna, hajawahi hata kununua nguo ya mtoto ni mimi kuhangaika na kukopa wakati msahahara wote anachukua yeye. Naomba ushauri wako kaka nifanye nini?

