KAKA USIACHE KUMPIGANIA DADA YAKO!!
Ujumbe huu ni wa kwako kijana wa kiume ambaye una dada nyumbani. Lakini pia, ujumbe huu ni kwa ajili ya kaka ambaye baba alifariki,yeye kama mtoto wa kiume amebaki kama baba wa familia au kiongozi wa familia yenu.
Nakushauri kaka,haupaswi kumtelekeza dada yako. Unapaswa kuwa nguzo muhimu na kumpigania kwenye maisha yake kwasababu baada ya BABA YENU upo wewe;
1. Usinyamanze kimya anapofanyiwa unyanyasaji kwenye ndoa yake. Baada ya baba yenu upo wewe,usikubali kwenye ndoa yake apigwe na kufanyiwa vitendo vya unyanyasaji. Msaidie kumshauri,kumfariji na kusuluhisha matatizo yao ili awe na furaha na amani. Hivyo ndivyo kaka anapaswa kuwa kama BABA.
2. Usinyamanze kimya dada yako anapougeuza mwili wake kuwa chanzo cha kipato(Kuuza mwili wake ili kupata pesa).
Kama anafanya hivyo kwasababu ya matatizo ya kifedha, msaidie pesa ya kuanzishia biashara au kutatua matatizo yake kama uwezo wa kumsaidia unao ili kumtoa kwenye ukahaba. Nimewashuhudia vijana wengi wakiwatandika makofi dada zao,sio kwa nia mbaya bali kurekebisha tabia zao ili kuondoa aibu ya familia. Kuuza mwili wake ili kupata pesa sio tu kujidhalilisha yeye bali FAMILIA YOTE INADHALILIKA.
3. Usinyamanze kimya dada yako anaponyanyaswa Kingono.
Katiwa mimba akiwa bado mwanafunzi na kukatishwa masomo yake, Kaka upo umekaa kimya unaangalia tu. Kabakwa, kapigwa picha za utupu na kudhalilishwa mitandaoni wewe unaangalia tu. Rafiki, kama kaka msaidie kupigania haki ya dada yako na kumlinda. Baada ya baba yenu, upo wewe…hakuna baba anayekubali familia yake idhalilishwe. Ukitaka kujua hasira za Mwanaume Kamili,gusa familia yake. Hivyo ndivyo na wewe unapaswa kuwa, MWANAUME KAMILI.
4. MFUNDISHE dada yako kuwa karibu na Mungu(Kushikilia maadili yake ya kiimani).
Kuwa karibu na Mungu au kuheshimu maadili yake ya kiimani kutamsaidia kuepukana na kuutumia mwili wake kama chanzo cha kipato lakini pia kutamsaidia dada yako kuishi katika ndoa yake vizuri na kama kaka hautaweza KUAIBIKA KWASABABU YAKE, atakuheshimisha.
5. Usinyamanze kimya dada yako anapokosa KUJIAMINI.
Kupoteza uwezo wa kujiamini kwenye maisha ndio chanzo cha kuteswa na kunyanyaswa katika mambo mbalimbali maishani. Mfundishe dada yako KUJIAMINI NA KUJIKUBALI.
6. Mhamasishe dada yako kupenda KUJIFUNZA.
Kuna msemo wa Kiingereza unasema,”The time when a man stops learning, is the time in which his life stops”. Msemo huu unatafsirika kuwa, “Muda ambao mtu anaacha kujifunza ndio muda ambao maisha yake yanafikia mwisho”.
Yaani, mfundishe dada yako asiache na apende kujifunza vitu vipya kila siku. Mfundishe kutafuta ufahamu na maarifa, hapo ndipo utafanikiwa kumsaidia yeye kufanikiwa katika ndoa yake lakini pia kufanikiwa kiuchumi na kutoka kwenye utumwa wa kunyanyasika.