MKE WANGU NUSU MTU, NUSU JINI
EPISODE 11
ILIPOISHIA
“Ni wazazi wako hawa?” nilijikuta nikiuliza bila kutarajia.
“Ndiyo, kwani vipi?”
“Mbona wadogo sana?”
“Hapana, mimi nina miaka hamsini, mke wangu huyu ana miaka arobaini na tano, ni wadogo sisi?” baba mtu alidB
ado kwangu ilikuwa ajabu kwani hakuna aliyeonekana kufikisha hata miaka thelathini na mitano…
“Ina maana…mbona hata mimi ni mkubwa kwenu,” nilisema nikibabaika.
Kwanza walicheka wale wazazi wote kisha baba yake Munil akasema:
“We huwezi kuwa mkubwa, wewe una miaka thelathini na moja kama sikosei.”
Nilishtuka sana kusikia vile japokuwa alisema kama hakosei, yaani alibashiri lakini ni kweli nilikuwa na miaka thelathini na moja wakati huo. Kwa nini asingesema nina miaka thelathini? Nilimwogapa sana lakini nikajibu:
“Ni kweli kabisa.”
“Sasa utasemaje sisi ni wadogo?”
Yaliishia hapo, nikajikuta nikiuliza:
“Hivi hii ni Bagamoyo gani? Maana sikujua kama Bagamoyo kuna majengo ya kifahari kama haya.”
“Hii Bagamoyo ya Majini,” alijibu mama’ke Munil.
“Majini maji au majini wale viumbe wabaya wanaoogopwa na binadamu?” nilidadisi tena.
“Majini maji,” alijibu baba Munil lakini sura ya mkewe na hata ya Munil zilionesha kutokuwa sawasawa. Nikawa najiuliza ni kwa swali la mwisho au! Nikakosa jibu lakini pia nikaamua kuwa mpole.
“Sasa kijana wewe ndiyo unataka kumwoa binti yetu, upo tayari au bado unapanga mipango?” swali hilo lilitoka kwa baba wa Munil.”Kusema ukweli wazazi wangu mimi nimenuia kumwoa kabisa Munil na nimejipanga kwa hilo, huenda baada ya mwezi ujao nikaleta posa kwenu.”
“Posa ndiyo nini?” baba Munil aliniuliza kwa mshtuko.
“Ni barua ya kujitambulisha.”
“Utambulisho gani tena? Si hivi umekuja kujitambulisha! Sisi tunachotaka kama kweli umeamua kumuoa binti yetu Munil tukufungishe ndoa sasa hivi hapahapa,” alisema baba.
“Nipo tayari,” hii kauli ya ‘nipo tayari’ nilijikuta inatoka bila kutarajia. Mdomo ulikuwa kama umeongozwa kusema hayo bila mimi mwenyewe kutaka. Sijui ni kwa nini!
Basi, baba Munil alisimama akaenda kuingia kwenye chumba f’lani. Alipotoka alikuwa ameshika
mkeka si mkeka, kapeti si kapeti, sijui kilikuwa kitu gani. Akautandika chini, akamwita Munil, akakaa juu yake. Nikaitwa na mimi, nikaenda kukaa sambamba na Munil.
Baba alitushika vichwa, akasema maneno kama kiarabu kwa muda wa kama dakika tano nzima anasema tu. Alipomaliza akatusimamisha huku akisema:
“Munil, kuanzia sasa huyu ni mumeo, mkaishi pamoja na mzae watoto lakini usikose kuja kututembelea wazazi wako kila mara.
Kwa kuwa unaweza kuendesha gari, utaondoka na lile la mama yako, nitamnunulia lingine. Pia kabla hamjaondoka, nitakupa pesa ukafanye biashara yoyote ile.”
Nilijikuta moyo wangu ukiwa baridi, nilijishika masikio na kuyatanua kwa vile nilihisi yamekaa vibaya ndiyo maana nikawa nasikia vile wakati si kweli.
“Wazazi ninaomba kusema kidogo,” nilisema nikiwa nanyoosha mkono juu.
“Ndiyo bwana, sema.”
“Mimi ninaishi kwenye chumba kimoja tu, halafu uswahilini, sasa mnaposema mnampa gari huyu nitapata tabu ya sehemu ya kuliegesha, afadhali tukajipange kwanza, kwa leo tutarudi na ile teksi tuliyokuja nayo.”
Mara, baba Munil alisimama na kwenda ndani, sikujua ni chumbani au kwenye nini! Aliporudi alikuwa ameshika mfuko mweusi, ndani sikujua mna nini, akauweka chini akiwa ameubana na miguu, akasema:
“Mimi ni mfanyabiashara mkubwa sana, fedha kwangu si tatizo ilimradi binti yangu asiishi maisha ya tabu.”
Akainama kidogo na kuingiza mkono kwenye ule mfuko, ulipotoka ulikuwa umeshika dola za Kimarekani tupu tena mpyaa! Ilikuwa ngumu kwangu kukubali kwamba baba Munil anaweza kuwa milionea kiasi kile tena akisema ni mfanyabiashara wa siku nyingi wakati umri ulionesha bado kabisa.
Alihesabu zile dola kisha akatumbukiza mkono tena na kutoa nyingine, akahesabu halafu akatumbukiza tena mkono, akatoa nyingine, mwishowe akawa ametoa zote. Kama ni wingi wa fedha ya noti ya shilingi elfu kumi za Tanzania palepale ningesema ni zaidi ya shilingi milioni hata mia moja.
Alizitumbukiza zile fadha kwenye uleule mfuko mweusi, akauinua na kuniletea nilipokaa huku akisema:
“Hizi ni dola, Munil,” alimwita binti yake.
“Abee baba.”
“Kama mtachenji mtapata kama shilingi milioni mia mbili. Lakini nashauri muweke banki, we unajua. Na kama ni benki, itumike akaunti ya mumeo, si ya kwako, wewe sasa huna amri juu ya mambo yako ila mumeo.”
Sijui nini kilitokea, ila nilianguka puu! Nilipokuja kuzinduka, nilijikuta nipo hospitali, nimezungukwa na Munil, shemeji yangu, yaani mke wa marehemu kaka na wauguzi watatu.
“Pole sana baby,” Munil alisema baada ya kuona nimefumbua macho na kuangalia.
Shemeji naye akasogea na kunipa pole kama Munil huku akisema Mungu atanisaidia.
“Kwani hapa ni wapi?” niliuliza.
“Ni zahanati hapa,” alijibu Munil.
“Ni wapi?”
“Bagamoyo.”
“Nimekujaje?”
“Ulianguka ghafla baby, wazee wakakumbiza hapa na gari.”
“Wao wako wapi?”
“Wameondoka, huenda wakarudi baadaye.”
“Shemeji umejuaje?”
“Nilimpigia simu mimi.”
“Ulipata wapi namba yake?”
“Nilichukua kwenye simu yako baby.”
Nilitaka kumuuliza Munil swali lingine kwamba, aliingiaje kwenye simu yangu? Maana ilikuwa na password lakini nikaacha.Wale wauguzi waliondoka, akaja daktari.
EPISODE 12
“Sasa mgonjwa wangu unaweza kuondoka, drip imeisha kwa hiyo unaendelea sawasawa, jiamini bwana,” alisema daktari bila kuniambia nijiamini kwa lipi.
“Basi kama umeruhusiwa tuondoke, gari letu liko nje,” alisema Munil huku akimwangalia shemeji ambaye naye alionekana kuwa na uso wa mshangao.
“Tunakwenda wapi?”
“Si tunarudi Dar.”
“Oke, wazee utawaambia?”
“Nitawaambia,” alisema Munil huku akichukua mfuko flani hivi na kutoka nao nje. Nikabaki na shemeji.
“Hivi shemeji, kwani wewe umeoa siku hizi?”
“Hapana shemeji.”
“Sasa huyu ni nani?”
“Huyu ni mchumba wangu shemeji, iko siku nitakuja kukutambulisha rasmi.”
“Mh! Mbona hali yake ya mwili inaonekana ana maisha mazuri sana?”
“Hata mimi nitakuwa na maisha mazuri shemeji.”
Mara, Munil aliingia:
“Tunaweza kwenda sasa.”
Nilitoka mwenyewe kitandani, nikatembea huku Munil akiwa amenishika mkono japokuwa sikuwa nahitaji msaada huo.
Lilikuwa gari la kifahari, jipya, jeupe pee, zuri sana. Ndilo ambalo Munil alikwenda kufungua mlango. Kwanza alizunguka na kunifungulia mlango wa mbele kwa abiria mimi kisha akarudi kufungua kwake, akapanda shemeji naye akapanda maana wakati huo tayari milango ilishajitoa kwenye loki.
Kusema kweli lilikuwa gari zuri sana. Sikuamini kama ni letu mimi na Munil. Niliona ni la Munil peke yake tena nilijikuta nikiamini kwamba, mimi na Munil hatutaweza kudumu.
“Gari zuri sana, jipya,” nilisema.
“Tena ndiyo nimeanza kuliendesha mimi leo,” alisema Munil.
Ukimya ulitawala barabarani, muda mrefu nilikuwa nawaza kuhusu gari na zile hela alizotoa baba yake Munil ambazo alisema ziingie kwenye akaunti yangu.
Nilitamani kumuuliza Munil kama zile pesa tunazo au baba yake alizirudisha kufuatia hali yangu ya kuanguka!
“Ule mzigo vipi?” nilimuuliza kwa wasiwasi.
“Upo, si huo huko nyuma.”
Niligeuka kuangalia, nikauona ule mfuko, ulikuwa jirani kabisa na shemeji ambaye naye alipoona naangalia mfuko akautupia macho.
“Huogopi Munil?” nilimuuliza.
“Nini?”
“Kuibiwa.”
“Ha! Katika maisha yangu hakutakuja kutokea kitu kama hicho, yaani mimi niibiwe haitatokea hata siku moja.”
“Usiseme hivyo, huwezi kujua,” alisema shemeji kwa sauti ndogo sana.
“Yaani nakuapia, hakuna siku hata moja ambayo mimi nitaibiwa na mtu,” Munil alisisitiza.
Mimi niliamua kukaa kimya lakini si kwa sababu nilipenda bali nilimtafakari Munil kwa jicho la tatu, kwamba yeye ni nani mpaka ajiapize kutoibiwa na mtu.
Shemeji yeye hakuendelea kukaa kimya, akaongea. Lakini ilionekana wazi kwamba aliongea ili kuvunja ukimya wa ghafla.
“Nimeipenda hiyo pafyumu yako we dada mdogo,” alisema shemeji.
“Hii inayotoa harufu?”
“Ee.”
“Nimeipata mbali sana, Dubai.”
“Kwani huwa unakwenda Dubai?” alihoji shemeji.
Kidogo nilianza kufurahi kwamba, maswali ya shemeji kwa Munil yanaweza kutoa mwanga wa mimi kuzidi kumjua Munil.
“Siendagi mimi, ila kuna mtu ananileteaga.”
“Naweza kupata na mimi kama hiyo kwa kumwagizia huyo mtu?”
Munil badala ya kumjibu, alinyoosha mkono kwenye boksi ndani ya gari hilo kushoto jirani yangu
akaminya mahali, mfuniko ukafungua, akatoa boksi lenye pafyumu, akampa shemeji kwa nyuma huku yeye akiangalia mbele barabarani.
“Kumbe unazo?”
“Ilibaki hiyohiyo moja,” alijibu Munil.
Lakini kusema ule ukweli, wakati mfuniko wa lile droo unafunguka, mimi kama niliona hakuna kitu lakini ghafla niliona mkono wa Munil ukishika boksi na kulitoa.
Halafu kwa mujibu wa baba yake kule Bagamoyo, lile gari lilikuwa jipya kabisa sasa yeye aliingiza boksi muda gani mle ndani? Na hata Munil mwenyewe alisema gari ameanza kuliendesha siku hiyo.
***
Tulifika Dar mpaka kwa shemeji, tukamshusha, kisha mimi na Munil tukaenda mpaka nyumbani kwangu. Munil aliegesha gari nje ya nyumba ambako ulinzi wake ni wasiwasi mtupu.
“Itabidi gari likalale kwenye sehemu yenye ulinzi,” nilishauri.
“Hapahapa, ulinzi upo mkubwa sana,” alinijibu Munil huku akishusha vitu vichache ukiwemo ule mfuko mkubwa wenye fedha.
Tulizama ndani kwetu, eti kuanza maisha mapya ya mke na mume. Mimi nimekuwa mume wa Munil, kwangu ilikuwa ndoto za kila usiku.
“Munil,” nilimwita kwa upole.
“Niambie mume wangu”
“Baba alisema pesa tukaweke kwenye benki gani?”
“Benki yako. Hata kama huna itabidi ufungue tu.”
“Unadhani ni sahihi mimi kumiliki fedha za baba mkwe wangu wakati wewe upo?”
“Ni sahihi, mimi ni mke, wewe ni mume, tatizo liko wapi sasa?”
“Siku tukiachana je?”
“Haitatokea. Kwanza kwa nini tuachane mume wangu? Una mpango huo kichwani?”
“Sina ila sisi ni binadamu”
“Weee…weee! Binadamu peke yako, mimi si binadamu, nikwambie kabisa.”
“Sawa wewe ni nani Munil, mbona unanitisha?”
EPISODE 13
“Mimi ni mtu. Kwani we hujui kwamba wanawake wote sisi ni watu nyiye wanaume ndiyo binadamu ingawa pia ni watu?”
“Kivipi Munil?”
“Kwa sababu mnatokana na ubini wa Adamu. Ndiyo likapatikana jina la bin Adamu ambapo watu wamezoea kusema binadamu. Lakini neno lenyewe ni bin Adamu, kama watoto wa kiume wengi unavyoweza kukuta wanaitwa bin Hemed, bin Jumaa lakini sisi wanawake ni binti.”
“Sawa nimekuelewa sana Munil. Lakini Munil huoni kama mimi kuweka fedha zote hizo benki naweza kuulizwa na serikali nimezitoa wapi?”
“Hakuna atakayekuuliza bwana, acha woga wako mume wangu.”
Siku hiyo tulilala wote na Munil mimi nikiwa kama mume wake kwa mara ya kwanza. Jambo moja ambalo lilinishangaza ni kwamba, wakati tunataka kulala baada ya kuongea kwa muda, nilimwambia Munil tuzime taa, akasema ataenda kuzima yeye.
Baada ya muda nilishtukia taa imezimwa lakini ninaamini hakuwa ametoka kitandani. Hiki kitendo ni cha pili kutokea kwake na kunishangaza.
“Ulikwenda kuzima taa?” nilimuuliza. “Ndiyo,” alinijibu huku nikijua si kweli.
***
Asubuhi na mapema, Munil ndiye aliyetangulia kutoka kitandani. Mimi nilipoamka nilimkuta ameshaoga na amevaa nguo nyingine, ni gauni refu jeusi. Nilimuuliza umetoa wapi hilo gauni, akanijibu alifuata nguo zake nyumbani kwake, yakaisha.
Ilikuwa wakati napiga mswaki nje kabisa, mama mwenye nyumba ambaye anaishi kwenye upande mwingine alinifuata hadi karibu akaniuliza:
“Huyo binti ni nani?”
“Mke wangu.”
“Umeoa lini?”
“Siku nyingi kidogo ila alikuwa kwao.”
“Kwao wapi?”
“Bagamoyo.”
“Uliwahi kufika?”
“Ndiyo, sasa ningeoaje kama ningekuwa sijafika kwa wazazi wake?”
“Sawa ila mimi nina”
Kabla hajamaliza kusema, Munil alitokea na yule mama mwenye nyumba akawa kama anaweweseka, kama anahisi kizunguzungu. Mara aniangalie kwa macho ya kulegea, mara amwangalie Munil na kumpa mkono kama anayemsalimia.
“Mama vipi kwani?” aliuliza Munil.
Lakini bado mama mwenye nyumba wangu akawa hasemi wala hafungui mdomo.
“Labda ana tatizo la ghafla, tumshike kichwani,” alisema Munil huku akifanya hivyo. Mara, mama akashtuka na kurudia katika hali yake ya kawaida, akaniangalia mimi, akamwangalia Munil kisha akasema anaomba msamaha kwa wote, akaondoka kurudi ndani kwake.
Munil aliniambia nipige mswaki haraka sana nirudi chumbani. Nikafanya hivyo.
“Hii nyumba tunatakiwa kuhama haraka sana mume wangu,” aliniambia.
“Kisa?”
“Si nzuri. Unajua huyu mama amekuwa akikuchezea siku nyingi sana. Kila unapolala anakuja kukukalia juu ya mwili wako. We hujagundua kuwa ukiamka asubuhi unakuwa umechoka sana?”
“Hilo ni kweli, ina maana yeye ndiyo kisa?”
“Haswa, ndiyo sababu. Mimi usiku wa kuamkia leo nimemtimulia mlangoni, alitaka kuingia. tena nimemwambia akirudia kitampata kitu kibaya zaidi.”
“Munil, kwani wewe ni mganga?”
“Aka! Mi si mganga ila huwa nasali sana kwa Mungu wangu.”
“Unanitisha Munil.”
“Usitishike bwana.”
Tulikunywa chai, tulipomaliza nilimwambia Munil nikatafute nyumba nzuri, akasema kwa siku hiyo nitapata nyumba nzuri sana lakini haipangishwi, nikamuuliza amejuaje, akasema anaamini hivyo.
Nilimbishia, nikaondoka. Lakini akasema nichukue kiasi cha dola nikabadili ili niweze kupata za kuweka
mfukoni. Hata sehemu ya kubadilishia nilikuwa sizijui kwa hiyo nilichofanya niliwauliza watu.
Kwa kiasi cha dola alizonipa Munil kwenye kubadili nilipata shilingi laki mbili. Eti ndiyo za kushika.
Niliwapata madalali, wakanipeleka kwenye nyumba nzuri sana. Waliniambia nisubiri wakaenda kuniitia mwenye nyumba ambaye alifika baada ya kama dakika ishirini na tano hivi. Alinichangamkia, akaniingiza ndani. Hakukuwa na mtu lakini kulikuwa na kila kitu kwa maisha ya binadamu, akasema watoto wake wapo shuleni, mkewe amekwenda kazini mjini Dar es Salaam.
Aliniingiza kila chumba, nikakubaliana naye kwamba ni nyumba nzuri, nimeipenda nitailipia maana ilikuwa na maegesho ya magari pia.Basi, wakati tunatoka yule mwenye nyumba akaingia chumbani na kubadili shati, akatoka akiniuliza nitalipia lini. Nilimwomba anipe nusu saa tu nifike nyumbani kwa mke wangu kuchukua pesa.
Nilimkuta Munil amelala chumbani akisema anahisi uchovu.
“Vipi kwenye nyumba mume wangu?” aliniuliza.
“Nimepata, tofauti na ulivyosema nitapata lakini haipangishwi.”
“Ni shilingi ngapi?”
“Kwa mwezi shilingi laki moja, vyumba vya kulala vitatu, sebule kubwa, stoo, choo, bafu. Kilichonifurahisha zaidi ni maegesho ya magari, wenyewe watahama baada ya sisi kulipa.”
Nikakumbuka kuwa, kumbe hata fedha niliyokuwa nayo ilitosha kulipia na kubaki salio zuri tu, nikamwambia nakwenda kulipia sasa, Munil akasema sawa lakini akaachia tabasamu.
Kufika, nilikuta mzee mmoja tofauti na yule anaingia ndani ya nyumba hiyo akiwa na mkewe. Alinikaribisha,akaniuliza shida yangu.
EPISODE 14
“Mzee mimi nimetokea kule juu, nilikuja awali hapa nikakutana na mwenye nyumba lengo ni kutaka kupanga nyumba hii, nilishafanya makubaliano naye, ila nilifuata pesa nyumbani.”
Nilishangaa mimi kusema hivyo halafu yule mzee akamtazama mke wake kisha akanigeukia mimi.
“Huyo mtu alikuingiza ndani?”
“Ndiyo, alinitembeza kila chumba akasema atahama baada ya mimi kumlipa.”
Wakati nayasema haya, kichwani nikaisikia sauti ya Munil ikisema…
“Utapata nyumba nzuri sana lakini haipangishwi.”
“Mimi ndiyo mwenye nyumba hii na sipangishi, huyo mtu uliyesema aliingiaje na unaona mimi ndiyo nafungua hapa!”
“Mimi sijui mzee, ila niliingia humu ndani kwako.”
Yule mzee alionekana kusinyaa kwa muda akiwa kama anayejiuliza ni nini kilitokea?
“Basi kijana umeliwa,” alimalizia kwa kusema hivyo huku akiingia ndani na mke wake.
Moyoni nilisema hata kama ni kweli nimeliwa, lakini mbona mzee mwenyewe hakuonesha kushtuka kwa kitendo cha mimi kuingizwa ndani mwake na mmiliki hewa yeye akiwa amefunga nyumba?
Niliona kuna mchezo. Niliondoka na miguu ya kunyong’onyea kurudi kwangu. Kwa mbali nilimuona Munil akikatiza mtaa. Nikajua alikuwa akitoka nyumbani kwenda mahali lakini yeye hakuniona.
Kufika nyumbani nilimkuta Munil amelala chumbani.
“Ha! Mke wangu, mbona kama nimekuona mahali unakatiza mtaa?”
“Mimi?” aliuliza kwa kushtuka Munil.”Wewe ndiyo, tena gauni hilohilo, nywele hivyohivyo ulivyo. Ni nini?”
“Utakuwa umeniona vibaya.”
Nilimueleza Munil kilichotokea kwenye nyumba akasema si nilikwambia mimi!
Nilimuaga Munil kwamba nakwenda kwa rafiki yangu mmoja maeneo ya stendi, akanikubalia.
Nilitoka nyumbani lakini badala ya kwenda kwa huyo rafiki yangu, mimi nilikwenda kwingine kabisa baada ya kughairi njiani.
Nilikwenda kukutana na msichana mmoja ambaye ilikuwa nifunge naye ndoa.
Niliingia kwake ambapo nilimkuta anakunywa chai. Alinipokea kwa furaha sana na kunikaribisha chai.
“Nimeshakunywa, nimeshiba sana.”
“Basi kaa,” aliniambia.
Ile nakaa tu, akaniambia.
“Nasikia umefunga ndoa Bagamoyo?”
“Mh! Nani kakuambia?” nilimuuliza kwa mshtuko mkubwa.
“Jamani, mbona siyo siri. Mimi nimeambiwa jana na Hawa, yule rafiki yangu halafu leo nikamsikia Rufina.”
“Siyo kweli bwana,” nilimficha.
Baada ya mazungumzo mafupi, mlango ukagongwa na sauti ya kike ikabisha hodi.
“Karibu, nani?” yule mwenyeji wangu alisema.
“Mimi.”
“Wewe nani sasa?” aliuliza mwenyeji huku akiuendea mlango. Alifungua huku mimi nikiwa namuangalia yeye nikiamini kwamba kama huyo aliyebisha hodi anamjua lazima uso wake utaonesha tabasamu.
“Khaa! Mbona hakuna mtu,” alisema akigeuka kuniangalia.
“Hakuna mtu? Au kaondoka?”
“Aondoke mara hii, kwenda njia gani? Maana hapa kwangu mtu akitokea kule unamuona hadi anapofika,” alisema huku akirudi kukaa na kufunga mlango.
“Hodi,” ile sauti ilibisha tena. Safari hii ikiwa kwa juu zaidi. Kidogo nilihisi kama sauti ninayoifahamu na kuizoea.
Safari hii yule mwenyeji wangu hakuitika, alisimama taratibu na kuufuata mlango akiwa anakaribia kushika kitasa kwa ndani, hodi nyingine ilibishwa.
“Hodii.”
Alifungua mlango haraka, lakini pia hakuona mtu.
“Jamani, si bure kuna kitu. Mbona hakuna mtu?”
“Hodiii.”
Safari hii sauti hiyo ilitokea mlango wa nyuma. Mwenyeji wangu akaenda, kabla hajafungua hodi ikapigwa usawa wa dirishani nilipokaa mimi, nikainuka haraka sana kuchungulia hakukuwa na mtu!
“Nahisi kuna kitu kinaendelea,” nilimuambia mwenyeji wangu.
“Ni kweli,” naye alisema huku akitetemeka.
“Au mimi nimekuja na balaa?”
“Sijui, utakuwa unajua mwenyewe.”
Tukiwa tunaongea hivyo, mara tukasikia sauti ya ajabu kutokea nje mlango mkubwa ikisema:
“Haya wee! Haya wee! Haya wee! Ihaaa! Haya we! Haya wee! Haya wee! Ihaaaaaaa.”
Nilisimama na kuaga kwamba naondoka kwa kupitia mlango wa nyuma. Cha ajabu sasa, niliposema tu mimi naondoka, napitia mlango wa nyuma sauti ya kicheko ilisikika mbele.
Nilitoka haraka sana na kutembea kwa kasi nilikiwa siangalii nyuma zaidi ya kulia na kushoto, nywele zilisisimka sana, damu mwilini ilikuwa ikitembea kwa kasi.
Niliamua kurudi nyumbani lakini sikupanga kumsimulia Munil kilichonipata.
Nilimkuta Munil amelala lakini aliponiona hakuonesha uchangamfu ninaojua na si kawaida yake tangu nianze kumfahamu.
“Baby, mbona kama huna raha?” nilimuuliza.
“Nipo kawaida mbona!”
“Hapana, hauko kawaida. Nakufahamu mke wangu.”
“Mume wangu,” aliniita.
“Naam.”
“Hebu kaa hapa,” aliniambia kisha nilipokaa akasema:
“Unadhani katika ndoa yetu kuna siku utanisaliti?”
EPISODE 15
“Haitatokea Munil, nakupenda sana.”
“Kweli!” Naamini uliwahi kuwa na wanawake kabla yangu! Je, unaweza kuachana nao?”
Alivyosema hivyo tu, nikajua Munil alijua nilikwenda kwa mwanamke wangu wa mwanzo ndiyo maana akawa hana raha na kuniambia maneno hayo ya kuniapiza.
“Naweza mke wangu.”
“Basi naomba ufanye hivyo kuanza leo hii.”
“Nimekuelewa mke wangu.”
Hapo ndipo nikamwona Munil akichangamka kwa mbali. Lakini na mimi dhamira yangu ikanisuta sana. Sasa nikayarejesha mawazo kwa yule mwanamke nilikokwenda, kwamba yale maajabu yalikuwa ni nini!
***
Ilikuwa ni usiku wa kama saa tisa hivi, nilishtuka kutoka usingizini, nikahisi kama kitandani niko peke yangu. Nilipeleka mkono upande aliolala Munil kweli nikabaini nilikuwa peke yangu.
Nikiwa nawaza atakuwa amekwenda wapi? Chooni, mara nikasikia mlio nje ya dirisha.
“Haya weee! Haya wee! Haya wee! Ihaaaa! Haya we! Haya weee! Haya wee! Ihaaaaaaa!”
Nilikurupuka kitandani kutaka kukimbia lakini Munil akanishika mkono palepale kitandani na kunirudisha kulala.
“Nini kwani mume wangu?”
“Kuna sauti za ajabu dirishani,” nilisema.
“Zikitokea wapi? Mbona mimi sizisikii?”
“Kutokea nje mke wangu halafu hizo sauti kama nimewahi kuzisikia mahali.”
“Mahali gani?”
“Sikumbuki. Lakini pia Munil hukuwepo kitandani wewe mke wangu!”
“Sasa kama sikuwepo kitandani nilikuwa wapi mume wangu?”
“Mbona nilipapasa sana hukuwepo?”
“Ulipapasa vibaya,” alisema Munil kwa sauti iliyoashiria kwamba hakuwa amelala kwa muda mrefu. Yaani si kwamba alitoka kuamka kama mimi.
Wakati tunaongea hayo, kulikuwa giza. Nilimjua ni Munil kwa sababu ya sauti tu na si kumwona sura.
“Sasa kama mume wangu wewe ndiyo unakuwa mwoga mimi itakuaje?”
“Wewe umesema hujazisikia hizo sauti kwa hiyo huwezi kuogopa kitu,” nilimjibu Munil. Akaniomba tulale na kuachana na mambo hayo.Kweli, ndani ya dakika kama tano labda nilipitiwa na usingizi mzito. Lakini kwenye saa kumi na moja nikashtuka na kukuta taa inawaka, Munil hayupo kitandani.
Nilijua ametoka kwenda uani kwa sababu kulianza kukucha.
Ilipita nusu saa, Munil alikuwa hajarudi. Nikatoka kitandani kumfuata. Nilifika chooni hakuwepo, bafuni hakuwepo, nilipotaka kutoka nje niliachana na wazo hilo kwa sababu niliona mlango wenyewe ulifungwa kwa vitasa vya ndani.
Nilishangaa hali hiyo. Nikajiuliza Munil anaweza kuwa wapi kama huko hakuwepo?
Nilirudi chumbani, ile naingia tu, nilimkuta Munil amelala chali kitandani akiangalia godoro.
“Munil,” niliita kwa mshtuko.
“Vipi, ulikwenda chooni?”
“Noo! Munil hunitendei haki. Mimi ni mume wako lakini wewe una vitu vyako unafanya kwa siri.”
“Kama vitu gani na kwa nini umeniambia hivyo?”
“Ulikuwa wapi Munil?”
“Kha! Kwani wewe umeniacha wapi?”
“Hukuwepo kitandani Munil.”
“Nilikuwepo, sasa ningetoka kwenda wapi?”
Sikuendelea na Munil, nilipanda kitandani kulala. Lakini sikupitiwa na usingizi tena. Wakati najiulizauliza kuhusu Munil, nikasikia taa ikizima tap! Nilichungulia kwa mbali na kubaini kwamba taa ilizima ndiyo lakini mzimaji ambaye naamini alikuwa Munil hakutoka kitandani kuifuata swichi ukutani.
“Unajua mume wangu sijui una matatizo gani, sijui nikupeleke kwa mganga wa kienyeji? Umekuwa mtu wa kuweweseka sana kuliko kawaida.”
“Mimi nahisi wewe una mambo ya maajabu sana. Si useme tujue moja.”
“Kama lipi mojawapo?”
“Hilo la kutokatoka halafu baadaye unasema eti ulikuwepo kitandani wakati mimi nimejua kitandani hakuna mtu.Eti Munil alikuja juu akidai nimemdhalilisha sana kwa kule kumwambia ana mambo yake ya ajabuajabu, aseme nijue moja.
“Unajua unamkasirisha na kumfedhehesha ambaye wewe humjui.”
“Kama nani zaidi ya baba yako na mama yako?”
Munil alicheka kicheko cha kejeli huku akionekana kama nasema nisichokijua.
“Unacheka nini sasa?”
“Sijacheka,” alisema akikaa kitandani. Uso wake ulikabiliana na mimi ana kwa ana, kidogo nikashtuka kwani nilimwona amekuwa na sura kama ya paka mweusi tiii!
“Haa! Munil,” nilihamaki.
Halafu yeye kwa upole akasema
“Natamani nihame hapa kwa muda lakini nitashindwa kwa sababu ya wewe mume wangu.”
“Uhame kwa sababu gani mke wangu?”
“Naamini uchawi wa huyo mama mwenyewe nyumba unakusumbua hadi sasa.
“Haniwezi yule hata iweje!”Nilihisi Munil anataka kukwepana na ukweli na kuhamisha mada kwa kuitumbukiza ya kwake.
EPISODE 16
“Mimi sisumbuliwi mke wangu ila nasema kwa ukweli kabisa kwamba huwa sikuelewi.”
“Mbona mimi ni salama sana mume wangu kwa nini jamani ushindwe kunielewa mimi?”
“Ina maana mimi sina akili sana kichwani mwangu au?”
“Unazo, ila nahisi unachanganyikiwa.”
Nakumbuka siku hiyo mvua ilinyesha sana kiasi kwamba mtu akitoka nje kuingia ndani lazima ajifute au asipojifuta aweke alama za miguu yenye matope.
Nilitoka kwenda kuoga ndipo nikakutana na kisa kingine cha ajabu na cha kutisha sana. Kule bafuni nilikuta alama za miguu ya ng’ombe, yaani kwato. Nikakumbuka kwamba siku moja niliwahi kusikia
kuhusu mwanamke kama ni jini anaweza kujibadilisha sehemu zote za mwili kasoro miguu tu kwamba lazima iwe kwato za ng’ombe.
Niliziangalia zile alama nikagundua baada ya kutoka bafuni zilitoka kwenda chumbani. Nilizifuata hadi zikawa zinapotelea jirani na mlango. Wakati nashangaa, Munil alifungua mlango kama vile mtu aliyesikia dalili za mtu kutembea.
Tulikutana uso kwa uso, mwenzangu alionekana amekasirika sana.
“Vipi?” aliniuliza.”Poa,” nilimjibu huku macho yangu yakikimbilia kwenye miguu yake lakini gauni refu alilovaa halikutoa nafasi ya mimi kumwona miguu yake.
Pale ndipo nilipobaini kwamba, tangu nimeanza kumjua Munil sijawahi kumwona miguu yake wala kujua anapenda viatu vya aina gani! Hilo lilkuwa halina ubishi. Hata nguo zilizokuwemo ndani ni nyingi lakini hakuwa na viatu, nikasema moyoni nitamuuliza baadaye sana.
Ghafla nilihisi joto la ajabu, mwili uliishiwa nguvu nikaanguka. Watu warefu, waliovalia nguo nyeupe wakiwa na mapembe mawili kichwani, kasoro mmoja tu alikuwa na pembe moja kwenye paji la uso walisimama pembeni yangu, wakainama na kunishika mkono kama wanataka kuniamsha.
Nilikataa, wakaniamsha kwa nguvu huku wakicheka. Walinibeba juu kwa juu hadi ufukweni na kunitishia kunitosa ndani ya bahari. Nilipopiga kelele walicheka kwa furaha lakini pia hawakuniacha, wakanirusha majini.
Nilisema mama nakufaa huku nikiwa hewani kwenda majini, akatokea Munil na kunidaka. Nikafurahi sana kugundua ni yeye.
“Huwezi kufa mume wangu wakati mimi mkeo nipo,” alisema Munil kwa sauti tamu kama mwanamke.
“Je, ikitokea ukatangulia kufa wewe hawa watu si wataniua mke wangu?” nilimwambia.
“Haitatokea mimi nikafa kabla yako wala mimi kufa. Mimi nipo tu mume wangu.”
“Una maana gani?”
“Mimi bado sana si wa kufa leo wale kesho.”
“Nimekuelwa sana lakini una maana gani kusema hivyo?”
“Mimi ni jini!”
Nilishtuka, nikajikuta nimelala kitandani huku Munil akinipungia kunipepea na feni ikipuliza kwa sana ili nipate hewa.”Pole sana,” aliniambia.
“Asante kwani ilikuaje Munil?”
“Ulianguka ghafla.”
“Halafu?”
“Nikakubeba kukuingiza chumbani.”
“Halafu?” “Halafu nini sasa si ndiyo umeshtuka sana hivi.”
“Mbona nilibebwa na watu wakaenda kunitupa baharini?”
“Halafu?”
“Halafu wewe ukanidaka.”
“Halafu?”
“Halafu ukasema wewe hutakufa, nitaanza kufa mimi nikakuuliza sababu ukasema sababu wewe ni jini, ni kweli mke wangu?”
“Ni kweli kwamba?”
“Wewe ni jini?”
“Hivi mume wangu ningekuwa jini ungeweza kuishi na mimi? Kuna binadamu amewahi kuishi na jini chumba kimoja, kitandani kimoja? Hebu kaulize wenzako watakwambia kama iliwahi kutokea.”
Nilipowaza sana nikaamini ikwamba wapo watu niliwahi kuwasikia wakisema kwamba binadamu anapokutana na jini anauguza au anapatwa maradhi ya ajabu, sasa iweje mimi niwe nalala naye kabisa halafu niendelee kuwa hai, si ningekufa?
Niliachana na mawazo hayo, Munil alionekana kuufuatilia sana uso wangu ili kujua unaongea nini lakini sijui aliuonaje, akaniuliza:
“Vipi kwa sasa, uko swa?”
“Niko sawa mke wangu.”
“Basi na wewe usiwe unaniwazia sana jamani,” alisema Munil huku akunisogelea na kunibusu. Mwili wangu ulisisimka, nikamwambia, akaniuliza nataka nini?
“Ah! Swali gani hilo mke wangu?”
Munil alivutia kwake akaniweka kwenye kifua na kuniletea kinywa chake, akatoa ulimi akiashiria kwamba na mimi nimpe wa kwangu Nilitoa ulimi, nikauingiza kwenye kinywa cha Munil, ukatalii humo kwa dakika kadhaa, nikamwona Munil akianza kunung’unika kimahaba.
Nilisema moyoni kwamba nitumie nafasi ile ya kukutana naye kimwili ili kubaini Munil alikuwa na miguu ya aina gani! Ni kweli ya kwato za ng’ombe au la!Huo ulikuwa usiku sasa na wakati nawaza hayo nikasikia taa! Giza!
“Umezima taa Munil?” nilimuuliza kwa mshtuko mkubwa maana ilipo swichi ya taa na kitandani tulipokuwepo sisi ni mbali, ni lazima mtu atoke kabisa kitandani kuifuata swichi.
“Nimezima mimi ndiyo.”
“Umezimaje?”
“Nilikwenda.”
“Siyo kweli, Munil usinifanye mimi ni mtoto mdogo aisee.”
Je, nini kiliendelea?