NAJIONA KABISA NISHAKUWA SINGLE MOTHER, NA SIKUWAHI KUFIKIRIA
Habari ya mchana kaka Spesho, please hide my name, Naomba nipewe ushauri labda nitapata amani ya Moyo maana naona kama dunia imenilemea sina furaha tena na haya maisha.
Ni hivi nilikutana na mume wangu nikiwa binti mdogo kabisa wa miaka 22, kwa wakati huo tuliishi kama wapenzi tu, mwaka 2017 tulitambulishana kwa wazazi wote wa pande zote na alinilipia mahali ingawa tayari alikuwa na mtoto mmoja ambaya alizaa na mwanamke mwingine ambaye aliachana naye na alishaolewa,baada ya hapo tulianza kuishi pamoja kama mke na mume.
Mimi ni mtumishi wa serikari na mume wangu yeye ni mfanyabihashara. Maisha yetu kwa kweli yalikuwa mazuri sana na yenye upendo na tulifanikiwa kujenga nyumba, kununua Mashamba , gari na tulijenga kibanda cha bihashara na kununua Kiwanja Dodoma, na aliamua kumchukua mtoto wake tuishi nae kwa wakati ule alikuwa na umri wa miaka minne.
Changamoto ilianza pale nilipojifungua mtoto wangu wa kwanza mwaka 2018 mume wangu alianza kunidharau na kutonithamini kama mkewe, kumbe alikuwa na mahusiano na wanawake wengine wa nje ambao miongoni mwao alizaa nao pia, nilivumilia Sana kwa kuwa ndoa ni uvumilivu.
Lakini mume wangu aliendelea kunidharau Sana na ilifika hatua hanishirikishi kitu chochote kile kinachohusu maendeleo zaidi ya ndugu zake alikuwa anawapeleka na kuwaonyesha miradi yake yote anayoifanya kwani alijenga nyumba mbili za kupangisha, pia Dodoma alijenga nyumba bila kunishirikisha ilifika hatua nikimuuliza kwa nini unafanya hivi “ananijibu kuwa kwani unakosa kitu gani humu ndani”
Kiukweli nilikuwa naumia Sana Ila nilivumilia na mwaka 2022 nilizaa mtoto wangu wa pili lakini Changamoto zilikuwa ni zaidi ya ile ya kwanza, kwani alikuwa anasafiri hata siku tatu haagi anaenda wapi? na atarudi lini, ukimuuliza anakuambia acha geti wazi nikirudi niingie, akiondoka asubui anarudi usiku akiwa amevaa nguo zingine tofauti na alizovaa asubui na zote ni zake, , nyie mateso yalikuwa ni mengi kwani ilifika hatua hatoi hela ya matumizi yoyote yale na akirudi anakuambia akute chakula, mnalala chumba kimoja lakini hamshiriki tendo la ndoa zaidi ya Mwaka pia ugomvi wetu lazima awashirikishe ndugu zake yaani ilifika hatua nachukiwa na ndugu zake, huku akipelekewa maneno ya kuwa namtesa na kumnyanyasa mtoto wake na ilifika hatua alimwamisha mtoto wake na kumpeleka kwa ndugu zake na sababu kubwa ni kwa nini afanye kazi za nyumbani wakati binti wa kazi yupo, na yeye mtoto wake ni wa kike, ukirudi kazini binti wa kazi anakuelezea kila kitu jinsi alivyofokewa na shemeji yake kuhusu mtoto wake kama amemkuta anaosha vyombo, ila niliendelea kuvumilia kwani ilifika hatua alikuwa ananipiga Sana na kuniambia nikitaka kuondoka niondoke tu, Mimi sitakuwa wa kwanza kuondoka kwake na hii ilitokana kuwa mkifanya sherehe yoyote ile anawaalikwa wanawake wake wote aliozaa nao na hawala zake ambao wanafahamika kwa ndugu zake na rafiki zake, anawaleta nyumbani kwangu yaani nilikuwa naumia sana, niliumwa nyongo isiyoisha.
Nilihama chumba na kuamia chumba cha watoto na nilijaribu kuwashirikisha mshenga na baadhi ya wazee ambao walijaribu kumsema lakini hakusikia kitu chochote kile na hatukufikia muafaka wowote ule, zaidi ya kuendelea kunyanyasika na na kugombana kila siku, kiufupi nyumba haikuwa na amani hata kidogo na ilifika muda alianza mahusiano na wafanyakazi wenzangu ambapo ugomvi uliendelea hadi kazini kwangu.
Ndipo mwaka 2023 nilipoomba kutoka nyumbani kwangu ili nikapumzike na ndipo nilipoamua kuondoka na kwenda kupanga nyumba mtaa wa pili. Baada ya hapo mume wangu hajawahi kunitafuta hata kuulizia hali ya watoto, hajui watoto wake wanakula nini, hajui hata ada za watoto zinalipwaje, nimejaribu kuongea nae hadi nimeshindwa, ila watoto wanampenda Sana baba yao na kila siku wanamuulizia na kuniambia mpigie simu baba tuongee nae, ila cha ajabu baba yao hataki hata kupokea simu zangu na yupo hapahapa tunapoishi ila hana muda kabisa, inafika hatua wanalia wanamtaka baba yao.
Jamani mnipe tu hata mawazo nifanyaje kurudi kwangu siwezi naogopa yale mateso na najiona kabisa nishakuwa single mother na sikuwahi kabisa kufikiria kama nitakuja kuishi maisha haya, na je napataje haki zangu za msingi kwa kile nilichokichangia wakati tunatafuta na kuishi pamoja. Au nihame tu Mkoa nikatafute maisha mengine huko kwingine?! Ila kinachoniumiza kwa nini hataki hata kuudumia watoto wake? Hali ya kuwa kipato anacho cha kutosha?

