JINSI UKIMYA ULIVYONIPA NDOA
PART 6
Mahusiano yetu yakaanza, kwa nguvu sana. Japo yalikuwa ya siri hakuna Mtu aliyekuwa anajua Zaidi yetu. Huyu kaka alinihakikishia kwamba ananipenda sana na yuko tayari kunioa. Kweli nami nikakubali na nikawa na amani moyoni sana tu.
Niwape umbea wa huku upande wa pili kidogo, bwana yule jamaa fundi simu baada ya Joyce kujifungua si akapotea, akawa hahudumii Mtoto wala Mama Mtoto. Na waligombana Joyce akarudi nyumbani kisa alimfumania jamaa na Mwanamke mwingine. Nasikia ugomvi ulikuwa mkubwa mpaka Mama yani Mama Joyce akaanza kumpigia simu yule mwanamke ambaye anatembea na huyu fundi simu, wakawa wanamtisha sijui aachane nae watamfanyia kitu kibaya. Fundi simu akapata taarifa akamuwakia Joyce balaa na akamwambia sikutaki kwanza ulinilazimisha kulala na Wewe.
Ugomvi ukawa mkubwa mpaka jamaa akapelekwa Serikali za mitaa kudaiwa matunzo, mpaka ustawi wa jamii. Mambo yalikuwa moto. Mama Mtu analazimisha jamaa kwakuwa kamzalisha mwanaye basi amuoe au aishi nae. Jamaa anasema hawezi kuishi nae kwani sio mwanamke wa type yake. Alitoa sababu nyingi ikiwemo ujeuri, uvivu, uchafu akasema sitaki siwezi. Nitalea Mtoto wangu ila Mama Mtu awe huru tu Mtoto akikua anipe Mtoto wangu akaolewe.
Mimi nikawa nimetulia tu nasikiliza ubuyu kwa mbali, maana mambo yalikuwa makubwa mpaka Joyce akataka kunywa sumu jamani mweeeh. Nikasema kwakweli Mungu amsaidie, alikuwa na hali mbaya sana.
Haya turudi kwenye yangu maana umbea huu nisije kusutwa 😀😀.
Huyu mchumba mpya akanipeleka kunitambulisha kwa baadhi ya ndugu zake walioko hapa Dar, na ni kweli walinipenda na tukawa karibu, tunawasiliana. Hata kukiwa na event yoyote kwenye familia yao ninaenda na kila Mtu alikuwa anajua kuwa Mimi ndio mchumba wa Eben na soon tutafunga ndoa.
Usitake kujua furaha na amani niliyokuwa nayo, nilikuwa na amani isiyo na kifani, yani acheni tu, niliona mambo yangu yamenyooka hivi 👉👉 kwenye mstari. Nikaanza kujiandaa kuwa Mke wa Mtu yani nikawa najinunulia kanga, vitenge, nguo nzuri, vyombo ili angalau nikiolewa mambo yawe supa.
Kuna siku Eben akaniomba twende kwa Mchungaji, akasema nataka twende kwa Mchungaji tupate Baraka zake ili mwezi ujao nikupeleke kwetu kwa wazazi wangu kukutambulisha ili mambo mengine ya endelee. Kwani wazazi wanadai nioe sasa. Kweli nikakubali na nikafurahi sana. Siku hiyo Eben akampigia Mchungaji akamwambia twende atakuwepo. Basi nikajiandaa vizuri tu, huyo mpaka kwa Mchungaji.
Tukafika kule Mchungaji alifurahi sana, alikuwa pamoja na Mama Mchungaji, wote walifurahi. Eben akawaeleza nia yake na mpango wake, Mchungaji akasema Mimi sina pingamizi basi endeleeni na michakato ya familia mkimaliza mtakuja na sisi kama kanisani tutafanya michakato yetu. Akatuombea na kumshukuru Mungu. Basi tulitoka pale tukiwa na furaha. Na Mchungaji na Mama Mchungaji walifurahi sana, hasa Mama Mchungaji akasema yani natamani sana Mwanangu Bite aolewe natamani sana nitafurahi sana.
Bwana Bwana sikujua Mimi kumbe pale kanisani kulikuwa na mabinti wengine ambao wamempenda kijana na kuna baadhi walishaonyeshwa kwenye ndoto kwamba atakuwa mume wao. Kuna binti alishaenda hadi kwa Mama Mchungaji kumwambia kuwa Mungu kamuonyesha kuwa Eben ndio Mumewe na walikuwa wanawasiliana kawaida sio ya kimapenzi.
Sasa Mama Mchungaji, kuna siku alikaa na baadhi ya viongozi wa kanisa, akawagusia kwamba kijana wetu Eben anataka kuoa, amemleta Binti yetu Bite amesema anamuoa Bite, wazee wa kanisa walifurahi, japo kuna Mama mmoja Mzee wa kanisa ambaye Binti yake ndio alionyeshwa na kuoteshwa kuwa Eben atakuwa Mumewe hakupenda, na alichukia.
Sina hili wala lile yule Mama mzee wa kanisa Alimtafuta Eben kuongea nae, sijui alimwambia nini lakini alimshawishi sana amuoe binti yake kwani ni msomi sijui, ana kazi ya maana. Eben akaja kuniambia ila hakuonyesha kujali, akasema nimeachana nao Mimi nakuoa Wewe Bite wewe ndio chaguo langu.
Baada ya muda nikashangaa mawasiliano ya Eben na yule binti yameongezeka. Wanapigiana simu, wanachat. Mara yule Binti anamletea zawadi Eben. Mimi nipo tu nikumuuliza anasema is just a Friend. Ikawa jumapili baada ya Ibada utakuta Eben anaenda kuongea na yule Mama Mzee wa kanisa na Mumewe na walikuwa matajiri, basi wataongea pale kama watu wanao fahamiana sana. Wakaanza kuwa karibu sana mpaka Eben akawa anaendesha gari la yule Baba siku zingine.
Baada ya muda nikaona Eben amekata mawasiliano na Mimi kabisaaa. Nikipiga hapokei, hanisalimii yani kimya kimya, kanisani ananichunia haniongeleshi basi ikawa hivyo.
PART 7
Mambo yakaanza kubadilika, mambo yakaanza kuwa meusi, vitu havieleweki. Eben kabadilika, hayupo tena vile romantic alivyokuwa, akawa Mtu wa ajabu kabisa. Hii iliniumiza sana.
Kama kawaida yangu Mimi ni Mtu wa kumbembeleza sana watu, nikaanza kumpigia simu, namtumia message namwambia Eben nakupenda, siwezi ishi bila wewe Eben, please nakuomba usiniache, usiniache Eben. Nakwambia hakujibu chochote akawa yupo kimyaa tu, message anazisoma ila hajibu.
Nikawa nikienda ibadani nakutana nae hanisalimii, hata nikimsalimia haitiki, nimejitahidi sana ila alikuwa ananionyesha dharau tu, na kuna muda anajifanya kama hanijui au hataki nimsemeshe.
Kuna siku niliumia sana, ilikuwa tumemaliza ibada, nikaamua kumfwata kumsalimia na angalau nimuulize nini shida. Ila aliponiona nakuja kwake akanyanyuka akaondoka, nikajaribu kumwita hakuitika. Nikaamua kumfwata lakini akawa ananikwepa. Baadae namuona ana washa gari anaingia huku yule binti na kaka yake wanapanda kwenye hiyo gari wakaondoka. Ni gari ya Baba yake Binti hivyo design kama alipewa awaendeshe kuwaleta kanisani. Naona akaona akiongea na Mimi nitamuharibia. Basi nikasimama naangalia gari linavyotoka na kuondoka. Nilijisikia vibaya sana,
Nilishindwa kujizuia ikabidi nimfwate mwalimu wangu wa kwaya kumueleza huku nalia, maana nisingeweza kurudi nyumbani vile.
Nikamwambia mwalimu kuna hili swala linaniumiza. Kuna kijana niko nae kwenye mahusiano na ameshanitambulisha kwa Mchungaji lakini amebadilika, ghafla tu haongei na Mimi tena, hapokei simu zangu wala kujibu message. Mwalimu akaniuliza kijana yupi huyo?, nikamwambia Eben. Mwalimu akasema aisee mbona huyu kijana anatoka na binti fulani ndio mchumba wake, nikamuuliza Binti gani, akasema yule Mtoto wa Mzee wa kanisa. Akasema hata juzi kuna mahali nimewakuta wakaniambia wako kwenye mahusiano na wanataka kufunga Ndoa. Nikamwambia mwalimu sasa nafanyaje na ninampenda.
Mwalimu akasema pale achana napo naona hela inatembea, ameamua kuoa mwenye hela mwenzie, wewe tulia tu utaumia. Akasema yule binti anatumia hela nyingi sana kwa Eben, anampa vitu vya thamani na gharama ili kumshawishi, na Eben kachanganyikiwa na hivyo vitu, achana nae. Daaah niliumia sana nikamwambia mwalimu niombee nina wakati Mgumu sana. Mwalimu akasema nakuelewa ila achana nae. Nikalia sana pale, baadae nikaamua kuondoka.
Basi nikawa mnyonge sana, sijui cha kufanya, sina wa kumwambia, nikaamua kurudi nyumbani. Usiku ule sikulala nililia sana sana sana. Kuna Dada yangu mmoja nafanya nae kazi alinipigia simu akanikuta ninalia, akauliza vipi Bite mbona hauko sawa. Nikaamua kumuelezea story nzima. Alisikitika sana, akasema hapa unahitaji msaada. Akasema hembu ngoja nakupigia muda si mrefu.
Akaniuliza hivi unamjua Pastor Anni, nikamwambia hapana, akasema aisee Mimi amenisaidia kwenye mambo mengi hasa Ndoa yangu, na wiki ijayo jumapili nimepanga niende kanisani kwake, akaniambia jipange jumapili tukamuone Pastor Anni, nauhakika atakusaidia, utavuka. Nikamwambia sawa
Basi wiki iliyofuata nilikuwa mnyonge sana, nikashindwa kwenda kabisa Ibadani. Nikamtumia message mwalimu wangu wa kwaya nikamwambia wiki hii ninadharula sitaweza kufika ibadani, akasema sawa.
Nikaendelea na kazi, huku najiandaa jumapili nionane na huyo Pastor Anni
PART 8
Ilikuwa jumamosi nimeamka moyo unauma sana, sikuwa na raha kabisa. Ndani yangu kuna sauti ikawa inaniambia utaweza kweli kuvumilia hii aibu, yani Eben aoe huku unaona hapana, bora ujiue tu, jiue. Wazo la kujiua likaja kwa nguvu sana, nikawa najiuliza najiuweje, nitumie njia gani nijiue.
Nikiwa kwenye kutafakari simu yangu ikaita, ni yule Dada wa kazini alikuwa ananipigia. Nikapokea huku nikiwa nalia. Akaniuliza Bite vipi, nikamwambia Dada nimechoka naona bora nife naumia Dada, akanijibu hapana Bite achana na hayo mambo, amka anza kujiandaa kesho tukamuone Pastor Anni nimeshamwambia namleta mdogo wangu. Nikamwambia sawa Dada asante.
Niwe mkweli ile simu iliniokoa, kwani baada tu ya kupokea na kuongea na yule Dada mawazo ya kujiua yakakata. Nikajikuta naanza kulia tu. Nilikumbuka mbali sana jinsi nilivyoishi maisha ya shida, kukataliwa na kuteseka, nikamkumbuka Mama yangu mambo aliyoyapitia kwenye maisha yake nikaanza kulia kwa uchungu sana, nililia sana. Nakumbuka siku hiyo siku toka nje, sikula nilikuwa tu kitandani nalia basi mpaka jioni inafika niko tu ndani.
Basi usiku nikajiambia acha nijiandae kwaajili ya ibada kesho kwa Pastor Anni. Nikaandaa nguo nikaweka kila kitu vizuri, nilipomaliza nikala nikalala. Asubuhi yule Dada alinipigia akasema tukutane stand ili twende pamoja. Basi nikajiandaa nikatoka huyo mpaka kituoni.
Tulifika ibadani, ibada ilikuwa nzuri sana, tuliomba sana sana ibadani mpaka nikapata amani. Baadae nikaenda ofisini kuonana na Pastor Anni, tukaanza kuongea. Pastor alifurahi sana kuniona, na kitu kilichonishangaza ni hiki Pastor kuniona tu akaniambia “YOU ARE SO BEAUTIFUL BITE, YANI UNA NGOZI NZURI YA KITAJIRI, UNA SHAPE NZURI AISEE UKO KAMA MISS TANZANIA” Haya maneno yalinigusa sana kwani sijawahi kuambiwa maneno haya, hakuna aliyewahi kuniambia kama Mimi ni mzuri hakuna, nimezoea kusikia maneno kama Wewe mbaya, una laana, hautokaa uolewa ðŸ˜ðŸ˜, hayo maneno ndio niliyozoea kusikia. Nikaanza kulia nikamwambia Pastor asante, Pastor akanikumbatia akaanza kuniombea.
Baadae akasema tukae basi tuongee, akaniambia niambie nini shida mrembo wangu. Nikaanza kumhadithia Pastor maisha yangu tangu mwanzo,
Jinsi Mama yangu alivyoachwa na Baba, tukaenda kukaa kwa Bibi,
Baadae Baba kunichukua na kunipeleka kwake, nikaanza kuishi na Mama wa kambo,
Mateso ya Mama wa kambo,
Kusoma, kifeli mitihani na Baba kunisusa,
Kusomea ufundi, kupata kazi,
Kupata mchumba kunitambulisha kwa wazazi na baadae mchumba kuniacha, na kutembea na Dada yangu hadi kumpa mimba.
Nilipofika hapo Pastor akasema Aisee Bite unabahati sana, yani umepitia mambo mengi makubwa na magumu ukiwa mdogo, niseme tu mbele hautakuwa na shida kwani hakutakuwa na jipya kwako.
Nikaanza kumpa sasa Story ya sasa ya Eben, alivyoniacha ghafla na kutaka kumuoa Binti mwingine pale pale kanisani, nikamwambia Pastor hili siwezi kulibabe naomba unisaidie. Yani mtu kanipeleka mpaka kwa Mchungaji halafu ghafla anakuacha kweli Pastor ðŸ˜ðŸ˜, nina weka wapi sura yangu, kama alikuwa hana mpango na Mimi kwanini aniaminishe hivi.
Pastor akasema sawa nimekuelewa mwanangu, sasa nisikilize, tena tulia unisikilize unielewe.
Akasema, unajua maisha ni safari ambayo imejawa na mambo mengi sana mazuri na mabaya. Lakini kwenye hii safari kuna hatma ambayo lazima itimie. Bila kujali changamoto, maumivu, aibu, unatakiwa upambane kuhakikisha hatma yako inatimia kwa gharama yoyote ile. Akasema hata siku moja usiishie njiani mwanangu never.
Pastor akasema ili hatma yako itimie ni lazima ujifunze kubadilika ili uendane na watu na mazingira. Kuna muda utahitajika kuwa so humble, basi kubali kushuka, kuna muda utahitajika kuwa mkali basi kuwa mkali, kuna muda utahitajika kujitenga basi jitenge, jifunze kwenda na mazingira.
Pastor akasema katika safari ya kutimiza Hatma zetu lazima tuwe makini sana na watu wa kwenda nao, kuna watu wa kuwashika na kuwang’ang’ania na kuna watu wa kuwaacha.
Pastor akasema mtu kama Eben aisee sio Mtu wa kumng’ang’ania, ni wa kumuacha. Eben ni wale watu wanaoongozwa na njaa na tamaa. Mtu kama huyu hupaswi kumuamini kwani yeye haongizwi na hisia au Upendo anaongozwa na njaa. Imagine mwanaume mwenye akili timamu anakuwaje driver wa Baba Mkwe mtarajiwa, anaendeshaje gari la ukweni wakati hata kuoa bado.
Pastor akasema Mshukuru Mungu huyo Eben kakuacha mapema kwani mngeweza kufunga Ndoa na angekuacha kwenye Ndoa, ingekuwa mbaya zaidi. Mwanaume asiye na msimamo wala maamuzi thabiti kwenye haya maisha ni wa kutupa mbali hafai kuwa nae karibu.
Nikwambie tu Eben hakufai, na nikwambie tu Eben si lolote si chochote, ni wa kawaida sana sana. Kwanza hana hadhi ya kuwa na Mwanamke mrembo kama Wewe. Wewe ni wa thamani sana mwanangu, unastahili kilicho Bora.
PASTOR AKASEMA NI JAMBO MOJA KUIJUA THAMANI YAKO LAKINI NI JAMBO LINGINE KUWAONYESHA WATU THAMANI YAKO.
WATU INABIDI WAIONE THAMANI YAKO KUPITIA WEWE MWENYEWE NA SI MTU MWINGINE
“JIFUNZE KUIONYESHA THAMANI YAKO”
PART 9
Pastor akaniambia Bite hivi unajua Wewe ni mwanamke wa thamani sana, yani Wewe ni Mtu muhimu sana kwenye jamii. Imagine unafanya kazi, umepanga unajilipia kodi, unajilisha bila kusaidiwa na Mtu, hauna Bwana wala nini unamudu mahitaji yako mwenyewe. Akasema bado unao uwezo wa kumsaidia Mama yako na Bibi kwa kuwapa mahitaji yao kila mwezi, hiyo ni sababu tosha ya kusema Wewe umebarikiwa. Ila tatizo lako wewe mwenyewe huoni kama umebarikiwa ndio maana upo upo unaruhusu watu wakudharau, wakukanyage na kukufanya wanavyotaka.
Pastor akasema wewe hujakosa Mwanaume wa maana wa kukuoa ila umejiweka kwenye viwango vya chini sana kiasi kwamba wanaokuja kwako ni watu wasio jielewa na wanakuchukulia vile wewe ulivyojiweka na wanakudharau. Inua viwango vyako, usiishi shida zako au historia yako, kuwa Binti unaejiamini na kujithamini, nakwambia tuone kama kuna mtu atakudharau.
Nikamwambia Pastor naomba unisaidie natokaje hapa, na nalihandle vipi hili swala. Au nihame kanisa. Pastor akasema hapana hakuna kuhama kanisa Kwasasa, tunakomaa nao pale pale ila fanya hivi.
Pastor akasema kwanza kubali kwamba umeachwa na Eben hakutaki tena, hilo likubali tu, kwamba Eben sio wako tena, na muache aende, muache apite kama wengine walivyopita. Na funga ukurasa wake kwenye maisha yako.
Pili msamehe Eben hakikisha hauna kinyongo nae kabisa, omba Mungu akupe Neema ya kusamehe na kumuachilia. Umtoe moyoni mwako na umuachilie kabisa na ifike wakati hata ukimuona Moyo wako uwe Mweupe tu wala hustuki. Kwani Moyo wako unahitaji kuwa wazi ili tuweze kumpokea na kumuweka Mume wetu ajae ambae Mungu atatupa.
Tatu badilisha mfumo wa maisha, anza kuwa binti wa viwango. Anza kufurahia maisha yako, yani kifupi jipe raha mwenyewe. Jinunulie nguo nzuri, viatu, perfume anza kupendeza na kunukia, kiufupi anza kuishi.
Nne akasema nataka uwe muombaji. Pastor akasema kila baya linalotupata limeanzia kwenye ulimwengu wa roho. Upo mlango kwenye ulimwengu wa roho unao ruhusu haya mabaya kupita. Roho ya kuachwa, kukataliwa, kuchukiwa, kurudi nyuma hizi zote kuna mahali zinapita. Kaa vizuri na Mungu anza kutengeneza maisha yako kwa upyaa. Mwambie Mungu niko hapa nifundishe njia zako. Pata muda wa kufunga na kuomba Mungu atengeneze maisha yako. Mwambie Mungu aanze upya na Wewe.
Pastor akasema wewe kuwa busy na Mungu tu utaona atakavyo kutendea.
Pastor akasema nataka uwe muombaji, uombe na ufunge haswa, lakini pia uwe binti wa viwango. Badilisha unavyovyaa, unavyotembea, unavyowasiliana na kuongea na watu, anza kuwa adimu usipatikane patikane kirahisi.
La Mwisho akasema nikuombe jitahidi sana kuwa MKIMYA, usiwe Mtu wa maneno mengi, usiongee chochote kwa Mtu yoyote zaidi ya Mungu pekee. Hata watu wakuulize kuhusu Eben au waseme chochote kaa kimya. Hata Eben akiongea kitu usijibu kaa kimya, kuwa mtazamaji zaidi na sio msemaji. Sisi tunaomba na tunaamini Mungu anashughulikia, hatuna haja ya kuongea kwa watu.
Akasema kuanzia Leo Eben mdharau, achana nae, ona kama hakuwahi kuwa mpenzi wako. Sahau kila kitu kuhusu Yeye hata ukikutana nae jifanye tu kama humjui, usimpe attention yoyote ile muache aendelee na maisha yake.
Aisee nilijikuta napata nguvu sana, nikaona mtazamo wangu umebadilika nikaanza kujiona watofauti.
Pastor akaniombea sana sana, na kuniomba nianze maombi ya mfungo kumsihi Mungu atengeneze maisha yangu, nikamwambia sawa Pastor nitaanza na kila ulichoniambia NITAKIFANYIA kazi na nitakupa mrejesho.
Basi tukaagana, tukaondoka.
Nikarudi nyumbani nikakumbuka maneno ya Pastor Anni kuwa “WEWE NI WATHAMANI, USIRUHUSU WATU KUKUDHARAU, ISHI MAISHA YAKO, FURAHIA MAISHANI YAKO”.
Hapo Hapo nikanyanyuka, nikaenda bafuni nikaoga, nikafungua kabati nikachukua kagauni flani hivi ka jeans kazuri nikakavaa, nikajipaka makeup 💄, nikajipulizia perfume. Imagine nguo nzuri nilikuwa nazo ila sikuwa navaa. Nikachukua Kawig kangu sipo, halafu nikaita Bolt anipeleke PIZZA HUT MIKOCHENI. Nikatoka huyo nikaenda PIZZA HUT nikaagiza PIZZA yangu na chips nikala taratibu, huku natafakari maneno ya Pastor Anni. Baadae nikamuomba mtu anipige picha achukue na viclip vidogo vya kupost kwaajili ya watesi.
Basi nikamaliza kula huyo nikaita tena Bolt, ikanifwata nikarudi zangu nyumbani. Sio siri ilikuwa ni mara yangu ya kwanza kujitoa Outing, ilikuwa mara yangu ya kwanza kupendeza, nilikuwa nafuraha sana sana.
Usiku nikaanza kupost zile picha na Video za Outing, nikashangaa Eben kaview picha zoteee 😀😀😀, na haikuwa kawaida yake, nikasema kweli PASTOR ANNI YUKO JUU na bado 🤣🤣
PART 10
Kesho yake jumatatu nikaanza maombi ya mfungo, nilianza kuomba rehema kwa Mungu kwaajili yangu na familia yangu. Nilimuomba Mungu anisamehe pale nilipokosea, anirehemu, amrehemu Baba yangu, amrehemu Mama yangu, asante familia yangu. Baadae nikaanza kumuomba Mungu anipe Neema ya kusamehe na kuachilia. Nikamsogeza Mama yangu wa kambo mbele za Mungu, nikamsihi Mungu amrehemu na amsamehee na Mimi anipe neema ya kumsamehe. Niliwaombea Watoto wake Joy na mwenzie nikaomba toba na rehema juu yao. Nikamwambia Mungu nawasamehe na kuwaachilia. Nikafuta kila laana waliotamka juu yangu, kila ubaya nikaufuta, nikasema kuanzia Leo najitenganisha na ubaya wao, ubaya wao hauta nipata kamwe.
Siku nyingine Nilimsogeza Eben mbele za Mungu, nakumbuka niliandika jina lake kwenye karatasi nikawa nimelishika huku naomba. Nikamwambia Mungu naomba rehema juu ya Eben kwa kila alilonifanyia ukamsamehe. Nikamuomba Mungu anipe neema ya kumsamehe na kuachilia. Nilimwambia Mungu nipe Neema ya kumsamehe Eben kabisa. Baadae nikachukua lile karatasi lenye jina lake nikaanza kulichana kwa hasira huku nalia nikasema kuanzia Leo Eben nakufuta kwenye maisha yangu, nakufuta kwenye Moyo wangu, kuanzia Leo nakuachilia hautakuwa kikwazo kwangu tena, hauta niumiza tena wala kunijeruhi maisha yangu bali utakuwa si kitu kwenye maisha yangu. Nakuachilia uende kwa amani nakutoa kwenye Moyo wangu. Aisee I wish ungeniona wakati nachana lile karatasi, nilikuwa nafanya kwa uchungu baada ya hapo nikalia sana sana sana, nililia baadae nikasema Mungu nakushukuru maana umenivusha nikasema Amen.
Niliendelea na mfungo wangu na maombi yangu. Pastor aliniambia hakikisha na usiku unaamka kuomba, omba mwambie Mungu akupe Amani, amani ya kweli inatoka kwake. Niliendelea hivyo kwa takribani wiki mbili.
Baada ya yale maombi kuna kitu kweli kilitokea, kwanza nilipata amani ya ajabu mnoo na moyo wangu ulikuwa mwepesi. Sikuwa tena na uchungu uchungu, nikaanza kuwa na amani na kupata furaha.
Kweli wanasema ukiwa na Amani hata Baraka zinakuja. Nilikuwa nacheza kikoba Ofisini na tukawa tunakaribia kuvunja, nikasema nikipata hela zangu nitajilipia ada nikasome Diploma. Hivyo nika Apply Chuo nikapata nafasi, nikalipa Ada na baadae nikaanza masomo. Nilikuwa nasoma masomo ya jioni, hivyo nikitoka tu kazini nawahi zangu chuo mpaka saa nne usiku ndio nafika nyumbani.
Maisha yangu yakabadilika kabisaaa, nikaanza kuwa na ratiba ya tofauti sana. Nikajitenga na kila mazingira yaliyokuwa yananipa huzuni. Lakini pia nikajifunza ukimya, nikaacha kueleza mambo yangu kwa watu. Kwa mfano issue ya Chuo sikumwambia Mtu yoyote, sio Baba, wala Mama hata kanisani hakuna aliyejua. Nilianza kufanya mambo yangu kimya kimya. Na nikaanza kupata Amani sana kwenye kila kitu.
Kanisani nikawa naenda nasali, ibada ikiisha huyoo nawahi zangu nyumbani kupumzika. Siongei na mtu wala kumtafuta Mtu. Lakini pia niliepuka kabisa maneno maneno, wale watu wa kanisani waliokuwa wananipa taarifa za Eben na mchumba wake niliwakatia, nikawa sipokei simu zao wala kujibu message, walinitafuta sana baadae wakachoka wakaniacha. Pastor aliniambia kaa mbali na habari mbaya, kaa mbali na taarifa mbaya. Basi nikajitenga nao.
Ilipita miezi minne sikumpigia simu Eben, wala kumtumia Message, na sio kawaida yangu, nilikuwa kimyaaa. Japo kila status ninayoweka anaiview nikasema acha iwe hivyo.
Ila nilibadilika, nikaanza kuvaa vizuri, navaa napendeza, nanukia nikifika ibadani watu wananiangalia hawanimalizi na baada ya Ibada huyoo napotea sipo.
Kuna siku tumemaliza ibada tukaambiwa vijana tubaki, tulikuwa na maandalizi ya siku ya vijana. Basi tukakaa kikao baada ya kumaliza kikao ile nanyanyuka namuona Eben ananifwata , anakuja upande wangu, nadhani alitaka kuniambia kitu. Huwezi amini nilinyanyuka, nikabeba pochi yangu sikumuangalia tena usoni, sikumsemesha chochote nikampita kama simjui, huku moyoni nasema shindwa kwa jina la Yesu. Akaita Bite Mimi kimya kama sisikii. Naona mwenyewe hakuamini. Hapo hapo nikaita boda nikapanda huyooo nyumbani.
Kuna siku alinipigia sana simu sikupokea, akatuma message sikujibu. Alinitafuta wiki nzima hanipati. Aliandika message samahani naomba kuongea na wewe nataka tumalizane, nikasema sasa tumalizane nini, mpuuzi tu sikumjibu.
Kuna siku nikaona Mwalimu wetu wa kwaya ananitafuta, nikapokea akasema Bite Eben anakutafuta anataka mmalizane kwani anakaribua kuoa. Nikamwambia mwalimu sina la kumalizana nae, hanidai simdai, aendelee tu. Mwalimu akashangaa jibu nililompa, akasema aisee haya Bite nikakata simu.
Aliendelea kunitafuta bila mafanikio, Kuna siku nimekaa nikaona simu ya Mama Mchungaji anapiga, nikasema ngoja nipokee, nikapokea Hallow Mama.
Mama Mchungaji akasema Eben kaja anataka mkutane kwa Mchungaji ili mmalizane kwani anataka kwenda kulipa Mahari. Hivyo nakuomba jumamosi ijayo uje ofisini ili muyamalize. Nikamwambia Mama Mchungaji, Eben hakuwa Mume wangu, hakuwa mchumba wangu, hakunitolea hata mahari sasa nimalizane nae nini, ana kipi cha kumalizana na Mimi. Mama Mchungaji akasema anaogopa isije fika siku ya Ndoa ukaharibu. Nikamwambia Mama kumbe hiyo ndio hofu yake, mwambie asijali sina huo mpango nimeshamfuta kwenye maisha yangu aendelee tu. Mama akasema sawa mwanangu kama nihivyo basi haina haja ya kuonana, tulijua bado una kinyongo, nikasema wala sina Mama yangu, endeleeni tu.
Baadae usiku nikaona Eben anapiga simu, alipiga sana sikupokea. Baadae akatuma message, eti nimekuita tumalizane kwa amani umekataa, sasa Mimi naoa nisikuone unanisumbua. Nikasema huyu acha ni mjibu kidogo afurahi, nakwambia unione wapi kaka kwa Ndoa ipi ya kusema niigombanie? Wewe hukuwa Mume wangu wala mchumba wangu hatuna cha kumalizana, Endelea na maisha yako Bwana achana na Mimi, huna nafasi tena kwenye maisha yangu.
Nikaona kasoma hiyo message akaanza kupiga, alipiga sana sikupokea. Akatuma message acha dharau pokea simu tafadhali pokea please sikupokea sikujibu.
Baadae Nikampigia Pastor Anni kumwambia kuhusu Eben kunitafuta, Pastor akasema huyo ameshazoea akikutafuta anakupata, ameshakudharau anafikiri bado unampapatikia, sasa kitendo cha kumchunia, hujibu message wala simu zake anaumia sana sana. Anataka akuone vile unahangaika. Tulia mwanangu kaza hapo hapo. Hakuna kitu kinamuuma Mtu aliyekudharau kama na wewe kumdharau, aisee wanaumia sana sana.
Pastor akasema na hakuna kumblock, Yeye sio adui yetu kabisa na wala hana sifa ya kuwa adui yetu.
INAENDELEA…………