𝗠𝗔𝗟𝗜𝗣𝗢 𝗞𝗜𝗧𝗔𝗡𝗗𝗔𝗡𝗜
ONYO: Wakubwa tu, kuanzia Miaka 18, ndio wasome hii Hadithi
Ep 13
Siku zilizidi kusogea, mapenzi yalizidi kuwa motomoto kati ya Haidali na Aneth, wote hawa walikuwa na ndoa zao lakini walikuwa wakizisaliti ndoa zao bila kujali hata mimba binti aliyokuwa nayo mtoto wa kike.
Ilipopita wiki mbili, ilikuwa ni siku ya kumbukizi ya kuzaliwa kwa binti, Erick alimtunuku zawadi ya gari mkewe, gari zuri la kutembelea aina ya Toyota Harrier, jipya kabisa.
Erick kwa upendo wa ajabu alienda kuirudisha leseni ya udereva ya mke wake kwani ilikuwa imeisha muda wake tangu alipoacha kuendesha gari kipindi cha mwaka mmoja uliokuwa umepita.
Alimpatia binti na alianza kwenda kazini na gari yake
Hata hivyo haikuchukua siku nyingi pia, aliletwa mfanyakazi wa ndani pale nyumbani, alikuwa akitokea Babati, yule msichana alikuwa anaitwa Katarina binti fulani hivi wa kimbulu mzuri kabisa.
Maisha ya nyumbani yalianza kubadilika, kukawa kumeshamrika shamrika kwa kipindi chote, usafi wa hali ya juu lakini Aneth alizidisha ubize kazini, mara nyingi alipenda kujirusha na Haidali.
Ilipofika mwezi wa kumi na mbili tarehe sita, binti alijifungua mtoto wa kiume, mwenye afya tele licha ya kuhujumiwa sana na boss wa mama yake kipindi alipokuwa tumboni.
Erick alifurahi sana, maana alikuwa ni mtoto wake wa kwanza katika maisha yake yote, alimpost kila mahali mtoto wake, lakini ilipopita miezi mitatu, martenity leave (likizo ya uzazi) iliisha na binti alirudi kazini vizuri tu.
Kipindi hiki binti alichokuwa ameshajifungua, alizidi kumpa penzi lake Haidali kila mara, lakini Erick hakuwahi kuhisi tofauti yoyote maana mara nyingi alikuwa akirudi nyumbani usiku na kuondoka ulfajiri na mapema.
Siku moja Erick akiwa amekaa zake kazini, alipokea simu kutoka kwa mtu asiyemjua maana ilikuwa ni namba mpya
“Broo” mtu huyo aliongea
“Hallo”
“Kwema kaka?” aliuliza mtu huyo
“Kwema kabisa, samahani upo online?” aliuliza mtu huyo ambaye Erick bado hakumjua
“Wewe ni nani?” aliuliza Erick
“Njoo online tutajuana kaka, nina jambo la muhimu sana nataka kukushirikisha”
Mtu huyo baada ya kumaliza sentensi hiyo, alikata simu yake na hata kumfanya Erick ashtuke kidogo hadi akajiuliza kunani?
Alisubiri kama dakika nzima ndipo akapokea ujumbe WhatsApp Ukisema “Mbona haupo online?”
Akaingia na kujibu “Niko online”
“Ok”
Yule mtu alitulia kwa sekunde kadhaa, ndipo zilitiririka jumbe zilizokuwa zimeambatana na picha, alizifungua zile picha akagundua ni za mke wake.
Hizi picha zilimuonyesha mke wake akiwa katika eneo moja, zilipigwa katika location moja, zote zilimuonyesha akiwa na Haidali licha ya kwamba Erick alikuwa hamfahamu Haidali kwa sura maana hakuwahi kufika ofisini kwa mke wake kabisa.
Hata hivyo zile picha zilikuwa sio mbaya kwani zilikuwa zikiwaonyesha tu wapenzi hao wasaliti wakiwa kwenye hoteli wamekaa mikao ya kawaida isiyo ya kimahaba.
Erick alimtumia ujumbe yule mtu “Wewe ni nani?”
Yule mtu akajibu “Broo mimi ni mzalendo nimeamua kukuambia tu mboga yako inaliwa na ugali wa jirani”
Erick hakuhangaika kumjibu tena mtu yule, alizidi kuzitazama zile picha, bado hakuona chochote kinachohashiria mapenzi.
Hata hivyo alizihifadhi zile picha kwenye programu ya google drive, halafu akamfuata Dullah na kumuonyesha kile alichotumiwa na yule mtu ambaye hakumjua
“Mh” Dullah aliguna kidogo halafu akaseme “Mmmh hhh”
“Nini kaka, unahisi kuna ukweli hapo?” aliuliza Erick
“Ni ngumu sana kujua kama kuna ukweli, lakini kama mtu kaamua kukutumia ujumbe kama huu, maana yake ana sababu, asingefanya hivi bure bure tu, ili kuujua ukweli lazima ufuatilie kwa undani” alisema mtaalamu Dullah
“Eti ee”
“Yeah”
Erick alifikiria kwa muda lakini hata hakujali sana, wala hakutaka kujua yule alimtumia ujumbe na zile picha ni nani…aliendelea na habari zingine
*
Sasa jioni wakati binti akiwa anarudi nyumbani, alikuwa anaongea kwenye simu na mdogo wake aliyekuwa akiitwa Janeth au Manka, ambaye huyu binti alikuwa ndiyo amemaliza kidato cha nne miezi kadhaa iliyopita
“Kwa hiyo mdogo wangu una mpango gani sasa?” aliuliza Aneth
“Mi hata sijui dada” alisema Manka
“Ilikuwaje ukafeli na wewe bwana?” alisema dada huku akiendesha gari yake taratibu
“Mi sijui, ila mitihani ilikuwa migumu eti”
“Una C ngapi?” aliuliza Aneth
“Nin C mbili”
“Mh sasa utarisiti au utaenda chuo?”
“Mi kurisiti hapana, sitaki shule bana embu nitafutie kazi kwanza huko”
“Mh maisha ya Dar unayaweza mdogo wangu?” aliuliza
“Hiyo da inasifika sana kwa ugumu natamani nipajue”
“Ngoja nikufanyie mpango mwishoni mwa mwezi huu uje upaone, kuna uzuri wa sura ila maisha ni magumu mdogo wangu”
“Jamani nitashukuru sana dada yangu, hamna shida mi nitakuja” alisema Manka
“Sawa, unikumbushe mimi nina mambo mengi sana”
“Sawa”
Baada ya maongezi ambayo yalikuwa ni marefu kidogo binti alikata simu, halafu alishika barabara ya nyumbani, kulikuwa sio mbali sana kutoka kazini.
Alipofika nyumbani cha kwanza kabisa alimuwahi mtoto wake na kuanza kumnyonyesha, baada ya kumnyonyesha mtoto alilala.
Mama akaenda kuoga na kujipumzisha kwa sababu kila kazi ilikuwa imeshafanywa na binti wa kazi, Katarina.
Siku hiyo kwa sababu wazo la tofauti lilikuwa limeshamuingia akilini, Kijana Erick aliwahi nyumbani mapema jioni, alipofika alimkuta dada wa kazi akiwa anaangalia TV
“Shikamoo” alisema binti huyo aliyekuwa na lafudhi ya kimbulu
“Marahaba” aliitika kwa mkato halafu akaingia mpaka chumbani alipokuwa akilala yeye na mkewe
Alimkuta mke wake akiwa amesinzia kabisa, lakin katoto kalikokuwa kamelala kando yake kalikuwa macho kakiangalia taa iliyokuwa ikiwaka juu huku mikono ikiwa kinywani kanavinyonya nyonya vidole vyake
Erick alimtazama mtoto halafu akatabasamu, bado hakuona kama anasalitiwa, alimuamini sana mke wake, licha ya kuwahi kumkuta na kashfa ya kutoka na rafiki yake, Amidu, lakini aliamini baada ya kumuoa mkewe amebadilika.
Erick alimnyanyua mtoto akawa amesimama naye katikati ya chumba anamchezea chezea, mtoto akaanza kucheka kila baba alipomtekenya kwa kidevu tumboni mwake. Baada ya mtoto kucheka sana, ghafla alibadilika na kuanza kulia sana.
Erick akajaribu kumbembeleza lakini alishindwa. Kutokana na sauti ya kilio cha mtoto, Aneth aliamka na kutazama ndo akakuta mumewe amesharudi
“Baba Chris….umesharudi”
“Yeah nimerudi” alisema mtaalam
Aneth aliketi kitandani halafu akampokea mtoto na kusema “Pole sana na majukumu”
Erick akajibu “Asante pole na wewe” alisema Erick
“Asante” binti alijibu huku akitoa nyonyo na kumpa mwanaye ainyonye.
Erick alipomtazama mkewe alikumbuka mambo mengi sana ambayo alishawahi kuyafanya naye, mambo ya maendeleo tangu awe naye hakika nyota yake ilifanikiwa kung’aa kama taa. Bado hakuona sababu ya kumchukia, alitamani aendelee kujua kama ni kweli au la
Akiwa anamtazama, mara simu ya Aneth iliyokuwa kwenye chaji iliwaka, huku ikitoa mlio wa mtetemo. Akaitazama na kukausha
Erick alipoliona hili aliamua kumfanyia kipimo cha kwanza, akamuuliza
“Ninaweza kuisoma hiyo message?” aliuliza huku akimtazama, macho yakagongana na kusema
Aneth akajibu “Kwanini unasema hivyo?”
Erick akajibu “Basi tu kwani kuna ubaya?”
Aneth alitabasamu na kusema “Soma tu wala usijali” aliongea lakini kiukweli, moyoni alikuwa na hofu kubwa sana maana alikuwa sio muaminifu kwa mume wake
Erick alitabasamu kisha akaifuata na kuishika akamtazama “Password nini?” aliuliza
Aneth naye akampachika swali “Kwani wewe siku zote huijui password yangu? Halafu si uliweka hadi fingerprint yako?” alisema
Ni kweli muda mrefu sana walikuwa wanaaminiana, tangu amuoe alikuwa akiijua password ya mkewe na hata fingerprint alikuwa ameweka kwenye simu ya mke wake akiamini ndiyo uaminifu
“Nilijua umeshabadilisha”
“Aka” binti alisema ila moyo ulikuwa ukimdunda, akawa anasali kimoyo moyo
Erick alipotia kidole chake tu, kweli simu ilitoka kwenye lock, akamtazama na kutabasamu, huku akizidi kumuamini kwa mara nyingine. Lakini Erick alipofungua kisanduku cha jumbe zilizoingia hivi, alikutana na ujumbe wa Haidali ndiyo alikuwa amemtumia muda huo.
EP 14
Aneth alikuwa anamtazama Erick kwa uoga, akiogopa lolote linaweza kutokea, moyo ulimuenda mbio, ukiangalia conversation kati yake na Haidali ilikuwa na message tatu za juu, huku zingine zikiwa zimeshafutwa.
Alikuwa anaogopa sana maana kama alivyojua mume wake alikuwa harudi nyumbani mapema, hasa pale alipompata housegirl, lakini siku hiyo aliwahi, na hii yote ni kwa sababu alikuwa amepata taarifa kwamba kuna mtu anammegea tunda lake.
Aliisoma ile message, ilikuwa ni ya kawaida ya kikazi, na ilikuwa ikisema hivi
“Hivi ile risiti ya malipo ya TRA uliweka wapi?”
Erick aliona ni message ya kawaida, halafu akaangalia za juu akakuta zote zilihusiana na masuala ya ofisini
Erick aligeuza macho akamtazama mkewe ambaye alionekana kujawa na wasiwasi, halafu akatabasamu, ndio binti kidogo akapata nafuu. Ile nafuu ilikuja kuondolewa na swali alilopachikwa lilikuwa hivi
“Hivi boss wako anaitwa nani?” aliuliza mtaalam Erick
Binti akashtuka akijua tayari kuna tatizo ndio akamuuliza naye swali “kwanini unaniuliza hivyo?”
Erick alitabasamu na kumtupia simu “Sawa kama unaona sio swali la msingi”
“Mh” binti aliguna na kuichukua simu akakuta ni message ya Haidali, aliogopa sana, ila alipoisoma ilimtia nguvu, akasema “Boss kumbe ndo katuma message” alisema binti Erick akawa anatoka zake pale chumbani bila hata kujali
Japokuwa Erick alimuamini mkewe lakini alipata wasiwasi, alipofika sebuleni aliketi kwenye kochi halafu akawa anaigusa kioo simu yake, huku akiwaza.
Baada ya dakika mbili alizirudia zile picha, na kuzitazama lakini bado hakumjua, maana zile picha hazikupigwa vizuri hivyo hakuweza kuijua vizuri sura ya Haidali, na wala hakuhisi kwamba Haidali anafanana na marehemu Amidu.
Alipoachana na zile picha, alipata wazo jipya la kitu cha kufanya. Bado Katarina, binti wa kazi alikuwa anaangalia runinga.
Ila kwa kuwa Aneth alikuwa na wasiwasi kidogo juu ya mumewe kutaka kusoma jumbe zake basi, aliamua kumfuata sebuleni na kumlalia begani huku akimuacha mtoto kitandani akiwa amesinzia tayari. Hizi shobo ndo ziliongeza wasiwasi mara dufu.
*
Kesho yake ilipofika mwamba Erick alienda zake kazini kama kawaida yake, siku ile alifanya kazi bila hata wasiwasi yoyote, lakini ilipofika mida ya saa saba mchana, alipokea mualiko kutoka kwa yule mtu aliyekuwa amemtumia picha za mkewe akiwa na Haidali hotelini
“Nije wapi na kuna nini?” aliuliza Erick
“Naomba tukutane Mbezi beach kiongozi, sihitaji hata mia yako mkuu” alisema
“Hahahaa…mia ya nini tena?” aliuliza
“Unaweza ukahisi mimi ni paparazzi, ila ungefika katika ofisi ambayo anafanya kazi mkeo basi ungejua jinsi gani anafanya uchafu mwingi sana”
Erick aliisoma ile message akapatwa na hasira sana, hasira zilikuwa sio kwa sababu ya mkewe, ila ni kwa sababu yule jamaa alikuwa anamkera, na alikuwa hajamtuma
Erick aliwaza mengi, aliona ni heri kuishi na mtu ambaye anakusaliti bila wewe kujua kuliko kujua inauma sana. Hata hivyo aliona ni bora akamtukana yule mtu aliyekuwa anajipendekeza.
Alimtumia ujumbe wenye tusi la nguoni
“We……..**** kwani nimekutuma umchunguze mke wangu? Acha afanye uchafu mi nimeridhika naye hivyo hivyo” alisema mtaalam kwa hasira
Yule mtu hakutuma ujumbe mwingine, wala yeye Erick hakufahamu ni nani yule anayempa taarifa kila siku.
Baadaye Erick alikuwa anapiga story na mfanyabiashara mwenzake aliyekuwa akiitwa Elisha, ndipo wakawa wanaongelea kuhusu hili suala la mtu asiyemjua kuwa anampa taarifa zinazohusiana na mke wake.
Elisha alimuuliza “Kwa hiyo umeamua kufanyeje?”
Erick akajibu “Mimi sihitaji kufanya jambo lolote kuhusu hili, nimeamua niendelee na mke wangu, bado sijamuhisi vibaya”
“Unajua nini?” Elisha alisema
“Sijui” Erick alijibu
“hata kama usipojua hili utakuwa umejiepusha na kuumia moyo, lakini utakuwa umejihatarishia maisha yako” alisema
“Kwanini Elisha?”
“Kwa sababu, unaweza ukawa ukajizuia lakini je yeye kama anafanya mambo hayo kweli, huoni kwamba ndiyo hatari ya kuwalea watoto wa wanaume wenzako au hata kupata magonjwa hatari?”
Erick alilisikia hili lakini hakujibu chochote, alimtazama tu huku akitafakari, ndipo Elisha akaendelea “Cha muhimu mfuatilie mzee, tutakupoteza”
Erick alipata wazo zuri sana kutoka kwa Elisha, aliona ni kweli asipofuatilia basi itakuwa ni hatari kwa maisha yake. Erick alichukua simu akataka kumpigia yule mtu ambaye alikuwa akimpa taarifa lakini ile namba haikupatikana tena.
*
KESHO YAKE
Ilipofika siku moja baadaye, Aneth alienda kazini asubuhi lakini siku hiyo ilikuwa tofauti kidogo kwani alimuacha mume akiwa amelala ndani
Kabla ya kuondoka alimuuliza
“Mbona leo umelala sana?”
Erick akajibu “Nitaenda baadaye kidogo”
“Haya kwa heri mi nawahi kazini”
“poa”
Aneth aliondoka zake, alipofika sebuleni alimpatia shilingi elfu kumi dada wa kazi kwa ajili ya matumizi ya siku ile.
Muda wa saa saba mchana Erick alipanda daladala na kuondoka moja kwa moja mpaka eneo ambalo alikuwa akifanyia kazi Aneth. Siku hiyo hakutaka kwenda na gari yake. Alipofika katika ofisi ile ya bima za vyombo vya moto, alimkuta Jonas akiwa amekaa katika ofisi ya nje akiwa anaandika vitu fulani kwenye kompyuta
“Karibu boss” alisema kwa ukarimu Jonas, walikuwa hawafahamiani kabla
“Asante sana” alijibu Erick huku akiangaza kushoto kulia, kweny ofisi ile, hakumshuhudia mtu mwingine pale ndani
“Karibu sana” Jonas alisema huku akiacha kazi yake na kumsikiliza Erick ambaye alikuwa kama mteja amekuja
“Sawa kabisa” Erick alikeri kwenye kiti cha wageni kisha akasema “Samahani ninahitaji bima, kuna gari yangu ya mizigo nimeagiza…mtanifanyiaje boss?” aliuliza
“Gari aina gani?’
“Canter” alisema
“Canter, ni milioni tatu……” alisema
“Anhaa”
Wakati Erick anazidi kuangalia kama hata kuna dalili ya mkewe pale ndani ndipo akamuuliza Jonas “Kwani wewe ndiye boss wa hii kampuni?”
Jonas akatabasamu kisha akajibu “Hapana, mimi ni mfanyakazi tu”
“Sawa…boss yuko wapi?”
“Boss ametoka kwenda kula”
“Ameenda mbali? Maana nilitaka kuongea naye pia”
“Sawa, labda umsubiri kama nusu saa hivi”
“Sawa kabisa”
Erick alitoa simu yake mfukoni akawa anaichezea chezea, ndipo akaingia dada mmoja alikuwa akiuza matunda yaliyokatwa katwa.
“Mambo kaka Jona” alisema yule mwanamke kwa amsha amsha alionekana mchangamfu sana
“Safi kwema Dorcas?” aliuliza Jonas
“Kwema, matunda leo vipi?”
“Nipe basi maana sijala kabisa” alisema Jonas
Yule dada alifunua kapu lake na kutoa chombo kimoja chenye matunda akamuewekea mezani na kumuuliza “Vipi yule dada leo hayupo?”
Jonas akasema “Hamna katoka….”
“Si umchukulie tu?’
“Kaenda kula nafikiri hawezi tena kula matunda”
“sawaa”
Jonas alitoa hela na kumpatia Dorcas, ndipo Erick naye akadakia “Naomba na mimi nipate tunda”
“Sawa kaka yangu” binti alifurahi na kutoa tena chombo kingine akampatia Erick
Baada ya kumlipa yule msichana aliondoka zake na kuwaacha wakiinjoy matunda.
baada ya kukaa pale kwa muda mrefu sana, bila ya Haidali na Aneth kurudi, Jonas alichukua simu na kumpigia Haidali
“Boss vipi hamjamaliza tu kula?” aliuliza huku akiwa ameweka loud speaker
“aaah bado si unajua nikiwa na beby nakula taratiibu” alisema Haidali bila kujua kwamba mume wa Aneth alikuwa pale ofisini na anasikia maongezi
“Hahahaa…unainjoy eti?’
“Nainjoy mimi, ila sio mbaya tunakuja sasa hivi hapo”
“Poa kuna mtu anakusikilizia” alisema
“Poa”
Erick alizidi kusubiri kama dakika kumi hivi, ndipo alipoingia Haidali peke yake na kumsalimia Erick halafu akaingia katika ofisi yake moja kwa moja.
Dakika moja baadaye Aneth aliingia akiwa anaongea na simu, ila alipofika pale ofisini alipigwa na butwaa baada ya kumkuta mume wake ameketi.
EP 15
Binti alisita katikati ya chumba cha ofisi akiwa kama vile kapigwa shoti, taratiibu simu iliyokuwa sikioni iliteleza akawa anaitoa taratibu kushuka sikioni, huku akimshangaa mume wake ambaye muda wote alikuwa anatoa tabasamu huku akimuangalia mumewe
Jonas alibaki akishangaa kwani alikuwa hawajui kabla “Erick” alisema Aneth
“Haaa….mambo” alisema Erick kwa tabasamu, ndipo Jonas akavua miwani ili awashangae vizuri
“Umekuja kutafuta nini huku?” binti alisema huku akisogea na kuketi kwenye kiti kando ya mumewe akawa anamshangaa
“Kwani kuna ubaya gani kuja kujua wewe unafanyia kazi katika mazingira gani?” aliuliza Erick
“Mmmmh” binti aliguna, na hakuwa na wasiwasi kwani alikuwa akiliona tabasamu la mumewe likamfanya akajua mumewe hajaja kwa shari yoyote
“Msinichanganye, kwani wewe ndo mume wa Aneth?” aliuliza Jonas
Erick alitabasamu na kumuangalia mkewe akimsubiri amsaidie kujibu, ndipo Aneth akasema “Ndio ni mume wangu….huyu ndo baba Chris”
“Hahaha…asee sijawahi kudhania kama nitamjua maana hata picha hatuonyeshagi”
“Tatizo mimi ni mbaya, hawezi kuwaonyesha”
“Hapana…….jamaniiii siwaonyeshagi kwa sababu….”
“Kwa sababu gani?” aliuliza Erick lakini Aneth akashindwa kujibu akacheka tu kwa nguvu
“Nambie umekuja kuniona au umekuja tu ofisini kuna mambo yako?”
“nimefika hapa nikawa nataka kuongea na boss… lakini nasikia anakula”
“Mh kwani hajaingia hapa?” aliuliza Aneth
“Boss…..ameshaingia si amepita hapa?” aliuliza Jonas
“Saa ngapi” Erick aliuliza
“Hujamuona na mmesalimiana hapa kama dakika tano zimepita”
“Ndo mwenye suti ya kijivu?”
“Ndio”
“we huyo mdogo mdogo?”
“Ndio”
“Hahaha sikujua, yuko wapi sasa” aliuliza Erick
“Yuko ofisini” Aneth aliinuka na kumshika mkono mumewe akasema “twende nikupeleke”
Erick aliinuka na kuanza kutembea na mkewe mpaka kule ofisini kwa Haidali. Alipofika ndani, Haidali alishtuka kidogo maana walikuwa wameshikana mikono, halafu kumbuka naye alikuwa ni mpenzi wake
“Boss, nimekuletea mteja” alisema huku akimkonyeza Haidali asije akafanya jambo lolote la kimahaba kwani angeiweka ndoa yake hatarini sana
“Oh karibu ndugu yangu” alisema Haidali kwa furaha huku mkono wake mmoja ukionyesha kiti kilipo ili mwamba aweze kukaa
“Asante sana” alisema Erick na kuketi
Aneth alimtazama huku bado akitabasamu ndipo akasema “Basi mimi nikuacheni”
“Hamna tatizo” aliongea Erick
Aneth alitoka, alipotoka tu hivi alikimbilia uani na kwenda kusimama kwenye kioo halafu akavuta pumzi ndefu na kujipepea kwa mikono
“Oh Mungu wangu eee…..ehhhe imekuwaje tena akaja huku?” alijiuliza kwa sauti ndogo “Sasa ningeingia na Haidali tumeshikana si ingekuwa ni hatari hii?” aliendelea kujiuliza
Hadi mkojo wa haraka ulimbana na kujikuta anajisaidia, halafu akatoka akiwa anahema kwa nguvu na kumfuata Jonas, akamuongelesha kwa sauti ya mnong’ono
“We J wewe, mnataka kuniua na presha?” aliuliza binti
“Kivipi?” Jonas aliuliza
“aliyemleta mume wangu hapa ni nani?”
“Hahaha…mimi hata sijajua kama ni mume wako, nimeona tu amekuja hapa”
“Daah, nimeogopa”
“Sasa unaogopa nini?”
“Acha tu, ndoa ni jambo la kukaa nalo makini ndugu yangu”
“Hahha”
Kidogo Jonas na Aneth walikuwa wamekwisha elewana, na hata kuwa marafiki sana. Walipiga story sana
Lakini vile vile kule ndani, Erick na Haidali walikuwa wakipiga story nyingi sana za kibiashara, Erick aliahidi kurudi kuja kufanya utaratibu wa kupata bima pale, ili amuungishe mtu aliyemuweka mke wake town.
“Karibu sana ndugu yangu” alisema Haidali baada ya kumaliza maongezi na Erick
“Asante sana ndugu yangu”
“Okay”
Erick alitembea kidogo halafu akageuka na kusema “Samahani sijaja na gari, vipi Mke wangu anaweza kunipeleka nyumbani?” aliuliza
“Ndio usijali ndugu usijali” alisema Haidali kwa uchangamfu
Erick alitoka, akamkuta mkewe akiwa anaongea na Jonas pale mapokezi, akamuambia Jonas “Broo asante sana”
Jonas akajibu “Karibu sana ndugu yangu
Erick alimgeukai mkewe kisha akamuambia “Nakuomba kidogo”
Aneth alitoka na mumewe pale ofisini mpaka nje, akamuambia “Mke wangu, nimefurahi kupajua ofisini kwako, licha ya kuwa ulikuwa ukinificha, ila ni sehemu nzuri na kuna ukarimu wa hali ya juu”
“Mmmmh….sikukuficha mume wangu but, unakuwaga sana bize”
“Haya mama…..nipeleke home sijaja na gari”
“ulikuja na nini?”
“Nilikuja na daladala”
“Gari iko wapi?”
“Iko nyumbani…leo sijaenda kazini kabisa” alisema mtaalam
“Mh kwanini?”
“Nilikuwa tu sijisikii…embu nipeleke basi mke wangu”
“Haya ngoja nichukue ufunguo”
“Okay”
Aneth aliingia ndani akachukua mkoba wake na kutoka kwa mwendo wa haraka, wakaenda hadi kwenye gari yake, walipanda na safari ilianza kuelekea nyumbani kwao, walipokuwa njiani walipiga story nyingi ila story kubwa sana iliyochukua takribani dakika kumi ni kujiuliza kwanini Haidali anafanana na Amidu
“Hawa sio ndugu?” Erick aliuliza
“Hapana sio ndugu”
“Mh, wanafanana sana” alisema Erick
“Sana”
Moyoni Erick alipata wasiwasi kwamba ule mfanano unaweza kupelekea mkewe kushawishika na kumsaliti kwa sababu alikuwa na mahusiano na marehemu Amidu kabla ya kifo kumfika mwaka na nusu uliopita
Siku ile Jonas alipotembea ofisini kwa Haidali alikuta namba ya Erick imeandikwa kwenye diary ya ofisi.
Akaichukua haraka huku akisema kwa sauti ndogo “Hii nina kazi nayo”
INAENDELEA

