NILIJIUNGA NA DINI YA SHETANI
ONYO: Wakubwa tu, kuanzia Miaka 18, ndio wasome hii Hadithi
Sehemu Ya 5
“Wewe ni nini? Ni mwili wako, akili zako, uzuri wako, mali au elimu yako? Kwa nini mtu akifa tunasema tunaenda kuuzika mwili wa fulani, huyo anayeumiliki mwili ni nani?” hayo yalikuwa baadhi ya maswali magumu ambayo ama kwa hakika yalinifanya nijikune kichwa. Uelewa wangu ukaanza kufunguka.
Niliendelea kusoma juu ya umuhimu wa kila mtu kujitambua na kufahamu thamani yake na malengo yaliyomleta duniani. Nikasoma kuhusu nguvu zinazozalishwa na watu bila ya wao wenyewe kujua kuanzia kwenye kauli, mawazo na matendo.
Mwandishi akafafanua kwa kina namna watu wanavyoshindwa kuzitumia nguvu walizojaaliwa ndani ya akili zao na kujikuta wakiishia kuishi maisha ya kifukara mpaka wanakufa. Akaeleza kwa nini watu wengine wanaishi maisha ya kifukara, mlo wa siku moja ukiwa ni tatizo kubwa kwao ilhali kuna wanaoishi kifahari, wakila, kunywa na kusaza.
“Wewe ndiyo uliyechagua aina ya maisha unayotaka kuishi, ukiamua kuwa tajiri, bila shaka utakuwa tajiri kwa sababu akili na mawazo yako vinazalisha nguvu kubwa ambayo inaweza kuyafanya yale uliyokuwa unayafikiria yatokee katika maisha halisi,” ilisomeka sehemu ya kitabu kile.
Niliendelea kushangaa kwani kila neno nililokuwa nalisoma kwenye kitabu kile, lilikuwa likiniamsha ari ndani ya nafsi yangu kutaka kufahamu kwa undani kilichokuwa kinazungumziwa. Mwandishi aliendelea kutoa mifano jinsi binadamu alivyojaliwa uwezo mkubwa wa kufikiri na kufanya kila analofikiri litokee.
Alitolea mfano watu wenye uwezo wa kupindisha vitu kama kijiko au chuma chochote kwa kukitazama tu, akazungumzia pia watu wenye uwezo wa kupasua glasi kwa kuitazama au kuhamisha kitu kimoja kwenda sehemu nyingine. Nilijiuliza kile kilichokuwa kinazungumziwa ni uchawi au nguvu za mawazo? Mwandishi alinijibu katika ufafanuzi kuwa hakuna uchawi katika suala lile na kila mmoja anaweza kufanya akifundishwa.
Nilipoendelea kusoma, kuna sehemu mwandishi alitoa mfano kwa kila msomaji kujaribu kujipima kama ana nguvu za mawazo kiasi gani. Na mimi nikajaribu.
Nilikaa sakafuni na kutulia, nikawa navuta pumzi ndefu na kuzitoa taratibu kupitia mdomo huku nikiwa nimeweka uzingativu wa kutosha akilini mwangu. Nikiwa katika hali ile, nilishangaa nikijihisi kitu tofauti kabisa kwenye mwili wangu. Nikawa ni kama nimehama kwenye ulimwengu wa kawaida na kwenda mahali nisipopajua.
Nilishtuka kwa nguvu hadi nikaanguka sakafuni, nikawa nafikicha macho ili kuhakikisha kama sikuwa kwenye ndoto. Nilikaa vizuri kisha nikaendelea kukisoma kile kitabu, safari hii nikiwa naelewa na kuamini kila nilichokuwa nakisoma kwani nilihakikisha mwenyewe kuwa kile kilichokuwa kinaelezewa hakikuwa porojo bali ukweli mtupu.
Nikiwa naendelea kukisoma kile kitabu, kumbe baba alikuwa amezunguka nyuma ya nyumba na kuja mpaka kwenye dirisha la chumba changu, akawa ananiangalia nafanya nini kwani nilikuwa nimetulia kwa muda mrefu.
“Unafanya nini? Aliniuliza kwa sauti ya ukali.”
“Najisomea baba, mitihani imekaribia,” nilimjibu huku nikijitahidi kukificha kile kitabu ili asikione.
“Hebu lete hicho kitabu,” aliniambia, nikawa nasita kama nimpe au la lakini kwa jinsi alivyokuwa ananitazama kwa ukali, ikabidi nifanye kama alivyoniambia. Nikampa kile kitabu huku nikitetemeka kuliko kawaida.
“Haaa! Unasoma kitabu cha kichawi? Unataka kujiunga na jamii za siri na dini ya shetani siyo? Hujui kama mimi baba yako ni mtumishi wa Mungu? Kwa nini unataka kunitia aibu?” alisema baba huku akiendelea kufunua kurasa za kile kitabu. Sikumjibu kitu, nikawa naendelea kutetemeka kwa hofu.
Akiwa na hasira za hali ya juu, nilimshuhudia akikichanachana kile kitabu, akatupatupa karatasi huku na kule huku akinitolea macho ya ukali. Kwa kuwa alikuwa upande wa nje, aliniambia nisitoke mle chumbani nimsubiri, nikajua anataka kuja kuniadhibu vikali, nikawa nafikiria namna ya kumkimbia.
Nilipata akili ya kukimbia haraka kabla baba hajaingia ndani na kuja kuniadhibu, nikatoka na kuingia chumba kingine, nikajifungia mlango kwa ndani. Nilimsikia baba akiingia ndani na kusukuma mlango kwa nguvu, nikawa natetetema kwa hofu.
“Yuko wapi?” nilimsikia baba akiuliza kwa jazba. Nilijibanza kwenye kabati la nguo la ukutani na kujifungia, nikawa namuomba Mungu asinione kwani kwa jinsi nilivyokuwa namfahamu, angeniadhibu vikali.
“Kwani kuna nini tena?”
“Huyu mwanao mshenzi sana, yaani anajifunza mambo ya dini ya shetani ndani ya nyumba yangu, leo atanikoma.”
“Mambo ya dini ya shetani? Ndiyo mambo gani hayo,” mama aliuliza huku akiwa haelewi kinachoendelea. Nilimsikia baba akimfafanulia kuwa amenikuta nikiwa nasoma na kujifunza mambo ya kichawi kwenye kitabu.
Mama alimuuliza yeye amejuaje kama nilichokuwa nakisoma kinahusu dini ya shetani? Nikawasikia wakianza kufokeana wenyewe kwa wenyewe. Nilishukuru sana mama kuingilia ugomvi ule kwani hiyo ndiyo ilikuwa ahueni yangu. Wakaendelea kujibizana, baba akatoka na kwenda kukusanya karatasi za kile kitabu changu alichokichanachana.
Akarudi ndani na kumuonesha mama, akawa anaziangalia huku na yeye akishangaa. Baadaye nilisikia wakianza kuzungumza vizuri, nikajua wameshapatana, hasira za baba zikawa zimepungua, nikatoka mafichoni na kufungua mlango.
“Njoo hapa,” nilimsikia baba akisema. Kumbe wakati nafungua mlango alikuwa ameshaniona, nikawa sina ujanja zaidi ya kujipeleka mwenyewe kwake. Mkononi alikuwa ameshika fimbo mbili ngumu, nikasogea huku nikiendelea kuomba kimoyomoyo.
Tofauti na nilivyotegemea, baba hakunipiga bali aliutumia muda ule kuzungumza na mimi kwa busara. Akaniambia nimshukuru mama kwani bila yeye kuingilia kati na kuniombea msamaha, ningekiona cha mtema kuni. Aliendelea kuzungumza na mimi kwa kirefu, akaniambia sitakiwi kujifunza au kushiriki kwa namna yoyote mambo yanayohusu imani ya dini ya shetani.
Kiukweli sikumuelewa anamaanisha nini kwani kile nilichokuwa nikikisoma kwenye kile kitabu alichokichana, hakikuwa na matatizo yoyote ukilinganisha na matendo yake aliyokuwa anayafanya gizani.
Hata hivyo, sikutaka kubishana naye kwa chochote, nikawa namsikiliza mpaka alipomaliza kuongea. Alipomaliza aliniambia niondoke ili waendelee kuzungumza na mama.
Kiukweli nilichukizwa sana na kitendo chake cha kunichania kitabu changu, nikajiwekea nadhiri kuwa lazima nitaenda kununua kingine.
Siku iliyokuwa inafuatia ilikuwa ni Jumapili, baba akatuambia tuvae vizuri kwa sababu ataenda kututambulisha rasmi kwenye kanisa jipya mbele ya waumini wengi zaidi tofauti na kule kijijini Itete.
Wenzangu walifurahia sana lakini kwangu mimi ilikuwa tofauti. Baada ya kugundua mambo aliyokuwa anayafanya baba, nilikosa imani naye kabisa, nikawa nachukizwa na tabia yake ya kuwadanganya watu, tena wengine wakiwa wamemzidi umri.
Jumapili ilipofika, kama baba alivyokuwa ametuambia, wote tulivaa suti mpya tulizokuwa tumenunuliwa, mama akavaa gauni lake jipya na kujifunga kilemba kama wafanyavyo wanawake wa Kinigeria, tukaondoka mpaka kanisani.
Baba alinipa Biblia yake nimshikie, akaniambia nisiende kukaa upande waliokuwa wamekaa waumini wengine pamoja na ndugu zangu, akaniambia nitakaa nyuma ya madhabahu. Sikuelewa kwa nini aliniambia vile lakini nilitii, nikawekewa kiti nyuma ya madhabahu na baba akaanza kuongoza ibada akitumia Biblia nyingine tofauti na ile.
Sehemu Ya 6
Baba alinipa Biblia yake nimshikie, akaniambia nisiende kukaa upande waliokuwa wamekaa waumini wengine pamoja na ndugu zangu, akaniambia nitakaa nyuma ya madhabahu. Sikuelewa kwa nini aliniambia vile lakini nilitii, nikawekewa kiti nyuma ya madhabahu na baba akaanza kuongoza ibada akitumia Biblia nyingine tofauti na ile.
Ulipofika muda wa kuwaombea wagonjwa na watu wenye shida mbalimbali, baba alishuka madhabahuni na kuja pale nilipokuwa nimekaa, akachukua ile Biblia niliyokuwa nimeishika, akarudi kwenye madhabahu na kuanza kufanya maombezi.
Wagonjwa na wenye shida mbalimbali walijitokeza kwa wingi lakini miongoni mwao, kuna mmoja alinishangaza sana. Jina lake alikuwa anaitwa Sinai na wakati tukiishi kijijini Itete, alikuwa akija nyumbani mara mojamoja na kuzungumza na baba. Kilichonishangaza ni kwamba alikuwa akitembelea magongo huku miguu yake ikiwa kama mtu mwenye ulemavu.
Nilishangaa sana Sinai amepata ulemavu lini na ilikuwaje kwani mara mwisho kumuona, hata miezi sita haikuwa imeisha. Nikanyamaza ili nijionee kitakachotokea. Baba aliteremka kwenye madhabahu na kusogea pale mbele wagonjwa walipokuwa wamesimama.
Nikamuona akiwapita wale wengine na kwenda moja kwa moja kwa Sinai, akaanza kumhoji maswali huku akimuwekea kipaza sauti mdomoni, watu wote waliokuwa kanisani wakawa wanasikia alichokuwa anakisema.
“Nilizaliwa nikiwa mlemavu, mama yangu alirogwa akiwa na mimba yangu, naomba uniombee nipone,” alisema Sinai, nikazidi kupigwa na butwaa kwani nilikuwa nikimfahamu vizuri na hakuwahi kuwa mlemavu.
Baba alimuwekea mikono kichwani, akaanza kumuombea huku akinena kwa lugha, nikaona Sinai ameanza kuongea hovyo kama mtu aliyepandwa na mapepo, kisha akaanguka chini. Baba akamshika miguu aliyodai ina ulemavu, akaendelea kuomba kwa nguvu.
Muda mfupi baadaye Sinai alijifanya amezinduka, akamshikilia baba mwilini na kujaribu kusimama, eti akaanza kusema miguu yake iliyokuwa na ulemavu wa kuzaliwa nao imepata nguvu baada ya kuombewa, akatupa magongo na kuanza kurukaruka kwa furaha.
Waumini wengine walishangilia sana wakiamini Mungu ametenda miujiza wakati haikuwa kweli. Nilimuona mama naye akishangilia japokuwa alikuwa akimfahamu vizuri Sinai kuwa hakuwa mlemavu na siyo kweli kwamba baba ndiyo amemponya. Watu wakatoa sadaka kwa wingi, nikapewa mimi nizishike.
Kwa kuwa nilikuwa nahitaji fedha kwa ajili ya kwenda kununulia kitabu kingine baada ya kile cha awali kuchanwa na baba, nilichomoa noti moja ya shilingi elfu kumi kwenye kapu la sadaka lililokuwa limejaa na kuificha kwenye mfuko wa koti.
Baada ya kumuombea Sinai, baba aliendelea kuwaombea wagonjwa wengine hasa wale waliokuwa na matatizo madogomadogo ambapo kila aliyeombewa, muda mfupi baadaye alitoa ushuhuda kuwa amepona na anajisikia vizuri. Kanisa liliendelea kulipuka kwa shangwe na vigelegele mpaka muda wa kumaliza misa ulipofika.
Japokuwa kapu la sadaka nililopewa na baba kushika lilikuwa kubwa, lilijaa noti walizotoa waumini kama sadaka. Nafikiri muujiza feki wa Sinai ulisaidia sana kuwafanya waumini watoe sadaka kwa wingi.
“Tangulia na huo mzigo kwenye taxi aliyokodi mama yako, ipo hapo nje inakusubiri, pitia mlango wa huku nyuma watu wasikuone,” baba aliniambia kwa sauti ya chini, akanionesha mlango wa kutokea ambapo niliinuka na lile kapu la sadaka, nikatoka nje ambapo nilimkuta mama akiwa na dereva taxi wananisubiri. Tukaondoka na kueleka nyumbani huku baba akiendelea kuagana na waumini wake.
Baada ya muda, baba alirejea akiwa kwenye teksi nyingine, akiwa na dereva na mtu mwingine ambaye sikumtambua haraka kwani hakushuka garini. Baba aliingia ndani na moja kwa moja akapitiliza mpaka sebuleni tulipokuwa tumekaa na mama tukiangalia runinga.
“Ule mzigo umeuweka wapi?” baba aliniuliza akimaanisha kapu la sadaka. Mama alimjibu kuwa lipo chumbani kwao, akaingia ndani kisha mama naye akamfuata. Niliutumia muda huo kutoka hadi nje, nikaenda kumuangalia yule mtu wa tatu aliyekuwa ameongozana na baba.
“Haa! Kumbe ni Sinai,” nilishtuka baada ya kugundua kuwa kumbe baba alikuwa amekuja na yule mtu aliyejifanya alizaliwa na ulemavu ambao uliisha muda mfupi uliopita baada ya kuombewa na baba.
Nilitamani kwenda kumuuliza ni kwa nini ametoa ushuhuda wa uongo ndani ya nyumba ya Mungu lakini nikaogopa anaweza kumwambia baba na kuanzisha matatizo mengine ambayo hayakuwa ya lazima.
Nilijibanza nikitaka kuona baba alikuwa amefuata kitu gani ndani. Baada ya muda nikamuona akitoka akiwa amebeba bahasha ya kaki mkononi iliyokuwa imetuna, nikajua kuwa lazima zilikuwa ni fedha. Alitembea harakaharaka hadi kwenye gari, akafungua mlango wa nyuma na kumpa Sinai ile bahasha.
Akamfuata dereva na kumpa maelekezo fulani kisha lile gari likaondoka pale nyumbani. Harakaharaka nilitoka pale nilipokuwa nimejificha na kurudi sebuleni, baba alipoingia ndani, alinikuta nikiwa nimekaa hivyo hakuhisi chochote
“Umefanya kazi nzuri sana leo kanisani, chochote ulichokiona kibakie kuwa siri yako, sawa mwanangu kipenzi,” baba aliniambia huku akiwa amekaa jirani kabisa na pale nilipokuwa nimekaa. Nilishangaa kwa jinsi alivyokuwa anazungumza na mimi kwa upole. Nikaitikia na kumwambia sitamwambia mtu yeyote. Nilimridhisha tu lakini kiukweli nilikuwa nachukizwa sana na matendo yake.
Baada ya kula chakula cha mchana, nilitoka bila kumuaga mtu yeyote, nikaenda moja kwa moja mpaka stendi kununua kitabu kama kile ambacho baba alikichana. Nilipofika nilitoa noti ya shilingi elfu kumi niliyoiiba kwenye sadaka za baba, nikampa yule muuzaji ambapo alinipa kitabu kama kilekile.
Ili kuzuia baba au mama wasigundue kilichokuwa kinaendelea, nilinunua kitabu kingine cha hadithi kiitwacho Usilie Tena Geneviv, nikachana kava lake na kumuomba yule muuzaji gundi, aliponipa nilibandika kava lile juu ya kitabu changu. Kwa harakaharaka kikawa kinaonekana kama kitabu cha hadithi nzuri za kusisimua kumbe haikuwa hivyo.
Nilipohakikisha kipo sawa, nilirudi nyumbani na kwenda kukificha chumbani kwangu. Nilipohakikisha hakuna mtu aliyenishtukia, niliingia chumbani kwangu na kujifungia, nikaanza kusoma kuanzia pale nilipokuwa nimeishia kabla baba hajanifuma.
Bado niliendelea kushangazwa na mada zilizokuwa ndani ya kitabu kile kwani kila nilichokuwa nakisoma kilikuwa kigeni kwangu lakini chenye manufaa makubwa.
Kutokana na uzito wa mada zenyewe, nililazimika kutafuta ‘ki-notebook’ kingine kidogo, nikawa naandika mambo ya muhimu niliyokuwa najifunza. Niliendelea kusoma hadi nikafika kwenye kipengele cha tahajudi (meditation).
Mwandishi alifafanua maana ya tahajudi na kueleza kuwa ni kitendo cha mtu kukaa katika hali ya utulivu na kutafuta usawaziko wa kimwili na kiakili. Akafafanua kuwa mtu anayetaka kufanya tahajudi, anatakiwa kukaa sehemu tulivu na kutulia huku mikono yake akiwa ameiweka kwa namna ya utulivu kabisa, kisha kuanza kuikabili akili yake.
Nilimuelewa mwandishi vizuri kuhusu namna ya kufanya tahajudi, akazidi kueleza kuwa mtu anapofanya meditation, anachofanya ni kuiruhusu akili yake kurudi katika hali ya asili ambapo uzingativu, usikivu, utulivu na uvumilivu huwa ni wa kiwango cha juu. Katika hali hii ya utulivu, mwandishi alieleza kuwa unaweza kuiamuru akili yako ifanye kile unachokitaka na kweli matokeo yakaonekana.
Akaendelea kueleza kuwa wakati mwingine, tahajudi huambatana na matumizi ya maneno fulani (mantra) kwa kuyataja na kuyarudiarudia mara nyingi ambapo kile kinachotamkwa au kunuiwa, hutokea ndani ya muda mfupi. Akaeleza kuwa hata wachawi wanapotaka kumroga au kumdhuru mtu, hutumia tahajudi.
“Mtu akitaka kukuroga, lazima awe anakujua jina lako ambapo hutafuta sehemu tulivu na kuanza kulitaja jina lako mara nyingi na kunuia kile anachotaka kitokee.
Kama anayelengwa si mtu anayejitambua, nguvu zinazorushwa humpata kirahisi na hapo ndiyo tunasema fulani amerogwa,” ilisomeka sehemu ya kitabu kile. Nikapigia mstari kwa kutumia penseli kwenye kipengele hicho.
Zikaelezwa faida za tahajudi ambapo niligundua kuwa ni kitendo chenye faida nyingi sana kwenye mwili na akili ya binadamu.
Baada ya kuhakikisha nimeelewa vizuri, nilikaa sakafuni kwa utulivu kabisa, nikawa navuta hewa kwa kutumia pua na kuitoa kupitia mdomo huku nikiwa nimefumba macho yangu. Nilijiachananisha na mawazo yote yaliyokuwa yananikabili, nikawa nafanya tahajudi.
Baada ya dakika chache, nilijikuta nikitokewa na hali ambayo sikuwahi kuihisi tangu nizaliwe.
Nilijihisi naelea angani, sehemu ambapo hakukuwa na mtu mwingine yeyote zaidi yangu. Nikawa naendelea kupumua kwa uhuru, nikivuta hewa kwa pua na kutoa kwa mdomo. Nilifurahia hali ile kwani kwa mara ya kwanza, nilijihisi nikiwa sina mawazo yoyote kichwani, sikuwa nikifikiria wala kuona chochote zaidi ya taswira yangu mwenyewe, nikiwa naelea kwenye giza.
Sehemu Ya 7
Sikujua nimekaa kwenye hali ile kwa muda gani lakini nilikuja kurejewa na fahamu zangu za kawaida na kugundua kuwa kumbe baba alikuwa ameingia chumbani kwangu na kusimama kwa muda mrefu akinitazama.
Nilishtuka na kujifikicha macho nikiwa siamini nilichokuwa nakiona mbele yangu. Sikujua baba alisimama pale kwa muda gani kwani hata wakati anaingia sikumsikia wala sikuhisi kitu chochote.
“Umeanza kuwa mchawi siyo? Kwa nini unawanga ndani ya nyumba yangu?”
“Baba mimi siyo mchawi, nilikuwa nafanya ‘meditation’, tumejifunza shuleni kuwa inasaidia kutuliza akili na kuijengea akili ya kufanya maamuzi sahihi na kufanya chochote tunachokiwaza kitokee.”
“Hakuna, usijifanye unajua kugeuzageuza maneno, haiwezekani nisimame kwa zaidi ya dakika ishirini hapa mbele yako bila kugundua kuwa kuna mtu anakutazama, ulikuwa unawanga na leo nitakufunza adabu,” alisema baba huku uso wake ukiwa umefura kwa hasira, alininyanyua kutoka pale sakafuni nilipokuwa nimekaa, akanibeba juujuu mpaka sebuleni.
Alinishika mikono yote miwili kwa kutumia mkono wake mmoja, nikamuona akifungua mkanda wa ngozi aliokuwa amevalia suruali yake, akaanza kunicharaza mwili mzima bila huruma.
Nililia kwa uchungu sana kwani niliona ananionea, sikuona kama kuna kosa lolote mimi kujifunza kufanya meditation kwani nilisoma kwenye kila kitabu kuwa huko ulaya elimu ile hufundishwa kwenye madarasa rasmi tofauti na hapa Tanzania.
Wakati anaendelea kunichapa, ili kujitetea nilimtishia kuwa akiendelea kuniadhibu nitatoa siri ya nilichokiona siku wakati tunahama kutoka kule kijijini Itete, nilivyomfuma akiwa na zana za kiganga chumbani kwake na jinsi alivyowadanganya watu kuwa amemponya Sinai ulemavu wakati tangu awali hakuwa na tatizo lolote.
Niliposema vile, baba aliniachia na kunipiga teke kwa nguvu, nikaenda kujigonga ukutani na kuanguka chini, nikasimama na kukimbilia nje huku nikichechemea mguu mmoja. Nililia sana siku ile mpaka macho yakabadilika rangi na kuwa mekundu kama nimemwagiwa pilipili.
Mama aliyekuwa ameenda sokoni kutafuta mboga, alirudi na kunikuta nikiwa nimekaa karibu na barabara ya kuingilia pale nyumbani, huku nikiwa naendelea kulia kwa kwikwi, mwilini nikiwa na alama nyingi za mikanda niliyochapwa na baba.
“Hee! Umepatwa na nini mwanangu,” aliniuliza mama huku akionekana kushtuka kutokana na hali aliyonikuta nayo. Sikumjibu kitu, kitendo cha kuniuliza kikawa ni kama kimeniongezea hasira na uchungu ndani ya moyo wangu, nikawa nalia kwa kwikwi huku nikijitoa kwenye mikono ya mama.
Alinibembeleza na kunikumbatia kwa upendo, akanishika mkono na kuelekea ndani, tukamkuta baba akiwa amesimama mlangoni.
“Huyo mwanao siku hizi anajifunza uchawi, nimemfuma kwa macho yangu akiwanga ndani ya chumba chake ndiyo nimemuadhibu,” alisema baba huku akionekana bado ana hasira na mimi.
“Muongo, yeye ndiyo mchawi,” nilisema huku nikiendelea kulia kwa kwikwi, baba akawa anataka kuja kuniongeza lakini mama alimzuia, wakaanza kujibizana wenyewe kwa wenyewe.
“Hata kama amefanya makosa ndiyo uniumizea mwanangu kiasi hiki? Cheki alivyovimba! Kwa nini unakuwa mkatili kiasi hicho mume wangu,” alisema mama huku na yeye akianza kulengwalenga na machozi.
Baba alishindwa cha kujibu, akaingia ndani na kutuacha tukiwa pale mlangoni na mama.
“Kwani baba yako amekukuta ukiwa unafanya nini?”
“Nilikuwa nafanya ‘meditation’,” nilimjibu mama, akanitazama kwa macho ya udadisi.
“Meditation ndiyo nini? Wewe nani kakufundisha?” aliniuliza, nikaanza kumfafanulia. Mama alionesha kutoridhishwa na majibu yangu, akaniambia nikitulia nitamueleza kwa kina. Akapasha maji ya moto na kuanza kunikanda mwili mzima. Nilikuwa nikisikia maumivu makali sana.
“Huyu mtoto tukiendelea kukaa naye hapa atatuletea matatizo makubwa sana, inabidi tumhamishie kwa baba yake mkubwa jijini Dar es Salaam.”
“Hapana mume wangu, huko ndiyo atazidi kuharibika, inabidi tubaki naye hapahapa ili tumdhibiti vizuri.”
“Hapana, nimeshasema lazima tumhamishie Dar, kwanza ameanza kutishia kuwa atatoa siri kwa waumini wangu kuhusu huduma hii ya maombezi na uponyaji.”
“Mh! Makubwa, lakini na wewe unazidi kuwa mkali kwa watoto mpaka inafikia hatua wanakuogopa kama simba, jirekebishe mume wangu, hawa wameshakuwa wakubwa sasa,” mama alikuwa akijadiliana na baba chumbani kwao.
Nilikuwa nimelala kwenye kochi huku nikiendelea kuugulia maumivu makali niliyokuwa nayahisi, nikawa nasikia kila kitu walichokuwa wanakizungumza.
Japokuwa mama alikuwa akipinga suala la mimi kupelekwa Dar, kimoyomoyo nilifurahi sana kwani ndani ya kile kitabu, kuna sehemu nilisomakuwa kuna vituo vingi jijini Dar es Salaam vinavyofundisha elimu ya utambuzi, nikaona hiyo ndiyo fursa pekee ya kujua mambo mengi niliyokuwa na hamu ya kuyajua.
Walijadilianakwa muda mrefu sana, baadaye nikamsikia mama akikubaliana na wazo la mimi kuhamishiwa jijini Dar kwenda kuishi na baba mkubwa ambaye alizaliwa tumbo moja na baba, akiwa ni mfanyakazi wa Mamlaka ya Bandari. Niliwahi kumsikia mama akisema kuwa baba mkubwa anaishi Kimara Kona, karibu na ofisi za FAJI (Familia ya Jitambue).
Nikiwa kule chumbani, niliamka na kuanza kurukaruka kwa furaha baada ya kupata uhakika kuwa siku chache zijazo nitahamia jijini Dar es Salaam. Pamoja na ujanja wangu wote, sikuwahi kufika Dar hata siku moja, nikaona huo ndiyo wakati muafaka wa kujifuta matongotongo kwenye macho yangu.
Kulipopambazuka, mama aliwahi kuja chumbani kwangu kunijulia hali kwani nililala nikiwa na maumivu makali baada ya kuadhibiwa vikali na baba.
“Umeamkaje baba,” aliniuliza mama huku akinishika shavuni kwa upole.
“Nimeamka salama mama, leo najisikia ahueni, siyo kama jana.”
“Pole mwanangu, utapona kabisa wala usijali, enhee niambie vizuri kuhusu ile sijui nini huko uliyokutwa unaifanya na baba yako jana.”
“Meditation?”
“Eeeh, hiyohiyo,” alisema mama huku akikaa vizuri kitandani kwangu, akawa ananipapasa kwenye majeraha yangu niliyoyapata baada ya kupigwa na mama.
Nilichompendea mama yangu, tofauti na baba, alikuwa akituonesha upendo wa dhati kiasi kwamba mambo yetu mengi tulikuwa tukimwambia yeye. Alikuwa mpole, mkarimu na msikivu kwetu ndiyo maana hata aliponihoji kuhusu meditation, sikuona ubaya wowote kumueleza.
“Kwa Kiswahili inaitwa tahajudi, ni kitendo kinacholeta usawaziko kati ya mwili, akili na roho. Huyafanya mawazo yatulie kabisa na hivyo kutoa nafasi kwa mwili usioonekana au roho kuinuka na kupaa kwenda kwenye ukamilifu wa kibinadamu,” nilimwambia mama.
“We mtoto, hayo mambo umeyajulia wapi? Mbona unajua vitu vikubwa kuliko umri wako? Mimi pamoja na umri wangu mkubwa ndiyo kwanza hayo mambo nayasikia kwa mara ya kwanza kutoka kwako,” alisema mama huku akikaa vizuri. Maelezo yangu kuhusu meditation yalimshangaza sana.
“Nimejifunza mwenyewe mama, kile kitabu ambacho baba alikichana ndiyo kilikuwa na mambo yote hayo.”
“Sasa baba yako na yeye angekuwa anayajua mambo haya si yangemsaidia sana kwenye kazi zake za uchungaji kuliko kutumia tunguri?” alisema mama, nikaendelea kumuelezea faida za tahajudi kama nilivyozisoma kwenye kile kitabu. Baada ya kuongea kwa muda mrefu na mama, aliniomba na yeye nimfundishe namna ya kufanya meditation.
Niliamka pale kitandani na kuchukua jamvi, nikatandika chini na kumwambia mama akae kama mimi nilivyokuwa nimekaa. Akakunja miguu na kukaa kama wafanyavyo waumini wanapokuwa kwenye ibada, mkao ambao wengine huuita ‘atahiyatu’.
Nilimwambia aiunganishe mikono yake kwa kupishanisha vidole vya mkono wa kushoto na wa kulia, nikamwelekeza kuyatuliza mawazo yake na kuhakikisha akili yake inafikiria jambo moja tu, pumzi alizokuwa anazivuta na kuzitoa. Alinielewa haraka kuliko nilivyofikiria, tukatulia kimya, muda mfupi baadaye kila mmoja akawa ameshachukuliwa kiakili na meditation.
Mimi ndiyo nilikuwa wa kwanza kurejewa na fahamu, nikasimama na kujinyoosha miguu ambayo ilikuwa inauma kutokana na kukaa kwa muda mrefu. Nikamtingisha mama taratibu, na yeye akazinduka lakini tofauti yake, yeye alishtuka sana wakati akirejewa na fahamu zake. Almanusra aanguke, nikawahi kumshika na kumkalisha vizuri.
“Heee! We mtoto mbona una miujiza kiasi hiki? Yaani nilikuwa naelea angani kama nyota au mwezi, sijawahi kuihisi hali kama hii tangu nizaliwe. Nilikuwa sijielewi kama nipo macho au nimelala, nimeshindwa kutofautisha kama hizi zilikuwa ni ndoto au maono, mbona maajabu?” alisema mama huku akisimama na kujinyoosha miguu.
Nikaendelea kumfafanulia kuwa ukiwa katika hali ile, roho ndiyo inayochukua nafasi ya mwili, nikamwambia kuwa hata vitabu vya dini vinaeleza kuwa mtu anapokufa, roho huwa inauacha mwili kama ilivyotokea tukiwa kwenye meditation.
“Lakini mwanangu, mbona nasikia kuwa haya mambo yanahusiana na dini ya shetani?”
“Mimi pia nimewahi kusikia hivyo kabla sijaamua kuutafuta ukweli lakini naona kama mambo ni tofauti. Hakuna cha dini ya shetani wala nini.”
“Unataka kusema duniani hakuna dini ya shetani?”
“Dini zote zinaamini kuhusu uwepo wa Mungu mmoja, hata jamii ya wajenzi huru nao wanaamini katika Mungu mmoja na siyo shetani kama watu wanavyoaminishwa uongo.”
“Mh! Mungu gani anayeruhusu watu kuwatoa wengine kafara? Mbona nasikia wajenzi huru huwa wanatoa kafara za damu?”
“Hakuna kitu kama hicho, hizo ni propaganda zilizopandikizwa na watu waliokuwa na masilahi yao binafsi, sijasoma sehemu yoyote inayoonesha kuwa wajenzi huru huwa wanatoa kafara za binadamu, ila kwenye Kitabu cha Mwanzo kwenye Biblia kuna sehemu inasema Ibrahim, baba wa imani aliambiwa na Mungu amtoe kafara mwanaye Isaka, sasa sijui uhusiano wake ni upi?”
“Biblia inatufundisha kuwa watu wa zamani walikuwa wanatoa kafara kwa Mungu kama ishara ya shukrani na kipimo cha imani lakini tangu kuja kwa mwana wa Adam, mambo yote yamebadilika kwani yeye alifunua mapazia ya mbingu na kumfanya binadamu awe na mawasiliano ya moja kwa moja na muumba wake.”
“Sasa mama, hivi…” nilitaka kumuuliza mama swali lakini akanikatisha.
“Sitaki maswali yako magumu, ngoja nikaandae chai, baba yako akirudi atataka akute kila kitu kipo tayari. Halafu nilitaka kusahau, wiki ijayo tutakusafirisha kwenda Dar kwa baba yako mkubwa, utasoma hukohuko mpaka umalize darasa la saba,” alisema mama na kufungua mlango, akatoka na kuniacha nikichekacheka mwenyewe kama mwendawazimu.
Hamu ya safari ilizidi kunijaa kiasi kwamba niliona siku haziendi haraka. Kila siku nilikuwa nikiwaza juu ya kufika Dar es Salaam, jiji ambalo nilikuwa nikizisikia sifa zake. Niliendelea kufanya maandalizi madogomadogo kama kufua nguo zangu na kuzinyoosha kisha kuzihifadhi kwenye begi.
Siku zilizidi kusonga mbele na hatimaye safari ikawadia. Japokuwa sikuwahi kufika Dar es Salaam kabla, baba aliniambia nitasafiri peke yangu na nikifika Ubungo, nitamkuta baba mkubwa ananisubiri. Aliniandikia namba zake za simu kwenye kikaratasi na kunipa maelekezo muhimu. Alfajiri na mapema wakanisindikiza mpaka stendi.
“Kuwa makini mwanangu, ukifika utulie na umsikilize baba yako mkubwa na mkewe, usithubutu kuonesha dharau wala utundu wa aina yoyote, sawa mwanangu?”
“Sawa mama, nimekusikia na nakuahidi kuwa mtiifu kwa siku zote.”
“Na tabia zako za kishetanishetani uziache, nitakuwa nampigia simu baba yako mkubwa mara kwa mara, kama hutaacha mambo yako nitajua cha kukufanya,” alidakia baba na kuingilia mazungumzo yangu na mama. Ilibidi tunyamaze kimya, baba akaendelea kuongea huku akiweka msisitizo juu ya mimi kuachana kabisa na kile alichokiita dini ya shetani.
Kimoyomoyo nilijisemea kuwa lazima nifahamu mambo mengi kuhusu elimu ya utambuzi na kuutafuta ukweli kama hicho kinachoitwa dini ya shetani kinahusiana na shetani kweli au ni propaganda za kuwachanganya watu akili.
Sehemu Ya Tatu 8
Baada ya muda niliianza safari. Kwa jinsi nilivyokuwa nimemzoea mama, nilijikuta machozi yakinitoka wakati akinipungia mkono wa kwa heri. Nilijisikia vibaya sana kwenda kuishi mbali naye kutokana na jinsi nilivyokuwa nampenda lakini kwa sababu ilikuwa ni lazima niondoke, sikuwa na la kufanya.
Basi liliianza safari kutoka jijini Mbeya alfajiri na mapema, tukasafiri kwa saa nyingi barabarani tukiyapita maeneo kama Makambako, Ipogolo, Ilula, Mikumi, Morogoro, Chalinze na hatimaye tukaanza kuingia jijini Dar es Salaam.
“Mbezi! Mbezi wakushuka,” nilimsikia kondakta wa gari akisema, nikajua tayari tumeanza kuwasili jijini Dar es Salaam. Baadhi ya abiria wakasimama na kuanza kujiandaa kuteremka. Nilipotazama pembeni, niliona watu wengi na magari yakipishana kwa kasi, nikawa nashangaa kwani kila kitu kilikuwa kigeni kwangu.
Sikuzoea pilikapilika za mjini, nikawa nashangaa kila kitu. Tuliendelea na safari, gari likawa linaenda taratibu kutokana na msongamano mkubwa wa magari. Nakumbuka miongoni mwa vitu nilivyokuwa navisikia sana kuhusu Jiji la Dar es Salaam, ni foleni kubwa barabarani ambayo sasa nilikuwa nikiishuhudia kwa macho yangu.
Kulikuwa na magari mengi barabarani kiasi cha kufanya tuchukue zaidi ya dakika arobaini kutoka Mbezi mpaka kwenye taa za kuongozea magari za Ubungo. Tulipofika hapo, gari lilisimama kwa muda, kwa kuwa niliwasikia watu wakisema kuwa hapo ndiyo Ubungo, nilichukua begi langu na kutaka kuteremka lakini kondakta akaniambia nisubiri mpaka tuingie stendi.
Hatimaye basi nililokuwa nimepanda likaingia kwenye stendi ya Ubungo na kusimama. Abiria wote wakaanza kuteremka, na mimi nikachukua begi langu na kuteremka. Kwa bahati nzuri kumbe baba mkubwa alikuwa tayari amewasili pale stendi akiwa na mkewe na mwanaye mmoja wa kike, nilipoanza kushuka tu, nikamsikia akiniita jina langu.
Nilifurahi sana kwani tayari nilishaanza kuchanganyikiwa, nikiwa sijui nielekee wapi. Walinipokea kwa furaha, tukakumbatiana na kusalimiana. Wakanipokea mzigo na kuniongoza mpaka nje ya stendi ambapo tulipanda teksi na safari ya kuelekea Kimara Kona alikokuwa anaishi baba mkubwa ikaanza.
“Tulizungumza mambo mengi kwenye gari, wakawa wananiuliza hali za wazazi na ndugu zangu wengine niliowaacha Tukuyu. Niliwajibu kuwa wote wapo salama na wanawasalimia sana. Baada ya muda, tulikuwa tayari tumefika Kimara, dereva akasimamisha taksi kisha tukateremka. Wenyeji wangu wakaniongoza mpaka nyumbani.
“Karibu sana, hapa ndiyo tunapoishi,” alisema baba mkubwa wakati akifungua geti, tukaingia ndani huku nikiwa na furaha tele ndani ya moyo wangu. Nilifurahi sana kufika Dar es Salaam. Kesho yake, baba mkubwa alienda kunitembeza mjini, akanipeleka Posta, tukaenda mpaka Feri na kuvuka ng’ambo ya pili, Kigamboni kwa kutumia kivuko.
Tulirudi na tukaelekea Kariakoo.
Kila kitu kilikuwa kigeni kwangu, kuanzia wingi wa watu, magari, maghorofa marefu na kila aina ya mambo ya kuvutia.
“Kumbe ndiyo maana wanasemaga mjini kuzuri, cheki maghorofa?” nilijisemea kimoyomoyo tukiwa tunakaribia Kariakoo. Tulipofika baba mkubwa alininunulia zawadi ndogondogo kisha tukaondoka. Akanipeleka mpaka Manzese, tukapanda mpaka kwenye daraja maarufu ambalo nilikuwa nalisikia sana nikiwa nyumbani Tukuyu.
“Na mimi nataka kupiga picha juu ya daraja,” nilimwambia baba mkubwa ambaye bila hiyana alimuita mpigapicha, tukapiga kadhaa. Nilipanga kwenda kuwaringishia wenzangu nikirudi Tukuyu kwani hakuna aliyewahi kufika Dar es Salaam zaidi yangu. Baadaye tulirudi mpaka nyumbani.
Tukiwa tumekaribia, nililiona jengo moja lililokuwa na maandishi ukutani yaliyosomeka FAJI. Kumbukumbu zangu zikarudi kwenye kile kitabu changu, nikakumbuka kuwa kilielekeza kuwa Kimara Kona kuna sehemu panaitwa Familia ya Jitambue au kwa kifupi FAJI ambapo elimu ya utambuzi inatolewa.
Nikashusha pumzi ndefu huku kimoyomoyo nikichekelea kwani kile nilichokuwa nakitaka sasa kilikuwa kimekaribia kutimia. Nilipaangalia vizuri kwa lengo la kukariri uelekeo ili nisipotee hata nikirudi peke yangu. Kwa kuwa haikuwa mbali sana na nyumbani kwa baba mkubwa, niliishika ramani vizuri.
Siku kadhaa baadaye, jioni niliaga nyumbani kuwa naenda kunyoosha miguu. Kwa kuwa tayari nilikuwa nimeanza kufahamu sehemu mbalimbali, niliruhusiwa, nikaelekea moja kwa moja pale kwenye jengo la FAJI, nikaenda mapokezi na kupokelewa na mwanamke mmoja wa makamo, akawa ananiuliza anisaidie nini.
“Nataka kuonana na mwalimu wa Utambuzi aitwaye Munga,” nilisema huku nikiwa sina uhakika na nilichokuwa nakiulizia. Sikumfahamu Munga ila kupitia kile kitabu nilichokuwa nimenunua, nilisoma kuwa mwalimu wa masomo ya utambuzi katika kituo hicho alikuwa akitambulika kwa jina hilo.
Mwanamke yule wa makamo aliyekuwa amekaa juu ya meza kubwa pale mapokezi, alinitazama kwa muda halafu ukimya ukatanda kwa sekunde kadhaa. Nilipomtazama machoni, niligundua kuwa alikuwa akitokwa na machozi. Sikuelewa sababu za kumfanya atokwe na machozi wakati nilimuuliza kistaarabu.
“Ma’mdogo mbona unalia? Kwani kuna nini?” nilimuuliza huku nikianza kuingiwa na wasiwasi mkubwa ndani ya moyo wangu. Alinitazama tena, badala ya kunijibu akaniuliza natokea wapi?
“Natokea Tukuyu, nimekuja kuishi kwa baba mkubwa, anakaa hapo mtaa wa pili,” nilimjibu, akaniambia kuwa Munga alishafariki dunia miezi kadhaa iliyopita. Nilishusha pumzi ndefu nikiwa siamini kile nilichokisikia.
“Amefariki?” niliuliza tena huku machozi yakianza kunilengalenga, nilisogea pembeni mpaka kwenye benchi, nikakaa huku mwili ukiwa umeniishia nguvu kabisa. Niliona kama safari yangu ya kutaka kufahamu mambo mengi kuhusu elimu ya utambuzi ilikuwa imefikia mwisho.
Nikiwa katika hali ile, mwanaume mmoja wa makamo aliyekuwa na mvi kichwa kizima, begani akiwa amebeba begi dogo, aliwasili. Akavua viatu nje na kuingia mpaka pale ndani, akanisabahi kwa uchangamfu kama tuliyekuwa tunajuana naye kwa siku nyingi, akaenda kumsabahi na yule mama wa makamo kisha akarudi na kukaa karibu yangu.
“Bila shaka wewe ni mgeni hapa,” aliniuliza, nikatingisha kichwa kama ishara ya kumkubalia. Akaniuliza kuwa uso wangu ulionesha kuwa nina majonzi, ni jambo gani lilikuwa linanisumbua? Kabla sijamjibu, yule mama wa mapokezi alidakia na kumweleza kuwa nilienda pale kumuulizia Munga, nilipopewa taarifa juu ya kifo chake ndiyo nikawa kwenye hali ile.
“Usijali, kama Munga hayupo wapo wengine wanaoweza kukusaidia ulichokuwa unakitaka, pengine kwa kiwango cha juu kuliko hata huyo Munga. Pia inawezekana unasikitika kwa sababu huelewi tafsiri ya kifo,” alisema yule mzee ambaye baadaye nilikuja kumtambua kuwa anaitwa Mhagama.
Angalau moyo wangu ulitulia, nikainua kichwa changu na kuanza kumtazama, akanipigapiga mgongoni kama ishara ya kunifariji, kisha akaanza kuniuliza juu ya historia yangu na asili yangu. Nilimjibu kuwa nimetokea Tukuyu, nikamweleza kuhusu familia yetu, kwamba baba yangu ni mchungaji na kumweleza jambo lililonipeleka pale.
“Unataka kujua kuhusu nini hasa?”
“Nataka kujitambua, nataka kujua kuhusu mimi na dunia ninayoishi. Nataka kujua uhusiano kati ya maumbile na ulimwengu,” nilimjibu, akanitazama kwa makini usoni kama anayejiuliza ‘utaweza kweli?’.
“Basi hakuna shaka, hapa ndiyo umefika, naamini kila unachohitaji kukijua utakipata, cha msingi ni uvumilivu wako na juhudi kwenye masomo,” aliniambia, nikamuomba anifafanulie kuwa kuna masomo ya aina gani yaliyokuwa yanafundishwa pale.
“Kuna madarasa mengi ya utambuzi, wanaoanza kuna darasa lao, wale wanaofahamu kidogo kuna darasa lao lingine na wale waliofuzu kuna darasa lao pia. Kuna madarasa ya meditation kulingana na ngazi kama ilivyo kwenye masomo ya utambuzi, naamini utafurahia,” alisema Mhagama huku akinitazama kwa furaha.
Baada ya maelezo yale, aliniambia kuwa nilikuwa nimefika siku muafaka kwani kulikuwa na mafunzo siku hiyo, akaniambia baada ya muda wanafunzi wengine wataanza kuwasili eneo lile.
Kweli baada ya muda, niliona watu mbalimbali wakiwasili eneo lile, vijana kwa wazee, wanaume kwa wanawake, wakawa wananisabahi kwa uchangamfu. Kitu nilichojifunza mapema ni kwamba wanafamilia wa Jitambue walikuwa na upendo mkubwa sana ndani ya mioyo yao. Kila aliyekuwa akinipita alikuwa akinisabahi kwa uchangamfu licha ya umri wangu mdogo, nikajihisi kama nipo nyumbani.
“Hata wewe ukianza kusoma masomo ya utambuzi, utajikuta taratibu ukianza kuwapenda binadamu wenzako na kuondoa roho za chuki, visasi, wivu na kuwawazia wengine mabaya. Hapa tunafundishana namna ya kuishi kama ambavyo Mungu alikusudia binadamu tuishi,” alisema Mhagama, nikashangaa kumsikia akimtaja Mungu.
“Mbona watu wanasema wanaojifunza utambuzi wanajifunza kumwabudu shetani?” nilimuuliza kwa shauku, akanitazama usoni na kuniambia kwa mafumbo: “Huwezi kuujua mti mpaka wewe mwenyewe utakapoamua kuwa mti.”
Nilitafakari maana ya fumbo lile lakini sikupata majibu, akaendelea kuniambia kuwa kuna falsafa na propaganda nyingi sana zinazoenezwa juu ya watu wanaoutafuta ukweli, akaniambia niwe makini na nielekeze nguvu zangu zote kwenye kuusaka ukweli badala ya kusikiliza maneno ya watu.
Baada ya kuniambia hivyo, tayari watu wengi walikuwa wameshaingia ndani ya jengo hilo, akanishika mkono na kuniambia nimfuate. Nilifanya kama alivyonielekeza, tukaongozana mpaka kwenye chumba maalum kilichokuwa upande wa kulia wa jengo lile.
Tukaingia na kukaa kwenye jamvi kama wenzetu tuliowakuta, majadiliano yakawa yanaendelea. Kuna hoja ilitolewa juu ya vyakula ambavyo binadamu anapaswa kula ili awe na afya njema ya akili na roho, watu mbalimbali wakawa wanachangia.
“Binadamu tuliumbwa kula mbogamboga, nafaka na matunda ndiyo maana hata mpangilio wetu wa meno (dental formula) ni tofauti na wanyama wanaokula nyama,” alisema mjumbe mmoja, mwingine akaunga mkono hoja ile.
“Ni makosa sana kuendekeza kula vyakula kama nyama nyekundu, vyakula vya kwenye makopo na vinywaji vyenye kemikali, maisha ya binadamu siku hizi yamekuwa mafupi, yaliyotawaliwa na magonjwa mengi kwa sababu tunaishi kinyume na Mungu alivyokusudia alipotuleta duniani.”
Nilivutiwa sana na mada ile, nikawa nasikiliza kwa makini. Baada ya kumaliza majadiliano, lilifuata zoezi la kufanya meditation kwa pamoja.
Hakuna kitu nilichokuwa nakisubiri kwa hamu kama muda huo wa kufanya meditation ya pamoja. Lengo langu lilikuwa ni kujifunza kama ninavyofanya meditation mwenyewe huwa napatia au nakosea, nikawa nasubiri kwa hamu kuwaona watu walionizidi umri na uzoefu wakifanya.
Tulielekezwa kukaa kwenye jamvi kwa mfumo wa duara, katikati pakawekwa mshumaa mkubwa uliokuwa unawaka. Tukaelekezwa kuwa siku hiyo tutafanya meditation ya mshumaa, kila mmoja akakaa vizuri tayari kwa kuanza.
Niliposikia kuna meditation ya mshumaa, shauku ndani ya moyo wangu iliongezeka maradufu, nikawa nasubiri nione inavyofanywa.
INAENDELEA

