Naolewa Na Nani?
MIAKA 33; Naolewa na nani? Nimekaa na Mwanaume kwa amiaka 4 alinipaelaka mpaka kwake kumbe ni Mume wa mtu!
Siku ya kwanza kwenda kwake, alichukua viatu vyangu na kuviingiza ndani. Nilimuuliza kwa nini anaingiza ndani wakati nyumba ina geti, akaniambia hapana, majirani wa hapa wambea sana, sitaki watu wajue mambo yangu. Ilikuwa nyumba kubwa yenye apartments tatu, ni kama nyumba tatu ndani ya uzio mmoja na kila mtu alikuwa na maisha yake.
Nilipata wasiwasi zaidi ambapo hakutaka hata nitoke nje. Kila kitu tulikifanya ndani, nikimuuliza kwanini hutaki nitoke, ananiambia majirani wambea, sitaki wajue mambo yangu. Nikawa nawaza, mtu mzima miaka 38 bado unahofia majirani, lakini sikutaka kumuuliza sana kwani sikutaka kumuudhi. Hata hiyo kunipeleka kwake nililalamika sana. Nyumba ilikuwa kubwa, ina vyumba vitatu vya kulala, sebule, na jiko. Ukiangalia jioni, lilionekana jiko la kike. Nikisema la kike, naamanisha vitu vyote vimepangwa vizuri, kuna karibu kila kitu, yaani mpaka kibao cha kukunia nazi. Kwenye friji kulikuwa na nyanya, karoti na kila kitu, ila hakutaka nipike.
Tuliingia kwenye chumba kimoja ambacho self. Akaniambia ndio chumba chake. Nilimuuliza mbona hutaki niingie vyumba vingine, akakasirika na kuniambia, “Mbona unanichunguza sana? Kama huniamini, unafanya nini hapa!” Kwa kweli, ili nisimuudhi, nilijikuta nakaa kimya, sikumuuliza tena. Akaniambia kuna mdogo wake wa kike huwa anaishi naye na mtoto, ndiyo sababu hakutaka niende kwake.
Hapo moyo ulitulia kidogo, ila saa kumi na moja alfajiri aliniamsha, akaniambia yeye anaenda kazini sijui kapigiwa na bosi wake. Nikamuambia basi ukirudi utanikuta, akaniambia hapana, siwezi kukuacha humu. Mimi naomba tu uondoke nitakuja kukuchukua siku nyingine. Alijaribu kujieleza sana, nilipogoma kuondoka nilimuona anabadilika, akawa mkali na kuanza kulalamika, “Ndiyo maana sitaki kuleta wanawake ndani, hawaheshimu watu, unataka kung’ang’ania nini!”
Aliongea mambo mengi, mwisho nikasema huyu hanitaki. Nikaamua kukubali nikaondoka zangu. Alinipeleka mpaka kwangu na tangu siku hiyo hakunipeleka kwake tena. Miaka 4 ya mahusiano nikiongelea mambo ya Kwenda kwake, akawa ananiambia, “Sijui mama yangu kaja,” ama, “Sijui kuna wadogo zangu, subiri waondoke,” yaani kila siku ni kitu kipya.
Siku moja nilikuwa na rafiki yangu, tumekaa sehemu tunakula, ghafla mpenzi wangu akapita. Hakujua niko pale, kuna watu alikuwa nao, kabla sijaongea chochote rafiki yangu akaanza kuongea, “Huyu naye kaja kufanya nini huku? Mbona ni kama ananifuatilia kila sehemu, hana haya wanaume, mtu ana mke wake lakini akikutongoza anajifanya anakupenda sana!”
Nilishtuka kidogo ila sikumuonyesha, nikamuuliza unamzungumzia nani? Akaniambia, “Si yule kaka wa (akataja kampuni anayofanya kazi), tuko jengo moja, ofisi moja na mke wake yuko pale pale. Lakini anajifanya yeye na mke wake hawako vizuri wakati dada wa watu anajiheshimu na ni mtu poa sana. Asubuhi wanaletana kazini lakini jioni anakuja kutongoza kama vile hajaoa.”
Aliongea mambo mengi, mimi nilikaa kimya nikijifanya kama vile sijui, ila huku mwili ulikuwa unatetemeka, jasho linanitoka, nahisi presha inapanda. Kila nikiwaza mipango niliyokuwa nayo na huyo mwanaume, kila nikikumbuka idadi ya wanaume ambao niliwakataa kwa ajili yake, kila nikifikiria miaka zaidi ya 4 niliyo naye, nilikutana naye nikiwa na miaka 29, sasa nina miaka 33, anazungumzia mambo ya kuachana.
Kila nikifikiria, alishawahi kuniambia niongee na Mama yangu kumuulizia taratibu za kwetu, kwa kweli nilihisi kuchanganyikiwa. “Una uhakika huyo kaka kaoa?” Nilijikuta naropoka, akashtuka na kuniuliza kwa nini unamjua? Nikamuambia, “Ndiyo, kuna rafiki yangu ana mahusiano naye.” Niliogopa hata kumuambia ni mimi!
“Kaoa tena ana ndoa ya kanisani!” Nilishtuka zaidi kujua kuwa yule mwanaume ni Mkristo, na ndoa ya kanisani, kumbe ni Muislamu. Akacheka na kuniuliza, “Kwa vile umesikia anaitwa Musa, ndiyo ukadhani ni Muislamu? Yule mbona Mu-RC, tunasali kanisa moja.”
Hamu yote ya kukaa iliisha, nilichukua simu na kujipigia. Nikajifanya kupokea, nikamuambia, “Baby nakuja,” nikajifanya nimeitwa na mpenzi wangu. Nikaondoka, rafiki yangu anajua nina mpenzi lakini kwa kuwa si rafiki wa karibu hivyo, basi hajui mambo yangu ya ndani. Nilitoka pale na kujaribu kumpigia simu mwanaume, lakini hakupokea. Nilimtumia meseji, “Ninajua kila kitu najau umeoea tena ndoa ya kanisani.” Nikatuma na nyingine, “Naomba tuzungumze,” lakini hakujibu.
Huwezi amini mwanaume hakunitafuta tena. Nilijaribu kumpigia simu hakupokea zaidi ya wiki mbili. Kuna siku nikaenda kumfuata kazini kwake, bila aibu akanigeuzia kibao, akaniambia, “Nimekuacha kwa sababu huna subira, unaskiliza maneno ya watu. Nilioa kweli, lakini mimi na mke wangu hatuko vizuri. Nilitaka nimuache lakini sitamuacha tena.”
Nilitamani hata kumfuata mke wake kufanya vurugu, lakini nikajiambia utajidhalilisha tu, acha mwenzako ana mke na maisha yake, wewe utaonekana kama yule dada anayegombania wanaume. Ingawa inauma sana lakini nimekubali kuachika. Nimeamua, miaka 33, sijui hata kama nitaweza kupata mtu mwingine wa kunioa, nawauchukia sana wanaume!

