BINTI USIZAE KABLA HUJAOLEWA, UWEZEKANO WA MWANAUME KUKUACHA NI MKUBWA MNO
Habari kaka, leo nimeguswa kuzungumza jambo , naomba upost pengine kuna mtu atajifunza kupitia mimi. Iko hivi kipindi nasoma chuo nilikutana na kijana mmoja ambae nilimuamini kwa haraka sana ni kijana mpole kwa muonekano basi tukawa marafiki na haikuchukua muda tukaingia kwenye mahusiano.
Mwanzoni mwa mahusiano aliniambia kuwa hatumii kilevi chochote, na alijifanya ni mtu mwenye hofu ya Mungu sana ( nadhani aliona kuwa mimi pia nipo hivyo ) basi nikamuamini …kadili siku zilivyokuwa zinaendelea nilianza kuona tabia zake halisi , kwanza alikuwa na mtoto na alinificha nilipogundua hilo nilikasirika , si kwa sababu ya kuwa na mtoto ni kwasababu ya kunificha hilo basi baadae yakaisha tukaendelea ya mahusiano , lakini nikaja kugundua ni mlevi wa kupindukia . lakini pia ni mtu wa wanawake mno yaaani hachagui habagui . Niliambia nafsi yangu kuwa mtu huyu hakufai bila kumwambia chochote nikawa too busy na masomo . baada ya wiki mbili nikaja gundua kuwa nina ujauzito wake na ugumu ulianzia hapo. nilipomwambia nina ujauzito yule kijana alianza kunibembeleza nitoe ujauzito kwa kusema kwamba tutapata mtoto wakati ukifika lakini mimi nilimkatalia nikamwambia siwezi kufanya unyama huo ambao utahatarisha usalama wa afya yangu . alijitahidi kuniomba sana lakini nilikataa na hapo ndipo nilianza kuona rangi zake halisi.
Aliniblock kila mahali aliblock namba zangu zote, na hata nilipomtafuta kwa namba nyingine aliponijua ni mimi aliiblock hiyo namba pia. Baadae wazazi walipata taarifa hiyo ( sikuwa nikiishi nao maana wao walikuwa mkoa mwingine na mimi nilikua mkoa mwingine nasoma). Hapo hali ndipo ilikuwa mbaya zaidi kwani wazazi pia walinitenga na kila waliponipigia ilikuwa ni kunisema na kunilaumu tu kuwa nimewaaibisha na narudisha nyuma huduma yao , walikuwa sahihi lakini kwa wakati ule yale maneno yao yalikuwa ni kama kugongea msumari wa moto kwenye kidonda ko ikafikia hatua mawasiliano na nyumbani yakakatika. Nilipitia kipindi ambacho kama sio Mungu huenda historia yangu ingeishia wakati ule.
Siku moja niliamua kwenda kwake kwa ajili ya kuzungumza nae na ndo siku tulianza kuishi wote ( ni jambo ambalo pia nalijutia sana ) nilienda sababu sikuwa na mtu mwingine anayenielewa japo yeye pia hakuwa akinihitaji lakini yeye ndio muhusika kwahiyo niliona ni bora nikae kwake lakini kwa hofu kubwa , niliogopa hata kunywa juice ambayo nimekuta anakunywa kwa kuhofia kuwekewa dawa ya kutoa ujauzito.
Alinifanyia vituko vya kila aina ili nikate tamaa na kuamua kutoa ujauzito lakini namshukuru Mungu alinipa hekima na nguvu niliweza kuishi pamoja na vituko vyake vingi … Nilifanikiwa kujifungua salama na Mungu alitujalia afya njema. Nilihisi baada ya kujifungua na kuona mtoto atabadirika lakini haikuwa hivyo mambo ndo yalikuwa mabaya zaidi. Mara kadhaa alikuwa akinifukuza kwa kunitupia vitu nje na hapo nilikuwa tayari nimeshamaliza chuo nipo tu nyumbani sina kazi wala biashara….
Baada ya kuona kila kituko amefanya na bado niko pale akashirikiana na familia yake kuanza kunitukana na kutaka nitoke basi ikawa huku ndani nafanyiwa vituko na kutoka kwa ndugu zake ni matusi na kejeri… siku moja alinitamkia kwa kinywa chake kuwa nikiendelea kung’ang’ania kukaa pale ndugu zangu watanikuta marehemu. Hapo ndipo niliona inatosha sababu mtu mwenyewe ni mlevi sana asije kunidhuru nikaacha mtoto hivyo mwanangu alivyofikisha mwaka mmoja niliondoka kwake nikaenda kupanga ..
Mungu alivyo mwema hatukuwahi kupungukiwa kitu nilianza biashara ndogo ndogo pale pale nyumbani nilipokuwa nimepanga, baadae kuna kazi nilipata ya kujitolea lakini nilikuwa nalipwa kidogo hivyo tuliendelea kuishi na mwanangu …..Na hakuna kipindi ambacho nilikuwa karibu zaidi na Mungu kama kipindi hiko na ndio kipindi ambacho nilimjua Mungu zaidi.. Lakini pia maneno yake ya kejeri kwamba mimi kwetu masikini ndio maana nilikuwa nang’ang’ania kukaa kwake yalinipa nguvu ya kupambana na kuuchukia sana umasikini ….nashukuru Mungu baadae nikapata kazi mahali pengine japo ilikuwa ya mkataba lakini ilinivusha pakubwa kwani hadi mkataba unaisha nilikuwa nimesave kiasi cha pesa hivyo nilianza biashara zangu na namshukuru Mungu nilipo sasa si kama nilivyokuwa huko nyuma na nina amani ya kutosha.
NB : 1. Mabinti usizae kabla hujaolewa , uwezekano wa mwanaume kukuacha kama hajakuoa ni mkubwa mno
2 . Lakini pia kijana usimpe mimba binti ambae huna matarajio ya kumfanya kuwa mke maumivu mnayotusababishia ni makubwa .
3. Unapopitia changamoto yeyote kuwa karibu zaidi na Mungu, atakufariji atakutia nguvu zaidi ya yote atakupa hekima ya kuweza kufanya maamuzi sahihi ili kutoka kwenye hiyo changamo na utapata amani tena , AYUBU 22: 21 ni mstari wa maisha yangu.
4. Mwanaume akishakwambia toa ujauzitoa jua kuwa hakupendi na hana nia yeyote na wewe kuendelea kumganda mtu huyo kunaweza kuharibu afya yako ya akili muhimu ni kukubali ulikosea ikatokea hiyo so ni vema kutulia na kuona namna ya kuishi pasi na kutarajia chochote kutoka kwa huyo mtu ….Ni miaka mitano sasa imepita namshukuru Mungu nina amani jamaa anamhudumia mwanae japo kwa kusukumana lakini anafanya namshukuru Mungu pia kwa hilo .

