USIWAHI KUDHARAU MTU KWA HALI YAKE YA SASA
Niliolewa na mwanamume mmoja aliyekuwa jirani yetu. Watu wote wa ukoo wake walikuwa matajiri walimiliki biashara kubwa, maduka, na nyumba za kifahari . Lakini familia yake ya karibu ilikuwa masikini sana. Hawakuwa na mali wala biashara kama ndugu zao wengine.
Mume wangu alikuwa akifanya kazi ya ulinzi kwa mmoja wa jamaa zake kwa mshahara mdogo sana haukutosha hata kwa matumizi ya wiki mbili . Cha kuhuzunisha zaidi ni kwamba ndugu zake hawakumjali kabisa. Walimchukulia kama mlinzi wa kawaida tu, si mtu wa familia
.
Siku moja aliugua na hakuweza kwenda kazini kwa siku tatu . Walikata mshahara wake. Hakulalamika. Hata hakuwaomba msaada kwa sababu wao ni wa familia yake. Aliendelea na kazi kana kwamba hakuna kilichotokea
.
Nilihisi uchungu moyoni kwa jinsi alivyodhalilika . Nilitamani aache kazi ile. Lakini alidumu nayo kwa miaka mitano tangu tufunge ndoa.
Siku moja nilihisi uchovu na maumivu yasiyo ya kawaida . Nilipogundua kuwa mjamzito, nilifurahi sana – nilikuwa nasubiri kwa miaka mingi. Nilipomwambia, alicheka kwa furaha
, lakini ghafla uso wake ukabadilika na kujaa huzuni
.
Nikamuuliza, “Mbona umebadilika uso, mpenzi wangu?”
Akanijibu, “Mtoto wetu anakuja, lakini sina hata shilingi ya kumnunulia nguo wala mahitaji yake.”
Nikamwambia, “Usijali, riziki yake italetwa na Yule anayewaruzuku ndege angani hawezi kutusahau sisi tulioko duniani.”
Maneno haya yalimfariji, akatabasamu tena.
Zilipofika siku za kujifungua, nilianza kuhisi maumivu makali sana. Mume wangu akamwita muuguzi aje nyumbani . Baada ya saa moja na nusu, muuguzi akasema haiwezekani kujifungua kawaida ni lazima nipelekwe hospitali
.
Tulikuwa hatuna hata senti. Mume wangu akaenda kutafuta msaada akarudi mikono mitupu . Nilimwambia asijisumbue, nikajifungia chumbani kimya ili watu wasisike kilio changu. Lakini maumivu yalikuwa makali mno
.
Hakuweza kunivumilia akaondoka mbio. Nikaogopa labda kaenda kwa jamaa zake kuwaomba msaada. Na kweli alivyorejea, machozi yakimtoka, nilijua wamemkataa .
Nikamwomba Mungu achukue roho yangu kuliko kuona machozi ya mume wangu aliyeumia na kufedheheka .
Muda si mrefu, hali ikatulia nikajifungua mtoto wa kike mzuri sana .
Muuguzi alisubiri malipo. Mume wangu akamwambia, “Naapa, malipo yako ni deni shingoni mwangu nitakulipa mara nitakapopata.” Muuguzi akatabasamu kwa huruma, akaondoka.
Nikamuomba mume wangu achane baadhi ya nguo zetu, tukamfunika mtoto wetu kwa vitambaa hatukuwa na hata kipande cha nguo cha mtoto .
Nilipomuuliza alikokwenda mara ya mwisho, akaniambia:
Alikwenda kazini kwa jamaa zake. Akakutana na mdogo wao, akamwomba pesa kama mkopo. Akajibiwa, “Siwezi kukusaidia nenda kwa msimamizi wa fedha.”
Msimamizi naye akasema, “Bila idhini ya mkurugenzi siwezi kutoa pesa.”
Alipotafuta mkurugenzi, akaambiwa ametoka. Akamkimbilia nje, akampigia kelele: “Subiri!” lakini hakusimama
Alirudi akiwa amevunjika moyo, mwili umelegea na machozi yanamtoka .
Nikamwambia, “Usijali, mpenzi wangu nimejifungua salama, Alhamdulillah.”
Kesho yake alikataa kurudi kazini. Akaenda sokoni kutafuta kazi. Baada ya saa nne, akarudi na vyakula vya kila aina, nguo, soksi, na mahitaji yote ya mtoto wetu . Uso wake ulimeremeta kwa furaha kama mtu aliyepata usiku wa Lailatul-Qadr
.
Nilipomuuliza alipataje kazi, akaniambia:
Alihangaika sana sokoni bila mafanikio. Kisha akakutana na rafiki wa zamani ambaye sasa ni mfanyabiashara wa mboga . Akamweleza hali yake.
Rafiki akasema kwa hasira, “La hawla! Kama ungekuja kwangu mapema, ningekupa hata roho yangu – si pesa tu.”
Akamkabidhi kalamu na daftari na kumuajiri kuandika mizigo ya wateja. Baada ya kazi, rafiki alimpeleka dukani, akanunua kila alichohitaji na kumpa pesa mfukoni.
Akamwambia, “Nitakuona kesho.”
Kesho yake, alirudi na pesa akasema, “Hii ni kwa ajili ya yule muuguzi.”
Nilipompelekea pesa, muuguzi akazikataa huku akilia .
Akasema, “Niliwaacha usiku ule nikiwa nimeacha malipo kwa ajili ya Allah. Nilijificha nisionekane nikiugua kwa uchungu wenu. Lakini niliporudi nyumbani, nilipigiwa simu hospitali niliyoomba kazi miaka minne iliyopita imeniajiri! Sasa mimi ni daktari wa uzazi!”
Nilishangaa kwa ukarimu wa Mungu alipoacha malipo kwa ajili ya Allah, Mungu akamlipa ndoto zake .
Mume wangu akaniambia tujiandae – tunahama kwenda mjini. Nikamuuliza kwa nini, akasema: “Rafiki yangu atanitumia matunda na mboga niwauzie wateja.”
Tukahamia mjini, tukaishi nyumba kubwa. Maisha yalianza kubadilika kwa neema ya Mwenyezi Mungu . Kila siku hali ilizidi kuwa nzuri.
Baada ya miaka mitatu, mume wangu alikuwa tayari mfanyabiashara mkubwa mwenye biashara yake binafsi . Na maisha yetu yakabadilika kwa subira, maombi, na rehema za Allah.
Funzo:
Subira, imani, na moyo wa kusaidiana hufungua milango ya baraka. Usiwahi kudharau mtu kwa hali yake ya sasa – hujui kesho yake. Na msaada unaotoa kwa nia njema, hurudi kwako kwa njia usiyoitarajia.
Je, wewe umejifunza nini?

