“Nilipewa Dawa ili Nirefuke” Msichana mfupi zaidi Kenya
Simulizi Ya Kweli
Chanzo: BBC
Alice Mbere mwenye umri wa miaka 27 kutoka nchini Kenya ni mtoto wa tano kati ya watoto 9 katika familia yake. Alizaliwa na kilo za kawaida lakini alipofika umri wa miaka mitano ndipo wazazi wake waligundua kuwa hana urefu wa kawaida, hapo ndipo wakaanza kutafuta ushauri kupitia madaktari tofauti.
“Nakumbuka daktari mmoja alinipa dawa ya kunywa asubuhi na jioni akisema nitarefuka, lakini dawa ziliisha na kimo changu bado kilisalia pale pale,” alisema Alice.
Alice aliendelea kutusimulia kwamba kila daktari alikua na maoni tofauti.
Wengine walisema ana matatizo ya mifupa. Mwingine alipendekeza upasuaji na kadhalika. Lakini hakuna hata mmoja aliyetoa suluhisho.
“Wazazi wangu walichoka, ilifika wakati baba yangu alisema kama kimo chake na hali yake haimuathiri wala haimdhuru basi muacheni abaki kama alivyo”
Alice ana urefu wa 85cm tu. Anajitambua kama mtu anayeishi na ulemavu. Alice ana hali inayojulikana kama short stature kwa kiingereza ama kimo kifupi. Na changamoto kubwa zaidi ilianza wakati alipoanza shule na kujiona tofauti na wengine.
Pamoja na watu kumuangalia kwa mshangao kila wakati.
“Nakumbuka nilipojiunga na shule ya upili, nilipowasili shuleni Mwalimu Mkuu alikataa nijiunge na shule hiyo, na kusema nafaa kupelekwa katika shule maalum ” Alice alinieleza.
Mwalimu mkuu wa shule hiyo alisema alice angehitaji kitanda maalum na huduma zingine maalum ambazo shule haikuwa na pesa za kukidhi mahitaji yake.
Amesema alihisi kubaguliwa na aliumia sana kwa matamshi hayo.
“Kuvunjika kwa mwiko siyo mwisho wa mapishi” Licha ya changamoto na misukosuko ya kupata elimu alijikakamua na kumaliza masomo yake, na baadae kuhitimu katika chuo kikuu cha Co-operative nchini Kenya, taaluma ya usimamizi wa wafanyikazi Human resources management.
“Changamoto ni nyingi kama mtu mfupi ama mwenye kimo kama changu, moja ni kutafuta nguo zinazonitosha”. Alice alisimulia.
Anasema hawezi kuingia katika duka la kawaida na kupata nguo kwa hivyo mara nyingi inamlazimu kuingia katika dula la watoto ili kupata mavazi yanayolingana na kimo chake.
Na mara nyingi pia nguo zake anashonesha maana ana fundi wake maalum anayemjulia vipimo vyake na kumshonea nguo zinazomtosha anapohitaji.
Hata hivyo, changamoto kubwa zaidi ya kuishi na kimo kidogo, anasema, ni kwamba kufikia mambo mengi inakuwa vigumu kwake, hasa wakati ninapojishughulisha na maisha yangu ya kila siku.
“Inakuwa vigumu kutafuta usafiri” anaeleza. Kwa sababu nahitaji kuinuliwa nikipanda gari la umma, nahitaji usaidizi katika kila kitu. Akiwa nyumbani ana kibao maalum cha kukanyaga ama kigogongo kwa kufungulia kabati, kuwenda msalani ,kupanda kitanda na mambo mengi.
Kuhusu maisha yake siku za usoni,amesema angependa kupata watoto na kwamba kwa sasa ana mchumba anayempenda mwenye kimo cha kawaida na ni mcheshi kama yeye. Anatarajia kuwa na familia yake kubwa na kwamba madaktari wamemhakikishia kuwa hilo linawezekana.
Wasia ama ushauri wake kwa watu wanaoishi na ulemavu ni kwamba watu ni tofauti na si lazima watu wafanane , kila mmoja na maisha yake. Kwa hivyo ni muhimu kujikubali na kuishi maisha ya kawaida licha ya changamoto unazopitia.