JINSI UKIMYA ULIVYONIPA NDOA
PART 11
Niliendelea kuwa kimya, hakuna aliyekuwa anajua nina fanya nini nina waza nini, au nina mpango gani Kwasasa. Wengi walinipigia simu kutaka kujua naongea nini kama zamani ila sikuwapa nafasi.
Niliendelea kuwa busy na kazi, Chuo, na ratiba zangu, nikajikuta nimepata confidence ya ajabu sana sana, yani najiamini najikubali na siogopi chochote.
Pastor alisema kila kitu kipe muda, baada ya muda utaelewa na utajua kila kitu, nikasema sawa. Basi nikaendelea kuwa kimya naendelea na maisha yangu.
Eben alienda kulipa Mahari, na siku analipa Mahari nikaona picha Mama yangu wa kambo na Dada zangu walikuwepo tena walikuwa wanacheza kwa furaha sana, na inaonyesha yule Mama Mzee wa kanisa ni shoga yake Mama yangu wa kambo maana walivaa sare, ndio nikaelewa sasa kumbe hata huu mchezo Mama pia amehusika. Nikajiambia moyoni niendelee tu kutulia.
Nikashangaa baada tu ya mahali kutolewa kesho yake asubuhi Mama yangu wa kambo akanipigia simu, akaniuliza uko wapi? Pole nasikia kijana aliyetoa mahari jana alikuwa na mahusiano na Wewe, nikamuuliza Mama kijana gani, mbona sikuelewi. Akauliza kwani hujasikia kanisani kuna uchumba, nikamwambia Mimi hata sijui niko busy na kazi na sina mahusiano na Mtu, kama ningekuwa nayo ningekwambia. Nikamuuliza nani kasema hayo maneno, Mama akabaki anahangaika aaah basi kama hujui kitu, haya. Akaniuliza unaendeleaje, nikamwambia sijambo na jumapili niko kanisani tutaonana. Mama akabaki anashangaa, haya nilijua hii issue inakuhusu nikasema usijehama kanisa. Nikamwambia hakuna cha kunihamisha kanisa jumapili utaniona uwe na Amani akasema sawa.
Nikakumbuka maneno ya Pastor Anni kuwa jifunze kuwavunja moyo adui zako, pale anapotarajia utalia Wewe cheka nikasema sawa kabisaaa, na nitawashangaza hawata amini.
Jumapili ikafika ikawa ni siku ya kuwatambulisha wachumba kanisani, nikasema siku hiyo nitaenda na hakuna kitu kitatokea. Nakumbuka nilinunua nguo mpyaa kiatu kipya High heels 👠👠, nilijipodoa vizuri tu nikapendeza. Na kufika ibadani huwezi amini nikaweka mstari mmoja na Eben alikuwa mtu wa tatu kutoka Mimi, nikasema sihami nakaa hapa hapa Leo anione.
Basi muda wa praise nilikuwa nacheza kwa step na viatu vyangu virefu weeeh yani full raha, muda wa sadaka sasa, nilisubiri watu wote wametoa Mimi nikawa wa mwisho mwisho na nikahakikisha watu wamekaa ndio Mimi nikaanza kutoka nyuma kwenda mbele kitoa sadaka. Aisee nilikuwa na muondoko wangu mmoja hivi hatari 🤣🤣 taratibu, nikatoa sadaka nikageuka kurudi namuona mtesi anatoa macho huyo, naona ananiangalia haamini.
Basi ibada ikaisha Pastor akawa anasoma matangazo Mimi nikanyanyuka huyoo kuondoka, kwahiyo muda wa kutangazwa uchumba nilikuwa nishaondoka, sikutaka shida yoyote. Niseme tu nilikuwa na amani isiyo ya kawaida, nilikuwa nina raha moyoni sana sana.
Jioni yake kulikuwa na Birthday ya rafiki yangu wa Chuo, hivyo nikawahi kurudi nyumbani nikajiandaa huyoo kwenye Birthday. Kama kawaida nikachukua video zangu na picha za kupostia watesi, na nilipendeza Bwana yani nilipendeza. Kama kawaida nikapost usiku, asubuhi naamka nacheck nakuta Eben kaview zoteee 🤣🤣, nikasema na bado utaview sana tu.
Maisha yaliendelea, nakumbuka ilikuwa mwezi wa kumi na wakapanga Ndoa yao iwe mwakani mwezi wa tisa, nikashangaa mbona wameweka Ndoa mbali hivyo, ila nikaachana nao .
Niliendelea kwenda kanisani nikiwa hivyo hivyo mkimya, mtulivu, na mnyenyekevu sana.
Niliendelea kumlilia Mungu anitendee na Mimi, nikawa naendelea na ratiba za maombi ya kufunga, kuamba shushani saa mbili na usiku kuamka kuomba na nikajikuta nina amani isiyo ya kawaida.
Kuna siku Mama alikuwa anaumwa, Bibi akanipigia simu kuwa wako hospital wanahitaji hela, Mama alikuwa ana harisha sana mpaka akaishiwa nguvu, hivyo wakamlaza ili kumuwekea madrip, nikamwambia Bibi nakutumia hela ya chakula halafu kesho nitatuma hela za Bill za hospital. Sasa sikuwa na pesa nakumbuka kwenye account yangu nilibaki na kama Elfu kumi na mbili, nikasema nikatoe Elfu kumi nimtumie Bibi halafu nipambane nipate hela za kulipia hospital kesho asubuhi.
Basi nikatoka Chuo nikapita mahali kuna Bank na kuna ATM, ilikuwa mida ya saa tatu usiku. Nafika pale kukawa na foleni ya watu watatu hivi. Ikafika zamu yangu nikaingia, ile naingiza kadi uwii nakuta salio liko elfu nane haliwezi toka, nikaishiwa pozi. Basi nikatoa kadi, nyuma yangu alikuwa mkaka kavaa pensi akaniuliza vipi, nikamwambia ingia kadi yangu inashida. Basi yule kaka akaingia. Mimi nikakaa nje chini kwenye kibaraza cha Bank nikaanza kulia nawaza nitapata wapi hela sasahivi nimtumie Bibi na Mama angalau wale chakula nikawa nimekaa nafuta machozi. Baadae likanijia wazo la kukopa MPAWA, hivyo nikatoa simu niangalie naweza kukopa kiasi gani. Kumbe wakati nalia yule kaka aliyeingia kwenye ATM alikuwa ananiangalia, nikaona ananifwata pale nilipokaa akachuchumaa akaniuliza vipi mbona unalia, nikashangaa napata nguvu za kumjibu, nikamwambia Mama yangu anaumwa amelazwa nataka kuwatumia hela angalau wapate chakula leo usiku, ili kesho niende kazini nimuombe muhasibu anipe advance salary. Nikashangaa anaingiza mkono mfukoni akatoa pesa akanipatia. Nikaogopa nikamwambia hapana naomba usinipe hela please, akasema usikatae nenda mtumie Mama. Akaniuliza unaelekea wapi nikupe lift, nikakumbuka Pastor alisema tusiwe wepesi, nikamwambia hapana asante nashukuru. Akasema inaonekana unaogopa sana, ila ni vizuri naomba chukua kadi yangu, nitumie message baadae ningetamani kujua hali ya Mama. Basi nikachukua ile kadi, nikamshukuru huku nalia nikamwambia asante sana, Wewe ni malaika umeshuka Leo kwaajili yangu. Nikamshika mkono nikaomba kumshukuru Mungu na kumuombea Mungu ambariki, nikamuona ananishangaa, akasema aisee binti mrembo hivyo halafu unajua kuomba namna hii aisee. Akasema naomba namba yako nikamwambia usijali nitakutumia message baadae. Akasisitiza please nitumie natama uwe unaniombea kila siku, basi nikacheka tukaagana.
Nikaona anaingia kwenye gari nzuri ni Benz nyeusi uwii, ina mlio fulani hivi. Wakati anaondoka nikachukua zile hela kuzihesabu ni laki mbili, nikasema whaaat laki mbili. Hapo hapo nikampigia Bibi nikamwambia gharama kiasi gani wakasema dripu na dawa zote elfu arobaini, nikamwambia nakutumia laki nyingine mtafanya usafiri na chakula Mimi nitakuja kesho asubuhi kuwaona.
Basi nikamtumia, nikatoka zangu huyo nikaanza kurudi nyumbani. Nikapita mahali nikanunua chips zangu mayai na mishkaki nikashushia na soda, huyo nikaenda nyumbani nikaoga nikalala.
Huwezi amini nimelala usiku nataka kumtumia Message yule mkaka naogopa, nakumbuka maneno ya Pastor Anni anasema usiwe mwepesi, ringa kidogo khaaah, ukipewa namba kaa kama siku mbili ndio utume message 😀😀, basi nikasema nitulie kesho jioni nitampigia.
Usiku nakwambia hata usingizi sikupata niko nimeshika ile kadi, nasoma majina tu anaitwa Kennedy daaah sikuwa naelewa inakuwaje ila nikasema hivi mkaka kama yule kijana, ana pesa anaweza kuwa hajaoa kweli. Hembu niache ujinga usikute ni Mume wa Mtu, lakini roho inaniambia hapa hajaoa. Nakwambia hata kuomba niliomba maombi machache sana kumshukuru tu Mungu yani 🤣🤣🤣
PART 12
Asubuhi niliamka nikawahi hospital, nikakuta Mama anaendelea vizuri tu na akawa amesharuhusiwa hiyo asubuhi hivyo tukakodi Bajaj hao mpaka nyumbani. Kufika nakamsaidia kumuogesha akavaa nikawaacha nikawahi kazini.
Nimefika kazini moyo haunipi nawaza kumpigia Kennedy, nikasema Bwana Pastor atanisamehe ila acha nimpigie nimshukuru kwa msaada wake. Basi mida ya Mchana nikasema nimpigie tu kumshukuru sio vibaya. Basi nikapiga simu, ikaita mara mbili akapokea Hallow, aisee nikaanza kutetemeka. Nikasema habari, bila shaka naongea na Kennedy, akasema ndio Mimi ni Kennedy, nani mwenzangu. Nikamwambia naitwa Bite tulikutana jana kwenye ATM ukanisaidia pesa kwa ajili ya Mama yangu. Akasema Oooh Bite mbona hukunipigia jana? Yani sijalala usiku kucha nasubiri simu yako. Nikamwambia niliogopa usiku nisije kukuletea shida kwa mkeo, akacheka akasema hapana Mimi sina Mke jamani sijaoa bado, nikasema basi nisamehe ila nimeona muda wa mchana ndio mzuri kukupigia.
Huwezi amini nilikuwa naongea maneno yamenyooka, kwa taratibu na kwa kituo. Akaniuliza Mama anaendeleaje? Nikamwambia hajambo ameruhusiwa Leo amesharudi nyumbani, akasema naomba uniruhusu nikamuone, nikamwambia yani uje kwetu? Akasema ndio kwani kuna ubaya, nataka kumuona Mama nimpe pole pia kwa kuumwa. Nikamwambia sawa karibu. Akasema naweza kuja Leo? Nikamwambia hapana Leo nina test chuo mpaka jumamosi Ndio nitakuwa na nafasi.
Akashangaa akaniuliza unasoma? Nikamwambia ndio nasoma huku nafanya kazi, akasema aisee hongera sana sana. Akaniuliza tena naweza kukuona lini, nikamwambia jumamosi ukija nyumbani utaniona, akasema hapana nataka kuonana na wewe ili tuongee, nikamwambia sijajua lini nitakujulisha. Akaniuliza unasoma wapi nikamtajia, akauliza unatoka saa ngapi nikamwambia mara nyingi mida ya saa mbili na nusu nakuwa natoka akasema sawa.
Basi nikafanya kazi jioni nikawahi chuo kufanya mtihani, na mida ya saa mbili na nusu nikawa ndio nimemaliza. Nikawa natoka nje taratibu kwenda kupanda Daladala. Kidogo nakaribia getini nasikia Mtu anaita Bite Bite kugeuka uwii Kennedy, amekuja Chuo kunifwata. Nikashangaa nikamwambia jamani imekuwaje mbona uko hapa, akasema nimekufwata Wewe, maombi yako ulioniombea juzi yalinibariki naomba na Leo uniombee. Basi tukacheka tukawa tunaongea huku tunatoka nje.
Akaniambia nimepark gari pale naomba tukaongee kwenye gari, basi tukatembea mpaka kwenye gari. Kufika nikamwambia naomba tuongee tu hapa nje sitaingia kwenye gari akasema Bite yani huniamini kiasi hicho, nikamwambia sio sikuamini lakini tahadhari ni muhimu sana. Akasema sawa acha tusimame hapa tuongee.
Akaanza kuongea pale akasema niwe mkweli nisipepese maneno Bite Mimi nakupenda, niseme tu tangu siku ile nimekuona moyo wangu haujatulia, Nakupenda na natamani kuwa na Wewe. Nikasema eeeh jamani ghafla hivyo hata hunijui, akasema Bite sema yote ila hilo ndio liko moyoni mwangu nakupenda sana sana natamani kuwa na Wewe.
Najua ni mapema ila nakupa muda ulifikirie, na hata ukitaka kunijua vizuri niko tayari kukuonyesha kila kitu changu ili uniamini.
Nikamwambia sawa nashukuru sana kwa kunipenda nimefurahi kusikia hivyo. Niseme tu naomba unipe muda nimuombe Mungu najua atanipa majibu sahihi, akasema sawa. Nikamwambia Mimi naondoka, akasema si nikupeleke nikamwambia hapana acha nipande tu daladala, nitapanda wakati mwingine. Akaingiza mkono mfukoni akataka kunipa hela, nikamwambia hapana usinipe hela juzi ulinipa hela nyingi badi ninazo. Akasema huwa naumia sana nikimpa mtu kitu halafu akakataa, nikamwambia nisamehe ila Leo sitapokea. Akaniambia basi naomba uniombee niende. Basi nikamshika mkono nikamuombea, akafurahi tukaagana.
Nikaenda zangu kupanda Daladala huku natetemeka, nikafika nyumbani akanipigia nikapokea akasema nilikuwa nauliza kama umefika, nikamwambia ndio nimefika asante sana, akasema sawa usiku mwema haya ubarikiwe.
Nikaingia zangu kuoga ile natoka nacheck simu nakuta muamala Tsh laki na nusu uwii, nikamtumia message nashukuru sana Mungu akubariki na akuzidishie.
Basi usiku sijalala nawaza huyu Kennedy ni nani, katokea wapi na inakuwaje hapa natoka vipi. Kesho yake nikaamua kumpigia Pastor Anni simu nikamwambia kuhusu Kennedy Pastor akasema Mwanangu njia za Mungu hazichunguziki, akaniambia nikuombe mwanangu OMBA, Baraka yoyote ile inapokuja huwa tunaiombea, anza kumuombea huyo Kennedy tena kwa mzigo haswa funga na kuomba kwa ajili yake. Acha kupagawa na pesa muombee.
Basi kesho yake nikaanza maombi ya mfungo kwaajili ya Kennedy, ili Mungu akalithibitishe neno lake na kama ni wa kwangu basi adumu asiishie njiani kama wengine.
Maisha yaliendelea jumamosi ilifika lakini Kennedy alikuwa amepata safari ya ghafla ya kikazi hivyo hakuwa kuja nyumbani kama alivyosema.
Jumapili nikajiandaa vizuri kwenda kanisani, kama kawaida gauni langu zuri, kiatu changu na pochi yangu, bila kusahau perfume matata. Basi huyoo nikatoka kwenda Ibadani.
Nafika ibadani kama kawaida nawaona watesi, nikajifanya kama siwaoni. Sikuwa na shobo na Mtu, nilikaa zangu kimya nasikiliza ibada. Ibada ilivyofika mwisho huyo nikawa natoka, kidogo Mchungaji na Mama Mchungaji wakaniita Bite njoo nikaenda kuwasalimia, akasema Mwanangu umebadilika sana sikuhizi, umekuwa mkimya sana, huongei umetulia uko tu busy na mambo yako, kuna tatizo, nikamwambia hapana niko sawa tu. Akasema lakini pia unapendeza uko so smart. Nikamwambia nashukuru Baba ni maombi yenu yananivusha. Basi wakaniaga nikaondoka.
Wakati natoka namuona Eben, ni kama alitaka kunisemesha ila nikamkwepa nikageuza shingo upande mwingine, nikatembea faster kuwahi boda, nikapanda nikaondoka. Hapo hapo akanitimia message Bite kuachana sio uadui tusalimiane basi sio dhambi, sikumjibu wala nini nika achana nae
PART 13
Pastor Anni alinisisitizia sana akasema kabla haujaingia kwenye mahusiano omba kwanza, wengi mkisha tongozwa na kupewa namba huwa hamuombi, mnakuwa mnahangaika na mko busy na kuchat, outing mpaka siku mahusiano yamevunjika ndio mnamkumbuka Mungu. Siri ni hii nakupa kabla haujaamua kutoka na Mtu au kuingia kwenye mahusiano na Mtu ingia magotini, zungumza na Mungu. Mkabidhi Mungu huyo Mtu na mwambie nini unataka.
Pastor akasema unatakiwa uombe kwa mzigo sana na ili uombe kwa mzigo unatakiwa kwanza uchoke na hali uliyokuwa nayo, uchoke na mazingira uliyokuwa nayo, uchoke na misukosuko ya mahusiano uliyopitia, ukishachoka utaingia magotini na kumwambia Mungu inatosha, inatosha Baba naomba ufanye kitu.
Pastor akasema hivi unajua maombi yana kawaida ya kuharakisha mambo? Yani unaweza kuomba Mungu akafanya kila kitu kwa wepesi na haraka. Sio lazima wote tukae kwenye mahusiano miaka mitatu ndio tuolewe hapana, wengine tunaweza kuingia kwenye maombi tukapokea upako wa kasi ( SPEED ANOINTING), tukirudi kwenye mahusiano mambo hayakawii miezi sita tu ndoa tayari.
Akaniambia binti omba omba, achana na kuchat na huyo Kennedy, achana na outing za dinner muombee kwanza ili hizo outing zikianza zikawe za kudumu.
Basi nikaanza maombi, nikaamua kufunga haswa kwaajili ya Kennedy, nikamwambia Mungu Kennedy amesema ananipenda na anataka kuwa nami, Baba ninaomba huyu isiwe ya muda mfupi, naomba kwa huyu ikawe ya kudumu. Nahitaji kuolewa, niwe na mji wangu, nahitaji kuwa na Watoto, nahitaji kuwa na furaha, nimechoka kuumizwa kila siku eeh Mungu nisaidie.
Nilikuwa naomba kwa mzigo sana, kuna muda naamka usiku nakumbuka niliyoyapitia najikuta naanza tu kulia, naliaaa naliaaaa namwambia Mungu inatosha safari hii hapana.
Kennedy alinitafuta akaniomba tuonane nikamwambia samahani nimeingia kwenye maombi ya mfungo wa wiki mbili, naomba nimalize mfungo ndio tuonane Kwasasa nimeamua kujichimbia.
Akasema whaaat sijawahi kukutana na Mwanamke wa aina hii, yani unaamua kutulia kumtafuta Mungu aisee nimekupenda.
Basi nikastopisha mawasiliano nae kabisa, nikakaa kimya. Kuna siku alipiga sana simu sikupokea, jioni natoka Chuo nikamuona kwa mbali yule nikabadilisha njia nikasema nakomaa hanioni, hanipati mpaka nimalize maombi. Pastor alisema Binti anaeijua thamani yake huwa ni ADIMU HAPATIKANI KIRAHISI.
Kuna siku akatuma message Bite nashindwa kulala naomba pokea hata simu yangu tu nikusikie, nikamjibu usijali Kennedy ngoja nimalize maombi nitakipigia, nakuombea Mungu akutunze. Akatuma vi emoji vya kulia.
Nakumbuka Pastor Anni alisema kuwa binti wa tofauti, usiwe mwepesi, kwani unafikiri huyo Kennedy hajawahi kutongoza wanawake, unafikiri hajawahi kuwa na mahusiano, alishawahi, usikute katongoza sana mabinti na usikute akitoa tu namba mabinti wanaanza kupapatika wanamtafuta na wanaonana, sasa Wewe kuwa watofauti CHANGE THE FREQUENCY, KUWA ADIMU, KUWA MTULIVU, KUWA MKIMYA, ACHA PAPARA, ACHA KUPAPATIKA TULIA. HATA KAMA UNA SHIDA SANA NA HAYO MAHUSIANO JARIBU KUJIZUIA, KAMA YAKO YAKO TU.
Nilimaliza wiki ya kwanza ya mfungo nikiwa kimyaa ni Mimi na Mungu tu. Nikaingia wiki ya pili ya mfungo, niliomba sana nikamwambia Mungu huu ni wakati wangu, nanyamazisha kila roho ya uharibifu, roho za mafarakano, roho za kukataliwa nazivunja katika Jina la Yesu, kila madhabahu za kichawi, kiganga zilizo kinyume na mafanikio yangu nazisambaratisha kwa Moto, nina nyamazisha kila adui aliyejipanga kuzuia Baraka zangu, namtekwteza kwa moto.
Pastor alinifundisha maombi ya Kimkakati nikachukua karatasi nikaandika Jina la Kennedy nikasema kama umekuja kwa mpango wa Mungu basi utakaa, utanioa na tutajenga familia, ila kama umekuja ili uniharibie maisha uteketee kwa Moto mapema sana. Niliomba kwa kumaanisha nikasema kama wangu basi akae.
Nilifunga wiki nzima tena mpaka jumapili nikamaliza. Jumapili nilienda ibadani kama kawaida na nikawa natamka kimoyo moyo nikasema huu ndio wakati wangu wa kuandaliwa meza huku watesi wangu wakiwa wanaona. Nikamwambia Eeh Yesu naomba unibariki huku watesi wangu wakiwa wanaona, nimedharaulika sana niheshimishe Baba yangu.
Nikiwa Ibadani Kennedy alipiga sana simu, nikamtumia message kuwa niko kanisani, akaniambia Bite unanitesa naomba nikuone baadae ukitoka Ibadani, nikamjibu nitakupigia, akasema Please Mama nisaidie.
Basi nikasali zangu, Ibada ilivyoisha huyo nikanyanyuka. Kama kawaida yangu sina story na mtu halafu nimependeza hatari 🔥🔥na nina confidence ya ajabu. Yani nilikuwa najiamini sana sana. Eben alikuwa ananiangalia tu hanimalizi, wakati natoka akanifwata akasema Bite naomba nikusalimie please nikamwambia nisamehe ninawahi kuna mtu ananisubiri mahali, akasema aisee najua nimekuumiza sana ila hunitendei haki, umenichukia moja kwa moja. Sikumjibu nikawa namsikiliza tu. Akasema sasahivi unafanya kazi wapi mbona umebadilika, nikacheka tu nikamwambia naomba niwahi nimechelewa kuna mtu ananisubiri. Yani sikumjibu hata swali lake moja, sikumpa nafasi ya kupiga story, yani nilikuwa namuona kama lijitu la ajabu limesimama mbele yangu. Nikasema kwanza ashukuru nimesimama kumsikiliza akae kwa kutulia tu. Wakati napanda boda akasema please naomba baadae tuongee nakuomba Bite, nikamwambia wa boda twende tuwahi please nachelewa. Tukamuacha katoa tu mimacho. Nikashangaa mchumba wa Mtu ana hangaika nini na Mimi, yani aniache kabisa.
Nilirudi nyumbani nikampigia Pastor Anni simu nikamwambia Mama nimehitimisha maombi yangu ya mfungo wa wiki mbili, nataka kutuma sadaka yangu naomba uniombee. Basi akaomba kumshukuru Mungu, nikamtumia SADAKA. Nikamwambia Mama naweza kumtafuta Kennedy akasema Yes kuwa huru tu.
Basi nikampigia Kennedy simu akapokea kwa upole sana, akasema Bite unanitesa, sijawahi kuteswa hivi na Mwanamke, nikamwambia nisamehe nilikuwa kwenye maombi. Akasema please naomba kukuona naomba nahitaji kuongea na Wewe. Nikamwambia sawa, akasema chukua Bolt tukutane Serena Hotel kuna Buffet pale nataka tukale maana umefunga wiki mbili upate nguvu MKE WANGU, nikashangaa akaniita MKE WANGU, nikastuka Mke wangu tena. Nikamwambia sawa saa moja nitakuwa hapo.
Nikaamini maneno ya Pastor Anni alisema ukiwa mkimya thamani inaongezeka, kuna raha mwanaume akikumiss aisee raha sana..
Kama kawaida nikavaa kigauni chekundu kizuri, na kiatu cheusi na kapochi keusi, perfume sasa uwii nilichanganya mbili. Nikaomba Mungu anitangulie, Nikaita Bolt ikaja huyo nikatoka.
Wakati natoka nikawa nafanya mazoezi ya muondoko kama wa Pastor Anni 🤣🤣
PART 14
Nilifika Serena nikashuka kwenye gari, nikawa namfwata alipo. Alikuwa amesimama karibu na mlango wa kuingilia, hivyo wakati natembea kumfwata akawa kabaki kaduwaa ananiangalia. Kufika akanikumbatia kwa nguvu akasema Bite unanitesa sana kwanini Mama hutaki tuonane, au hunipendi. Nikamwambia hapana nilikuwa kwenye maombi. Basi akanishika mkono kuelekea ndani kwenye viti. Akasema mbona nakuona tofauti, you look so beautiful. Basi Tukafika akanivutia kiti nikakaa na Yeye akakaa akasema karibu kipenz, nikasema asante.
Akaanza kuongea akasema sio siri tangu nimekutana na Wewe naona tofauti, nimetokea kukupenda sana Bite, sijui ulikuwa wapi siku zote. Wewe ndie mwanamke niliyekuwa nakutafuta miaka yote. Kama kawaida siongei sana natabasamu tu kwa upole.
Nikamuuliza kwani Wewe nani, unaishi wapi, familia yako jee. Akaniambia Mimi naitwa Kennedy ni Mtoto wa Professor fulani nikastuka. Akasema Mimi ni Mtoto wa tatu kuzaliwa, Baba yangu ni Professor ila Kwasasa umri umeenda anaishi CANADA na Mama yangu. Lakini pia Dada yangu na kaka yangu mkubwa pia wako huko. Hapa Tanzania nipo Mimi na mdogo wangu anaenifwata wa mwisho anaitwa fulani. Akasema sijaoa ila nina Mtoto, kuna Mtu nimezaa nae na nilipanga kumuoa ila ilishindikana, tumesumbuana sana, nikaamua kumuacha nikasema nitaoa mwanamke mcha Mungu. Akasema Mama wa Mtoto ameshaolewa na anamaisha yake yupo Ulaya na Yeye ila Mtoto Yupo Canada anaishi huko na wazazi wake.
Akaniuliza kuhusu Mimi, nakumbuka Pastor Anni alitukataza kujielezea sanaa, nikaongea kwa ufupi tu, nikamwambia naitwa Bite nimezaliwa peke yangu kwa Mama yangu, Mama yangu aliolewa ila waliachana na Baba nikiwa mdogo, hivyo tukaondoka na Mama kwenda kuishi na Bibi ndio mpaka Leo nimelelewa na Mama na Bibi. Baba yangu yupo na ana Mke mwingine, nikaishia hapo. Sikutaka kuongea chochote kuhusu mateso, sijui mahusiano hapana niliongea kwa ufupi basi.
Basi wakati tunakula akasimama akaja karibu yangu akapiga magoti akasema Bite Naomba nikuoe, Naomba tufunge Ndoa uwe Mke wangu, Wewe ndio mwanamke hasa niliyekuwa nakutafuta, nikaanza kulia nikamwambia kwanini mbona hunijui vizuri, akasema sihitaji kukujua vizuri nakupenda naomba tuoane 😭😭😭 nilishindwa kuzuia machozi basi akachukua tissue akaanza kunifuta.
Nikamwambia sawa Kennedy nipe muda, akasema sina muda wa kusubiri Bite, nakuomba Wewe ndio faraja yangu. Nilikosa majibu nikabaki natoa machozi. Akasema nitakupa kila unachotaka, am here to make you happy. Niko tayari kwa lolote. Nikamwambia sawa Kennedy nitakujibu soon usijal. Akasema Mimi najua Wewe ndio Mke wangu na sihitaji mwanamke mwingine zaidi yako.
Basi tukala tukamaliza, akaniambia Leo naomba upande gari langu naomba nikakuonyeshe mahali ninapoishi upaone kwa nje ili siku nyingine uje tu. Basi akanipeleka kwake masaki, Bonge la jumba kuna mimbwa na walinzi akaniambia naishi hapa na mdogo wangu wa mwisho, tuko wenyewe na wafanyakazi tu. Nikamwambia sawa.
Basi tukaingia kwenye gari akanipeleka kwangu, kufika nikamwambia Mimi naishi hapa nimepanga chumba kimoja master akasema hapana naomba nikuhamishe, nikamwambia usijali niko comfortable kabisa. Basi tukaagana akaondoka.
Tukaanza kuwasiliana, Nakwambia akaanza kupiga simu, kila siku jioni lazima anifwate Chuo anirudishe nyumbani, hataki nipande Daladala. Akipiga simu sijapokea ugomvi, ana wivu balaa. Kila siku ugomvi, mara aje nyumbani usiku, nikamwambia Kennedy mbona uko hivyo akasema naogopa kukupoteza Bite bora nikuoe nitulie.
Sasa ikabidi nimfwate Mama Shushani nikamwambia hapa natoka vipi Pastor. Ukiangalia mambo niliyopitia sikutaka kabisa yajirudie. Pastor akasema hapo tulia hii Ndoa iende kijeshi, hapa hatuwaambii watu, ni Mama na Bibi tu wapokee mahali hakuna send-off wala kitchen party kimya kimya, maana ukisema umshirikishe Mama wa kambo aisee atatuharibia, subiri uolewa utawapa taarifa. Hata kanisani usiwaambie, olewa kimya kimya. Yani kimya kimya, nikamwambia Pastor sawa.
Basi nikarudi nikamwambia Kennedy nimekubali tuoane, nimekubali uwe Mume wangu. Ila nikamwambia Mama yangu na Bibi hawana uwezo, wameomba ukishatoa Mahari tufunge Ndoa wao hawana sherehe yoyote, akasema nakuelewa Bite hata Mimi sitaki sherehe kubwa nataka tuoane tu halafu sherehe tutaenda kufanya Canada kwa wazazi wangu.
Akaniambia ongea na Mama na Bibi baada ya wiki mbili nakuja kutoa Mahari, nakumbuka ilikuwa November, akasema nitasafiri kidogo kikazi mwezi wa pili narudi tufunge Ndoa. Nikamwambia sawa.
Huwezi Amini nilianza tena mfungo wa wiki mbili kuombea mchakato wa Mahari, sikumwambia Mtu yoyote zaidi ya Mama Bibi na Ndugu wa Mama.
Siku ikafika wakaja watu wachache tu wakatoa Mahari nikavalishwa na Pete basi. Mahari ilikuwa ni Milioni kumi. Mama akasema tutengwe Milioni mbili baada ya Harusi tumpe Baba yako, na tumwambie hiyo ndio Mahari yote. Nikasema sawa tukacheka 🤣🤣
Alinipeleka kanisani kwao ambapo wazazi wake walikuwa wanasali, tukaonana na wachungaji wakatuombea, tukawapa tarehe ya Ndoa, na tukalipia gharama zote, wakatupa masharti ikiwemo kupima afya. Kesho yake tukaenda kupima majibu yakarudi kanisani. Basi tukamaliza kihivyo.
Huwezi amini niliishi kwa hofu sana, Kennedy akasafiri kikazi nje ya nchi, aliniachia hela nyingi sana za matumizi, akaniambia jipange nikirudi Tunafunga ndoa unahamia masaki please hautakuwa hapo tena. Nikasema sawa hamna neno. Ukaanza mchezo wa Video call, kila akipiga simu ni video call tu, tunaongea weeeh mpaka. Kiufupi alikuwa ana hamu na Mimi yani alikuwa so so excited kunioa, alikuwa anaona kama kaokota dhahabu yani.
Basi ile Pete baada ya Kennedy kuondoka nikaivua nikaiweka kabatini, sikutaka Mtu yoyote ajue kama naolewa yani ilikuwa siri siri kubwa.
PART 15
Mama na Bibi walisisitiza sana nisiende tena kule kanisani wala kuonana tena na Mama wa kambo. Wakasema yule Mama mchawi anaweza hata kukuua ili tu usiolewe. Nikawauliza nifanyaje, Mama akashauri nimtafute Baba niongee nae nimuage kuwa nimepata kazi mkoani akasema sema Tabora, na kanisani jumapili ukawaage kuwa unaenda Tabora kikazi halafu usionekane tena. Nikasema sawa.
Basi Nikamtafuta Baba, kama mnavyojua huwa ananidharau yani hanaga attention na Mimi kabisaaa, basi nikamwambia Baba nimepata kazi Tabora natakiwa niende, kazi gani akauliza, nikamwambia ya kiwandani, akasema Wewe nawe kazi zako hizi hazina kichwa wala miguu haya sawa safari njema. Nikamwambia sawa utaniagia kwa Mama akasema sawa nikaondoka.
Jumapili nikajiandaa nikaenda kanisani, wakati wageni kusalimia na wenye ushuhuda, na Mimi nikanyanyuka kwenda mbele. Nikaona watu wametoa macho wanajiuliza nataka kusema nini. Basi muda wangu ulipofika nikamsalimia kanisa halafu nikaaga nikawaambia nawashukuru kwakuwa nami kwenye nyakati zote, Mungu amenipatia kazi Tabora hivyo kesho nitakuwa nasafiri kwenda Tabora kureport kazini. Mchungaji akasema kanisa tusimame tumuombee binti yetu Mungu amlinde na kumfanikisha.
Niseme tu kwa machungu yale niliyopitia sikuwa tayari tena kwaajili ya machozi mengine, nimekaa kwa tabu sana hapa kanisani, nimevumilia mengi ila sasa Ndio Wakati wa kuachana nao. Pastor aliniambia kamwe usiondoke mahali wakati wa matatizo, ondoka wakati wa amani. Nilitamani sana kuondoka na kuhama kanisa tangu kipindi kile, ila Pastor alinizuia akasema sio wakati sahihi, subiri wakati utafika utaondoka bila shida. Akasema Bite hakikisha una ondoka mahali wakati wa amani, wakati ambao wanakuhitaji. Basi nikamshukuru Mungu nikawaaga wote nikaondoka huyooo.
Niliamua kubadilisha namba za simu, nikasajili line mpya nikapata namba mpya nikaanza kutumia, hivyo nikawa sipatikani kabisa kwa namba za zamani. Nikafunga ukurasa wote wa zamani, Nikaanza kuishi maisha mapya kabisa. Nikasema Kwasasa HAKUNA tena maumivu, uchungu, vilio yani naanza kuishi upya, naandika historia mpya.
Kennedy alirudi, akanipeleka kwenye maduka ya Nguo za harusi sinza nikachagua gauni simple zuri, tukafanya booking ya salon kwaajili ya kupambwa na vyote akalipia.
Siku ikafika, nilikuwa naomba tu Mungu anivushe, nikawa nasema Yesu nivushe.
Finally Ndoa ikafungwa, nikawa Officially MRS KENNEDY 😭😭😭🙏🙏🙏. Ilikuwa kama ndoto. Mama yangu alilia sana wakati Ndoa inafungwa. Baadae ya kanisani tukaenda Hotelini na watu WACHACHE tukala Chakula, tukakaa cake basi tukaondoka.
Nilihama pale nilipokuwa nakaa vitu vyangu vyote nikampa Mama yangu zikiwemo nguo, viatu, kitanda, kabati na kila kitu nikampa Mama, sikuwa navihitaji tena.
Nilikuwa namaliza Chuo mwezi wa sita, ikabidi tusubiri nimalize Chuo ndio tusafiri. Kazi kule niliacha akaniambia nakuomba utulie itabidi tusimamie wote Miradi ya familia. Nikamwambia sawa.
Basi nikaanza kuishi masaki, Nikawa napelekwa Chuo na gari na driver, mambo ya daladala tena basi. Nikaanza kuishi kizungu kabisa, maisha ya supermarket tu, hadi nyanya naenda Shoppers kununua.
Mume wangu alifurahi kuniona yani humo ndani ilikuwa ni kubebwa tu kama Mtoto. Bado niliendelea kuwa mkimya, mtulivu, mwenye adabu nyingi tu na hicho kitu Mume wangu alikifurahia, hata tukigombana siongei kwa ukali Mimi ni taratibu tu kwa amani.
Baadae nilibeba ujauzito, hivyo mpaka namaliza chuo nilikuwa mjamzito. Baada ya kumaliza Chuo ndio safari ya kwenda kwa wakwe ikaanza, tulijiandaa na kila kitu kikakamilika. Ila usiku kabla sijapanda ndege nilimpigia Baba yangu mzazi nikamwambia Baba nashukuru sana nimepata mwanaume ila kutokana na changamoto za hapo nyumbani nilishindwa kusema, ila Baba yangu nimeolewa na hapa naishi na Mume wangu. Mahari yangu Mama alipokea na nikawaomba wasikwambie mpaka nikwambie mwenyewe. Mahari yako watakutumia.
Nikamwambia Baba hapa nasafiri naenda Canada, Mungu akubariki na akutunze nakupenda. Huwezi Amini Baba akaanza kulia kwenye simu, akasema uko wapi mwanangu nikamwambia Airport napanda ndege sasahivi.
Akasema mwanangu nisamehe, nisamehe kwavyovyote niliyokufanyia, kama Baba sikusimama kwenye nafasi yangu kukulinda kama mwanangu, nisamehe mwanangu. Najua nimekuumiza sana naomba msamaha.
Nikamwambia Baba usijali nimeshakusamehe na Wewe naomba unisamehe pale ambapo nilikosa akasema nimekusamehe mwanangu. Akasema basi ukifika huko tuwasiliane mwanangu, nikamwambia sawa.
Airport nilikuwa na Mama, Bibi, Baba mdogo, nililia kwa uchungu sana, nikawaaga basi hao, tukaondoka. Nikapanda Ndege kwa mara ya kwanza 🙏🙏
PART 16
Kwanza pale pale kanisani baada ya kuaga Mama yangu wa kambo na Ndugu zangu wakanifwata na siku hiyo Baba alikuwepo ibadani, akaniambia kila laheri mwanangu Mungu akutangulie, angalau ubadilishe mazingira upate na mwanaume wa Kijijini huko akuoe. Aliongea kwa dharau sana ila sikujali.
Usiku ule nilivyofika nyumbani, Eben alinitafuta sana alipiga simu sikupokea, akanitumia message akasema
“Bite kwanza naomba unisamehe sana kwa yote niliyokufanyia, huwezi amini hata Mimi nakosa Amani, ila najutia uamuzi wangu wa kukuacha. Akaandika ujumbe tena akasema Mimi sikupenda kukuacha ila Mama yako wa Kambo alikuja kwangu akaniambia nisikuoe Wewe, Wewe una laana ya Mama yako na mikosi, ukipata mwanaume lazima akuache au mwanaume analoose yani anashuka kiuchumi. Akasema una roho ya kukataliwa, pia Mama yako ni mchawi akasema usikute Wewe umeniloga.
Bite nisamehe baada ya yale maneno kweli nilikuchukia na nikaogopa kuendelea na wewe ndio maana nikapata ujasiri ule wa kukuacha.
Lakini napitia magumu huyu binti ni kweli nimemtolea Mahari lakini nadhani sitaweza kumuoa, kwanza anajisikia, hana adabu muda wote ni amri tu, ana mawasiliano na wanaume wengine wengi tu, na hapa hatuongei tuna kama mwezi. Kuna siku nilimpigia simu akawa hapatikani baadae kumuuliza hakutaka nimuulize Ndio hivyo akaninyamazia na Mimi nimeamua kunyamaza. Hivyo hatuna mawasiliano. Inaonyesha anaetaka Binti aolewe ni Mama wa Binti ila Binti mwenyewe hayuko tayari kwa Ndoa.
Bite Ulivyoaga kwenda Tabora nimefurahi kwani nimeona ni nafasi yangu ya kurudiana na Wewe, naomba tuanzie tulipoishia Bite, nakuomba sana. Nije Tabora tuendeleze mahusiano yetu, tuoane huko huko Bite please nakuomba.
Aliandika message nyingi, akatuma na Voice note kibao analia, akasema Mimi ndio mwanamke wa maisha yake. Sikujibu hata moja.
Nilimwambia Pastor, Pastor akasema huyo muache sindano imuingie na bado, hapa tushaijua vita yetu ni kubwa mnoo, inamaana Mama wa kambo bado anapambana kukuharibia maisha basi potea kabisa. Eben alinipigia sana simu, Pastor akasema mjibu tu nitakutafuta ngoja nifike Tabora nitulie nitakutafuta.
Ila baada ya muda wakati Kennedy anakaribia kurudi ilinibidi nibadilishe line ya simu kuepuka matatizo. Maana Kennedy nae ana wivu sana kutwa yuko na simu yangu.
Nimefunga ndoa nzuri ya heshima, kweli ile dinner party walikuja watu maarufu na matajiri na zilipigwa picha nyingi nzuri ila sikupost hata moja. Pastor akasema subiri ufike Canada ndio upost.
Niligraduate Chuo tulifanya sherehe ndogo masaki walikuja Mama, Bibi Baba Mdogo yule aliyenilipia ada ya kusomea cherehani na Ndugu wachache wa Mama, walikuja pia watu wazito ndugu zake na rafiki zake Kennedy ila sikupost pia. Nikatunza picha, Pastor akasema tulia ukifika Canada unaanza kushusha tukio moja moja kwa utaratibu ili sindano iwaingie🤣🤣.
Mimba ilianza kunisumbua, kutapika tapika ovyo lakini Mungu alinisaidia baada ya muda ikaacha.
Wakati nasafiri kwenda Canada ndio nikampigia Baba yangu simu nikiwa Airport kumuaga na kumueleza kuwa Mimi nimeshaolewa na sasa ni mjamzito, Baba nikamuacha analia. Lakini pia pale pale nilimpigia Mama Mchungaji kumueleza kila kitu, nilimwambia Mama nisamehe niliondoka hapo nikasema naenda Tabora ila sio kweli niliamua kuondoka sababu ya maumivu makali niliyokuwa nayo Mama. Mama Mimi nimeolewa na hapa niko Airport nasafiri kwenda Canada kuonana na wakwe zangu, nitakuwa huko kwa muda kidogo. Naomba mnisamehe kwa yote niliyowahi kuwakosea hata hili la kuolewa kwa siri mnisamehe. Mama Mchungaji hakuamini, akasema Bite unasema kweli nikamwambia ndio Mama. Nikamwambia tutawasiliana nikirudi Tanzania nitakuja niagie kwa Baba. Baadae wakaanza kupiga simu sikupokea tena. Mama wa kambo alipiga simu sana sikupokea, wale Dada zangu walipiga simu sikupikea baadae nikaizima simu huyo nikapanda Ndege.
Kufika Canada kweli Baba Mkwe ni Mtu mzima sana na ana tatizo la miguu anatembea na magongo au automatic wheelchair, walikuja airport kutupokea walifurahi sana. Mama Mkwe alinipenda akanifurahia sana, na walivyosikia ni mjamzito weeeh ndio furaha ikazidi.
Kwa Mume wangu wamezaliwa wanaume watatu na Mwanamke mmoja ambae ni wifi yangu, shemeji yangu mkubwa ameoa huko Canada ila kaoa Mzungu na ana Watoto wote walikuja walinipenda wakanifurahia.
Baba Mkwe akasema nikae pale mpaka nijifungue kwani baada ya kufika kule nilianza kuumwa kidogo ila baadae nikawa sawa.
Mume wangu alirudi Tanzania kikazi akasema kaa huku na Mama ukijifungua utarudi, kaa utulie uwape company wazazi.
Niseme tu ilikuwa kama ndoto, sikuwa naelewa nini kinatokea kwangu, niliendelea kumshukuru Mungu sana kwa uaminifu wake.
Basi Baada ya muda nika jifungua Mtoto wa kiume, wakwe zangu walifurahi sana, nilipewa zawadi nyingi sana ikiwemo gari zuri sana.
Baadae sasa ndio nikafungua Insta yangu, nikaanza kupost picha moja moja.
Kuna siku niliamka tu nikaweka picha zangu za harusi ila Mume wangu nimemficha sura, nikapost kumshukuru Mungu na kumshukuru Mume wangu kwa kunisitiri. Watu sasa wa kanisani walistuka, akiwemo Eben nae alistuka, akanifwata DM akasema malkia wangu umeniacha why Bite why? Sikumjibu nikasema aende huko
Baada ya wiki nikapost picha za graduation, weeeh wakastuka tena, hongera sana Bite hongera, hadi Dada zangu wale wakawa wanacomment. Mmoja akasema Bite wewe ni msiri sana 😀😀
Hawajakaa sawa nikapost video nasafiri kwenda Canada, mpaka nafika napokelewa, picha za sherehe Canada weeeh walichoka, wakaanza Dada kumbe uko Ulaya Daaah tukumbuke na sisi, unaambiwa vijana wa kanisani walijaa DM kuniomba niwakumbukee. Sikuwa najibu.
Sasa wiki iliyopita nimepost picha zangu za mimba na video nikiwa hospital mpaka kujifungua. Nikapost Mtoto japo nimeficha sura. Nikaona Dada yangu Joy kacomment My Son I love you, ukija bongo Mamkubwa nitakubeba mwanangu, yani ni comment za upendo tu.
Niseme tu kwa ufupi niko Canada, sasahivi nimejifungua tayari nina Mtoto wa kiume, hakika Mungu ni muaminifu.
NISEME TU WATESI WAMEPIGWA NYUNDO YA UTOSI, HAWAAMINI KILICHOTOKEA. SASAHIVI NINA MAISHA YANGU YA FURAHA NA AMANI SANA. HAKIKA MUNGU AMEFANYA TENA KWA UKUU.
NIKUTIE MOYO NA WEWE RAFIKI YANGU USIKATE TAMAA, KWA MUNGU HAKUNAGA KUCHELEWA WALA KUWAHI, KILA MTU ANAFIKA KWA WAKATI WAKE.
MUNGU AWABARIKI, NAWAPENDA
MWISHOOOOO