Sijui Ni Wangapi Nimewaambukiza Mpaka Sasa
Mimi ni mwanafunzi wa chuo, binti mwenye sura ya kawaida lakini anayejua kuitumia. Natabasamu na kuongea kwa upole, lakini ndani yangu nimebeba maumivu makali sana. Na leo, nimeamua kusema ukweli wangu, kwa sababu nimechoka kubeba mzigo huu peke yangu.
Nilipoingia darasa la sita, familia iliniamini sana, nilikuwa nakaa kwa dada yangu mkubwa, alinihudumia kama mama. Shemeji yangu,mume wa dada yangu alikuwa kama baba kwangu. Lakini usiku mmoja uliharibu kila kitu,alinibaka, nilijichukia sana.
Dada yangu hakutaka kusikia haya mambo,alisema namkosea heshima mume wake. Nilikua nalia kila usiku. Hakuna aliyeniona,hakuna aliyeniuliza “uko sawa?”
Miaka ikaenda niliendelea kusoma, lakini nikawa siyo yule yule tena. Nilianza kuwa na hasira na wanaume,nikawa siamini mtu yeyote. Nilijifundisha kuficha chuki yangu ndani ya tabasamu na nikaanza mpango wangu wa kulipa kisasi. Bila kujua, nilikuwa nimeambukizwa virusi vya UKIMWI na shemeji yangu.
Nilipofika chuoni, nikageuka kuwa mtu mwingine nikawa natafuta wanaume hasa waliooa nilikuwa nawafanya wanione kama mwanamke wa ndoto zao nikawaambia maneno wanayotaka kusikia, nikawapa mapenzi ya kuwakoleza,na baada ya hapo, nilihakikisha wanakuwa sehemu ya kisasi changu.
Sijui ni wangapi nimewaambukiza mpaka sasa wengi wao ni waume za watu, viongozi wa makanisa, walimu, wafanyabiashara na sijawahi kuwaambia ukweli. Niliamini kama mimi niliumizwa bila huruma, basi nitafanya dunia yote ilie pamoja nami.
Lakini leo… leo nimechoka kuvaa tabasamu la kishetani huku nikiungua kwa ndani.Najua ninachokifanya si sahihi,lakini je, ni nani aliyenisaidia kipindi nilipokuwa nalia na unyanyasaji niliofanyiwa?
Siombi huruma yenu maana ni mfu mtarajiwa,naomba ushauri tu.
Je, naweza kubadilika?
Nawezaje kuiponya nafsi yangu yenye uchungu?
Nawezaje kurudisha utu wangu uliopotelea kwenye visasi?