NILIMUUA MUME WANGU KICHAWI ILI NICHUKUE MALI ZAKE
Mwanamke kutoka Kaunti ya Kisii aliyetambulika kwa jina la Anne amefunguka kuhusu kisa cha kuumiza na kushtua cha jinsi tamaa ilivyompelekea kufanya kosa lililobadili maisha yake.
Akizungumza wakati wa mahojiano na Tales Extraz, Anne alieleza jinsi tamaa yake ya kuchukua mali ya marehemu mumewe ilimsukuma kufanya jambo ambalo sasa anajutia sana.
Kulingana na Anne, mumewe alikuwa mwanamume tajiri ambaye alikuwa na nyumba kadhaa Nairobi, Kisii, Nakuru, na Eldoret. Alisema alilemewa na tamaa na kuanza kufikiria jinsi ya kutawala mali yake yote.
Jambo hili lilimpelekea kupanga hatua ya hatari ya kumnyamazisha ili aweze kurithi kila kitu peke yake.
Anne alizidi kufichua kuwa mamake alihusika na uchawi na kumuelekeza nini cha kufanya.
Kufuatia maagizo ya mamake, alidai alitumia uchawi kumuua mumewe. Hata hivyo, baada ya kifo chake, mambo hayakwenda kama alivyotarajia.
Alieleza kwamba wakati wa mazishi ya mume wake, ukweli wa kushtusha ulijitokeza. Aligundua kwamba mume wake alikuwa na watoto wengine kutoka kwa ndoa ya awali, jambo ambalo hakuwahi kujua.
Kulingana na mila zao za kitamaduni, watoto wa kwanza kutoka kwa ndoa ya kwanza walikuwa na haki ya kurithi mali. Hii ilimaanisha Anne aliachwa bila chochote licha ya yote aliyoyafanya.
Akiwa amejawa na majuto, Anne anasema anatamani angalijua kweli mapema. Alikiri kwamba kama angejua kuhusu watoto wengine, hangeweza kamwe kuchukua hatua kama hiyo. Sasa anaishi na hatia na maumivu, akisema matendo yake yaliharibu maisha yake badala ya kuyaboresha.

