NATAMANI SANA KUFANYWA ILA MUME WANGU SASA
Nimeolewa sasa ni mwaka wa 8. Tulipoanza safari ya ndoa, nilidhani tumepata msingi wa furaha na upendo wa kudumu. Lakini baada ya mwaka mmoja tu, mume wangu akaongeza mke mwingine. Cha kuniuma zaidi ni kwamba aliyemuoa ni jirani yangu wa karibu kabisa. Nilihisi kama moyo wangu umepasuka vipande vipande,kwanza kwa sababu ni jirani, na pili kwa sababu tangu wakati huo mume wangu alianza kunitenga.
Mambo yalibadilika ghafla. Akawa hataki kushiriki tendo la ndoa na mimi. Nikimgusa, mara nyingi hunikatalia. Na siku chache ambazo anakubali, ni dakika moja au mbili tu, kisha anamaliza kana kwamba ni kazi ya haraka, si tendo la upendo. Nilipojaribu kumwambia aniachie ili niishi maisha yangu, alikataa. Nilishawahi hata kutoroka nyumbani kwa uchungu, lakini akanifuata na kunirudisha kwa kunibembeleza kwa pesa. Hata hivyo, moyo wangu haukupata faraja.
Tumebarikiwa kupata mtoto mmoja. Lakini mwenzangu hajabahatika kupata mtoto. Hata hivyo, bado mume wangu anaonekana kumpa yeye upendo na nafasi kubwa kuliko mimi. Kuna nyakati tunalala kama kaka na dada kwa miezi mitano au sita bila yeye kunikumbuka kama mke. Nikimkumbusha mimi, ananisikiliza kwa muda mfupi, kisha ananisahau tena. Nimechoka kumkumbusha kila mara. Nimechoka kuomba nafasi ya kupendwa moyoni mwake. Nimechoka kuishi kama mke wa jina tu.
Naona wazi kabisa ameshapata mtu anayempenda kwa dhati. Mimi nipo tu, kama kivuli cha ndoa. Nafsi yangu imedhurumiwa. Wenzetu wana ruhusiwa kuwa na wake wanne, lakini sisi wanawake hatujaruhusiwa kuwa na waume zaidi ya mmoja. Nikizini, namuogopa Mungu kutenda dhambi. Lakini kuendelea kuishi hivi, bila heshima, bila upendo, bila kufanywa, ni kama adhabu kwangu. Kuniacha hanitaki. Kuendelea kuishi hivi mimi siwezi. Nimefika mwisho wa uvumilivu.
Najiuliza: nifanyeje ili nijinasue? Nifanyeje ili nipate tena heshima na amani ya moyo? Nimebaki kama mfungwa wa ndoa, kama nimepoteza thamani yangu. Nalia moyoni, nahisi kama dunia imenigeuka.

