UCHAWI WA BIBI YANGU UMENIFANYA NIISHI MAISHA MAGUMU SANA
Mimi ni msichana mwenye umri wa miaka 24 na nina mtoto mmoja. Kabla sijapata mtoto nilikuwa nikisumbuliwa na matatizo ya kiafya kwa muda mrefu sana. Mama yangu alinipigania kila hospitali, tulikosa majibu. Tulienda hata kwa manabii, bado hakukuwa na mabadiliko. Baadaye tukaenda kwa wataalam wa jadi nao wakasema tatizo langu linasababishwa na bibi yangu mzaa mama. Ukweli ni kwamba bibi mara kadhaa amewahi kunitamkia maneno mabaya na kunikatia tamaa, lakini sikuwa na uhakika.
Nikiwa bado naumwa, nilikuwa ninaishi kwa dada yangu mjini ilhali mama alikuwa kijijini. Hatimaye nikapata mchumba ambaye alinipenda na akanipigania sana kwenye afya. Alikuwa mwanaume wa kwanza kabisa kukutana nami kimwili. Alipanga kuja kujitambulisha nyumbani, na kwa bahati nzuri bibi yangu alikuwa amefika mjini kwa mama mdogo wakati huo, hivyo wakaonana.
Siku ya kuondoka, mchumba alitoa pesa kwa heshima na kumpa bibi. Lakini baada ya siku kadhaa, alianza kuniuliza kuhusu uchawi na kama bibi yangu ana mambo hayo. Nilimficha ukweli nikamwambia hapana. Ghafla mambo yakabadilika, akaniambia hawezi kuendelea na mimi kwa sababu hataki kurukwa kiroho. Tukaachana.
Kuanzia hapo, kila mwanaume aliyepanga kuja kwetu kunioa au kujitambulisha alikimbia bila sababu ya msingi. Hali yangu ya kiafya ikaendelea kuwa mbaya. Nilikuwa nikiwaza kama kweli bibi alikuwa ananisababishia matatizo haya.
Baadae nikakutana na mwanaume aliyekuwa mtu mzima, miaka 40 na kitu. Alinisaidia sana, lakini akawa hataki kupima afya na nikagundua anaishi na virusi. Nikaanza kumkwepa polepole. Alinipa pesa ya nauli nikaondoka mjini kurudi kwa mama kupata tiba upya.
Wakati niko kwa mama, maisha yalikuwa magumu. Mama hakuwa tena na nguvu ya kufanya kazi za vibarua. Tuliendelea kumwomba Mungu. Baadae nikakutana na mwanaume mwingine wa miaka 34. Nilimpa ukweli kwamba mimi ni mgonjwa na nimepitia mateso mengi. Akanijibu kwamba hakuniona kwa mwili tu, bali ananipenda pamoja na matatizo yangu.
Alikuja nyumbani kujitambulisha, na mama alimpa ukweli wote juu ya hali yangu. Akaahidi kunipenda na kunisimamia. Alipambana sana na mimi, hadi nikaanza kupata nafuu. Aliniambia hakuna mwanaume mwingine angeweza kutumia pesa zake kwa mtu ambaye hana mpango naye kama asingekuwa na dhamira ya kweli.
Alitaka tuishi pamoja, na baadae tuwaze ndoa. Ila kule alipokuwa anaishi kulikuwa na wapangaji wengi, wakiwemo wanawake waliokuwa na chuki juu yangu bila sababu. Kulikuwa na msichana mmoja ambaye alikuwa na ukaribu wa ajabu sana na mchumba wangu kiasi kwamba alikuwa akija kwangu kuniomba nguo za bwana wangu azivae. Bwana wangu alianza kunichukia taratibu, akawa hataki kuongea nami, vituko vikawa vingi.
Hatimaye tukagombana na akanifukuza. Nikaondoka nikarudi kwa mama. Siku chache baadae nikaanza kuumwa na nikagundua nina ujauzito wake. Ingawa tulikuwa hatuelewani, wakati wa kujifungua alituma pesa zote za matibabu. Nilizaa kwa upasuaji. Alikaa kimya mpaka mtoto akafikisha siku 40 ndipo akarudi kwenye mawasiliano akisema hataki kunichukia kwa sababu siwezi kukosea kumzidi mtoto wake.
Lakini bwana huyu hana msimamo — mara ananiambia yupo kwa ajili yangu na mtoto, mara anatoweka. Wakati mwingine anaongea vizuri sana, siku nyingine anakasirika na kuninyamazia. Nikamwambia ukweli: kama hanitaki, aniweke huru ili nilee mtoto nami nifanye maisha. Lakini anasisitiza kwamba hanichukii, anampenda mtoto, na pia ananipenda ila maisha yamekuwa magumu kwake.
Hadi sasa sijui msimamo wake. Hali yangu ya kiafya bado haijatengemaa, na bibi yangu bado anaendelea kunifuatafuata kiroho. Naumia sana kwa sababu sioni kama baba wa mwanangu anapanga maisha ya pamoja nami. Mara anasema anatafuta maisha mazuri kwa ajili ya mwanae, mara ananikaushia.
**Sasa kaka Spesho, naomba ushauri:
Nifanyeje kuhusu huyu baba wa mwanangu?
Nimsubiri?
Au niachane naye kimya kimya nilee mtoto mwenyewe?
Je, niendelee kumwomba Mungu anipiganie au niweke nguvu katika maisha yangu bila kumtegemea?**
Naomba ushauri maana maisha yamenichosha, lakini sijui lipi sahihi la kufanya.

