ALINIKATAA NIKAAMUA KUMUOA DADA YAKE, AMEMCHUKIA SANA
Habari kiongozi, Naomba nikushirikishe mkasa huu kwenye mahusiano yangu, naishi Dodoma kikazi. Mwaka 2014 nilipopata ajira na kupangiwa Dodoma nilikutana na dada mmoja kwa jina Maria wakati huo akiwa mwaka wa kwanza Chuo Udom..
Nilimpenda sana na kwa wakati huo na yeye alionesha kunipenda tukawa kwenye mahusiano yenye furaha na amani so nilijitoa kwake kwa kiasi kikubwa kwa maana sikutengemea kama ipo siku anaweza kunigeuka. Alipomaliza chuo na kupata kazi ya ualimu (Shule ya private) huko Kilimanjaro aliniomba nilipangishie nyumba na kununua vitu vya ndani kama kitanda n.k ili iwe ni rahisi nikienda huko badala ya kwenda kulala hotel na nilifanya hivyo.
Cha ajabu alianza kubadilika taratibu akisingizia kazi inamfanya awe busy muda mwingi na nikimwambia naenda kwake amaleta sababu mbalimbali kama vile yuko amepangwa kufundishwa masomo ya usiku huko shule.
Kuna siku niliforce kwenda akaniambia tukutane mjini (hotel) kitu ambacho nilikataa na kweli hadi narudi sikuweza kuonana naye akawa hata simu zangu hapokei alikata katu kwenda huko nilipompangishia.
Nilirudi Dodoma na ikawa ni mwendo wa ugomvi na kunitamkia maneno ya kama vile sijitambui, nampigia makelele na mwisho alinitamkia kuwa tuachane
na huo ndo ulikuwa mwisho wa mahusiano.
Naomba nikurudishe nyuma kipindi anasoma chuo nilishawahi kumsindikiza kwenye mahafari ya dada yake huko Manyara akiwa anahitimu chuo cha uuguzi cha kushangaza sikutambulishwa kwa ndugu zake na hata akiulizwa aliwaambia kuwa mimi ni shemeji yake. Kwa sababu tulienda huko Manyara na usafiri wa private nilihusika kuwasafirisha ndugu zake kutoka sehemu moja kwenda nyingine kitendo kilichopelekea kupata mawasiliano ya dada yake (mhitimu) nilipompeleka salum.
Nikurudishe nyuma baada ya mpenzi wangu kumaliza chuo kabla ya kupata kazi aliishai na dada yake ambaye kwa wakati huo yeye alikuwa tayari kashaajiriwa na serikali huko Dar es salaam Muhimbili. Wakati mpenzi wangu akiwa kwa dada yake inasemekana mara kadhaa dada yake alikuwa akimuuliza kama mimi na yeye tuna mahusiano ya kimapenzi lakini mdogo mtu (Maria) alimkatalia katu kuwa katuna mahusiano.
Sasa basi mara kadhaa dada yake alikuwa akinisalimu na kunishukuru sana kwa namna nilivyojitoa siku ya mahafari yake na ilifika muda ukaribu ukawa mkubwa sana wakati huo mahusiano na mpenzi wangu yamekwisha na huo ndo ulikuwa mwanzo wa mahusiano mapya na dada yake yalipoanzia na nilivyojaribu kuwashirikisha baadhi ya wazee kuomba ushauri walinipa baraka za kuendelea na dada yake kwa sababu mimi sikumwacha ila yeye.
Habari zilipomfikia Maria (mdogo mtu) kuhusu mahusiano yangu na dada yake vurugu zilikuwa nyingi sana akimtuhumu dada yake kumchukulia mpenzi wake lakini kesi hiyo ilivyofika kwa wazazi wake waliitupilia mbali kwa kuulizwa kwa nini hakunitambulisha siku ile ya mahafari ya dada yake? hata kama sio kwa wazazi alikuwepo shangazi ama hata dada yake. Swali jingine aliulizwa na wazazi wakati dada yake anamuuliza mara kadhaa kwa nini alimficha kama ni kweli?
Nilipeleka barua ya uchumba ya kumchumbia dada yake ikapokelewa na ndoa ikafungwa licha ya kupeleka pingamizi pia kanisani kwa baba paroko. Hadi sasa ni miaka 10 ya ndoa tumebahatika kupata watoto watatu, wawili wa kiume na mmoja wa kike ila mpaka sasa kwa miaka hiyo yote ndugu hao wa tumbo mmoja hawajawahi kuongea licha ya juhudi mbalimbali za kuwapatanisha.
Naomba msaada wako nifanye nini ili waweze kuyamaliza hawa ndugu wa tumbo moja maana Maria kwa sasa wameshaolewa ana maisha yake. Asante na Mungu akubariki.

