MPENZI WANGU AMINA
ONYO: Wakubwa tu, kuanzia Miaka 18, ndio wasome hii Hadithi
Sehemu ya Nne
Amina na Elias walishituka sana baada ya kunisikia nikimuita Amina. Wakaachiana haraka sana, Elias alinitazama na alionekana kuingiwa na woga ndani yake. Amina hakutikisika zaidi ya kubaki ananitazama huku akiwa bado ameegemea pale pale ukutani alipokuwa ameegemea.
Sikutaka kusikiliza maelezo yoyote yale kutoka kwao kwani tayari nilikuwa nimeshashuhudia kila kitu nilichopaswa kukishuhudia. Kwa hasira nilimkimbilia Elias alipokuwa amesimama kisha nikaruka juu huku nikiwa nimekunja ngumi ambayo niliipeleka moja kwa moja kwa Elias ikalisalimie shavu lake.
“Paaah!!!” Ngumi yangu nzito ilitua shavuni kwa Elias ambae alijitahidi kujizuia asianguke lakini uzito wa ngumi yyangu ulimpeleka chini moja kwa moja.
Sikuwa na muda wa kumsubiri anyanyuke kwani nilimfuata pale pale chini na kumkaba shingoni, kisha nikammiminia ngumi tatu za haraka haraka usoni kwake jambo lililomfanya Elias anaanze kulia kama mtoto mdogo kwa maumivu aliyoyahisi.
Amina kuona vile alinifuata na kunikumbatia kwa nyuma, mgongoni akinitaka nimuachie Elias lakini nilimsukuma pembeni kama karatasi. Sijui hata zile nguvu nilizitolea wapi, kisha nikaendelea kumshushia makonde Elias ambae alikua anajitahidi kujiziba uso wake ili nisimuumize zaidi. Mie sikulijari hilo kwani nilidhamiria kabisa kumdhuru Elias hivyo nilikuwa nampiga popote pale ambapo ngumi zangu ziliweza kutua.
Amina kuona vile aliona ni bora akaombe msaada kwa wanafunzi wenzetu. Kwa haraka sana alinyanyuka kisha akaanza kukimbia kuelekea kwenye darasa lililokuwa karibu na pale nilipokuwa nampigia Elias.
“Elias anakufa huku Jamani msaada Giiii atauwa…..” Amina aliongea huku akiwa analia baada ya kuingia kwenye darasa la karibu ambalo lilikuwa na wanafunzi wa kidato cha tatu.
“Unasemaje hebu ongea taratibu nikuelewe” Mwalimu aliyekuwamo mule darasani alimuuliza Amina amwelezee kinachoendelea.
“Mwalimu Gift na Elias wanapigana huku, watauana hao” Amina alimweleza mwalimu yule huku akiwa analia.
Mwalimu kusikia vile, aliamua kuongozana na Amina kuelekea huko alikoelekezwa. Wanafunzi nao hawakuwa mbali kwani walifuatia msafara kwa nyuma kwenda kushuhudia tukio lile.
Mwalimu pamoja na wanafunzi wote hawakuamini walichokiona. Walimkuta Elias akiwa amelala chini kama mfu, huku damu nyingi zikiwa zinamvuja. Muda huo mimi nilikua nimesimama huku nikihema juu juu kwa hasira. Akili yangu ilikuwa haijakaa sawa bado kwani kitendo kile nilichokuwa nimekifanya nilikua naona kipo sawa kabisa.
Mwalimu alinisogelea nilipokuwa kisha akaanza kunipiga makofi mfululizo ambayo sikuwa hata nayahisi ukali wake. Moyo na akili yangu vilikuwa na maumivu zaidi hata ya hayo makofi ambayo niliona kama mwalimu ananipapasa tu,
“Mbebeni mwenzenu mumuwahishe hospitali” Mwalimu aliwaamuru wanafunzi wenzangu wambebe Elias. Na aliendelea kunishushia kipigo ambacho sikuwa nakihisi kabisa.
Mbele za macho yangu nilikuwa namtazama Amina ambae alionekana kuwa analia, ndio Amina alikua analia!!! Na muda ule nilijua fika aliyekuwa analiliwa pale hakuwa mimi bali ni Elias. Ukweli ule uliuvunja sana moyo wangu, maumivu niliyokuwa nayahisi pale hayakuwa ya kuelezeka kwa kinywa hiki hiki cha mwanadamu. Akili yangu iilikuwa inawaza mengi yasiyotamkika, kubwa zaidi niliwaza ni kosa gani kubwa nililomtendea Amina kiasi cha kuniadhibu kiasi kile, niliwaza, inamaana Amina amekosa wanaume wengine wote huko nje hadi akatoke na rafiki yangu kweli, sikuwa na majibu.
Nilipelekwa ofisini, huko nilifika na kufungiwa kwenye moja ya ofisi za pale shuleni, tayari mwalimu alikuwa ameshapiga simu polisi kuwajulisha kuhusu tukio lile, alifanya hivyo ili kusaidia upatikanaji wa PF3 mapema kwa ajili ya matibabu ya Elias pindi atakapofikishwa hospitali.
Baba yangu hakuwa na neno zaidi ya kubaki akishangaa, alijaribu kujiuliza ni nini kilichonikumba hadi kufikia hatua ile ya kumpiga mtu nusu kumuua, hakupata majibu.
“Kwahiyo mwalimu unanisaidiaje juu ya mwanangu najua polisi wakishafika hapa watahitaji kuondoka nae” Baba yangu alimuuliza mwalimu Justus
“Mzee wangu sina msaada wowote ule zaidi ya kukuomba tuwasubiri polisi wafike maana haya ni maagizo yao kuwa mwanao afungiwe mahala peke yake hadi watakapofika” Mwalimu Justus alimjibu baba yangu
“Sawa mwalimu naelewa hilo lakini kumbuka huyo ni mtoto bado tunapaswa kumkingia kifua”
“Mzee wangu….. Naona kama unapoteza muda wako hapa cha kukuomba labda hebu fanya kuiombea afya ya Elias huko aliko asije kufariki maana akishafariki tutazungumza mengine hapa” Mwalimu Justus alimwambia baba yangu kauli nzito yenye ukweli ndani yake iliyomfanya awe mpole.
Maombi na sala kichwani mwa baba yangu viliongezeka, pamoja na kwamba nilikuwa nimekosea kupigana lakini hilo halikubadilisha uhalisia wa kwamba mimi nilikua bado ni mwanae hivyo ilikuwa ni wajibu wake kunitetea.
Polisi walifika na kuelezwa kila kilichokuwa kimetokea. Baada ya kuwa wamejiridhisha na maelezo ya mwalimu walimuomba baba yangu wazungumze nae. Baba aliwaitikia na walimweleza uhalisia wa mambo jinsi yalivyokuwa.
“Hadi muda huu hali ya mgonjwa ni mbaya sana huko hospitali na haijulikan kama ataamka au lah hivyo basi mzee wetu tutaondoka na mwanao hadi kituoni huko tutakaa nae hadi pale mgonjwa atakapozinduka”.
“Sawa nawaelewa sana ndugu zangu vipi hakuna namna yoyote ya kunisaidia ili mwanangu asiende kulala polisi”
“Mzee wetu bila kukuficha kitu, hakuna tunaloweza kukusaidia zaidi ya kukuomba uzidishe maombi zaidi kesi hii isije badilika na kuwa kesi ya mauaji” Polisi yule alimalizia kuongea kisha akamuomba mwalimu Justus awaelekeze walikokuwa wameniweka.
Polisi walikuja na kunichukua, moja kwa moja hadi kituoni. Huko nilifika na kukabidhi vitu nilivyokuwa navyo mapokezi kama viatu, mkanda wa suruali na karamu za kuandikia kisha nikaelekezwa niingie rumande.
Labda niseme jambo moja hapa, katika umri wangu huu wa miaka thelathini na saba nadhani hilo ni moja ya tukio ambalo sintokaa nilisahau hadi naingia kaburini.
Nakumbuka wakati naingia rumande kwa mara ya kwanza siku ile nilikuwa na miaka kumi na saba tu. Nakumbuka nilipokelewa na harufu kali iliyokuwamo mule ndani, joto kali iliyokuwamo mule ilifanya midume yote iliyokuwamo mule ndani ivuje jasho lililokuwa linatoa harufu kali kwani mule ndani hakuna aliyepewa nafasi ya kuoga bila kujali umekaemo kwa muda gani.
Mbaya zaidi ndoo kubwa iliyokuwa mule rumande kwa ajili ya kujisaidia haja ndogo na kubwa ilifanya hali ya hewa ibadilike zaidi kila ilipofunuliwa ili watu wajisaidie.
Cha ajabu kuna watu niliwakuta mule ndani wakiwa wameshaizoea ile hali na hawakuonekana kusumbuliwa kabisa na ile hali kwani walikuwa wanapiga stori zao kama kawaida huku wakicheka sana.
Kwangu mimi nilijihisi Kufa kufa hivi, joto kali jumlisha na ile harufu kali vilinizidia kiasi cha kunifanya nianze kuhisi kizunguzungu hivyo ilibidi nitafute mahala na kuketi.
Nikiwa nimeketi pale, geti la rumande lilianza kupigwa pigwa kwa nguvu na afande aliyekuwa nje akiashiria watu wote wasogee nyuma. Haraka haraka watu wote walirudi nyuma kwa woga kisha geti lile likafunguliwa na katika hali nisiyoitarajia askari wale waliingia ndani wakiwa wamemshikiria jamaa mmoja aliyekuwa amevalia chupi tu, yaani hakuwa na kitu kingine kwenye mwili wake zaidi ya hiyo chupi kisha wakamrushia ndani kwa nguvu jambo lililopelekea yule jamaa aanguke chini kwa nguvu na kuanza kuugulia maumivu.
Kwa kumtazama tu alionekana kuwa ni mtu aliyetoka kupigwa sana. Mwili wake wote ulikuwa unamtetemeka na alionekana kutokuwa na nguvu hata za kujigeuza zaidi ya kubaki pale pale chini ametulia akiugulia maumivu.
Huruma ilinijaa, nilijikuta namuonea huruma yule jamaa, ni kama niliyasahau matatizo yangu kwa muda, hali aliyokuwa nayo ilionekana kuwa mbaya sana lakini hakuna aliyeonekana kujali
“Braza kwani jamaa kafanya nini hadi apigwe hivyo?” Nilimuuliza Mshikaji mmoja aliyekuwa amekaa pembeni yangu
“Mwenzio ana mada kesi hapo alipo”
“Mada kesi?!!, unamaanisha nini kaka”
“Kaua mwenzako hapo alipo, huna haja hata ya kumuonea huruma anastahili kabisa kipigo hicho” Yule mshkaji alinieleza, na alionekana kumaanisha kila alichokiongea.
Ilibidi nimtazame tena yule jamaa aliyekuwa amelala pale chini jinsi alivyokuwa ameumia vibaya kwa kipigo kisha nikawaza inamaana na mimi kama Elias akifariki huko hospitali basi kipigo kama cha huyo jamaa kinaweza kunikuta.Nilijikuta naanza kupata woga na kujutia maamuzi yangu ya kumpiga Elias. Na jambo pekee nililokuwa nimebakisha ni kuuombea uhai wa Elias ili nitoke salama mule rumande………
Elias alifikishwa hospitali ya Mwadui na kuanza kupatiwa matibabu. Madaktari walitumia zaidi ya lisaa limoja kumshona uso wake ambao nilikua nimeuhatibu vibaya sana. Amina yeye muda wote alikua amekaa nje ya wodi aliyokuwa anatibiwa Elias na muda wote alikua analia tu. Mwalimu na wanafunzi kadhaa pia walikuwapo, na wote kwa pamoja walionekana kuwa na mawazo juu ya hali ya Elias ambae walimfikisha hospitali pale akiwa hajielewi kabisa.
“Dokta vipi hali ya mgonjwa” Mwalimu Justus alimuuliza daktari baada ya kumuona akitokea katika chumba cha matibabu.
“Mgonjwa wenu anaendelea vizuri, na hivi tunavyoongea ameshapelekwa wodini akapumzike lakini itahitajika watu watatu wajitokeze kwa ajili ya kumchangia damu kwani amepoteza damu nyingi sana” Dokta alimaliza kuzungumza kisha akaondoka zake na kumuacha mwalimu Justus na wanafunzi wake wakijadili kuhusu suala lililokuwa mbele yao la kuchangia damu.
Siku mbili zilipita ndio Elias akaruhusiwa kurudi shule, taarifa zile zilikuwa nzuri sana kwa wazazi wangu maam Amina na baba yangu ambao wote walikuja kituoni kwa pamoja kwa lengo la kunitoa rumande. Baba alifanya mambo yote aliyoelekezwa na polisi na baada ya kumaliza niliruhusiwa kutoka.
Nilikua na furaha sana ya kutoka siku hiyo kwani siku tatu hizo nilizokuwa nimelala mule mahabusu kwangu niliziona kama ni mwaka vile. Mama Amina alinikumbatia baada ya kuniona na kunipatia pole lakini baba yangu yeye aliishia kunitazama tu na zaidi alitueleza mimi na mama Amina tufanye haraka tuondoke tusije chelewa usafiri wa kuturudisha nyumbani Kahama.
Tukiwa njiani, njia nzima sikuwa naongea, japo mama Amina alijitahidi sana kunisemesha bila Mafanikio. Akili yangu haikuwa sawa, mambo niliyokuwa nimeyashuhudia mule mahabusu yalinifikirisha sana. Nadhani nilipaswa kupelekwa humo ili nikajifunze zaidi kuhusu maisha. Jambo moja kubwa nililojifunza nikiwa rumande ni ushirikiano, kwani kwa siku zote zile mbili kamili nilizokuwamo mule ndani baba yangu hakuwahi kuniletea hata andazi moja lakini sikulala njaa kwa sababu ya ushirikiano waliokuwa nao wale watuhumiwa wenzangu, kwani hakuna mtu aliyeletewa chakula na akakila peke yake, ilikua ni kama amri ya kuwa atakayeletewa chakula basi wote lazima tutakigawana chakula kile.
Tulipofika nyumbani moja kwa moja nilikwenda kulala. Sikutaka hata kula chakula chao walichokuwa wameniandalia,
“Usiwaze sana mke wangu bado anamawazo huyo atakuwa sawa” Baba yangu alimtoa hofu mama Amina ambae muda wote alionekana kuwa na wasiwasi na mimi.
BAADA YA MIEZI MIWILI
Penzi la Amina na Elias lilishamiri, hakuna ambae hakujua tena kuhusu mahusiano mapya kati ya Elias na Amina. Wapo waliowabariki na wapo waliomuona Elias kama msaliti kwani Amina alikua ni mpenzi wa rafiki yake wa karibu sana. Elias hakujari hilo kwani alikua ameshampenda Amina na Amina aliridhia kuwa naye kwa moyo wake wote.
Vidonda na maumivu aliyoachiwa na Gift hakuyakumbuka tena kwani tangu atoke hospitali Amina alikuwa mstari wa mbele kumuhudumia. Kiufupi Elias hakupata tabu ya kujihudumia kwani alihudumiwa na Amina kimwili na kiroho pia, hivyo kupona kwake lilikua ni suala la muda tu.
Muda ulizidi kwenda na mitihani ilizidi kukaribia, lakini kadri muda ulivyozidi kwenda Amina alianza kuhisi mabadiliko makubwa kwenye mwili wake ambayo hakuwa anayaelewa. Kwanza alianza kuwa ni mtu anayekuwa anahisi uvivu sana na mara kadhaa alianza kuwa anasumbuliwa na kizunguzungu ambacho kila mara alipokuwa anamweleza Elias aliishia kuambiwa ajitahidi kunywa maji mengi yatamsaidia.
Amina pia alianza kubagua vyakula, mara nyingi alikuwa anajikuta anashindwa kula wali na badala yake akawa anakula ugali tu. Jambo hilo hakuwa analielewa kabisa kwani kiuhalisia Amina alikuwa anajifahamu sana ya kuwa anapenda sana wali kuliko ugali, sasa vipi mara hiyo aanze kukataa kula wali na badala yake apende kula ugali tu, Hakuelewa.
Ukiachana na yote hayo Amina alianza kuwa mtu wa kuhisi kichefu chefu sana kilichompelekea awe anatapika mara kwa mara kitu kilichomfanya ahisi kuwa atakuwa anaumwa sana hivyo akaomba ruhusa ya kwenda hospitali akapime ili ajue shida ni nini hasa iliyokuwa inamsumbua.
“Tumekupima vipimo kadhaa na tumegundua kuwa wewe ni mjamzito” Daktari alimueleza Amina ambae hakutaka kuamini alichokisikia,
“Dokta unasema? Mimi nina nini? Mimba!!!! Acha basi kunitania dokta” Amina aliuliza mfululizo kutaka apatiwe majibu aliyoyahitaji
“Ndio vipimo vinavyoonesha binti yangu, nadhani huu ni muda wa kutulia na kujipanga ujue utailea vipi hiyo mimba, baba wa mtoto si unamfahamu?” Daktari alimalizia kwa kuuliza swali ambalo Amina aliliona ni kama anaoneshwa dharau hivi.
“Unamaanisha nini kuniuliza kama baba wa mtoto namfahamu? Au unahisi mimi ni Kahaba sio?” Amina alimuuliza daktari kwa jazba
“Hapana sio hivyo nili…………”
“Nyamaza huko usije kunivuruga zaidi, eti baba wa mtoto namfahamu?!! Kwa kunionaje labda, huo udaktari wako usikupe haki ya kujaji maisha ya wenzako kirahisi rahisi hivyo” Amina aliongea kwa hasira sana kisha akatoka ndani ya chumba cha daktari akiwa na hasira sana.
Hasira zile hazikuwa ni hasira kwa ajili ya daktari yule bali hasira zile zilikuwa ni hasira dhidi yake. Amina alihisi kujichukia kwa uzembe alioufanya wa kuruhusu kubeba mimba hali ya kuwa anajijua yeye bado ni mwanafunzi.
“Ooh!! Mungu wangu nitaanzia wapi kumweleza taarifa hizi Elias hadi anielewe” Amina aliwaza bila kupata majibu, akawaza hata kama atawaza sana hakuna kitakachobadilika hivyo palikua na ulazima wa kumfuata Elias na kumueleza hali halisi ili aamue yeye mwenyewe ni nini cha kufanya.
“Mpenzi wangu mbona leo unaonekana kama haupo sawa” Elias alimuuliza Amina baada ya kumuona yupo kimya sana.
Tayari Amina alikuwa ameshamuomba Elias wakutane mahala wazungumzo lakini tangu wakutane Amina alikuwa kimya tu asije cha kuongea.
“Mmmh!! Unasema” Amina aliuliza kana kwamba hakumsikia Elias alichoongea
“Nakuuliza hivi mpenzi wangu….. Upo sawa kweli? Nakuona upo kimya sana”
“Aanh!! Eti eeh nipo kimya sana”
“Ndio upo kimya sana hadi unanitisha niambie shida nini Amina wangu”
“Elias mimi ni mjamzito” Amina aliona aongee moja kwa moja kilichomfanya amuite Elias pale kwani alikuwa anakosa kabisa maneno sahihi ya kumueleza.
“Wewe ni mjamzito,……..Amina unamaanisha nini kusema hivyo?!!” Elias aliuliza
“Nina mimba yako Elia”
“Mimba yangu?!! Hebu kuwa siriazi bhana, hiyo mimba iko wapi hadi useme ni ya kwangu”
“Swali gani hilo sasa Elia, mimba si ipo tumboni kwangu, nitaibebea wapi unadhani kama sio tumboni kwangu”
“Aanh kumbe!!! Sasa kama mimba ipo tumboni kwako unauhakika gani ni ya kwangu?” Elias alimuuliza Amina swali ambalo hakulielewa
“Unamaana gani kuniuliza hivyo Elia”
“Nina maana gani? Huelewi? Au ndio unajitoa akili tu hapa, unadhani nitaamini vipi kuwa hiyo mimba ni ya kwangu wakati upo nayo wewe Amina” Elias aliongea maneno yaliyomfanya Amina akose cha kuongea, akabaki anamtazama kwa muda Elias ambae alionekana kubadilika sana, hakuwa Elias yule tena wa dakika kumi zilizopita kwani Elias huyu alikuwa na sura Tofauti kabisa, sura yenye ndita na iliyoonekana kuwa na hasira sana.
“Ndio unataka kusema hii mimba nimejipachika mwenyewe au?” Amina alimuuliza Elias
“Hayo umeyasema wewe sasa, hebu fikiria hata ungekuwa wewe ungeikubali wakati unajua kabisa mpenzi wako hajatulia” Elias aliongea maneno ambayo yalimchanganya zaidi Amina
“Unamaanisha nini kusema sijatulia?”
“Usichokielewa nini hapa, kama kweli ungekuwa umetulia ungekubali kutoka na mimi wakati unajua nilikua rafiki wa mwanaume wako?……. Aya tuachane na hayo labda nikuulize swali moja tu kama kweli uliweza kumsaliti mshkaji wangu kwangu ni kipi kitakachokufanya ushindwe kunisaliti mimi kwa watu wengine huko? Nijibu”
Amina kusikia vile aliishiwa nguvu kabisa, na taratibu alijikuta anaanza kukaa chini na kuanza kulia. Alijikuta anajutia maamuzi yake ya kuwa na Elias. Ni kweli alikuwa ameachana na Gift lakini kutoka na Elias kimapenzi hakuwahi kuwaza kama kutakuja kumuadhibu hivyo,
“Naomba uniambie Elia kama hii mimba umeikataa au vipi ili nijue moja” Amina alimuuliza Elias huku akiwa analia,
“Hapana, umenielewa vibaya, sio kwamba nimeikataa hiyo mimba lakini nachojaribu kukueleza hapa ni kuwa fanya kuipeleka hiyo mimba kwa baba yake halali, tatizo haujatulia Amina nitakuamini vipi mimi” Elias alimaliza kuongea kisha akaondoka zake huku akimweleza Amina aache mazoea naye kabisa.
Amina alijikuta anaanza kulia kama mtoto mdogo. Hakutaka kuamini kama Elias ndiye aliyembadilikia kiasi kile. Hakujua ni nini afanye tena baada ya hapo. Wazo kubwa kwa muda ule lililokuwa limeitawala akili yake ni kuitoa ile mimba, hakutaka kulea kiumbe kisichokuwa na baba hivyo alihitaji kuchukua maamuzi ya haraka sana kutimiza lengo lake hilo,
“Sidhani kama nitaweza kufanya suala hili peke yangu nitahitaji msaada wa nje” Amina aliwaza, tayari alikuwa ameshafikiria jambo la kufanya. Hivyo aliamua kunyanyuka pale chini alipokuwa amekaa na kisha akajifuta machozi yake kisha akaanza kutembea kuelekea ofisini kwa mwalimu wa zamu.
Alipofika alimuomba mwalimu yule simu yake apige nyumbani kwao. Mwalimu hakumnyima kwani hiyo nayo ilikua ni kazi yake kuwasaidia wanafunzi wawasiliane na wazazi wao. Amina akapiga simu ile ambayo ilianza kusikika ikiita upande wa pili,Amina akaamua kusogea pembeni ili kuepusha mwalimu asisikie atakachokiongea,
“Halloo!!!” Niliongea baada ya kupokea ile simu
“Gift, ni wewe?” Amina aliniuliza,sikuwa na haja ya kuuliza ni nani anayeniuliza kwani sauti yake nilikuwa naifahamu sana.
“Ndio ni mimi Amina niambie” Amina kusikia nimemjibu alianza kulia kilio ambacho sikukielewa japo kiliniumiza na mimi pia kwani sikupenda kabisa kusikia Amina akiwa na huzuni, furaha ndicho kitu pekee nilichohitaji awe nacho Amina wangu
“Amina mbona hivyo unashida gani” Nilimuuliza Amina
“Giiih naomba unisaidie” Amina aliongea huku akiwa anaendelea kulia
“Nambie Amina niambie chochote kile nitakusaidia…….” Nilimweleza Amina kwa kujiamini sana kwani sikupenda kumuona Amina akiwa na shida au tatizo lolote lile
“Naogopa sana Gift sijui hata nifanye nini yani”
“Huna haja ya kuogopa Amina wee nieleze tu sawa”
“Aya sawa, Giiih nina mimba mwenzio na nina hitaji kuitoa”
Amina alinieleza maneno ambayo yaliupatia ganzi moyo wangu nikajikuta namuuliza bila kutarajia
“Mimba?!! Ya nani Amina?!! Elias au?!!”
Sehemu ya Tano
“Mbona una maswali mengi hivyo, jibu ni moja tu hapa unanisaidia au?” Amina alionekana kukasilishwa na maswali yangu
“Ni lazima nikusaidie Amina niambie nachopaswa kufanya sasa” Ilibidi nimkubalie kwani sikutaka kumkwaza.
Amina aliposikia nimemkubalia ombi lake alinipatia mpango wake wa jinsi alivyokuwa amewaza. Nilimsikiliza kwa makini kisha tukakubaliana mpango huo tutautimiza kuanzia siku inayofuata aniache kwanza nijiandae kwa ajili ya zoezi hilo lililokuwa mbele yetu. Tukakubaliana na kuagana. Amina akakata simu.
Baada ya Amina kukata simu nilijikuta naanza kupata maswali kadhaa kichwani mwangu yasiyokuwa na majibu. Kubwa zaidi nilichojiuliza ni kuhusu huo ujauzito wa Amina, niliwaza, kama ni kweli Amina ana mimba ni kwa nini anataka kuitoa? Na je baba wa mtoto ni nani?!! Mimi au Elias, nilikosa majibu. hivyo ikanibidi niachane na mawazo yale ambayo nilijua fika hata nikiwaza vipi siwezi kupata majibu yake.
Jambo la kwanza nililowaza kufanya ni kwenda duka la dawa lililokuwa karibu na nyumbani kwetu, huko nilikwenda na kuulizia dawa za kutolea mimba,
“Mimba mnayotaka kuitoa ni ya miezi mingapi” Dada aliyekuwa ndani ya lile duka aliniuliza
“Umri?!! Nadhani ni miezi miwili sasa” Nilimjibu
“Una uhakika ni ya miezi miwili” Yule dada aliniuliza
“Ndio nina uhakika” Nilimkubalia japo sikuwa na uhakika, ilibidi nimuongopee ili kutimiza lengo langu lililokuwa limenipeleka pale dukani.
Yule dada aliniomba elfu arobaini kwa ajili ya dawa nikampatia, kisha akanielekeza matumizi ya zile dawa ambayo niliyasikiliza kwa umakini sana nisije kuyakosea wakati wa zoezi lile la utoaji wa mimba.
“Najua itakuwa ni kazi sana ila usiogope, kila kitu kitakuwa sawa” Yule dada alimalizia maelezo yake kwa kunieleza kauli hiyo ambayo sikuizingatia sana.
Nilirudi nyumbani, moja kwa moja hadi kwenye kibubu changu nikakivunja na kisha nikachukua pesa zote nilizokuwa nimezitunza. Nilihitaji kuondoka jioni ile ile ili kesho yake nikafanye mpango wa kumchukua Amina shuleni. Baada ya kuwa nimeshajiandaa niliondoka nyumbani bila hata kuaga, kwani nilijua sitakua na majibu sahihi ya kuwaeleza wazazi wangu watakaponiuliza nakokwenda.
Safari yangu ya kutoka Kahama iliishia Maganzo Shinyanga ambapo nilichukua chumba cha kulala kwa lengo la kulala usiku ule hadi kesho yake asubuhi.
Asubuhi ilipofika, nilikwenda moja kwa moja hadi kituo cha maboda boda nikakodi boda moja kwa lengo la kunipeleka hospitali ya Mwadui iliyokuwa inapatikana ndani ya kijiji cha Mwadui ambacho chote kiujumla kilikuwa kimezungushiwa uzio nadhani ni kwa sababu za kiusalama za kulinda madini ya Almasi yanayopatikana pale.
Ilikuwa ni safari ya zaidi ya dakika ishirini kwa boda kutoka hapo Maganzo hadi Mwadui hivyo malipo yake yalikuwa juu kidogo ambayo hayakunipa shida kuyalipa,
“Kuna mtu tunakwenda kumchukua na kurudi nae hapa mjini lakini hatakiwi kuonekana wakati tunatoka nae humo ndani” Nilimweleza yule boda.
“Usijali kaka hizi ndio kazi zetu zinazotuweka hapa mjini shaka Ondoa kabisa” Yule boda alinitoa wasi wasi.
Mpango wetu mimi na Amina ulikuwa ni kwenda kumtorosha hospitali Amina ambako atakwenda kwa kisingizio cha kuwa anakwenda kupima afya yake kwani bado anajihisi kuumwa.
Kwa kuwa tulikuwa na lengo la kumtorosha Amina, yule boda alinishauri tupitie njia za siri kwenda na kurudi ili kuepusha mambo ya kuonekana na walinzi waliokuwa wanalilinda geti kuu la kijiji cha Mwadui, nikamkubalia. Safari yetu ilianza mida ya saa mbili asubuhi, yule boda alikuwa anaijua kazi yake kweli kwani hatukupata shida kabisa kuingia Mwadui hadi tunafika hospitali hakuna kipingamizi chochote kile tulichokutana nacho njiani.
Ile kufika hospitalini, tulimkuta Amina akiwa anatusubiria,
“Mbona umechelewa hivyo” Amina aliniuliza
“Usafiri ulikuwa wa shida sana” Nilimjibu
“Mzigo wangu uko wapi kwanza” Amina aliniuliza, nikampatia begi nililokuwa nalo akalichukua na kwenda nalo ndani ya hospitali huku akitutaka tumsubirie pale nje ya kuwa atarudi baada ya muda.
Ndani ya lile begi kulikuwa na nguo za nyumbani ambazo nilimnunulia kwa lengo la kubadilisha. Amina alibadilisha nguo zake za shule na kuziweka ndani ya lile begi alilokwenda nalo mule ndani ya hospitali kisha akavaa zile nguo nilizokuwa nimemnunulia. Baada ya kuhakikisha yupo tayari alitoka nje na safari ya kurudi mjini ikaanza.
Safari yetu ya kurudi mjini pia haikuwa na changamoto yoyote ile kwani yule bodaboda alitumia njia ile ile tuliyokuja nayo mwanzo ambayo ilionekana kuwa na usalama. Tulifika maganzo mida ya saa nne za asubuhi. Moja kwa moja tukaelekea kwenye lodge niliyokuwa nimefikia huko tulifika na kuagiza chai kwanza kabla ya kuanza mambo mengine.
Nilimweleza Amina kuwa nimeshauriwa dawa zile azitumie usiku ndio muda mzuri kwani hadi kufikia asubuhi kesho yake kila kitu kitakuwa kimeshamalizika, akanielewa. Nikamweleza ila kabla ya yote hayo kuna vitu nilihitaji kuzungumza nae
“Sidhani kama nitakuwa nina majibu ya maswali yako unayotaka kuniuliza” Amina alinieleza baada ya kusikia nataka kuzungumza nae
“Lakini huoni kama nina haki ya kujua kila kitu kwanza kabla ya yote?” Nilimuuliza
“Itakusaidia nini hata kama ukishajua”
“Haya basi sawa naomba unieleze tu jambo moja. ……. Mimba hii tunayoitoa ni ya nani?!!”
Amina alinitazama kwa muda kabla hajanijibu,
“Hivi kweli katika maswali yako yote hilo ndilo umeona ni swali la msingi sana kulijua jibu lake?”
“Ndio nadhani napaswa kujua hata jibu ya hilo swali langu moja au nakosea?”
“Aya sawa kwa kuwa umetaka kujua……. Hii mimba ni ya Elias na sio yako kama unavyowaza” Amina alinijibu, jibu lililonifanya nijikute nashusha pumzi nzito sana, ni kama nilikuwa nashukuru Mungu hivi, kiukweli sikuwa nataka kushiriki kukitoa kiumbe changu kwa Amina.
“Mbona kama umefurahi kusikia mimba hii sio yako?” Amina aliniuliza
“Hapana hata sijafurahia ila nawaza ni kwanini umeamua kuchukua maamuzi hayo ya kuitoa mimba hiyo” Nilimjibu kwa swali ambalo nilijua hatoweza kulijibu
“Nadhani swali lako nimeshalijibu, hayo mengine niachie mwenyewe” Amina alinijibu kisha akapanda kitandani kwa lengo la kulala, sikutaka kumzuia kwa sababu sikuwa na kitu kingine cha kuongea naye zaidi. Kitu pekee kilichokuwa kimebakia mbele yetu ni kusubiria ifike jioni kwa ajili ya kuanza zoezi letu la kuitoa ile mimba.
“Amina….. Amina……. amka basi muda umeshakwenda sana” Nilimuamsha Amina ambae alionekana bado kuwa na usingizi sana
“Mmmh unasema? Kwani usiku umeshafika Giih!!” Amina aliniuliza
“Hapana, amka ukaoge, ili twende tukale mapema tuna mambo mengi ya kufanya baadae” Nilimweleza
Amina kusikia vile aliamka, akaenda kuoga bafuni na baada ya muda akarudi chumbani na kubadilisha nguo kisha tukatoka pamoja nje, huko tulikwenda na kutafuta chakula tukala kisha tukaanza kupiga stori za hapa na pale. Amina aliniuliza kuhusu wazazi nyumbani na mimi nilimuulizia habari za masomo shuleni, hatukuongelea kabisa habari za mahusiano, ni kama tulichora mstari wa mazungumzo yetu.
“Nadhani turudi Lodge sasa” Nilimueleza Amina ambae nilimuona ameshaanza kunywea, nadhani woga ulikuwa umeshaanza kumuingia. Hata mie nilikuwa na hofu lakini sikutaka kuionesha kwa Amina, nilihitaji kuwa jasiri ili kumfanya Amina awe na amani.
Tulifika lodge, tukaingia ndani ya chumba chetu kisha nikatoa mashuka yote kitandani yaliyokuwa yametandikwa kisha nikatandika shuka langu nililokuwa nimekwenda nalo.
“Chukua hizi nguo ukavae huko chooni” Nilimpatia vitenge Amina ili akajifunge kwani alipaswa kubadilisha kabisa zile nguo alizokuwa amezivaa ili asije kuzichafua na damu wakati mimba inapotoka.
Amina alikwenda bafuni kubadilisha nguo, baada ya muda akarudi akiwa tayari. Nilimtazama kwa kumtamani sana, vazi lile la kitenge lilinipagawisha lakini sikutaka kuziruhusu hisia zile zinichanganye,kwani nilijua fika tukio lililokuwa mbele yetu halikuwa tukio la kuzihitaji hisia hizo.
“Naomba uketi kitandani, Kuna vidonge hapa nahitaji kukuwekea huko chini” Nilimueleza Amina ambae hakunielewa ninachokimaanisha,
“Vidonge? Vidonge gani hivyo unahitaji kuniwekea?” Amina aliniuliza
“Hivi hapa, nimeelekezwa nikuwekee huko chini kati kati ya mapaja yako na vingine utakaa navyo mdomoni” Nilimueleza
“Hapana, siwezi kukubali, hata mimi mwenyewe naweza kujiwekea naviomba nikajiwekee mwenywe kikubwa wewe nielekeze namna ya kufanya” Amina alionekana kumaanisha alichokiongea, sikutaka kubishana nae, nikampatia vile vidonge ili nianze kumuelekeza namna ya kuvitumia.
Amina alivipokea lakini kabla sijaanza kumuelekeza chochote kile simu yangu ilianza kuita, ikabidi niitazame. Elias alikuwa ananipigia, Amina naye aliliona hilo kwani alilisoma jina la mpigaji kwenye kioo cha simu yangu hivyo tukabaki tunatazamana, kichwani niliwaza nisiipokee simu ile lakini vidole vya mikono yangu vilinisaliti, nikajikuta naipokea ile simu,
“Oya Giih Amina ametoroka shule na anatafutwa kinoma, vipi labda anaweza kuwa amerudi nyumbani?” Elias aliniuliza
“Amina ametoroka?!! Kwa sababu gani?” Nilijifanya kama sijui kinachoendelea
“Acha tu Giih najuta kiukweli najuta sana kwa niliyomfanyia Amina”
“Unajuta?! Mbona sikuelewi, kwani umemfanya nini Amina eenh!!”
“Ni mambo yetu binafsi lakini kama utamuona Amina mwambie anisamehe sana yalikuwa ni masihala tu sikutegemea kama atachukua maamuzi haya” Elias aliongea. Amina muda wote huo alikua anatusikiliza tu, na alionekana kama kutaka kuongea jambo lakini alishindwa.
“Sawa nitamueleza kila kitu kama atakuja nyumbani maana hata sie bado hatujapewa taarifa kama Amina ametoroka shule”
“Ok sawa mwanangu naomba unisaidie sana kwa hilo najuta sana hapa nilipo”
“Sawa usiwaze nitafikisha ujumbe wako” Elias akakata simu, Amina akasimama kutoka pale kitandani alipokuwa ameketi kisha akaanza kuzunguka mule chumbani kama mtu aliyechanganyikiwa hivi, akawa anakaa mara anasimama bila kuzungumza chochote,
“Vipi Amina mbona sikuelewi?” Nilimuuliza
“Nadhani sikupaswa kuwa hapa Gift”
“Unamaanisha nini kusema hivyo Amina mbona sikuelewi”
“Kila kitu tunachokifanya hapa tunakosea sana Gift, Hauoni kama nitakuwa namkosea baba wa hiki kiumbe nachotaka kukitoa?” Amina aliniuliza
“Unamkosea vipi? Hebu nieleweshe”
“Gift usichokielewa nini hapa? Hauoni kama Elias bado anamuhitaji mtoto wake, alafu mimi nipo hapa nataka kumtoa?………. Aaaanh!!! Kweli mimi ni mjinga sana” Amina aliongea maneno ambayo yalinichanganya kidogo
“Amina….. Hebu tulia kwanza, mbona nakuwa kama sikuelewi, inamaana unataka kusema unataka kuhairisha kuitoa hiyo mimba ama!!!”
“Ndio, Gift siwezi kuitoa mimba hii hali ya kuwa baba yake hajaniruhusu” Amina alinijibu kwa ujasiri, macho yake yalionesha alichokuwa anakiongea alikuwa amekimaanisha, nguvu ziliniisha kwani sikujua ninapaswa kufanya nini kwa muda ule.
Nilijikuta nakaa kitandani, mwili wote ulichoka ghafla, sikutegemea kama Amina angeweza kunibadilikia haraka kiasi kile,
“Sasa Amina kama ulikuwa huna uhakika wa kile ulichokuwa unataka kuja kukifanya ni kwa nini ulinipigia simu nije huku?” Nilimuuliza Amina, tayari moyoni mwangu nilijihisi kujawa na hasira
“Mbona nakuwa kama sikuelewi Giih au furaha yako wewe ni kuona naitoa hii mimba sio?!!” Amina alinijibu kwa kuniuliza swali
“Tatizo lako Amina unakuwa sio muelewa, hivi unajua ni gharama kiasi gani nimetumia hadi muda huu?!! Au unadhani unanimudu sana ndio maana unakuwa na uwezo wa kuamua chochote kile ukitakacho?!!”
“Gift najua utanilaumu sana hapa, Aya naomba samahani kwa kukusumbua ila ndio hivyo nimeshaamua hii mimba sintaitoa tena” Amina alinijibu kwa Jeuri,
“Aaanh sawa!! Kama umeamua hivyo mie sina cha kukupinga ila naomba nikwambie kitu kimoja Amina, usije kunishurikisha tena kwenye mambo yako wewe na Elias, Kamwe!!! yaani hata kama kitokee nini maana naona kabisa tunakoelekea sidhani kama nitakuwa na nguvu za kukusaidia tena” Nilimueleza kwa jazba Amina ambae hakuonesha kuzijari hisia zangu
“Wewe amua utakavyoamua ila ndio hivyo nimeshaamua bhana” Amina alinijibu kwa dharau.
Kwa hasira nikaingia mfukoni na kutoa elfu kumi nikaitupia kitandani kisha nikachukua vitu vyangu na kuviweka kwenye begi kisha nikatoka zangu kwenda nje ya kile chumba tulipokuwa. Amina alijaribu kuniuliza nakoelekea lakini sikumjibu chochote, moyoni nilikuwa nimeshadhamiria kuondoka zangu kurudi nyumbani Kahama.
Sikutaka kuwaza kabisa kuhusu Amina atakavyorudi shule kwani nilijua atafika tu, pesa niliyokuwa nimemuachia nilijua itamtosha kabisa kumfikisha hadi shule na chenji ingebaki.
Nilifika Kahama nikiwa nimechelewa sana hivyo nikaogopa kwenda nyumbani hivyo nikaamua kuelekea kwenye moja ya Bar maarufu niliyokuwa naifahamu pale kahama iliyokuwa inapatikana mitaa ya Phantom. Huko nilifika na kuagiza bia kadhaa, kisha nikaanza kuzinywa taratibu. Sijui hata nilikuwa nawaza nini kufanya hivyo kwani hiyo ndiyo ilikuwa mara yangu ya kwanza nakunywa bia.
Mwanzoni nilikuwa na lengo la kunywa bia chache tu lakini kadri muda ulivyozidi kwenda mbele nilijikuta nazidi kuagiza bia tena na tena hadi zikanizidia na kupelekea nizimie pale pale kwenye meza niliyokuwa nimekaa.
Kesho yake asubuhi niliamka na kujikuta ndani ya chumba ambacho sikukielewa na nilikuwa nimelala nikiwa mtupu. Sikujua nimefika vipi mule ndani, na wakati naendelea kuangaza ndani ya kile chumba mlango wa kile chumba ulifunguliwa na akaingia binti wa makamo kwa umri nilimkadiria kwenye miaka 20 hadi 23 hivi.
Yule binti alitabasamu baada ya kuniona,
“Naona umeamka sasa” Yule binti alinisemesha
“Ndio,…… Vipi nimefikaje hapa” Nilimuuliza yule binti huku nikiwa nalivuta shuka nililokuwa nalo nijifunike vizuri ili kuzuia yule binti asiendelee kuuona utupu wangu.
“Hapa ni kwangu jisikie Amani kabisa, jana nilikusaidia pale bar baada ya kuona umezima na nilifanya hivyo kuepusha watu wabaya wasije kukufanyia mambo mabaya” Alinieleza
“Annh sawa asante,…….. Sasa vipi kuhusu nguo zangu” Nilimuuliza
“Zipo nje nimezianika baada ya kuzifua, ulizichafua sana (akatabasamu) Inamaana unataka kusema haukumbuki chochote kile kilichotokea jana?!!” Aliniuliza, nikamkubalia kwa kutikisa kichwa, akacheka sana,
“Basi kama ni kweli unavyosema haukumbuki chochote kile itabidi uachane na pombe kabisa” Yule binti alinieleza, nikawa sina cha kumjibu zaidi ya kubaki nikijionea aibu kwani nilikuwa nimeshahisi tu kuwa usiku wa jana naweza kuwa nilifanya vitu vya aibu sana ambavyo sikutaka kuvijua.
“Ngoja kwanza nikuletee supu unywe ukate hizo pombe zako” Yule binti alinieleza, akaanza kutoka kuelekea nje lakini nilimzuia kwanza nikamuuliza,
“Samahani dada, unaitwa nani kwani?”
“Naitwa Koleta” Alinijibu kisha akatoka nje.
Koleta alinitengea supu nzito ya mbuzi, na aliweka chapati moja tu lakini nyama zilikuwa ni za kutosha na mchuzi kama wote uliokuwa umechanganyiwa ndizi kadhaa. Koleta alinisihi nisibakishe hata kidogo supu ile kwani ndio itakayoupatia mwili wangu nguvu tena za kufanya majukumu mengine. Niliinywa ile supu na kuimaliza yote, kisha nikaingia bafuni kuoga, nilipotoka Koleta alinipatia nguo zangu nivae kwani zilikuwa zimeshakauka, nikazivaa.
“Koleta, naomba niondoke sasa mie niwahi nyumbani” Nilimuaga
“Jamani mbona mapema sana si ungebakia hadi jioni ukanipatia kampani”
“Unajua nini Koleta, natamani sana kubaki lakini nyumbani najua wazazi wangu watakuwa na wasiwasi sana kuhusu mimi kwani hawajui nilipo hadi sasa naomba niende tu naamini mimi na wewe tutaendelea kuwasiliana” Nilimweleza Koleta ambae alinielewa, tukabadilishana mawasiliano kwa ajili ya kuwa tunawasiliana kisha nikaondoka zangu.
Huo ndio ukawa mwanzo wa ukaribu wangu mimi na Koleta. Muda mwingi nilijikuta nautumia kuwasiliana na Koleta, kama si kwa kuongea kwenye simu ama kuchati basi tulikuwa tunakutana kabisa na kuzungumza.
Koleta alikuwa ni binti mcheshi sana asiyeishiwa stori. Muda wote alikuwa ni mtu wa utani sana. Pamoja na yote hayo kitu nilichokipenda zaidi kutoka kwake ni upambanaji wake, katika umri wake huo wa miaka ishirini na tatu tayari alikuwa ameshaweza kujitegemea. Biashara yake ya kuuza mchele ilikuwa inampatia pesa za kujikimu kwa kila kitu alichokihitaji. Mipango aliyokuwa nayo juu ya maisha yake ilikuwa ni mipango mikubwa sana iliyonifanya mara nyingi nijione kama si kitu mbele yake kila tulipokuwa tunazungumzia habari za kimaendeleo.
“Haina haja ya kujiona umechelewa sana Gift ndio kwanza una miaka kumi na saba haraka ya maisha ya nini sasa?” Koleta alikuwa anapenda sana kunieleza maneno hayo kila mara kunikumbusha kuwa nisiwe na haraka na maisha kila kitu kitakuja kwa wakati wake.
Nikiri jambo moja hapa, Koleta ndiye aliyenifanya nijisemee moyoni ya kuwa nitakapomaliza kidato cha nne sitaendelea na masomo yangu bali nitajichanganya na maisha mtaani kujitafuta. Pia kwa kipindi chote kile nilichokuwa na Koleta, mawazo juu ya Amina yalipungua sana kwani sikuwa mtu niliyemuwaza sana tena Amina kama ilivyokuwa mwanzo.
Siku zilisonga mbele, muda wa kurudi shule ukawadia hivyo ikanibidi niende nikamuage Koleta,
“Jamani Gift kwahiyo shule unakwenda lini?” Aliniuliza
“Kesho asubuhi naamkia stendi kwa ajili ya safari” Nilimweleza Koleta ambae alionekana kuhuzunika sana, nikamueleza sitachukua muda sana huko kwani ni muda wa wiki mbili tu nitakuwa nimesharudi tena Kahama.
Tulipiga sana stori siku ile, usiku ulipofika nikamuaga Koleta ya kuwa nirudi nyumbani ili nikapumzike mapema.
“Sawa Gift haina shida ila nilikuwa naombi moja kwako kabla haujaondoka” Koleta alinieleza
“Niambie chochote kile nakusikiliza”
“Naomba basi hata nikukumbatie kabla haujaondoka” Koleta aliniomba, sikuwa na sababu ya kumkatalia, nikamkubalia.
Koleta alinisogelea na kunikumbatia, alinikumbatia kwa muda, nikawa najaribu kumtoa baada ya muda kuwa umepita lakini Koleta alikuwa amening’ang’ania, hivyo ikabidi nimtazame vizuri ili kumuomba aniachie lakini nilishindwa kufanya hivyo kwani nilishangaa kuona macho ya Koleta yakiwa yamebadilika rangi na kuwa mekundu na yalikuwa yanatokwa na machozi.
“Koleta shida nini?!!” Nilimuuliza, lakini hakunijibu, zaidi aliendelea kunikumbatia tu huku akiendelea kulia hivyo ikabidi nianze kumbembeleza kwa kumfuta machozi machoni mwake huku tukitazamana.
Wakati naendelea kumfuta machozi Koleta aliacha Kulia, tukabaki tunatazamana kwa muda, Koleta hakutana kunieleza hisia zake kwa maneno tena kwani aliamini wakati mwingine vitendo vina nguvu zaidi ya maneno hivyo alinyanyua miguu yake ili kujiruhusu kunyanyuka na kunisogelea pale nilipokuwa kisha akanichumu mdomoni mwangu. Alipomaliza alirudi nyuma kama mtu aliyekuwa anajutia hivi kitendo alichokuwa amekifanya, mie sikutaka hilo litokee hivyo nilimvutia kwangu Koleta kisha nikamshikilia vizuri ili kuirahisisha kazi yangu ya kubadilishana nae juisi za midomo yetu.
Kilichofuatia baada ya hapo sote kwa pamoja mimi na Koleta tulijikuta tukiwa kitandani tukiivunja amri ya sita ile iliyoandikwa na nabii Mussa kama alivyoagizwa na Mungu ya kuwa tusiivunje amri hiyo kamwe kabla ya ndoa.
Sehemu ya Sita
Naikumbuka vizuri sana ile mechi yangu ya kwanza kucheza na Koleta, mechi ambayo ilihitaji vipindi vitatu vyenye heka heka za kutosha, nakiri kusema Koleta alikuwa amenipania sana siku ile kwani hakuniachia hata sekunde moja ya kupumzika, muda wote alitaka nimpelekee mashambulizi kwa kumpigia pasi ndefu tu tena za haraka haraka, hakutaka kabisa mambo ya pasi fupi fupi kwani alidai zinaupozesha mchezo na kufanya mechi iboe. Kiukweli naweza sema kwenye mechi zangu bora kuwahi kucheza siwezi itoa mechi ile mimi na Koleta tulipocheza kwa mara ya kwanza.
“Baby naomba usiende kunisaliti basi huko shuleni kwenu” Koleta alinieleza baada ya mechi yetu kuisha. Sikutaka kumjibu chochote kile kwani nilihofia kumpatia ahadi ambayo nilijua fika nisingeweza kuilinda.
Kesho yake asubuhi sana niliamka na kuanza safari ya kurudi shule. Nakumbuka nilifika shule mida ya saa nane mchana, nikapokelewa vizuri na mwalimu aliyenieleza niende darasani kwani wanafunzi wenzangu walikuwa bado hawajamaliza masomo yao ya siku ile, nikamtii na nikaianza safari yangu ya kuelekea darasani.
Nilifika darasani kwetu na kubisha hodi, mwalimu aliyekuwamo darasani alinipokea na kunitaka niende nikakae kwenye siti yangu. Nilielekea hadi kwenye siti yangu na kumkuta Elias akiwa amekaa pale, nilifika na kumtazama, sikutaka kumsemesha chochote kile. Elias alielewa nilichokuwa nakihitaji hivyo alinyanyuka na kunipisha kwenye kiti changu, nikakaa.
Nilimtazama Amina aliyekuwa pembeni yangu kama sijamuona kwani sikumsalimia, na hadi kipindi kinaisha hatukuwa tumezungumza chochote kile mimi na Amina ambae aliamua kuondoka tu mara baada ya kipindi kile kuisha. Nikamuona Elias anamkimbilia Amina, kisha akamshika mkono na wakaamua kuondoka pamoja. Kitendo kile kwa kiasi fulani kikanitia wivu kiasi moyoni mwangu japo nilijitahidi kuupotezea wivu ule.
Maisha yangu shuleni tangu nimerudi hayakuwa sawa tena kama mwanzoni kwani watu wawili wa muhimu sana, Amina na Elias wote kwa pamoja nilikuwa sisemezani nao. Amina aliamua kukata mawasiliano na mimi kabisa kwani aliamua kubadili hata siti ya darasani aliyokuwa anakaa mwanzoni ilimradi tu awe mbali na mimi.
Elias pia hakutaka mazoea na mimi, kwani alianza kwa kuhama bweni tulilokuwa tunaishi pamoja na kuhamia bweni jingine, kisha akamshawishi Amina atoke pale alipokuwa anaketi na mimi darasani na badala yake ahamie kwake na kweli Amina alifanya hivyo kama nilivyosema hapo mwanzo.
Suala la mimi kutozungumza nao halikuniumiza hata kidogo, ila kilichokuwa kinanitesa nafsi yangu ni ule ukaribu waliokuwa nao, ni kama nilikuwa najitazama mimi kwa Elias nilivyokuwa na Amina kabla hatujaachana, yaani Elias alijua fika kuuvaa uhalisia wangu kwa Amina kwani alikuwa anafanya vile vile nilivyokuwa nafanya mimi na Amina kipindi tupo pamoja. Kiukweli hali ile ilikuwa inanitesa sana kiasi cha kufanya nishindwe kuielekeza akili yangu kwenye masomo kwani muda wote nilikuwa najikuta namuwaza tu Amina bila kutaka.
Mitihani iliwadia tukafanya, sijui wenzangu waliifanyaje lakini kwa upande wangu mitihani ile niliifanya kutimiza wajibu tu, kwani mambo mengi nilikuwa sijasoma na hata nilipotaka kusoma akili yangu ilishindwa kwa sababu ya mawazo juu ya Amina wangu kuwa na Elias.
Tulimaliza kufanya mitihani yetu ya kidato cha nne, tukaruhusiwa kurudi nyumbani, ilikuwa ni shangwe sana kwa watu wengi ikiwemo na mimi ambae nilifurahia kwa mambo makuu mawili. Moja, kumaliza kidato cha nne kwa upande wangu haikuwa rahisi kwa sababu ya heka heka nyingi nilizozipitia lakini Mungu alisimama na kuniwezesha nimalize. Mbili, nadhani hii sababu ya pili ndiyo iliyonipatia furaha zaidi kwani Amina na mimi tulikuwa tunarudi nyumbani Kahama na Elias alikuwa anakwenda kwao Kagera, yaani kwa maana hiyo ni kama kusema Amina na Elias walikuwa wanaachana bila kuambiana kuwa wameachana.
Mimi na Amina tulirudi nyumbani, tukafikia kwetu ambapo ndipo baba yangu na mama yake Amina walipoelewana kuwa tutakuwa tunaishi hapo. Tofauti na mimi niliyeonekana kuwa na furaha ya kurudi nyumbani, Amina yeye alionekana kuwa ni mtu wa mawazo sana na alipenda kujitenga peke yake muda wote. Amina hakuwa tena mtu aliyependa kuongea na hakuwa mtu wa kucheka ama kufurahia hata kama litokee jambo gani la kufurahusha, yeye hakufurahia.
Hali ile kwa namna fulani ilikuwa inanitesa hata mimi ambae nilikuwa namshuhudia mara nyingi. Baba na mama wao muda mwingi walikuwa wanautumia makazini kwao, Lakini sikutaka kumuuliza kwani ni kama nilikuwa nimeshajipatia majibu yangu tayari.
Kwanza nilihisi Amina anaweza kuwa na mawazo juu ya ujauzito alionao ya kuwa ataanza vipi kuwaeleza wazazi wetu. Pia niliwaza huenda Amina akawa ana mawazo juu ya mpenzi wake Elias ambae yupo mbali nae kwa muda ule, hivyo niliamua kumuacha adili na mambo yake mwenyewe hadi pale atakapotaka kunieleza yeye mwenyewe changamoto inayomkabili tushauriane.
Mie nilianza kuwa bize na biashara ya mchele ambayo nilikuwa nafundishwa kuifanya kwa ukaribu sana na Koleta ambae aliniahidi kunielekeza biashara hiyo jinsi inavyofanywa. Koleta alinielekeza kila hatua aliyoifahamu, kwani alihitaji niifahamu vyema biashara ile ambayo nilionesha nia ya kutaka kuijua.
“Mume wangu, una kichwa cha kuelewa sana mambo haraka” Koleta alinieleza, nikabaki namtazama tu bila kuongea chochote kile. Ni kama sikuwa nataka Koleta aniite vile lakini nilikuwa nashindwa kumueleza ukweli kwani alionekana kunipenda sana. Kwa upande wangu Koleta nilimuona kama mshkaji wangu tu hata ile kulala nae kwangu niliona kama bahati mbaya na sikutaka kurudia tena kufanya nae jambo hilo.
“Giih, leo naomba twende ukalale kwangu basi nimekumisi sana mpenzi wangu” Koleta aliniomba
“Mmmmh!!! Sidhani kama leo itawezekana Koleta” Nilimjibu
“Kwanini sasa isiwezekane, au ushapata mwanamke mwingine huko nje”
“Hapana sio hivyo, ni kwamba nyumbani leo nipo mwenyewe, wazazi wangu ameenda safari itabidi niilinde nyumba haiwezi kubaki peke yake” Ilibidi nimdanganye Koleta kwani sikutaka kwenda nae kwake, kwa kuhofia kitakachokwenda kutokea huko baada ya kwenda.
Kishingo upande Koleta alinikubalia, tukaagana nikarudi nyumbani. Kufika nyumbani nilipitiliza chumbani kwangu nikaoga na kubadili nguo kabla ya kurudi sebuleni kwa ajili ya kula chakula cha usiku.
Nilivyofika sebuleni sikukuta chakula mezani, ikabidi nielekee jikoni kutazama huko nako sikukuta chakula wala dalili za chakula kuwa kilipikwa mahali pale. Nikawaza kwanini Amina hajapika na wakati hiyo haikuwa kawaida yake kabisa, ni kweli hatukuwa na stori sana lakini Amina hakuwahi hata mara moja kuacha kunipikia hivyo nikawaza niende chumbani kwake nikamtazame kujua ni nini kinachomsibu hadi ashindwe kunipikia chakula.
“We Amina” Nilibisha hodi huku nikiwa naliita jina la Amina ambae hakuwa akiniitikia lakini sikuacha kwani nilihisi huenda yakawa ni mapozi yake tu ya kutokutaka kuzungumza na mimi.
Nilijikuta nabisha hodi kwa zaidi ya dakika tano bila majibu hivyo nikaamua najaribu kuufungua mlango kuona kama upo wazi, mlango ukafunguka nilipoujaribu kuufungua, hivyo nikausukuma na kuingia ndani ya chumba cha Amina.
Sikutaka kuamini nilichokishuhudia mule ndani, Amina alikuwa amelala chini sakafuni na alikuwa anatokwa na mapovu mengi mdomoni mwake.
“Oooh Mungu wangu!!!” Nilijikuta najisemea kwa nguvu kisha nikamfuata Amina pale alipokuwa amejilaza.
Sikutaka kupoteza hata sekunde moja tena, akili yangu ilikuwa inawaza kumsaidia Amina ambae nilijua fika alikuwa na shida. Nilimbeba mikononi mwangu na kuanza kutoka nae nje ambako nilifika na kuita boda haraka ambae Nilimweleza atupeleke kituo cha afya kilichokuwa karibu na pale tulipokuwa tunaishi.
Tulifika kwenye Dispensary moja ya karibu na nyumbani ambapo tulipokelewa haraka,
“Ana shida gani huyu?” daktari aliniuliza kabla ya kuanza huduma, nikamweleza
“Nadhani amekunywa hivi vidonge( huku nikimuonesha yule daktari vile vidonge nilivyokuwa navyo) kwani nimevikuta chumbani kwake pale chini alipokuwa amelala”
“Ok sawa, tusubiri hapo tukamsaidie ndugu yako” Yule daktari alinieleza, ikabidi nielekee kwenye benchi lililokuwa pale Dispensary kisha nikaketi.
Siti haikukalika hata kidogo kwani muda wote nilikuwa na mawazo juu ya uhai wa Amina ambae nilikuwa nahisi huenda alikuwa anataka kujiua. Nikiwa ni mwingi wa mawazo bado ndipo nikakumbuka kuwa kulikuwa na kikaratasi nilichokichukua kutoka kwenye mikono ya Amina wakati namchukua chumbani kwake hivyo nikakitoa na kukifunua kwa lengo la kukisoma.
“Najua unaweza kunichukua kwa haya nitakayokueleza lakini huu ndio uhalisia wenyewe. Mimi bado ni kijana mdogo sana kuwa baba, na nina ndoto nyingi za kutimiza ambazo naona ninaweza shindwa kuzitimiza kwa kujifanya baba bora kwa kiumbe nisichokihitaji kwa sasa. Ni hivi Amina, hutonisikia nikikutafuta tena katika maisha yako kwahiyo fanya namna utoe hiyo mimba, na uendelee na maisha yako kama kawaida kuliko kung’ang’ania uhalisia wa mambo usiokuwepo.
Kuwa na maisha mema”
Nilimaliza kusoma barua ile iliyonitia hasira kwani nilijua fika ni barua iliyokuwa imetoka kwa Elias.
“Kijana naomba tuzungumze mara moja” Daktari alinisemesha na kunitoa kwenye wimbi zito la mawazo niliyokuwa nayo,
“Ndio hakuna shida” Nilimjibu na kusimama toka pale nilipokuwa nimekaa tukasogea pembeni kwa ajili ya kuzungumza.
“Sasa kijana huyu ndugu yako inavyoonekana amekunywa dawa nyingi kupitiliza, nadhani alikuwa anataka kujitoa uhai wake lakini kwa kuwa umemuwahisha tumeshamsaidia na hivi navyoongea na wewe hapa nina mpango wa kutoa taarifa polisi kuhusu tukio hili” Daktari alinieleza taarifa ambayo sikuishangaa kwani nilikuwa nimeshahisi kile alichokuwa anataka kukitenda Amina lakini suala la kuripoti taarifa zile polisi ndilo ambalo nilionekana kutokuafikiana nalo.
“Aaanh daktari usitufanyie hivyo, naelewa unafuata protokoo lakini jaribu kumuelewa ndugu yangu ni mengi anapitia kwa sasa naomba tusifike huko tafadhari”
“Kwahiyo kama anapitia mengi ndio ajitoe uhai wake? Hivi unajua ni watu wangapi tunaowapokea hapa kwa siku ambao wanaletwa wakiwa mahututi na msaada wao pekee unakuwa ni kwa Mungu wao lakini huyu anataka kujiua kweli?” Daktari alionekana kuchukizwa sana na kitendo cha Amina kutaka kuijua.
Ilinichukua zaidi ya nusu saa kumshawishi daktari asimripoti Amina polisi. Ndipo daktari akanielewa na kunieleza kama itatokea tena Amina amejaribu kujiua nisifikirie hata kidogo kumrudisha kwenye Dispensary yake, nikamkubalia na kumshukuru sana kwa kunielewa.
Amina aliruhusiwa kutoka pale Dispensary kesho yake mchana, tukarudi nyumbani. Amina alikuwa kimya sana kwani alionekana kutokutaka kuzungumza na mimi chochote kile, lakini mimi nisingeweza kulikalia kimya suala lile kwani lilihusisha uhai wake hivyo nilisubiria hadi tufike nyumbani ndio nizungumze nae.
Tulivyofika nyumbani, nilianza kwa kuingia jikoni na kumpikia chakula laini Amina, ndizi na samaki pamoja na juisi ya parachichi kisha nikampatia ale. Amina alikula kidogo sana akaniomba aende kupumzika kwanza. Nikamueleza kabla ya kwenda kupumzika nahitaji kuzungumza nae,
“Tutazungumza tu Gift naomba niende kulala kwanza” Amina alinieleza huku akiwa ananyanyuka toka kwenye kiti alicho kuwa amekikalia
“Nimeisoma barua aliyokutumia Elias” Nilimweleza Amina ambae alibaki amesimama akinitizama kisha nikaendelea kuongea
“”Inamaana Amina suluhisho la mambo yote haya uliona ni kujitoa uhai wako sio?”
“Naomba usiongee usichokijua Gift tafadhari”
“Nisiongee nisichokijua? Kipi hicho? Wewe kuachwa na Elias au kuhusu hiyo mimba uliyonayo? Nieleze” Amina alionekana kama kutokuwa tayari kunijibu kwani alinitazama kwa muda kisha akataka kuanza kuondoka lakini nilimzuia kwa kumshika mkono wake
“Nieleze Amina nisichokijua nini hapa?”
“Niachie Gift”
“Siwezi kukuachia hadi unieleze, kumbuka umetaka kujiua wewe” Nilimweleza Amina ambaye alibwatuka kwa hasira
“Kwahiyo kama nilitaka kujiua wewe inakuhusu nini? Maisha si ni yangu……” Hakumalizia kuongea alichokuwa anataka kukiongea kwani tayari nilikuwa nimeshampiga kofi kali la shavuni kwake lililompeleka chini, kisha nikamfuata pale chini na kumueleza
“Usinifanye mie kama mjinga Amina, kuhangaika kote kule kukuokoa maisha yako alafu unaniambia nini? Nikuache kisa maisha ni yako? Hivi ulifikiria kweli hata watu utakaotuacha utatuacha na hali gani kweli, hebu acha kuwa mbinafsi wa uhai kwa kisingizio cha kusema maisha ni yako tusikuingilie” Niliongea kwa hasira sana.
Amina kusikia maneno yale alianza kulia, alilia sana kiasi cha kushindwa kuongea. Nilichokifanya mimi ni kumtazama alie kwanza ili aondoe machungu aliyokuwa nayo moyoni mwake.
“Sidhani kama Elias aliwahi kunipenda” Amina alianza kuongea maneno hayo baada ya kuwa ameacha kulia.
“Moyoni mwangu ni kama nilikuwa nalijua hilo lakini nilijikaza ili nisionekane kama nimekosea kuchagua mwanaume baada ya kuachana na wewe” Amina aliongeza
“Kwanini unasema hivyo” Nilimuuliza
“Elias alikuwa ni mpenda sifa sana mbele ya macho ya watu, Alionesha kunijari sana tukiwa mbele ya watu lakini alikuwa ni mtu Tofauti kabisa pindi tulipokuwa tukibaki peke yetu, hakuonesha kunijari kabisa”
“Sasa kama ni hivyo mbona hata wewe ulionekana kuwa na furaha kuwa nae”
“Sikutaka watu wajue kama mimi na Elias hatupo sawa hasa ukizingatia jinsi mahusiano yangu mimi na wewe yalivyokuwa hapo mwanzo kabla ya Elias”
“Aya sawa nimekuelewa, kwanini ulitaka kujiua sasa?” Nilimuuliza.
“Unajua Elias alinieleza kuwa atanihudumia kwa kila kitu na alinishawishi sana nisiitoe mimba hii, sasa sasahivi imeshakuwa kubwa na haiwezi kutoka ndio ananieleza maneno hayo kweli, Aya naanzaje kulea mtoto asiye kuwa na baba mimi?” Amina aliniuliza, nikamtazama kisha nikamueleza
“Amina ni watoto wangapi wamelelewa bila baba zao? Au mama zao? Kwani hao sio binadamu au kuna kipi kilibadilika kwenye maisha yao baada ya kulelewa na mzazi mmoja, hebu fungua moyo kisha mkubali huyo mtoto mbona kila kitu kitakuwa sawa tu”
“Sio rahisi kama unavyosema Gift, siwezi mie” Amina alinieleza
“Inawezekana sana kama utakubaliana na uhalisia wenyewe Amina”
Nilijitahidi sana kumshawishi Amina ambae alinielewa, tukakubaliana wazazi wetu watakaporudi jambo la kwanza kuwaeleza ni juu ya ujauzito ule aliokuwa nao Amina.
Kweli baba na mama walivyorudi kutoka kazini, tuliwafuata na kuwaeleza hali halisi kuwa Amina ni mjamzito. Baba yangu hakuongea chochote, ni kama alipigwa na butwaa, sijui ni kwanini lakini nilihisi labda hakuongea chochote kwa sababu ya mama Amina ambae alihuzunishwa sana na taarifa zile zilizomfanya alie sana.
“Lakini nyie watoto mnatutaka nini kwani? juzi kati kaka yako alitueleza habari za kutokutaka kuendelea kusoma ya kuwa anajiingiza kwenye biashara, alafu leo hii na wewe unatuletea habari za mimba kweli?” Mama Amina aliongea kwa uchungu sana.
“Aya tueleze baba wa mtoto ni nani? Unamfahamu?” Baba yangu alimuuliza Amina ambae hakutaka kumtaja kabisa Elias. Kitendo kile kikatafsiriwa na mama yake kama ni kumlinda aliyemuharibu,
“Amina toka nyumbani kwangu” Mama Amina aliongea kwa ukali.
“Lakini mama……”
“Lakini nini, toka kwangu hadi uniletee huyo mpuuzi wako aliyekuharibu” Mama Amina aliongeza na alionekana kumaanisha alichokiongea.
Licha ya kumshawishi sana asimfukuze Amina nyumbani, mama Amina alikuwa amedhamiria kweli kutenda tukio hilo ambalo alilifanikisha, Amina akafukuzwa nyumbani usiku ule wa saa tano huku akilia sana.
Mie sikutaka kumuacha ateseke peke yake huko nje hivyo nilimfuata.
“Unataka nini Gift, umeona sasa ushauri wako ulichoniletea?” Amina alionekana kunilaumu sana kwa ushauri wangu.
“Sidhani kama huu ni muda wa kulaumiana bali tukae tutulie tujue ni kipi tunachopaswa kufanya kwa sasa” Nilimweleza Amina ambae alionekana kuwa ameshajikatia tamaa asijue nini cha kufanya.
“Itabidi nikutafutie kwanza sehemu ya wewe kwenda kulala” Nilimueleza Amina kisha nikamuomba tuondoke pamoja kwenda mahala fulani.
Amina alinifuata, tukapanda boda iliyotupeleka sehemu niliyomwelekeza yule mtu wa boda. Tulifika sehemu husika tukashuka kwenye boda kisha tukaelekea kwenye moja ya nyumba ambayo nilifika na kugonga mlango ambao haukupita muda sana ule mlango ukafunguliwa.
“Oooh!!! Giih!!! What a surprise karibu!!” Koleta alinipokea kwa furaha
“Asante K ila nimekuja na mgeni tunahitaji msaada wako” Nilimueleza Koleta huku nikimtizama Amina ambae alikuwa kimya muda wote.
Koleta alimtazama Amina kisha akatabasamu,
“Chochote kile kwa ajili yako Giih ntafanya niambie tu” Koleta alinieleza
“Huyu ni Amina, naomba umuhifadhi hapa kafukuzwa nyumbani” Nilimueleza Koleta ambae hakutaka kutuuliza swali jingine zaidi ya kutukaribisha ndani, tukaingia.
Sikutaka kukaa sana kwani nilihitaji kurudi nyumbani, hivyo niliwaaga, Koleta akaniomba anisindikize kidogo nikamkubalia tukatoka nje pamoja na kumuacha Amina akiwa amekaa kitandani kwa unyonge sana.
“Bila kukukosea Gift naomba nikuulize jambo, Huyo binti uliyemleta ni mtu wako au?” Koleta aliniuliza baada ya kuwa tumetoka nje
“Ha…hapana Koleta sio hivyo ni dada yangu huyo japo sio wa tumbo moja”
“Dada yako? Aya amefukuzwa kwao kisa nini?”
“Ana ujauzito hapo alipo na nyumbani wamemueleza asirudi bila muhusika wa hiyo mimba”
“Aanh kumbe, duh!! Pole yake sana”
“Ndio hivyo Koleta usiwe na wasiwasi kabisa juu yake n I dada yangu tu”
“Basi sawa nimekuelewa……. ila kwakuwa umeleta suala la mimba nadhani huu ni muda muafaka wa kukueleza jambo langu pia” Koleta alinieleza
“Jambo gani tena” Nilimuuliza
“Gift hapa nilipo nina mimba yako”
“Unasema? Una nini Koleta?”
“Nina mimba yako Giih usichokielewa nini hapa”
“Lakini si Tumefanya mara moja tu?!!” Nilimuuliza Koleta kwa mshangao, nae pia akaniuliza
“Kwani hiyo mara moja haiwezi tia Mimba?”
Sehemu ya Saba
Kauli ile ya Koleta ilinifanya niweweseke kidogo kumjibu,
“Ankha!!! Ha… Ha…. Hata kama Koleta ndio mara moja kweli? Ukapata na mimba?”
“Habari ndio hiyo Giih wewe jiandae tu kuwa baba kwani sina mpango wa kuitoa mimba hii” Koleta alinieleza. Hapo ndio nikajua kuwa Koleta hakuwa ananishirikisha habari ile bali alikuwa ananipatia taarifa juu ya ujauzito aliokuwa nao.
Sijui hata kilitokea nini ila nilijikuta nakosa nguvu kabisa ya kubishana na Koleta kwani nilimkubalia kila kitu alichonieleza usiku ule, tukaagana, nikarudi zangu nyumbani.
Usiku ule ulikuwa mrefu sana kwangu, mawazo juu ya ujauzito aliokuwa nao Koleta ulinichanganya sana akili yangu. Niliwaza maisha yangu yatakuwaje baada ya hapo kwani muda sio mrefu nakwenda kuwa baba. Hofu moyoni mwangu ilinitawala kwani niliwaza kama nitaweza kweli kuwa baba bora kwa mwanangu bila kupata majibu hivyo nikabaki nikiuachia muda majibu ya maswali yangu hayo.
Sijui hata ni saa ngapi usingizi ulinipitia kwani nilipokuja kufumbua macho tayari asubuhi ilikuwa imeshafika. Hivyo niliamka na kujiandaa kwenda kwa Koleta. Sikutaka hata kunywa chai nyumbani.
Nilifika kwa Koleta na kuwakuta Koleta na Amina wakiwa wamekaa nje wakifua nguo. Walionekana kuwa na furaha sana kwani walikuwa wanaongea huku wakicheka sana. Nilijikuta napata amani moyoni mwangu isiyoelezeka. Nadhani ni kwa sababu sikutegemea kuwakuta wakiwa katika hali ile, hivyo nikajumuika nao kupiga stori pamoja.
“Nimempenda sana wifi yangu ni mchangamfu sana” Koleta alinieleza baada ya Amina kuwa ametuacha na kuingia ndani kupumzika.
“Kweli nyie watoto wa kike siwawezi yaani mara hii tu mmeshazoeana kama mnafahamiana miaka mingi”
“Sasa wewe ulitakaje? Utukute hapa tukiwa tumenuniana au” Koleta aliniuliza, tukajikuta wote tumeanza kucheka pamoja.
“Koleta lakini nina jambo nahitaji tuzungumze peke yetu”
“Niambie tu Gift nadhani hapa tupo wenyewe”
“Sawa ni kweli…… (nikavuta pumzi na kuishusha kwa nguvu) Unajua nini Koleta naogopa sana mwenzako” Nilimweleza
“Oooh Gift unaogopa nini tena”
“Namzungumzia huyo mwanangu, sijui kama nitaweza kumlea ipasavyo maana najiona kama mimi bado ni mdogo sana”
Koleta kusikia vile alinitazama, kisha akaniomba nimtazame, nikamtazama
“Unajua nini mume wangu, haina haja ya kuogopa mambo ambayo hayajatokea bado kikubwa tu hapa ni kujiandaa vyema na mambo ya mbele sawa?” Koleta alinieleza, nikamkubalia.
Tulijikuta tunaongea mambo mengi sana pale. Bila kutegemea nikajikuta naanza kupanga mambo mengi sana ya kimaisha na Koleta ambayo sikuwa nimewaza kuyaongea mbele yake hata siku moja.
Siku zikazidi songa, mama Amina akaendelea kushikilia msimamo wake wa kutokutaka kumuona Amina hadi pale atakapompeleka mtu aliyempatia mimba.
Mimi na Koleta tukawa wapenzi rasmi, sikuwa na sababu ya kuendelea kumpotezea Koleta kwani alionekana kunijari na kusapoti kila kitu nilichokuwa nafanya hivyo nikawa namuhudumia kila kitu kama mke wangu.
Kazi yetu ya kuuza mchele tukawa tunaifanya kwa ushirikiano mkubwa sana, Koleta akanishauri tumfundishe na Amina biashara ile ya kuuza mchele, tukafanya hivyo. Amina alionekana kuifurahia sana biashara ile ambayo aliifanya kwa moyo wake wote.
Kwa kuwa Koleta na Amina walikuwa wanaishi pamoja, mimi sikutaka kuharakisha kuondoka nyumbani na badala yake niliendelea kuishi kwa wazazi wangu, na kila mara nilipokuwa namuhitaji Koleta kimapenzi tulikuwa tunafanya namna ya kukutana bila kubughuzi uhuru wa mtu hasa Amina ambae alikuwa anaishi na Koleta.
Miezi ikasogea, Amina akawa ni mtu wa kwanza kujifungua na alijifungua mtoto wa kike ambae alimuita Koleta kwa sababu ya heshima kubwa aliyokuwa nayo kwa mtu huyo.
“Nakuheshimu sana kama dada yangu wa damu Koleta ndio maana mwanangu nitampatia Jina lako” Amina aliongea maneno yaliyomfanya Koleta alie kwa furaha.
“Kiukweli sikutegemea kama nitakuja kupata mtu wa kuniheshimisha kama wewe Amina” Koleta aliongea akimweleza Amina ambae naye alikuwa analia muda huo.
Koleta naye akafuatia kujifungua, naye pia akajifungua mtoto wa kike na aliamua kumuita jina la rafiki yake Amina kwa sababu ya heshima aliyokuwa nayo kwa rafiki yake huyo.
Kwa ufupi tu, Amina na Koleta walipendana sana na walichukuliana kama ndugu na sio marafiki tena kama ilivyokuwa huko mwanzo.
MIAKA MIWILI BAADAE.
“Unajua kuna kitu huwa nataka kukwambia ila nashindwa” Koleta alinieleza
“Kitu gani hicho tena mke wangu unanitisha”
“Hata usiogope ni jambo la kawaida tu”
“Hata siogopi, niambie sasa nakusikiliza”
“Ni kuhusu wewe na Amina, hivi unajua naifahamu historia yenu vizuri sana”
“Historia gani tena mbona sikuelewi” Nilijifanya kama simuelewi Koleta anachokiongea.
“Usijifanye haunielewi huko, unadhani sijui kama Amina alishawahi kuwa mtu wako?:
“Mtu wangu? Nani kakuambia maneno hayo?”
“Wee unafikiri nani ataniambia kama sio Amina mwenyewe”
“Ila huyo binti hana kifua kabisa kumbe…”
“Muone huko, au ulifikiri ukiniambia ukweli nitamuonea wivu Amina?”
“Hapana sio hivyo, sema sikudhani kama ni wazo zuri tu, kwanza kwanini umenieleza maneno haya leo”
“Usichokielewa nini, nadhani Amina bado anakupenda ndio maana unaona hadi leo hajawahi kuwa na mwanaume mwingine tena baada ya wewe na Elias”
“Maneno yako tu hayo nadhani ameamua kuwa bize na malezi kwanza”
“Aya shauri yako sasa?” Koleta aliniambia
“Mbona sikuelewI mke wangu unanipigia pasi kwa Amina au?” Nilimuuliza swali ambalo lilimfanya Koleta anipige kibao cha mgongoni
“Mwone huko umalaya tu ndio uliokujaa” Tukaanza kutaniana hapa na pale mimi na Koleta.
Maneno ya Koleta kwa kiasi fulani yaliniingia. Nikawaza, kweli Amina hajawahi kuwa na mwanaume yeyote tangu aachane na Elias na sikuwahi elewa ssababu ya yeye kufanya hivyo ni nini. Nikaona ni bora niende kuzungumza nae juu ya suala hilo kujua kama lina ukweli wowote ule, kama ni kweli mimi ndio sababu ya yeye kutokuwa na mahusiano mengine tena.
“Kuna wakati natamani hata ungekosea kuoa Gift lakini ona, mkeo anavyokujali na kukupatia kila kitu unachokihitaji” Amina alinieleza.
“Kwanini unasema hivyo Amina”
“Umeniuliza kama ni kweli bado nakupenda, jibu ni ndio lakini siwezi kuwa na wewe kwa sababu ya Koleta rafiki yangu sipaswi kumlipa ubaya huu” Amina alinieleza
“Ubaya gani Amina, kwa ninavyoona hata mke wangu unatamani niwe na wewe kwani ndiye aliyenieleza taarifa za wewe kunipenda bado” Nilimweleza Amina
“Kweli wanaume wote ni mbwa, huyo Koleta aliyekuambia bado nakupenda je kuna kauli yoyote alikueleza kuwa uje kunishawishi niwe na wewe? Naomba unijibu” Amina aliniuliza swali ambalo sikuwa na jibu lake la moja kwa moja.
“Hata kama hajanieleza nije kukutongoza Amina, sasa kwanini amenieleza kuhusu upendo wako kwangu wakati anajua kabisa njnavyokupenda?”
“Unamkosea sana mkeo Gift, usimfanyie hivyo tafadhari l, au umesahau ya kwangu mimi na Elias tulivyokutenda wewe? Aya niambie tuliambulia nini zaidi ya kuachana vibaya, ona mwanangu Koleta ni matokeo ya usaliti wetu kwako, unafikiri napenda sana kumlea mwanangu peke yangu hali ya kuwa najua baba yake anaweza kuwa hai huko nje kusikojulikana?”
Amina alinieleza maneno makali yaliyokuwa yamejaa ukweli mchungu ndani yake. Nilijikuta nakosa cha kumjibu zaidi ya kubaki namtazama tu kama sanamu. Amina aliniacha na kuondoka zake.
Kiukweli nilijiona kama mjinga, niliwaza ni wapi nilitolea zile nguvu za kutaka kumsaliti mke wangu tena kwa rafiki yake wa karibu sana Amina. Sikupata majibu zaidi ya kupata wazo la kwenda bar moja nikanywe bia mbili tatu ili kukiweka kichwa changu sawa.
Nilifika bar na kuagiza bia kadhaa nikaanza kuzifyonza taratibu, wakati naendelea kunywa , simu yangu ilianza kuita, kutazama alikuwa ni mke wangu Koleta, nikampokelea
“Mume wangu uko wapi?” Koleta aliniuliza, sauti yake iliniambia kama kulikuwa na tatizo kwa jinsi nilivyoisikia
“Vipi kwani?”
“Nadhani inabidi uje nyumbani mara moja kuna tatizo”
“Tatizo gani tena?” nilimuuliza Koleta, lakini Koleta alinisisitizia niwahi kwenda nyumbani tu.
Ilibidi niahirishe kuendelea kunywa zile bia, nikalipa bill na kuondoka zangu haraka sana kwa kutumia usafiri wangu wa gari ambalo tayari nilikuwa nimeshalinunua.
Nilifika nyumbani na kumkuta Koleta akiwa ameketi sebuleni huku akiwa amejiinamia,
‘Mke wangu shida nini?” Nilimuuliza, Koleta akanitazama, macho yake yalikuwa mekundu sana ikimaanisha alikua analia, moyoni mwangu nikaingiwa na hofu lakini hata kabla sijaulize tena Koleta akaanza kunitupia lawama,
“Ndio umefanya nini sasa mume wangu eeeh!!! Umefanya nini mume wangu” Koleta aliongea kwa uchungu huku akiwa anajipiga piga kifuani kwake.
“Shida nini kwani mke wangu” Nilimuuliza, Koleta hakuweza kunijibu zaidi ya kunipatia karatasi aliyokuwa ameishika mfano wa barua ambayo niliipokea na kuanza kuisoma.
“Koleta ndugu yangu!!! Nipende kukushukuru sana kwa kuwa mtu wangu wa karibu sana kwani wewe ndiye uliyenifanya hata vipindi vigumu kwenye maisha yangu nivione si chochote.
“Maisha yangu ya giza yalipata nuru tena baada ya kukutana na wewe hivyo kamwe siwezi na sitaweza kuja kukulipa wema wako kwa kukutenda mabaya”
“Asante sana Koleta kwa kunionesha nini maana ya upendo. Najua fika unajua ni jinsi gani ninavyompenda Gift lakini licha ya yote hayo kwangu alipata maumivu tu, lakini kwako nachoona ni upendo wa dhati uliokithiri, nikiri kusema sijawahi kumuona Gift akiwa ni mtu wa furaha muda wote kama kipindi hiki alichokuwa na wewe, Asante sana kwa kulifanikisha hilo”
“Nisiongee sana Koleta, Nakuachia Gift wangu naomba umtunze, nadhani unajua fika kuwa mwanaume huyo kwangu hapindui (Leo amenieleza eti bado ananipenda hahahaha) ila nakuomba unilindie mwanangu ambae unajua fika ni damu ya nani hiyo japo hukuwahi niuliza”
“Muwe na Maisha mema, Wako Bff AMINA”
Niliisoma ile barua mara kadhaa bila kuielewa,.
“Inamaana unataka kusema Amina ameondoka?” Nilimuuliza Koleta
“Usichokielewa nini hapo, ndiyo Amina ameondoka na Sidhani kama atarudi tena, maskini rafiki yangu” Koleta alinieleza kwa uchungu sana
“Na vipi kuhusu mwanae, mbona na yeye kamuacha sasa?” Niliuliza tena, Koleta akasimama na kunisogelea nilipokuwa kisha akawa ananipiga piga kifuani
“Mjinga kweli wewe mwanaume, hivi hata macho ya kutazama huwa huna au? Huyo mtoto ni damu yako Gift” Koleta alinieleza maneno ambayo sikuyaelewa
“Damu yangu? Inamaana unataka kusema Koleta ni mwanangu?” Niliuliza
“Ndio Gift, ni wewe tu ndiye ambae haulijui hilo nadhani hata wazazi wako wanalifahamu hilo, we huoni mtoto anavyokufanana hivyo hadi pua”
Maneno yale ya Koleta yalinimaliza nguvu kabisa, nikawaza inawezekana vipi nisimtambue mwanangu kwa zaidi ya miaka miwili na kila siku namuona. Nilijikuta na mimi naungana na Koleta kuangua kilio cha uchungu. Nililia kwa mengi ila kubwa ni kwamba nililia kwa kuondokewa na Amina ambae haikujulikana ameelekea wapi lakini kama haitoshi aliamua kuondoka na kuniachia zawadi nyingine ya mtoto ambae nilijua fika kila nitakapo kuwa namtazama basi ni lazima ningemuwaza yeye Amina.
Hakika Amina alijua kuniweza, matendo yake yalionesha ni jinsi gani alivyokuwa ananipenda, hakukuwa na haja ya kusikia maneno yake tena. Kitendo kile cha kuamua kumlea Koleta peke yake bila kunieleza kama mimi ndiye baba yake mzazi kilinigusa sana kwani kwa kufanya hivyo huenda hata angeiyumbisha familia yangu mimi na Koleta kwani ni ukweli usiopingika, nilikuwa nampenda sana Amina kuliko kitu chochote kile lakini niliamua kuyaacha yote ya nyuma kwa ajili ya familia yangu.
Hivyo nilijikuta najiapiza kumlea na kumtunza mwanangu Koleta kwa kumpatia malezi bora ishara ya shukran za dhati kwa Amina mpenzi wangu ambae sikujua kama nitakuja kuonana nae tena.
MWISHO

