MPENZI WANGU AMINA
ONYO: Wakubwa tu, kuanzia Miaka 18, ndio wasome hii Hadithi
Sehemu ya Kwanza
Maisha ni kuchagua na mimi nilichagua kumpenda Amina katika maisha yangu yote bila kujali ni nini kitakachotokea katikati yetu.
Ngoja kwanza, kwa majina naitwa Gift Mathayo Lugwisha ni mtoto wa pekee nyumbani kwetu, baba huwa anadai hakutaka iwe hivyo lakini ndio ishakuwa hivyo, ndoto yake ilikuwa ni kuwa na watoto kumi na mbili yaani alipanga kumiliki timu nzima na kocha wake lakini haikuwa hivyo kwani mama alimsaliti baba, hivyo baba akaamua kumpatia talaka yake mama na akanichukua mimi kwenda kuishi nae. Sijawahi kumwona tena mama yangu hadi leo.
Baba naye hakutaka tena kujiingiza kwenye ndoa , hivyo alinilea peke yake kwa msaada mkubwa wa bibi yaani mama yake baba.
Kiukweli nilipatiwa malezi bora sana anayopaswa kupatiwa mtoto hadi nafikia umri wa kujitegemea sikumbuki kujihisi mpweke kabisa kila nilipokuwa nyumbani.
Naposema nyumbani namaanisha nyumbani tu, yaani nyumbani kwa baba na bibi yangu ila tofauti na hapo maisha yangu yamekua na upweke mkubwa sana na hiyo ni kwa sababu ya machaguzi yangu.
Kama nilivyosema mwanzo maisha ni kuchagua, na mimi niliamua kuchagua maisha ya upweke kwa sababu ya kumpenda mwanamke mmoja tu naye si mwingine bali ni Amina, Kivipi?
Mimi na Amina tulikutana mara ya kwanza mwaka 2014 wakati naingia kidato cha nne katika shule moja inayopatikana huko Mwadui Shinyanga ya kuitwa Mwadui Secondary School. Mimi nilikua muhamiaji katika shule ile vivyo hivyo kwa Amina naye alikuwa muhamiaji pale.
Kwa kuwa wote tulikua wahamiaji haikutuwia ugumu kufahamiana kwani nakumbuka mimi ndio nilitangulia kufika shuleni, na baada ya wiki moja Amina naye akafatia, Siwezi kuisahau siku ya kwanza namuona Amina, naikumbuka vizuri sana siku ile hadi hii leo, ilikuwa ni kwenye kipindi cha Mathematics, kipindi changu pendwa sana lakini cha ajabu siku hiyo nilikua najihisi usingizi balaa, hivyo sikuwa namsikiliza kabisa mwalimu kwani usingizi ulikua umenizidia na nilikua nalala kila nilipokua napata muda japo kwa kuiba ili nisionekane na mwalimu.
Ndipo mlango wa darasa letu ukafunguliwa, macho ya wanafunzi wote darasani yakatazama mlangoni kuona ni nani anayeingia Kasoro mimi ambae nilikua bado nipo bize na usingizi wangu.
Akaingia mwalimu wa nidhamu Mr Justus akiwa anaongozana na Amina kisha akasalimiana na mwalimu mwenzake na kumweleza ametuletea mwanafunzi mpya ambae alimuamuru ajitambulishe “Hi!!! My name is Amina Rashid(Habari zenu, Majina yangu naitwa Amina Rashid)” Amina alijitambulisha kwa sauti moja nyororo ambayo sikuwahi kuisikia kutoka kwa mtu yeyote yule tangu dunia hii iumbwe, sauti ile ilinifanya niamke kutoka usingizini na kutazama mbele, La haula!!! Haikuwa sauti tu, hata urembo aliokuwa nao Amina nikiri kusema kuwa hakuna mwanafunzi wa kiume mle darasani ambae hakummezea mate.
“Gift hiyo siti pembeni yako anakaa nani?” Mwalimu aliniuliza
“Haina mtu mwalimu” Nilimjibu haraka haraka mwalimu ambae alimwelekeza Amina aje kuketi kwenye siti ya pembeni na ninapokaa.
Ni kama Mungu alikua upande wangu, kwani niliona kama kila kitu kinatokea kwa haraka sana “Mambo” Amina alinisalimia huku akiwa anatabasamu, tabasamu lile likanifanya niione sifa nyingine ya Amina kwenye uso wake, Amina alikua na vishimo viwili kwenye mashavu yake yaani dimpozi, ugonjwa wangu mimi huo, kiukweli niliweweseka nikashindwa hata kuijibu ile salamu, nikabaki namtazama tu nisiongee kitu.
Washikaji zangu walikuwa wananichora (wananitazama) wakaanza kucheka chini chini kwa kuniona domo zege. Amina hakujali sana mimi kutokumuitikia salamu yake, akavuta kiti chake na kuketi ili amsikilize mwalimu aliyokuwa anayafundisha.
Kipindi hakikupanda tena, akili yangu yote ilikuwa kwa Amina , muda mwingi niliutumia kumtazama tu, sikuwa na nguvu za kuacha kuitazama sura yake iliyokuwa imejua kupangiliwa na mwenyeji Mungu.
“Unanitazama sana shida nini?” Huo ulikuwa ni ujumbe wa kikaratasi ambacho Amina aliamua kuniandikia baada ya kuona namtazama sana. Ujumbe ule ulinifanya niache kumtazama na kuangalia mbele bila kumjibu chochote kile.
“Mbona haujanijibu, nimekuuliza shida nini” Amina alinipatia kiujumbe kingine tena, nikakisoma, na nikaamua kukijibu
“Nikisema wewe ni mrembo sana utaniamini?” Amina alisoma ujumbe wangu wa karatasi, nikamwona anatabasamu lakini hakunijibu chochote kile zaidi ya kukikunja kile kikaratasi na kukiweka kwenye begi lake.
“Nimekwambia wewe ni mrembo sana” Nilimtumia meseji nyingine Amina ambayo nayo aliisoma na kuiweka kwenye begi lake
Kitendo kile kikanitia unyonge sana, nikajihisi nimewahi sana kuzicheza karata zangu “Dah itakuwa ameshaniona muhuni” nilijiwazia na tayari nilijipatia majibu kuwa ndio hivyo nishampoteza Amina wangu kizembe namna hiyo.
Kipindi cha Mathematics kiliisha, vikafatia Vipindi vingine ambavyo navyo vilianza na kuisha bila ya mimi na Amina kusemezana. Wakati tupo kipindi cha mwisho kabisa cha siku hiyo zikiwa zimebaki kama dakika ishirini hivi kipindi kuisha, nikawaza kama kumpoteza Amina nishampoteza sasa kwanini nisimpoteze mazima kwa kujilipua kabisa na kuzielezea hisia zangu kwake ndipo nikaamua kuchukua karatasi na kumwandikia maneno haya,
“Mbona hivyo Amina unanitisha ujue” kisha nikampatia asome huku mimi nikiwa nimetazama mbele.
Haikuchukua dakika Amina akanigusa na kunipatia kikaratasi alichokuwa amenijibu “Kwanini unasema hivyo?”
“Kosa langu nini sasa hapa kukusifia au, mbona umeninunia ghafla”
“Hapana hata sijakununia mbona”
“Sasa kama haujaninunia mbona hukunijibu sms yangu nilivyokwambia wewe ni mrembo?”
“Naomba basi tuzungumze kipindi kikiisha wanafunzi wenzetu wakishaondoka darasani sawa” Maneno ya Amina yalinishtua kidogo moyo wangu, sikutegemea kama angeweza kuniambia vile, yaani atake kuzungumza na mimi baada ya vipindi kuisha, tena peke yetu mimi na yeye tu.
“Sawa” Nilimkubalia.
Kipindi cha mwisho kiliisha, wanafunzi wakaanza kuondoka kurudi mabwenini kwa lengo la kwenda kujiandaa na chakula cha mchana. Mimi na Amina hatukuondoka, tulibaki tumeketi kwenye siti zetu tukiwa kimya bila kuongea chochote kile. Sijui Amina alikua anawaza nini muda ule lakini kwa upande wangu sikuwa najua cha kuongea baada ya wanafunzi wote kuisha mle darasani.
“Vipi unanitaka?”
“U….u…Unasema?” Nilijikuta nauliza swali baada ya kujibu swali aliloniuliza Amina.
“Nimekuuliza kama unataka kuwa na mimi kwenye mahusiano? Amina aliniuliza tena swali lake na mara hiyo alikuwa amelifafania zaidi ili nimwelewe alichokuwa ameniuliza. Nilimtazama kwa muda kabla ya kumjibu, Amina alikua amenikazia macho, hakuwa na aibu hata kidogo Tofauti na mimi niliyekuwa naona aibu hata kumtazama,
“Nimekuuliza swali mbona haunijibu” Amina alinisemesha tena
“Swali lako gumu sana ujue”
“Kwahiyo haujui unachotaka kutoka kwangu si ndio?”
“Hapana sio hivyo Amina”
“Ila kumbe nini sasa…….”
“Nikisema kwamba sitaki kuwa na wewe nitakuwa nakudanganya nahitaji sana kuwa na wewe lakini……….” Kabla hata sijamalizia kuongea Amina alinikatiza
“Sawa tutakua wapenzi kuanzia leo sitaki kujua hizo sababu nyingine” Amina aliniambia vile huku akitabasamu. Nadhani udhaifu wangu mkubwa kwa Amina ni tabasamu lake naweza kusema hivyo kwani nazikumbuka vyema hisia zangu muda ule Amina ananiambia kuwa tumeshakuwa wapenzi, ukweli ni kwamba sikuwa tayari bado kuwa na Amina kimapenzi lakini lile tabasamu lake ndilo lililoninyima ujasiri wa kumkatalia alichokuwa amenieleza.
Sijui hata kwanini nilitaka kukataa kuwa naye kwani Amina alikuwa na kila sifa za mwanamke ambazo mwanaume rijali alizihitaji kutoka kwa mwanamke wake.
“Tutakutana jioni sasa mpenzi wangu” Amina alinieleza vile kisha akachukua begi lake na kuondoka zake kwenda bwenini kwao, aliniacha nikiwa bado nimesimama pale kwenye siti yangu nikiwa siamini kilichokuwa kimetokea.
Sehemu ya Pili
Nguvu za kwenda hata bwenini sikuwa nazo kabisa, nilibaki nimeketi tu mule darasani nikijisikilizia. Baada ya muda kupita niliamua kuelekea moja kwa moja hadi dining Hall (Sehemu ya kupatia chakula) ambako nilijua nitakutana na mshkaji wangu Elias ambae kivyovyote vile nilijua tu ni lazima atakuwa amekuja na vyombo vyangu.
Kweli kama nilivyowaza, Elias alikuwa ameshanichukulia na chakula changu,
“Oii G mbona umechelewa hivyo nina ubao kish***nzi leo ujue” Elias alinisemesha, tayari alikua ameshaanza kula bila kusubiria jibu langu.
“Gift…… Gift…….”,Nilisikia kama jina langu unaitwa na hata kabla sijageuka kutazama ni nani aliyekuwa ananiita, nilishangaa narukiwa na mtu mgongoni kwangu kitu kilichofanya nishtuke kidogo, nikageuka na kutazama kuona ni nani huyo aliyenirukia,
“Hahahahahah mbona umeshtuka hivyo” Amina aliniuliza swali lililonifanya nibaki nimeduwaa nisijue cha kumjibu.
Sikuwa peke yangu ambae nilionekana kushangazwa na ujio wa Amina pale kwangu, bali hata mshkaji wangu Elias naye alionekana kushangaa, wanafunzi wenzangu pia mule Dining wengi wao walikuwa wanatutazama, kitendo cha Amina kunirukia kiliwashangaza wengi kwani hakuelewa ukaribu wangu mimi na Amina umeanza tangu lini.
“Yaani huwa sipendi kula peke yangu vipi naweza kujumuika nanyi hapa tule wote?” Amina alituuliza mimi na Elias,
“Ndio karibu haina shida” Elias alimjibu Amina ambae aliweka chakula chake kwenye meza yetu na kuanza kula.
“Vipi G wewe hauli au” Elias aliniuliza baada ya kuniona bado nimesimama bila kuketi kwenye kiti kwa ajili ya kula chakula changu.
Swali lile lilimfanya Amina ahairishe Kula, akaanza kunitazama, ni kama alikuwa anataka kuona ni nini nitakachokiamua pale, mimi sikutaka shida yoyote ile, hivyo niliamua kuketi na kuanza kula jambo lililomfanya Amina atabasamu, nadhani alitabasamu kwa furaha.
“Namfahamu mwenzako tu kwani unaitwa nani wewe?” Amina alimuuliza Elias wakati tunaendelea kula,
“Naitwa Elias na wewe nani vile?”
“Amina……….. Nyie ni marafiki sio?”
“Sio marafiki tu sisi ni zaidi ya ndugu kwa hapa tulipofikia au naongopa G?”
“Ni kweli tulishapita Levo ya urafiki sie”
Nililijibu swali la Elias ambae alionekana kuchangamka wakati anaongea na Amina.
“Kumbe, basi hata nikikueleza siri ya rafiki yako unaweza kuitunza kama siri yako eti” Amina alimuuliza Elias
“Hilo ni swali kwani? Nina siri nyingi sana za mwamba hapa na hakuna hata moja iliyovuja hadi leo” Elias alitamba,
“Basi sawa nimefurahi kusikia hivyo”
“Vipi kwani kuna jambo unataka kunieleza au?”
“Lipo ndio sema sidhani kama ndugu yako atafurahia nikikweleza”
“Usijali hata, G hanaga noma weh nieleze tu Amina”
“Kweli kabisa?”
“Niamini mimi Amina”
Amina kusikia vile alinitazama, ni kama alikuwa anataka kuniomba jambo lakini alishindwa, muda wote huo mie nilikuwa kimya nawasikiliza tu wanavyozungumza bila kutia neno lolote lile.
“Kwakuwa umetaka kujua shemeji yangu nitakwambia, Gift na mimi ni wapenzi” Amina alimweleza Elias
“Weeeeeh acha basi kunitania” Elias alionekana kushangaa
“Naanzaje kukutania sasa shemeji yangu si umuulize G kama nakudanganya sasa” Amina alijitetea.
Elias kusikia vile alinitazama, mie sikumtazama, Elias moja kwa moja akajua taarifa zile alizokuwa ameambiwa na Amina zilikuwa ni za ukweli. Bila kutarajia Elias alianza kucheka, sio kucheka tu alicheka sana kiasi cha kufanya wanafunzi wengine waanze kututazama pale tulipokuwa tumekaa.
“Kweli watu wasiri sana, nashukuru kukufahamu shemeji yangu, jisikie huru kabisa kwangu kama ni shemeji umepata sasa” Elias alijitapa.
“Naomba ukimaliza kula tuzungumze kidogo pembeni” Amina aliniomba, sikuwa na kipingamizi zaidi ya kumkubalia.
Kweli tulivyomaliza kula Elias aliondoka na vyombo vyangu na kutuacha mimi na Amina tunazungumza,
“Mbona kama sikuelewi G” Amina aliniuliza swali ambalo sikulielewa
“Haunielewi vipi?”
“Naona kama haujafurahia mimi kujitambulisha kwa Elias au nimekosea”
“Sijafurahia vipi sasa, au nini kinachokufanya useme hivyo?”
“Nakuona tu kama huna raha hivi au labda nalazimisha mahusiano kwako nambie nijue” Amina aliniuliza
“Hapana, mbona umefika mbali hivyo Amina siko poa tu” Nilijitetea.
“Kweli?”
“Kweli kabisa Amina, kwanini nisipende sasa wewe kujuana na Elias” Nilijitahidi kumwondolea hofu Amina ambae alikubaliana nami japo sikumuona kama ameridhishwa na majibu yangu. Tukaagana akarudi bwenini kwao na mimi nikaenda bwenini kwetu.
Huo ndio ukawa mwanzo wa mahusiano yetu mimi na Amina, mwanzoni sikuwa huru kabisa kujionesha kwa watu kuwa tulikua wapenzi, tofauti na Amina yeye muda wote ni kama alitaka kila mtu afahamu kuwa alikuwa kwenye mahusiano na mimi.
Amina alikuwa huru sana kufanya chochote na mimi bila kujali macho ya watu, alipenda sana kutembea na mimi huku tukiwa tumeshikana mikono, hakuona aibu kunikumbatia kila mara tulipokuwa tunakutana na wakati mwingine kunipiga mabusu kabisa.
Kama nilivyosema mwanzoni sikuwa huru kabisa lakini kadri siku zilivyokuwa zinakwenda mbele ndivyo nilivyojikuta naanza kuzoea na kujikuta nakuwa huru na mimi kufanya chochote na Amina wangu bila woga wowote ule.
Amina alinieleza kuwa kabla hata ya kuhamia shuleni kwetu alikuwa ameshanuia moyoni mwake kuwa mwanaume wa kwanza atakayemtongoza hapo shuleni basi ndiye atakayekuwa mpenzi wake na atafanya lolote lile kwa ajili ya mpenzi wake huyo. Naona kama bahati hiyo iliniangukia mimi kwani ukiachana na kwamba mimi ndiye niliyeanza kumtongoza Amina, kumbe hata jibu langu lilikuwa limeshaandaliwa hata kabla ya Amina kufika shuleni kwetu.
Shule yetu ya Mwadui ilikuwa ni shule inayoendeshwa kwa kusimamia maadili ya dini ya kikristo kwani ilikuwa chini ya kanisa la KKKT (Lutheran). Hivyo kuna mambo ambayo yalikua yanapingwa sana shuleni kwetu hasa mahusiano. Tayari mimi na Amina tulikuwa tumeshapewa onyo na mwalimu wa nidhamu kuwa kama tutaendelea kuonekana tupo pamoja basi wazazi wetu wangeitwa shuleni na sisi kupewa taarifa ya kufukuzwa shule.
Pamoja na yote hayo hatukuonekana kutaka kusikia, ndio kwanza kila siku penzi letu lilizidi kukua, hakuna kitu ambacho hatukuwahi kufanya mimi na Amina kama wapenzi, ndio hakuna kitu ambacho hatukuwahi kufanya, kila kitu kinachotakiwa kufanywa na wapenzi basi sie tulikifanya bila kujali mazingira yaliyokuwa yanatuzunguka.
Siku moja tukiwa darasani tunajisomea mwalimu wa nidhamu alitufuata wote n a kutueleza tumfuate ofisini kwake. Wito ule haukuwa wa kushangaza kwetu kwani tulikuwa tumeshauzoea.
Tulifatana na mwalimu hadi ofisini kwake, kufika ofisini kwake tulishangaa kuwakuta wazazi wetu wanatusubiria huko, yaani baba yangu na mama yake AAmina. Walipotuona kwa pamoja walitabasamu, tabasamu ambalo kiuhalisia lilinitia woga moyoni mwangu, sijui mwenzangu Amina yeye alilichukulia vipi lile tabasamu.
“Wazazi wenu wanataka kuzungumza na nyie mie nipo nje nawasubiria” Mwalimu wa nidhamu aliongea vile kisha akatupisha.
Tulianza kwa kuwasalimia wazazi wetu, kisha wakatuomba tukae ili wazungumze na sie
“Huyu ndio kijana wangu Gift” Mzee wangu alimweleza mama Amina ambae alinitazama kwa tabasamu pana usoni mwake,
“Nashukuru kukufahamu mwanangu” Mama Amina aliongea vile huku akinipatia mkono wake, tukashikana mikono kisha naye akamtazama mwanae Amina na kumweleza baba yangu,
“Na mimi huyu ndio binti yangu Amina naona wanalingana lingana tu na mwanao Gift” Mama Amina alimalizia kuongea maneno yaliyomfanya baba yangu acheke kidogo kitu kilichozidi kunichanganya kwani sikujua kilichokuwa kinaendelea pale.
“Mama, huyu ndiye mwanaume uliyeniambia unamleta kumtambulisha kwangu kama mumeo ajae?” Amina alimuuliza mama yake swali lililonichanganya kidogo
“Unasema? Mume? Au sijaelewa nini hapa…….. Unaongea nini Amina huyu ni baba yangu ujue” Nilijikuta nauliza maswali mfululizo kwa paniki kitu kilichofanya baba yangu aniombe nitulie kwanza anielezee.
“Mwanangu sitaki kuwa mpweke tena, nahitaji kuwa na msaidizi na mimi” Mzee wangu alinieleza.
Hakujua maneno yale yalivyokuwa yananichoma moyoni mwangu, niliwaza itawezekana vipi mama wa mpenzi wangu awe mke wa baba yangu mzazi, yaani ni kama nilikuwa napewa taarifa za kuanza kumuheshimu Amina na kumchukulia kama dada yangu, nitaweza vipi mie niliwaza.
Kiukweli nilijihisi kutaka kuchanganyikiwa ghafla………….
“Vipi Gift mbona sikuelewi” Baba aliniuliza
“Hapana baba nipo kawaida tu” Nilimjibu baba kumuondoa wasiwasi lakini kiukweli sikuwa sawa kabisa, taarifa zile ziliichanganya sana akili yangu. Mbaya zaidi sikuona kama ni taarifa zilizomchanganya Amina ambae muda wote alionekana kuwa sawa kabisa.
“Nashukuru kukufahamu sana baba yangu” Amina aliongea na baba yangu huku akiwa ametabasamu.
“Nashukuru pia kukufahamu” Baba yangu aliitikia
“Unaona sasa mume wangu hapakuwa na ugumu wowote ule ulikua unaogopa bure” Mama Amina aliongea na baba yangu ambae alionekana kufurahia sana kila kitu kilichokuwa kinaendelea pale.
Muda wa wazazi wetu ulifika kuondoka, wakaondoka huku wakiwa na furaha sana. Ni mimi tu ndiye niliyeonekana kujali sana taarifa zile. Ilinibidi nimwombe Amina tuzungumze kwanza kabla ya kurudi darasani.
“Unaonekana kama haujashtushwa kabisa na taarifa hizi za wazazi wetu” Nilimuuliza Amina
“Cha kunishtua nini sasa hapo? Au kipi cha ajabu ambacho haujawahi kukishuhudia hapa? Hebu waache wazazi wetu waufurahie uzee wao bhana”
“Haujanielewa Amina, sipo hata huko mie, nachojaribu kuwaza hapa ni kuhusu mahusiano yetu, itawezekana vipi mimi na wewe kuwa pamoja huku wazazi wetu nao wanataka kuoana?”
“Hahahahahaahahah” Amina alianza kucheka sana kitu ambacho sikukielewa.
“Unacheka nini sasa mbona sikuelewi”
“Gift….. unafurahisha sana ujue inamaana hadi sasa haujajua bado kama tumeshaachana” Amina alinieleza maneno hayo huku akiwa anacheka, nikadhani ananitania hivyo ikanibidi nimuulize kama yupo siriazi au ananitania.
“Nipo siriazi mie, mahusiano yetu yameishia pale wazazi wetu walivyojitambulisha kuwa wapo pamoja na wanahitaji kuishi pamoja”
“Amina…… acha basi kunitania mbona Unaongea maneno makali hivyo alafu kiwepesi sana”
“Gift naona unanichelewesha tu hapa naomba uniache nirudi zangu darasani “ Amina aliongea maneno yale kisha akaanza kuondoka.
Sikutaka kukubaliana na ukweli uliokuwa mbele yangu,nilimkimbilia Amina na kumzuia asiendelee na safari yake.
“Amina mbona hivyo mpenzi wangu, haya mambo mbona yanazungumzika usinifanyie hivyo mwenzako” Nilimweleza Amina maneno hayo kwa hisia, tayari machozi yalikua yameanza kunitoka.
“Gift nakuomba kuwa mwelewa basi”
“Nakuwaje mwelewa sasa kwenye suala kama hili Amina wewe ndio sio mwelewa”
Amina kuona kama sipo tayari kumuelewa alianza kuondoka lakini nilimzuia, akawa analazimisha kuondoka hivyo hivyo kwa nguvu lakini alishindwa kwani tayari nilikua nimeshamkamata mkono wake kwa nguvu kitendo kilichofanya tuonekane kama tunagombana.
Wanafunzi waliokuwa kwenye madarasa ya karibu walianza kutuchungulia kupitia madirisha ya madarasa yao. Wapo walioanza kupiga kelele za shangwe ambazo sikuzijali hata kidogo. Nia na dhumuni langu kwa muda ule lilikuwa ni kumtaka Amina anielewe na si vinginevyo.
Baada ya mvutano wa kama dakika tano, walimu kadhaa walifika pale, mwalimu wa nidhamu akatutaka tuelekee ofisini kwake .
“To my office right now (Nendeni ofisini kwangu sasa hivi)” Mwalimu yule wa nidhamu kwa majina ya Justus aliongea kwa hasira.
Tulielekea hadi ofisi ya nidhamu, huko mwalimu alitueleza tupige magoti kabla ya kuanza kuzungumza naye.
“Eenhe nyie wapendanao leo imekuwaje hadi mkaanza kupigana hadharani” Mwalimu Justus alituuliza kwa ukali kidogo.
Mie sikuwa na nguvu za kuzungumza kabisa kwani hasira zilizokuwa zimenijaa kifuani mwangu hazikuelezeka, na nilijikuta nalia mfululizo, sikuweza kujizuia kabisa. Ila pamoja na yote hayo Amina alionekana kuwa Tofauti na mimi. Ukiachana na hasira alizokuwa nazo juu yangu, Amina alitaka kunieleza msimamo wake bayana tena mbele ya mwalimu wetu
“Mwalimu, nimeshamweleza mara kibao Gift kuwa simtaki na sitaki kuwa nae labda unisaidie wewe kumweleza labda atakuelewa” Amina aliongea maneno makali yaliyoshindilia zaidi Msumali wa moto kifuani mwangu.
Kusikia vile mwalimu Justus alinitazama kwa muda bila kuongea chochote kile kisha akamtazana Amina na kumweleza kuwa aelekee darasani na aniache mie mule ofisini. Amina akaondoka zake.
Baada ya Amina kuondoka mwalimu Justus aliniamuru ninyanyuke kisha niketi kwenye kiti cha mule ofisini, nikafanya vile kisha mwalimu Justus akaniambia nimueleze ukweli wa kila kilichotokea na kinachoendelea kuhusu mimi na Amina. Sikuona Haja ya kumficha tena mwalimu hivyo Nilimweleza ukweli wa kila kilichokuwa kimetokea.
Mwalimu alinisikiliza kwa umakini sana, hakutaka kuniingilia, aliniacha nizungumze hadi nimalize, kisha akanyanyuka na kuchukua karatasi moja na kalamu ya kuandika.
“Mdogo wangu huu ni mwezi wa ngapi?” Aliniuliza
“Ni mwezi wa tisa mwalimu” Nilimjibu
“Sasa nisikilize kwa makini mdogo wangu, mwezi kesho kutwa unaingia kufanya mitihan yako ya mwisho kumaliza kidato cha nne, namaanisha nini kusema hivyo, huu ni muda wako wa kuwa makini sana na masomo na si kitu kingine chochote kile, si umesema Amina mnaenda kuishi nae pamoja mtakaporudi nyumbani?” Aliniuliza na nikamkubalia
“Sasa hebu fanya hivi kwa muda huu uliobakia……Komaa na kitabu mdogo wangu, soma sana na usiiruhusu akili yako iwaze mambo mengine, najua ni ngumu ila inawezekana kama utaamua alafu mtakaporudi nyumbani ndio ukakomae na Amina wako si umesema unampenda sana na huwezi ishi bila yeye?” Aliniuliza tena na nikamjibu Ndio.
“Basi hakikisha unafaulu mitihani yako, hakuna mwanamke anayependa mwanaume zezeta sawa mdogo wangu”
Mwalimu Justus alinieleza mambo mengi sana kuhusu maisha siku ile, hakuwa tena mwalimu wangu bali aliamua kuwa kama kaka yangu, kikubwa alichonishauri nisisahau kilichonipeleka shule na nilimwelewa sana hivyo akaniambia nirudi darasani kujisomea.
Nilikwenda hadi darasani, huko nilifika na kumkuta Amina akiwa ameketi kwenye siti yake, hatukusalimiana zaidi ya kubaki tukimsikiliza mwalimu aliyekuwamo darasani anafundisha. Mwalimu alipomaliza kufundisha aliondoka na kutuacha sie tukijiandaa kutoka kwani hicho ndio kilikuwa kipindi cha mwisho kwa siku hiyo.
“Samahanini jamani wanadarasa naombeni kuzungumza nanyi kabla hamjaondoka” Amina alisimama na kuwaomba wanadarasa wasiondoke kwani anataka kuzungumza nao. Kweli wote waliketi na kumsikiliza nikiwemo na mimi.
“Kama mlivyoona tukio la pale nje lililomfanya mwanafunzi mwenzenu hapa (huku akinishika begani) hadi akalia, ujumbe ni mfupi tu ya kuwa mimi na Gift tumeachana kwa hiyo jimbo lipo wazi” Amina aliongea vile kisha akaanza kucheka.
Wanafunzi wote darasani walibaki wanamtazama Amina, hakuna aliyemwelewa, lakini hiyo haikuwa sababu ya yeye kuacha kuendelea kucheka
“Mimi na Gift tumeachana jamani msichoelewa nini hapa mbona kama mnanishangaa” Amina alikazia.
Hasira zilinijaa kifuani, kicheko kile cha Amina pia kilizidi kunizidishia hasira zangu, niliwaza ni kama kweli kulikuwa na ulazima kiasi hicho cha kuwatangazia wanafunzi wenzetu kuhusu mimi na yeye kuachana, jibu likawa ni hapana.
Bila kutarajia nilijikuta nimenyanyuka pale nilipokua nimekaa kisha nikamshika Amina kwa nguvu, nikamtwanga ngumi mbili za nguvu kwenye pua yake zilizompeleka chini moja kwa moja na kumfanya azime pale pale. Wanafunzi wenzangu wote walishtuka pia kwa kudhania kuwa labda naweza kuwa nimeua.
Sehemu ya Tatu
Hasira Hasara!!! Ni msemo wa kawaida ila wenye maana kubwa sana. Binafsi msemo huo nilikua sijawahi kuuelewa hadi siku hiyo ambapo nilimshuhudia Amina akianguka chini kama mzoga mbele ya macho yangu.
Kelele za wanafunzi wenzangu mule darasani ndio zilizonitia hofu zaidi. Elias mshkaji wangu hakutaka kupoteza muda, alihitaji kuchukua maamuzi ya haraka ili anisaidie rafiki yake hivyo alimfuata Amina pale chini alipokuwa ameanguka kisha akaanza kujaribu kumuamsha bila mafanikio.
Wanafunzi wenzangu kadhaa nao walimsogelea Amina na kuanza kumsaidia Elias kumuamsha. Lakini hakuna kilichobadilika, Amina aliendelea kuwa kimya pale chini kitu kilichofanya wanafunzi wenzangu washauriane kumbeba na kumuwahisha kwa nesi wa shule.Wakafanya hivyo upesi baada ya wote kuwa wameafikiana.
Taarifa zilifika ofisini kuhusu tukio lile, mwalimu Justus akaniita tena ofisini kwake na hiyo ikiwa ni mara ya pili kwa siku hiyo. Nilipofika tu ofisini mwalimu Justus hakutaka kusikiliza maelezo yangu zaidi ya kunishushia viboko mfululizo hadi pale aliporidhika ndio akaamua kuchukua barua aliyokuwa ameshaindaa tayari kwa ajili yangu.
“Nenda nyumbani ukaniletee wazazi wako” Mwalimu Justus alinieleza huku akiwa ananipatia ile barua.
Maneno ya mwalimu Justus yalikua yameeleweka sana lakini nilitaka kuyapinga kwa kujaribu kuomba msamaha labda nitaeleweka lakini ilikua ni kama natwanga maji kwenye kinu kwani mwalimu hakuelewa na alisisitiza niondoke shuleni mara moja bila kupoteza muda.
Hivyo ilibidi nielekee bwenini kwetu, huko nilikwenda kubadilisha nguo zangu na kuchukua baadhi ya vitu ambavyo nilivihitaji kurudi navyo nyumbani.
Safari yangu ya kurudi nyumbani ikaanza. Nakumbuka safari ile ilikuwa fupi sana kufika nyumbani, nafikiri ni kwa sababu ya mawazo mengi niliyokuwa nayo kichwani mwangu. Cha ajabu sikuwa nawaza kabisa kuhusu baba yangu, akili na mawazo yangu yote yalikuwa kwa Amina mpenzi wangu. Muda wote nilikuwa nawaza kama atakuwa amezinduka huko shuleni nilikomuacha. Nilijikuta najiona mjinga na nilizilaumu sana hasira zangu ambazo niliona ni kama ndio zilikuwa zimepigilia msumali wa mwisho wa mimi na Amina kuachana.
Nilifika nyumbani lakini sikumkuta mzee hivyo nikafanya utaratibu wa kuwasiliana nae, akanieleza kuwa yupo njiani anaelekea Arusha na mama yake Amina hivyo nifanye kwenda kwa bibi nikamsubiri huko. Sikubisha hivyo nikaanza safari nyingine ya kuelekea kwa bibi kwenda kumsubiri baba atakaporejea.
☆☆☆☆☆☆☆☆☆☆☆☆☆☆☆☆☆☆☆☆☆
Amina alizinduka baada ya nusu saa toka afikishwe kwa nesi wa shule, mkononi mwake alikuwa ameshachomwa sindano na kutundikiwa dripu ya maji kwa ajili ya kumuongezea nguvu.
Nesi alimtoa hofu kwa kumueleza kuwa asijali kwani baada ya muda atakua sawa. Elias hakutaka kutoka ndani ya chumba kile tangu Amina alipokuwa amezimia. Alitaka kumwona Amina akiwa sawa hivyo hakutaka kuwa mbali naye. Yote hayo alifanya kama kuniwakilisha rafiki yake ambaye muda wote huo nilikua nimesharudishwa nyumbani bila hata kuagana nae.
“Gift yuko wapi?” Amina alimuuliza Elias
“Yupo bwenini amepumzika, hawezi kuja huku” Elias aliamua kumuongopea Amina, hakutaka kumpatia wasiwasi kwani lengo lake kubwa lilikuwa ni kuhakikisha anaona afya ya Amina inakuwa sawa tena.
“Kwanini asiweze kuja? Au hataki kuniona mimi?”
“Hapana sio hivyo, mwalimu Justus ndio ameelekeza hivyo, amemzuia kusogea kabisa karibu na wewe kuepusha maafa zaidi”
Kusikia vile Amina alianza kulia kwa kugugumia taratibu, hakutaka kutoa sauti japo machozi yaliyokuwa yanambubujika mashavuni mwake yalimsaliti.
“Shem shida nini tena mbona unalia”
“Jamani Gift wangu najua atakua ananichukia sana muda huu” Amina alijibu
“Hapana hata usiwaze hivyo shem, G anakupenda sana zaidi ya unavyofikiria”
“Nalijua hilo lakini nitafanya nini sasa mie? Ni lazima mmoja wetu alipaswa kuchukua maamuzi magumu ili kuweka mambo sawa, na mimi ndio nimechagua kuwa mbaya Elia”
Amina aliongea maneno ambayo Elias hakuyaelewa, hivyo ikabidi amuulize Amina ni nini alichokuwa anamaanisha kwa kusema hivyo.
Amina ilimbidi amwambie Elias kila kitu kilichokuwa kinaendelea, hakumficha hata kitu kimoja. Amina alimweleza Elias kuwa bado ananipenda sana lakini ameamua kuchukua maamuzi magumu ya kuachana na mimi mapema kwani anaona sio sawa kuwa na mimi tena hali ya kuwa wazazi wetu wanakwenda kuoana, hivyo ameamua kuepusha mengi mabaya yanayoweza kuja kutokea huko mbele.
Elias alimuelewa sana Amina,pia alimuonea huruma sana kwani muda wote aliokuwa anaongea machozi yalikuwa yanamtoka na alijaribu kujizuia bila Mafanikio. Elias alimtia moyo Amina ya kuwa hilo nalo litapita.
Elias na Amina walizungumza sana siku ile kitendo kilichowafanya watengeneze ukaribu ambao hawakuwa nao mwanzo.
Elias aliamua kuchukua jukumu la kumlea Amina kipindi chote ambacho alikua anaumwa. Mazoea yaliongezeka hadi pale alipopona lakini hawakuacha kuendelea kuwa karibu. Amina alimuomba Elias abadili siti yake ya darasani na kwenda kuketi nae pale nilipokua nakaa mimi hadi pale nitakaporejea, Elias hakubisha akafanya hivyo.
Ukaribu wao haukuwa wa kawaida kwani kila sehemu walikuwa pamoja. Walipenda Kula pamoja dining, walipenda kuketi pamoja mida ya ibada za kanisani hata shughuli zote za shule walifanya pamoja.
Wanafunzi wenzangu wakaanza kuhisi labda Elias na Amina ni wapenzi lakini walikanusha kila mara walipoulizwa. Hakuna kati yao aliyekubali japo nafsi zao ni kama zilikuwa zinatamani skendo hiyo ingekuwa ni ya ukweli. Tayari hisia za kimapenzi juu yao zilikuwa zimeshajengeka. Kila mtu alikuwa anamtamani mwenzake lakini hakuna aliyeweza kuzieleza hisia zake. Labda ni kwa sababu ya ukaribu wangu kwao ndio maana walijikuta wanashindwa kuongea kile kilichokuwa kinawatafuna nafsi zao.
Amina yeye hisia zilimzidia hivyo aliamua kuchukua maamuzi magumu ambayo alijua fika yataniumiza sana. Amina aliamua kumweleza Elias kuwa anahitaji kuzungumza nae usiku wa siku hiyo baada ya kumaliza kujisomea masomo ya jioni. Elias hakuwa na hiyana zaidi ya kuitikia wito wa Amina.
Kweli usiku masomo yalipokwisha wanafunzi wote walitawanyika na kwenda mabwenini kwa ajili ya kulala isipokuwa Elias na Amina ambao walikuwa na miahadi ya kuzungumza usiku huo.
“Nakusikiliza Amina, naona upo kimya sana wakati watu wote wameshaondoka……..” Elias alishindwa kuendelea kuongea kwani Amina alikuwa amemsogelea na kumchumu mdomoni mwake kisha akarudi nyuma na kuanza kumtazama bila kuzungumza chochote kile.
Elias hakutaka kupewa ishara nyingine tena, tayari alikuwa ameshaelewa ni nini ambacho Amina alikuwa anakihitaji kwa muda ule. Taratibu alimsogelea Amina kisha akazipeleka lipsi zake na kuzikutanisha na lipsi za Amina ambae alizipokea bila kipingamizi chochote kile kisha wote kwa pamoja wakaanza kubadilishana mate.
Ukurasa rasmi wa mahusiano kati ya Elias na Amina ulifunguliwa rasmi usiku ule. Kila mmoja wao kati ya Amina na Elias walionekana kukifurahia kitendo chao cha kubadilishana mate. Hawakutaka kujali tena kuhusu mimi, hisia zao ndicho kitu pekee walichokitazama kwa muda ule. Mioyo yao iliwaaminisha ya kuwa wanapendana sana na hawawezi kuacha kuwa pamoja kisa mimi.
Mimi nyumbani nilikaa kwa muda wa wiki tatu kabla ya baba yangu kurudi kutoka Arusha na kuniomba nirudi nyumbani kutoka kwa bibi yangu nilikokuwa nimeenda.
Baba yangu alitaka kujua ni kwanini anahitajika shuleni, Nilimweleza ukweli ya kuwa nimepigana ila sikumwambia kama mtu niliyepigana nae alikua ni Amina. Baba yangu kusikia vile alikasirika sana na alitaka kuniadhibu lakini alizuiriwa na mama Amina ambae alikuwepo muda wote ule tuliokuwa tunazungumza.
Baba alinieleza ya kuwa nimshukuru mama yangu kwa kunitetea kwani isingekuwa hivyo angenibutua sana. Kwa upande wangu mama Amina sikumuona kama mkombozi wangu bali nilimuona kama adui yangu kwani nilimuona kama mtu aliyesababisha mimi na Amina tuachane, hivyo sikuwa na nia ya kumshukuru kwani bila yeye nisingefikia hatua hiyo ya kumpiga Amina.
Usiku ulifika tukalala, kesho yake mapema tuliamka kwa ajili ya safari kuelekea shuleni. Tulivyofika shule, mwalimu Justus alitupokea ofisini kwake na alimweleza baba yangu kuwa anataka kunirudisha nyumbani rasmi nikasubirie muda wa kufanya mitihani ya kumaliza shule ndio nirudi kufanya mitihani.
Baba yangu alijitahidi sana kunitetea lakini msimamo wa mwalimu Justus ulikua vile vile, haukubadilika
“Nisamehe sana mzazi mwenzangu, lakini hatuwezi kuvumilia matukio kama haya na tunafanya yote haya ili kuepusha kujirudia kwa matukio kama haya kwa wanafunzi wengine” Mwalimu Justus alikazia.
Baba yangu hakuwa na cha kufanya zaidi ya kukubaliana na ukweli, hivyo alinieleza niende nikachukue vitu vyangu kwa ajili ya kuondoka.
Nilielekea bwenini kisha nikachukua vitu vyangu kwa lengo la kuondoka lakini kabla sijaondoka Elias alifika bwenini. Nilifurahi sana kumuona na tulikumbatiana kwa furaha, Elias aliniuliza kama nilikuwa na mpango wa kuondoka bila kumuaga,
“Hapana sio hivyo mshkaj wangu, nisingeweza kuja darasani si unajua tena ni muda wa masomo huu na mimi siruhusiwi kuwa hapa shuleni” Nilijitetea
“Hata kama mshikaji wangu, ila vipi umeambiwaje ofisini” Elias aliniuliza
“Nimeambiwa nirudi nyumbani, nitarudi shule muda wa mitihani kuja kufanya mitihani tu”
“Duh!!! Pole sana ila hapa sijaja kwa ajili yangu, Amina ameniagiza mwanangu” Elias alinieleza maneno ambayo sikuyaamini.
“Amina amekuagiza? Kwangu mimi? Anataka nini tena?!” Nilijikuta nauliza maswali mfululizo
“Usiwe hivyo bwana, Amina anahitaji kuzungumza na wewe anaumia sana kuona yeye na wewe hampo sawa twende ukamsikilize” Elias alinieleza.
Ikabidi tutoke bwenini na kuelekea maeneo ya vyoo vya wanawake, huko ndiko Elias aliniambia ya kuwa Amina yupo huko ananisubiria. Nilifika maeneo hayo na kumkuta Amina akiwa ameegemea ukuta mmoja wa choo kwa nje, na alikua ameinama kama mtu mwenye mawazo hivi,
“We mrembo mbona hivyo stress zote hizo za nini?” Nilimuuliza Amina baada ya kuwa nimemkaribia pale alipokuwa.
Amina alinyanyua kichwa chake na kunitazama, alionekana kuwa mnyonge sana, na aliponiona tu machozi yalianza kumtoka. Ilinibidi nimsogelee hadi pale alipokuwa kisha nikamuuliza anasumbuliwa na nini mbona analia.
“Gift nisamehe sana….. Nisamehe G …….” Amina aliniomba msamaha huku akiendelea kulia
“Haujanikosea chochote kile mbona, ni mimi ndiye nayepaswa kukuomba msamaha Amina”
“Hapana G, najuta sana mwenzio nisamehe sana” Amina aliongeza, na aliendelea kulia sana.
Hivyo ilinibidi nimsogelee karibu zaidi kisha nikamkumbatia na kuanza kumbembeleza huku nikimweleza ya kuwa asijisikie vibaya kwa sababu yangu kwani kila nilichokifanya nilikifanya nikiwa na akili zangu timamu na hapo nilikua nalipia gharama za maamuzi yangu. Pia nilimuomba msamaha kwa kumpiga siku ile, Amina alinielewa na baada ya muda alinyamaza ndipo nikapata muda wa kuzungumza nae. Muda wote huo Elias alikuwa amesimama pembeni yetu akitutazama na pia alikua anaangalia mazingira kuhakikisha usalama wa eneo lile tusije kukutwa na mtu yeyote eneo lile.
“Vipi Amina upo poa lakini” Nilimuuliza Amina
“Ndio, mie nipo salama sana, vipi nyumbani baba yako hajakasirika sana”
“Hapana hata, mama yako kanitetea sana, mzee hajanigusa kabisa”
“Usinitanie bhana, kwani mama yangu tayari ameshaamia kwenu?” Amina aliniuliza
“Ndio, sasa hivi wazazi wetu wanaishi pamoja”
“Aaanh sawa” Amina alinijibu, ukimya kidogo ukapita tukitazamana, ni kama nilikua na mambo mengi kichwani mwangu niliyohitaji kuzungumza na Amina lakini nilishindwa kufanya hivyo. Hivyo ikanibidi nimuage tu.
“Mie niondoke sasa, mzee ananisubiria nisimuweke sana”
“Okay sawa, au twende pamoja na mimi nikamsalimie baba”
“Hapana haina haja, wewe nenda darasani tu usijali sana kuhusu mzee wangu” Nilimkatalia Amina, nadhani hofu ya ukweli kujulikana ilikuwa imenitawala, sikutaka kabisa baba ajue kama mtu niliyegombana nae alikua ni Amina.
Nilirudi bwenini na kuchukua mizigo yangu, ofisini nilimkuta baba akiwa ananisubiri.
“Nimeongea na mwalimu wako hapa ameniruhusu nionane na Amina naomba uende ukaniitie kwanza nimsalimie kabla hatujaondoka.” Baba alinieleza maneno ambayo sikutaka kuyasikia kwa muda ule japo uwezo wa kumkatalia sikuwa nao hivyo ilibidi nimkubalie japo kishingo upande kumridhisha.
“Sawa baba wacha nikamuite”
Nilijua sehemu ya kumpata haraka ilikuwa ni darasani kwao, nilielekea huko kwani wakati naachana nae kule chooni alinieleza kuwa anarudi darasani muda huo huo.
Nilifika darasani, nikabisha hodi kisha nikamsalimia mwalimu niliyemkuta mule darasani kisha nikamuulizia Amina. Mwalimu alijaribu kumuita bila Mafanikio, wanafunzi wenzangu wakaniambia kuwa ametoka darasani muda sana hivyo nikawaza haraka haraka huenda labda akawa bado yupo ile mitaa ya chooni na akili yangu ilinieleza nielekee huko nikamtazame.
Nilielekea hadi huko chooni, ni kama nilikuwa nashauku ya kumuona tena Amina, kwani muda wote niliokuwa natembea kuelekea kule chooni sikuacha kuangaza macho yangu huku na huko kutazama labda naweza kukutana nae njiani.
Ile nafika chooni pale nje nilipokuwa nimemuacha Amina, sikutaka kuamini nilichokiona, Amina alikuwa ukutani ameegemea kwenye ukuta ule, alafu mbele yake Elias alikuwa amesimama karibu yake, mkono wake mmoja alikuwa ameupitisha kukizunguka kiuno cha Amina na mkono wake mwingine alikuwa amemshikilia vyema Amina shingoni kwake. Elias alikuwa ameinama kidogo ili alingane na Amina ambae yeye alikuwa ameinyanyua miguu yake kidogo ili kumsaidia Elias amfikie vyema pale alipokuwa na alikuwa amenyanyua mikono yake yote miwili kuzunguka nyuma ya shingo ya Elias.
Tukio lililokuwa linaendelea pale lilikuwa ni tukio la kubadilishana juisi za vinywa vyao. Amina alikuwa anampatia Elias juisi yangu ambayo alikuwa amezoea kunipatia mimi kila mara ninapoihitaji. Mbaya zaidi Amina alionekana kufurahia kitendo kile kwani alionekana kumpatia ushirikiano aliouhitaji Elias.
Nilijikuta naanza kutetemeka, hasira zilinijaa kifuani, nilihisi kama nakabwa kwenye koo langu, machungu niliyoyahisi pale hayakuelezeka, sikuwahi kuwaza kushuhudia jambo kama hilo tena mapema kiasi hicho, yaani wiki tatu tu zilitosha kabisa kumfanya Amina anisaliti, tena na mshkaji wangu wa karibu sana? Hapana, sikutaka kuamini.
“Aminaaaaa…………..” Nilijikuta namuita Amina kwa hasira.
INAENDELEA

