𝐍𝐈𝐋𝐈𝐌𝐓𝐄𝐒𝐀 𝐌𝐓𝐎𝐓𝐎 𝐖𝐀 𝐊𝐀𝐌𝐁𝐎 𝐁𝐈𝐋𝐀 𝐊𝐔𝐉𝐔𝐀 𝐍𝐈 𝐌𝐖𝐀𝐍𝐀𝐍𝐆𝐔 𝐍𝐈𝐋𝐈𝐘𝐄𝐌𝐓𝐔𝐏𝐀𝐆𝐀 𝐌𝐒𝐈𝐓𝐔𝐍𝐈 𝐊𝐈𝐏𝐈𝐍𝐃𝐈 𝐂𝐇𝐀 𝐍𝐘𝐔𝐌𝐀\
Episode 26
Ndani ya siku mbili tangu Tony na mke wake wafike Dar es salaam, Majaliwa alifanikiwa kupata VISA za kusafiria nje ya nchi. Maandalizi ya safari kuelekea India yalikamilika kwa asilimia mia kilichobakia ni siku na saa ifike ili waweze kuondoka. Ni Majaliwa na Tony ambaye alifahamika kama Baba mzazi wa Jasmine. Majaliwa yeye alijua anampeleka kwenye matibabu Baba wa mzazi wa mke wake kumbe hata yeye ni Baba yake mzazi. Suala ya yeye kutaka kusafiri alilifikisha mpaka kwa wazazi wake ambao ni Kareem na Radhia. Siku moja kabla ya safari, Kareem na Radhia wakajiandaa kwenda nyumbani kwa Majaliwa ili kuonana na wazazi wenza, yaani wazazi wa mke wa mtoto wao. Ilikuwa mara ya kwanza kabisa kwa wazazi wa Majaliwa na wazazi wa Jasmine kukutana. Wote walikuwa hawafahamiani kwa sura kwa kipindi chote ambacho vijana wao waliishi pamoja kama mume na mke.
****
Kiyoyozi kilipuliza taratibu kabisa na kusambaza upendo wa hewa safi kwa watu wote waliokuwemo ndani ya nyumba ya Majaliwa. Sauti za watu zilisikika sebuleni wakipiga stori mbalimbali zinazohusu utofauti wa maisha ya mjini na kijijini. Majaliwa na Jasmine wao walisimama kidete kusema kwamba maisha ya kijijini ni bora kuliko mjini huku wazazi wao Tony na Kidawa wakisema maisha ya mjini ni bora kuliko kijijini. Ulikuwa mdahalo kati ya wenyeji dhidi ya wageni. Kila mtu alitetea upande wake kwa hoja za msingi. Ilikuwa yapata majira ya saa 5 asubuhi. Muda huo walikuwa wanawasubiri wageni pale ndani ambao ni wazazi wa Majaliwa. Wakati stori zikiendelea pale sebuleni, Ghafla mlango ukagongwa. Jasmine aliinuka kwenye sofa na kwenda mlangoni kufungua. Alipofungua tu akakutana uso kwa uso na wakwe zake. Ni Kareem na Radhia ndo waliwasili pale ndani muda ule. Jasmine aliwakaribisha ndani wageni kisha akafunga mlango. Wakati Kareem na Radhia
wanaelekea kukaa kwenye viti, Ghafla Radhia akaganda mithili ya mtu aliyepigwa na shoti ya umeme. Mbele ya macho yake alimshuhudia mwanaume ambaye anamchukia kuliko wanaume wote duniani. Mwanaume ambaye alimpaga ujauzito na kumtelekeza kwenye mataa. Hakuwa mwingine bali ni Tony. Hata Tony nae alimuona Radhia na akashtuka kwa marefu na mapana. Ilikuwa uso kwa uso kati ya Tony na Radhia.
“TONY!” Radhia alimuita Tony kwa mshangao. Tony nae akajibu;
“RADHIA!”
Majaliwa, Jasmine pamoja na Kareem walishangaa kuona wale watu wanafahamiana. Kidawa yeye alipoiona sura ya Radhia alimkumbuka vyema sana maana alimchukuliaga mpenzi enzi za ujana wao. Kareem alikuwa wa kwanza kuketi kisha Radhia nae akafuatia huku akimtazama Tony. “Wazazi wangu, Sijui niwaletee vinywaji gani?” Jasmine aliwauliza wakwe zake.
Kareem aliomba aletewe maji ya baridi, Radhia hakuhitaji kinywaji chochote maana akili yote ilishavurugika. Jasmine alimletea maji Baba mkwe wake, Kareem akapokea na kuyanywa. “Wazazi wangu, Karibu sana nyumbani. Naona leo imekuwa siku nzuri sana maana nimewakutanisha watu ambao mnafahamiana. Kwanza kabisa naomba nichukue fursa hii kutoa utambulisho kwenu ili kila mtu ajue nafasi yake kwa mwenzake.” Majaliwa alizungumza maneno hayo kisha akatulia na kuvuta pumzi kwa sekunde kadhaa kisha akaendelea kuongea;
“Wazazi wangu, (Alimtazama Kareem na Radhia) Hawa mnaowaona hapa ndo wakwe zangu mimi. Ni wazazi halisi wa mke wangu Jasmine.” Majaliwa alizungumza maneno hayo kisha akatulia kwa sekunde kadhaa. Baada ya huo utambulisho Majaliwa akawageukia wazazi wa Jasmine na kusema;
“Wakwe zangu eeh, Hawa mnaowaona mbele yenu ndo wazazi wangu mimi. (Akiwanyooshea mikono
Kareem na Radhia)”
Baada ya huo utambulisho,
Mwanamama Radhia alishusha pumzi ndefu sana kisha akasema; “Maja mwanangu! Huyo mwanaume unayemuita mkwe wako anaitwa Anthony Hyera maarufu kama Tony. Yeye ndo mwanaume aliyenipa mimba yako na kunikana kwa sababu ya huyo mwanamke. Hao wote walishirikiana kunifukuza kama mbwa wakati huo nimekubeba tumboni. Huyo mshenzi ndo Baba yako mzazi.” Radhia alizungumza maneno hayo kwa jazba kubwa sana huku akitokwa na machozi baada ya kukumbuka matukio ya miaka ya nyuma. Pale ndani ghafla hali ya hewa ikabadilika watu wakaanza kuvuta pumzi ya moto licha ya uwepo wa kiyoyozi. Vijasho vilianza kuwavuja watu huku wakiwa hawaamini kabisa masikioni yao kwa kile walichokisikia.
Majaliwa alihisi kuchanganikiwa huku Jasmine mapigo ya moyo yakimuenda kasi.
“Si….si…..sijakuele…. sijakuelewa
mama. Unamaanisha nini kusema hivyo? Kwa…. kwa…. kwahiyo…. kwahiyo….. Jasmine na mimi…. Jasmine na….na…..na…..” Majaliwa alishindwa kuendelea kuongea akajiinamia chini huku akiwa ameshika kichwa chake.
“Ba…. Ba…. Baba! Hebu zungumza kitu basi! Hiki kilichozungumzwa kina ukweli Baba? Mbona hukuwahi kuniambia kama una mtoto mwingine tofauti na mimi? Kwa….kwa…. kwahiyo…. kwahiyo
ulini….ulinidanganya kwamba mimi ndo mtoto wako wa pekee sio? Kwahiyo Maja ni kaka yangu sio? Kwahiyo siku zote nalala kitanda kimoja na kaka yangu wa damu? Kwahiyo nimebeba mimba ya kaka yangu wa damu? Hii haiwezekani Baba. Tafadhali Sema basi sio Antony wewe Baba. Ha…ha…. haiwezekani mimi na Maja tuwe kaka na Dada. Maja ni mume wangu na nampenda
sana Baba. Hii hai…hai… haiwezi kuwa kweli Ba……” Jasmine akashindwa kuendelea kuongea akaunganisha kilio cha kwikwi.
Tony alikohoa kidogo kisha
akamtazama Radhia na kumwambia; Hivi Radhia, Mimi na wewe si tulishamalizana lakini? Ile mimba si nilishakuambia sio yangu? Kwanini unaendelea kuniandama lakini? Unahisi utapata faida gani ukishawaharibia ndoa hawa vijana? “Sikiliza Tony, Kukataa kwako mimba hakuwezi kufuta mahusiano yako ya ki damu hata ungetumia maneno ya Quran au Biblia. Damu yako wewe ndo ilihusika kumtengeneza Majaliwa kwahiyo hakuna kitu kinachoweza kufuta huo uhalisia. Hata muonekano wa sura zenu zinatosha kutoa majibu bila kutumia vipimo vya DNA. Labda tu nikuulize kitu Tony, Unapata raha gani kuona watoto wako mwenyewe wanaoana wao kwa wao? Dunia ni ndogo sana Tony, Haya ni malipo ya kukataa watoto. Kama kweli Jasmine ni mwanao wa damu basi nina uhakika wa asilimia mia kwamba Jasmine na Majaliwa wana DNA zinazofanana.” Radhia aliweka nukta kisha akamgeukia Majaliwa na kumwambia;
“Majaliwa mwanangu, Huyo mkwe wangu ni dada yako wa damu na huyo mshenzi ndo Baba yenu. Mimi nimemaliza, Ngoja niwaache maana siwezi kuendelea kumtazama huyo mzee wa hovyo…… Mume wangu, Naomba tuondoke.” Radhia alizungumza maneno hayo kisha akaondoka pale ndani.
Episode 27
Kareem nae aliinuka kwenye sofa kisha akamsogelea Majaliwa na kumwambia;
“Maja! Unatakiwa kukaa chini na Jasmine kisha jadilini namna ya kulishinda hili jaribu. Hili suala linawahitaji nyie wenyewe mlimalize tena kwa kutumia ukomavu wa akili. Mimi naondoka, Kama mtanihitaji basi mtanipigia simu. Kwa sasa tulizeni kwanza akili zenu.” Kareem alizungumza maneno hayo kisha akaondoka pale ndani.
Majaliwa, Jasmine, Tony na mke wa Tony ndo walibaki pale sebuleni. Kimya kilitawala huku kila mmoja akiwa amejiinamia kivyake. Mama yake Jasmine alimsogelea mwanae kwenye sofa alipokaa lakini Jasmine akainuka na kwenda moja kwa chumbani kwake. Hakutaka kabisa kuguswa na mtu yeyote kwa wakati huo. Majaliwa aliinua macho yake na kumtazama Tony kwa jicho kali sana. Tony nae aliinua macho yake na kumtazama Majaliwa. Sura mbili zinazofanana zikawa zinatazamana. Tony ndani ya moyo wake alikiri kabisa kwamba ni kweli Majaliwa ni mwanae. Lakini pia hata Majaliwa kwenye moyo wake alikiri kabisa kwamba Tony ni Baba yake baada ya kuona wamefanana sura. Wakati Tony na Majaliwa wakitazamana, Ghafla Jasmine akatoka chumbani akiwa na mkoba wake. Jasmine alipita pale sebuleni na kutoka nje moja kwa moja bila kuzungumza na mtu. Mama yake Jasmine akatoka nje na kumfuata mwanae lakini tayari alishachelewa. Jasmine alishapanda gari la mume wake na kuondoka kabisa. Mama yake Jasmine alirudi ndani na kutoa taarifa kwamba Jasmine ameondoka na gari. Majaliwa alimtazama Mama Jasmine kisha akamtazama Tony kwa hasira. Mwanaume hakuzungumza chochote badala yake akainuka na kuelekea chumbani kwake. Tony na mkewe walibaki wakimsindikiza Majaliwa kwa macho. Majaliwa alipofika chumbani kwake akajitupa kitandani kama mzigo huku akiandamwa na msongo mzito wa mawazo. Kila alipokitazama kitanda, mashuka na mito ya kulalia ndivyo alivyozidi kuteswa na mawazo. Hakutegemea kabisa kama penzi lake na Jasmine litafikia tamati namna ile. Jasmine ni mwanamke aliyekuwa anampenda kuliko kitu chochote kwenye dunia. Ni mwanamke aliyempa dhamana ya maisha yake na kuamini wataishi wote milele.
Inakuaje tena Jasmine awe dada yake? Majaliwa alijikuta anazidi kuchanganikiwa. Stress alizokuwa nazo alihisi akiendelea kubaki pale chumbani basi anaweza kufa. Mwanaume aliamua kuondoka kabisa pale ndani na kutokomea mtaani. Kwa wakati huo hakuwa na nguvu hata ya kutaka kujua Jasmine ameelekea wapi. Pale ndani wenyeji wote waliondoka na kubaki wageni ambao ni Tony na mke wake, Kidawa. Mpaka kufikia muda huo wenyewe walishachanganikiwa maana kile kilichotokea kilikuwa na madhara makubwa sana upande wao. Lakini pia walijawa na hofu kubwa kwenye mioyo yao kwa kuwa hawakujua Binti yao ameelekea wapi na atakuwa kwenye hali gani.
****
Majira ya saa 11 jioni juu ya alama, Jasmine alirejea nyumbani na gari lile lile aliloondoka nalo mchana. Alipofika akateremka kwenye gari akiwa na mkoba wake kisha akazama ndani ya nyumba. Pale sebuleni kulikuwa na wazazi wake lakini akawapita kama hajawaona kisha akaenda moja kwa moja chumbani kwake. Mama alimfuata mwanae, aliposukuma mlango haukuweza kufunguka. Jasmine alijifungia kwa ndani ule mlango. Baada ya kufika chumbani, Jasmine alifungua mkoba wake kisha akatoa maswaki miwili pamoja karatasi fulani nyeupe. Alizishika mkononi zile karatasi na kuanza kuzisoma taratibu kabisa. Machozi ya uchungu yalitiririka kutoka kwenye mboni za macho yake na kudondokea kwenye ile karatasi. Ilikuwa karatasi ya majibu ya vipimo vya DNA kutoka hospitali. Muda ule alipotoka alienda hospitali kufanya vipimo vya DNA kupitia mswaki wa Majaliwa na wake. Majibu ya DNA yalionesha dhahiri kwamba Majaliwa na Jasmine ni watoto wa Baba mmoja. Ni majibu ambayo yalimuumiza sana moyo Jasmine baada ya kugundua yule aliyekuwa anamuita mume kumbe ni kaka yake wa damu. Jasmine hakuamini kabisa kuona penzi lake na Majaliwa ndo limefikia tamati muda ule. Zile ndoto zao za kuishi wote kama mke na mume mpaka kufa hatimaye zimefikia tamati. Ule upendo na raha zote walizokuwa wanapeana kitandani hazipaswi tena kuendelea. Sasa vipi kuhusu mtoto wao aliyekuwa tumboni kwa wakati huo? Je akishazaliwa atamuitaje Majaliwa? Baba au Mjomba? Vipi kuhusu yeye mwenyewe wamuite nani na huyo mtoto? Mama au Shangazi? Kilichokuwa kinafuata ni fedheha kubwa sana kwenye macho ya walimwengu. Kichwani kwa Jasmine kulikuwa na mvurugano wa akili ulioambatana na maumivu makali ya moyo. Hakuwahi kabisa kuwaza kama siku moja atakuja kuachana na Majaliwa. Mahusiano yao yalikuwa ya ukweli na uaminifu sana.
Walipendana kwa miaka mingi kiasi kwamba walizoeana na kuishi kama marafiki. Walipendana bila mipaka wala masharti. Kwa hakika lilikuwa pigo kubwa sana kwa wote wawili. Ukiachana na fedheha ambayo wangeipata kwenye jamii kwamba ndugu wawili wameoana na kuzaa mtoto, Kitu kingine kilichoumiza mioyo yao ni kuwa hawawezi tena kuwa kwenye mahusiano ya kimapenzi, uchumba wala ndoa.
Jasmine alivuta droo la kabati kisha akatoa peni na karatasi na kuanza kuandika ujumbe. Alitumia takribani dakika mbili kumaliza kuandika kile alichokuwa amekusudia. Baada ya hapo alichukua simu yake kisha akaanza kupekua pekua mpaka alipoifikia namba ya simu iliyoandikwa “My Life Partner.” Ni namba ya Majaliwa ndo aliisevu kwa
hilo jina lililobeba tafsiri ya “Mwenza wa maisha yangu.” Jasmine alibonyeza kwenye kitufe cha meseji kisha akaanza kuandika ujumbe aliokusudia kisha akatuma kwa Majaliwa. Baada ya hapo akazamisha mkono kwenye mkoba na kutoa vidonge visivyokuwa na idadi. Aliinuka kitandani na vile vidonge na kuisogelea meza iliyokuwa na jagi la maji pamoja na glasi. Kilichofuata sasa, huwezi kuamini asee…….
Episode 28
Upande wa pili Majaliwa alionekana mitaani akizurura bila kuwa na muelekeo maalumu. Ni mara baada ya kuondoka kule nyumbani kwake akahisi labda kelele za mitaani zingemsaidia kupunguza mawazo. Wakati anatembea tembea, Ghafla muito wa meseji ukasikika kwenye simu yake. Majaliwa alitoa simu yake mfukoni kisha akatazama kwenye skrini na kugundua kwamba ni meseji kutoka kwa Jasmine. Ilibidi sasa aifungue ile meseji kisha akaanza kuisoma taratibu;
“Maja! Nimetoka hospitali kufanya vipimo vya DNA kupitia miswaki yetu na majibu yamethibitisha kwamba mimi na wewe ni watoto wa Baba mmoja. Mimi na wewe ni ndugu wa damu Maja. Sisi hatukupaswa kuwa wapenzi na hatuwezi tena kuendelea kuwa wapenzi. Lakini Maja, Vipi sasa kuhusu hili tumbo? Vipi kuhusu huyo mtoto aliyetumboni mwangu? Unadhani akizaliwa atakuitaje wewe?
Atakuita Baba au Mjomba? Vipi upande wangu? Nitawezaje mimi kuishi bila wewe Maja? Nitawezaje mimi kukuita kaka ilihali moyo wangu una jina lako Maja? Nitawezaje mimi kufuta kumbukumbu za mapenzi yote niliyoyapata kwako? Nahisi kabisa siwezi kuacha kukupenda Maja. Kiukweli kabisa naumia mimi Maja. Moyo wangu unauma kiasi kwamba nashindwa kuhimili haya maumivu. Naomba unisamehe sana kwa uamuzi mgumu nilioamua kuuchukua. Najua ulikuwa na shauku kubwa sana ya kuja kumuona mwanao lakini hilo haliwezi kutimia Maja. Naomba usiache kuniombea dua kwa Mwenyezi Mungu ili anipunguzie adhabu ya kaburi. Hii dunia sio yangu tena Maja, Wakati unasoma ujumbe huu tambua kwamba mimi na mwanao hatupo tena dunia. Nakupenda sana Maja na nakutakia maisha mema yenye amani na furaha…. UNTIL WE MEET AGAIN….” Majaliwa alimaliza kuisoma meseji hiyo huku akitetemeka mwili mzima. Ni meseji iliyoshtua mapigo yake ya moyo kwa marefu na mapana. Pale pale akapiga namba ya Jasmine ikibidi amzuie kufanya uamuzi wa kujiua lakini kwa bahati mbaya simu
iliita ya Jasmine iliita bila
kupokelewa. Majaliwa alipiga tena na tena lakini simu iliita bila kupokelewa. Pale pale akachukua Taxi na kumwambia dereva ampeleke nyumbani kwake. Njiani Majaliwa alimtaka dereva aendeshe kwa spidi kwa kuwa kuna mtu anamuwahi yupo kwenye hatari. Dereva alijitahidi kuendesha kwa spidi kama
alivyoombwa. Majaliwa alijikuta anatetemeka kama amemwagiwa maji yenye barafu mwili mzima. Hofu kubwa ilitanda kwenye moyo wake kufuatia ile meseji ya Jasmine. Taxi lilikuwa spidi sana lakini Majaliwa aliona linajivuta kama kokoteni. Mwanaume alitamani kupaa ili awahi kufika nyumbani amuwahi Jasmine. Alipiga simu tena na tena huku akiwa na imani kwamba Jasmine atapokea simu. Upande wa pili, Jasmine alikuwa na hali mbaya sana kitandani.
Povu zito lilikuwa linamtoka mdomoni huku akiugulia maumivu ya tumbo. Ni sekunde chache tu zilibaki kwa Jasmine za kuvuta pumzi ya dunia baada ya kumeza vidonge visivyokuwa na idadi. Jasmine alichagua kujitoa sadaka na mwanae aliyetumboni ili kuepuka fedheha na aibu iliyokuwa mbele yao. Lakini pia hakuona kama anaweza kuendelea
kuishi na kuifurahia dunia bila penzi la Majaliwa. Wakati Jasmine yupo kwenye sekunde za mwisho kabisa za kuvuta pumzi ya dunia, aliendelea kusikia muito wa simu yake na alijua mpigaji ni Majaliwa. Jasmine akiwa kwenye hali mbaya alipata hamu ya kusikia sauti ya Majaliwa kwa mara ya mwisho. Mtoto wa kike akajitahidi kuinua mkono ili aweze kupokea ile simu lakini mkono ukawa mzito. Alijitahidi kwa mara nyingine na awamu hii akafanikiwa. Kwa mbali kabisa akasikia sauti ya Majaliwa ikimwambia;
“No! Jasmine usijiue! Tafadhali sana naomba usichukue huo uamuzi.
Nisubiri basi kuna kitu nataka kuja kujadili na wewe. Plizi usife Jasmine, tayari nimeshapata ufumbuzi wa sakata letu. Jasmine! Jasmine! Jasmine! Mbona kimya Jasmine! Naomba usife Jasmine! Kama ukifa mimi nitabaki na nani Jasmine? Usife tafadhali, Mimi nakupe…”
Aisee, Huwezi kuamini Jasmine hakumaliza kusikia Majaliwa akimwambia anampenda kwani tayari roho yake ilishaachia mwili. Upande wa pili Majaliwa aliganda na simu sikioni baada ya sauti ya kukoroma ya Jasmine kutosikika tena. Majaliwa alijua tayari ameshachelewa, Jasmine ameshafariki. Taxi lilimfikisha mpaka nyumbani kwake, akalipa pesa kisha akateremka na kukimbia mkuku mkuku mpaka ndani. Alipofika ndani aliwakuta wazazi wa Jasmine wapo kwenye mlango wa chumba wanamgongea Jasmine afungue. Majaliwa hakutaka kuuliza badala yake akapiga teke mlango lakini haukufunguka. Akapiga tena kwa nguvu kama mara tatu na ndipo mlango ukafunguka baada ya kitasa kujiachia. Baada ya kufanikiwa kuvunja mlango, Majaliwa pamoja na wazazi wa Jasmine wote wakazama ndani ya chumba. Kile walichokiona mbele yao kiliwanyong’onyeza mioyo. Kila mmoja alishuhudia mwili wa Jasmine ukiwa kitandani huku akiwa na mspovu mdomoni. Majaliwa akiwa kama Daktari alimgusa Jasmine zile sehemu zenye fahamu lakini akagundua kwamba tayari Jasmine ameshafariki dunia. Majaliwa alilia sana asee! Mama yake Jasmine nae alilia sana huku akiwa amemkwida shati mume wake na kumwambia kwamba yeye ndo amesababisha.
Pale kitandani kulikuwa na pakiti zilizokuwa na vidonge alivyomeza Jasmine. Lakini pia kulikuwa na karatasi ya majibu ya DNA pamoja na miswaki. Majaliwa alielewa kila kitu kuhusu ile miswaki maana mmoja ilikuwa wake na mwingine ni wa Jasmine. Aliishika ile karatasi ya majibu kisha akaisoma. Alipomaliza kuisoma aliweza kupata uhakika kwamba ni kweli wao ni ndugu. Ni kweli kabisa Baba yake mzazi ni Tony. Lakini pia kulikuwa na karatasi yenye ujumbe mfupi alioacha marehemu.
Majaliwa aliichukua ile karatasi kisha akaisoma huku akiwa na maumivu makubwa moyoni. Ni ujumbe fulani ambao ulikuwa unawahusu wazazi wa Jasmine. Majaliwa alimpatia Tony ile karatasi, Tony akaipokea kisha akaanza kuisoma;
“Wazazi wangu, Mtanisamehe sana kwa uamuzi niliochukua. Najua nimewaacha kwenye wakati mgumu lakini imebidi iwe hivyo ili niepukane na hii fedheha. Nataka kuwaambia kitu kimoja tu wazazi wangu, Nyie ndo chanzo cha haya matatizo yote yaliyotokea. Mimi nimekufa kwa sababu yako wewe Baba. Laiti kama ungempa malezi kaka Majaliwa basi haya yote yasingetokea kwani tungekuwa tumeshajuana hivyo tusingeweza kuwa wapenzi. Nawatakia maisha mema wazazi wangu na msiache kuniombea mtoto wenu.” Hayo ndo maneno yaliyoandikwa kwenye ile barua. Barua hiyo ilimtoa machozi Tony na kumfanya ajutie makosa yake ya siku za nyuma.
Kifo ni kama kugusa, mtu unacheka nae dakika ya kwanza, dakika ya pili anavuta. Hatimaye Jasmine alifariki akiwa na mwanae tumboni. Kwa hakika lilikuwa pigo kubwa sana kwa Tony na Kidawa ambao walimpoteza mtoto wao wa pekee kwenye ndoa yao. Ni mtoto ambaye walikuwa wanamtegemea kwa kila kitu kwenye maisha yao. Jasmine ndo alibebaga jukumu zima la kuwatunza wazazi wake maana Baba hakuwa na uwezo tena wa kutafuta pesa kutokana na matatizo yake ya miguu. Kifo cha Jasmine kilibeba pigo zito sana kwenye maisha ya wazazi wake. Mwili wa Jasmine ulisafirishwa nyumbani kwao Songea kwa ajili ya mazishi. Gharama zote za usafiri na mazishi kwa ujumla zilikuwa chini ya Majaliwa. Majaliwa, Kareem na
Radhia walikuwa miongoni mwa watu waliosafiri kutoka Dar es salaam kwenda Songea kushiriki mazishi. Baada ya kuondoka kwenye ardhi ya nyumbani kwao kwa miaka zaidi ya 22, Hatimaye Radhia alirejea tena nyumbani kwao. Aliondoka akiwa maskini na hatimaye alirejea akiwa na utajiri. Kila mwanakijiji aliyekuwa anafahamu historia yake alibaki mdomo wazi baada ya kujua Radhia ametoboa kimaisha na sasa mwanae ni Daktari. Ni yule yule mwanae ambaye alikataliwa na mwanakijiji mwenzao ama rafiki yao Tony. Wengi walisubiri kuona picha linalofuata kati ya Tony na mwanae aliyemkataaga hapo awali. Lakini pia gumzo kubwa lililotawala kwenye mazishi ni kuhusu chanzo cha kifo chake Jasmine.
Dunia haina siri kila kitu kilikuwa wazi kwa wanakijiji na watu wakajikuta wanapata fundisho kupitia Tony. Takribani siku mbili zilitosha kutamatisha suala zima la mazishi. Kila kitu kilipita salama huku marehemu akiwa tayari amehifadhiwa ndani ya nyumba yake ya milele. Baada ya mazishi kutamatika, Watu walikuwa huru kurejea majumbani mwao. Kwa upande wa Majaliwa, Kareem na Radhia nao hawakuwa na jambo lingine la kusubiri hivyo walijiandaa kwa ajili ya kurudi mjini. Walipaki kila kitu kinachowahusu kwenye gari dogo walilosafiri nalo kisha wakawaaga juu juu wafiwa ambao ni Tony na mkewe Kidawa. Kareem na mke wake, Radhia walipanda kwenye siti za nyuma kisha Majaliwa akazunguka upande wa pili ili akakamatie usukani wa gari. Mwanaume alifungua mlango wa gari, Ile anataka kuingia tu akavutwa shati. Majaliwa aligeuza shingo na kutazama nyuma akakutana uso kwa uso na mtu mzima Tony. Pale pale Tony akaenda chini na kupiga magoti licha ya kuwa na tatizo la miguu. Majaliwa aliganda kwa ajili ya kumsikiliza mzee anataka kuongea nini. Tony alianza kudondosha machozi ya kiutuuzima huku akisema;
“Mwanangu, Unaondokaje na kuniacha bila kuzungumza chochote na mimi? Mimi ndo Baba yako mzazi na wewe ndo mwanangu wa pekee uliyebakia kwenye hii dunia. Naomba unisamehe sana kwa yote yaliyotokea hapo awali. Ni akili za ujana tu ndo zilinifanya nikukane licha ya kujua kwamba wewe ni mwanangu. Naomba usiniache nikiteseka mwanangu maana kwa sasa sina uwezo tena wa kufanya kazi. Dada yako Jasmine ndo alikuwa msaada pekee kwenye maisha yangu ila ndo hivyo tena ameshaondoka. Nisamehe sana mwanangu, Mimi ndo Baba yako kwahiyo nipe basi heshima na thamani yangu kwa kukuleta duniani.” Tony alizungumza maneno hayo na kumfanya Majaliwa adondoshe kwa uchungu.
Majaliwa alimtazama Tony kisha akamwambia;
“Sikiliza Mzee, Ile juzi nilikusikia kwa
masikio yangu ukimkumbusha mama yangu kwamba ulishamalizana nae kipindi ana mimba. Binafsi sina haja ya kukushukuru kwa kunizaa kwa sababu ulifanya kwa starehe zako ndo maana ulimtaka mama yangu atoe mimba yangu na alipokataa ukaamua kumtelekeza. Ngoja nikuambie kitu mzee, Baba sio yule anayezalisha na kutelekeza, Baba ni yule anayehudumia mtoto mpaka anakua. Hii ni saa 4:25 asubuhi natamka rasmi kwamba wewe sio Baba yangu na sijawahi kabisa kutamani kuijua sura yako inafananaje. Baba yangu mimi anaitwa Kareem, Yeye ndo alinilea mpaka nimekua. Mtoto ni kama maua ya bustanini, Ili ufurahie hewa safi kutoka kwenye maua hayo basi ni lazima uyamwagilie na kuyatunza baada ya kuyapanda. Kuyapanda pekee pasipo kuyamwagilia na kuyatunza hayawezi kustawi na kukupatia hewa safi. Mtoto ni hadhina kubwa sana kwa maisha yako ya baadae kwa sababu nguvu uliyonayo leo haiwezi kudumu milele. Kuna muda utafika utashindwa kabisa kuwa na nguvu ya kutafuta hivyo mwanao anaweza kukupambania kama ulivyompambania yeye alipokuwa mdogo. Fainali ni uzeeni, Nakutakia kila la kheri katika maisha yako mzee.” Majaliwa alimaliza kuzungumza kisha akazama ndani ya gari, akawasha, akafunga vioo na taratibu kabisa gari likaanza kuondoka.
Tony alibaki akilisindikiza kwa macho lile gari huku akitokwa na machozi ya uchungu. Roho ilimuuma sana kuona mwanae anaondoka huku akiwa amemkana hadharani kabisa. Tony akapiga ngumi ardhini kwa nguvu huku akilia uchungu sana. Mmoja kati ya watu waliokuwa wanatazama lile tukio alisikika akisema;
“DAH! AMA KWELI USELA NA UJANA UNA MWISHO JAMANI.
TUHAKIKISHE TUNAWATUNZA NA
KUWALEA WATOTO WETU MAANA
FAINALI NI UZEENI. HIZI NGUVU
TULIZONAZO LEO HATUWEZI KUWA
NAZO KESHO. NGUVU ZINAISHA ILA
MIPAMBANO HAIISHI MPAKA
TUNAPOINGIA KABURINI.”
𝑴𝑾𝑰𝑺𝑯𝑶 𝑲𝑨𝑩𝑰𝑺𝑨 𝑾𝑨 𝑹𝑰𝑾𝑨𝒀𝑨 𝒀𝑬𝑻𝑼