𝐍𝐈𝐋𝐈𝐌𝐓𝐄𝐒𝐀 𝐌𝐓𝐎𝐓𝐎 𝐖𝐀 𝐊𝐀𝐌𝐁𝐎 𝐁𝐈𝐋𝐀 𝐊𝐔𝐉𝐔𝐀 𝐍𝐈 𝐌𝐖𝐀𝐍𝐀𝐍𝐆𝐔 𝐍𝐈𝐋𝐈𝐘𝐄𝐌𝐓𝐔𝐏𝐀𝐆𝐀 𝐌𝐒𝐈𝐓𝐔𝐍𝐈 𝐊𝐈𝐏𝐈𝐍𝐃𝐈 𝐂𝐇𝐀 𝐍𝐘𝐔𝐌𝐀
Episode 16
[NYUMBANI KWA KAREEM]
Stori zilinoga sana kati ya Radhia na rafiki Landina. Siku hiyo Radhia alitembelewa na Landina nyumbani kwake maana ilishakuwa desturi kwa marafiki hao kutembeleana na kupiga stori mbalimbali. Radhia ambaye kwa wakati huo alikuwa anatambulika kama Mama Fetty alimchagua Landina kuwa mshauri wake katika maisha. Mpaka kufikia muda huo Landina yeye alikuwa anafanya kazi kwenye saluni moja ya kike na alikuwa anaishi kwenye chumba cha kupanga. Bado hakuwa na mume ila alikuwa na mpenzi.
“Kama nilivyokuambia sasa shoga yangu, Jitahidi kumshawishi shemeji awe anaandika jina la Fetty linaandikwa kwenye mali anazomiliki vinginevyo mwanao wa kambo ndo atapewa kipaumbele kwa sababu ndo mtoto wa kwanza wa shemeji alafu ni wa kiume.
“Mmh! Mume wangu hawezi kuandika jina la mtoto yeyote kwenye mali zake na hata ikitokea akaandika basi ataandika jina la Majaliwa maana anampenda sana kuliko Fetty. Ila nikuambie tu shoga yangu, Kila kitu hapa ndani kitabaki mikononi mwa wanangu maana nataka kumshushia Kareem watoto wa kutosha. Huyo Maja ataondoka hapa mikono mitupu wala hanisumbui kabisa na ananiogopa kama Simba.
“Na unavyomkanda kweli asikuogope jamani. Ila punguza kumtesa mtoto wa watu maana siku mume wako akijua italeta shida kwenye ndoa yako.
“Aah, Wapi! Baba Fetty hawezi kujua maana Maja mwenyewe nimempa mkwara mzito sana.
“Mmh! We kiboko shoga yangu. Lakini hata mimi nisingeweza kuishi na mtoto wa kambo kama mwanangu. Naamini hata nikiolewa sitoweza kuishi na mtoto wa mwanamke mwenzangu. Alafu naomba kujua shoga yangu, Hivi mumeo anawasiliana na mama yake Maja? “Aah, Wapi! Tangu walipombwagia mtoto miaka hiyo mpaka leo hawajawasiliana kabisa. Mwanamke mwenyewe hajulikani kama yupo hai au amekufa.
“Mmmh! Ni hatari kwa kweli. Yani mimi siwezi kufanya huo upumbavu wa kumwacha mwanangu mchanga kwa Baba yake hata kama nimegombana nae. Nitaondoka na mwanangu na kwenda kuishi nae mbali. Alafu nimekumbuka kitu, Hivi shemeji anajua kwamba ulishawahi kuzaa mtoto akafariki?
“Mmh! Hajui kwa kweli na sijawahi kumwambia kama nilishawahi kuzaa hapo awali. Yeye anajua Fetty ndo uzao wangu wa kwanza kumbe mwenzake nilishazaaga huko kiji….” Kabla hajamaliza kuongea mlango ukasukumwa na kufunguka. Bwana mdogo Majaliwa alionekana akiingia pale ndani akiwa na sare za shule pamoja na begi lake la daftari mgongoni.
“Wow! Naona umerudi mapema leo.
Safi sana nilikuwa nakusubiri kwa hamu sana wewe mtoto. Leo si umeondoka asubuhi bila kufanya usafi wala kuosha vyombo? Sasa kama kawaida adhabu yako leo hauli chakula wala kitu chochote hapa ndani. Hebu kwanza sogea hapa wewe mshenzi.” Radhia alimwambia Majaliwa maneno hayo.
Majaliwa alipiga hatua bila wasiwasi na kumfuata Radhia. Radhia alishangaa sana kuona Majaliwa anatembea kwa kujiamini sana tofauti na siku zote maana alikuwa akimuita basi anaenda kwa hofu na woga. Majaliwa alimfikia Radhia ambaye ni mama yake wa kambo.
“Naona leo unatembea kwa kujiamini sana wewe mtoto. Kwahiyo ushaanza kuota mapembe mbele yangu sio? Unatamba huniogopi eeh? Au umenisahau eti? Naongea na wee…..” Kofi zito likatua kwenye shavu la Majaliwa kutoka kwenye mkono wa Radhia.
Radhia akainua tena mkono ili amuongeze kofi lingine Majaliwa lakini ghafla akasikia sauti ikisema “Inatosha! Acha inatoshaa!” Ni sauti iliyosikika ikitokea kwenye dirisha la nyumba. Sauti hiyo Ilikuwa ya Baba mwenye nyumba Kareem. Mlango ulifunguliwa kisha akaonekana Kareem akiingia ndani. Radhia alibaki na hamaki na taharuki kubwa sana moyoni. Akili ilipata kiwewe na kuhisi kuchanganikiwa maana tayari alishajua siri yake ya kumtesa makali imefichuka. Kareem alipiga hatua mpaka pale alipokuwa mke wake kisha akasimama mbele yake. Radhia akaanza kutetemeka maana sura ya mumewe tayari ilishachafuka. Kareem alimtazama Radhia kisha akamtazama Majaliwa aliyekuwa amejishika shavu huku machozi yakimtoka. Alichokifanya Kareem ni kumshika mkono mwanae kisha akaenda kukaa nae kwenye sofa la pembeni. Landina yeye alijua yajayo hayafurahishi hivyo akaona akae mbali na ugomvi wa familia isiyomuhusu. Ilibidi sasa aage juu juu na kuondoka pale ndani. Nyumba ikibaki na wahusika wenyewe ambao ni Baba, Mama na mtoto ambaye ni Majaliwa. Muda huo mtoto wa mwisho ambaye ni Fetty alikuwa shuleni. Radhia alimtazama mume wake Kareem kwa kuvizia wakati huo Kareem amemtumbulia macho Radhia.
“Mama Fetty mke wangu, Unajua sikuwahi kufikiri kama una roho mbaya kiasi hiko. Hivi huyu mtoto amekukosea nini mpaka unampitisha kwenye chungu cha moto? Kitu gani kimekusukuma mpaka umuone huyu mtoto kama adui yako? Yaani mpaka chakula ninachotafuta kwa jasho langu bado unamnyima mwanangu? Inawezekana vipi mwanangu aishi kama mtumwa? Bado ukaona haitoshi ukaamua kuharibu ndoto za huyu mtoto kwenye elimu. Unataka aje kuwa nani hapo? Nisikilize Mama Fetty, tena nisikilize kwa umakini. Kabla sijakuoa nilikuambia nina mtoto ambaye anakuhitaji wewe kama mama yake. Nilikuambia kabisa kama utakubali kuolewa na mimi basi uwe tayari kuwa mama wa familia, mama wa wanangu wote tutakaowazaa na huyu mmoja ambaye tayari amezaliwa. Sikukulazimisha kukuoa bali ulikubali kwa hiari yako mwenyewe. Ulikiri mwenyewe kwamba utamlea Majaliwa wangu kama mwanao wa kumzaa. Je haya ndo malezi mke wangu? Mbona Fetty humpigi kama ngoma? Mbona humfanyishi kazi za ndani kama punda? Mbona humzuii kwenda shule? Kwahiyo uliposema nisikuletee dada wa kazi ulikuwa unamtegemea Majaliwa sio? Dah! Hii imeniuma sana mke wangu. Imeniuma kuliko kawaida.” Kareem alizungumza maneno hayo kwa uchungu sana kisha akajiinamia chini.
Radhia aliinuka kwenye sofa alipokaa kisha akapiga magoti na kuanza kumfuta Kareem pale alipokuwa. Alipomfikia akamwambia, “Nisamehe sana mume wangu.
Nimekosa mimi sitorudia tena.”
Radhia aliongea kwa unyenyekevu. “Radhia, Kufanya kosa si kosa bali kosa ni kurudia kosa. Hili nisamehe lakini naomba lisijirudie tena hapa ndani. Tayari nimeshajua kwamba huna moyo na macho ya kumtazama Majaliwa kama mwanao kwa kuwa hujamzaa hivyo sikulazimishi kumpenda. Sikulazimishi kumpenda Maja lakini naomba usimtese wala kumzuia kupata haki zake za msingi. Endapo ukirudia kumfanyia Maja hayo uliyomfanyia mwanzo basi huo ndo utakuwa mwisho wako wa kuishi hapa ndani kama mke wangu. Nakupiga talaka tatu bila kupepesa macho.” Kareem aliongea maneno hayo kisha akainuka na kuelekea chumbani.
Baada ya kufika chumbani alijilaza kitandani huku miguu ikining’inia chini. Kichwani alikuwa na mawazo mengi sana mwanaume kuhusiana na lile tukio lililokuwa linaendelea ndani ya nyumba yake. Suala la mwanae kunyanyaswa na mke wake ndani ya nyumba yake lilimuumiza sana mpaka korodani za uzazi. Lakini pia kuna jambo alikumbuka wakati ule Radhia na Landina wanazungumza pale ndani huku yeye akiwa dirishani anasikiliza mazungumzo; “Alafu nimekumbuka kitu, Hivi shemeji anajua kwamba ulishawahi kuzaa mtoto akafariki?
“Mmh! Hajui kwa kweli na sijawahi kumwambia kama nilishawahi kuzaa hapo awali. Yeye anajua Fetty ndo uzao wangu wa kwanza kumbe mwenzake nilishazaaga huko kiji….”
Baada ya kukumbuka maneno hayo, Kareem akajua kumbe mke wake alishawahi kuzaa mtoto ingawa hakuwahi kumwambia kabisa. Lakini alijiuliza swali, Inawezekana vipi awe aliashazaa wakati stori aliyoipata ni kwamba alikimbiaga kijijini baada ya kulazimishwa kuolewa? Kuna hisia tofauti kidogo zilimjia mwanaume lakini hakutaka kujipa muda wa kulifikiria hilo. Kwa wakati ule akili yake ilikuwa kutafuta tiba juu ya hatima ya mwanae Majaliwa. Muda ule ule Radhia akaingia chumbani kwa mwendo wa woga na wasiwasi. Akakaa kitandani na kuanza kumpasa papasa mume wake kifuani huku akimwambia,
“Nisamehe sana mume wangu,
nakuahidi hili halitojirudia tena. Nakiri kosa langu na kuanzia leo nitampenda Majaliwa. Naomba usifikirie kabisa kuniacha kumbuka tayari tumeshazaa mtoto na anahitaji malezi yetu mimi na wewe.
“Sikiliza Mama Fetty, Kwanza kabisa nimeshakusamehe. Pili, sio lazima umpende Maja ama sikulazimishi kumpenda Maja lakini naomba usimtese wala kumnyanyasa. Tatu, wiki hii namleta msichana wa kazi hapa ndani atakuwa anakusaidia kazi za ndani kwahiyo muache huru Maja asome na kucheza na watoto wenzake. Alafu kwanini hukuwahi kuniambia kama ulishawahi kuwa na mtoto?”
Radhia alijikuta anaweweseka baada ya kusikia swali linalohusu mtoto wake wa kwanza kabisa kumzaa. Aliganda kwa muda huku akitafakari jibu la swali maana tayari alishajua Kareem alisikiliza maongezi yake na Landina.
Episode 17
Radhia alitafakari kwa sekunde kadhaa kisha akapata jibu la kumpa mume wake juu ya swali alilomuuliza. “Nisamehe sana mume wangu kwa kushindwa kukuambia kuhusu hilo. Ila ukweli ni kwamba sipendi kuzungumza maisha yangu ya nyuma kwa sitaki kukumbuka maisha niliyopitia. Niliteseka sana na maisha mpaka nikapata mimba na mwanangu akafariki akiwa mchanga. Sitaki kabisa kukumbuka yale maisha kwa sababu yananiumiza moyo kila nikikumbuka.” Radhia alijitetea kwa namna hiyo.
Kareem hakutaka kutengeneza mdahalo juu ya lile suala hivyo akaamua kufunga mjadala huku akiwa tayari ameshajua kwamba mke wake alishawahi kuwa na mtoto ila akafariki. Tangu siku hiyo mambo yakabadilika pale ndani. Majaliwa akaanza kupata haki zake za msingi kama mtoto katika familia. Alikula, alilala, alipata uhuru wa kucheza pamoja na kwenda shule kama watoto wengine. Lakini hayo yote hayakubadilisha moyo wa Radhia juu ya upendo wake kwa Majaliwa. Bado Radhia hakuwa na upendo kwa mwanae wa kambo lakini hakumtesa wala kumzuia kupata haki zake za msingi. Hata Majaliwa mwenyewe hakuwa na mapenzi kabisa na mama yake wa kambo. Kareem alifanikiwa kumpata msichana wa kumsaidia mke wake kazi za ndani ili kukata kabisa mzizi wa fitina. Hilo lilikwisha kwa namna hiyo. Majaliwa akaanza upya kunawiri kimwili na kiakili. Kule shuleni maendeleo yake kinidhamu na kitaaluma yakawa mazuri. Miezi michache baadae, Yeye (Majaliwa) pamoja na wanafunzi wenzake wa darasa la saba wakaingia katika chumba cha mtihani wa kumalizia elimu ya msingi. Hilo likapita salama
na hata matokeo ya mtihani yalipotoka, Majaliwa alikuwa miongoni mwa wanafunzi waliofaulu na kufanikiwa kuchaguliwa kujiunga na elimu ya sekondari. Kwa hakika ilikuwa habari njema sana kwa Majaliwa baada ya kuona ndoto zake za kwenda sekondari zimetimia. Lakini pia hata Baba yake, Kareem alifurahi sana kuona mwanae amepiga hatua moja mbele katika safari yake ya masomo. Siku zote Kareem alikuwa anataka mwanae asome mpaka kufikia elimu ya juu kabisa (Chuo kikuu). Kareem aliamini kabisa hata ikitokea akafariki basi elimu pekee itaweza kusimama kwenye nafasi yake yeye kama mzazi na kumwongoza mwanae Majaliwa. Majaliwa alichaguliwa kujiunga na shule ya sekondari ya bweni hivyo ikawa bahati sana kwake kwenda kuishi mbali na mama yake mlezi. Kareem alimfanyia mwanae maandalizi ya kutosha yaliyogharimu kiasi kikubwa cha pesa. Aliweka sawa kila kitu ili kuhakikisha mwanae anaenda kusoma bila kupata changamoto zozote za kiuchumi. Alimnunulia mwanae kila kitu kinachohotajika, akalipa michango yote ya shule na kumpa pesa ya matumizi isiyokuwa na kipengele. Kwa upande wa Radhia yeye hakufurahishwa kabisa na lile suala ndani ya moyo wake. Aliumia sana kuona Majaliwa anatumia pesa za familia wakati huo yeye hatokuja kunufaika na elimu ya Majaliwa. Radhia alijua kabisa kama Majaliwa atafanikiwa kielimu basi atakayekuja kunufaika ni mama yake mzazi ambaye kwa sasa yupo mafichoni. Alichoamini yeye ni kwamba Fetty ndo mtoto anayeweza kumnufaisha kupitia elimu yake. Muda huo Fetty ndo kwanza alikuwa anatarajia kuingia darasa la kwanza.
****
Hatimaye Majaliwa alifanikiwa kuripoti shuleni akiwa na sare za mwanafunzi wa kidato cha kwanza. Kwa miaka minne ya masomo,
Majaliwa alitakiwa kuishi bwenini pamoja na wanafunzi wenzake. Ni rasmi sasa Majaliwa akafanikiwa kutoka mikononi mwa mama wa kambo ambaye hakuonesha kabisa kufurahia uwepo wake katika uso wa dunia. Majaliwa alifurahia sana maisha mapya ya bwenini ambayo yalimpa uhuru wa kupambania ndoto zake. Hiko ndo kipindi ambacho Majaliwa alijifunza mambo mengi sana kuhusu maisha kwa kuwa aliishi na watu kutoka familia tofauti tofauti. Akiwa huko shuleni alizingatia sana matakwa ya Baba yake juu ya kusoma kwa bidii na kufaulu mitihani. Bwana mdogo alisoma kwa bidii sana na kujikuta anakuwa miongoni mwa wanafunzi wanaofaulu mitihani kwa alama za juu kabisa. Bidii yake katika kujisomea ikamfanya awe na akili nyingi sana darasani hivyo akajikuta anapendwa na walimu. Aliishi kule bwenini katika muda mihula yote ya masomo na akawa anarudi nyumbani kwao kipindi cha likizo ndefu. Kipindi hiko cha likizo bado alikutana na changamoto kutoka kwa mama yake wa kambo ila awamu hii hazikumfanya akose amani. Tayari akili yake ilishaanza kukua na kutambua kwamba hakuna binadamu anayependwa na watu wote. Kwanza kwanini alazimishe kupendwa na Mama wa kambo wakati hata Mama yake mzazi tu hampendi ndo maana alimuacha akiwa mchanga na kutokomea uarabuni. Dogo alishajiwekea msimamo kwamba sio lazima apendwe na kila mtu, akipendwa na Baba yake tu inatosha. Zile chuki za mama yake mlezi dhidi yake hazikumfanya awe mnyonge, Muhimu alichokitazama yeye ni kupata haki zake za msingi tu kama mtoto wa ile familia. Siku, wiki, miezi na miaka ikakatika. Hatimaye Majaliwa alimaliza kidato cha nne na kufaulu vizuri mtihani hivyo akachaguliwa kuingia kidato cha tano na sita. Huko nako aliendeleza bidii katika masomo maana alibakisha hatua chache sana za kufikia ndoto yake ya kwenda chuo kikuu. Miaka miwili ya kidato cha tano na sita ni kama vile kulala leo na kuamka kesho, Hatimaye Majaliwa alifunga rasmi ukurasa wa masomo ya sekondari. Alifunga ukurasa kwa ufaulu wa kishindo hivyo ndoto yake ya kwenda chuo kikuu ikatimia. Alipata nafasi ya kujiunga na chuo kikuu cha Dar es salaam kusomea shahada ya utabibu. Ndoto yake kubwa ilikuwa ni kuwa daktari wa binadamu. Mpaka kufikia muda huo tayari umri ulisogea hivyo Majaliwa hakuwa tena mtoto bali alikuwa kijana mtu mzima mwenye uwezo wa kujisimamia na kujiongoza mwenyewe. Hata Kareem na Radhia nao umri wao ulisogea kidogo na tayari walishaongeza mtoto mwingine wa kike. Sasa familia ikawa na jumla ya watoto watatu. Licha ya Majaliwa kuchukiwa na mama yake mlezi lakini yeye hakuwachukia ndugu zake. Aliwatazama kama ndugu zake kwa kuwa ni damu ya Baba yake. Suala la Majaliwa kuwa na akili nyingi za darasani lilimfanya Radhia aone wivu na kuongeza chuki kwa kuwa mwanae Fetty hakuwa na akili kabisa darasani. Suala hilo lilimfanya Kareem ampende sana Majaliwa kuliko Fetty. Wakati Majaliwa anasubiri muda wa kuripoti chuo ufike akawa anashinda kwenye biashara za Baba yake. Kareem alikuwa anamuamini mwanae Majaliwa kiasi kwamba alikuwa anamuacha kwenye biashara zake na kila kitu kikawa kinaenda sawa. Hiko kitendo kilikuwa kinamuumiza sana kichwa Radhia maana alikuwa anaona kila dalili ya Majaliwa kuwa mrithi na msimamizi wa mali za Baba yake. Wakati Radhia anamuwazia Majaliwa kwenye mali za urithi, Majaliwa yeye hakuwa na wazo lolote kuhusu mali za Baba. Kijana alikuwa anawaza kutafuta mali zake mwenyewe kupitia elimu. Majaliwa alifanikiwa kuripoti chuoni na kuanza rasmi mwaka wa kwanza wa masomo. Alibukua kitabu mwaka wa kwanza akamaliza, akabukua tena, mwaka wa pili nao akamaliza, akabukua tena, mwaka wa tatu nao akamaliza. Mwaka wa nne ambao ndo wa mwisho kabisa katika kozi yake ndo ulibakia mbele yake. Kabla ya kuanza masomo ya mwaka huo wa mwisho, Majaliwa alirudi likizo nyumbani kwao. Likizo hiyo iliambata na tukio zito sana lililoibuka pale nyumbani kwao.
Ni tukio gani hilo? Twende pamoja tutafahamu…
Episode 18
[NYUMBANI KWA KAREEM]
Ilikuwa yapata majira ya saa 4 asubuhi, ukimya ulitawala sana ndani ya nyumba huku sauti ndogo ya vyombo ikisikika kutokea jikoni.
Jemima ambaye ni msichana wa kazi ndo alikuwa jikoni akiendelea na majukumu yake ya kusafisha vyombo. Muda huo huo Majaliwa alikuwa sebuleni amejilaza kwenye sofa huku akichezea simu janja yake. Muda huo akili ya Majaliwa ilikuwa inawaza chuo tu kwani likizo ilikuwa ukingoni kuisha na zilibaki siku chache tu kabla ya kwenda kuanza mwaka wa mwisho wa masomo. Ndani ya chumba kimoja cha kulala, Radhia alionekana akizunguka zunguka peke yake pale chumbani huku akitafakari kitu. Ni wazi kabisa alikuwa na msongo mzito wa mawazo ndo maana alikuwa anaenda mbele na nyuma, kulia na kushoto huku akiwa na karatasi fulani mkononi.
“Majaliwa! Majaliwa! Majaliwa! Hivi inawezekana vipi jina lako ndo liandikwe kwenye hii karatasi?
Kwanini wewe wakati hujazaliwa peke yako? Hii haiwezekani kabisa.!” Ni maneno ambayo Radhia alijisemea kwa sauti ya chini chini huku akijipiga piga na karatasi kichwani. Haikuwa karatasi ya daftari ama kitabu bali ni hati miliki ya ile nyumba ya Kareem. Huwezi kuamini kumbe Kareem alishaandikaga siku nyingi sana jina la Majaliwa kwenye hati miliki ya nyumba yake. Miaka yote ambayo Radhia aliishi pale ndani kama mke hakuwahi kabisa kuiona hati miliki ya ile nyumba wala hakuwahi kujua kama hati miliki ina jina la Majaliwa. Siku hiyo Radhia aliamua kupekua kwenye droo siri la mume kisha akazitafuta nyaraka za mali zote za Kareem ili ajue kilichoandikwa. Kwa hakika siku hiyo Radhia alichanganikiwa sana baada ya kujijenga tafsiri ya kwamba wanae aliowazaa hawana chao kwenye ile nyumba ya Baba yao. Muda ule ule Radhia akakurupuka na kutoka chumbani kwake kwa spidi. Alifika sebuleni na kumkuta Majaliwa lakini hakuongea nae chochote badala yake akampita kama kivuli na kuelekea nje ya nyumba. Baada ya kufika nje ya nyumba akachukua taxi na kumpa maelekezo ampeleke sehemu fulani. Majaliwa hakumjadili kabisa mama yake hivyo akaendelea na mambo yake. Muda huo Kareem alikuwa kwenye biashara zake. Ile safari ya Radhia ilifikia ukomo kwenye chumba anachoishi Landina. Hakutumia dakika nyingi kufika kwa sababu hakukuwa na umbali kutoka nyumbani kwake.
“Mmh! Shoga yangu, Mbona ghafla sana na simu yako imenishtua kweli.
Kuna amani kweli huko utokako?” Landina alimuuliza Radhia mara baada ya kuwasili.
“Mmh! Shoga huko nyumbani mambo sio mambo. Kumbe jina la Majaliwa ndo limeandikwa kwenye hati ya nyumba shoga yangu.
“Wee! Usiniambie! Kwahiyo mume wako ndo kafanya hivyo?
“Yeah! Sasa nani mwingine afanye hivyo wakati yeye ndo mwenye nyumba?
“Mmh! Hiyo mbaya! Hapo tayari kashatengeneza mazingira ya kuwanyima haki ya urithi watoto wengine. Hapo tayari inaonesha kwamba Majaliwa ndo mmiliki wa nyumba nyie wengine ni wapangaji. “Hebu nishauri basi shoga yangu nifanye nini?
“Dah! Unajua Radhia tangu siku nyingi nilishakuambia fanya juu chini mwambie shemeji akufungulie biashara yako mwenyewe kubwa ili umiliki mali zako binafsi. Hiyo ingekusaidia kwa sababu ukimtegemea mtu anaweza kufa alafu ukabaki mtupu.
“Tatizo sio mimi Landina. Ni mume wangu mwenyewe ndo hapendi nikafanye kazi au biashara. Yeye anataka niwe mama wa nyumbani tu.
“Aah! Hiyo mbayaa!
“Ndo hiyo sasa, Hebu nishauri basi nifanye nini kuhusu hili suala la
Majaliwa kuandikwa kama mmiliki wa nyumba.
“Okay! Hapo kwanza unatakiwa kujua kwamba hakuna namna ya kuweza kubadili hilo jina kwenye hiyo hati. Hapa njia ni moja tu, unatakiwa kuchukua uamuzi mgumu ili wanao wapate haki yao.
“Uamuzi mgumu? Kama upi sasa?
“Subiri kidogo…” Landina akainuka na kulisogelea begi lake. Baada ya kulifikia akalifungua kisha akatoa kikaratasi kidogo kilichokunjiwa kitu ndani yake.
“Hebu shika hii..” (Alimpatia Radhia kile kikaratasi) Radhia alipokea kisha akamuuliza Landina; “Hii nini sasa shoga yangu?
“Hebu fungua kwanza.
Radhia alifungua kile kikaratasi na kukuta unga fulani wenye rangi ya shaba. Alishangaa kidogo maana hakujua ni kitu gani amepatiwa.
“Hii nini sasa shoga yangu?
“Hiyo ni sumu inayoua taratibu kabisa ndani ya masaa sita. Hiyo sumu inamuua mtu huku akiwa amelala. “Kwahiyo unamaanisha nimuue Maja sio?
“Hilo ni jibu Radhia, Hebu uliza swali.
“Mmh! Huu mtihani mzito kwangu Landina. Kumuua mtu sio kitu chepesi ujue. Hiyo roho mimi naitoa wapi jamani? Kiukweli yule mtoto simpendi ila sio kwa kiwango cha kukatisha maisha yake.
“Hebu acha utoto shoga yangu. Hii ndo njia pekee ya kuwatafutia haki watoto wako na wewe mwenyewe ubaki na mali. Kama Majaliwa atakufa basi mali zote za Kareem zitakuwa halali ya watoto wako.
“Dah! Ni kweli lakini hapa inabidi tu nifanye maamuzi magumu kwa ajili ya wanangu. Siwezi kukubali wanangu waje kuishi maisha magumu kama niliyoishi mimi mama yao. Hakuna namna, Majaliwa lazima afe tu.
“Safi sana! Hayo ndo maamuzi sasa.
Mimi nafanya hivi kwa ajili ya kukusaidia wewe shoga wangu. Sisi tumekuja mjini kutafuta maisha na najua kabisa ukipata wewe basi nimepata mimi..”
Aisee, Hatimaye mambo yalishakuwa makubwa! Chuki ya Radhia kwa
Majaliwa ilishafikia kwenye kilele cha mwisho kabisa cha uadui. Suala lilikuwa moja tu kichwani kwa Radhia, Kuhakikisha Majaliwa anakufa.
Episode 19
Ndani ya chumba cha Radhia na Kareem, hali ya hewa ilikuwa shwari sana kutokana na uwepo wa kiyoyozi kilichomwaga ubaridi. Licha ya ubaridi uliokuwepo lakini bado jasho lilitiririka kwenye mwili wa Radhia aliyekaa kitandani huku akiitazama meza iliyokuwa mbele yake. Pale juu ya meza kulikuwa na hati miliki ya nyumba huku kwa pembeni kukiwa na kikaratasi chenye sumu ya kuua binadamu baada ya masaa sita. Macho ya Radhia yalikuwa kwenye ile karatasi yenye sumu huku akili yake ikitafakari kwa kina juu ya maamuzi anayotaka kuyachukua. Radhia alikumbuka namna Majaliwa anavyowapenda ndugu zake na hata ndugu zake wanavyompenda kaka yao. Mara nyinyi Majaliwa alikuwa anatumia muda wake kumfundisha Fetty mada mbalimbali za darasani huku akimsisitiza kusoma kwa bidii.
Lakini pia muda mchache uliopita, Radhia aliporudi pale nyumbani akitokea kwa Landina alimkuta Majaliwa anacheza na mdogo wake wa mwisho huku akimchekesha na mtoto alikuwa anafurahi sana. Ni yule mtoto wa mwisho wa Radhia na Kareem ambaye alikuwa na miaka takribani minne mpaka kufikia muda huo. Ni upendo mkubwa sana ambao Majaliwa aliuonesha kwa ndugu zake licha ya kwamba hakuzaliwa nao na mama mmoja. Majaliwa aliwapenda sana ndugu zake kwa kuwa walizaliwa na Baba yake na siku zote Baba yake alikuwa anamsisitiza sana Majaliwa awapende ndugu zake hata kama mama yao anamchukia yeye. Kadri Radhia alivyokuwa anakumbuka upendo wa Majaliwa kwa ndugu zake ambaye ni wanae yeye, akajikuta anapata wakati mgumu wa kufanya uamuzi wa kumwaga damu. Nafsi ilikuwa inamsuta lakini akili ikawa inamwambia anatakiwa kufanya vile kwa faida ya watoto wake hapo baadae. Kama ikitokea Kareem anakufa basi nyumba itakuwa ya Majaliwa na hapo lazima mama yake mzazi atajitokeza na atakuja kuishi nae pale ndani huku wao wakifukuzwa. Hizo ndo zilikuwa akili
za Radhia, Akili zisizokuwa na akili kuwaza kumuua mtoto ambaye hawazi chochote kuhusu urithi. Mtoto ambaye anapambania ndoto zake kwenye masomo ili amiliki mali zake mwenyewe. Hitimisho lililopatikana kichwani kwa Radhia ni kwamba, “MAJALIWA MUST DIE” Yaani
Majaliwa lazima afe. Muda ule ule Radhia akaichukua ile hati miliki ya nyumba kisha akafungua droo na kuirudisha pale pale alipoiweka mume wake. Aliweka kwa umakini mkubwa ili mume wake asije kujua kama alipekua nyaraka zake. Baada ya kumaliza kuweka akafunga droo lakini kabla hajazamisha mpaka mwisho akasita kidogo. Ni kama vile kuna kitu alikiona kwa chini kabisa ya lile droo. Ni kitu ambacho kilimshtua kidogo hivyo akataka kukitazama kwa mara nyingine tena kwa umakini zaidi. Alifungua tena droo kisha akaingiza mkono na kutoa kile kitu. Kilikuwa kipande bangili chakavu yenye rangi ya shaba. Radhia alikitazama kipande kile huku mikono yake ikitetemeka kama jenereta. Ni kama vile alikuwa anaifahamu ile bangili. Pale pale akainuka haraka haraka na kwenda kwenye kabati lake nguo. Alipolifika kabati akaanza kuchambua nguo kama mwendawazimu huku
akionekana kutafuta kitu. Alipekua na kupekua akafika chini kabisa. Huko alikutana na kitambaa fulani kilichofungwa. Alikichukua kitambaa hiko kisha akakifungua na kukutana na kipande kingine cha Bangili. Kile kipande kilikuwa kinafanana rangi na kile alichokikuta kwenye droo la vitu vya mume wake. Alivichukua vile vipande kisha akaviunganisha pamoja na vilionekana kufiti pamoja na kuunda Bangili iliyokamilika. Ni wazi kabisa vile vipande ndo viliundaga ile bangili ila vilitenganishwaga kwa kuvunjwa.
“Hapana! Haiwezekani! Haiwezekani kabisa nasema. Hii imefikaje hapa?” Radhia alijisemea maneno hayo baada ya kuitambua vyema ile bangili.
Aliikumbuka ni Bangili ya bahati aliyopewaga na marehemu Bibi yake miaka mingi iliyopita. Bangili hiyo alikuwa anaivaaga kwenye mkono wake wa kulia na mara ya mwisho kuivaa ilikuwa siku ambayo alimtelekeza mwanae na kwenda mjini kutafuta maisha. Hiyo siku aliamua kuivunja vipande viwili ile Bangili kisha kipande kimoja akamuachia mwanae pale msituni na kingine akaondoka nacho mwenyewe. Radhia aliamini kabisa kwa kuwa ile bangili ni ya Bahati basi itamsaidia mwanae kupata msaada na kwenda kulelewa kwenye maisha mazuri. Kile kipande kimoja alikichukua kwa ajili ya msaada wake mwenyewe maana alikuwa hajui aendako. Baada ya kukumbuka hivyo Radhia alihisi kuchanganikiwa. Akarudi tena kwenye droo la mume wake baada ya kukumbuka kuna kitu kingine alikiona ingawa mwanzo hakukitafakari. Alipofika kwenye droo akachuchumaa chini kisha akatoa bahasha zote za kaki zilizokuwa ndani ya lile droo. Chini kabisa akakuta sweta pamoja na kipande cha khanga. Radhia alikunjua lile sweta pamoja na kile kipande cha khanga akajikuta anashtuka kwa mara nyingine. Ni miaka mingi sana ilipita lakini aliweza kukumbuka vyema zile nguo. Kile kipande cha khanga ndo
alimvalishaga mwanae Bahati kama nepi siku ya mwisho kabisa alipomtelekeza msituni. Alikumbuka vyema enzi hizo hakuwaga na pesa ya kumnunulia mwanae nepi hivyo alichanaga khanga zake vipande vipande na kutumia kama nepi. Lakini pia lile sweta lilikuwa la kwake kabisa na mara ya mwisho alitumia kumfunikia mwanae pale msituni baada ya kuhisi khanga pekee haitoshi kumkinga na baridi lililokuwepo kwenye yale mazingira. Mpaka kufikia muda huo Radhia akajikuta anachanganikiwa kuliko kawaida. Maswali mengi yakaanza kugonga kwenye kichwa chake kufuatia kile alichokuwa anakiona. Radhia alihisi kabisa kwa namna yoyote ile Kareem alimuokota mwanae Bahati kule msituni. Na kama alimuokota, Je yupo wapi sasa huyo Bahati? Radhia akaanza kurudisha kumbukumbu zake nyuma kuanzia siku ya kwanza kabisa alipokutana na Kareem na kuanza kuishi nae kama mke na mume. Alimkuta Kareem akiwa na mtoto wa miaka tano. Mtoto ambaye inasadikika hakunyonya kabisa maziwa ya mama yake baada ya mama kumbwaga mtoto kwa Baba mtoto (Kareem) kisha akatokomea uarabuni. Cha ajabu ni kwamba Kareem alikuwa haongeleagi kabisa kuhusu mama mzazi wa yule mtoto. Lakini pia huyo mama wa mtoto ameshindwa kumtafuta mwanae au kumjulia tu hali tangu alipomuacha akiwa mchanga mpaka kufikia umri wa utu uzima. Inamaana huyo mama bado hajarudi huko uarabuni? Au amefariki? Au hapajui wapi anapoishi mzazi mwenzake na mwanae? Au hamtaki tu mwanae aliyemzaa mwenyewe kwa uchungu?
Inawezekana vipi? Hayo maswali ndo yalikuwa kichwani kwa Radhia kwa wakati huo. Huyo mtoto mwenyewe ndo Majaliwa. Kwani Majaliwa ni nani? Mbona kama ndo yule Bahati wangu? Radhia alijikuta anaitupa kwanza ile sumu huku akitetemeka mwili mzima baada ya kuhisi anayetaka kumuua ni mwanae aliyemuweka tumboni kwa miezi tisa na kumzaa kwa uchungu.
Episode 20
Radhia alitoka haraka chumbani na breki yake ikawa sebuleni. Pale sebuleni alimkuta msichana wake wa kazi akiwa na mwanae. “Jemima! Maja yupo chumbani kwake?” Radhia alimuuliza msichana wake wa kazi kwa jazba.
“Hapana dada, Maja katoka sasa hivi.
“Ameenda wapi?
“Wala hajaniambia anakwenda wapi ila alinifuata jikoni akaniachia huyu mtoto na kuniambia anatoka mara moja.
“Hebu mpigie kwanza simu.” Jemima alivuta simu yake na kumpigia Majaliwa. Kwa bahati mbaya simu iliita bila kupokelewa. Alipiga takribani mara tatu lakini simu haikupokelewa. Kitendo cha Majaliwa kushindwa kupokea simu kilimvuruga sana Radhia akiwa kama mzazi. Kwa mara ya kwanza kabisa alijikuta anapata wasiwasi kuhusu Majaliwa. Radhia alijiangushia kwenye sofa kwa kishindo huku akiwa na msongo wa mawazo. Muda huo alianza kuitafakari kwa umakini zaidi sura ya Majaliwa na kujikuta anaiona taswira ya Tony. Alikumbuka siku ya kwanza Landina kumuona Majaliwa alimfananisha sura na Tony. Hapo sasa Radhia akazidi kupata picha halisi kwamba Majaliwa ndo yule mwanae aliyemtelekeza msituni takribani miaka kumi na nane iliyopita. Pale sebuleni Radhia alishindwa kukaa, akainuka na kwenda chumbani kwake. Alipofika akavuta simu yake na kumpigia mume wake Kareem. Kwa bahati nzuri simu ya Kareem iliita na kupokelewa. Radhia alimtaka Kareem asichelewe kurudi nyumbani siku hiyo. Kareem alishangaa sana maana haikuwa kawaida kupigiwa simu na kuambiwa asichelewe kurudi nyumbani.
****
Majira ya saa 1 usiku, Majaliwa alirudi nyumbani kwao tangu ule mchana
alipotoka. Alipofika tu ndani ya nyumba akashangaa kuona anakimbiliwa na mama yake wa kambo kisha akakumbatiwa kwa hisia kali za mapenzi.
“Nakupenda sana mwanangu…
Naomba unisamehe sana Babaa. Nakupenda sanaaa…” Radhia alizungumza maneno hayo huku akizidi kumkumbatia Majaliwa. Majaliwa akabaki na mshangao maana hata siku moja hakuwahi kuambiwa yale maneno wala kukumbatiwa na mama yake wa kambo. Akawa ameganda huku
alijiuliza kipi kimetokea au kuna njama gani inataka kufanywa na mama yake dhidi yake. Wakati wakiwa kwenye kumbatio, Baba mwenye nyumba nae ndo akawa anawasili muda ule. Mlio wa gari ukamfanya Radhia amuachie Majaliwa na kwenda chumbani. Ni kama vile alikuwa akimsubiri kwa hamu sana mume wake siku hiyo. Majaliwa nae akaenda chumbani kwake huku akiendelea kutafakari kile alichofanyiwa na mama yake muda ule. Kareem aliteremka kwenye gari kisha akazama ndani ya nyumba. Pale sebuleni hakumkuta mtu yeyote hivyo akaongoza moja kwa moja mpaka chumbani kwake. Alipofika tu alimuona mkewe akiwa amekaa kitandani huku akiwa hana kabisa sura ya tabasamu tofauti na siku zote. Kareem alishangaa sana na alipotupa macho mezani
akajikuta anashtuka kwa marefu na mapana kwa kile alichokiona. Aliona kipande cha Bangili, Khanga pamoja na sweta. Ni vitu ambavyo alivihifadhi kwa siri kwa miaka mingi sana. “Mume wangu! Naomba uniambie hivi vitu umevitoa wapi?” Radhia alimuuliza Kareem kabla hata ya salamu.
“Kwahiyo ndo salamu hiyo mke wangu?” Kareem alimjibu Radhia huku akilege
“Samahani! Shikamoo mume wangu…. Vipi huko utokako?” Kareem hakujibu chochote badala yake akasogelea meza kisha akavitazama vile vitu alivyoulizwa. “Kwahiyo mke wangu hivi vitu ndo vimekufanya unipigie simu na kunitaka nirudi nyumbani mapema? Hivi ni vitu muhimu sana kwa Maja ndo maana niliviweka kwenye lile droo. Nimevitunza kama kwa miaka mingi sana kwa sababu vina siri nzito. Muda ukifika nitavitumia kama vielelezo kufikisha ujumbe kwa mwanangu Maja. Hivi ni vitu muhimu sana mke wangu kwahiyo nakuomba usivitoe tena kwenye droo tafadhali.” Pale pale Kareem alimshuhudia mke wake akilegea mwili na kupiga magoti chini huku akitokwa na machozi kama mtoto.
“Mu… mu…. mume wangu! Mimi hapa…. Mimi hapa … ndo…. ndo Mama…. Mama mzazi wa Majaliwa. Mimi ndo nilimtelekeza Majaliwa msituni na wewe ukaja kumuokota. Majaliwa ni mwanangu mimi Kareem.” Radhia alizungumza maneno hayo huku akiendelea kutiririkwa na machozi.
Maneno ya Radhia yalimshtua
Kareem kwa marefu na mapana.
Mwanaume hakuamini masikio yake kwa kile alichokisikia kutoka kwenye kinywa cha mke wake. Eti yeye ndo mama mzazi wa Majaliwa? Kivipi? Alimzaa lini? Lakini amejuaje kama Majaliwa aliokotwa msituni? Hapo ndipo Kareem alipotokwa na jasho licha ya kiyoyozi kumwaga baridi. “Kareem mume wangu! Hebu shika hiki kipande bangili kisha jaribu kuunganisha na hiko kipande ulichokuwa nacho wewe.” Aliongea huku akimkabidhi Kareem kipande cha Bangili.
Kareem alipokea kipande cha Bangili kutoka kwa Radhia huku akiyaona ya Firauni baada ya kustaajabu ya Mussa. Alipounganisha vile vipande vikafiti vizuri sana na kutengeneza bangili halisi.
“Huo ndo uhalisia wa hiyo Bangili mume wangu. Ni Bangili niliyopewa na marehemu Bibi yangu kama zawadi. Bibi alinipatia na kuniambia hiyo ni Bangili ya bahati hivyo niitunze vizuri na niweze kuishi nayo katika siku zote za maisha yangu. Ile siku niliyotengana na mwanangu ndo siku
ambayo niliigawanya hiyo Bangili na kumwachia mwanangu kipande kimoja na mimi nikaondoka na kipande changu. Nilikuwa na imani kwamba kipande nilichokiacha kwa mwanangu kingeweza kumsaidia kwa kuwa nilishawekeza imani yangu kwamba ni Bangili ya bahati. Lakini pia bado nakumbuka hiko kipande cha khanga ndo nilikitumia kama Nepi kumvalisha mwanangu. Maisha yangu yalikuwa magumu sana, sikuwa na uwezo wa kumnunulia mwanangu Nepi za dukani hivyo nilichana Khanga zangu na kumvalisha mwanangu. Na kuhusu hilo sweta nilimfunikia mwanangu mara ya mwisho ili kumkinga na baridi kali pale msituni. Hilo sweta ni langu, kwenye zile picha za zamani nilizowahi kukuonesha nilishapigia ila naamini hukuzingatiaga tu. Kareem mume wangu, Yule Maja ni mwanangu mimi. Kiukweli kabisa roho inaniuma mimi, Kumbe Maja ni mwanaa…..ngu.” Radhia aliongea huku akizidi kulia na awamu hii akawa anatoa na sauti kabisa.
Aisee! Kareem alihisi koo lake limekauka hivyo akamimina maji kwenye glasi kisha akachamba koo.
INAENDELEA…………………..