𝐍𝐈𝐋𝐈𝐌𝐓𝐄𝐒𝐀 𝐌𝐓𝐎𝐓𝐎 𝐖𝐀 𝐊𝐀𝐌𝐁𝐎 𝐁𝐈𝐋𝐀 𝐊𝐔𝐉𝐔𝐀 𝐍𝐈 𝐌𝐖𝐀𝐍𝐀𝐍𝐆𝐔 𝐍𝐈𝐋𝐈𝐘𝐄𝐌𝐓𝐔𝐏𝐀𝐆𝐀 𝐌𝐒𝐈𝐓𝐔𝐍𝐈 𝐊𝐈𝐏𝐈𝐍𝐃𝐈 𝐂𝐇𝐀 𝐍𝐘𝐔𝐌𝐀
Episode 05
Radhia alifika kwenye barabara kuu ya magari kisha akasimama na begi lake la mgongoni. Muda huo machozi yalikuwa yanamtiririka kutokana na
kitendo cha ukatili alichokifanya kwa
mwanae wa damu. Magari mbalimbali yakawa yanampita pale barabarani huku macho yake yakiwa makini kuangazia mabasi yaendayo Dar es salaam. Hazikupita dakika nyingi akafanikiwa kusimamisha Basi, baada ya kusimamisha akapanda kisha dereva akang’oa gari. Kama utani vile Radhia alimtelekeza mwanae kwenye kichaka kisha akapanda gari kuelekea mjini. Baada ya kukaa kwenye siti, konda akamfuata na kumdai nauli. Radhia alifungua zipu ya begi lake kisha akatoa pesa na kumkabidhi konda. Pesa yote aliyokuwa nayo iliishia kwenye tiketi maana yake hakubakiwa na hata senti tano ya kununua maji ya kunywa. Mbaya zaidi alikuwa anaenda kwenye mji ambao hakuwa na ndugu wala rafiki. Hakujua hata ni wapi anapoenda kufikia na hiyo ndo ilikuwa mara yake ya kwanza kabisa kwenda Dar es salaam. Kiufupi safari yake ilikuwa ya mawazo
ukijumlisha tukio la kimtelekeza mwanae mchanga ndo kabisa akawa anaandamwa na majonzi.
Radhia akajikuta analia kwa sauti ya chini kila alipokumbuka amemuacha mtoto wake katika kichaka bila msaada wowote. Hakujua ni muda gani angepata msaada wa kuokotwa na kama msaada ungechelewa maana yake mtoto huyo angeweza kufa kwa njaa. Kwa hakika nafsi yake ikiwa inamsuta sana na kujilaumu kwa kitendo ambacho amekifanya.
Wakati anaendelea kulia kuna mwanaume mmoja aliyekaa siti moja na Radhia alikuwa anashuhudia kile kilio. Jamaa alitambua kwamba kuna kitu hakipo sawa kwa abiria mwenzake hivyo ikabidi amuongeleshe ili ajue ni kipi kinamsibu.
“Vipi Sista, Shida nini mbona unalia tangu umekaa kwenye hii siti?” Jamaa alimuuliza Radhia swali hilo. Radhia aliposikia lile swali ikabidi afute machozi kisha akamtazama yule jamaa.
“Kaka, Ni changamoto tu za maisha.”
Radhia alimjibu jamaa “Duuh! pole sana Sista ila
changamoto ni kwa kila mtu hata sisi unaotuona humu wote tunapitia hizo changamoto. Huna haja ya kulia kwa sababu changamoto tumeumbiwa sisi wanadamu. Hakuna mwanadamu asiyepitia changamoto katika maisha yake. Lakini pia ili uweze kufanikiwa basi ni lazima ukutane na changamoto. Siku zote mafanikio yapo ndani ya uzio wa changamoto.” “Sawa kaka nashukuru kwa maneno yako ya faraja. Nashukuru sana kaka yangu.
“Okay! Usijali dada yangu. Vipi lakini umepatwa na msiba au?
“Hapana sio msiba, Ni maisha tu. “Okay! Pole sana, Naomba uniambie kipi kimekusibu ili nijue jinsi ya kukusaidia.
“Ni stori ndefu sana kaka yangu sijui hata wapi nianzie kukuelezea. “Anzia popote pale mimi nitakuelewa. “Sawa nitakueleza kwa kifupi tu maana stori ni ndefu sana kaka yangu. Mimi naitwa Radhia Juma. Ni mtoto wa pekee katika familia ya Baba na mama yangu. Nilipoteza wazazi wangu wote wawili nikiwa na miaka 10 tu. Tangu hapo nikawa nalelewa na Baba mdogo. Kila rangi ya maumivu na mateso niliweza kuiona chini ya malezi ya Baba mdogo. Licha ya kufaulu vizuri mtihani wa darasa la 7 lakini Baba mdogo aligoma kunisomesha. Nimelelewa na kukulia kwenye mazingira ya mateso na manyanyaso ambayo Binadamu wa kawaida hayamstahili. Yote tisa, Kumi ni kwamba Baba mdogo alichukua pesa kwa mzee mmoja pale kijijini ili mimi niolewe naye. Ni mzee mwenye umri mkubwa kuliko hata Baba yangu mzazi. Huyo mzee tayari ana wake wawili na watoto wakubwa walionizidi umri. Maandalizi yote ya ndoa tayari yalishakamilika ili niweze kuolewa na kuwa mke wa tatu wa huyo mzee. Ukweli ni kwamba mimi sikuwa tayari kuolewa nae hivi unavyoniona
nimetoroka huko kijijini.”
Jamaa alimtazama Radhia kwa jicho la huruma sana kufuatia ule mkasa. Ukweli ni kwamba yote mkasa aliozungumza Radhia haukuwa na ukweli wowote ila aliamua kudanganya ili apate msaada kwa urahisi. Alijua kabisa kama ataongea ukweli kwamba amemtupa mtoto basi asingepata msaada kutoka kwa mtu yeyote. Radhia hakuwahi kuishi na Baba yake mdogo ila aliishi na Bibi yake baada ya wazazi wake kufariki. Lakini pia kilichomkimbiza kijijini sio kuchaguliwa mume bali ni ugumu wa maisha. Yule jamaa alijikuta anaguswa sana na mkasa wa uongo kutoka kwa Radhia.
“Dah! Pole sana mdogo wangu. Kumbe hayo mambo ya kutafutiwa mume bado yapo hapa nchini?
Kwahiyo sasa hivi unaelekea wapi?
“Naenda Dar es salaam.
“Kuna ndugu zako wengine wanaishi huko sio?
“Hapana! Sina ndugu yoyote anayeishi Dar es salaam.
“Sasa unaenda kwa nani?
“Sina mwenyeji yoyote, Mimi naenda tu kama mkimbizi.
“Na vipi umeshawahi kufika Dar es salaam au hii ndo mara yako ya kwanza?
“Sijawahi kufika, Hii ndo mara yangu ya kwanza.
“Kwahiyo unafikia Gesti au unaenda kupanga chumba?
“Ha….. Ha… Hapana! Hapa nilipo sina hata senti tano ya kununua maji. “Duh! Hii ni hatari sana mdogo wangu maana unapoenda utakutana na magumu zaidi ya huko ulipotoka.
Lakini kwanini usingekimbilia kwa ndugu zako wengine wa huko huko kijijini?
“Kaka! Mimi sina ndugu mwingine kwenye hii dunia zaidi ya Baba mdogo tu. Huo ndo uhalisia wa maisha yangu.
“Dah! Pole sana lakini huku Dar es salaam unapoenda sio rahisi kama unavyofikiria ukizingatia kila kitu
kinahitaji pesa. Ili ule na ulale basi lazima utumie pesa. Kama huna pesa basi unaweza kula jalalani na kulala vichochoroni mwisho wa siku ukabakwa na wahuni. Labda tu nikuulize swali moja, Ni kazi gani unaweza kuifanya ili nione namna gani naweza kukusaidia.
“Kaka! Mimi nipo tayari kufanya kazi yoyote ile kaka yangu. Iwe kuuza duka, kusaidia Maman’tilie au kazi za ndani. Naomba unisaidie kaka yangu maana naona kiza kinene sana mbele yangu.”
Jamaa alijikuta anapata hisia za kumsaidia Radhia. Aliwaza kwa sekunde kadhaa kisha akamwambia
Radhia;
“Sasa mdogo wangu, Nafikiri imekuwa bahati sana kwako kukutana na mimi kwa sababu mke wangu amekuwa anahitaji mdada wa kumsaidia kazi za nyumbani. Kuanzia sasa hutakiwi kulia tena kwa sababu msaada umepata. Mimi ndo mwenyeji wako, utaenda kuishi nyumbani kwangu kama mfanyakazi na nitakulipa mshahara.
“Nashukuru sana kaka yangu kwa msaada wako. Sijui niseme kitu gani ili kuonesha shukrani zangu kwako. “Usijali kwa hilo mdogo wangu, Wa kushukuriwa ni Mungu pekee maana yeye ndo amenipa nguvu na moyo wa kukusaidia. Lakini pia yeye ndo ametukutanisha kwenye hili gari na hii siti. Kuwa na amani kabisa Radhia, Mimi naitwa Vonso.”
Episode 07
Safari iliendelea kusonga mbele mpaka wakafika kwenye kituo ambacho magari husimama ili abiria wajipatie chakula na kujisaidia haja zao. Gari lilisimama kisha konda akawatangazia abiria wake kuwa watakuwa na dakika kumi tu za kwenda kujisaidia na kununua chakula. Abiria walishuka kutoka kwenye gari akiwemo Radhia pamoja na Vonso. Baadhi walienda vyooni kujisaidia na wengine wakaenda kununua vyakula. Radhia yeye alielekea chooni kisha akarudi kwenye gari bila kununua chakula. Ukweli ni kwamba hakuwa na pesa yoyote ya kununua hata andazi. Baada ya dakika kumi kumalizika abiria wote walikuwa tayari wamesharudi ndani ya gari wakiwa na vyakula vyao kwa ajili ya kuendelea na safari. Vonso alifungua mfuko wa chakula alichonunua kisha akampatia Radhia pleti moja na yeye akabaki na pleti moja. Ni pleti zenye chipsi mayai na soda ndo zilikuwa mikono mwa Vonso na Radhia. Radhia alimshukuru sana Vonso kwa kumnunulia chakula vinginevyo safari ingekuwa ndefu sana kwake. Safari iliendelea kusonga mbele huku Vonso akimpigisha Radhia stori za hapa na pale kuhusu maisha ya Dar es salaam wanakoenda. Vonso yeye alikuwa mkazi wa Dar es salaam ila alisafiri tu kikazi na siku ile ndo alikuwa anarejea nyumbani kwake. Mnamo majira ya saa 11 jioni juu ya alama Basi likawasili katika stendi kubwa ya mabasi ndani ya jiji la Dar es salaam. Abiria wote wakateremka kwenye Basi kwa ajili ya kuanza safari mpya kuelekea kwenye makazi yao. Ilikuwa mara ya kwanza kabisa kwa Radhia kukanyaga ndani ya ardhi ya Dar es salaam. Ardhi yenye rangi zote za starehe katika nchi ya Tanzania.
Vonso akiwa sambamba na Radhia wakaenda sehemu zinakopaki bajaji kisha wakapanda na kuanza safari nyingine. Ni safari fupi ya kuelekea mahali anakoishi Vonso. Dakika takribani 15 zilitosha kuwafikisha nyumbani Vonso na Radhia. Vonso alikuwa na nyumba yenye ukubwa wa wastani tu. Ni nyumba yenye muonekano mzuri sana kuanzia nje mpaka ndani. Lakini pia alikuwa anaishi na mke wake ndani ya nyumba hiyo huku wakiwa wamebarikiwa mtoto mmoja wa kike mwenye umri wa miaka minne. Kwa wastani umri wa Vonso ni miaka 35. Alikuwa mwajiriwa kwenye kampuni fulani inayojihusisha na masuala ya ujenzi. Baada ya Vonso na Radhia kufika, Vonso akabisha hodi mlangoni na hazikupita sekunde nyingi mlango ukafunguliwa.
“Ohooo! Mume tena! Jamani anaona umeamua kunisapraizi tena kama kawaida yako.” Hiyo ilikuwa ni sauti ya mke wa Vonso mara baada ya kufungua mlango na kukutana uso kwa uso na mume wake.
Mke wa Vonso alishangaa kidogo baada ya kumuona Radhia lakini hakuwa na wasiwasi na mume wake hivyo akawakaribisha ndani huku akiwapokea mabegi.
Walifika sebuleni kisha wakaketi kwenye sofa. Mke Vonso alisogelea friji kisha akatoa jagi la maji pamoja na glasi mbili. Alimimina maji kwenye glasi zote mbili kisha akampatia moja mume wake na nyingine akampatia Radhia. Baada ya kusambaza maji nae akaketi kwenye sofa alilokaa mume wangu wake. “Eenhe, Niambie mume wangu, Habari za huko utokako?
“Habari ni safi tu mke wangu, Vipi za hapa nyumbani?
“Hapa nyumbani ni nzuri ingawa sio sana.
“Vipi kuna tatizo lolote?
“Yeah! Nilikumiss sana mume wangu.
“Hahahah! Hilo tu?
“Eeh, Hilo tu mume wangu.
“Sawa, Hata mimi niliwamiss pia wewe na mwanangu. Kwanza yupo wapi huyo mwanangu?
“Kashalala tayari.
“Mmh! Ammy wa kulala muda huu kweli? Au anaumwa?
“Wala haumwi naona michezo yake imemchosha sana leo.
“Okay! Sasa mke wangu, nadhani umestaajabu kidogo kuona huu ugeni hapa nyumbani. Huyu anaitwa Radhia,
Ni mzaliwa na mkazi wa huko Songea. Mengi kuhusu huyu Binti nitakuambia baadae tukiwa chumbani lakini kwa kifupi ni kwamba huyu Binti ataishi hapa nyumbani kwa ajili ya kutusaidia kazi. Nakumbuka kila siku ulikuwa unanidai mdada wa kukusaidia kazi za hapa ndani kwahiyo leo nimemaliza deni lako. Sasa ni ruksa kwenda kwenye biashara zako, Radhia atakuwa hapa nyumbani akimlea Ammy.
“Wow! Yani mume wangu katika siku ambazo umejua kunifurahisha basi ni leo. Radhia! Karibu sana mdogo wangu na ujisikie kama upo nyumbani. Sina mashaka yoyote juu yako kwa sababu namwamini sana mume wangu. Hapa ndani utaishi na sisi kama familia ila kikubwa tu utimize majukumu yako. Karibu sana na ujisikie upo nyumbani.
“Nashukuru sana dada kwa mapokezi yako ya upendo kwangu. Nawaahidi nitawajibika vyema kwenye majukumu yangu kwa moyo mmoja. Nawaahidi nitakuwa mwaminifu na mchapakazi siku zote. Lakini pia nawaahidi nitaishi kwa upendo na mtoto wenu kama mwanangu wa kumzaa.” Radhia alizungumza maneno hayo kwa upole na unyenyekevu huku neno la mwisho likimuadhibu nafsi.
Nafsi ilimuuma kwa kuwa mwanae wa kumzaa alishamtelekeza msituni hivyo alijiona mama mbaya sana. Laiti kama angekuwa na upendo na mwanae basi asingeweza kumtupa kisa ugumu wa maisha badala yake angekubali kufa nae kwenye hayo hayo maisha magumu.
Hatimaye Radhia akapokelewa vizuri kwenye nyumba ya Vonso. Alikabidhiwa chumba chake cha kuishi pale ndani. Usiku ulipofika walikula chakula kama familia na hapo ndipo Vonso akamtambulisha Radhia kwa mwanae kama Aunty. Ammy ambaye ni mtoto wa Vonso akawa anamtambua Radhia kama Aunty yaani Shangazi. Muda wa kulala ulipofika, Kila mtu akaenda kupumzika chumbani kwake. Usiku ule Vonso alimsimulia mke wake stori nzima kuhusu Radhia mpaka kufikia muda ule. Mke wa Vonso alijikuta anamuhurumia Radhia baada ya kusimuliwa mkasa iliomsibu huko kijijini kwao. Mkasa wa Radhia ndo ukazidi kumpa mke wa Vonso msukumo wa kuishi na Radhia pale ndani. Siku iliyofuata Radhia akaanza rasmi majukumu yake ya kazi. Tayari alishaoneshwa mazingira atakayokuwa anafanya usafi pamoja na mipaka yake. Hivyo ndivyo mambo yalivyokuwa kwa mwanadada Radhia baada ya kufika ndani ya jiji la Dar es salaam. Nuru mpya iliangaza kwenye maisha yake kwa kuwa alikuwa na uhakika wa kula, kulala na kupata pesa. Lakini sasa, licha ya nuru kumuangazia lakini bado hakuwa na furaha kabisa. Nafsi yake ilikuwa na mgogoro mzito ambao ulimtesa kwa kipindi kirefu sana juu ya mwanae. Kichwani alijiuliza maswali mengi sana juu ya mwanae aliyemtelekeza. Je bado yupo hai au amekufa? Kama yupo hai, Je atalelewa kwenye maisha ya kifahari au ya dhiki? Vipi atapendwa au atanyanyasika? Hayo ni baadhi ya maswali aliyojiuliza Radhia na kumfanya akose majibu. Tumbo la uzazi lilimuuma, nafsi ikamsuta na kumfanya ajilaumu kwa kuchukua ule uamuzi. Alihisi kabisa hata kama angemchukua mwanae basi asingekosa msaada kutoka kwa Vonso na mkewe maana walionekana kuwa na mioyo safi. Radhia alijikuta anaumia kuliko kawaida licha ya kupata afueni ya maisha. Ile amani ya moyo ilitoweka kabisa katika nafsi yake.
Episode 08
Taratibu kabisa siku zilisonga na miezi ikawa inakatika huku Radhia akiendelea kufanya kazi kwa Vonso. Kwa kiasi kikubwa furaha ilirejea upya kwa Radhia na kujikuta anasahau kama alishawahi kuzaa na kumtelekeza mtoto. Aliishi kwenye familia ya Mr Vonso kwa upendo na amani na kuonekana kama ndugu na sio mfanyakazi. Kadri siku zilivyozidi kwenda ndivyo Radhia alivyozidi kubadilika kimuonekano. Ule uzuri na shepu lake lililopotea vyote vikarejea na kumfanya awe mzuri maradufu.
Aliridhika na maisha, mwili ukajijenga na ukanawiri ipaswavyo. Kwa muonekano wa macho Radhia alionekana kama yeye ndo mama mwenye nyumba sio mfanyakazi. Utii, heshima, upendo na bidii ya kazi ndo vilimfanya Radhia apendwe na watu wote pale ndani. Hata yule mtoto wa Mr Vonso, Ammy akawa anampenda Radhia kuliko hata wazazi wake. Alihama kabisa chumbani kwa wazazi wake na kuanza kulala na Aunty yake Radhia. Ule upendo wa yule mtoto kwa Radhia kuna muda ulikuwa unamtonesha kidonda Radhia kwa kumfanya amkumbuke mwanae
aliyemtelekeza msituni. Hilo lilimuumiza sana lakini hakuwa na namna maana kama ni maji basi tayari yalishamwagika. Aliendelea kuishi na kufanya kazi kwa Mr Vonso huku akiendelea kupokea mshahara wake kila mwisho wa mwezi. Hivyo ndivyo mambo yalivyokuwa ndani ya nyumba ya Mr Vonso.
****
[BAADA YA MIAKA MITANO]
Ilikuwa yapata majira ya saa nane mchana. Siku hiyo Mr Vonso hakwenda kazini kwa kuwa ilikuwa siku ya weekend. Akiwa ameketi sebuleni mlango uligongwa, Alinyanyuka pale kwenye kiti alipokuwa amekaa na kwenda mlangoni kufungua.
“Oooh! Kareem! Aisee, karibu sana nyumbani rafiki yangu. Naona umeamua kunisapraizi leo.” Vonso alizungumza maneno hayo baada ya kukutana uso kwa uso na mgeni aliyefika nyumbani kwake. Ni rafiki yake anayeitwa Kareem na walikuwa na muda mrefu sana bila kuonana. Kwanza kabisa walikumbatia kwa furaha kisha wakaachiana baada ya sekunde kadhaa. Vonso
akamkaribisha Kareem kwenye sofa na yeye akaketi pembeni yake. “Dah! Ndugu yangu, Kitambo sana hatujaonana. Hivi ni miaka mingapi sasa imepita tangu tulipoonana mara ya mwisho?
“Mmh! Kwa haraka haraka nafikiri ni miaka tano au sita hivi imepita. Nakumbuka mara ya mwisho tulionana Kimara wakati napeleka mzigo Congo.
“Dah! Ni muda mrefu sana ndugu yangu. Vipi lakini harakati zinaendaje ndugu yangu?
“Harakati zipo poa kabisa vipi hapa nyumbani?
“Hapa nyumbani ni shwari kabisa. “Vipi shemeji yangu bado upo nae maana nyumba imepoa sana.
“Hahahah! Shemeji yako bado yupo ni yule yule Mama Ammy unayemjua wewe.
“Mashaallah! Hongereni sana kaka kwa kudumu kwenye ndoa. Hivi Ammy, Si ameshakua mkubwa kwa sasa?
“Yeah! Yupo darasa la tatu sasa hivi. “Duh! Kweli ni muda mrefu sana umepita na miaka inaenda kasi sana. “Yeah! Umri ndo huu unazidi kwenda ndugu yangu. Vipi lakini upande wako, Tayari umeshaoa kimya kimya?
“Hapana bro, Bado sijaoa ila tayari nina mtoto wa kiume.
“Ooh! Hongera sana, Hebu muoe basi huyo Mama mtoto wako. Unasubiri nini sasa Kareem?
“Nasubiri mke mwema, Ndoa sio kwa kila mwanamke kaka.
“Sasa Kareem, Kama mwanamke ameweza kukuzalia sasa atashindwaje kuwa mke kwako? “Braza Vonso, Kumbuka kwamba hata wanawake wahuni wanakuwaga na vizazi kwahiyo kuzaa sio kigezo cha kumfanya mwanamke kuwa na sifa za kuwa mke. Kuna wanawake wengine
wanastahili kazalishwa tu ila hawastahili kuolewa. Mimi kwa sasa natafuta mwanamke aliyetayari kuwa mke na kutunza familia. Nataka mwanamke wa kumlea mwanangu maana bado ni mdogo na anahitaji malezi ya mama bora.
“Anhaa! Sasa nimekupata vizuri Kareem. Kwahiyo huyo mwanao yupo kwa mama yake sasa hivi?
“Hapana! Mtoto yupo kwa Bibi yake, Mama yangu mimi. Kwa sasa lengo langu ni kupata mke ili nikamchukue mwanangu niishi nae mwenyewe. Nahitaji kumtunza mwanangu na kumlea mwenyewe katika malezi bora ili baadae aje kunitunza. “Hayo sasa ndo maamuzi ya kiume Kareem. Siku zote fainali uzeeni maana hizi nguvu ulizokuwa nazo sasa hizi hautakuwa nazo tena kwa miaka ijayo. Nguvu zinaisha ila mipambano haiishi mpaka unaingia kaburini. Alafu vipi kuhusu zile kazi zako za kusafiri, utaweza kweli na ndoa?
“Bro, Ile kazi nimeshaacha rasmi siku ya jana kwahiyo kwa sasa focus yangu ni biashara tu. Nashukuru Mungu nimeshajenga nyumba na nina pesa ya kutosha kufanyia biashara. Hapa tayari nimeshawasiliana na dalali anitafutie fremu pale Mwenge ili nifungue duka la urembo na vipodozi. Kwa sasa nahitaji kuishi na mke ili niwe karibu na mwanangu maana huwa nam’miss sana ninapokuwa mbali nae kwa muda mrefu.
“Anhaa! Hapo umefanya uamuzi mzuri sana kufanya shughuli zako hapa hapa mjini. Ujue hizi kazi za kusafiri safiri zinawafanya watu kutengana na familia zao kwa muda mrefu. Unakuta watoto wanamzoea na kumpenda mama peke yake kwa kuwa muda wote wanamuona yeye tu. “Ndo hivyo kaka, Muda wowote kuanzia sasa nikipata mwanamke mwenye sifa ninazotaka basi nitakushtua tupeleke posa maana wewe ndo mshenga wangu. “Hahahah! Hilo limekwisha ndugu yangu. Kanzu na kofia ninazo kwahiyo hilo limekwisha kabisa.
“Alafu mbona shemeji na mwanangu Ammy siwaoni sasa?
“Ooh! Kumbe sikukuambia kwamba shemeji yako ametoka? Yeye katoka ila muda si mrefu atarudi. Mwanao
Ammy yeye ameenda kucheza maana yeye ndo waziri wa michezo kwa wenzake hapa mta….” Kabla hajamaliza kuongea sauti ya mlango ikasikika ukifunguliwa.
Kila mtu akahamishia macho mlangoni na ndipo mke wa Vonso akaonekana akiingia ndani. “Ooh! Jamani! Kumbe kuna ugeni? Mbona sikutaarifiwa kama shemeji yangu unakuja leo?” Mke wa Vonso alizungumza maneno hayo mara baada ya kuingia pale ndani. Kwa hakika ilikuwa sapraizi kwake kuweza kumuona Kareem maana ni miaka mingi imepita tangu walipoonana. Mke wa Vonso alikuwa anamtambua Kareem kama rafiki mkubwa sana wa mume ila harakati za utafutaji ndo ziliwatenganisha. Kareem alikuwa mtu wa kusafiri na magari makubwa ya mizigo kuelekea nje ya nchi na alikuwa anamaliza mpaka mwaka akiwa nchi za watu. Kiumri Kareem alikuwa mdogo sana kwa Vonso. Mpaka kufikia muda huo Vonso alishatimiza miaka 40 huku Kareem akiwa na miaka takribani 33. Mke wa Vonso alisalimiana na Kareem kisha akamkaribisha kwa furaha sana pale ndani.
“Mume wangu, Hivi mgeni ameshakunywa hata soda?” Mke wa Vonso aliuliza
“Mgeni kasema hataki soda anataka mia sita yake.” Vonso akajibu kwa utani na kuwafanya wote wacheke. “Shemeji, Unatumia soda gani? Au unatumia juisi ya matunda?
“Dah! Kiukweli kwa sasa sihitaji soda wala juisi shemeji yangu.
“Mmh! Lakini koo si litakauka kwa stori shemeji yangu?
“Hahahah! Kawaida tu shemeji yangu. Hapa labda unipatie maji tu yanatosha.”
Baada ya Kareem kutaka maji, Mke wa Vonso akaanza kumuita kwa sauti Radhia aliyekuwa jikoni muda huo.
Alimuita Radhia mara mbili ndipo Radhia akaitika kwa sauti akiwa kule jikoni. Baada ya Radhia kuitika, Mke wa Vonso akamuagiza maji na kumwambia apeleke sebuleni kwa ajili ya mgeni. Hapo sasa Radhia akashtuka kidogo baada ya kujua kwamba kuna mgeni pale ndani. Ndani ya sekunde chache tu Radhia akafika sebuleni akiwa na jagi pamoja na glasi kwenye mikono yake. Alimsalimia Kareem kwa macho ya aibu kisha akamimina maji kwenye glasi na kumpatia huku akiwa ameinama kwa heshima. Huwezi kuamini, Kareem alipokea ile glasi na kuiweka mdomoni huku akiwa amegandisha macho yake kwenye uso wa Radhia. Ni kama vile akili yake ilihama kwenye sayari ya Dunia na kuhamia Jupita kwenye ulimwengu wa mapenzi.
Episode 09
Vonso na mkewe walimuona Kareem akiwa ameduwaa kumuangalia Radhia.
“Radhia mdogo wangu, Vipi chakula kipo tayari?” Mke wa Vonso alimuuliza Radhia.
“Ndio dada kipo tayari nimeivisha muda huu tu.” Radhia alijibu. “Okay! Waandalie basi watu wale.” Mke wa Vonso alimwambia Radhia huku akielekea chumbani kwake. Radhia nae akaondoka pale sebuleni na kuelekea jikoni kupakua chakula. Kwa mara nyingine tena Kareem akawa anamsindikiza kwa macho Radhia.
“Oya ndugu yangu? Vipi mbona kama akili imeruka ghafla?” Vonso alimuuliza Kareem na kumfanya ashtuke.
“Ooh! Sorry! Abee! Naam!” Kareem aliitikia kwa kuweweseka. “Nini shida ndugu yangu? Mbona unamshangaa sana yule mwanamke?
“Aah! Ni kwa sababu sijawahi kumuona kaka. Hivi ni ndugu yako au ni ndugu yake shemeji?
“Huyu alikuja kama dada wa kazi lakini kwa sasa tunaishi nae kama familia. Ni takribani miaka tano tupo nae hapa nyumbani na yeye ndo amemlea Ammy mpaka amekua.
“Oooh! Kumbe!
“Yeah! Ni mwanamke mmoja smart sana ndo maana tumeamua kuishi nae kama ndugu wa familia.” Muda ule ule Radhia akafika pale sebuleni akiwa na hotpot ya chakula pamoja na sahani mbili. Alipakua chakula kwenye sahani kisha akawakaribisha mezani Vonso pamoja na Kareem. Radhia akaondoka na kurudi jikoni huku Vonso na Kareem wakianza kujipatia chakula. Stori zilizoendelea pale zilikuwa za kawaida kuhusu maisha yalivyokuwa tangu walipoachana miaka kadhaa iliyopita. Waliendelea kupiga stori huku wakiendelea kujipatia chakula taratibu kabisa. Lakini sasa, Bado akili ya Kareem ilikuwa inamuwaza mwanadada Radhia. Baada ya kumaliza kula,
Kareem hakuchukua muda mrefu sana akawaaga watu wote pale ndani kisha akaondoka. Mwanaume aliondoka huku akiwa na taswira ya Radhia kichwani kwake. Hata usiku ulipofika alishindwa kupata usingizi akiwaza juu ya uzuri wa Radhia pamoja na matendo yake machache aliyoyaonesha. Kareem alihisi kabisa huenda Radhia ndo mwanamke
anayemtafuta siku zote. Alihisi kabisa kama Radhia ameweza kuishi na kumlea mtoto Vonso kwa takribani miaka tano basi anaweza pia kuwa mama bora wa watoto wake. Swali likabaki kichwani kwake, atumie mbinu gani ili kuhakikisha Radhia anakuwa mke wake. Amtumie rafiki yake Vonso au amfuate Radhia mwenyewe akazungumze nae? Hilo ndo swali lililokuwa kichwani kwa
Kareem. Baada ya kuwaza kwa muda akaona kabla hajafanya chochote ni vyema amshirikishe Vonso kwa kuwa ni rafiki yake na pia nia yake ilikuwa njema sana. Kareem hakuwa na lengo la kumchezea Radhia bali alitaka kumuoa kabisa. Siku iliyofuata Kareem alimtafuta Vonso kwa ajili ya mazungumzo. Walikutana kwenye nyumba mpya ya Kareem ambayo
alimaliza kuijenga. Vonso alistaajabu sana kuona Kareem ameweza kujenga nyumba kubwa sana kuliko umri wake. Ni nyumba ya kisasa iliyojitoshelezea kila kitu ndani yake. Ni nyumba kubwa na nzuri kuliko hata ile ya Vonso.
“Duh! Hii ni nyumba kweli kweli rafiki yangu. Hapa sasa ni kweli unahitaji mke wa kuitunza hii nyumba maana wewe mwenyewe huwezi kufanya usafi. Hongera sana kwa kujenga huu mjengo rafiki yangu.” Vonso alimpongeza Kareem baada ya kufika pale mjengoni.
“Braza, Mimi tayari nimeshakutana na mwanamke anayestahili kuolewa na mimi. Hilo ndo kubwa zaidi lililofanya nikuite hapa tuzungumze.
“Hahahah! Safi kabisa! Nilitegemea kabisa huwezi kuchukua muda mrefu kumpata mwanamke unayemuhitaji. Haya sasa toa location tupeleke kabisa mahari yao tuchukue kilicho chetu haraka iwezekanavyo. “Hahahah! Tulia basi kaka mbona haraka haraka.
“Haraka haraka ndo inahitajika kwenye Uislamu hasa hasa mtu anapotaka kutimiza jambo la kheri. Kufunga ndoa ni kutimiza nusu ya dini Sheikh wangu. Hata Quran inasema mambo makuu matatu yanayotakiwa kufanyika kwa haraka ni pale mtu anapotaka kuoa, anapotaka kuslimu na kitu cha mwisho ni kuzika pindi mtu anapofariki.
“Sawa umeeleweka Sheikh Vonso, Sasa ngoja nikuambie kitu Sheikh wangu. Unajua Vonso wewe ni rafiki yangu sana na heshima yangu kwako ni kubwa sana ndo maana nakutazama kama kaka yangu. Bro, Kama nitakuwa nimekukosea kwa hiki ninachotaka kukuambia basi naomba uniwie radhi. Kiukweli kabisa nimetokea kumpenda sana Radhia. Tangu nilipomuona ile jana moyo wangu ukakiri kabisa kwamba yeye ndo mwanamke niliyekuwa namsubiri siku zote. Licha ya uzuri alionao lakini pia anaonekana ni mwanamke mwenye heshima na busara. Naamini kabisa Radhia anafaa kuwa mke wangu.” Kareem alizungumza maneno hayo na kumfanya Vonso ashtuke kidogo kisha akashusha pumzi ndefu. “Kareem, Unamaanisha unayemtaka ni Radhia yule mfanyakazi wangu sio? “Yeah! Huyo huyo mfanyakazi wako. “Hahahah! Unajua ile jana nilikuona kama akili yako imepaa hivi baada ya kumuona Radhia pale ndani. Ule muda nilikuwa nakupigisha stori ila akili yako haikuwepo kabisa kwenye maongezi yetu. Anyway, Kwanza kabisa nikutoe wasiwasi juu ya kunivunjia mimi heshima kwa sababu macho hayana pazia umemuona amekuvutia. Yule Radhia sio ndugu yangu wa damu kwahiyo hakuna sheria yoyote inayoweza kukuhukumu kwamba umenivunjia heshima. Laiti kama angekuwa ndugu yangu wa damu basi kungekuwa na shida maana wewe na mimi ni marafiki kwahiyo ndugu yangu ni ndugu yako. Kwa hili kuwa huru kabisa rafiki yangu lakini naomba nikuulize swali kidogo.
“Sawa niulize Bro nakusikiliza.
“Hivi ni kitu gani haswa kimekufanya umpende Radhia na kuamini kwamba ni mwanamke anayefaa kuwa mke wako wakati hujapata hata muda wa kumsoma tabia zake?
“Bro! Mimi nakujua vyema sana wewe na shemeji yangu ni watu wazuri sana. Kama Radhia ameweza kuishi na nyie kwa miaka takribani tano na mkampa jukumu la kumlea mtoto wenu basi ni wazi kabisa yeye ni mwanamke mwenye maadili mazuri. Hata ile jana nilipomtazama machoni niligundua kwamba yeye ni mwanamke mwenye sifa zuri na za kupendeza. Naomba msaada wako katika hili Bro ili niweze kumuoa. “Sawa mimi nipo tayari kukusaidia kwa nafasi yangu maana hili ni jambo la kheri kwa Mola wetu na pia ni fursa ya maisha kwa Radhia. Kwangu mimi Radhia ni kama mdogo wangu maana nimeishi nae nyumbani kwa upendo na amani kwa kipindi kirefu sana.
Najua kabisa alikuja mjini kutafuta maisha kwahiyo inapotokea fursa nzuri kwake siwezi kumuwekea kizuizi. Najua kabisa hawezi kuzeekea nyumbani kwangu hivyo kuna muda utafika itabidi akajenge familia yake
mwenyewe akiwa kama mama. Sasa hapa changamoto ni moja tu Kareem, Wewe unampenda Radhia lakini je yeye anakupenda?
“Dah! Hapo ndo pagumu kaka ila naweza kuongea nae ingawa haitakuwa rahisi kunielewa haraka kwa sababu hanijui kiundani zaidi. Lakini Braza Vonso mimi naamini hili suala wewe ndo unaweza kulimaliza kwa sababu Radhia anakuamini sana na anaweza kukuelewa ukimwambia ukweli kuhusu mimi. Wewe ndo unaweza kumpa sifa zangu hivyo itakuwa rahisi kwake kuweza kukubali kuolewa na mimi.
“Ni kweli ni rahisi sana kwangu kuzungumza na Radhia lakini sio rahisi kumfanya akubali. Mimi nitajaribu kwenda kuongea nae lakini sitotumia cheo changu kumlazimisha akubali kuolewa na wewe. Nitampa uhuru afanye uamuzi wake mwenyewe ili nisimkumbushie yale matatizo ya miaka 5 iliyopita yaliyomfanya akimbie kijijini na kuja mjini.
“Matatizo? Matatizo gani hayo yaliyomkumba Radhia?
“Ni stori ndefu kidogo ila kilichotokea ni kwamba…” Vonso alianza kumsimulia Kareem ule mkasa aliosimuliwa na Radhia ile siku ya kwanza kabisa walipokutana kwenye gari. Ni ule mkasa wa uongo wa kulazimishwa kuolewa ambao Radhia aliutunga na kumsimulia Vonso ili apate msaada kiurahisi. Vonso alipofikia nukta ya mwisho ya simulizi, Kareem akajikuta anamuhurumia sana Radhia. Ule mkasa ukamfanya azidi kupata shauku ya kumuoa Radhia ili abadilishe mazima historia ya maisha yake. Kareem alimuachia Vonso kazi yote ya kuzungumza na Radhia huku akiwa na matumaini kila kitu kitaenda sawa. Mwanaume alitaka mwanamke wa kujenga nae familia pamoja na kumlea mwanae ambaye tayari alishazaliwa na alimuacha kwa bibi yake.
Episode 10
Baada ya kumaliza kuongea na Kareem, Vonso alirejea nyumbani na kukaa kitako na mkewe ili kumshirikisha kwenye lile suala. Vonso hakutaka kufanya uamuzi juu juu bila kuzungumza na mkewe ili ajue mtazamo wa mke wake juu ya kile walichojadili na Kareem. Wakiwa chumbani Vonso alimsimulia mke wake kila kitu kuhusu Kareem kumpenda Radhia. Ukweli ni kwamba lile suala liliwaweka njia panda Vonso na mkewe kwa sababu kuu mbili. Kwanza kabisa lile jambo lilikuwa la kheri na ni bahati kubwa sana ilimshukia Radhia akiwa ndani ya nyumba yao. Pili, hawakutamani kabisa Radhia aondoke pale ndani kwa sababu alikuwa na umuhimu mkubwa sana pale ndani kwa miaka yote waliyoishi pamoja. Radhia alishageuka mwanafamilia kwenye ile nyumba ya Vonso hivyo kuondoka kwake kungeacha pengo kwa kiasi fulani.
“Mmh! Sasa hapa mume wangu itakuwaje maana sitamani kabisa Radhia aondoke hapa ndani lakini pia kumzuia kuondoka kwenye suala kama hili ni sawa na kumzibia ridhiki. Hii ni bahati kubwa sana kwake kupendwa na Kareem maana anaenda kubadilisha rasmi status yake ya maisha.
“Hilo lipo wazi mke wangu, kwa namna tulivyoishi na Radhia hapa ndani na mazuri yote aliyotufanyia hatupaswi kabisa kumzibia ridhiki kwa ajili ya manufaa yetu binafsi. Tumeishi na Radhia kama ndugu kwenye familia yetu kwahiyo acha sasa akaishi kwenye familia yake. Hata huyu Ammy kuna muda utafika ataachana na familia yetu na kwenda kuanzisha familia yake. Hapa tunapaswa kuzungumza na Radhia mwenyewe na tumfikishie ombi la Kareem tuone atakachoamua mwenyewe. Sisi hatutamlazimisha kufanya maamuzi, kwahiyo kukubali au kukataa hiyo ni juu yake mwenyewe. Kama atachagua kuolewa basi ni sawa na kama atachagua kuishi na sisi basi ni sawa pia. Kikubwa tu tusihusike kumzibia bahati, acha ajizibie mwenyewe. “Sawa nimekuelewa vyema mume wangu na mimi nitajitahidi kumsihi akubali kuolewa maana kupata ndoa sio rahisi kwenye dunia ya sasa. Lakini pia Kareem ni mwanaume anayejitambua na ana kipato kizuri sana kwahiyo anaweza kubadilisha maisha yake. Hii ni bahati kubwa sana kwa Radhia kwahiyo asije akaipiga teke.”
Hayo yalikuwa mazungumzo kati ya Vonso na mkewe na hivyo ndivyo walivyomaliza kuzungumza. Wote kwa pamoja walikubaliana wazungumze na Radhia juu ya ombi la Kareem la kutaka kumuoa.
****
Mnamo majira ya saa 3 usiku juu ya alama, Vonso na mkewe walimkalisha Radhia kitako sebuleni kwa ajili ya kumfikishia ujumbe wa Kareem. Wakati Vonso akiwaza neno la kuanza kuzungumza, Radhia yeye alikuwa hajui chochote kinachotaka kuendelea. Muda huo kila mtu alikuwa kimya huku macho yao yakiwa kwenye TV. Muda huo huo sauti ya Vonso ikasikika ikimuita jina
Radhia;
“Radhia,
“Abee kakaa!
“Unamkumbuka yule mgeni aliyekuja juzi nikakutambulisha kuwa ni rafiki yangu?
“Ndiyo kaka namkumbuka vizuri sana si ndo yule ulisema anaitwa Kareem?
“Yeah! Ndo yeye wala hujakosea. Mimi na jamaa ni marafiki wakubwa sana na urafiki wetu ulianzia kwenye kazi kipindi hiko nilikuwa naendesha gari la kampuni kupeleka mizigo nje ya nchi. Kareem sio tu rafiki bali ni ndugu yangu kwa kuwa urafiki wetu ulishapitiliza kwenye kiwango cha juu kabisa cha urafiki. Sasa Radhia, Yule kijana yaani Kareem tangu ile juzi alipokuona alitokea kukupenda na yupo tayari kukuoa. Huo ndo ujumbe alionipatia mimi kama mzazi wako hivyo nimekufikishia Binti yangu.” Radhia alishtuka na kuganda kwa sekunde kadhaa baada ya kusikia kauli ya Vonso. Ni kama vile hakuyamini masikio yake kwa kile alichokisikia.
“Radhia!
“Abee! Naam! Abeee..
“Vipi umeelewa nilichozungumza? “Ndio kaka nimekuelewa lakini mimi simjui kiundani zaidi sasa naweza kuolewa na mtu nisiyemfahamu? Nitajuaje kama ni mwanaume sahihi kwangu?
“Ni kweli upo sahihi kabisa mdogo wangu lakini nikuhakikishie tu
kwamba Kareem ni mwanaume anayejitambua, mwaminifu na mwenye upendo wa dhati. Jamaa hana kabisa makandokando kama ilivyo kwa wanaume wengine. Ni mtu mmoja smart sana na hana mambo mengi. Mimi namfahamu na kumjua vizuri Kareem kwa sababu ni rafiki yangu. Hii ni bahati kubwa sana kwako Radhia kwa sababu kuna wanawake wengi huko mtaani wanatamani kupata nafasi ya kuolewa na jamaa lakini hawapati. Kareem ni mpambanaji sana na katika ule umri tayari ameshajenga hapa mjini na amebarikiwa kipato. Hii ni nafasi adhimu kabisa ya kubadilisha maisha yako mdogo wangu.” Vonso aliweka nukta baada ya kuzungumza maneno hayo.
Mke wa Vonso nae akaongezea kwa kusema;
“Radhia mdogo wangu, Ndoa sio rahisi kupatikana hapa mjini. Kuna wanawake wengi wanazurura mitaani na kwa waganga kutafuta ndoa lakini wewe imekufuata hapa hapa nyumbani. Nakuthibitishia kabisa endapo utakubali kuolewa na Kareem basi utakuwa umepata mwanaume sahihi kabisa katika maisha yako. Kusema ukweli yule shemeji yangu ni mwanaume mwenye kila sifa za kuwa mume. Ni mtu mmoja mwenye moyo safi na ana hofu ya Mungu. Kiufupi ni kwamba hautojutia kuolewa nae ila utajutia kwanini ulichelewa kukutana nae. Na kingine ni kwamba sisi hatukufukuzi hapa nyumbani wala hatukulazimishi kuolewa na Kareem. Maamuzi ni juu yako mwenyewe, kuolewa au kubaki hapa nyumbani.” Mke wa Vonso alimwambia Radhia maneno hayo kwa unyenyekevu wa hali ya juu.
Vonso nae akaongezea kwa kusema;
“Radhia, Kama alivyosema dada yako kwamba hatukufukuzi hapa nyumbani kwa sababu bado tunakuhitaji kwenye hii familia. Wewe ni ndugu yetu kabisa kwahiyo mimi na mke wangu hatupo tayari kukutengenezea mazingira magumu au kukukosesha furaha. Maamuzi yapo chini yako mwenyewe kukubali au kukataa ndoa. Kuwa huru kufanya uamuzi utakaoona sahihi kwako. Kwenda kuwa Mama mjengo kwa Kareem au kuwa kuwa dada mjengo hapa ndani. Lakini kumbuka pia kuna maisha baada ya kuwa dada mjengo maana hata mtoto hawezi kuishi na wazazi miaka yote. Kuna muda unafika mtoto anaacha familia ya wazazi na kwenda kuanzisha familia yake. Hilo pia usisahau kulitazama wakati unafanya chaguo. Kumbuka hayo ni maisha yako Radhia”
Mpaka kufikia hapo Vonso na mkewe wakaweka maiki chini na kusubiri jibu la Radhia. Radhia alivuta pumzi ndefu kisha akasema;
“Kaka na dada, Mimi nimewaelewa vizuri sana na nimeuona upendo wenu wa dhati kwangu. Kwenye hili suala naomba mnipe muda kidogo tu wa kutafakari kisha nitawapa jibu. Lakini kabla sijatoa jibu naomba nikutane na huyo Kareem mara moja ili nizungumze nae jambo.
INAENDELEA………….