𝐍𝐈𝐋𝐈𝐌𝐓𝐄𝐒𝐀 𝐌𝐓𝐎𝐓𝐎 𝐖𝐀 𝐊𝐀𝐌𝐁𝐎 𝐁𝐈𝐋𝐀 𝐊𝐔𝐉𝐔𝐀 𝐍𝐈 𝐌𝐖𝐀𝐍𝐀𝐍𝐆𝐔 𝐍𝐈𝐋𝐈𝐘𝐄𝐌𝐓𝐔𝐏𝐀𝐆𝐀 𝐌𝐒𝐈𝐓𝐔𝐍𝐈 𝐊𝐈𝐏𝐈𝐍𝐃𝐈 𝐂𝐇𝐀 𝐍𝐘𝐔𝐌𝐀
Mkasa Wa Kweli
Episode 01
Ni ndani ndani kidogo katika kijiji kimoja kipatikanacho mkoani Ruvuma katika wilaya ya Songea. Ni kijiji kidogo kilichojulikana kwa jina la Mizula. Kulikuwa na Binti mmoja anayefahamika kwa jina la Radhia. Radhia ni Binti wa miaka 18 aliyekuwa anaishi na bibi yake katika kijiji hiko. Wazazi wa Binti huyo tayari walishafariki wakati Radhia akiwa mdogo. Bibi ndo alichukua jukumu la kumlea Radhia tangu akiwa mdogo mpaka kufikia muda ule. Radhia na bibi yake walikuwa miongoni mwa wanakijiji waliokuwa wanaishi kwenye maisha duni sana pale kijijini. Bibi tayari umri ulishamtupa mkono hivyo hakuwa na nguvu tena ya kufanya kazi. Ni kijijini kabisa kama ujuavyo elimu sio kipaumbele kwa watoto wengi hivyo Radhia hakubahatika kupata elimu ya sekondari licha ya kufaulu katika mtihani wake wa darasa la saba. Hali ya maisha ndo ilichangia kwa kiasi kikubwa
kukwamisha safari ya masomo ya Binti huyo. Pigo lingine liliibuka kwa
Binti Radhia baada ya Bibi yake kufariki dunia kwa maradhi ya uzeeni. Huo ndo ulikuwa mwanzo wa maisha ya upweke kwa Binti Radhia. Radhia alijikuta kwenye mitihani mizito sana ya kidunia hasa hasa katika utafutaji wa chakula. Yote tisa, kumi ni kwamba Radhia alikuwa ni msichana mrembo sana aliyetingisha mioyo ya vijana wengi wakiume pale kijijini. Hata watu wazima wenye wake zao walijikuta wanavutiwa na binti Radhia. Kijana Anthony Joseph maarufu kama Tony ndiye mwanaume pekee aliyebahatika kukubaliwa na kupendwa na Binti Radhia. Kijana huyo alikuwa dereva wa bodaboda pale kijijini. Anthony alitokea kumpenda sana Radhia. Alibadilisha muonekano wa Radhia kwa kiasi fulani kwani alikuwa anamjali, anampenda na kumthamini. Maisha ya Radhia yalibadilika na kuwa mazuri baada ya kuingia kwenye mahusiano na Tony. Alipewa huduma zote anazotakiwa kupewa mwanamke na mwanaume wake. Kwa hakika Radhia aliyafurahia mahusiano yake na kuamini kwamba Tony ndo mtu pekee aliyebaki katika maisha yake. Ndani ya mwezi mmoja wa mahusiano yao, Radhia alianza kujihisi utofauti katika mwili wake. Alihisi uchovu, kichefuchefu, kutapika na kuanza kuchukia baadhi ya vyakula. Hali hiyo ikamfanya aende hospitali kupima afya yake. Alifika hospitali nakufanyiwa vipimo na ndipo akagundulika kuwa na ujauzito wa wiki mbili. Radhia alitoka nje ya hospitali huku akiwa na furaha kubwa moyoni. Alikuwa na shauku kubwa ya kumjuza mpenzi wake Tony juu ya taarifa hiyo. Alipofika tu nyumbani kwao jambo la kwanza lilikuwa kumpigia simu Tony. Kwa
bahati nzuri simu ya Tony iliita na kupokelewa;
“Hello mume
“Yes Mke, Uko poa?
“Niko poa kabisa, Kuna kitu nataka kukuambia bebiiiii. “Kitu gani hiko mpenzi?
“Ni kitu kizuri sana nafikiri utakifurahia sana siku ya leo. Fanya basi tuonane ili nikuambie.
“Aah! Si uniambie tu mpenzi. Si unajua mimi nipo kazini muda huu.
“Basi, Nitakuambia baadae tukionana maana nikikuambia kwenye simu ladha itapungua.
“Hahahah! Unaonekana unafuraha sana leo Radhia.
“Yeah! Ninafuraha sana tena sanaa. Au sijui nikufuate huko ulipo? Kwanza uko wapi muda huu?
“Niko njiani naendesha nimempakiza mteja kuna sehemu nampeleka. “Anhaa sawa,Basi ukimshusha naomba uje hapa kwangu mara moja uchukue zawadi yako.
“Hahahah! Basi sawa nitafanya hivyo.
“Sawa naomba basi usichelewe Tony na kuwa makini huko barabarani.
“Poa poa usijali Ma mtu..”
Hayo yalikuwa mazungumzo kati ya Radhia na mpenzi wake Tony. Baada ya nusu saa kupita, Tony alikwenda kwenye kibanda alichokuwa anaishi Radhia. Alipofika akamkuta Radhia akiwa na sura yenye tabasamu pana sana. Radhia alinyanyuka pale alipokuwa amekaa kisha akamkumbatia Tony kwa bashasha. Tony akabaki na mshangao maana haikuwa kawaida ya Radhia kumpokea kwa ile staili. Radhia alionekana kuwa na furaha kuliko siku zote za mahusiano yao. Tony Alijiuliza kichwani mwake. Ni kitu gani kikubwa nimekifanya kwa huyu mwanamke mpaka anakuwa na furaha kubwa kiasi hiki? Je ni zawadi gani hiyo ambayo anataka kunipatia?
Tony alijiuliza bila kupata majibu. Baada ya sekunde kadhaa walijitoa kwenye kumbatio kisha wakakaa kwenye viti.
“Nambie Ma mtu, Ipo wapi hiyo zawadi yangu?
“Otea kwanza ni zawadi gani nataka kukupa?
“Daah! Hapo pagumu sana mchumba maana mimi sio nabii.
“Hahahah! Sawa hebu kamata hii Tony.” Radhia aliongea huku akimpatia Tony kikaratasi fulani. Tony alipokea ile karatasi kwa mshangao sana.
Baada ya kupokea akakifungua na kuanza kukisoma.
“MIZULA DISPENSARY” Hayo ndo maneno yaliyosomeka juu ya ile karatasi. Tayari Tony alishaelewa kwamba ile karatasi imetoka katika zahanati ya kijiji. Alipojaribu kusoma maelezo yaliyofuatia alishindwa kuelewa kile kilichoandikwa.
“Radhia! Bado sijaelewa chochote juu ya hii karatasi.
“Hahah! Kipi hujaelewa sasa Babaa? Kuanzia muda huu wewe ni Baba kijacho. Yale maombi yetu hatimaye Mungu ameyasikia na sasa mimi ni mjamzito Tony.
“Mjamzito? Sasa kama wewe ni mjamzito unaniambia mimi nifanyaje?
Kwanza ujauzito wa nani?
“Khaa! Tony jamani! Sasa ujauzito uwe wa nani wakati wewe ndo mpenzi wangu.
“Una uhakika huo ujauzito ni wangu kweli?
“Ndio ni wako Tony.
“Sasa kama ni wangu mbona unao wewe?
“Aah! Tony jamani, Hebu kuwa serious basi.
“Okay! Sasa sikia wewe demu, Kama huo ujauzito ni wangu na unataka mahusiano yetu yaendelee basi nenda kaitoe hiyo mimba. Kama hutaki kutoa basi mpelekee hilo tumbo aliyekupa hiyo mimba. “Unasemaje Tony! Unataka mimi niitoe hii mimba? Hapana Tony huko umefika mbali sana. Hivi wewe si ndo yule uliyekuwa unaniambia nikubebee mimba utailea? Si ndo wewe uliyeniambia nikikubebea mimba utanioa? Mbona unabadilika sasa Tony jamani? Alafu ni dhambi pia kuua kiumbe kisichokuwa na hatia. Hebu muogope Mungu basi Tony. “Oya we demu naomba ufungue masikio yako na unisikilize kwa umakini sana. Mimi sijajipanga kuingia kwenye majukumu ya kuhudumia mtoto muda huu. Bado sijajipanga kuwa na familia kwa sasa. Mimi bado sina pesa kwahiyo usinitwishe mzigo mkubwa ukaja kunielemea. Mimi ni kijana mdogo sana ndo kwanza nimeanza kula ujana. Subiri kwanza nimalizie ujana alafu ndo niwaze kuhusu familia. Hapa cha kukusaidia labda ni pesa ya kutoa hiyo mimba tu.
“Mimba sitoi Tony. Kama mimi nilizaliwa basi na hiki kiumbe nacho kitazaliwa.
“Hahaha! Kwahiyo huo ndo msimamo wako sio? Okay sawa kwa kuwa umeamua hivyo basi pambana na hali yako Binti. Na cha kuongezea hapo kuanzia leo naomba usinipigie simu wala usinitafuta kwa ajili ya kuniambia chochote kile. Naomba ufute namba zangu na za kwako nazifuta. Sahau kabisa kama ulishawahi kuwa na mahusiano na mimi.”
Baada ya kuongea maneno hayo. Tony akapanda kwenye pikipiki kisha akaondoka kwa hasira. Radhia akawa anamuita Tony kwa sauti ya huzuni huku akimsindikiza kwa macho. Furaha yake iligeuka kuwa huzuni na kujikuta akiwa katika hali ya simanzi na majozi. Hakutegemea kabisa kama Tony angebadilika ghafla baada ya kumpa ule ujauzito. Ni Tony yule yule aliyemuahidi Radhia ndoa endapo atambebea ujauzito, Ndiye Tony yule yule aliyekimbia baada ya kutimiziwa matakwa yake.
Episode 02
Tony alifika katika kijiwe chao cha kupaki bodaboda. Aliwakuta marafiki zake wakipiga stori mbalimbali kama ilivyokuwa kawaida yao. Tony akawasabahi kisha akapaki pikipiki yake na kukaa pembeni, mbali kidogo na wenzake.
“Oya Tony mbona hivyo mzee? “Aah! Kawaida tu mwanangu. “Kawaida vipi mwanetu wakati hatujakuzoea hivyo bhana. Njoo ujumuike na wana tupunguze stress za maisha.” Timo alimwambia Tony maneno hayo huku akimfuata kule alipoketi.
“Bro usiwaze nimeamua tu kukaa huku mwenyewe maana nina mawazo sana leo.
“Daah! Kwani tatizo nini mwanetu mpaka unakuwa na mawazo kiasi hiko?
“Kuna jambo linanichanganya sana ndo maana najikuta nakuwa na mawazo hivi.
“Ni jambo gani hilo?
“Shemeji yako, mwanangu.
“Shemeji! Shemeji kafanyaje?
“Ni mjamzito.
“Mjamzito! Hahaha, Sasa hilo ndo jambo linalokupa stress? Kwanza kabisa nikupe hongera zako Tony.
Kidume umeshapanda mbegu bado kuvuna tu. Kuitwa Baba sio rahisi hongera sana kaka.
“Hongera ya nini kaka wakati sijajipanga kuingia kwenye majukumu sasa hivi. Me nimemwambia demu aitoe tu sina mpango wa kuwa na mtoto sasa hivi.
“Dah! Hapo sasa unafeli mwanangu. Wewe ni mtoto wa kiume kwanini usipambane ukalea mimba. Kumbuka fainali uzeeni kaka kipindi hiko hauna nguvu ya kupambania tonge. “Hilo naelewa Timo tatizo ni kwamba huu sio muda sahihi wa kuitwa Baba. Nataka kumalizia ujana kwanza. Unadhani Kidawa akijua kwamba nimempa mimba Radhia itakuwaje?
Si ataniacha mazima?
“Kwahiyo mwanangu unataka kukataa damu yako kisa Kidawa mcharuko? Yule kimada ndo akufanye ukatae damu yako? Hapo unazingua mwanangu, Kama ningekuwa mimi basi ningeipambania hiyo mimba. Binafsi natamani sana demu wangu ashike mimba lakini ndo hivyo hapati. Wewe ambaye Mungu amekujali uzao unataka kukufuru. Ila nini mwanangu, Tutaongea vizuri baadae maana kuna abiria wangu namfuata Kichangani hapo.
“Poa poa mwanangu ila ndo hivyo siwezi kulea mimba kwa sasa kwanza pesa yenyewe ngumu sana hapa kijijini alafu ndo kwanza naanza kutafuta maisha.”
Hayo yalikuwa maongezi kati ya Tony na rafiki yake Timo wakiwa kwenye mgundi wao wa bodaboda.
****
Majira ya saa tatu usiku Radhia alikuwa kitandani amejilaza huku akitokwa na machozi. Siku hiyo alikuwa na msongo mzito wa mawazo kutokana na majibu ya Tony juu ya lile suala la ujauzito. Radhia aliwaza kwanini Tony amembadilika baada ya kumpa mimba. Lakini pia aliwaza atumie mbinu gani ili aweze kumshawishi Tony akubali kulea ile mimba. Hakutaka kabisa kukata tamaa hivyo aliamini kwa namna yoyote ile atafanikiwa tu kumshawishi Tony. Usiku ule ule Radhia aliamua kumpigia simu Tony. Simu ya Tony iliita lakini haikupokelewa. Akajaribu kupiga kwa mara ya pili lakini bado haikupokelewa. Radhia alijipa moyo huenda Tony atakuwa barabarani anaendesha. Bado mtoto wa kike aliendelea kuwaza mpaka usingizi ulipomchukua. Mpaka siku mbili zinakatika, hakukuwa na mawasiliano yoyote kati ya Radhia na Tony. Licha ya Radhia kumtafuta sana Tony kwenye simu lakini Tony hakupokea kabisa. Radhia alishindwa kuvumilia jambo lile hivyo akaamua kwenda kwenye chumba alichokuwa anaishi Tony. Alipofika alisikia sauti ya mziki ukiimba na mlango ulifungwa kwa ndani. Radhia alibisha hodi na baada ya dakika moja kupita mlango ukafunguliwa. Cha ajabu ni kwamba aliyetoka ndani hakuwa Tony bali ni mwanamke akiwa na khanga moja mwilini. Radhia alishtuka kwa marefu na mapana baada ya kumuona mwanamke huyo.
“Mbona asubuhi asubuhi jamani watu tumelala na mabwana zetu tunakatishana raha. Hebu sema shida iliyokuleta, Mbona unaniangalia hivyo?” Mwanamke huyo aliongea maneno hayo huku akimtazama Radhia kwa dharau.
“Sa.. sa.. samahani naomba uniitie
Tony.” Radhia aliongea kwa sauti ya unyonge na kigugumizi.
“Wewe ni nani yake?” Mwanamke huyo alimuuliza Radhia kwa dharau. “Mwambie ni Radhia ndo anakuita yeye ataelewa.”
Yule mwanamke akaingia ndani kumuita Tony. Hazikupita dakika nyingi Tony akatoka ndani akiwa amevaa kipensi cha kulalia. Yule mwanamke nae akatoka nje.
“Umefuata nini maskani kwangu?
Tony alimuuliza Radhia kwa hasira. “Tony hiyo ndo salamu? Hivi umepatwa na nini wewe mwanaume? Leo hii wewe wakuniuliza mimi nimefuata nini maskani kwako? Mbona umebadilika sana Tony?
“Sikiliza wewe mwanamke, Ongea jambo lilokuleta usinipotezee muda kuna shughuli yangu sijamaliza huko ndani.
“Hivi Tony kosa langu mimi ni nini haswa? Kubeba ujauzito ndo sababu ya wewe kunifanyia haya yote. Nakupigia simu hutaki hata kupokea Tony. Kipi nilichokukosea mimi? “Hahahah! Sikiliza Radhia, Mimi na wewe tulishamalizana kwahiyo acha kunifuatilia. Alafu nilishakuambia hiyo mimba sio yangu mtafute mwanaume aliyekupa.
“Tony! Hivi unionei huruma hata kidogo? Hivi umuogopi Mungu kweli? Wewe ndo Baba wa hiki kiumbe kilichopo tumboni, unadhani nitaishije mimi endapo utanitelekeza?
“Sikiliza tena kwa umakini wewe demu, Leo iwe mwanzo na mwisho kuja hapa ghetto kwangu. Kama utarudi tena basi sitaongea kama hivi ninavyoongea leo. Awamu ijayo nitaongea kwa vitendo.”
“Hey Bibi weee, Hebu ondoka basi mbona unakuwa king’ang’aa? Mwanamke ukiachwa achika basi hakuna sio kuendelea Kung’ang’ania kupendwa mahala usipopendwa. Mimi ndo Kidawa, Mrs Tony Og wengine feki. Kama ulijibebesha mimba ukajua utaolewa basi imekula kwako.” Yule mwanamke aliyekuwa na Tony akamwambia Radhia maneno hayo kwa dharau na kejeli.
“Tony! Ahsante sana kwa kila kitu.
Mimi naondoka ila tambua hiki kiumbe unachokikataa ni chako kabisa. Kupitia hili umenipa funzo kubwa sana wewe Tony. Ahsante sana na nakutakia maisha mema.” Radhia aliongea maneno hayo huku akitokwa na machozi ya huzuni. “Sawa ondoka mama, wewe uliona wapi mchezaji akifunga goli anasimama bila kukimbia kwenda kushangilia? Hebu ondoka nataka kuinjoi na mke wangu.” Tony aliongea kisha akamsukuma kwa nguvu Radhia.
Radhia akarudi nyuma kwa kuyumba kisha akadondoka chini.
Tony alimshika kiuno Kidawa wake kisha wakazama ndani na kufunga mlango. Radhia akainuka pale chini kinyonge sana kisha akaanza kuondoka huku akichechemea.
Episode 03
Ni rasmi sasa Radhia akatakiwa kuanza maisha ya kujitegemea kwa kila kitu bila msaada wa Tony. Mtoto wa kike akaanza kupambana na mimba yake kuhakikisha anajitimizia mahitaji yake mwenyewe. Alianza kupika vitumbua na kuviuza lakini biashara ikawa inamvuta shati na kujikuta anafeli mazima. Hapo sasa akapata wazo la kutafuta kazi ya kusaidia kwa wamama wanaouza
vyakula. Kadri siku zilivyozidi kusonga ndivyo Radhia alivyozidi kupitia changamoto za maisha. Radhia alihisi kukata tamaa lakini ghafla akapata tumaini jipya. Ni siku ambayo alitembelewa na rafiki yake wa kike aitwaye Landina. Radhia
alimkaribisha ndani rafiki yake kisha
wakaanza kuzungumza; “Vipi shoga yangu maisha yanaendaje? Landina alianza kuzungumza.
“Yanaenda hivyo hivyo Mungu anasaidia shoga yangu.
“Vipi kuhusu Tony, Bado amegoma kuwasiliana na wewe?
“Dah! Kiukweli mawasiliano yetu yalishaisha tangu siku nyingi sana. Ni
mwezi wa pili sasa hatuna mawasiliano.
“Duh! Sasa unaishije Radhia? “Hivyo hivyo najipambambania mwenyewe shoga yangu. Ile biashara ya vitumbua imedoda siku hizi naunga unga tu kwa watu napata pesa ya kusukuma siku. Ila kiukweli kabisa nateseka sana shoga yangu. Kuna muda namuhurumia sana kumkalisha na njaa mwanangu aliye tumboni.
“Dah! Pole sana shoga kwa magumu unayopitia. Sasa sikia Radhia mimi mwenzako kuna mama namsaidia
kuuza chakula kijiji cha pili. Huyo mama kwa sasa anahitaji mdada mwingine wa kutusaidia kazi maana wateja ni wengi sana siku hizi. Sasa kama upo tayari kufanya hiyo kazi basi twende nikakuunganishe kwa boss wangu ili uanze kesho. “Landina, Mimi nipo tayari kufanya hiyo kazi shoga yangu. Kiukweli utakuwa umenisaidia sana rafiki yangu.
“Basi hilo limekwisha Radhia, Kesho saa 12:00 alfajiri nitakupitia ili tukaanze kazi pamoja. “Nashukuru sana Landina kwa msaada wako. Ahsante sana kwa kuwa nami katika kipindi hiki kigumu. “Basi poa shoga yangu, Ngoja nifike kwanza nyumbani maana nimechoka sana leo. Hakikisha tu unajiandaa ili kesho tuondoke.”
Hayo yalikuwa mazungumzo kati ya Radhia na rafiki yake Landina. Ni mazungumzo yaliyofufua matumaini ya Radhia kuishi kama binadamu wengine. Asubuhi na mapema ya siku iliyofuata Landina alimpitia Radhia na kwenda nae kule anakofanya kazi yeye. Wao walikuwa wa kwanza kufika kabla ya bosi hivyo wakaanza kufanya usafi nakuweka mazingira vizuri. Dakika chache baadae bosi mwenye kibanda akafika na kuwakuta Landina na Radhia. Walisalimiana kisha Landina akamtambulisha Radhia kwa bosi wake.
“Dada, Huyu anaitwa Radhia ndo yule rafiki yangu niliyekuambia nitakuja nae kama atakubali.
“Anhaa kumbe ndo huyu, Karibu sana mdogo wangu. Mimi naitwa Edina jina maarufu ni Mama P. Karibu sana mdogo wangu.
“Asante sana dada Edina nashukuru sana kwa mapokezi yako.
“Sawa! Vipi Landina ulishaongea nae mwenzako kila kitu kuhusu mshahara?” Mama P alimuuliza Landina.
“Ndio dada niliongea nae kwahiyo anajua kila kitu kuhusu malipo.” Landina alijibu.
“Sawa tuendeleeni na kazi maana muda sio mrefu wateja wataanza kuja.” Mama P aliongea na ndipo kazi za kuandaa chakula zikaanza kufanyika rasmi.
Hivyo ndivyo mambo yalivyokuwa. Hatimaye Radhia alipata kibarua cha kumsaidia kuendesha maisha yake. Angalau sasa akapata afueni ya maisha.
“Vipi shoga yangu kazi ni ngumu eeh? “Wala sio ngumu ni kawaida tu ila sijajua tu huko mbeleni itakuaje maana hili tumbo ndo litakuwa kikwazo.
“Ni kweli Radhia maana hilo tumbo likishafikia miezi 6 tu hupaswi kufanya kazi ngumu kwa ajili ya kumlinda mtoto.
“Landina, Mimi sina namna yoyote yakufanya zaidi ya kufanya kazi hata likifikisha miezi 9. Itabidi tu nifanye kazi maana sina mtu yeyote wa kunipambania Landina. Najua kabisa nitakuwa namtesa mwanangu lakini atanisamehe tu maana nafanya yote kwa sababu yake tu. Ni imani yangu kwamba Mungu atanilindia mwanangu na kwa kudra zake nitajifungua salama.
“Ni kweli Radhia, mkubwa Mungu tu yeye ndo tunapaswa kumuomba ili akufanyie wepesi ujifungue salama. Mimi nitakuwa bega kwa bega na wewe kwa kila hatua unayopita. Jambo la msingi kwa sasa wekeza hivi visenti kidogo unavyopata kwa ajili ya maandalizi ya kujifungulia.”
Hayo yalikuwa mazungumzo kati
ya Radhia na Landina wakiwa njiani wakitokea kazini.
Furaha kwa kiasi chake ilirejea upya kwa Radhia. Mtoto wa kike alipiga magoti chini na kumshukuru Mungu kwa kupata ile kazi. Ni kazi iliyompa matumaini ya kuishi na kulea tumbo lake bila kutegemea msaada wa Tony.
Episode 04
Siku zilisonga na miezi ikakatika.
Radhia na Landina waliendelea kufanya kazi kama kawaida kwenye kibanda cha chakula cha Mama P. Bado biashara ilikuwa inaenda vizuri na ule ujio wa Radhia akaongeza wateja kwa kiasi fulani. Kibanda cha Mama P kikawa na wateja wengi kuliko kwenye vibanda vya
Maman’tilie wenzake. Muonekano wa Radhia ulichangia sana lile ongezeko la wateja. Radhia alikuwa msichana mrembo sana kwenye macho ya
vijana wa kiume. Binti alibarikiwa sura nzuri yenye mvuto pamoja na shepu la kwenda. Baadhi ya wateja walikuwa wanamtongoza na kumtaka kimapenzi bila kujali tumbo lake.
Wote waliomtongoza Radhia hakuna hata mmoja aliyemkubaliwa kwa sababu Binti hakutaka kabisa kuharibiwa mwanae wa tumboni. Lakini pia alitokea kuwaogopa sana
wanaume kwa kuamini kwamba wote akili zao ni kama Tony. Siku zikasonga huku tumbo la Radhia kukua na kuzidi kuikaribia siku ya kuingia leba. Bado aliendelea kufanya kazi kwa Mama P na kujiwekezea akiba kidogo kidogo kwa ajili ya kujifungulia. Miezi miwili ya mwisho kabla Radhia hajaingia leba, Mambo yakabadilika pale kwenye biashara. Biashara ikawa ngumu sana kama unavyojua kubadilka kwa misimu kunavyobadilisha hali ya biashara. Mambo yakaanza kuwa magumu kwenye ofisi ya Mama P kiasi kwamba faida ikawa haipatikani. Ikabidi sasa ofisi ifungwe kwa muda ili kupisha upepo mbaya. Sio Mama P tu, Hata akina Maman’tilie wengi walifunga vibanda vyao. Kwa kiasi kikubwa lile suala lilimuathiri sana Radhia pamoja na rafiki yake Landina ambao kuanzia muda huo hawakuwa na kazi. Kitu pekee ambacho kilikuwa na unafuu kwa Radhia ni kwamba tayari alishajiwekezea kiasi fulani kwa ajili ya kulipia gharama za kujifungulia.
“Radhia rafiki yangu. Mimi naenda Dar kutafuta maisha maana hapa Songea najichelewesha tu. Ni vile tu una tumbo lakini laiti kama usingekuwa na tumbo basi tungeondoka wote shoga yangu. Mimi nakuombea ujifungue salama rafiki yangu hayo mengine yatajulikana mbele ya safari.” Ni maneno ya mwanadada Landina akimuaga rafiki yake Radhia baada ya kuchoka kuishi kijijini. “Sasa Landina, Unaendaje mjini wakati hauna sehemu yoyote ya kufikia? Na unaenda kufanya kazi gani sasa?
“Radhia, Ule mji wa Dar ni mkubwa sana na kuna nyumba nyingi sana kwahiyo siwezi kukosa pakufikia. Lakini pia kuna kazi nyingi sana kule mjini kwahiyo siwezi kukosa kazi. Kiufupi nipo tayari kwenda kufanya kazi yoyote ile hata kuuza ndizi kwenye beseni ila sio kubaki hapa kijijini. Hapa kijijini maisha yanazidi
kuwa magumu sana kwangu maana sina kazi yoyote sasa hivi.
“Sawa rafiki yangu, Ni uamuzi mzuri sana maana ni kweli maisha yamekuwa magumu sana hapa kijijini. Jua kali, mazao yamekauka mashambani, biashara haziendi kwahiyo ni njaa tupu. Nenda kachonge njia rafiki yangu huenda mwaka wowote nami utanipokea huko mjini. Kiufupi natamani sana kama tungeenda wote lakini kwa hali yangu ya sasa nitashindwa kuhimili changamoto za mjini. Binafsi nakutakia bahati njema huko uendako na wakati unatafuta maisha yako, ukiyaona na ya kwangu naomba unichukulie.”
Hayo ni mazungumzo ya marafiki wawili, Landina pamoja na Radhia. Ni mazungumzo ya kuagana kwa marafiki hao wawili baada ya kuishi muda mrefu pale kijijini. Landina alifanya uamuzi wa kwenda Dar es salaam kutafuta maisha baada ya kushindwa kuyaona maisha yake pale Songea. Hata Radhia nae alitamani sana kama wangeondoka wote ila ndo hivyo tumbo lilimzuia kabisa. Landina alisafiri kutoka Songea mpaka ndani ya jiji la Dar es salaam kujaribu bahati yake.
****
[MIEZI MIWILI BAADAE]
Baada ya subra ya muda mrefu hatimaye Radhia akaingia Leba kwa ajili ya kujifungua. Kwa kudra za Mwenyezi Mungu, Radhia alijifungua salama na kubahatika kupata mtoto wa kiume. Aliamua kumpatia mtoto wake jina la Bahati huku akiamini imekuwa bahati kwake kumzaa salama mwanae licha ya changamoto alizopitia. Ni rasmi sasa Radhia akaingia katika ulimwengu wa kulea na uzuri ni kwamba bado alikuwa ana akiba ya pesa kidogo ambayo iliweza kumsaidia kuendeshea maisha kwa siku chache. Tukirudi upande wa pili, Tony alipata taarifa ya kujifungua kwa Radhia lakini hakuthubutu kwenda kumuona mtoto wala kumtafuta Radhia. Moyoni alikuwa anajua kabisa kwamba mtoto ni wake lakini alichagua kumkana na kujiweka mbali. Na kwa namna Mwenyezi Mungu anavyojua kulinganisha matukio, Yule mtoto alifanana sana na Tony. Hapo sasa baadhi ya watu wakamfikishia taarifa Tony juu ya muonekano wa mtoto huyo. Licha ya wambea kumfikishia Tony habari kwamba mtoto amesadifu sura yake lakini Tony akaendelea kukana kwamba yule mtoto sio mwanae. Muda huo Tony alikuwa bize na penzi la mrembo Kidawa.
Episode 05
Tangu Radhia alipojifungua maisha yakawa magumu sana upande wake. Ile pesa ya akiba aliyojiwekea ikawa inaisha siku hadi siku. Mahitaji yalikuwa mengi sana kuliko uwezo wake. Kitu pekee kilichozidisha hali ngumu ya maisha ni kwamba hakuwa na uwezo wa kwenda kutafuta kibarua wala kufanya biashara na mtoto mchanga. Ilifikia hatua alikuwa anakula kupitia msaada wa majirani zake. Suala la kulala njaa kwake ikawa kawaida. Radhia alipauka ngozi na kupoteza kabisa ule mvuto na uzuri wake. Maisha yalikuwa magumu sana kwake kiasi kwamba alihitaji sana msaada wa Baba mtoto wake lakini ndo hivyo Tony aliamua kuwatelekeza. Lakini mwisho wa siku kabisa akapata wazo la kumrudia tena ili aweze kuzungumza nae kwa mara nyingine. Radhia akaenda kwa Tony kutia huruma ili apate msaada. Alifika kwa Tony akamuelezea shida zote anazopitia yeye pamoja na mwanae. Kwa mara nyingine tena Tony akamfukuza Radhia na mwanae kama mbwa.
“Tony, Hii ndo mara yangu ya mwisho kabisa kuja kwako. Katu abadani isije ikatokea siku yoyote ukaniuliza chochote kuhusu huyu mtoto.
“Sawa ondoka, Nimeshakuambia huyo mtoto sio wangu. Sihitaji mzigo wowote kwahiyo niacheni huru na maisha yangu.
“Sawa Tony, Ahsante sana.”
Hivyo ndivyo Radhia alivyoagana na Tony kwa mara ya mwisho.
Radhia akaondoka na majonzi mazito sana nyumbani kwa Tony huku akiwa na mwanae mgongoni. Siku hiyo hali ilikuwa tete sana upande wake kiasi kwamba hakuwa na uhakika hata wa kula. Akiwa njiani alipata wazo la kwenda kule kazini anakofanyia kazi mama P. Alihisi huenda vibanda vitakuwa vimefunguliwa kwa mara nyingine baada ya miezi miwili kupita. Huo ndo ulikuwa msaada wa pekee kwa upande wake. Radhia aliamini kabisa kama atamkuta Mama P basi atampatia msaada hata wa kazi. Kwa bahati mbaya alipofika pale kibandani hakumkata mtu yeyote. Kibanda kilikuwa kimefungwa na mazingira yalionesha ni muda mrefu sana biashara haikufanyika eneo lile. Radhia akazidi kuchanganikiwa na kukata kabisa tamaa ya kuishi. Kila alipomtazama mwanae akajikuta anazidi kuandamwa na mawazo huku akitokwa na machozi. Aliwaza sana atafanya nini ili aweze kumlea mwanae kwenye mazingira kama yale. Muda huo akapata wazo la kumtafuta rafiki yake Landina huenda angeweza hata kumsaidia. Huyo sasa ndo alikuwa tegemeo la mwisho upande wake. Ni muda mrefu sana ulipita bila kuwasiliana nae kwani tangu Landina alipofika Dar es salaam namba yake ikawa haipatikani. Siku hiyo Radhia akajaribu tu kumpigia kwa mara nyingine lakini akasikia sauti ikimwambia namba anayoipigia imefungiwa. Radhia akajikuta anakata tamaa kabisa maana Landina ndo alikuwa tegemeo lake kubwa kwenye maisha yake. Siku hiyo Radhia alitembea sana bila kujua hata mahali alipokuwa anakwenda. Ni baada ya kutoka kijiji cha pili alipotembelea kwenye kibanda cha Mama P. Baada ya kutoka pale hakurudi tena kijijini kwao badala yake akawa anaranda randa kama chizi na mwanae mgongoni. Kila alipojaribu kuomba msaada alikosa. Mwisho wa siku akawa anatembea tu bila kujua mahali alipokuwa anakwenda. Safari yake ikamfikisha mpaka kwenye barabara kubwa ya lami iendayo mjini. Alisimama pembezoni huku akiyatazama magari machache yanayoenda mjini. Mpaka kufikia muda huo tayari yalishafikia majira ya saa 11 jioni. Kuna wazo jipya lilipanda kichwani mwake akiwa pale barabara. Alichokifanya ni kuanza kujikongoja kurudi kijijini kabla giza halijaingia. Mpaka kufikia majira ya saa 2:00 usiku, Radhia alikuwa tayari ameshafika kwenye kibanda alichokuwa anaishi. Alipofika tu atamtafuta mteja wa kitanda na godoro lake kisha akamuuzia. Aliuza kwa pesa ndogo sana ambayo hailingani kabisa na thamani ya vitu. Baada ya kuuza vitu vyake vya ndani akatandika nguo chini kisha akamlaza mwanae. Muda huo huo akaanza kupanga nguo zake kwenye kibegi kidogo cha mgongoni. Kwa namna alivyokuwa anaonekana ni wazi kabisa alikuwa anajiandaa kusafiri kuelekea mahali fulani kuishi. Ni kweli hilo ndo lilikuwa wazo lililomfika kichwani baada ya kuwaza sana. Radhia aliona ni bora aende mjini kutafuta maisha baada hali kuzidi kuwa tete upande wake pale kijijini. Aliamini kabisa huko mjini huenda ndo ridhiki yake ilipo na sio pale kijijini. Fikra zake zilikuwa kwenda ndani ya jiji la Dar es salaam. Aliamua kufuata nyayo za rafiki yake Landina kwa kuamini kwamba kati ya yale maelfu kwa mamilioni ya majumba basi hatoweza kukosa sehemu ya kuishi. Aliamua kuchukua uamuzi huo akiwa tayari kukabiliana na changamoto zote atakazokutana nazo ndani ya jiji hilo. Wapi atakwenda kufikia? Jibu la hilo swali alikuwa nalo Mungu ila yeye hakuwa na mwenyeji yeyote wa kumpokea. Mnamo majira ya saa 10 alfajiri Radhia akiwa na mwanae mgongoni alianza kutembea kuelekea kwenye barabara kubwa ya magari yaendayo mikoa mbalimbali kupitia mkoani Morogoro. Alitembea umbali wa lisaa zima kuitafuta barabara hiyo kwani ilikuwa mbali kidogo na kijiji alichokuwa anaishi. Alikatiza kwenye mapori na mashamba yaliyotenganisha vijiji. Hatimaye akaifikia barabara kubwa ya magari yaendayo mikoani. Pembezoni kidogo mwa barabara kulikuwa na kichaka fulani kidogo. Radhia alitazama kulia na kushoto, nyuma na mbele lakini hakuona mtu. Alichokifanya ni kuzama kwenye kile kichaka kisha akatandika khanga vizuri na kumlaza mwanae pale chini. Baridi ilikuwa kali sana pale msituni kiasi kwamba khanga aliyomfunika haikutosha kumkinga mtoto. Radhia akatoa sweta lake kwenye begi kisha akamuongezea kwa juu mwanae.
Alivua Bangili kwenye yenye rangi ya shaba kwenye mkono wake kisha akaivunja katikati. Kipande kimoja alikiweka juu ya kifua cha mwanae na kingine akakiweka kwenye begi lake la nguo. Baada ya kufanya hivyo akaanza kumtazama mtoto wake huku machozi ya uchungu yakimtoka. Muda huo katoto kenyewe kalikuwa kamelala. Muda huo magari ya kwenda mikoani yalishaanza kupita kule barabara. Radhia alimtazama tena mwanae pale chini kisha akasema;
“Bahati mwanangu, Samahani sana! Samahani sana mwanangu kwa kushindwa kukulea. Haya ni maamuzi magumu zaidi niliyowahi kuyafanya katika maisha yangu. Sina njia nyingine ya kuweza kukusaidia zaidi ya kukuacha hapa mwanangu. Naamini kabisa sehemu hii Mungu atakulinda na kukupatia mtu wa kukutunza na kukulea katika maisha yaliyo bora. Huko mjini ninakoenda najua naenda kuteseka kwa kuwa sina ndugu wala jamaa hivyo nikiondoka na wewe basi mambo yatakuwa magumu zaidi kwa sababu nitashindwa kufanya kazi. Tutakula nini kama sitofanya kazi? Tutaishi vipi kama sitofanya kazi. Sihitaji kukuona unateseka mwanangu. Nenda kaishi popote pale na wazazi wowote ilimradi usiteseke tu mwanangu. Wazazi sio kuzaa tu, wazazi ni kuhudumia watoto kwahiyo mimi na Tony hatustahili kuwa wazazi wako kuanzia sasa. Am sorry mwanangu, Ni changamoto tu za maisha ndo zinatutenganisha mimi na wewe.” Radhia alimbusu mwanae kwenye paji la uso huku akimdondoshea machozi. Yale machozi yalimfanya yule mtoto afumbue macho na kumtazama mama yake. Huwezi kuamini, Radhia akainuka na kuondoka huku akimuacha mtoto wake wa miezi mitatu pale kichakani. Kwa mbali kabisa akasikia sauti ya mwanae akilia lakini hakutaka hata kutazama nyuma. Alikaza roho kisha akaondoka kuelekea barabarani.
INAENDELEA………