UTAJIRI WA MAJINI ULIVYOITESA FAMILIA
PART: 03
ILIPOISHIA,
“Usiniue mme wangu.!.usiniue” Mundiri alibaki ameganda na kisu mkononi kwa mshangao mkubwa…
SONGA NAYO…
“‘Chinja huyo jogoo afu kinga damu hiyo!” Dr. Majini alipaza sauti kwa Mundiri ambaye alikuwa ameshikwa na butwaa.
Mundiri alimshika shingo kwa mara nyingine kisha akataka kumchinja lakini wakati kisu kinakaribia kwenye shingo, aliona sura ya mke wake huku akiwa amemuangalia kwa huruma.
Alibaki ameganda na kushindwa kumchinja kwa mara nyingine ndipo Dr. Majini alipomwambia,
“‘Safari hii ni ndefu na wala sio rahisi kama unavyodhani. Tunafanya hivi ili kurejesha nyota yako ambayo itakufanya kuwa tajiri mkubwa na mtu maarufu mkoa mzima wa Iringa hata nchi nzima. Kila unaowaona wanamiliki mali nyingi, basi jua wamepita kwenye mikono yangu. Kwa kuwa umeshakula kiapo, jini langu linasubiria damu na ukishindwa basi utauwawa wewe”
Kuambiwa hivo , Mundiri alifumba macho kisha akachukua kisu chake na kuanza kumchinja jogoo huyo.
Alikaza mkono wake lakini cha maajabu jogoo alishindwa kuchinjwa.
“Hapa kuna mchezo umefanyika!, kuna watu wanataka kunichezea akili. Sasa wewe rudi nyumbani afu nitakupa maelekezo mengine..”
Mundiri aliondoka kisha akapitia hospitali usiku huo kuona hali ya mke wake inaendeleaje.
Baada ya kufika hospitali, alikuta ndugu wa Suzy pamoja na majirani wakiwa wamekaa kwenye kibaraza kwa nje huku wakiwa wanaendesha maombi kwa sauti ya chini.
Mundiri alishutuka sana na kugeuza sura yake kisha akaingia ndani kabisa kimyakimya.
Aliomba kuonana na mgonjwa lakini alikataliwa kwani mda ulikuwa umeisha wa kuonana naye.
Basi usiki huohuo aliondoka kuelekea nyumbani ili kuwaangalia watoto.
Wakati yupo njiani, alijishika mfukoni na kujikuta ana shilingi elfu 5 tu.
Alisikitika sana . Alipiga moyo konde mpaka alipofika nyumbani.
Alishangaa kuona giza limetanda nyumba nzima huku watoto wake Aderck na Ivona wakiwa wanalia.
Aliingia ndani na kisha akawasha mwanga wa simu,
” Kwanini mnalia?” Aliwauliza.
” Njaa…” Aderck alijibu
” Hamjala!”
“Ndiyo ..”
” Na kwanini mpo kwenye giza?”
“Umeme wameukata..”
” Nani kaukata?”
” Ni mbaba fulani mnene kasema ukilipia umem utaunganishiwa tena..”
Mundiri aliishiwa nguvu kabisa.
Alitoka nje akiwa ameshika kichwa kisha akawanunulia Mandazi matatu mmoja mawili na mwingine moja.
Aliwaletea lakini Ivona alishindwa kula kwani alikuwa mdogo huku akimuita mama yake mda wote.
Akiwa katika hali hiyo, gafla alisikia mlango unagongwa kwa nje.
Alifungua na kuona kikundi cha watu watatu hivi.
” Karibu …” aliwakaribisha huku mmoja akiwa kama anamfananisha hivi.
” Asante tumeshakaribia” Yule aliyekuwa anamfananisha, alijibu.
Mundiri kwa hofu alisogea karibu ndipo alipowaona vizuri.
” Ohh kumbe ni wewe boss ” alimwambia baba mwenye nyumba.
” Ndiyo sahamani lakini naomba usinichukulie vibaya..” baba mwenye nyumba aliongea..
” Kuna nini?” Mundiri aliuliza.
” Naomba uwafungulie hawa wapangaji wapya wanataka kuangalia nyumba jinsi ilivyo maana wewe tumeshindwana. Ni mwezi wa pili sasa umepita hujalipa kodi..”
” Boss wangu nakuomba sana univumilie kwa siku chache hizi nitakupa hela yako. Hapa nilipo mke wangu anaumwa yupo hospitali hela yote imeishia kwake na sijui anatoka lini . Nipo chini ya miguu yako naomba unisaidie..”
.
” Hii ni biashara kama biashara nyingine, leo hii watoto wangu wamefukuzwa shule kwa sababu ya Ada . Sasa matatizo yako hayawezi kuathiri familia yangu. Nakuomba uondoe mizigo yako braza..” Baba mwenye nyumba aliongea.
“Nionew huruma nami mwanaume kama wewe, sio kwamba napenda lakini imetokea hivo lakini nakuhakikishia hela yako ntakupa. Nimepitia kipindi kigumu sana hasa biashara zangu kuyumba ndo maana nipo hivo. Nipe hata wiki 1 nijichange..”
Mundiri alibembeleza kama mtoto mdogo huku machozi yakimlengalenga machoni.
“Unaponiona hapa, nimeshalipwa hela ya mwaka mzima kutoka kwa wapangaji hawa hivo basi sina ujanja mwingine na hela nimeshaitumia”
Mundiri alibaki anakuna kichwa ndipo alipojaribu kupiga simu kwa rafiki zake ili wamkopeshe lakini aliambulia patupu.
“Basi njooni kesho ili nipate pa kuweka mizigo yangu” mundiri aliongea kwa uchungu.
“-Sawa kesho saa nne nyumba iwe wazi..”
Waliondoka na kumuacha Mundiri akiwa anawaza na kuwazua .
“Kwanini mimi lakini?, nimekosa nini duniani humu?” Alijiuliza maswali ambayo hayakuwa na majibu.
Usiku huohuo, alianza safari ya kwenda kwa Dr. Majini mara baada ya kuwaacha watoto wakiwa wamelala.
Mnamo mida ya saa 6 za usiku,,alifika kwake na kubisha hodi kisha akafunguliwa.
“”Karibu mbona umerudi kuna nini?”
” Dr. Hapa nina mawazo mpaka kichwa kinaniuma sana…”
” Kuna nini?”
” Nyumbani nimekatiwa umeme, na baba mwenye nyumba kanipa notice kesho niondoke. Mfukoni hapa nina 2000 tu na sina chakula hata nyumbani..”
” Kwahiyo unataka nikusaidieje?”
“Shida yangu niweze kupata pesa za haraka kama inawezekana…”
“Inawezekana ila itabidi umtoa kafara mtoto wako mmoja mda huu “
“Dr. Hakuna njia nyingin hata kumtoa baba mwenye nyumba kafara?”
” Hapana unatakiwa kutoa kafara kwa mtu wako wa karibu au mtoto wako”
Aliinamisha kichwa chake chini…
” Upo tayari?” Alimuuliza.
“Ndiyo nipo tayari ..”
” Sawa kwakuwa ni mtoto, nenda ukamuamshe kisha mtembeze kwa nje miguu tupu kisha zoa udongo uliokanyagwa na unyayo wake afu niletee”
“Sasa Dr. Si watajua kuwa nimemuua?”
” Hakuna atakayejua…”
” Sawa ngoja niende nakuja mda si mrefu..”
Mundiri akiwa kama amepagawa hivi, alielekea nyumbani na baada ya kuwasiri, alimchukua Ivona mtoto wake wa pili mwenye umri wa mwaka mmoja na nusu kisha akamkanyagisha kwenye udongo kwa nje.
Baada ya kukanyaga, alizoa mchanga huo na kuufunga kwenye mkuko.
Alimrudisha ndani kisha akambembeleza mpaka aliposinzia.
Bila kuchelewa, Mundiri alianza kuelekea kwa Dr. Majini huku akiwa ameshajitoa mhanga liwalo na liwe ili apate pesa.
JE MTOTO IVONA ALIPONA?
JE PESA ALIPATA AU LA?
PART: 04
Mnamo usiku wa manane huku mwili mzima ukiwa umelowana jasho, Mundiri aliwasiri tena kwa Dr. Majini akiwa ameshikilia mfuko mweusi wa nailoni ambao kwa ndani ulikuwa na udongo kutoka kwenye nyayo za mtoto wake mchanga aitwaye Ivona.
“Karibu tena…” Dr. Majini alimkaribisha Mundiri.
“Asante..” Mundiri aliitikia huku akiwa anapumua kwa haraka kweli.
Alimkabidhi mfuko huo kisha akatia udongo kwenye kibuyu kidogo sana ambacho kilikuwa kinateleza kama upara wa mzee mwenye pesa.
Alimimina na dawa nyingine pamoja na manyoya ambayo aliyatoa kwenye mkia wa chui.
Baada ya kufanya hivo, alichekecha kibuyu hicho huku akiimba nyimbo ambazo Mundiri hakuweza kujua ni lugha gani.
Ndani ya dakika kama 5 hivi, Mundiri alisikia sauti ya mwanawe ikitokea kwenye kibuyu hicho kidogo huku akilia.
Aliogopa sana na kumwambia Dr. Majini,
“‘Samahani, sikujua kama mtoto atalia kiasi hiki! Naomba kama kuna njia nyingine tofauti na hii ndo utumie kwani moyo wangu unaumia..”
“‘Hee!, kutoa roho ya mtoto sio kazi ndogo hivo unapaswa kuvumilia na zoezi litachukua dakika 40 mpaka lisaa limoja”
Baada ya kuambiwa hivo, Mundiri aliinamisha kichwa chini kisha akaendelea kusubiria huku mapigo ya moyo yakimuenda kasi sana.
Wakati mambo yako hivo, huko nyumbani, mtoto Ivona mwenye umri wa mwaka mmoja na nusu, alianza kupiga kelele sana na kulia kwelikweli hasa Dr. Majini alipochekecha kibuyu chake.
Tumboni mwake alihisi mkuki unachoma na kuachia.
Kwakuwa alikuwa mdogo sana, Ivona hakuweza kuongea hali iliyomfanya azidi kupiga kelele mpaka ndugu yake Aderck aliyekuwa na miaka mitano alipoamka.
“‘Baba…baba…” Aderck aliita bila kujua baba yake hayupo .
Baada ya kuita bila kujibiwa, aliamka akawasha Tochi kisha akammulika mdogo wake aliyekuwa anajiviringisha kwa maumivu makali sana.
Alijaribu kumbemba na kumbembeleza kama alivyokuwa anafanya mama yake lakini haikuwezekana.
Aderck alishindwa nini cha kufanya ndipo alipomtoa kitandani na kumuweka sebuleni.
Kwakuwa ilikuwa usiku wa manane huku pakiwa pametulia, Aderck aliamua kupiga yowe kama kuashiria hali ya hatari ndipo Masumbuko na mkewe waliposhutuka na kuulizana,
“Hee ina maana watoto wamewaacha peke yao?” Masumbuko aliuliza.
” Kwani wameenda wapi?”Mke wa Masumbuko aliuliza.
“‘Kang’atwa na nyoka na kukimbizwa hospitali..”
“Heee!”
“Ndo hivo…”
Waliamka haraka kisha wakafika nyumbani kwa Mundiri ndipo walipokutana na kilio kikali kutoka kwa mtoto Ivona.
Bila kuchelewa, waligonga mlango ndipo Aderck alipofungua huku akidhani ni baba yake.
Masumbuko na mkewe, waliingia ndani na kubaki wameduwaa kwa jinsi walivyomuona mtoto Ivona akijirusha.
“‘Baba yako kaenda wapi?” Masumbuko alimuuliza Aderck.
“‘Baba sijui kwenda ..mimi lala mtoto analia”‘Aderck alijibu.
Mke wa Masumbuko maarufu kama mama Masumbuko, alimnyanyua Ivona kisha akaanza kumbembeleza lakini hakusita kulia .
“Mhh..mtoto huyu atakuwa anaumwa au kang’atwa maana anahisi maumivu..'”Mama Masumbuko alimwambia mmewe.
“‘Sasa tunafanyaje maana wazazi wake wapo hospitali..!”
“‘Hakuna namna nyingine tofauti na kumkimbiza hospitali…”
“‘Sawa si kwanza tuwapigie simu?” Masumbuko aliuliza.
“‘Hapana mme wangu, ebu vaa haraka twende uzuri tuna pikipiki ndani yatajulikana huko..:’Mama Masumbuko aliongea.
Masumbuko alimchukua Aderck na kwenda naye kwake kisha akampeleka chumbani kulala pamoja na watoto wake.
Bila kuchelewa, alitoa pikipiki mpaka kwa Mundiri .
Walimfunga milango yote kwa usalama na kuanza safari ya kuelekea hospitali ambayo haikuwa mbali sana.
Mtoto alizidi kupiga kelele huku mama Masumbuko akiwa amemkumbatia kwelikweli.
Wakati wanakaribia kumfikisha hospitali, Dr. Majini aliona zimesalia dakika chache sana kabla ya mtoto huyo kutolewa kafara.
Aliongeza kasi sana kwa kuchekecha kibuyu hicho kisha akakiweka chini ndipo Mama Masumbuko aliposhangaa kuona mtoto huyo kanyamaza gafla.
“‘Hee! mbona kanyamaza gafla?” Alimuuliza mme wake ambaye alisimamisha pikipiki.
“‘Anajitingisha au kakata roho..?” Alimuuliza huku mapigo ya moyo yakimuenda kasi.
“‘Bado kwa mbali anapumua…””Mama Masumbuko aliongea.
“Mke wangu, ebu mshike vizuri na Mungu atusaidie tufike hospitalini akiwa mzima kwani tofauti na hapo sijui kama watatuelewa kwani tumefanya kosa kumleta bila kuwajulisha…”
“Hee! Kwamba sisi ndo tumemuua au!?, hilo haliwezi kutokea ebu twende mme wangu”
Waliendelea na safari na hatimaye walifika hospitalini ndipo waliposhuka.
Ile Mama Masumbuko anataka kuingia na mtoto huyo ndani, gafla alishangaa kuona hajitingishi tena ndipo…
JE ILIKUWAJE?
PART: 05
Baada ya kuona mtoto hajitingishi, mama Masumbuko alihaha kweli huku akikimbilia hospitini.
Ile anafika mlangoni, alikutana na mhudumu ambaye alimuangalia mtoto kisha akamwambia,
“‘Mtoto huyu ashapoteza maisha kama inawezekana mnaweza kuondoka naye ili kupunguza gharama..”
“‘Hee!, ” Mama Masumbuko alipigwa na butwaa huku akiwa hajui nini akifanye na mmewe.
Wakati wanawaza na kuwazua, Masumbuko aliamua kumpigia simu Mundiri kisha akamueleza yote yaliyotokea.
Mundiri aliyekuwà kwa Dr. Majini alipewa kitita cha shilingi milioni moja kama mkopo kisha akaaga.
Kwakuwa alishapewa taarifa, aliunganisha moja kwa moja mpaka hospitalini ndipo alipowakuta Masumbuko na mkewe wakiwa wamekaa pembeni huku wamemfunika mtoto.
“‘Enheeh! , taarifa ulizonipa ni kweli au ?”aliuliza kwa mshangao.
“‘Ni kweli mtoto huyu hapa kashapoteza maisha na tumeongea na mhudumu akasema kwakuwa ni usiku basi tuondoke naye ndo nikaamua kukutaarifu..” Masumbuko aliongea.
Mundiri alifunua kanga taratibu ndipo alipokutana na maiti ya mtoto wake hali iliyomfanya aanze kufoka sana.
“‘Hee!, mmeuua mtoto wangu!..mmemuua mtoto wangu!, sikubali akafanyiwe vipimo..”
“Jamani yamekuwa hayo tena!, mtoto tumemtoa akiwa analia sana sasa sababu ipi mpaka tumuue!” Masumbuko aliongea kwa mshangao.
” Mtoto wangu hakuwa anaumwa chochote na nimemuacha salama sasa leo hii hapumui tena!, sikubali hata kidogo…”
Ndani ya mda mfupi, watu walikusanyika ndipo.waipoubeba mwili wa mtoto huyo kwenda kuufanyia vipimo kuona nini kimemuua.
Wakati mchakato wa vipimo unaendelea, Masumbuko na mkewe waliwekwa chini ya ulinzi mkali sana.
Walijaribu kujitetea lakini Mundiri hakuwapa hata nafasi ya kuongea.
Habari zilisambaa kwa haraka mpaka Suzy akazipata juu ya mwanaye kupoteza maisha.
Alinyanyuka kwa mshutuko mkubwa licha ya kutokuwa na nguvu mpaka nje.
Baada ya kufika nje, alikuta watu wamewazunguka Masumbuko na mkewe.
” Naomba mwanangu!..naomba mwanangu!, hajawahi hata kuumwa iweje leo?” Suzy aliongea akilia huku akitaka kuwaponda na tofali.
” Kwanini mnatusingizia kumuua mtoto mdogo ambaye hana hata makosa !, tuna ubaya gani na mtoto huyu!, kama kweli mmeamua kututwika mzigo huu basi …” Mama Masumbuko aliongea kwa uchungu.
“Unaongea nini sasa!” Suzy alimjia juu na kutaka kumng’ata.
Walimshika kwa mara nyingine kisha wakawakamata Masumbuko na Mkewe na kuwahifadhi chumba cha emergence.
Wakiwa katika chumba hicho, Mama Masumbuko alianza kulia huku akimwambia mme wake,
” Mme wangu!, wema wako unatupeleka jela na hii kesi hatuwezi kuikwepa. Nilishakwambia mambo ya familia za watu tuyaache sasa ona. Nani atakuwa mlezi wa watoto wetu?, nani atalinda nyumba na mali zetu?”
” Mke wangu!, tulia na nisikilize!, ni kweli kesi ni ngumu hasa kwa kukosa kutoa taarifa kipindi tunamleta lakini kwakuwa kaenda kupimwa na haonekani kuwa na jeraha, basi watatoa majibu. Kuwa na amani hizi ni changamoto tu ..”
Masumbuko alimwambia mkewe.
“Usichukulie simple suala hili!, hata kama hatujahusika akilipeleka mbele ya sheria tutakaa ndani kwa mda mrefu jambo ambalo litakuwa limetuathiri sana!..”
” Subiri majibu mke wangu wala usipanic”
Baada ya mda mfupi, Madaktari walikamilisha vipimo vyote lakini hawakuona ugojwa wowote wala dalili yoyote…
Walimpatia Mundiri majibu ndipo alipozidi kuwaka na kusema,
” Haiwezekani afariki bila sababu yoyote!, mda huu naomba mnisindikize tuwapeleke kituo cha polisi” Mundiri aliongea.
” Wakati mwingine anaweza kupoteza maisha kutokana na mshutuko hivyo usishangae” Daktari aliomwambia Mundiri.
Mundiri hakutaka kuelewa chochote kile ndipo alipoamua kufanya maamuzi magumu.
Vilio na kusaga meno vilitawala hospitalini hapo mpaka wakawatuliza kwa nguvu ili wasiwapigie watu kelele..
” Sasa mda huu naomba twende wote mpaka kituo cha polisi ndo wakajibu mashitaka. Sijakubaliana na maelezo yao maana madaktari wanadai hana ugonjwa wowote..”.
Wakati Masumbuko na mkewe wanasubiliwa kuburuzwa polisi, Suzy hali yake naye iligeuka gafla mara baada ya kudondoka chini huku akiwa hawezi hata kuongea.
“Hee! Nini tena hii!” Ndugu zake na Suzy walishangaa ndipo walipombeba na kumrudisha wodini huku akiwa haongei wala hajitingishi….
JE ILIKUWAJE?
INAENDELEA…………