TULICHOMFANYA YULE MCHAWI HATAKUJA KUSAHAU KAMWE
SEHEMU YA 21
Safari ikazidi kusonga kuelekea kusiko julikana.Ilikuwa muda wa usiku sana na giza lilikuwepo kiasi,kiasi fulani kulikuwa na nuru ya mbala mwezi.Tulitembea tukiwafuata wale watu ambao mpaka wakati huo hawakufahamu kama tulikuwa nyuma yao!.
Sasa kuna mahali walifika yule wa mbele akampatia mwenzie aliyekuwa nyuma ishara ya kwamba inapaswa wasimame,waliposimama pale kwa muda ndipo kuna watu wengine ambao nilipowahesabu walikuwa ishirini,sasa ukijumlisha na wale wa lile kundi la kwanza ambao walikuwa wa tano akiwemo Headmaster pamoja na Ema,jumla yao ilifanya kundi lote la watu kuwa ishirini na tano.Basi ndipo nikamuona yule mzee Makono akiwa kwa mblele akiongoza jahazi huku akiendelea kuimba nyimba za kisukuma na wenzie kuitikia.
Baada ya safari ya muda mrefu ndipo sasa tukafika kulipokuwa na mashamba yaliyokuwa yamepandwa mtama,ule ulikuwa mtama kwasababu nilikuwa ninafahamu namna mahindi yalivyo na mtama ulivyo hata ukiwa bado haujakomaa,kwahiyo sikuwa na shaka kabisa kwamba lile lilikuwa shamba la mtama kwasababu pia lilikuwa shaghala baghala,tofauti na mahindi yanayopandwa kwa kuacha nafasi na kwa mstari!.Walipofika hapo mzee makono alipiga mruzi kama vile anachunga ng’ombe.
Basi wale jamaa waliokuwa wakimsaidia ile kazi walikimbia kuelekea mbele ambapo walianza kuwapanga wale watu na kuwapa majembe,majembe yale hayakuwa kama haya ambayo sisi tunalimia kawaida,yale yalikuwa kwa mbele yamechongoka kama Mundu!.Baada ya kukabidhiwa yale majembe kila mtu alikuwa akipewa ishara na kuanza kulima kwa spidi kali mno!.
Hakuna jambo ambalo mpaka leo siwezi kusahau kama lile la watu kulimishwa kichawi huku nikiwa nashuhudia kwa macho yangu,miaka ya nyuma kwa stori za vijiweni nilidhani yawezekana ikawa tu stori watu wanajitungia lakini baada ya kushudia mimi mwenyewe ndipo nikaamini kwa hakika uchawi upo na unafanya kazi kubwa mno!.Kwa spidi ile waliyokuwa wanatumia wale watu kiukweli haikuwa ya kawaida!.Niliendelea kumtazama Headmaster na Ema wanavyohenyeshwa kuna muda huruma iliniingia sana lakini sikuwa na nmna!.
Kutokana na ule udharirishaji wa Ba’mdogo mbele ya wanafunzi niliona kabisa anachokipata ndicho anachokistahili,ningeweza kumwambia Monica amwambie mama yao awasaidie lakini niliona ngoja wapitie shubiri,kwa upande wa Ema sikuwa kabisa na huruma nae na nilitaka amenyeke kishenzi maana alikuwa na mdomo mrefu sana!.
Monica “Huyo ndugu yako juzi nilimwambia akajifanya mjanja,ngoja wamfundishe adabu”
Mimi niliendelea kutulia na kujionea mwenyewe huku moyoni nikifurahia kupendwa na Monica maana isingekuwa hivyo na mimi uenda ningekuwa ni miongoni mwa wahenyeshwaji!.Wale watu walipalilia lile shamba bila kupumzika hata kidogo!.
Mimi “Hivi hawachoki?”
Monica “Unataka ukajaribu?”
Mimi “Hapana,mi nimeuliza tu!”
Monica “Hapo hakuna kuchoka,utaenda kuchoka huko kwako lakini hapo hauchoki”
Basi tuliendelea kutazama lile shuruba walilopata wale watu na kiukweli hakukuwa na huruma hata punje!.
Baada ya muda mrefu kupita,ndipo nikasikia tena mruzi unapigwa kwa nguvu!,alikuwa ni yuleyule mzee makono akatoa ishara ya kwamba wamemaliza lile eneo na kilichofuata ni kuhamia eneo jingine ili kazi ya kulima iendelee!.Lile zoezi lilimaliza kukiwa kunakaribia mapambazuko kabisa!.
Monica “Tuondoke”
Mimi “Nyumbani?”
Monica “Nikurudishe kwenu niwahi kwenda kulala”.
Mimi “Wamemaliza”
Monica “Pakishapambazuka kama hivi hakuna ujanja,watawarudisha tu”
Basi tukaondoka lile eneo mpaka nyumbani,tulipofika nyumbani Monica hakutaka kuondoka na akanitaka kile kibuyu nilichokuwa nimekishika nikiweke pale pembezoni ya mlango kama ilivyokuwa mwanzo na akanitaka nisimame nae pale ukutani mpaka Ema na Ba’mdogo watakaporejeshwa!.
Basi haukupita muda kuna jamaa aliingia na Ema mpaka ndani akawa amemlaza pale kitandani!,sasa ile jamaa anataka kutoka ni kama alikuwa na mashaka sana akaanza kuangaza chumba kizima lakini hakuona chochote!,ndipo akawa ametoka nje!.Sasa wakati Monica anataka kutoka pale tulipokuwa akanibana tena na kunitaka nitulie kimya kabisa!,mara ghafla aliingia mle chumbani mzee makono na yule jamaa aliyemlaza Ema pale kitandani!,walijaribu kuangaza chumba kizima lakini mzee makono nikaona ni kama alikuwa na mashaka!,basi wakazungumza na yule jamaa kisukuma kisha wakawa wametoka nje!.Kiukweli niliingiwa uoga na hofu kubwa mno!.
Mimi “Hawajatuona kweli?”
Monica “Hivi unamjua mama yangu au unamsikia?”
Aliendelea “Mama ndiye mkubwa hata huyo mzee haoni ndani,mama hajawahi kushindwa!”
Monica “Hivi Umughaka huwa huniamini ninapokwambia nitakulinda?,wala hakuna anayeweza kutuona hapo,hao ni wadogo sana mbele ya mama”
Baada ya kunihakikishia hivyo kiukweli sasa moyo wangu ulipata amani!.
Monica “Mimi naondoka,nikuombe usimuamshe huyo ndugu yako mpaka atakapoamka mwenyewe”
Aliendelea “Jioni nitakuja kukuchukua,Bibi yangu aliyemzaa mama anakuja na mama alisema nije kukuchukua nikakutambulishe”.
Mimi “Sawa”
Baada ya kuniambia hivyo akawa ametoweka,nilimuitikia kishingo upande nilakini moyoni sikutaka kabisa kwenda kwao maana niliogopa viboko na adhabu ya Ba’mdogo,sikuwa na namna ilibidi niwe mtumwa wa penzi la Monica,ingawaje kuna muda niliona kabisa ananipenda na ndiyo maana mimi sikupata taabu na shuruba za wachawi pale kijijini,zile feva zilifanya nikampenda sana Monica!.
Baada ya Monica kuondoka na kile kibuyu ndipo nilivua zile nguo nilizokuwa nimevaa nikaavaa nguo nyingine na kupanda kitandani!,sasa nilipopanda kitandani ndipo kumuangalia Ema miguuni nikakuta bado anatope la shambani!,sasa sikufahamu ndiyo ulikuwa utaratibu wao au walijisahau kuwaosha au waliwaacha vile kwa kusudi la kuwakomoa,nilipanga lile swali ningeonana na Monica nimuulize!.Muda huo ilikuwa saa 11 alfajiri,sikuweza kabisa kulala niliamua kushuka kwenye kitanda na kwenda kukaa kwenye kiti.
Siku hiyo sikuwa na haraka kabisa ya kwenda kufata miwa nilitaka Ema aamke nione ataniambia nini!.Sasa ilipofika saa 12 asubuhi jamaa bado alikuwa amelala huku akiendelea kujigeuza geuza kitandani akichafua shuka na yale matope!.
Nilichukua mswaki nikaanza kusukutua na kunawa uso hapo kando ya bafu!,sasa wakati nikiwa ndani nilimsikia Maza mdogo akiita “Emaaaa…..” wewe Emaaaaa”.
Baada ya kuona aliyekuwa anamuita haitikii akaanza kuniita “Umughaka!”
Mimi “Naaam”
Basi nikaenda nikafungua mlango wa sebuleni ambao mara zote ulikuwaga unarudishiwa tu kwakuwa haukuwa na komeo!.
Mimi “Mama shikamoo”
Maza mdogo “Marhaba”
Aliendelea “Hebu ingia”
Mimi “Wapi mama,huko?”
Maza mdogo “Ndiyo,njoo”
Basi nikausogelea mlango nikagonga ndipo mama mdogo akaja kunifungulia!.
Maza mdogo “Hebu muangalie baba yako mdogo”
Basi nilipomtazama dingi mdogo miguuni pia alikuwa na tope la kufa mtu!.
Mimi “Amelitolea wapi?”
Maza mdogo “Mi sijui kwakweli,hii nyumba mbona kila siku maajabu hayaishi!”.
Mimi ” Kwani Ba’mdogo hakutoka kweli?”
Maza mdogo “Huyu usiku kucha nimelala nae hapa,atoke usiku aende wapi?”
Niliamua kukausha na sikutaka kabisa kufungua domo langu na kumueleza mtu jambo lolote!.,Pengine ningewaambia kwa makusudi mema tu lakini nikaogopa wasije kunituhumu na mimi ni mshirikina!.
Maza mdogo “Baba Mary……wewe baba mary”
Maza mdogo “Amka basi”
Ba’mdogo aliendelea kujigeuza kana kwamba yuko kwenye godoro la sita kwa sita kumbe kigodoro chenyewe kilikuwa kidogo tu cha kusukimia maisha pale kijijini!.
Basi mimi ilibidi nitoke nje ili niwache wao humo ndani wakiendelea kuamshana!.Sasa nilipoingia chumbani kwetu nilikuta Ema akiwa ameshaamka na miguuni hakuwa na tope,inaonekana wakati mimi nikiwa kule chumbani kwa Headmaster yeye baada ya kuamka alienda kunawa,hata lile shuka lililokuwa limechafuka alikuwa amelitoa na ametandika shuka jingine!.
Sasa nikasubiri aongee jambo lolote lakini jamaa akapiga kimya,pengine alidhani uenda sifahamu chochote,kimoyo moyo niliona kabisa hata ile adhabu aliyokuwa amepewa ilikuwa ndogo kutokana na namna alivyokuwa na kiburi!.
Haukupita muda ba’mdogo naye akawa ameamka kutoka chumbani kwake akawa ametoka nje!.
Ba’mdogo “We Umughaka”
Mimi “Ndiyo ba’mdogo”
Nilitoka nje kuona alichokuwa ameniitia.
Ba’mdogo “Huyo yuko wapi?”
Mimi “Yupo chumbani Baba”
Mimi “Ema”
Ema “Eeenh”
Mimi “Njoo unaitwa”
Ba’mdogo “Hivi na nyie mmefanywa hivi kama mimi?”
Wakati Ba’mdogo anazungumza alikuwa akizuonyesha miguu yake iliyokuwa imejaa matope.
Mimi “Hapana baba mimi kwangu sijaona”
Ema “Hata mi kwangu sijaona”
Hapo ndipo nikajua Ema anaweza asiwe na akili timamu,yaani alidhani mimi sijamuona miguuni akiwa na matope!,sasa nilishindwa kuelewa kwanini alikuwa akificha,hiyo yote ni kwamba alidhani mimi nitamcheka na kwenda kumtangaza!,kiukweli nilibaki namshangaa!.Sasa nikawa najiuliza lile shuka atalifuaje?,nilibaki kumshangaa tu kiukweli!.
Ba’mdogo “Haya mambo hapa kijijini yameshakuwa ya kawaida na tukijaribu kuyasema hatueleweki”
Aliendelea “Yule mzee nae akaja hapa nikampatia mpaka hela lakini hamna alichokifanya”
Sikutaka kabisa kusema jambo lolote,mzee aliyekuwa akimsema ni yule ambaye wakati wa kuchezwa ngoma pale kwao Monica alishapewa adhabu na kuliwa kabisa!.
Ba’mdogo “Nataka nifanye tukio kubwa hapa kijijini kwa hawa washenzi ndipo niondoke”
Ba’mdogo “wao si wanajifanya wajanja!,ngoja uone”
Basi baada ya tafakari na kushangaana pale kila mtu aliendelea na mambo yake,mimi kama kawaida sikutaka kupoteza muda nilielekea kuchukua miwa.
SEHEMU YA 22
Baada ya kufika senta niliendelea na biashara yangu ya uuzaji wa miwa kama kawaida!,sasa ilipofika jioni muda ambao wanafunzi walikuwa wametoka shule,nilimuona Mwise siku hiyo tena akiwa na marafiki zake wakiwa wanakuja hapo senta,safari hii sikutaka kabisa mazoea na mtoto wa mtu,niliamua kuuchuna na sikuwa na shobo nae kabisa!.Sasa yeye alidhani uenda ningemuita ila mwanaune niliamua kula buyu la hatari!,alikuwa anajiangalisha kwangu lakini kila nikimcheki kwa jicho la kuibia najifanya kupiga stori na jamaa yangu aliyekuwa akiuza kata mbuga.
Walipo maliza kufanya kilichokuwa kimewapeleka hapo senta waliondoka huku mimi nikijifanya niko bize kipiga stori na jamaa lakini kiukweli moyo wangu ulikuwa unauma sana!.Siku hiyo mama mdogo hakuka kabisa hapo senta na sikufahamu sababu ni nini!.
Ilipofika jioni mida ya saa 12 nilirudisha ile miwa iliyokuwa imebaki kwa yule mama na mimi kuianza safari ya kurejea nyumbani.Nilifika nyumbani mida ya saa 1 usiku kuelekea saa 2,niliingia jikoni nikachukua dumu la maji nikaondoka zangu kuelekea lamboni kuchota maji ili nije kuoga nijiweke safi kwasababu Monica alikuwa ameniambia angekuja kunichukua!.
Sasa wakati napandisha nyumbani nikakutana na Ema akiwa bado amevaa nguo za shule akiwa na Deborah,mimi napandisha na wao wakiteremsha!.
Deborah “Mambo umughaka”
Mimi “Poa,vp?”
Deborah “poa!,aya baadae!”
Nilipata mashaka kidogo kwasababu haikuwaga tabia ya Deborah nikionana nae kuacha kupiga stori na mimi,sikuumiza kichwa sana maana niliamini mpumbavu Ema atakuwa amenikandia sana kwa demu wake!,kwasababu hata wakati Deborah ananisalimia jamaa alikuwa anajitembeza taratibu huku akinikaushia!.Basi nilibeba zangu dumu nikanyoosha zangu nyumbani!.
Nilipomaliza kuoga niliingia jikoni fasta kupika ili atakapokuja Monica akute nikiwa nimemaliza kila kitu!.Kama nilivyosema hapo awali ya kwamba,kule kwenye kile kijiji kutembea usiku haikuwa shida,shida ilikuwa ni wachawi tu,lakini mambo ya wezi na majambazi hayakuwepo kabisa,kuna matukio machache sana yaliwahi kufanyika kule senta yaliyohusu wezi lakini yalikuwa yakuhesabika na hayakujirudia tena!.
Nilipomaliza kupika nilichukua sinia nikafunika ugali nikauweka mezani,kisha nikachukua mabakuli ya mboga nikapakua mboga kisha nazo nikapeleka sebuleni,sasa niliendelea kuona ndani kwa Headmaster kuko kimya hata mwanga wa taa au tochi haukuonekana!.Nilisogea karibu nikaanza kugonga ule mlango kuwakaribisha kwa ajili ya chakula lakini nikaona kimya!,nilipoangalia vizuri mlangoni nikakuta kuna kofuli,basi niliamini watakuwa wametoka.
Basi nilichukua sahani nikakata ugali wa kunitosha size yangu nikaanza kula!.Nimekula mpaka namaliza si Ba’mdogo wala Maza mdogo aliyerudi,nikakumbuka uenda kwa kuwa ilikuwa ijumaa labda watakuwa wameondoka kwenda mjini,lakini isingekuwa rahisi kwasababu niliondoka kwenda senta nikawaacha hapo nyumbani,halafu pia ile Hiace ya kuelekea mjini ilikuwaga inaondoka saa 12 asubuhi,niliamini uenda watakuwa wametoka tu na walikuwepo hayo mazingira ya kijijini.Kilicho fanya pia kujiuliza uenda wakawa wameenda mbali ni kitendo cha Ema na mpenzi wake Deborah kujiachia usiku ule bila presha!.Nilirudishia ule mlango wa sebuleni nikarudi zangu chumbani kwetu!.
Mpaka inafika mida ya saa 3 sikumuona Ema na nikajua kabisa headmaster na mkewe watakuwa wameenda mbali.Mpaka muda huo sikumuona Monica hivyo nikaamua kujilaza huku nikiwa namsikilizia.
Haukupita muda nikasikia mlango wa nje unagongwa!,nilienda kuufungua ndipo nilikuta alikuwa Monica!.
Mimi “Karibu”
Monica “Ulikuwa umelala mpenzi wangu?”
Mimi “Nimekusubiri sana”
Monica “Nilikuwa napika,nisamehe”
Mimi “Sikunyingine usiwe unagonga bhana utaniletea shida!”
Monica “Unadhani mimi mjinga?”
Aliendelea “Nimejua hawapo ndiyo maana nimegonga”
Mimi “Umejuaje?”
Monica “Twende nyumbani tunachelewa”
Basi niliingia ndani nikavaa viatu nikatoka zangu,nilifunga ule mlango wa chumbani kwetu na komeo lakini sikuweka kufuli!.Ule wa nje nilirudishia tu tukaondoka zetu na Monica.Mara ya kwanza kutembea na Monica ilikuwa ni kutuliza tu uwendawazimu wa abdala kichwa wazi lakini sikumpenda kabisa,sasa kadri siku zilivyokuwa zikienda ndivyo ulikuwa uniambii kitu kwa yule binti wa kisukuma na kiukweli kuna wakati nilikuwa naona ni kwanini nilichelewa kumfahamu maana alikuwa akinijali sana,licha ya kwamba papuchi ilikuwa ni moja ya sababu ya kumpenda lakini sura yake nzuri pia ilinivutia zaidi,alichokuwa amekosa yule binti wa kisukuma ni matako makubwa tu ambayo ndiyo ulikuwa ugonjwa wangu wakati huo,lakini kwingine kote alikuwa amekamilika binti wa watu wala nisimseme vibaya!.
Mimi “Umeambia ulijua hawapo,umejuaje”
Monica “Nishakwambia mpenzi wangu usiwe unauliza uliza maswali,utaelewa tu siku moja”
Aliendelea “Nimemuona ndugu yako wakati nakuja akiwa na mpenzi wake”
Mimi “Umekutana nao?”
Monica “Kuna mahali nimewaona wanaongozana”
Mimi “Nadhani tupite pale kwao Deborah ili nikamuulize kama headmaster ametoka anarudi au harudi maana muda umeenda”
Monica “Ningekwambia lakini unaweza usiniamini,twende ukamuulize!”.
Basi tulichepuka na kuacha ile njia kubwa na tukashika njia ya kuelekea kwao Deborah,basi tulipofika Monica alisimama kwa mbali kidogo hakutaka kuongozana na mimi!.
Monica “Nenda utanikuta nakusuniri hapa”
Nilipofika kwenye boma la ile nyumba kwa mbali nikaona taa ikiwa inawaka kwenye kile kinyumba alichokuwa akilala Deborah na nikaelewa watakuwa bado macho!.Basi nilipofika nikasikia watu wakiongea kwa sauti za chini lakini cha ajabu niligonga sana ule mlango bila mtu kutoka wala kuitikia!.Sikutaka kupoteza muda niliondoka zangu kimya kimya kama mtu aliyetengwa na wazazi wake,nilikuwa najiuliza maswali mengi sana nikawa nakosa majibu!.Nilifahamu kabisa Ema atakuwa amemlisha sumu mbaya Deborah kwasababu haikuwa kawaida ya Deborah kunidharau kiasi kile.
Monica “Umemkuta”
Mimi “Nimewasikia kabisa wanaongea lakini wamekataa kuniitikia”
Monica “Huyo ndugu yako anakiburi sana,wewe subiri ajifanye mjanja”
Aliendelea “Baba yako na mama yako mdogo kuna mahali wameenda na wangekuwa wanajua wanajisumbua wangebaki wakatulia”
Mimi “Kwani unajua walipoenda?”
Monica “Tuondoke tunachelewa”
Basi tulitembea kwa haraka kuelekea kwao Monica,jambo lilikuwa ni lilelile la kufika mapema ingawa palikuwa mbali.Sasa nilipofika niliwakuta watu kadhaa wakiwa pale nje wakiwa wamekaa wakipiga stori huku wakiwa wameshaa taa ikiwa juu ya jamvi.
Mama Monica “Karibu mwanangu”
Mimi “Shikamoo mama”
Mama Monica “Marhaba mwanangu,karibu”
Mama yake Monica alinyanyuka kwenye kiti alichokuwa amekaa akawa amenikabidhi nikalie.Basi haukupita muda nikaona Monica anebeba kimeza kidogo anakileta mahali nilipokuwa nimekaa!.Baada ya kuileta ile meza na kuiweka vizuri akawa ameingia ndani ndipo akaja na vyungu akawa ameviweka chini ya meza,alirudi tena akaja na mabakuli akaanza kupakua mboga,kisha akaendea ugali wa udaga na kuukarisha juu ya meza,alinikaribisha kwa kupiga magoti hadi chini!.
Mwanaume nikaanza kula,kumbe nilikuwa nimeachiwa bata ambaye alipikwa kwa ajili ya bibi yake aliyekuwa amekuja kuwatembelea,kwakweli nilikula sana japo nilikuwa nimeshiba maana nilimisi sana nyama ya bata!.Baada ya kumaliza kula mama yake Monica alianza kuongea kisukuma na yule mwanamke mzee ambaye nilifahamu kabisa ni bibi yake Monica kwasababu alikuwa amekwisha kunitonya!.
Mama Monica “Mwanangu,huyu ni mama yangu”
Mimi “Ooh sawa”
Baada ya kuongea na mimi kisha akawa anaongea na bibi yake Monica!.
Monica “Bibi hajui kiswahili ndiyo maana unaona mama anaongea nae kilugha”
Basi tuliendelea kupiga stori za hapa na pale na Monica, sasa muda ulivyozidi kwenda bibi yake Monica akasimana akawa ameingia ndani,nadhani aliingia kulala!.Baada ya kuingia ndani,mama yake Monica alisogeza kiti mahali nilipokuwa nimekaa na Monica.
Mama Monica “Mwanangu kwanza nikupe Pole kwa uliyayaona jana”
Mimi “Aaah mama wala usijali”
Mama Monica “Sasa mwanangu nisikilize kwa makini”
Aliendelea “Niliwahi kukwambia haya yote nayafanya kwa ajili ya binti yangu,nakuomba usije kumuacha mwenzako”
Mimi “Siwezi kumuacha mama”
Mama Monica “Sawa”
Aliendelea “Sasa ila mwalimu anachokifanya si jambo jema,angetulia ningemsaidia”
Mimi “Amefanya nini mama?”
Mama Monica “Maalimu anaenda kwa waganga akitaka kufahamu wanaomuaharibu”
Aliendelea “Mmmmh ngoja tumuone”
Mimi “Mama kwanini usimsaidie tu ba mdogo?”
Mama Monica “Yule mwalimu aliwahi kunitukana mwanangu,wewe hujui tu!,na hata niliposikia unaishi kwa mwalimu nilikujaribu ukanibebea kuni zangu,nilipoona wewe ni kijana mzuri na mwanangu kukupenda nikaona nikusaidie wewe!”
Aliponiambia ya kwamba nimewahi kumbebea kuni nilishituka sana lakini sikutaka kuonyesha!,niliendelea kujipa moyo nikiamini kwasasa hawezi kunifanyia jambo baya kwasababu nilikuwa kwenye mahusiano na binti yake,nilifahamu kabisa ile familia niya kishirikina lakini kwakuwa walikuwa wakinilinda sikuwa na namna!.
Mama Monica “Hata huko walipoenda wameenda kupoteza muda tu mwanangu”
Mimi “Kwani wameenda kwa mganga”
Monica “Wewe nilikwambia nikikuambia hutoniamini,ngoja mama akueleze sasa”
Mama Monica “kwani hujui mwanangu?”
Mimi “Nimetoka senta sijakuta mtu nyumbani mama”
Mama Monica “Hawawezi kukwambia mwanangu”
Aliendelea “Sasa kesho kuna vitu nitakupatia uende navyo nyumbani na nitakuja mwenyewe baadae kukuelekeza namna ya kufanya!”
Mama Monica “Kwakuwa hata hivyo yule mbwa anataka kuniulia nyinyi wanangu nitamshikisha adabu halafu baada ya hapo nitapandishwa cheo”
SEHEMU YA 23
Baada ya mazungumzo ya muda mrefu pale nje,mama yake Monica alituaga akawa ameingia ndani kwa ajili ya kulala,basi na sisi hatukutaka kupoteza muda kabisa tukawa tumeingia ndani ya kwa ajili ya kulala.Ilipofika asubuhi niliamaka mapema nikawa nimemwambia Monica inapaswa nielekee nyumbani!,siku hiyo nakumbuka ilikuwa jumamosi.
Monica “Subiri basi mama aamke kwanza”
Basi Monica alinipatia maji nikanawa uso kisha nikarudi ndani kusubiri hadi mama yake aamke maana alikuwa ameniambia usiku ya kwamba angenipatia kitu ambacho ningeenda nacho nyumbani ili kitusaidie!.
Ilipofika mida ya saa 1 asubuhi mama yake Monica alikuwa ameshaamka na alikuja kugonga mle ndani nilimo lala ili atusalimie,wakati huo nilikuwepo mimi peke yangu na Monica alikuwa yupo jikoni akiandaa uji kwa ajili ya mlo wa asubuhi!.
Mama Monica “Hujambo baba”
Mimi “Sijambo mama,shikamoo!”
Mama Monica “Marhaba,baba yangu”
Aliendelea “Mbona mapema yote hii,unawahi wapi?”
Mimi “Nilitaka kuwahi nyumbani mama nikaendelee na shughuli zangu,siunajua tena ninapaswa kuelekea senta”
Mama Monica “Ni kweli baba”
Aliendelea “Basi njoo umsalimie bibi yako”
Basi nilitoka mle chumbani nikaelekea mpaka nje ya mlango wa ile nyumba aliyokuwa amelala bibi yake Monica!.Kwakuwa kisukuma changu kilikuwa cha salamu tu na kuombea maji ilibidi mama yake Monica niwe naongea halafu na yeye anamtafusiria bibi maana alikuwa hakijui kiswahili hata tone!.
Baada ya salamu na mazungumzo mafupi,mama yake Monica akawa amenitolea kiti nje akanitaka nikae nisubiri uje uive ninywe wakati ambao yeye ananiandalia mitishamba na dawa aliyokuwa ameniambia angenipatia.Kiukweli niseme tu ukweli,mama yake Monica alitokea kunipenda sana na kuna muda nilikuwa nikifika pale kwa Monica najihisi niko kwenye dunia nyingine,mara kwanza nilikuwa naogopaga sana,lakini baada ya kuhakikishiwa usalama wangu,kwakweli sikuwa naogopa tena!.Yule mama alikuwa yuko radhi afanye jambo lolote ili mimi na mwanaye tusalimike!.
Basi haukupita muda Monica akawa ameivisha uji na maboga akatenga kwenye jamvi!,nilishuka kutoka kwenye kiti na kukaa kwenye jamvi kwa ajili ya kupata brekifasti!,kama ambavyo nilisema hapo awali,ile familia haikuwa na hela ila ilikuwa na uchawi wa kutosha!,kunywa uji usiyokuwa na sukari halikuwa jambo la mjadala na kiukweli japo sikuwahi kunywa uji wa sukari hapo kwa Monica lakini uji ulikuwaga mtamu sana kwasababu walikuwa wakiweka maziwa!,hivyo kuufanya kuwa mtamu sana!.Nilipomaliza kupata ile brekifasti,mama yake Monica aliniita ndani ya nyumba kubwa kule alikokuwa amelala bibi yake Monica.
Mama Monica “Mwanangu nisikilize kwa makini!”
Aliendelea “Najua wewe na mwanangu mtakwenda kuniletea mjukuu hivi karibuni,hivyo wewe ni mtu muhimu sana kwasasa katika familia hii”
Mama Monica “Najua Mwalimu Wambura ni Mkurya wa Musoma huko na ndiyo maana ni mjeuri,ila wewe nimekupenda kwakuwa unanisikiliza sana mwanangu,nakuomba usije ukachukua roho ya mwalimu Wambura!”
Aliendelea “Naamini hautanitesea mwanangu pekee Monica”
Mama Monica “Baba yake alikufa angali bado mdogo,hivyo nimemlea kwa matatizo makubwa mno!”
Aliendelea “Tulihamia huku baada ya kufukuzwa huko Ilungu-Magu,na hii yote ni kwasababu ya baba yake Monica”
Mama Monica “Haya yote unayoyaona tumerithishwa na huyu bibi yako unayemuona ningali binti mdogo”
Aliendelea “Kwakuwa baba yake Monica alitaka kuniulia mwanangu wa pekee kwenye michezo yao,ndipo huyu bibi yako tukasaidiana kummaliza kabla hajafanya jambo baya”.
Aliendelea kusema “Baada ya mambo kuharibika ndipo tukahamia hapa,kutoka huko Ilungu”.
Aliendelea kusema “Hivyo nikuombe mwanangu,hata nikifa leo,nakuomba umtunze mwenzio kwa gharama kubwa maana aliniambia anakupenda sana”.
Aliendelea kusema “Mwanangu hajasoma,lakini ni mwerevu na anajua mambo mengi,hivyo na wewe nakuomba umpende!.
Kiukweli siku hiyo mama yake Monica aliamua kunipasulia ukweli kuhusu mwananye na familia yake kwa ujumla, ndipo nikaona kabisa nilikuwa nimethaminiwa kwa kiasi kikubwa na ile familia.
Mimi “Mimi nampenda sana Monica mama na sitaki kumpoteza na yote uliyoongea nimekusikia!”.
Mama Monica “Sawa nisubiri nakuja”.
Mama yake Monica aliingia chumbani akawa anazungumza na bibi yake Monica kisukuma.Sasa wakati nikiwa nasubiri mama atoke chumbani,ndipo Monica naye akawa ameingia ndani!.Haukupita muda mama yake Monica alitoka ndani akiwa amebeba furushi la mfuko wa rambo la blue!.
Alianza kuufungua ule mfuko kisha kutoa vitu ambavyo sikuvielewa.
Mama Monica “Kamata hii”
Aliendelea “Hiyo niliyokupa ukifika pale nyumbani kwenu,nenda kule nyuma lilipo dirisha la chumba cha Mwalimu na uhakikishe unachimbia chini usawa wa dirisha!”.
Mimi “Sawa mama”
Aliendelea “Kamata na hii”
Alisema ” Hii naomba umwambie mwalimu aogee yeye na mkewe,halafu wakimaliza kuoga wajipake hii hapa”.
Aliendelea kusema “Wewe na mwenzio pia mfanye hivyo hivyo,baadae nitakuja mimi mwenyewe na nitakupatia maelekezo namna ya kufanya”
Mama Monica “Nataka kumsaidia mwalimu ili aepukane na hii fedheha ya yule mpumbavu na wenzie”
Aliendelea “Mwalimu amewahi kunitusi na tulikuwa hatusalimiani,ila inapaswa akushukuru sana wewe”.
Mimi “Mwalimu hatakataa nikimwambia?”
Mama Monica “Wewe mwambie,akikataa shauri yake”
Aliendelea “Kama anataka kuondoa fedheha na kumuahibisha mbaya wake mwambie atumie,akikataa usimlazimishe muache”.
Mimi “Nashukuru sana mama”
Mama Monica “Andaeni sherehe kesho mtafurahi na itakuwa fedheha hapa kijijini”
Basi baada ya mama yake Monica kunikabidhi zile dawa nikawa nimeaga na kuondoka kurudi nyumbani.Muda huo ilikuwa yapata saa 3 asubuhi.
Baada ya kutembea kwa muda namshukuru Mungu nikawa nimefika nyumbani salama,nilipofika mida hiyo bado sikumkuta mtu yeyote pale nyumbani!.Basi niliingia stoo nikachukua jembe nikazunguka kule nyuma ya nyumba ambako kulikuwa na dirisha la chumba alichokuwa analala Ba’mdogo.Nilichimba haraka haraka na kufukia ile dawa kama ambavyo mama yake Monica alikuwa amenielekeza.
Nilipomaliza nilirudisha jembe stoo kama kawaida,nilichukua dumu la maji nikaelekea lamboni kuchota maji ili nije nikaoge ile dawa ambayo alinipatia maelekezo na kututaka wote tuoge kama tunataka kuwa salama ikiwemo Headmaster na mkewe!.Basi baada ya kumaliza kuoga nilianza zoezi la kuosha vyombo na kumwaga ule ugali nikiyokuwa nimeupika jana na ukakosa walaji!.
Baada ya ile kazi iliyochukua muda wangu mwingi,niliingia ndani kulala!.Nilishituka nikiwa naamshwa na Ema mida ya Saa 7 mchana,wakati huu jamaa alikuwa akijechekelesha chekelesha na nikajua kutakuwa na kitu lazima kwasababu haikuwa kawaida yake,mara nyingi alikuwaga akiharibu mahali basi alikuwa akinichangamkia sana kwakuwa mimi nilikuwa mtetezi wake!.
Mimi “Vipi”.
Ema “Mwanangu si Headmaster amenifuma nampiga Deborah mate”
Mimi “Amekufuma wapi”
Ema “Situlikuwa tumesimama pale karibu na ule muale”.
Mimi “Sasa amewaona vipi”
Ema “Yaani mwanangu na mimi sifahamu,nimeshituka namuona huyu hapa”
Mimi “Amekwambia nini”
Ema “Ametuchora tu,hajaniambia chochote”
Nilijua tu atakuwa ameharibu mahali na ndiyo maana akajifanya kuja kwangu na kuanza kujichekesha!,kimoyo moyo nilimuhurumia maana nilijua fika stiki atakazokutana nazo si za kitoto!.
Sasa ilipofika mida ya saa 9 alasiri nilitoka zangu ndani na kwenda kumsalimia Headmaster ambaye alikuwa amesharudi,lakini haikuwa kawaida yake nilivyomuona,kiukweli alio alionekana kama mtu aliyekata tamaa na kuchoka kwingi,sasa sikufahamu huko alipokuwa ameenda kilikuwa kimemkuta nini!.
Headmaster “Hivi mwalimu Dani huwa unafahamu anapokaa”
Mimi “Hapana,sijawahi kufika kwake”
Headmaster “Hebu mwambie huyo mjinga aje nimuagize”
Basi nilitoka kwenda kumuita Ema.
Headmaster “Wewe mwalimu Dani siunapafahamu anapokaa?”
Ema “Eeenh,napajua”
Headmaster “Nenda ukimkuta umwambie akupatie mzigo wangu,na uwahi kurudi”.
Basi baada ya Ema kuondoka,nilimwambia baba nilikuwa nina mazungumzo nae yeye pamoja na mama.
Headmaster “Kwani huwezi kuniambia mimi mpaka awepo mama yako mdogo?”
Mimi “Ni vizuri akiwepo na mama baba”
Headmaster “Sawa,nilimuacha kwa mama Salome,ngoja tumsubiri arudi”.
Nilitaka awepo Maza mdogo maana nilifahamu ningemwambia Headmaster angeweza kukataa,ila Maza mdogo akiwepo isingekuwa rahisi yeye kukataa!.
SEHEMU YA 24
Baada ya Maza mdogo kurudi,ulikuwa ukiwaangalia yeye na Headmaster ilionekana kuhuzunika sana na sikuelewa sababu ilikuwa ni nini!,nimewazoea mara zote tukiwa pale sebuleni eidha tukila chakula au tukiwa tumekaa,mara zote mazungumzo yenye utani na ucheshi mwingi huwa yakishika kasi,safari hii imekuwa tofauti kabisa!.
Headmaster “Ulisema ulikuwa na jambo la kutuambia,ni jambo gani hilo bhana”
Mimi ” Ni jambo la kawaida tu Baba”
Mimi “Baba mimi nina rafiki yangu wa kike anaitwa Monica,na niseme tu ukweli baba ile siku uliyoniadhibu ni kweli nili lala kwao”.
Mimi “Sasa nimeamua Kuwaita ili niwashirikishe jambo”
Mimi ” Yule binti kiukweli kwao ni wataalamu wakusaidia watu na wameshawasaidia watu wengi,sasa huwa nikienda kwao kumsalimia ananielezaga mambo mengi kuhusu hii nyumba tunayoishi”.
Sasa niliamua mambo mengine kukoleza chumvi ili mradi tu waniamini na wakubali hatua za haraka zifanyike!.
Mimi ” Jana nilipotoka senta nilikutana nae njiani akawa amesema nimsindikize hadi kwao,sasa nilipofika kwao mama yake akaanza kuniambia kuna mtu amewahi kuja hapa nyumbani kufanya zindiko,sasa lile zindiko lilifeli kwasababu yule mtu aliuawa kichawi”
Sasa baada ya kusema hiyo sentensi,nikaona Headmaster na mkewe wanaangaliana kwa mshangao!.
Mimi “Yule mama aliniambia adui wa hii nyumba ni mzee makono!”.
Headmaster “Hivi huyo mzee makono ndiye nani?”
Mimi “Kama unakumbuka baba nimewahi kukwambia nilikutana nae akaniambia anakusalimia na akajitambulisha kwamba anaitwa makono”
Headmaster “Sawa nakumbuka lakini najaribu kuvuta picha ni mzee gani huyo”
Mimi “Unakumbuka ile siku Ema amening’inizwa darasani?”
Headmaster “Mmh!”
Mimi “Sasa siulikuja na wazee wawili kama unakumbuka,yeye ni yule mwemamba mrefu”
Headmaster “aaaaaaah!,hivi kumbe ndiyo anajiita makono!”
Maza mdogo “Ni nani?”
Headmaster “Si yule mzee lameki”
Headmaster “Sawa,sasa hapa ndipo naanza kupata picha!”
Aliendelea “Basi hilo jina litakuwa la kisukuma au la kwao huko,kama ni yule mzee jina lake ni Lameki”
Aliendelea “Na alikuwa rafiki yangu sana lakini siku za karibuni naona ananikwepa sana”.
Headmaster “Sisi bhana tumekuelewa na labda kwa niaba ya mama yako mdogo nikuombe radhi kwasababu kuna mahali tulienda na tukaambiwa mambo mengi sana,hata suala wewe kumchungulia mama yako akiwa anaoga haikuwa kweli,tumeambiwa ni mtu mmoja ambaye anazo nguvu za kutosha tu,na kwa maelezo yako sasa angalau nduyo napata mwanga”.
Aliendelea “Kumbe matukio yote yanayofanyika hapa ndani kuna watu ndiyo wanatufanyia hiyo michezo na tumeambiwa anayeongoza genge ni mwanaume mwenye nguvu haswa,sasa namna ya kukabiliana nae ndiyo changamoto,ingawaje kuna dawa tumepewa ndo tunataka kuzijaribu tuone!”
Alisema “Je mama yake huyo binti anapatikana wapi?”
Mimi “Wao wanaishi kule masairo”
Headmaster “Aisee mnazurura,hadi Masairo ushafika!”
Aliendelea “Huyo mama yukoje?”
Basi baada ya kumuelezea namna mama yake Monica alivyo,mzee alishangaa sana!.
Headmaster “Siyo mke wa mzee Kulola kweli?,maana kwa unavyoniambia ni kama yeye”
Aliendelea “Yaani yule mchawi ndiyo unasema anasaidia watu?,wale inasemekana walifukuzwa huko vijijini kwasababu ya uchawi!”
Baada ya kuniambia hivyo nikaona kabisa bila kujitetea nitaharibu mambo!.
Mimi “Hata mimi mara ya kwanza baba nilikuwa nasikia watu wanasema hivyo,lakini nilivyombananisha yule binti alikataa na hata pia nikaongea na mama yake akaniambia walikuwa wanasingiziwa tu,hakukuwa na ushahidi dhidi yao”
Headmaster “Mimi na yule mama hatupatani na yeye analijua hilo,kuna kipindi nilimtukana sana”
Mimi “Lakini baba asingekuwa mtu mwema asingeniambia haya yote”
Maza mdogo “Ila kweli,kama ni mchawi unadhani angesema hivyo?”
Mimi “Kuna dawa alinipatia jana akawa amesema tuitumie na kama ukikubali mimi nitamuita aje atusaidie ili kumnasa mtu anayetusumbua”
Headmaster “Hiyo dawa iko wapi?”
Basi niliondoka kwenda ndani kuchukua ile dawa na kuileta!.
Headmaster “Ndiyo hii?”
Mimi “Ndiyo baba”
Maza mdogo “Matumizi yake yakoje?”
Mimi “Hii tunaogea watu wote mama”
Maza mdogo “Baada ya hapo”
Mimi “Nitaenda kumuita mama yake Monica aje atuelekeze cha kufanya”
Headmaster “Shida tukitumia dawa zote hatutajua ni nani ametusaidia”
Aliendelea “Sawa,ngoja tumuone huyo mama,kama amekwambia yote hayo inawezekana akawa mkweli “
Kwakuwa nilifahamu ikifika usiku mama yake Monica angekuja kama alivyokuwa ameniahidi,sikuwa na presha na niliwaambia ningemfata kumbe mimi nilikuwa ninaujua ukweli.
Headmaster “Hivi huyo mjinga bado hajarudi tu”
Mimi “Bado sijamuona”
Headmaster “Ngoja licheze na dunia,sikuhizi badala ya kusoma limeanza kuhangaika na wanawake!”
Aliendelea “Mabinti wa hii shule niwa kuhangaika nao?,ngoja acheze na hiki kijiji kama hatujamuacha hapa”.
Baada ya maelekezo ya namna ya kutumia ile dawa,namshukuru Mungu walikubali na walioga!,sasa kitu kilichokuwa kinasubiriwa ni mama yake Monica kuja,niliwaambia ikifika jioni nitaenda kumuita,lengo langu lilikuwa ni kusubiri mpaka atakapokuja mwenyewe maana nilichoka kutembea mpaka Masairo ambako kulikuwa mbali!.
Headmaster alihuzunika sana kusikia ya kwamba aliyekuwa akitufanyia uhuni pale nyumbani alikuwa huyo mzee aliyejiita makono ilihali jina lake ni Lameki.Nakumbuka Headmaster alisema akipatikana huyo basi angejuta kuzaliwa!.
Ilipofika mida ya saa 11 jioni,niliwaaga nikasema naelekea kwao Monica kumchukua mama yake!,sasa kwa muda ule niliona nitembee kwa kukimbia ili niwahi kufika maana palikuwa mbali!.Baada ya safari ya muda mrefu kidogo nilifanikiwa kufika kwao Monica.
Nilimkuta bibi yake Monica akiwa amelala kwenye jamvi kwa nje!,nilipiga hodi yule bibi akaitikia kisukuma,sasa kasheshe ilikuwa ni kuongea nae kumuuliza Monica na mama yake wako wapi kwasababu sikuwakuta!,nilipojaribu kumuuliza kwa kiswahili,yeye alinijibu kwa kisukuma,niliamua kusimama kando ya nyumba ili kuvuta muda angalau nikiamini wangekuja maana walikuwa wamemuacha bibi peke yake.
Baada ya muda kwenda ikiwa inakaribia saa 1 usiku,nilimuona Monica akiwa anakuja akiwa amebeba gunia kichwani na jembe mkononi!,alipofika nilienda kumtua ule mzigo ndipo nikakuta alikuwa amebeba mihogo mibichi.
Mimi “Mlienda shambani?”
Monica “Eeeh!,umekuja muda mrefu?”
Mimi “Nimekuja muda ndiyo”
Mimi “Mama yuko wapi?”
Monica “Anakuja,nimuacha hapo nyuma”
Mimi “Sasa hii mihogo mtamenya saa ngapi?”
Monica “Hii itamenywa kesho,nani wakumenya sasa hivi nimechoka”
Mimi “Sawa,kesho nikipata nafasi nitakuja kuwasaidia kumenya”.
Ile mihogo ilikuwa ni ile michungu(rumala) iliyokuwa inavundikwa ikishamenywa kwa ajili ya kutengenezea unga wa muhogo(Udaga).
Basi haukupita muda mama yake Monica naye akawa amekuja na yeye akiwa na mzigo wa mihogo kichwani.
Mimi “Mama shikamoo”
Mama Monica “Marhaba mwanangu”
Aliendelea “Umefika zamani?”
Mimi “Ndiyo mama,nimefika muda tu”
Mama Monica “Tusamehe mwanangu,tulienda kuchimba mihogo tumtengenezee bibi yako unga wa kuondoka nao”
Mimi “Sawa mama haina shida”
Mimi “Sidhani kama nitakaa sana,maana nimetumwa ba Ba’mdogo “
Mama Monica “Mwalimu anasemaje?”
Mimi “Mama niliwaeleza jambo uliloniambia na wamekubali”
Mama Monica “Kweli?”
Mimi “Kweli mama”
Mama Monica “Basi wewe nenda ukawaambie nakuja,ngoja nijiandae nikawachukue wenzangu tunakuja”
Sikutaka kupoteza muda nilitoka nduki kurudi nyumbani kwasababu ilikuwa tayari ni usiku!.Nilifika nyumbani mida ya saa 2 usiku nikamueleza headmaster na mkewe na wao wakawa wanawasubiri!.
Kila mtu hapo nyumbani alikuwa amekwisha kuoga ile dawa na hata Ema ambaye nae pia wakati naondoka sikkumuacha ila alipo rudi alipewa maelekezo namna ya kuoga ile dawa!.
Sasa wakati usiku tukiwa tunakula,nilisikia mlango wa nje unagongwa,Ema alienda kufungua ule mlango na alikuja kuniita akisema naitwa!.Basi nilinyanyuka kuelekea nye ndipo nikamuona mama yake Monica akiwa na wale wanawake wawili,safari hii walikuja wakiwa wamevaa nguo za kawaida na wametanda Khanga!.
Mimi “Karibu mama”
Mama Monica “Haya tushafika,hao wapo?”
Mimi “Wapo mama,ingieni ndani?”
Basi waliingia mpaka uani wakawa wamesimama,mimi niliingia ndani kumwambia headmaster.
Mimi “Amekuja baba”
Headmaster “wewe msukuma njoo tule bhana”
Mama Monica “Nyie endeleeni sisi tumekula”
Headmaster “Toa viti hapo nje”
Basi nikatoa viti vya idadi ya wale kina mama nikapeleka!.
Tulivyomaliza kula,headmaster alitoka nje na mkewe ili kumsikiliza mama yake Monica!.
Headmaster “Mmh!,we msukuma lete maneno”
Mama Monica “Mimi nipo mkurya”
Mazungumzo ya kutaniana kati ya headmaster na mama yake Monica yalipokwisha maliza,sasa usiriasi ulichukua nafasi!.
Headmaster “Huyu kijana wangu amenifikishia yote uliyomwambia,na sisi tumeyapokea kwa mikono miwili”
Aliendelea “Hebu nisaidie maana nimeshahangaika sana na sijui nitakulipa nini nikifanikiwa”
Aliendelea “Hayo yaliyopita tuachane nayo,mimi na wewe tuanzie hapa sasa!”
Mama Monica “Tusipoteze muda,nileteeni karai na maji”
Nilichua karai nikasogezea mama yake Monica.
Alisimama akafungua mfuko uliyokuwa na makorokoro mengi yasiyoeleweka,alichukua unga akawa amemwaga ndani ya yale maji kwenye karai,baada ya hapo alizungumza kisukuma na mmoja ya wale kina mama ndipo mmoja wapo akawa amebeba lile karai na kutoka nje,haukupita muda akawa amerudi yale maji ndani ya karai yakiwa yameisha!.
Mama Monica “Leo wabaya wako wapo kwenye kikao mwalimu,hivyo wakiishatoka tu lazima waje hapa,wakifika hapa ndipo wataipata freshi”
Aliendelea “Sasa nawapatia hii kitu kila mmoja ahakikishe analala nayo kwa kuishikiria na usije ukaiachia”
Alitukabidhi watu wote kitu kikiwa kimeshonwa na kitamba kigumu mno,mimi sikupata shaka kuelewa kwamba ile ilikuwa ni irizi!.
Mama Monica “Hizi hapa mtapakaa kila mtu usoni kabla ya kulala”
Aliendelea “Mwalimu shika hii”
Headmaster alipewa kibuyu kidogo kama kile ambacho nilipewa mimi siku ile.
Mama Monica “Hiki kibuyu hakikisha unakiweka nyuma ya kona ya mlango”
Headmaster “Sawa”
Mama Monica “Mwanangu shika hii”
Na mimi pia alinikabidhi kile kibuyu kidogo na akanitaka nikiweke nyuma ya mlango kwenye kona.
Mimi na ndugu zangu hawa tutakuwa mazingira ya karibu,hivyo msiwaze!.
Headmaster “Kwahiyo hapa ushamaliza?”
Mama Monica “Kila kitu tayari”
Aliendelea “Msije mkapiga kelele kwa mtakachokiona,mkipiga kelele tu ,mtakuwa mmeharibu kila kitu!”
Mama Monica “Kama kuna mtu anajua hatokuwa mvumilivu aseme kabisa”
Baada ya hilo swali na wote kumuhakikishia tutakuwa wavumilivu ndipo aliendelea akasema.
Mama Monica “Mwalimu utakachokishuhudia wewe simama na chukua kibuyu nilichokupatia na ukifungue kikae wazi”
Aliendelea “Ukishakifungua tu,huyo mbaya wako atajuta kuitembelea hii nyumba”
Baada ya muda mama yake Monica na wale kina mama waliaga kuondoka,Headmaster na mkewe walitoka kuwasindikiza.
SEHEMU YA 25
Baada ya Headmaster kutoka kuwasindikiza wageni,tuliamua kukaa kikao cha kifamilia na kuzungumza mambo kadhaa yaliyotuweka sawa.Sasa kila mtu alielekea chumbani kulala,baba mdogo na mkewe waliingia chumbani kwao,mimi na Ema pia tuliingia chumbani kwetu kulala.
Siku hiyo mle chumbani hakuna aliyepata usingizi kabisa,kabla ya kulala nakumbuka tulipakaa usoni dawa aliyokuwa ametupatia mama yake Monica,pia tukashikiria na zile hirizi mkononi kama alivyokuwa ameagiza tufanye!.Kadri muda ulivyokuwa ukisonga tuliona kimya,mimi nilianza kupitiwa na usingizi maana nilikuwa nimechoka sana!,kumbe wakati mimi napitiwa na usingizi,Ema yeye alikuwa macho kabisa na jamaa alikuwa na shauku ya kuona ni kitu gani kingetokea!.
Sasa ilipofika mida ya saa 8 usiku,nilishitushwa na Ema akiniamsha!.
Ema “Umesikia hicho kishindo?”.
Mimi “Hapana,kishindo cha kitu gani?”
Ema “Kutakuwa na kitu nadhani!”
Ema alikuwa akiniambia kwa sauti ndogo kabisa na yenye uoga ndani yake!.
Mimi “Nyamaza”
Niliamka kitandani nikaenda kuwasha taa,nilifahamu kabisa kile kishindo Ema alichosikia hakikuwa cha kawaida na uenda wale jamaa wakawa wamekuja kama kawaida yao,kiukweli mimi kwa upande wangu sikuwa kabisa na hofu kwasababu kwa siku chache nilikuwa nimeshazoea yale mazingira ya kuwaona wachwawi laivu!.Nilimwambia na kumbusha Ema ya kwamba chochote atakachokiona asipige kelele wala kushituka!.
Haukupita muda,mara ghafla wakaonekana watu watatu wakiwa wamesimama mle chumbani huki wakiwa uchi kama walivyozaliwa,watu wale safari hii walikuja wawili wanaume na mmoja akiwa mwanamke!.Niliwaangalia kwa kuibia kama vile sielewi chochote!,Ema alikuwa akitetemeka sana na nilimpatia ishara ya kwamba atulie kabisa!.Basi nadhani yule mwanamke alihisi jambo maana niliona anamsogelea Ema akawa kama anamtisha aone kama amemuona,sasa alipoendelea kumtisha Ema nikaona anaweza kupiga kelele,nikaanza kumpigisha Ema stori ili kupotezea ile hali!.
Mimi “Mwanangu wewe piga kimya kabisa wala usimfanye chochote yule demu”
Ema “Yule demu mwanangu anazingua kinoma”
Mimi “Halafu Headmaster alisema ukamuamshe aandae yale masomo”
Ema “Halafu kweli umenikumbusha,ngoja nikamuamshe!”
Sasa wakati tunaongea yule mwanamke alirudi kwa wenzie na wakaendelea kushangaa shangaa,tulichokifanya na Ema pale kwa ule muda mfupi ni hakika walidhani hatuwaoni kumbe lengo lilikuwa ni kumuondolea Ema uoga na kuwapoteza maboya!.
Ema aliamka akatoka kwenda kumgongea Headmaster chumbani kwake ili aje ajionee!,sasa wakati Ema ameondoka,nilianza kujipigisha mruzi wa uongo na kweli ili kuikabili ile hali kwasababu ilikuwa inatisha si kitoto!..
Headmaster “Umughaka tacho omahe”
Baba alipotoka nje aliniita kwa kilugha nikawa nimetoka nje,sasa alianza kutueleza ya kwamba tusishituke na tuendelee kuwa watulivu,alitwambia Ema achukue madaftari tuelekee wote sebuleni ili iwe rahisi kuwakabili,mimi nilimwambia wao wakae sebuleni na mimi nirudi chumbani kukaa karibu na kibuyu kwa kazi maalumu!.
Basi wale watu wakawa wamepotea ghafla mle chumbani!,nilitoka nje kwenda kumwambia Headmaster.
Headmaster “Ngoja tusubiri,yawezekana wakawa wameshituka”
Mimi “Lazima warudi”
Headmaster “Halafu mbona yule mzee hayupo?”
Mimi “Uenda leo kawaagiza hawa”
Wakati tukiwa tunaendelea kuongea pale,Maza mdogo akamwambia Headmaster kwa kikurya kwamba,wale watu wako kule chumbani kwake na anawaona,Headmaster akamwambia atulie na asipige kelele!.Sasa tukiwa tunaendelea kuongea pale sebuleni huku Headmaster akijifanya kumpigisha Ema pindi,tukasikia kishindo kikubwa tena pale uani!.
Haukupita muda akawa ametokea yule mzee makono akiwa na usinga mkononi huku akiwa uchi kama wenzie!,akaja mpaka pale sebuleni huku tukiendelea kumpimia tu!,aliendelea kuangaza huku na huko na hatimaye akawa ameingia mle chumbani kwa Headmaster.Basi baada ya kuingia chumba cha Headmaster,Headmaster aliinuka kwa ghadhabu huku akisema “Lero n’uramanye uwe tombanyoko” (Leo utanitambua).
Sasa Headmaster alipoingia chumbani alijifanya kuongea na mkewe huku wakiwatazama,sasa nadhani mzee makono aliwaambia wale watu waende wakawalete watu wa kwenda kulima ili wakifika watuunganishe na sisi tuondoke!,wale watu watatu walitoweka wakamuacha mzee makono mle chumbani akitaka kufanya mambo yake ili amchukue Headmaster kama kawaida aje atuunganishe na sisi tuelekee kwenye kilimo cha usiku kisichokuwa na tija!.
Wale watu walipotoweka tu na mzee makono kubaki mwenyewe,Headmaster alichukua kile kibuyu alichopewa na mama yake Monica akakifungua,alipokifungua tu!,yule mzee akaanza kucheza kwa kuzunguka mle chumbani kama mwendawazimu!.Headmaster alituita tukaingia kumtazama,yaani kuna muda nilianza kumuonea huruma maana alikuwa kama amepagawa kwa kushikwa ugoni.
Kadiri muda ulivyokuwa ukienda,wale watu waliotumwa na mzee makono hawakurudi kabisa na nadhani watakuwa walishituka mapema!.Ile hali ilifanya maza mdogo kutoka kule chumbani akabaki mzee makono akizunguka chumba kizima kama mwendawazimu.Usiku huko hakuna mtu aliyepata usingizi kabisa,tumekuja kushangaa imefika saa 11 alfajiri bila kujua!.
Sasa ilipofika saa 12 asubuhi,Mama yake Monica alikuja akiwa na wale kina mama,alihuzunika sana kwanini tuliamua kuwaachia wale watu watatu wakaondoka!.
Mama Monica “Mwalimu nilikwambia,nadhani sasa unaniamini”
Headmaster “Sikuzote Msukuma nakuamini,si leo tu!”.
Mama Monica “Kwanini mmewaachia wale washenzi?”
Headmaster “Wameondoka wenyewe”
Mama Monica “Nilikwambia wakifika tu,ungefungua kibuyu”
Headmaster “Nilipoingia chumbani kufungua kibuyu wakawa wameondoka akabaki mzee lameki”
Mama Monica “watasimuliana,hakuna kilichoharibika”
Aliendelea “Haya sema,unataka tumfanye nini huyu mzee”
Headmaster “Nadhani kama kuna uwezo muondolee uwezo wake asije akaponyoka halafu mengine utaniachia mimi”
Mama Monica “Huyu ameshakwisha,hapa hawezi kukuponyoka kamwe”
Aliendelea “Mimi namshughurikia halafu nakuachia wewe utajua cha kumfanya”.
Basi mama yake Monica alimsogelea yule mzee akachukua ule usinga kisha akamvua shanga alizokuwa amejivika kuanzia begani kuteremkia kiunoni!,baada ya hapo kuna dawa alimpatia Headmaster akamwambia kukishapambazuka vizuri atampaka ile dawa na kisha atamuondoa mle ndani!.Mama yake Monica na wale kina mama waliondoka wakawa wamemuacha mzee makono humo ndani akizinguka kama mwehu!.
Kulipopambazuka,Headmaster alielekea kwa mwenyekiti wa kijiji na kutaka yowe ipigwe karibia kijiji kizima ili wananzengo wahalifiwe ya kwamba kulikuwa kuna tukio kubwa la kushangaza!,Basi yowe ilipigwa na watu wakawa wanakuja pale nyumbani huku wengine mikoni wakiwa wameshika mapanga na mafimbo!.Haukupita muda mrefu watu wakawa wamejazana pale nyumbani huku wengine wakichungulia dirishani wakishangaa lile tukio!.
Ilipofika mida ya saa 3 Asubuhi baada ya watu kujazana pale nyumbani,Headmaster alifanya kama alivyoambiwa afanye na mama yake Monica,baada ya kupakwa dawa yule mzee alikurupuka akawa anashangaa sana!,alikuwa akizunguka kitafuta usinga wake lakini hakuuona,ndipo Headmaster aliamrishwa na wananzengo ya kwamba amtoe yule mzee nje ya nyumba ili akapambane na viboko vilivyokosa huruma!.
Yule mwenyekiti aliamuru yule mzee avishwe nguo hadi kwenye ofisi ya serikali ya kijiji lakini wananzengo wakagoma,walisema inapaswa atembezwe kijiji kizima huku akila mboko na inapaswa siku hiyo hiyo ahame kijiji!.
Basi nakumbuka Headmaster alimuagiza Ema akalete viboko ili aanze nae mle ndani kwasababu alikuwa akimtafuta sana,viboko vilipoletwa kiukweli yule mzee alichezea kiasi kwamba sikutaka hata kuangalia,viboko vilipozidi aliamua kutoka ndani spidi akikimbilia nje,kufika nje wananzengo wakamdaka nako wakaanza kumsulubisha!.
Alitembezwa kijiji kizima huku akiwa uchi kama alivyozaliwa,kiukweli lilikuwa ni tukio la aibu mno!,sasa walipomfikisha kwake wananzengo hawakutaka mjadala,walimwambia avae nguo kisha atoke,alipotoka waliwasha moto nyumba yake na kila kitu kiliteketea kwa moto!.
Baada ya pale alirudishwa serikali ya kijiji na kutakiwa apotee kwenye kile kijiji ndani ya masaa 2!,hakutakiwa kubaki pale na wananzengo walimwambia watamuua endapo angebaki kwa siku hiyo!.
Lile tukio lilivuta hisia kubwa sana pale kijijini na kiukweli lilimpatia Headmaster ujiko na heshima sana ingawaje mimi ndiye niliyepambana sana mpaka kufikia ile hali.Headmaster aliogopeka sana tangu siku ile lile tukio litokee na hakukuwahi tena kuwa na mambo ya ajabu pale nyumbani.
Headmaster kwa baadae alihama ile shule na kuhamia huko Biharamulo ambako amejenga na anaishi hadi leo,mimi niliondoka na kurudi nyumbani kisha kuelekea shuleni Advance!.
Ema yupo hapo Shinyanga anauza duka la vipuri vya magari,amejenga na anaishi hapo hapo shinyanga.
Monica kuna wakati niliambiwa yupo Mwanza ila sijajua ni Mwanza sehemu gani!,kuna mtu nilikutana nae wa pale kijijini akawa ameniambia hivyo,kwasababu baada ya mimi kuondoka pale kijijini sikurudi tena hivyo tukawa tumepotezana na mpenzi wangu huyo!.
Mimi kwasasa nipo Dar es salaam napambana na maisha ya kukimbizana!,nina kiboda boda changu japo kimekwisha lakini tunapambana na maisha!.
MWISHO.