TULICHOMFANYA YULE MCHAWI HATAKUJA KUSAHAU KAMWE
Hadithi Ya Kweli
SEHEMU YA 1
Miaka ya fulani baada ya kumaliza shule ya sekondari,niliamua kwenda kumsalimia Ba’mdogo aliyekuwa mkuu wa shule fulani ya sekondari hapo kwenye hicho kijijini.
Wana kijiji walikuwa wakimpa heshima kubwa Ba’mdogo kwasababu wanafunzi wote waliosoma kwenye ile shule walifaulu kuendelea na elimu ya Sekondari ya upili(Advance),japo shule ile ilikuwa ya kata na kwa mwaka ule nilienda mimi ilikuwa imefaulisha kwa awamu ya kwanza,yaani toka hiyo shule ianzishwe wanafunzi waliokuwa wamefika kidato cha ilikuwa tayari ni mara moja,hivyo nilipofika mimi wale nilowakuta ndo walikuwa wa awamu ya pili.
Sasa kwa mwaka ule wa kwanza wanafunzi wa kidato cha nne walimaliza 12 na wote walifaulu kuendelea Advance tena walienda kwenye shule za vipaji maalumu ikiwemo Ilboru.Sasa wanakijiji kiukweli walimpenda sana Dingi mdogo kwa kujitolea kuwaleta waalimu wa ziada ambao kile kijiji kilikuwa kinawalipa.
Nilipofika nilikuta pale kwa Ba’mdogo kila siku iendayo kwa Mungu ilikuwa inakuja Galoni ya maziwa fresh lita 5, kile kijiji kilikuwa na wafugaji wengi sana wa mifugo ya kila aina! Yaani kumuona mwanakijiji anamiliki ng’ombe elfu 10 ilikuwa kitu cha kawaida,sasa mbali na maziwa, kila Jumapili alikuwa analetewa kuku jogoo mmoja na mwanakijiji.
Ba’mdogo aliwahi kuniambia waliwahi kukaa kikao na wana kijiji wakakubali kila kaya kuwa wanakamua maziwa kulingana na zamu walizokuwa wamewekeana kwa ajili ya mwalimu mkuu ikiwemo kitoweo hicho cha kuku.
Nilipofika mara ya kwanza kwa sababu ya uroho na ulafi, nilikuwa nakunywa yale maziwa kwa wingi kana kwamba kesho hayatokuja mengine,yaani kila niliposikia kiu ya maji mimi nilitwanga maziwa, baadae sasa baada ya kuzoea ilifika sehemu tukawa tunayaangalia na tunaishia kuyamwaga tu maana hakukuwa na wakumpa.
Pale kwa Ba’mdogo baada ya mimi kufika,ni kama nilifanya wapumue maana kazi za hapa na pale nilikuwa nikizifanya mimi, ilikuwa ikifika ijumaa dingi mdogo alikuwa akiondoka kuelekea mjini kwa familia yake na ikifika jumapili jioni alikuwa akilejea.
Sasa kwa wakati huo dingi mdogo alikuwa akiishi na bwana mdogo mmoja alikuwa wa rafiki yake ambaye baada ya kufeli shule mahali fulani alimpatia namba na jina akawa amerudia pale kidato cha pili,hivyo nilipofika mimi tukawa watu watatu.
Japo kulikuwa ni kijijini lakini kulikuwa na maisha fulani ya amani sana,kulikuwa na Lambo kubwa ambalo wanakijiji walikuwa wakijipatia maji ya mahitaji yao hapo. Kwa upande wa umeme ulikuwa bado haujafika na wana kijiji walitumia Solar na Majenereta.
Ilipokuwa ikifika wikiendi nilikuwa ninashuka senta kwa ajili ya kuangalia mpira,wakati huo nilikuwa shabiki wa kutupwa wa Arsenal, ingawaje hivi leo sina mahaba kama hapo zamani kwasababu timu haieleweki nini inafanya. Yaani ilikuwa ni bora nilale na njaa kuliko kwenda kuitazama timu yangu pendwa ya Arsenal.
Kwenye ule ukumbi jamaa alikuwa anatumia jenereta na malipo ilikuwa Tsh 100 kwa wakati ule, sasa lile jenereta lilikuwa likiwashwa wakati wa mechi inapoanza tu ili kuokoa mafuta, yale mambo ya kuangalia uchambuzi wa kina Thomas Mlambo na Robert Marawa yalikuwa hayapo.
Sasa nilikuwaga nikimaliza shughuli zangu hapo nyumbani ikifika saa nane mchana,huyoooo naondoka zangu na kurudi mpaka gemu nihakikishe zimeisha ndo narudi nyumbani. Yule jamaa aliyekuwa hapo nyumbani hakuwa mpenzi wa mpira ila alikuwa mpenzi wa papuchi, yaani alikuwa anatembeza stiki si kwa wanafunzi wenzie tu, hadi wanakijiji.
Kutoka hapo nyumbani hadi ufike senta ilikuwa kilomita 3, kwenda na kurudi inakubidi utembee kilomita sita. Kiukweli kile kijiji hakikuwa na ujambazi wala vibaka, shida ya pale ilikuwa Uchawi!
Aiseeee sijawahi kuona asikwambie mtu.
SEHEMU YA 2
Sasa siku moja nakumbuka ilikuwa kati kati ya wiki nadhani kati ya J4 au J5, siku hiyo kulikuwa kuna mashindano ya Uefa champions ambapo timu yangu pendwa ilikuwa ikicheza na Chelsea.
Nilijiandaa mapema kabisa ilipofika mida ya saa 1 usiku nikamwambia Dingi mdogo anipe ruhusa na bila ajizi akaniruhusu kwenda kutazama kabumbu, japo alinisisitiza nisiende maana wakati wa kurudi ingekuwa shida lakini mwanaume sikutaka kuelewa hata kidogo. Baada ya kuona nimekuwa mbishi na mpira uko kwenye damu aliamua kuniruhusu huku akisema “Uwe makini maana huu mji siyo huko ulikotoka, huu mji una wenyewe”.
Basi nikamuomba yule jamaa tuondoke nae jamaa akagoma akasema yeye anajisomea,sikutaka kuchelewa ikabidi niondoke zangu. Plani yangu ilikuwa ni kwamba niondoke hiyo saa 1 ili kufika kwenye ngoma 2 niwe nimefika nikapige soga na kubadilishana mawazo na mashabiki wengine pale kwenye banda huku tukisubiri mpira uanze.
Sasa kwenye ile njia ya kwenda hapo senta ulikuwa ukifika katikati ya senta na mahali ninapoishi kulikuwa na miti miwili mikubwa mno ya miembe ambayo sikuwahi kuona ikitoa miembe kwa miaka 2 niliyokaa hapo kijijini.Ile miembe ilikuwa pembeni ya ile njia,yaani ile barabara ilikuwa ikipita katikati ya ile miembe miwili mikubwa.
Kwa kuwa siku hiyo ndiyo ilikuwa mara yangu kwanza kupita hapo usiku nilikuwa naona kawaida tu na wala sikuogopa chochote.
Baada ya kufika kwenye banda la mpira ilibidi nisubiri hadi luninga itakapowashwa,ulipofika muda jenereta liliwashwa na tukaingia ndani kwa ajili ya kutazama mpira,kama nilivyosema mechi ilikuwa kati ya Arsenal na chelsea na ilikuwa ligi ya mabingwa hiyo ilikuwa mwaka 2004. Arsenal tulipigwa Goli 2-1 tukiwa kwenye uwanja wetu wa nyumbani Highbury,nakumbuka Goli letu lilifungwa na Jose Antonio Reyes huku yale ya Chelsea yalifungwa na Frank lampard na mchezaji mwingine ambaye nishamsahau!
Basi bana baada ya mechi kumalizika hiyo mida ya saa tano usiku kila mmoja akatawanyika kwenda alikotoka na mimi nikashika njia yangu kurudi nilikotoka,Japo ile mechi tulipoteza lakini furaha yangu mimi ilikuwaga kuwaona Arsenal tu hata ifungwe vipi nilikuwa napata amani ya moyo.
Sasa ile njia niliyotokea mimi nilijikuta nipo pekee yangu kwasababu kule nilipokuwa nina kaa ilikuwa ni njia maalumu ya kwenda shule na nyumba za walimu,hivyo hakukuwa na mwana kijiji aliyekuwa akielekea kule,basi nikaanza kutembea kuelekea nyumbani!
Kila nilipopiga hatua ndivyo ukimya ulivyokuwa kuwa ukitawala,kulikuwa na giza la kitakatifu kwa usiku huo,zilikuwa ni sauti za wadudu wale waliao usiku tu ndizo zilisikika.Nilipotembea sana ndipo sasa kwa mbali baada ya kuikaribia ile miembe kama umbali wa mita 500 nikaona ikiwaka moto mkubwa sana. Ilibidi nisimame kwanza nitazame vizuri uenda nilikuwa sijaona vizuri.
Kweli bana!,ilikuwa ni ile miembe ikiwaka moto, sasa nikawa najiuliza ni nani alikuwa amewasha ule moto?,basi nikajipa moyo nikaendelea kupiga hatua nikiamini uenda kulikuwa kuna watu wikuwa wameichoma kwa bahati mbaya,sasa ajabu kadiri nilivyokuwa nikisogea ndipo moto nao unapungua!,kiukweli nilibaki kushangaa sana na wakati huo akili yangu haiwazi mawazo ya kijinga kuhusu wachawi!
Basi baada ya kufikia kabisa ile miembe sikuona moto wala moshi,sasa nilipofika katikati ya ile miembe,nilihisi kama watu wanacheka kwa nguvu mno huku mwili wangu ukisismka sana!,yaani hadi nilihisi vinyweleo vimesimama, nilichofanya niliinama nikakamata ndala nilizokuwa nimevaa nikatoka nduki kama mwendawazimu, sasa baada ya kufika mbele kabisa ilibidi nisimame nipumzike maana nilikuwa nahema kama mbwa mlafi!,Niligeuka tena kuitazama ile miembe kwa mbali nikashangaa kuona tena ikiwaka moto,kiukweli ilibidi niondoke hilo eneo kwa haraka sana.
Namshukuru Mungu nilifika nyumbani usiku huo ikiwa inakaribia saa 7 usiku,nilimgongea yule dogo ambaye kwa wakati huo alikuwa yuko macho bado akiendelea kupiga buku.Baada ya kunifungulia mlango alishangaa nikihema kwa nguvu kama nilikuwa nafukuzwa.
Jamaa “vipi mbona unahema sana”
Mimi ” Nilikuwa nakimbia niwahi kufika”
Jamaa ” Mpira umeisha?”
Mimi ” Umeisha ila tumepigwa”
Sasa baada ya maswali na majibu kadhaa hapo ndani ikabidi nimuulize yule jamaa maswali kadhaa!.
Mimi ” Hivi ulishawahi kutembea usiku huku”
Jamaa “Hapana,mwisho wangu ni saa 12 tu inapaswa niwe ndani,siunamjua tena ticha alivyo mkora!”
Mimi ” wakati narudi nimepita pale kwenye miembe nimekuta inawakata moto”
Jamaa “Ile miembe ya kule chini?”
Mimi ” Eenh ile ya pale chini”
Jamaa ” Ina maana imechomwa moto?”
Mimi ” Hapana,yaani wakati naikaribia ilikuwa inawaka moto,ila baada ya kuifikia nikakuta hakuna moto wowote na nikasikia pipo zinacheka kishenzi”
Baada ya kumsimulia jamaa akaanza kucheka sana huku akiniambia “Kijana naona unachezea kifo”
Jamaa” Ile njia haifai hata kidogo sema tu nilishindwa kukwambia,siku nyingine ukiwa unaenda mpirani uwe unapitia ile njia ya kule lamboni”
Sasa jamaa njia aliyoniambia ni njia ndefu mno ya kuzunguka,lakini ile ya kwenye miembe ni fupi.
Jamaa ” Hapa mbona sisi tumepata taabu sana,usione sasa hivi kumetulia ukadhani tulikuwa salama”
Mimi ” Kumetulia kivipi?”
Jamaa ” Kuna siku nimerudi kutoka shule kuja kupika nikakuta mavi ya mtu kwenye dumu la unga”
Jamaa akaendelea ” Tumefanyiwa vituko mno hadi ikabidi Ticha akaitisha kikao cha wazazi na wana kijiji na akatishia kuondoka huku ndipo angalau mambo yakapungua,huku ni hatari sana kijana kuwa muangalifu utapotea”
Baada ya jamaa kunipa maelezo hayo kidogo niliogopa sana na shida ikawa nitaangalia wapi mpira?
SEHEMU YA 3
Baada ya kuambiwa yale maneno na yule jamaa kiukweli ilibidi niwe na tahadhari ingawa mpaka wakati huo sikutaka kabisa kuamini mambo ya kishirikina.
Sasa nakumbuka Jumamosi moja kama kawaida niliamka na shughuli za hapo nyumbani zilichukua nafasi ikiwemo kwenda lamboni kuchota maji na kuleta hapo nyumbani.
Headmaster ambaye alikuwa ba’mdogo wangu yeye ijumaa tu alikuwa ameshaondoka kuelekea mjini kuiona familia yake, kama nilivyowaambia ya kwamba, kila ilipofika Ijumaa ya kila wiki alikuwa akiondoka na kurejea jumapili jioni kwa ajili ya mambo ya shule!
Sasa siku hiyo kulikuwa kuna mechi kati ya Arsenal na Blackburn ambayo ilikuwa inachezwa saa 12 jioni, lakini pia kulikuwa na mechi nyingine!,kama kawaida ilipofika saa 11 jioni nilimwambia jamaa tuondoke tukacheki gemu akagoma akadai ataenda kusoma baadae kwao na demu wake! Basi nikachukua zangu tochi au taa ya sola kwa ajili ya kumulika njiani pindi nitakaporudi maana ingekuwa usiku.
Kipindi kile kulikuwa na vile vitaa vya sola ambavyo ulikuwa unaviweka juani vinapata chaji halafu usiku vinamulika kama taa ya umeme, vilikuwa na mwanga sana!,sasa hapo nyumbani vilikuwepo 2,moja alikuwa anaitumia Headmaster chumbani kwake na nyingine alikuwa anaitumia jamaa kule kwenye chumba alichokuwa akilala.
Ile nyumba ilikuwa na chumba na sebule pamoja na stoo,lakini kwa nje pia kulikuwa na chumba kimoja ambacho pembeni yake kulikuwa na jiko ambalo humo humo ilikuwa stoo. Kulikuwa na milango miwili mikubwa, mmoja ulikuwa wa mbele ambao mara zote ulikuwa ukifungwa lakini pia kulikuwa na mlango wa nje ambao ulikuwa umeshikamanishwa na ukuta wa fensi,huu mlango ndiyo ulitumika mara zote kutoka na kuingia!
Sasa wakati naondoka nilimwambia jamaa anipe kile kitaa chake niende nacho halafu yeye angetumia kile cha Headmaster.
Niliondoka zangu kuelekea kucheki boli kama kawaida,ijapokuwa jamaa alinionya kuhusu ile njia sikutaka kabisa kuacha kwasababu ilikuwa fupi kuliko ile aliyokuwa amenielekeza ya kupitia lamboni ambayo ilikuwa ya mzunguko!.Wakati huo mvua ilikuwa imemaliza kunyesha kama siku mbili zilizopita,hivyo bado ardhi ilikuwa na unyevunyevu wa kutosha!
Nilifanikiwa kufika lakini nilikuta tayari mechi imekwisha kuanza. Sasa baada ya kutazama mechi ya Arsenal ambayo tulishinda 2-0,nilitazama na mechi nyingine. Mpaka namaliza kutazama mechi ilikuwa yapata saa 3 usiku,nikaamua sasa ni wakati wa kurudi nyumbani.
Kabla sijaondoka niliwaza nipite njia ipi kati ya zile mbili,lakini nilifikiria ile njia ya lamboni ilivyo ya mzunguko ingenichukua muda mrefu kufika,nikaona nirudi na ileile niliyoizoea,nikajifariji kwa kuwa nilikuwa na taa ya sola hivyo kisingeharibika kitu!
Basi bana nikaanza mdogo mdogo kupiga kwato huku nikimulika mulika kwa madaha njia nzima,nina tochi tena!,utaniambia nini!.Sasa kadri nilivyokuwa nikisogea ndivyo utulivu na ukimya ulivyo tawala,kama kawaida nikawa nimeikaribia ile miembe miwili ambayo kila nikifika hapo moyo wangu unashituka sana,sasa safari hii sikuona moto wala nini, nikasonga kuikaribia ile miembe,sasa nilipofika katikati ya ile miembe mikubwa nikahisi kuna mtu nyuma yangu na nikageuka ghafla lakini sikuona mtu, nikahisi yalikuwa mawenge tu ya kitete,kiukweli nilikuwa nasisimkwa na nywele sana kila nikifika hilo eneo!.
Sasa ili kujiamini na kutoa uoga,niliamua kunyanyua kile kitaa na kuanza kumulika juu ya ile miembe angalau nione kuna nini ili nipite kwa amanj, nilipomulika sikuona chochote, sasa ile nashusha tochi chini ghafla nikajikuta nimejikwaa kwenye kitu ambacho sikukiona hapo awali, kiukweli nilianguka pale chini na ile taa ikawa imeanguka kwa mbele na kuzimika, ndala moja pia ikawa imechomoka mguuni nikawa nimebakiwa na moja, sasa nikawa najiuliza nini kile ambacho kimefanya nimejikwaa mpaka nimeanguka, niliamka kwenda kuchukua kile kitochi nikawa nakiwasha nimulike kutafuta ndala yangu ili nivae niondoke lakini kinagoma kuwaka,sasa ikabidi nianze kukipiga piga nikadhani uenda kilipata hitilafu!
Nimekipiga piga sana hatimaye kikawa kinawaka na kuzima, kinakaa muda kinawaka halafu kinazima, nikaendelea kukipiga tena sasa kikawaka kama ilivyokuwa mwanzo, ikabidi nianze kumulika kuitafuta ndala yangu itakuwa imehangukia wapi!,sasa ile namulika kwa nyuma nikaona mtu amelala akiwa uchi wa mnyama!,daaah nikashituka sana na nikataka kukimbia lakini nikajikaza na kuanza kuita kwa nguvu “wewe ni nani?” Niliita sana lakini mtu yule alikuwa hasemi wala hatikisiki,nikagundua uenda ndiye aliyefanya nikadondoka ingawa wakati najikwaa nilihisi kitu kama jiwe na maeneo yale hakukuwa na mawe!.
Sasa akili yangu ikadhani uenda yule mtu alikuwa mlevi ambaye alikuwa amekunywa pombe zikamzidi akawa amelala pale chini,nilisahau kutafuta ile ndala akili yangu ikaamia kwa yule jamaa,nilimsogelea na kuanza kumtikisa kwa mguu huku nikisema ” wewe….wewe….wewe” lakini hakuamka,nilipomulika vizuri nikagundua ile ilikuwa maiti na hakuwa mlevi kama nilivyodhani.
Hakuna siku ambayo sitakuja kuisahau kama ile siku na ndipo nikaamini kuna wachawi!,sikumbuki nilifikaje nyumbani mpaka wakati huo maana nilipopata kumbukumbu nilijikuta nipo kwenye mlango wa nyumbani nikiwa ninahema balaa! Kibaya zaidi pale nyumbani nilikuta jamaa hayupo na mlango wa kuingia ndani ukiwa umefungwa kwa nje na kofuli,niliamua kukaa chini kwanza ili kutuliza presha nikawa najiuliza kile nilichokiona kilikuwa kweli au uenda nilikuwa naota? Baada ya kutulia kwa dakika kadhaa, kujiangalia chini nilikuwa peku na kile kitochi nacho sina mkononi!.
Sasa nikawa nimekaa pale nje kwa uoga mwingi,kwakuwa jamaa aliniambia angeenda kwao demu wake kusoma nikaondoka kuelekea kwao yule demu wake ili nikachukue funguo nirudi kulala,wakati naenda nilipitia njia ya lamboni lakini sikutaka kabisa kutembea ilibidi nikimbie maana ilikuwa usiku wa saa 4 kuitafuta saa 5, kiukweli nilikuwa nikifika kwenye vichaka nilikuwa napita kwa spidi kali mno kama ngiri!
Nilipofika kwa na yule demu wake jamaa nikaona mbwa wanaanza kubweka kwa sana!,sasa ile boma yao ilikuwa imezungukwa na miti na katikati kulikuwa na zizi kubwa la ng’ombe,nyumba aliyokuwa akilala yule binti na mdogo wake ilikuwa kwa pembeni ambako ilinibidi kufanya kazi ya kuzunguka ili kuwakwepa wale mbwa!
Nilipofika kwa nyuma nilichungulia kwenye upenyo wa kidirisha nikaona kuna mwanga,basi angalau moyo wangu ukatulia nikajua walikuwa wakijisomea.Nilianza kugonga nikimuita jamaa ili asikie aje anipe funguo za nyumba,sasa wakati nagonga na kumuita jamaa yule demu wake aliuliza “we nani?”
Mimi ” Mimi Umughaka”
Demu ” oooh,ngoja nije”
Basi yule demu akafungua nyumba akaniambia “Zunguka huku mbele”.
Kwakuwa alikuwa ametoka nje,sikuwa tena na mashaka kuhusu wale mbwa.
Mimi ” Mambo Debo”
Deborah “Poa umughaka”
Deborah “vipi mbona usiku?”
Mimi ” Mwambie ema aniletee funguo”
Deborah “Kwani hayupo nyumbani?,na wewe kwani ulikuwa wapi?”
Mimi ” Mimi natoka senta kuangalia mpira,wakati naondoka aliniambia angekuja huku kwa ajili ya kujisomea”
Baada ya yale maelezo yule demu akaniambia wala huyo jamaa aliyeitwa emmanuel hakwenda kwake,sasa akaniambia huenda alienda kwa rafiki yake mmoja alikuwa akiitwa maganga.
Mimi “Duuu sijui nitafanyaje na mlango amefunga”
Deborah ” Kwani kwao maganga hupafahamu?”
Mimi ” mimi napajua hapa kwenu tu Debo,kwao marafiki zake sipajui!”
Debo “Nisubiri nivae nije nikupeleke”.
Mimi “Kama ni mbali tusiende ni bora nikarudi ili nisije kupishana nae njiani”
Debo ” Yule mimi naijua akili yake,unadhani anarudi muda huu,utakaa nje mpaka uchoke,wewe subiri nije nikupeleke”
Basi baada ya Deborah baada ya kujiandaa alitoka ndani na taa ya chemri tukandoka kuelekea kwa huyo Maganga ambaye ni rafiki yake na jamaa ambapo Deborah aliyekuwa demu wa jamaa alidhani uenda angekuwa hapo!
Tulipofika hapo kwao Maganga tulianza kumgongea,cha ajabu jamaa akatoka akionyesha kabisa alikuwa amelala!.
Maganga ” Mambo vipi”
Deborah ” Poa,Ema yuko wapi?”
Maganga “Alipita hapa mida fulani akaniambia anaenda kupiga buku kwao Jackson”
Deborah “Jackson yupi?”
Maganga “Jackson Mashida”
Maganga “Kwani kuna nini?”
Deborah “Aah ameondoka na funguo za nyumba,sasa ndugu yake alikuwa anazihitaji!”
Maganga ” Nendeni kwao Jack mtamkuta”
Basi tuliondoka tena nikifuatana na binti Jasiri Deborah,ingawa ilikuwa saa 5 ya usiku lakini Deborah hakuonyesha kabisa kujali hilo,nadhani kwakuwa wao walikuwa wamezaliwa vijijini na kukulia huko haikuwa taabu kwao!.
Haikupita muda tukawa tumefika kwa huyo dogo tuliyeelekezwa kwao.
Tulipofika Deborah aligonga mlango na hatimaye mlango ulifunguliwa!.
Jamaa “Oooh Debo mambo”
Debo “Poa,vipi”
Debo ” Ema yuko wapi?”
Jamaa akaanza kuita “Oyaa ema,njoo unaitwa huku”
Sasa kile kinyumba kilikuwa na chumba na sebule halafu juu kimeezekwa kwa nyasi,mimi wakati huo nilikuwa nimesimama kwa mbali kidogo,Deborah yeye alikuwa pale mlangoni.
Jamaa haikuchukua muda akawa ametoka nje.
Aliponiona akaanza kusema ” Aaah kaka,nilijisahau nikaondoka na funguo,ila ningewahi kurudi”
Sasa anasema angewahi kurudi wakati muda huo ni saa 5 ya usiku!,nilimtazama kwa jazba lakini ilibidi nikaushe,sikutaka kunyesha kuchukizwa!
Sasa kumbe wakati ameenda kuchukua funguo ndani si ikasikika sauti ya binti,nadhani kuna kitu alikuwa akimuiliza na jamaa akimjibu.
Kumbe wakati huyo Jackson yeye akipiga buku hapo sebuleni,ema yeye alikuwa akivinjari na kibinti fulani kule chumbani!.
Aliponiletea funguo ndipo Deborah akaanza kumuuliza ” Ema huyo ni nani?”
Jamaa akawa anajifanya kama hajasikia “Unasema?”
Baada ya kukabidhiwa funguo nilikuwa namsubiria Debo tuondoke lakini binti wa watu akaanza kuwaka,akaiweka ile taa chini akasukuma mlango akazama mpaka ndani!,baada ya muda akatoka amemkwida binti fulani ambaye alikuwa yupo na chupi tu!,ngumi na makonde ya kike yakaanza kurindima hapo na matusi juu!.
SEHEMU YA 4
Ngumi na makonde yaliendelea pale huku matusi mazito mazito yakichukua nafasi,kiukweli yule Deborah alikuwa na nguvu sana,alikaweka chini kale kabinti akawa anakasukumia ngumi za kike zisizo kuwa na idadi,sasa yule Ema yeye alipoingia ndani hakutoka nje,ilibidi mimi na huyo jamaa aliyeitwa Jackson tuingilie kati ule ugomvi kuachanisha!.
Deborah alikuwa amechukia sana huku akimporomoshea matusi yule mshikaji wake Ema ambaye hakutaka kabisa kutoka nje!.
Mimi ” Debo nisikilize,hebu achana na haya mambo ya ugomvi tuondoke,ni usiku sana sasa hivi”
Debo ” Hapana umughaka wewe nenda mimi niache”
Kiukweli alikuwa amejaa sumu sana kwa wakati huo!.
Baada ya kuona lile timbwili haliwezi kuisha muda huo,nilimvuta yule jamaa ambaye aliitwa Jackson nikamwambia amchukue huyo dada aliyekuwa akipigwa ampeleke kwao vinginevyo mambo yangekuwa makubwa.
Mimi “Jack hebu sikia,wewe mchukue huyo demu umpeleke kwao ili hawa wabaki wawili wazungumze yataisha”
Jackson “Unajua huyu demu jamaa amekuja nae hapa sijui kamtoa wapi mi ndo mara ya kwanza namuona na wala si mwanafunzi wa skuli”
Mimi “Hebu mwambie Ema namuita”
Nilitaka kusovu ile ishu ili isiendelee kutupigia kelele pale nimchukue binti wa watu Deborah turudi tulipotoka.
Jackson “Jamaa anasema wewe sepa”
Mimi ” Anasema nisepe,nisepe wapi?,umemwambia namuita?”
Jackson “Nimemwambia lakini kasema wewe ndiye umemleta huyu demu wake kumfanyia fujo”
Baada ya jamaa kuniambia vile nikaona kumbe yule Ema ni mjinga wa hali ya juu,mimi kikichonipeleka pale ni funguo na wala si mambo ya kijinga kama alivyodhani,sasa hakutaka kabisa kutoka nje kuja kuongea na mimi aliamua kukatalia ndani.
Sasa nikamwambia Jack amchukue yule binti amtoe waende pembeni ya nyumba wajifanye amempeleka ili iwe rahisi kwa Deborah kutoka pale,kweli!,baada ya muda kupita Deborah alipunguza hasira na nikamwambia tuondoke akawa amekubali lakini wakati tunaondoka alikuwa akimtukana sana Ema matusi ya nguoni!.
Tuliondoka sasa kuishika njia ya kuelekea nyumbani huku nikiamini baada ya sisi kuondoka Jack na yule demu wangerudi maana nilimwambia ajidai anamsindikiza ili kwa debora iwe rahisi kuondoka!.
Deborah “Huyu mjinga atanitambua mimi ni nani,we ngoja uje uone!”
Mimi “Huyo ni mshikaji wako debo msamehe tu,ameteleza”
Deborah “Wewe umekuja juzi tu,huyu mjinga huijui akili yake,mara kibao tu nishamfumania,kuna siku nimemfuma akiwa na rafiki yangu”
Basi ikabidi nifunge bakuli langu ili niendelee kumsikiliza Debo akifunguka kwa hasira.
Deborah “Ema ni mshenzi sana,wewe hujamjua vizuri!,yaani safari hii labda ahame shule lakini vinginevyo atanijua mimi ni nani!”
Basi pamoja na kumtaka amsamehe Ema lakini ilionekana kama natwanga maji kwenye kinu!,baada ya mwendo mrefu nilimfikisha kwao na mimi ikabidi nielekee nyumbani usiku huo.Kiukweli lilikuwa giza totoro na sikuwa na tochi na nilikuwa peku!.
Nilipofika nyumbani,nilichota maji kwenye pipa nikaingia bafuni kuoga,baada ya kuoga niliingia jikoni kuangalia jamaa kama alikuwa amepika lakini nikakuta chakula kimeisha,inavyoonekana alikuwa amepika chakula kinachomtosha yeye mwenyewe akala akamaliza,sasa sikutaka kumtupia lawama maana siku zote mtembezi hula miguu yake!.Ilibidi kwa usiku ule nilale na njaa.
Asubuhi kulipo pambazuka,niliwahi kuamka mida ya saa 12 nikasema niende kule kwenye ile miembe miwili nikatafute kile kitochi kabla watu hawajaanza kupita ile njia wasije kuokota kile kitaa halafu nisiwe na majibu ya kumpa Ba’mdogo!.
Niliondoka hiyo asubuhi kwa kukimbia mdogo mdogo mpaka lile eneo la tukio,nilipofika pale cha kwanza kabla ya yote nilitazama kama bado ile maiti ipo au la!,kitu cha ajabu ule mwili haukuwepo lile eneo!,nilibaki najiuliza ni nani aliuweka pale hiyo usiku lakini nikakosa majibu,mpaka wakati huo nilikuwa siamini kabisa ishu za uchawi!,sema nilikuwaga naogopa kutokana na kusimuliwa kuhusu lile eneo.
Basi nikaanza kutafuta ile tochi bila mafanikio,nilicho ambulia kupata ni zile ndala zangu tu!.Niliwaza ningemwambia nini mzee atakaporudi maana ni lazima angeiulizia ile tochi!.
Baada ya kuitafuta kwa muda na kuikosa ilibidi niondoke kurejea nyumbani,nilipofika nyumbani cha kwanza ilikuwa ni kuingia jikoni na kukoroga uji maana nilikuwa nina njaa ya kufa mtu!.Mpaka wakati huo yule jamaa alikuwa bado hajarudi nyumbani.
Nilipomaliza kunywa uji nikakusanya nguo zangu na kuelekea lamboni kwa ajili ya kufua!.
Nilimaliza kufua mida ya saa 4 asubuhi,sasa wakati naondoka zangu kurudi nyumbani nikamuona demu mmoja alikuwa anafua nguo upande wa wanawake,kiukweli alikuwa na mtungi wa maana ila sura ilikuwa ya baba yake(mbovu).Sikuweza kumfuata maana kule kulikuwa na akina mama wengine wakifua hivyo nikaogopa kwenda,nikasema kama nikimuona siku nyingine ingebidi niimbe nae ili awe poozeo langu hapo kijijini!.
Basi nilipofika nyumbani nikamkuta mshikaji keshafika,sasa ajabu ni kwamba nilipo mpa hai jamaa akanikaushia.
Mimi “Mbona nakupa hai unauchuna?,nini shida?”
Ema “Achana na mimi wewe jamaa,kwani lazima niitikie?”
Kiukweli yale majibu yaliniskitisha sana na nikajiuliza ni kipi ambacho nilimkosea,kama ni jana usiku mimi nilienda kwa ajili ya kufuata ufunguo,na nilikuwa najitahidi sana kumtetea kwa demu wake lakini jamaa alidhani mimi ndiye chanzo cha yote!.
Basi na mimi sikutaka kujikomba kwake ilibidi nikaushe,nilipanga kumsimulia mkasa niliokutana nao usiku lakini kwasababu hakutaka maongezi na mimi ilibidi nikaushe!.
Ilipofika mida ya jioni mzee alirejea kutoka mjini kama kawaida!.
Usiku huo jamaa alianza kutafuta kile kitaa kwa ajili ya matumizi lakini hakutaka kuniuliza maana alikataa kuongea na mimi,sasa na mimi nikawa namchora tu!,yaani alisahau kabisa kama jana yake tu alikuwa amenipa wakati naenda kutazama mpira!.
Sasa nadhani uzalendo ulimshinda akaniuliza.
Ema ” Hivi ile tochi iko wapi mbona siioni?”
Mimi “Umetafuta kila sehemu umeikosa?”
Ema “Haionekani”
Mimi ” Sijui sasa itakuwa wapi”
Namshukuru Mungu jamaa hakukumbuka kabisa kama jana yake tu alikuwa amenipa halafu yeye akabaki na ile ya Headmaster.
Sasa kwakuwa jamaa alikuwa amezira,hakutaka kabisa stori na mimi na ulipofika muda wa kulala alichukua godoro lilikuwa limechomekwa juu ya mbao za dari akatandika chini akalala,mimi nikalala kitandani kama kawaida!.
Ile shule ilikuwa na madarasa manne pamoja na ofisi ya mkuu wa shule na ofisi ya walimu wengine,yaani kuanzia form 1 hadi form 4 kulikuwa na darasa moja moja,shule nzima ilikuwa na walimu wanne pekee ukiongeza na Headmaster.
Walimu wawili walikuwa wameajiriwa na serikali na walimu wengine wawili walikuwa wanalipwa na kijiji,sasa walimu wote hao wao walikuwa wanakaa kule senta,hapo shuleni tulikuwa tunakaa sisi maana kulikuwa na nyumba moja tu ya Headmaster.
Sasa nakumbuka baada ya kupita wiki kadhaa ndani ya mwezi huo wa 3 mwaka 2004,siku hiyo mimi baada ya kumaliza kula nikaenda zangu kulala,jamaa yeye akabaki sebuleni akiwa anasoma,sasa ilipofika mida ya saa 5 naye akawa amekuja kulala,kama kawaida yake hakutaka kabisa kulala na mimi pale kitandani akawa anatandika chini analala.
Sasa usiku mkubwa nikashitushwa na kelele zikiwa zinaita “Mamaaaaa…….Mamaaaaaaa……..Mamaaaaaaa”.
Hizo kelele zikawa zinaita kule madarasani,sasa nikaamka kutazama chini kwenye godoro jamaa sikumuona nikajua uenda atakuwa sebuleni anasoma.
Haukupita muda ba’mdogo nae akawa ameamka na kutoka nje kuja kutuita.
Ba’mdogo “Mnazisikia hizo kelele kama mimi navyosikia?”
Mimi “Ndiyo baba na mimi nimeamka kwasababu ya hizo kelele”
Ba’mdogo “Hebu mwambie Ema anipe hilo panga”
Mimi “Ema hayupo”
Ba’mdogo ” Hayupo?,ameenda wapi?”
Mimi “Nimeamka sijamkuta baba”
Ba’mdogo “Ina maana jana hakulala hapa”
Mimi”Alilala baba,sema niliposhituka sijamkuta”
Sasa wakati naendelea kumjibu headmaster zile kelele zikaanza tena
“Mamamaaa…..Mamamaaaaa…..mamamaaaaaa”
Sasa safari hii tulisikia sauti ilikuwa ya Ema na ilisika kile madarasani!,hatukujua ametoka vipi nje maana milango ilikuwa imefungwa na makomeo!
SEHEMU YA 5
Ba’mdogo ” Hebu ingia humo stoonj niletee panga”
Basi nikachukua tochi nikaingia stoo nikatoka na panga.
Ba’mdogo ” Shika hizi gambuti(Gun boot/Rain boot) uvae”
Ba’mdogo “Hakikisha unakaa nyuma yangu”
Mimi “Sawa baba”
Basi Ba’mdogo akafungua mlango tukatoka nje kuelekea kule kwenye vyumba vya madarasa ambako sauti ilikuwa ikitokea.Mpaka wakati huo hatukuwa na shaka kabisa kwamba ile sauti iliyokuwa ikisikika ilikuwa ni sauti y Ema.
Kiukweli mimi nilibaki kushangaa sana kwasababu sikufahamu jamaa alitokaje nje na milango yote ilikuwa imefungwa kwa ndani,pili,nakimbuka jamaa mara mwisho alipomaliza kusoma aliingia ndani akafunga mlango na kuingia kulala.Nilibaki najiuliza sana maswali yasiyokuwa na majibu.
Basi tukawa tunatembea kwa kunyata kuelekea lile darasa ambalo Ema alikuwa akilia akihitaji msaada!.Ba’mdogo alikuwa ameshika tochi mkono wa kushoto na kulia kukiwa na Panga huku mimi nikiwa nyuma yake.Tulipofika pale kwenye Darasa ambalo kelele zilisikika mara gafla kukawa kimya ajabu.
Ba’mdogo akaanza kuita “Ema..”
Aliendelea kuita “Ema unanisikia?”
Pamoja na kuita lakini kulikuwa ukimya wa ajabu.
Basi baba alivua koti alilokuwa amevaa akaniambia nimshikie.
Kwa ukakamavu akasonga mpaka kwenye mlango wa darasa,alipofika mlangoni akaniambia nimsogelee,wakati huo mimi macho yangu yalikuwa hayatulii kwa hofu,nilikuwa nageuka kila muda kuangalia nyuma isije ikawa kuna mtu nyuma yetu.Nilikuwa najisemea endapo mambo ya kiharibika ningetoka nduki kurudi nyumbani nikamuacha dingi mdogo akipambana.
Basi ba’mdogo akausukuma ule mlango kwa panga,hakuingia ndani bali aliishia pale mlangoni akawa anachungulia kwa tahadhari kubwa.Baada ya kumulika mle ndani ya darasa kwa umakini ndipo tukamuona mtu amening’inizwa kwenye mbao za kenchi kichwa chini miguu juu huku akiwa uchi kama alivyozaliwa.
Ba’mdogo aliendelea kumulika pande zote za lile darasa ili kuona kama kuna watu,sasa wakati huo bado tunachungulia kwa uoga na tahadhari kubwa,basi aliingia ndani akaniambia na mimi niingie.
Alipo mulika kwa makini ni kweli alikuwa Ema na safari hii ni kama alikuwa haelewi chochote,sasa baba akawa anaita ” Ema….Emaaa”.
Aliita sana lakini mtu aitiki wala hatikisiki,ndipo akaniambia “Hebu nipe hilo koti”.Baada ya kumpa koti lake,alisogea mpaka pale katikati ya chumba akaanza kumpiga na lile koti huku akiita “Ema……wewe Ema”.
Ghafla jamaa alishituka tena akaanza kupiga kelele kama mwanzo,ndipo tukatoka nduki mle darasani baada ya ule mshituko na zile kelele!.
Baada ya dingi mdogo kutoka nduki ndipo nikasema kumbe hatari haina baba mdogo wala baba mkubwa!.Ukimya ulitawala kwa muda ndipo sasa tulirudi tena pale mlangoni.
Ba’mdogo akaanza kuita tena “Emaa…”
Alipoita kama mara tatu jamaa akazitambu a sauti.
Ba’mdogo “Emaaa”.
Ema “Eenh”
Ba’mdogo “Ni mimi mwalimu Wambura”
Baada ya jamaa kusikia ni Headmaster alikuwa akimuita akaanza tena kulia huku akiomba msaada.
Ema “Nisaidie mwalimu naumia”
Ema “Nisaidie nakufaaa….nisaidie nakufaaa”
Ba’mdogo “Sawa nyamaza nimekusikia”
Basi baba mdogo alisogeza dawati akapata balansi akapanda juu ya dawati akazikata kamba zilizokuwa zimemfunga jamaa miguu.Baada ya kukata zile kamba jamaa alianguka mzima mzima chini huku akipelekea na baba kukosa balansi naye akawa ameanguka chini.
Nilisogea mpaka pale kwa Ba’mdogo na kumsaidia kumnyanyua jamaa aliyekuwa yuko hoi bin taabani.
Sasa baada ya kummulika mgongoni alikuwa na alama za kutosha za fimbo ambazo zifanya jamaa kuvimba mgongo.
Ba’mdogo aliniambia tumnyanyue tumpeleke nyumbani,mpaka wakati huo jamaa alikuwa uchi kama alivyozaliwa na hatukujua nguo alizokuwa amevuliwa zilikuwa zimewekwa wapi!.Muda huo ilikuwa yapata saa 8 usiku.
Baada ya kumfikisha nyumbani akiwa hoi,baba aliniambia nitoe lile godoro alilokuwa analalia na kulipeleka pale sebuleni ili akalale kule.Sasa wakati nikiwa nimelitandika lile godoro na kumlaza Ema ambaye alikuwa anaugulia maumivu ya stiki za mgongoni ambazo hatukujua ni nani alikuwa akimuadhibu,mara ghafla tukaanza kusikia mbuzi analia kule jikoni ambako pia ilikuwa stoo.
Mara ya kwanza nilidhani uenda nitakuwa nimesikia vibaya lakini alipolia mara ya pili ndipo Ba’mdogo nae akawa amesikia.
Ba’mdogo “Huyo siyo mbuzi analia”
Mimi “Nami pia nimesikia baba”
Basi wakati tukiwa tunashangaana,yule mbuzi akalia tena.
“Meeeeeee…….meeeeee”
“Huyo mbuzi anayelia ni wa nani?” Lilikuwa ni swali la Ba’mdogo.
Mimi “Mimi sifahamu Baba”
Ba’mdogo “Sasa kama ufahamu ametokea wapi?”
Mimi “mimi hata sijamuona na niliingia kuchukua panga muda si mrefu,lakini baba kungekuwa na mbuzi wakati napika ningemuona”
Baba mdogo alipigwa na butwaa sana!,basi akaniambia “Hebu muangalie huyu”.
Basi mimi nikabaki pale sebuleni namuangalia Ema,yeye akatoka kwenda jikoni ambako mbuzi alikuwa akilia.
INAENDELEA…….

