MKASA WANGU WAKATI NAUTAFUTA UTAJIRI
Miaka hiyo nikiwa ni kijana mwenye nguvu, walikuja kijijini kwetu jamaa wawili wameongozana na MZUNGU. Muda wote MZUNGU yuko kimya tu, zaidi ya salamu yake ya Jambo Toto, hata wazee aliowakuta aliwasalimia hivyo.
Jamaa wakatoa photo album iliyokuwa na picha ya vitu kadhaa walivyokuwa wanavitafuta. Kulikuwa na picha ya pasi ya mkaa ya Shaba nyekundu, mkuki wenye kichwa (ncha ya DHAHABU), sarafu ya Rupia ya Ujerumani, gudulia la kuhifadhia maji lenye rangi ya bronze na vitu vingine vingi.
Basi wazee wetu wakaziangalia zile picha na wanakubaliana kwamba ni KWELI hizo Mali ZIKO msituni pale kijijini kwetu.
Kimbembe kikaanza wakati wa kufuata taratibu za kuingia msituni. Msituni huko ni ukoo mmoja tu wenye ruhusa ya kuingia kufanya matambiko, nyie wote wengine mnaishia nje ya msitu kwenye bonde lenye nyasi ndefu.
Watu wa ukoo huo wengi walikuwa wameshahamia Dar es Salaam, wengine walokole na wengine wako nje ya nchi kwa sababu ya kisomo chao, pale kijijini mwana ukoo ule kwa wakati huo hayupo.
Basi wazee wetu wakashauri tuachane na biashara hiyo kwani hasira za mizimu ya kwetu ni hasira ya moto, Kali sana na madhara yake ni makubwa mno.
Vijana tukaonywa na kuaswa kuwa kuna hatari kubwa sana mbele yetu iwapo tutaingia msituni kuchukua Mali hizo bila utaratibu.
Tukiwa tumeenda machungani, vijana sita wa kamati ya roho kuchukuchu tukaingia mzigoni, tukaanza kupanga Namna ya kwenda kui face mizimu.
Tukakubaliana kila mmoja akatafute mganga wa kumchanja na kumkinga dhidi ya hasira za mizimu.
Mimi kwetu nilikuwa kijana wa mwisho kuzaliwa na mlinzi wa boma, basi siku mbili kabla ya kuondoka, nikaaga nyumbani kwamba naenda wilayani kutafuta KAZI ya ukarani wa kuhesabu kilo za nafaka, ulikiwa ni msimu wa mavuno.
Baba alikataa kabisa lakini na Mimi nikakaza shingo kibishi, hatimaye siku ya Siku nikaondoka alfajiri nikaongea na wavuvi wakanipeleka hadi visiwani huko, nilikuwa nimeshaelekezwa wapi kuna mganga mkali.
Nilikuwa na mzigo wangu wa kuku kadhaa na mbuzi wawili. Nilipofika kisiwani sikupata taabu sana kumpata Mzee mwenyeji wangu wa kunifanyizia dawa.
Tukafanya dawa kwa siku tatu mfululizo, usiku na mchana, kuchanjwa, kutambikiwa, kuogeshwa madawa, kufukizwa mafusho, kufanya maapizi, NK ndio zilikuwa ibada zenyewe.
Siku ya tano nikaambiwa nisilale, ibada zitaanza SAA tano usiku hadi majogoo. Baada ya mlo wa usiku nikawa nje nakusanya kumi, maana niliambiwa tutafanya tambiko la kukanyaga moto, kumeza moto, na kulala juu ya moto, ili balaa lolote nitakalotupiwa na mizimu liungue. Lengo la ibada ya usiku huo ilikuwa ni kunibadilisha Mimi niwe kiumbe cha moto nisiyedhurika na lolote wala chochote.
SAA tano ikafika, akaja Mzee akiwa ameongozana na binti yake, wakaniamuru nivue nguo zote, nikavua, nikasogezwa hadi kwenye lile lundo kubwa la kuni, nikaambiwa kabla moto haujawashwa, niuzunguke ule moto mara saba huku nikiongea maneno fulani hivi ambayo nilikuwa sijui maana yake na hadi leo siyakumbuki.
Baada ya hapo likaletwa karai kubwa lenye maji baridi sana ya kutoka mtoni, nikaingizwa humo, kisha moto ukawashwa.
Taratibu maji yakaanza kupata moto, moto ukaendelea kuongezeka kwenye maji hadi nikawa sina tena uwezo wa kustahimili joto lile. Nikawa nalia kwa maumivu MAKUU.
Mganga akaamuru nitoke, nipakwe asali mwili mzima. Likaletwa kibuyu cha asali na nikapakwa mwili wote. Nikapewa SAA moja ya kupumzika.
Baada ya hapo nikapakwa dawa nyingine yenye harufu Kali sana. Nikaambiwa niuzunguke tena moto huku nikiongea maneno yale niliyokaririshwa.
Likaletwa chepe, uchatwa moto mwingi nikaambiwa nikanyage nisiogope, nikakanyaga ule moto, kutokana na dawa niliyopakwa sikusikia maumivu hata kidogo. Nikalazwa chini, nikafukiwa na mchana hadi usawa wa shingo, ukaletwa mkaa, ukawekwa juu yangu kama wafanyavyo kina mama wakipalia pilau. Nikakaa na huo mkaa hadi ukaishiwa nguvu kabisa.
Baada ya hapo nikaambiwa zoezi limekwisha, bado ibada moja tu ya shukrani.
Basi kuna mbuzi mmoja alikuwa amebakia, na kuku mmoja. Mganga akaita vijana wake, mbuzi na kuku vikachinjwa, vikawa vinaandaliwa. Mganga akaanza kutengeneza nyungu nyingine ya kufukiza, akachanganya madawa, nikapewa shika jekundu nijifunike nikafukizwe.
Ile nyungu ilikuwa ni bangi Kali sana, nikakohoa na kupiga chafya zisizo na kikomo, hatimaye nilitolewa pale jicho likiwa nyanya na stimu za kutosha.
Enzi hizo ndio zilikuwa Zama za viroba vya Konyagi, nikaandaliwa viroba vitatu, na muda huo kuku kaiva, nikaletewa firigisi, moyo, maini, shingo, kibawa, na kipaja, nikala kwa pupa mno, njaa ilikuwa Kali na Konyagi ilikuwa inanikwangua tumbo.
Mapande kadhaa ya mbuzi zile sehemu laini zinazoiva kwa wepesi nazo nikaletewa, nikaambiwa nishibe nikapumzike.
Kwa mara ya kwanza nikapewa sehemu nzuri ya kulala, mchumba safi chenye sakafu ya saruji, mlango wa mbao, godoro la Sufi likilotandikwa mashuka yote mekundu.
Usingizi ukiwa unaanza kunichukua, nikasikia mlango ukigongwa, alikuwa ni mganga, Akaniambia nilale siku nzima, akamleta na Yule bintiye kwamba aniliwaze na aniburudishe na kunipumzisha kabla sijaenda kuzitafuta Mali za Ujerumani.
Nilikuwa na uchovu na libido kama lote, nilisimamia show mpaka nikalala kama mfu.
Kesho yake alfajiri nikafanyiwa mipango ya boti, nikarudi home. Nilipofika nyumbani nikaanza kuulizia habari za mwenzangu, wamefikia wapi na kujiimarishia ulinzi?
Wawili bado walikuwa hawajamaliza mambo yao hivyo ikabidi tuwasubiri ili tuliingie pori wote kwa pamoja.
Baada ya Siku kadhaa nikaanza kuona hali tofauti mwilini mwangu, maumivu makali wakati wa kukojoa, baada ya Siku mbili nikagundua kuwa nina usaha unachuruzika uumeni, halaula, nimelikwaa GONO. Aibu hii nitaiweka wapi kijijini? Na Mimi utajiri nautafuta kwa ajili ya mwali wangu Semeni, ambaye amenitunzia bikira yake tangu avunje ungo?
Nikauza mbuzi, nikahamia kwa mjomba Kijiji jirani, nikajitibu huko hadi nikapona. Mganga kanisababishia GONO, Hawana sio mganga, ni Yule binti yake. Hapana sio Yule binti aliyenisababishia GONO, Ila ni Yule MZUNGU WA Jambo Toto!!! Hapana naye namsingizia tu, Ila ni zile Mali za Ujerumani. Hapana nazo nazisingia, ni tamaa zangu tu zankupata utajiri wa mang’amung’amu. Yessss….. Hili ndio jibu sahihi. Mizimu imenipiga kabla hata sijavamia msitu wa tambiko.
Mizimu unisamehe sana, nikajiapiza kutoisaliti tena mizimu yetu, na kutowasikiliza wakubwa zangu kukakomea hapo.