Kilinichopata, Baada Ya Kumuacha Mke Wangu Kwa Dharau
Mimi na mke wangu ni walimu kitaaluma, ingawa kwa sasa mimi sifundishi tena. Tulipokutana, tulikuwa wote tunafundisha katika shule moja binafsi inayoheshimika. Baadaye, tukaanzisha biashara ya vipodozi – ingawa ukweli ni kwamba mke wangu ndiye aliyefungua biashara hiyo kwa kutumia akiba yake, kwani mimi sikuwa na imani sana na biashara. Nilikuwa naona kama biashara ni ya kina mama.
Nilipuuza sana biashara hiyo hadi siku moja nilipomuona akipiga mahesabu. Nilishangaa alivyokuwa anapata pesa nyingi. Nikaanza kuchukua biashara hiyo kwa uzito. Nikamshawishi mmoja wetu aache kazi ili asimamie biashara. Kwa kuwa tayari niliona kuna faida, nilijitolea kuacha kazi. Biashara ikashamiri. Ndani ya miaka mitano tulikuwa na maduka mawili ya jumla, mtaji ukapanda hadi milioni 200. Tulijenga nyumba, tukapata gari, maisha yakawa mazuri mno. Nilikuwa nenda China kuchukua mizigo kila kitu kilikuwa kama ndoto.
Lakini kama kawaida, pesa huleta kiburi. Nikaanza kuchepuka na wanawake wa mjini. Nilijikuta nampa mwanamke mwingine kila kitu nyumba, kodi ya milioni na ushee kwa mwezi, mavazi, anasa. Nikawa naishi naye karibu muda wote. Mke wangu alikuja kugundua, akamfuata yule mwanamke, akamkabili kwa maneno. Nilirudi nyumbani na hasira, nikamwambia mke wangu maneno makali sana kwamba nilimuoa kwa sababu nilikuwa maskini, lakini sasa si wa hadhi yake. Nilimdhalilisha kwa maneno ambayo siwezi hata kuyakariri. Nilijua yeye ndiye chanzo cha mafanikio yetu, na hiyo ilinifanya nijisikie duni hivyo nilipotafuta namna ya kumkandamiza, nilitumia maneno makali.
Niliwahusisha hata ndugu zangu, nikaanza kumchafua nikisema eti ni mchawi, hana msaada kwao. Kwa kuwa wengi walikuwa wanamwonea wivu, waliniunga mkono kasoro baba yangu. Baba alinambia maneno mazito: “Mwanangu, kuna wanawake wa kuoa na wa kula nao maisha. Wewe tayari ulipata wa kuoa. Usiache wake kwa sababu ya sura au starehe.” Lakini sikusikia. Nilimwambia mke wangu aondoke.
Tuligombana, nikamfukuza. Aligoma kuondoka. Nikaanza vituko, nikamletea mwanamke nyumbani. Mwisho nikajiondokea mwenyewe.
Nilimnyang’anya mke wangu biashara. Akabaki na kazi yake ya ualimu. Akafungua duka dogo tu, akauza online kama zamani. Hakuwa na cha kutegemea isipokuwa nguvu zake. Nilikuwa sijali.
Sasa yule mwanamke niliyehamia kwake akanionesha dunia. Matumizi makubwa, utoto mwingi, heshima hakuna. Ukiuliza anaenda wapi – “kwa marafiki”, ukiuliza biashara gani – “hayakuhusu”. Hata simu yake siwezi kuigusa. Matumizi ni makubwa sana, wigi la milioni 7 ni kawaida. Nikajikuta natumbukia kwenye madeni. Nikamwoa kwa nguvu nikidhani atabadilika nikafanya harusi kwao. Lakini hata baada ya ndoa, hakupenda watu wajue kuwa ameolewa. Hata marafiki zake hawakujua mimi ni nani. Heshima haikuwepo. Tulianza kusafiri pamoja hadi China, lakini tukarudi bila mzigo, hela yote inakwenda kwenye starehe.
Nilijua baadaye kuwa hata mimba hataki anatumia vidonge. Nikimuuliza, anasema: “Sijafikia kuzaa, na siwezi kuzaa na wewe, angalia watoto wako walivyo.” Nililia, nilivunjika moyo. Nikamwambia tuachane, akakubali kirahisi, akaondoka bila kuaga. Nikamfuatilia, kumbe yuko Dodoma na mume wa mtu! Akanambia: “Si ulinitamkia talaka? Wewe si mume wangu.” Nilianza kumuomba msamaha, nikaomba mpaka kwa mama yake lakini badala ya kusaidia, akanitumia namba za kutuma hela. Sikuwa na amani.
Siku moja mwisho wa mwaka nikashika simu yake, nikakuta video yake ya ngono akiwa na mwanaume mwingine. Alikuwa amejirekodi. Nilipomuuliza, akanambia: “Wewe si umeachana na mimi? Hujanihudumia, sina sababu ya kukuogopa.” Nililia kama mtoto. Biashara ilishakufa, kodi sina, vitu vya ndani vyote akavichukua akaondoka. Sijui alienda wapi.
Sikuwa na namna, nikalazimika kurudi kwa mke wangu wa kwanza. Nikajinyenyekeza, nikamuomba msamaha kwa moyo wote. Akaniambia: “Karibu, lakini usijaribu kuniingilia.” Sasa niko nyumbani, lakini mambo ni magumu. Mke wangu naye ana mwanaume wake. Anarudi nyumbani asubuhi. Nikimuuliza, ananiambia: “Umeondoka miaka miwili, unadhani nilikuwa nashinda vipi? Watoto wanasoma. Umeacha kila kitu. Tulikula jasho langu.”
Sina wa kunisaidia. Deni kila kona, biashara hakuna, nguvu sina, ndugu wamenikataa. Naumia, nimechanganyikiwa. Mke wangu yuko na mwanaume mwingine, lakini bado yuko nyumbani kwangu. Najua analala kwa mwanaume, lakini sina pa kwenda. Sijui nifanye nini tena. Nimebakia na maumivu, majuto, na upweke.