MCHEPUKO WA RAISI
Chapter 2
Kuna siku Linda alimuuliza Monica kwa ujanja, Hivi ile nguo yako ya bluu uliyovaa siku ile ukiwa na mzee, bado unayo? Monica akajibu kwa mbwembwe, “Ninayo mwanangu, na sijaiosha kabisa, ina kumbukumbu zote!”
Linda akamwambia, Basi usiioshe, iweke hivyo hivyo kama kumbukumbu. Lakini moyoni Linda alikuwa anajua kuwa ile nguo ni bomu la atomiki.
Mwaka 1998, mwanasheria Kenneth Starr alikuwa anafukuzia skendo nyingine ya Clinton, lakini Linda akamvutia pembeni na kumwambia: “Acha kutaabika, huku kuna mzigo wa kutosha!” Akamkabidhi zile kanda za sauti na kumwambia kuhusu ile nguo ya bluu.
Habari zilipovuja kwenye magazeti na TV, dunia ilisimama. Hillary Clinton alishtuka kama mtu aliyepigwa na butwaa. Bill Clinton akaitisha kikao cha dharura na kusema ile sentensi yake maarufu: “Sikuwa na uhusiano wa kimapenzi na huyo mwanamke.”
Hapo ndipo mchezo ulipogeuka kuwa vita ya kisheria. Upande wa mashtaka ukasema, “Kama hujamgusa, tupe ile nguo ya bluu tuifanyie vipimo vya DNA!”
Wakati mwanasheria Kenneth Starr alipopata ile nguo ya bluu kutoka kwa Monica kupitia kwa Linda Tripp, alijua kashashinda mechi. Walichukua ile nguo na kuipeleka maabara kufanya vipimo vya DNA.
Matokeo yalipotoka, yalikuwa positive 100%. Ikathibitika kuwa mzee Clinton alikuwa amedanganya dunia nzima na jopo la majaji. Hapo ndipo mzee mzima alianza kutoa jasho la dharura. Alilazimika kurudi tena kwenye TV, lakini safari hii hakuwa na ile jeuri ya mwanzo. Kwa sauti ya upole na unyonge, akakiri Ni kweli, nilikuwa na uhusiano usiofaa na Miss Lewinsky.
Sasa piga picha Hillary anajisikiaje. Dunia nzima inajua mume wake kachepuka na binti mdogo ofisini kwake. Inasemekana Hillary alikuwa na hasira kiasi kwamba Bill alilazimika kulala kwenye sofa la White House kwa wiki kadhaa!
Lakini Hillary alikuwa mwanasiasa mjanja. Alijua akimwacha Bill kipindi hicho, maadui zao wangeshinda. Akaamua kusimama naye Stand by your man. Alitokea hadharani na kusema hii ni njama kubwa kutaka kumuangusha Rais. Hapo ndipo Hillary alipoonyesha kuwa yeye ni mwanamke wa chuma.
Wakati mzee Bill anapambana kubaki madarakani, Monica Lewinsky maisha yake yalianza kuwa jehanamu. Vyombo vya habari vilimshambulia kila upande. Watu walimtukana, walimcheka, na kumwita majina mabaya.
Yule binti aliyekuwa na macho ya mahaba na umbile la kuvutia, ghafla akawa mtu anayechukiwa zaidi Marekani. Alipoteza kazi, alipoteza marafiki, na akawa hawezi hata kutembea mtaani bila kuzungukwa na mapaparazi. Monica alikuja kugundua kuwa kwenye mchezo wa wakubwa, mdogo ndiye anayeumia zaidi.
Baraza la Wawakilishi lilipiga kura ya kumtoa Clinton madarakani, lakini Baraza la Seneti likamuokoa. Bill Clinton akabaki kuwa Rais mpaka anamaliza muda wake mwaka 2001. Alitoka madarakani akiwa bado anapendwa na watu wengi, lakini jina lake lilibaki na doa la maisha ambalo haliwezi kufutika.
MWISHO

