ROHO YAKE INADAI
ONYO: Wakubwa tu, kuanzia Miaka 18, ndio wasome hii Hadithi
Sehemu Ya 8
Asubuhi ya saa moja na nusu …
.
“Olivia!” Mama akaita. Akajaribu kufungua mlango, haufunguki! Akapigapiga kioo kumshtua, hamna majibu. Olivia alikuwa anatazama mbele, akitabasamu, akipeleka usukani kushoto na kulia.
.
.
“Mama,” Brian akaita. Alikuwa ameshaanza kupata hofu. Wisconsin alimshika Mama Brian mkono akamwambia, “Huyo si Olivia!” mara Olivia aliyekuwepo kwenye gari akageuza uso wake na kuwatazama. Ajabu uso wake ulibadilika ghafla na kuwa mweupe pe kama kitambaa. Michirizi meusi ikachipuka usoni. Macho yamekuwa meusi ti na fidhi zake zikajazwa na meno mithili miba.
.
.
Mioyo yao ikawalipuka. Hakuwa Olivia! Mara gari likaanza kwenda. Olivia aliyekuwapo ndani akiangua kicheko haswa. Walilikimbiza lakini ikafikia pahala wakachoka, wakabaki wamesimama wakitazama gari layeya. Wanahema kama mbwa.
.
.
Mara gari nalo likasimama, kama umbali wa hatua hamsini za mtu mzima toka walipo. Wakatazamana. Ila kabla hawajalijongea, wakamtafuta kwanza Olivia. Hakuwapo miongoni mwao.
.
.
Walipotazama vema, kumbe walimwacha nyuma wakiwa wanalikimbilia gari. Taratibu alikuwa anakuja kwa kukimbia akiwa amechoka haswa, anaburuza miguu.
.
.
Lakini kabla hajawafikia, nyuma yake, kwa mbali, walimwona kuna mtu anamjia. Mtu mrefu mweusi. Hawakujua mtu huyo ni nani, ila alikuwa anakuja kwa kasi mno! Mioyo ikawalipuka.
.
.
Brian akapayuka, “Olivia, kimbia!” lakini Olivia hakuwa anaweza kukimbia tena zaidi ya pale. Miguu yake haikuwa na uwezo huo tena.
.
.
Na mtu yule nyuma yake alikuwa anakaribia kwa mafungu na mafungu. Basi Brian akajikuta anaanza kukimbia upesi kumwendea Olivia. Alikuwa akikimbia huku akiita. Alipomfikia akamnyaka mtoto huyo na kuanguka naye chini. Yule mtu aliyekuwa anamkimbiza, akapita vuuup kama kivuli! Haikuonekana tena ameelekea wapi. Alipotea kana kwamba mwanga wa umeme ukizima.
.
.
Wisconsin na Mama Brian wakasonga karibu. Wakamnyanyua Brian na Olivia toka barabarani. Mama akamtazama Olivia kwa kumkagua, “Upo sawa?”
.
.
Olivia akatikisa kichwa. “Ndio, niko sawa.” uso wake ulikuwa na woga sana. Alimkumbatia Mama Brian kwanguvu akilia.
.
.
“Nyamaza, Olivia. Yatakuwa sawa, usijali,” mama akamtuliza. Akambusu kwenye paji lake la uso na kumyanyua kumweka kwenye nyonga yake. Wakajongea gari na kukwea, wakaliwasha na kutimka zao. Gari halikuwa na shida tena kama hapo awali.
.
.
“Inabidi tumalize kazi ndani ya siku tatu tu,” akasema Wisconsin. “Endapo siku hizo zikizidi, tutakuwa katika hatari ya kupoteza maisha.”
.
.
“Kwanini?” Mama Brian akauliza.
.
.
“Punde tutakapoanza kushughulika na mihimili, kazi itakuwa kubwa sana. Kama vita hiyo ikizidi zaidi ya siku tatu basi ni wazi tutakuwa tumeshindwa. Ni siku tatu tu zimebaki tangu mwezi kupevuka kuwa kamili. Inabidi tutumie siku hizo, vinginevyo itatuwia vigumu.”
.
.
Basi baada ya maneno hayo hakukuwa na soga zinginezo. Kulikuwa kimya tu. Bado watu walikuwa na mashaka, wakawa wanatazama huku na kule madirishani wakiomba wafike salama.
.
.
**
.
.
Saa tatu asubuhi …
.
.
Kilikuwa ni kipindi cha pili, somo la Jografia. Ingawa Brian alikuwa darasani, akili yake ilikuwa mbali sana. Alikuwa anamtazama mwalimu, ungeweza kudhani yupo makini, lakini akili yake ilikuwa kwenye masumbuko.
.
.
Alikuwa anawaza mambo yaliyotukia jana, lakini zaidi alikuwa anawaza kumhusu yule mhimili wa pili baada ya Padri Alfonso. Atakuwa ni nani? Akaweka tama akiendelea kuwaza.
.
.
Muda si mrefu, akamwona kuna mtu anaingia darasani . Hakumwona mtu huyo ni nani, ila alikuwa ni mwanaume aliyekuwa amevalia koti refu jeusi na kofia. Alimnyookea mwalimu na kuongea naye kidogo wakinong’ona. Brian akawatazama kwa umakini.
.
.
Walizungumza kwa kama dakika moja wakipeana ishara ya kutikisiana vichwa kwa kuelewana. Punde kidogo katika maongezi yao, wakiwa wananong’ona, wakataja jina la Brian! Brian akaduwaa. Hakusikia maneno yote yale waliyokuwa wanayazungumza isipokuwa lile jina lake tu.
.
.
Akajiuliza ni nini mwalimu wake na yule mgeni asiyemjua walikuwa wanaongelea mpaka kumtaja? Mara maongezi yao yakakoma, walinyamaza kwa kama sekunde mbili, alafu wakageuza nyuso zao kumtazama Brian. Kisha wakatabasamu.
.
.
Brian akapigwa na kofi la hofu. Yule mwanaume mgeni alikuwa ameziba uso wake kwa rangi nyeupe na nyekundu hivyo hakuwa anatambulika. Mwalimu naye alikuwa amegeuka uso wake ukiwa unatisha kusivyo kawaida.
.
.
Katika namna ya ajabu, wakiwa wanatembea kana kwamba wanapelekwa na umeme, wakaanza kusonga kumfuata Brian! Walikuwa wamekodoa macho na mikono yao wameinyoosha kumkamata kijana huyo.
.
.
Brian akapatwa na woga sana. Akajibania ukutani kwanguvu akijikunyata. Akafumba macho na kukunja uso wake kwa hofu. Punde akahisi mkono wa baridi ukiwa umemkamata, akapiga kelele kali.
.
.
“Brian!” mwalimu akaita. Brian alipofungua macho, akamwona mwalimu wake akiwa amesimama kando. Ndiye yeye alikuwa amemshika. Hakukuwa na mtu mwingine pamoja naye! Darasa zima lilikuwa limetulia, wanafunzi wote wanamtazama.
.
.
“Brian, una shida gani?” mwalimu akauliza akimtazama kwa ukaribu. “Uko sawa?”
.
.Brian akakwapua mkoba wake na kwenda nje ya darasa. Akaketi nje kwenye benchi akiendelea kuwaza kile alichokiona. Alihisi anachanganyikiwa. Aliona atoke mazingira hayo ya shule aende kuliwaza akili yake huko nje.
.
.
Akatembeatembea akiwa amedumbukiza mikono yake mfukoni. Akatazama magari na makazi ya watu. Akatazama wapita njia na anga, angalau akili yake ikapumzika. Hapo ndiyo akapata wazo la nini cha kufanya.
.
.
Upesi akaanza kutembea akielekea upande wa mashariki na ilipo shule yao. Baada ya kutembea kwa kama dakika nane tu, akawa amefika mbele ya ofisi kubwa ya mtaa waishio. Hapo akatoa karatasi kadhaa kwenye mkoba wake na kuzishika mkononi. Zilikuwa ni karatasi zenye nembo na jina la shule yake.
.
.
Akazama ndani ya ofisi, akajitambulisha kwa majina na kusema haja yake kwa dada wa mapokezi ya kuwa amekuja kufanya ‘projekti’ fupi kama mojawapo ya kazi walizopewa huko shuleni.
.
.
“Sitachukua muda wako, dakika tatu zinanitosha kabisa. Nahitaji kufahamu tu watu ambao wamefanya kazi kwa muda mrefu sana hapa ofisini, kujua idadi yao ili tuone ni namna gani vizazi tofauti vinavyofanya kazi kwa pamoja,” akajieleza Brian akijitahidi kutopepesa macho yake. Basi yule mdada wa mapokezi akamtazama kidogo kisha akatikisa kichwa, “Nyie wanafunzi huwa wasumbufu sana …” akasema huku akiwa anafungua droo yake. “Mkija hapa hamjui kama watu wana kazi zao, nyie mnataka tu mfanyiwe ya kwenu mwende!”
.
.
Akafunga droo na kumpatia Brian karatasi kadhaa, Brian akaanza kuzipitia kwa wepesi. Alichukua muda mfupi sana, dakika moja tu, akayarejesha.
.
.
“Umemaliza?” akauliza dada wa mapokezi akistaajabu. Brian akatabasamu, “Ndio, ahsante.” akanyanyuka na kutoka ndani ya ofisi. Akatembea upesi kuelekea getini, ila kabla hajatoka, akakutana na Brewster. Mzee huyo alikuwa ametoka kubandika matangazo ya watu wengine waliopotea kwa usiku wa jana. Alimtazama Brian kisha akamuita kwa sauti yake kavu. Brian akahofia.
.
.
“Hujambo?” Brewster akasalimu akisogea karibu.
.
.
“Sijambo.”
.
.
“Mama yako anaendeleaje?”
.
.
“Vizuri.”
.
.
Brewster akanyamaza kwa muda kidogo akiwa anamtazama Brian. Akamsogelea karibu zaidi.
.
.
“Brian, usije tena ukaingia nyumbani kwangu pasipo ruhusa, sawa?”
.
.
Brian akameza mate pasipo kusema jambo.
.
.
“Tumeelewana?” Brewster akauliza tena akimkodolea macho Brian.
.
.
“Mimi sikuingia kwako,” Brian akajitetea. “Sijui ni nini unazungumzia.”
.
.
Brewster akatabasamu na kuuliza, “Brian, unadhani kuna kitu unaweza kufanya ukanificha?” kabla Brian hajajibu, Brewster akaongezea, “Natambua kila jambo, Brian. Mimi si mzee wa kawaida kama unavyowaza.”
.
.
“Najua!” Brian akasema akitikisa kichwa. “Najua wewe si mzee wa kawaida.” Brewster akatabasamu kusikia maneno hayo kisha akasema, “Ni vema umelitambua hilo. Kuwa makini basi.”
.
.
“Nishakuwa makini,” akajibu Brian kisha akaondoka zake. Hakujua amepatia wapi nguvu ya kumjibu Brewster namna ile. Moyo wake ulikuwa unapiga lakini akijikaza kisabuni.
.
.
.**
.
.
“Nimeshajua ule mhimili mwingine wa Helo!” akasema Brian, Wisconsin na Mama yake wakimtazama. Walikuwa wameketi sebuleni katika majira haya ya jioni ya saa kumi na moja.
.
.
“Brian!” Mama akamkatiza mwanaye. “Usiniambie ni Brewster!”
.
.
“Ndio! Ni yeye!” Brian akasisitiza.
.
.
“Sikia, Brian. Najua unamchukia Brewster, ila si kiasi hiko! Tafadhali.”
.
.
“Mama, si kwamba namchukia, hapana! Nimethibitisha kabisa. Brewster ndiye yule mhimili wa pili. Tazama … Helo, Hernandez Lorenzo, alikuwa ni mtu mwenye asili ya latini. Jina lake linaeleza vema juu ya hilo, hata pia kwa Padri Alfonso, jina lake ni ushahidi. Lina asili ya kilatini.”
.
.
“Sasa vipi kuhusu Brewster?” Mama akauliza. “Nalo lina asili ya Latini?”
.
.
“Hapana. Leo nilienda kufuatilia kule kazini kwa Brewster, ofisi ya mtaa, nikagundua kuwa jina lake la mwisho ni lenye asili ya Latini, nalo ni Lorenzo! Kwa ufupi Brewster huitwa Brelo. Mpaka hapo kutakuwa kuna shaka juu yake?”
.
.
Wisconsin aliyekuwa anakuna kidevu chake akaguna. “Ni bayana atakuwa anahusika. Ila watu hawa wawili watakuwa wana mahusiano gani na Hernandez?” akauliza.
“Ni lazima watakuwa wana mahusiano fulani, mlishawahi kuwaona wakiwa pamoja?” Wisconsin akauliza.
“Hapana!” Mama Brian akajibu kisha akamtazama Brian, naye Brian akaunga mkono hoja ya kuwa hawajawahi kuwaona watu hao pamoja. Wisconsin akabidua mdomo wake kwa kutafakari. “Pengine huwa wanakutana tusifahamu,”
“Labda,” Mama Brian akaunga mkono hoja. Wisconsin akawakumbusha tena ya kwamba wana siku tatu tu za kufanya maamuzi na kumaliza kazi kwahiyo basi wataanza kutumia usiku wa siku hiyo kuanza kukaribia lengo lao.
“Leo itabidi twende kanisani,” akasema Wisconsin kisha akamtazama Brian. Akarudia kusema, “Leo itabidi twende kanisani.”
“Kufanya nini?” Brian akauliza.
“Kufanya upekuzi,” Wisconsin akajibu. “Itabidi tuwatembelee watu hao kwa njia ya nyama na ya kiroho pia. Inabidi tujue mazingira yao kwanza kabla ya kukabiliana nao … kiuhalisia bado hatujajua upande upi ni wadhaifu zaidi.”
“Kwahiyo leo tutaenda kwa mtindo gani?” Akauliza Brian. Wisconsin akamjibu, “Kwa nyama … kwa miili yetu ya kawaida.” Brian akaridhia lakini ikiwa wazi kuwa ametwaliwa na hofu. Wisconsin akasimama na kwenda zake akimtaka, itakapofika majira ya saa tano usiku, wawe tayari kwa ajili ya safari.
Basi kama wasemavyo kuwa muda husonga zaidi ukiwa unangoja, nao ukawadia kwa upesi, Wisconsin akamtaarifu Brian, ambaye alikuwa yu tayari, waende zao. Walikuwa wamebebelea kurunzi na silaha baridi, mathalani chepeo dogo la kufytua na panga ambavyo walivitia kwenye begi. Lakini pia kwa kuficha nyuso zao, wakabebelea pia barakoa kisha wakaelekea eneo husika.
Wakiwa wamebebelea kila aina ya tahadhari, wakarusha macho yao wakiwa wamejibana kwenye ukuta wa kanisa. Kulikuwa kimya, mazingira yalikuwa tulivu kabisa. Ndani ya kanisa taa zilikuwa zinawaka pia vilevile kwenye makazi yanayopakana na kanisa, yaani ya watumishi, nayo yalikuwa kwenye mwanga. Mbali na hapo maeneo mengine yalikuwa kizani.
Ndani ya kanisa kulikuwa kuna watu wawili wakiwa wanafanya usafi, wote walikuwa ni wanawake waliovalia nguo nyeusi. Mbali na hapo hapakukuwa na mtu yeyote aliyekuwa anaonekana machoni.
“Sasa tunaendea wapi?” akauliza Brian. Wisconsin akapekua kwanza eneo kwa macho yake mepesi alafu akasema, “Tutaenda mule kutazama!” kidole chake alikionyeshea kwenye stoo ya kanisa.
Wakangoja punde, wafanya usafi wale wakamaliza kazi yao na kufunga milango ya kanisa kisha kujiendea zao. Sasa wakasonga langoni, wakakuta kumefungwa.
“Sasa?” Brian akauliza. Mara Wisconsin akatoa ‘plies’ yenye meno ya ncha kali, akamega kitasa wakazama ndani. Kulikuwa giza, taa zilizimwa. Na kwa usalama wao, hawakuziwasha, wakanyookea moja kwa moja kule stoo. Wakawasha kurunzi zao na kuangaza.
Wakiwa humo wanaendelea na upekuzi, kwenye moja ya nyumba ya watumishi wa kanisa, mwanaume mmoja akaona mwanga kwenye dirisha la juu la chumba cha stoo. Mwanaume huyu alikuwa mpana mwenye mustachi na nywele za kahawia. Alikuwa ni kasisi.
Alipata shaka kuona mwanga ule, akatazama majira yake na kuona si sawa. Aliporudisha tena macho kule stoo, akaona mwanga huo ukiwa wafifia na mara kukua, akagundua ni kurunzi. Hapa akapata shaka zaidi. Basi kutibu nafsi yake, akatoka ndani akatazame huko kunani.
Akabebelea gongo mkono wake wa kuume na kutembea upesi kuendea kanisa. Alipofika, akaona sababu ya yeye kuwa na shaka zaidi, kwani aliukuta mlango ukiwa umevunjwa. Akawasha taa na kuangaza. Hamna kitu.
Akaanza kujongea kuelekea stoo akitembea kwa staha. Alipofika napo akawasha taa, hamna kitu. Alitazama vema akaona vitu vikiwa vimeparanganyika kuashiria kuwa viliguswa. Akapata na maswali, yu wapi mvamizi huyo?
Mara akasikia sauti ya kishindo cha mtu nyuma yake, akatazama upesi. Huko napo hakuona kitu, lakini pale madhabahuni akaona joho la madhabahu likiwa linacheza, basi akahisi hapo pana mtu. Akasonga.
Alipofika akafungua upesi, akamwona Brian, lakini kabla hajafanya jambo, akastaajabu amekitwa kichwani, akadondoka kupoteza fahamu. Lakini kinyume na matarajio, akatiririka ngazini na kujikita kichwa. Hamaki akafa!
Wisconsin na Brian wakapata mshangao haswa, nini wafanye? Basi kwa kufikiria upesi, wakambeba kasisi yule na kumtoa nje waende kumtupia huko. Kwakuwa kulikuwa na giza, hawakuonekana, wakafika korongoni na kuumwagia huo mwili.
Ila kabla hawajaenda, Wisconsin akaona jambo. “Ngoja!” akamwambia Brian akimshika bega. Akamulika kule korongoni kisha akasema, “Twende kule!”
“Kufanya nini huko?” Brian akauliza. Wisconsin hakujibu, badala yake akaongoza safari kwenda huko. Brian akaongozana naye na ajabu baada ya muda kidogo wakajikuta ndani ya korongo kubwa ambalo hawakuwazia kuwapo. Korongo hilo lilikuwa linaelekea msituni zaidi na zaidi.
Wakalifuata na kutazama wakitumia kurunzi yao. Walipotembea kwa takribani dakika sita, wakaona mwili wa mwanamke mmoja ukiwa umetupiwa huko. Wakautazama, hawakuwa wanautambua. Wisconsin akaupiga picha mwili huo kwa kutumia kamera yake ya kizee, kisha wakaendelea kutazama kwa kusonga mbele.
Lakini Brian hakuwa ameridhia kabisa juu ya hili. Hakuwa anataka waende mbele zaidi maana alikuwa amejawa na hofu kubwa. Kia hatua waliyokuwa wanapiga kusonga mbele ilimfanya aogope zaidi na zaidi.
“Wisconsin!” Brian akaita na kusema, “Turudi nyumbani.”
“Brian, umeanza woga saa hii?” Wisconsin akastaajabu. “Kama waogopa bonde hili, tutapanda hayo ya mbele?” Basi Brian akapiga moyo konde, wakaendelea kusonga. Lakini sasa kila walipokuwa wanazidi kwenda mbele wakawa wanaona maiti zaidi na zaidi! Wisconsin alizipiga picha, mwishowe akachoka.
Walistaajabu wingi wa maiti zile, haswa juu ya nani ambaye amewaua wote hao? Na kwasababu gani? Wakaendelea kusonga zaidi na zaidi wakizama msituni, ila punde Brian akamshika Wisconsin mkono na kumwambia, “Ebu mulika kule!” ulikuwa ni upande wao wa kushoto umbali wa hatua kama kumi na tano za mtu mzima.
Wisconsin akamulika. Hakukuwa na kitu.
“Vipi, Brian?”
“Niliona mtu kule … mtu amesimama!”
“Una uhakika?” Wisconsin akauliza akirejesha kurunzi yake eneo aliloambiwa na Brian.
“Ndio, nina uhakika! Nimeona mtu kule.”
“Pengine macho yako, tumalizie kisha tuondoke zetu upesi!” Wisconsin akashauri. Ila kabla hawajasonga tena, Brian akamwona mtu upande wao wa kulia. Alikuwa ni mwanaume mrefu mweusi. Hakuwa anaonekana vema. Brian akamshtua Wisconsin na kumwambia amemwona mtu kule.
Wisconsin alipomulikia kurunzi, ajabu kurunzi ikazima! Akaipigapiga kiganjani, haikuwaka! Na sasa hapo ndipo yeye aliposhuhudia kuwa kweli kule alipoambiwa atazame, kuna mtu! Akahangaika sana na kurunzi, hatimaye ikawaka.
Akamulikia huko, ajabu hawakumwona mtu!
“Tuondoke!” Wisconsin akasema akitangulia. Wakaanza kukimbia upesi kutoka eneo hilo. Ila kabla hawajafika mbali, kurunzi ikazima kabisa! Wakawa hawaoni pa kukanyaga. Ubaya hata mbalamwezi nayo haikuwapo kuwaangazia.
Wakawa wanaenda kipofu wakikanyaga miili ya watu. Wakidondoka na kuanguka. Wakipepesuka na kukazana. Wakiwa wamejawa na hofu kuu vifuani mwao.
Punde nyuma yao wakaanza kuhisi kuna mtu yuaja. Walisikia kishindo kikali kikitembea kwa kasi. Na ndani ya muda mfupi, Brian aliyekuwa nyuma, akadakwa bega lake na kuvutwa kwanguvu. Akapiga kelele kali akidondoka chini!
“Brian!” Wisconsin akaita. Hakuwa anaona kinachoendelea ila akisikia sauti ya mtu akiburuzwa na kugugumia kwa kufungwa mdomo. Akarudi kiupofu akikodoa macho yake akitamani kumwokoa Brian.
“Brian!” Wisconsin akaita kwa hofu. “Upo wapi?” sauti ya Brian akigugumia ikaendelea kufifia ikipotelea. Ghafla mwanga mkali mweupe ukamulika na kumfanya Wisconsin afiche macho yake kwa maumivu. Mara akasikia amri, “Mikono juu! Tulia vivyo hivyo!”
Akiwa amefichama macho yake dhidi ya mwanga mkali, akayatupa nyuma yake kumtafuta Brian. Bahati akamwona kijana huyo akiwa chini, naye amejikinga na mwanga mkali uliokuwa unawamulika.
.
Wakasikia mtu yule anayewamulika akiwajongea. Walikuwa wamesimama tuli, mtu huyo aliposonga karibu zaidi yao ndipo wakagundua alikuwa ni polisi, akiongozana na Dada mmoja mnene ndani ya sare yake.
.
.
Polisi akawaamrisha waondoe barakoa zao upesi na wanyooshe mikono yao juu, lakini swala hili likawa gumu. Wisconsin hakuwa radhi kutii agizo hilo, hata Brian naye alisita kulitenda. Walizihitaji barakoa zile kwenye nyuso zao. Polisi akarejea amri yake kwa nguvu, “Ondoa barakoa hizo!” akiwa amewaonyeshea mdomo wa bunduki.
.
.
Polisi huyu alikuwa mnene kwa umbo, mfupi. Amevalia kofia, uso wake umekatwa na mustachi mwembamba.
.
.
Mara Wisconsin akaigiza kubanwa na kikohozi. Akakohoa kwanguvu akiwa amedaka kifua chake kwa maumivu. Polisi akazubaa. Haraka Wisconsin akainyaka bunduki ya polisi kwa mkono wake wa kuume, mrefu wenye nguvu, akaivuta na kumkandika nayo Polisi kwenye paji lake la uso, Polisi akadondoka chini kama kifusi!
.
.
Wisconsin akafoka, “Kimbia, Brian!” kisha wakaanza kukimbia upesi ndani ya msitu. Wisconsin aliitupa bunduki ya polisi wakiwa huko njiani, wakatokomea.
.
.
“Upo sawa?” Dada akamuuliza Polisi aliyekuwa anaugulia kwa maumivu huku akimsaidia kunyanyuka.
.
.
“Niko sawa, wapi wameelekea?” Akauliza Polisi akiangazaangaza. Paji lake la uso lilikuwa jekundu. Dada akamwonyeshea upande, na mara mwanaume huyo akaanza kukimbia kwenda huko. Mwili wake ulikuwa mzito sana, alipokimbia kwa hatua kadhaa akajihisi kuchoka!
.
.
Alisimama akahema kama mbwa. Alimradi alipata silaha yake, basi akaona hamna haja ya kukimbizana na wahalifu. Kwa msaada zaidi akawataarifu wenziwe kwa kutumia ngowe ya mawasiliano kisha akarejea kumkuta Dada.
.
.
“Twende!” akamwambia akiongoza njia.
.
.
“Umewaacha wauaji waende?” Dada akastaajabu.
.
.
“Sitaweza kuwapata humo msituni,” akasema Polisi alafu akageuka na kumtazama Dada. Bado alikuwa anahema kana kwamba mbweha. Akamwambia, “Usijali, tutawapata tu. Nimeshawatarifu wenzangu. Bils shaka ndani ya muda mfupi watakuwa wameuzingira msitu huu kwa ajili ya doria.”
.
.
Kabla Dada hajatia neno, Polisi akamuuliza, “Ulikuwa una taarifa yoyote juu ya miili ya watu hawa iliyotupwa huku?”
.
.
Dada akatikisa kichwa chake na kusema, “Hapana. Sikuwa najua chochote. Kama isingekuwa nimeona damu kule kanisani nikafuatilia, basi hata sasa nisingekuwa najua kama eneo hili lina maiti za watu.”
.
.
“Una uhakika?” Polisi akauliza akimkazia macho Dada. “Ndio, nina uhakika!” Dada akajitetea, naye akiwa ametoa macho.
.
.
“Unajua ni miili mingi,” Polisi akasema. “Inakuaje ukashindwa kutambua?”
.
.
Dada akajibu, “Sina taratibu ya kuja huku korongoni. Hamna mtu yuaja huku.” Polisi akaguna na kusema, “Mna kesi ya kujibu ninyi nyote. Lazima mtoe maelezo yenye kuleta maana.”
.
.
Baada ya kusema hayo, Polisi yule akasonga zake mbele kutoka humo korongoni, nyuma yake Dada akimfuata. Akapiga hatua tatu, mara kurunzi lake lenye mwanga wa fujo likazima!
.
.
“Pumbavu!” akalaani. Sasa kulikuwa giza kabisa hata kuonana ni ngumu! Alipigapiga kurunzi lakini haikuwaka abadani, akastaajabu ni nini shida. Betri zilikuwa nzima, nayo kurunzi ilikuwa mpya tu.
.
.
Akiwa anahangaika na kurunzi hiyo, mara Dada akapiga kelele ghafla akisema, “Kuna mtu!” Polisi akarusha macho yake kutazama kule alipoonyeshea Dada, hakuona kitu! Akauliza, “Ni nini shida yako?”
.
.
“Nilimwona mtu kule!” Dada akajibu.
.
.
“Na giza lote hili?” Polisi akauliza akikejeli, kisha akasema, “Ebu twende. Fanya upesi!” wakaendelea kutembea wakienda kwa makisio. Wakatembea kwa hatua tano tu, mtu yule ambaye Dada alimwona, mrefu mweusi, akajiri tena kandokando yake! Dada akapiga kelele kali.
.
.
Polisi alipogeuza shingo yake kutazama, akastaajabu amedakwa koo na kuchanwa. Akavuja damu lukuki akikoroma kuelekea kifoni. Mikono yake iliyomziba koo ikajawa na damu pomoni. Akiwa anatetemeka, akadondoka chini na kufa.
.
.
Dada akapiga kelele za woga. Naye punde akazabwa kibao kikali, akapaa na kudondokea mbali kama gunia la mkaa. Kabla hajajigeuza, miguu ya muuaji ikawa imemfikia kwa ajili ya kumaliza kazi.
.
.
**
.
.
“Mpo sawa?” Mama Brian akauliza. Wisconsin na Brian wakazama kwanza ndani na kujitupia kochini ndipo kumjibu. Punde huko nje gari la polisi likakatiza na king’ora chake.
.
.
Wisconsin na Brian walikuwa wamechoka mno. Wanahema kwanguvu. Walipata wasaa mchache wa kuvuta pumzi zao kisha ndiyo wakaendelea na maongezi.
.
.
“Tumefanikiwa … kwa kiasi chake,” Wisconsin akaeleza. Mara hodi ikagongwa mlangoni. Punde kidogo Mama Brian akaenda kufungua mlango.
.
.
“Habari yako?” alikuwa ni Polisi. Kwa idadi walikuwa wawili, mmoja yu karibu na mlango, mwingine yu kwa nyuma kidogo.
.
.
“Safi,” Mama Brian akajibu na kuuliza, “Kuna shida yoyote, afisa?”
.
.
“Haujasikia au kuwaona watu wowote wakikatiza muda huu?” Polisi akauliza huku mikono yake akiishikisha mkanda wake mpana wenye kifuko cha kuhifadhia bunduki ndogo.
.
.
“Watu? …” Mama Brian akatahamaki. “ Hapana! Sijawaona.
“Mbona upo macho mpaka muda huu?” Polisi akauliza. Mama Brian akatazama eneo lote la jirani, ni nyumba yake tu ndiyo ilikuwa mwangani. Akatabasamu kidogo na kusema, “Nilikuwa natazama maigizo kwenye runinga mpaka sasa.” Polisi akatupa macho yake ndani kuangaza. Hakukuwa na mtu isipokuwa viti vitupu tu.
Akauliza. “Unaishi na nani?”
“Wanangu wawili, wa kike na kiume,” Mama Brian akajibu.
.
.
Polisi akauliza, “Hao pekee?” Mama Brian akajibu, “Ndio, hao pekee.”
.
.
“Una uhakika?” Polisi akauliza akimkazia macho.
.
.
“Ndio, hao pekee!” Mama Brian akastaajabu akisema, “Najua watu nikaao nao.”
.
.
“Tunaweza pekua ndani?” Polisi akamuuliza, asingoje ruhusa akazama ndani akifuatiwa na mwenziwe, wakaanza kupekua ndani. Sebuleni wakaona viatu vya kiume pea mbili vikiwa vimejawa na matope.
.
.
“Vya nani hivi?” Polisi akauliza.
.
.
“Vya mwanangu!” Mama Brian akajibu. Moyo wake ulikuwa umeanza kukita upesi. Alijawa na woga. Polisi alivichukua viatu hivyo na kuvinusa, akaviona vina joto kumaanisha vimetoka kuvaliwa muda si mrefu. Hakusema jambo, wakaendelea kupekua mule ndani sehemu moja baada ya nyingine wakianza na jikoni.
.
.
Walipoelekea vyumbani, Mama Brian akapata shaka zaidi. Alifichama kinywa chake kwa mkono akiwa ametoa macho. Alijua ameshakwisha. Nini atafanya Brian na Wisconsin wakitiwa nguvuni?
.
.
Chumba cha kwanza, Polisi wakamkuta Olivia akiwa kitandani amelala. Wakatazama uvunguni na kufungua makabati kuangaza, hawakuona kitu. Basi wakatoka na kuendea chumba cha pili. Huko wakamkuta Brian akiwa amejifunika shuka, amelala. Tena akikoroma na kuacha mdomo wake wazi kana kwamba mtu aliyelowea usingizini.
.
.
Polisi wakatazamana alafu mmoja wao, yule kimbelembele, akafunua shuka la Brian kumkagua miguu. Brian alikuwa amevalia suruali ileile aliyotoka nayo msituni, ilikuwa imejawa na matope. Polisi wakapata shaka juu yake. Lakini kabla hajamwamsha, polisi mmoja, yule akaae nyuma, akasema, “Tazama!”
.
.
Mwenzake akageuka upesi kutazama. Ilikuwa ni dirishani. Wakasonga na kutazama vema, huko wakaona watoto wawili wa kike wakiwa wanatembea kana kwamba watu waliovunjikwa na viungo. Wamefumba macho wakitembea kwa upofu.
.
.
“Wapo na nani?”
.
.
“Wenyewe!”
.
.
“Wanaenda wapi?”
.
.
“Sijui!”
.
.
Walitazama nyuma na mbele yao, hakukuwa na mtu akiongozana na watoto hao. Basi wakaona vema, mmoja atoke kwenda kutazama na mwingine abaki mule chumbani. Basi yule Polisi aliyembele ya mwenziwe, akatoka.
.
.
Alipofika huko nje, akawaita watoto hao wawili waliokuwa wanatembea, lakini hawakumsikia. Walikuwa ni wa kike, mapacha, wamevalia nguo za kulalia.
.
.
Polisi akawajongea na kuwatazama vema. Akajitahidi kuwaamsha asifanikiwe. Mwenzake alikuwa dirishani akimtazama kana kwamba runinga.
.
.
“Mnaenda wapi? … Hey! Hey!” akawapigapiga mashavu. Akawatikisatikisa kichwa lakini bado.
.
.
Muda kidogo, yule polisi aliyekuwa amekaa dirishani akimtazama mwenzake, akamwona mtu fulani akiwa anakuja kumjongea mwenziwe na wale watoto. Alimtazama mtu huyo lakini hakuweza kumtambua. Mtu huyo alikuwa akiambatana na mtoto mwingine kwa pembeni yake.
.
.
Akajaribu kumshtua mwenzake, “Tazama nyuma yako! Hey! Tazama!”
.
Mwenzake huyo alipotazama, kabla hajajitetea na bunduki yake, akanyakwa koo na kunyanyulia juu haswa kisha akaminywa kwanguvu mpaka koo lake kuanza kuchuruza damu. Bunduki ambayo huenda ingemsaidia kutetea uhai wake, ikadondokea chini.
.
.
“Hapana! Hapana!” mwenzake akatahamaki pale dirishani. Upesi akatoka kwenda kumsaidia mwenzake abaki na pumzi. Alipofungua mlango, akamnyooshea mtu yule bunduki na kumfyatulia tatu. Ajabu hazikusaidia. Zaidi yule mtu wa ajabu akamtupia mwenzake chini na kumfuata yeye kwa kasi!
.
.
Naye akamyaka shingo na kumnyanyua juu, akamminya koo na kumpasua, kisha akalichanja na kumfanya avuje damu kama sharubati toka kwenye kopo. Polisi huyo akapoteza uhai. Dubwana hilo likamtupa na kisha likapotea zake!
.
.
Baadhi ya watu wakafungua milango na madirisha kutazama. Milio ya risasi iliwaamsha na kuwapa mashaka. Wakaona maiti mbili za polisi na wale watoto wakiwa wanatembea. Kwakuwa hali ilikuwa shwari, wakatoka kwenda kutazama.
.
.
Waliwaokoa wale watoto na pia wakatoa taarifa polisi wakidhani polisi wameuawa na majambazi baada ya kurushiana risasi.
.
.
Muda mfupi, polisi wengine wakaja na kuanza kuipemua miili na kukusanya taarifa toka kwa washuhudiaji. Hawakuelewa jambo. Hakuna aliyesema amewaona hao watu waliokuwa wanapambana na polisi, lakini pia vilevile hakuna aliyetoa maelezo ya kueleweka juu ya watoto wale mapacha waliokuwa wanatembea wenyewe usiku huo.
.
.
Wakiwa kwenye mahangaiko ya kutafuta taarifa sahihi, Mama Brian akatoka akiwa amejikunyata, amejifunika blanketi, akawaambia polisi, “Mimi najua nani waliyekuwa wanapambana naye.” kwa maelezo zaidi, polisi mmoja akaongozana na Mama Brian kwenda ndani kumhoji.
.
.
“ … Mtu huyo ndiye ambaye hupoteza watoto kila siku. Polisi hao walipotaka kuwaokoa watoto hao, ndipo akajiri na kuwamaliza,” Mama Brian akaeleza. Polisi akamuuliza, “Unamjua yupoje na wapi anaishi?”
.
.
Mama Brian akanyamaza kwanza kisha akauliza, “Hata nikisema mtasadiki?”
.
.
“Usijali,” Polisi akamtoa hofu. “Unaweza tu kueleza.” basi Mama Brian akamweleza kinagaubaga ya kuwa mtu huyo ni Helo, Hernandez Lorenzo, wa miaka mingi iliyopita. Nyumba yake ipo msituni na anafanya kila anachofanya kwa ajili ya kulipiza kisasi kwa mji wa Boston.
.
.
Polisi akanakili maelezo yake yote, ila yakamletea shaka kwenye kuamini. Simulizi ile ilikuwa ni ya kufikirika zaidi kuliko uhalisia. Ni kwa namna gani mtu mfu akarejea na kufanya mauaji?
.
.
“Nashukuru sana.” Polisi akampatia mkono na kunyanyuka, “Naweza kwenda sasa. Au kuna cha ziada wataka kuniambia?”
.
.
Mama Brian akamjibu, “Ndio, kipo!”
.
.
“Niambie.” Polisi akasema akimpatia masikio yake kwa utulivu. Mama Brian akasema, “nendeni mkatazame kwenye korongo la kanisa …”
.
.
.
**
.
.
.
Gari la polisi lilisimama, wakashuka wanaume wawili waliovalia sare. Mmoja wao alikuwa ni yule Polisi aliyemhoji Mama Brian. Mkononi alikuwa amebebelea ngowe ya mawasiliano na bunduki ndogo. Mwenzake anayemfuatia alikuwa mikono mitupu ila viganja vyake vikiwa karibu na mkanda wake uliobebelea silaha.
.
.
Ndani ya muda mfupi, wakaonana na Padri Alfonso na Dada Magdalena, wakawafanyia mahojiano mafupi kabla ya kuwataka waongozane kwenda korongoni. Padri Alfonso akapata shaka, akauliza, “Afisa, kuna lolote lile?”
.
.
“Tunataka kupatazama!” Polisi akasema kwa amri basi Padri Alfonso na Dada Magdalena wakaongozana nao kwenda huko kwenye korongo. Walipofika, polisi hao wakangaza na kuangaza, hawakuona kitu.
.
.
“Mnaweza kutuambia mnatafuta nini ili tuwasaidie?” akauliza Padri Alfonso. Polisi akamwambia, “Usijali.” kisha wakajikokota zao kwenda kwenye usafiri wao na kutimka.
.
.
“Hamna kitu!” akasema Polisi dereva na kuongezea, “Nilijua tu mama yule atakuwa na matatizo.” wakayoyoma wakati Padri Alfonso na Dada Magdalena wakiwatazama. Walipoishilia, Padri Alfonso akauliza, “Watakuwa wameambiwa na nani kuhusu korongo lile?”
.
.
Dada Magdalena akajibu, “Si wengine bali wale waliokuja kulitembelea.” Basi Padri Alfonso akashusha pumzi ndefu na kusema, “Nadhani umefikia mwisho wao!” na mara katikati yao akasonga mtumishi mwingine. Naye alikuwa ni Dada kama yule Magdalena, akasimama kandokando yao na kuuliza, “Nami nafanyaje?”
.
.
Padri Alfonso akamtazama na kuweka mkono wake begani. Kumbe alikuwa Dada yule aliyekumbwa na kadhia na yule polisi wa mwanzoni wakiwa korongoni kuwafuata wakina Brian.
.
.
“Dada Marietta, wewe bado u mpya kabisa,” akasema Padri Alfonso. “Utafanya kazi pamoja na Dada Magdalena akuonyeshe namna ya kuenenda. Ila bila shaka usiku wa leo umekuwa mrefu sana, tuuache uende.”
.
.
Dada hao wakainamisha vichwa vyao, Padri akaenda zake.
.
.
**
.
.
Saa nane ya mchana …
.
.
Akiwa juu ya baiskeli yake, Brian alirusha macho yake huku na kule kuangazia kama kuna tangazo jipya la watoto waliopotea. Hakukuwapo, yote yalikuwa ya zamani. Mpaka anafika nyumbani hakuona tangazo lolote tofauti na yale aliyoyaona hapo kabla.
.
.
Akazama ndani na kuteta machache na Wisconsin juu ya mpango wao. Bwana huyo akamwambia kuwa siku hiyo wataenda kumtembelea Brewster majira ya usiku. Brian akauliza, “Haitakuwa hatari kutokana na yale yaliyotokea jana yake?”
.
.
Wisconsin akakuna kidevu chake na kumwambia Brian, “Hatuna muda, ni lazima tufanye hivyo. Kama tusipoyatembelea maeneo haya tukiwa na mwili wa nyama, basi itakuwia vigumu utakapoenda huko kiroho. Lazima ujue ni maeneo yapi utakayokatiza na kuyafanyia kazi.”
.
.
Basi japo kishingo upande, Brian akaridhia. Akala na kupumzika kidogo. Baadae kwenye majira ya jioni akajikwea kwenye baiskeli yake na kwenda kule kwenye makazi ya marehemu Dkt Hamill. Alipoingia, akaegesha baiskeli yake pembeni kidogo ya geti kisha akaanza kusonga kuendea jengo hilo.
.
.
Akiwa bado hajalifikia, akastaajabu kusikia sauti ya geti likifungwa. Akapata shaka. Haraka akakimbilia getini na kujaribu kulifungua. Halikufunguka. Akajaribu kwanguvu zote lakini bure, hakuweza kufungua. Akajiuliza nani kamfungia humo?
.
.
Akapigapiga geti kwanguvu akiita watu wamsaidie lakini hakuna mtu aliyemsikia wala kujali. Mpaka mikono ikawa inamuuma asifanikiwe kitu. Mara akasikia sauti nyuma yake ikimwambia, “Acha kujichosha, Brian.”
.
.
Haraka akatazama nani huyo amwongeleshaye, hamaki akamwona Brewster! Alikuwa amesimama mbele ya mlango wa jengo akiwa ameshikilia bakora ya kutembelea. Yu ndani ya suti nyeusi na kofia yake.
.
.
“ … tupo wawili tu humu, acha kusumbuka.” akamalizia na kisha akatabasamu. Brian akamuuliza, “Ni nini unataka kwangu?”
.
.
“Unajua nitakacho,” Brewster akamjibu kisha taratibu akaanza kusonga kumjongea. “Nilijitahidi sana kukuepusha na kifo, lakini …” akabinua mdomo wake. “ … hukutaka kusikia, Brian. Umekuwa mkaidi sana. Sasa mimi nifanye nini?”
.
.
Brian akamnyooshea mkono na kumwamuru, “Usinisogelee!” Brewster akaangua kicheko kisha akauliza, “Nikikusogelea, utanifanya nini, Brian?” Kabla Brian hajajibu, Brewster akiwa anatembea taratibu, akasema, “Leo ni mwisho wako. Hamna mtu wa kukusaidia, ni mimi na wewe tu … mimi na wewe, Brian.”
.
.
Brian akapiga kelele kuomba msaada. Brewster akacheka sana mpaka kushika mbavu zake. Akakohoa mara kadhaa na kusema, “Brian, acha kupoteza nguvu zako bure. Ni-me-ku-a-mbi-a …” wakati Brewster anaongea akawa anabadilika toka kwenye ubinadamu kwenda kwenye ushetani. “… u-po-na-mi-mi-tu! Ni we-we-na-mi-mi-tu!”
.
.
Uso wake ukageuka na kuwa wa mnyama. Mikono yake ikavimba na kuchomoza makucha vidoleni. Ulimi ukamtoka nje na meno yakapandana kwana kwamba tengo la miba! Miguuni akavalia kwato za ng’ombe.
.
.
Brian akaogopa sana. Akakimbia kuufuata ukuta na alipoenda mbali akajitahidi kuurukia ukuta atorokee kwa nje, lakini ukuta ulikuwa mrefu sana. Hata aliponyoosha mikono yake, hakufua dafu. Akajaribu na tena na tena. Mara mkono wake wa kuume ukafanikiwa kushika kingo ya ukuta. Akijitahidi kuunyoosha mkono wa pili, ule wa kushoto, udake ajivute, akashikwa na kuvutwa chini! Akadondoka na kulalama kwa maumivu.
.
.
Brewster akamdaka shingo na kumminya kwanguvu. Brian akaanza kutapatapa.
.
“Nakumaliza, Brian!” akasema Brewster ambaye hakuwa binadamu tena bali mnyama. Brian akaendelea kutafuta pumzi yake na kupigania uhai wake pasipo mafanikio. Ni bahati wakati anatafuta la kufanya, akamkita Brewster kwenye sehemu zake za siri na kumsababishia maumivu makali!
.
.
Akamwacha Brian na kukimbizia mikono yake yote sehemu zake za siri, ndipo Brian akachoropoka na kukimbia haswa. Alikuwa anahema kana kwamba mbwa. Na baada ya muda mfupi akawa haonekani wapi amekimbilia.
.
.
Basi Brewster akiwa anagugumia sana kwa maumivu, akasimama, bado uso wake ukionyesha anahisi maumivu, akatazama huku na kule kumtafuta Brian. Macho yake yalikuwa mekundu yaliyojawa na hasira.
“Nitakuua, Brian!” akasema akiwa anakunja ngumi yake kwanguvu. Meno anayasaga.
.
.
Akanguruma kana kwamba simba kisha akaanza kumsaka Brian ndani ya eneo hilo akitumia pua yake kama nyenzo kuu. Akanusanusa na kusonga. Akanusa na kusonga. Akatazama kushoto na kulia. Akasonga.
.
.
Mwishowe akafika nyuma ya nyumba ambapo aliamini Brian atakuwa huko. Akaangaza macho, kheri akaona mlango ukiwa wazi. Akaamini alikuwa sahihi. Akasonga na kuzama ndani, bado akitumia pua yake kama dira.
.
.
Alipoendelea kunusa zaidi, akajikuta mbele ya kabati kubwa. Hapo akaguna kwa kebehi na kusema, “Unaweza kukimbia, Brian, ila si kujificha.”
.
.
Mara akaanza kufungua milango ya makabati kwa pupa na kutupia humo macho yake kutazama. Mlango wa kwanza, hakubahatika kuona kitu, wa pili nao wa tatu, hakukuwa na kitu zaidi ya nguo tu! Sasa mlango uliobakia, ule wa nne, akajua Brian yupo humo.
.
.
Basi akavuta pumzi kwanza, alafu puh! Akaufungua. Loh! Namo hakukuwa na kitu. Hajakaa vema, kabati likaanza kuinama. Akadhani pengine ni macho yake, kumbe lah! Kabati lilikuwa linadondoka.
.
.
Likamparamia na kumwangusha chini kama mbuyu. Brian akatoka kwa nyuma yake na kukimbia upesi kwenda ndani. Muda mfupi, hauonekana tena wapi alipoelekea.
.
.
Brewster aliyeachwa akiwa amevamiwa na kabati, akalalama sana kwa maumivu. Kana kwamba kabati lile ni bua, akalinyanyua na kulitupia kando kwa nguvu! Kabati likaparanganyika na kuwa vipisi vya mbao.
.
.
Uso wake ulikuwa unatoa damu na alikuwa pia amekasirika maradufu. Akapiga kelele kali na kunyanyuka kisha kwa pupa akaanza kumsaka Brian! Akanusa na kufuata harufu mpaka kufika chumba kimoja ambacho kilikuwa kimefungwa. Akabamiza mlango kwanguvu, ukavunjika kutengeneza tobo!
.
.
Akaubamiza tena na tena, mlango ukawa inyang’anyang’a, akazama ndani na kuangaza. Hakukuwa na mtu, chumba kilikuwa kitupu kabisa. Hakuamini macho yake, mbona amesikia harufu humo? Alipotazama vema, akagundua ya kuwa Brian alikuwa ametupia nguo yake humo.
.
.
Akaifuata na kuinyanyua kuipeleka puani. Akainusa. Ama kweli, alikuwa amedanganywa! Akasaga meno yake kwa hasira kisha akatoka humo chumbani.
.
.
.
**
.
.
“Tafadhali, kubali! Tafadhali! Tafadhali!” Brian alilalama akiwa anaibonda simu ya mezani kiganjani mwake. Alikuwa anataka kuwasiliana na polisi ama familia yake lakini simu hiyo ilimsumbua. Kila alipotia namba, ikakata. Kila alipotia namba …
.
.
“Shabash!” akalaani. Akiwa yu kifua wazi, mjawa na hofu, akawaza nini cha kufanya. Hakuwa anajua sasa. Endapo Brewster angelitokea hapo basi angemmaliza mara moja.
.
.
Akatazama kushoto na kulia. Makabati hayakuwa sehemu salama ya yeye kujificha. Na hata kitanda kilichokuwamo humo ndani hakikuwa na uvungu.
.
.
Akiwa anawaza vivyo, mara akaona simu ile ya mezani ikiwa inawaka taa. Taa ndogo nyekundu ambayo ilikuwa imepachikwa kwenye kitako chake. Basi haraka Brian akapata moyo. Upesi akaikwapua simu hiyo na kuibandika sikioni, akapiga polisi.
.
.
Simu ikaita mara mbili, mara ikapokelewa na sauti ya kike.
.
.
“Unaongea na idara ya Polisi, Boston. Una dharura yoyote?”
.
.
Kabla Brian hajafungua mdomo, mlango ukabamizwa kwanguvu na kupasuka! Kutazama akamwona Brewster, macho kwa macho. Akiwa amejawa woga, akapayuka simuni kuwa anahitaji msaada kuna mtu anataka kumuua.
.
.
“Upo wapi? Tupe anwani yako tafadhali!” sauti ile ya kike ikanguruma. Brian kufungua mdomo wake, Brewster akawa tayari ameshamfikia. Akamnyonga shingo yake kwanguvu!
.
.
Bado Brian alikuwa ameshikilia simu mkononi. Brewster alikuwa anamtazama kwa hasira na hamu ya kumfundisha adabu. Kutetea uhai wake, Brian akambamiza Brewster usoni kwa kutumia simu ile ya mkononi.
.
.
Simu ikavunjika na kumwacha Brewster bado yupo ‘gado’. Kwa upesi, Brian akanyanyua tena kitako cha simu na kumkandika nacho Brewster usoni, karibu kabisa na jicho lake la kushoto, hapo Brewster akahisi maumivu. Jicho lake lilijeruhiwa pia.
.
.
Brian akamng’ata mkono kwanguvu, kwa hasira Brewster akamtupia ukutani yeye akiugumia maumivu. Brian akakajibamiza na kulala akihisi maumivu makali kichwani. Alipomtazama Brewster akamwona akiwa anajirepea kukaa sawa. Akafikiria upesi na kuona ni hekima kuruka kupitia dirishani kuliko kukaa humo angoje kuuawa.
.
.
Akajivuta upesi, akipumbaza maumivu aliyokuwa nayo, akasongea dirisha na kujitupia huko nje pasipo kujali kuna urefu wa aina gani. Akafikia bustanini na kujeruhi mguu wake wa kushoto kwa kujichanja na ua kubwa komavu. Mguu ukawa unavuja damu. Tumbo nalo na kifua vyamuuma mno. Alikuwa ameruka toka ghorofa ya pili!
.
.
Akatema damu na kutazama kule juu alipotoka, dirishani akamwona yule dubwana akiwa anamtazama. Basi akajikokota kusimama, kisha akanza kujongea kwenda getini. Mwendo wake wa chechema sababu ya majeraha.
.
.
Brewster akabinua mdomowe. Na hamaki, kufumba na kufumbua, naye akajitupa kurukia kule chini! Akafikia kwato zake na kusimama imara kabisa. Taratibu akaanza kumfuata Brian akiwa anajua ashakuwa njiwa wake. Hana haja ya kumfukuza.
.
.
“Huu ni mwisho wako, Brian. Haijalishi ni namna gani unauchelewesha.”
.
.
Brian akakunja shingo kumtazama. Uso wake nao ulikuwa unavuja damu toka upande wa kulia wa paji lake la uso. Macho yake yalikuwa mekundu … mekundu yakionyesha maumivu mazito anayopitia.
.
.
“Simama, Brian. Naapa hutosikia maumivu hata kidogo. Nitakumaliza pasipo maumivu yoyote yale,” akasema Brewster huku akisugua kwato zake ardhini. Brian hakujali, akaendelea kusonga kwa mwendo wake wa kinyonga. Punde, Brewster akakimbia na kusimama mbele yake. Alikimbia kwa kasi sana, si ya binadamu. Kiganja chake kipana kikadaka shingo ya Brian na kumnyanyua juu! Akamuuliza, “Utajitetea na nini hivi sasa?”
.
.
Brian akiwa ametulia kana kwamba mtu anayengoja kifo kimtwae, akachuruza damu mdomoni. Tone lake likamdondokea Brewster jichoni na kumfanya kiumbe huyo afumbe macho. Akapepesapepesa na kuyafungua tena.
.
.
Ajabu alipotazama, akaona mkono wa Brian ukiwa unaishilia kooni mwake. Hakutambua nini kilichotokea, ila ghafla akahisi maumivu makali mno na damu zamtiririka! Kumbe Brian aliuwa ana kipande ha chupa mkononi mwake. Kipande alichokiokota wakati ananyanyuka toka pale chini alipoangukia.
.
.
Alimkita nacho Brewster mara tatu shingoni pasipo kukoma, Brewster akayakodoa macho haswa! Brian asiwe hata na lepe la huruma, akaendelea kumtoboatoa shingoni kana kwamba anataka kutengeneza nyavu. Damu zikamruka kwa hasira!
.
.
Upesi Brewster akamwachia na kisha akadaka shingo yake iliyokuwa inavuja damu pomoni. Akalia kwa uchungu wa maumivu. Akamtazama Brian kwa hasira, akajaribu kumdaka ila mkono wake ukalegea kwa kukosa nguvu. Akadondoka chini akiendea pumzi yake ya mwisho.
.
.
Brian akabaki akimtazama kandokando yake. Pale Brewster alipokata pumzi, akamtupia kipande kile cha kioo alichomuulia nacho, yeye akaenda zake taratibu akifuata geti. Taratibu kwa mwendo wa kinyonga. Kabla hajafikia geti, akatazama nyuma. Haki alikuwa amemuua dubwana.
.
.
Simulizi ya daudi na Goliathi.
.
.
“Mungu wangu, Brian!” Mama akatahamaki baada ya kumwona mwanae. Ndiyo kwanza Brian alikuwa amewasili eneo la nyumbani. Alikuwa anakokota baiskeli yake ambayo punde aliiangushia kando na msingi wa nyumba.
.
.
Mama yake akamsogelea upesi kumtazama.
.
.
“Nini kimekutokea?” Mama akauliza akiwa anamkagua kwa macho. Punde mlango ukafunguliwa, Wisconsin akatoka ndani. Naye akarusha macho yake kumtazama Brian kisha haraka akasonga eneo la tukio.
.
.
“Alikuwa ni Brewster,” Brian akasema na kusita. “… Nimemuua!”
.
.
Mama akaziba mdomo wake kwa kiganja chake cha kulia. Akauliza, “Umemuulia wapi? Watu wamekuona?” Brian akatikisa kichwa na kujibu, “Hamna aliyeniona. Tulikuwa peke yetu.”
Mama akamtazama mguuni, akamwona akiwa amelowanisha suruali na kiatu chake kwa damu.
.
.
“Twende ndani, hapa si salama,” akashauri Wisconsin. Mama akaona ni stara, hata hivyo Brian alikuwa anahitaji huduma ya kwanza. Upesi wakazama ndani na Mama akamshughulikia Brian kwa dakika kadhaa kabla ya kukaa na kuendelea na maongezi yao.
.
.
“ … alibadilika na kuwa mnyama,” Brian akasema kwa sauti yake ya pole. “Alitaka kuniua. Aliahidi kufanya hivyo. Kila alipodaka shingo yangu nilimwona akiwa na dhamira hiyo. Kunimaliza.”
.
.
Akaweka kituo kirefu akitazama mkono wake wa kuume ambao ulifungwa ‘bandage’. Kwa muda kidogo akamezwa na kumbukumbu juu ya namna mkono huo ndio ulivyomkita Brewster kwa chupa mpaka kumuua. Akasema, “sikumbuki ni roho ya namna gani ilinivaa. Nahisi nami nilikuwa mnyama kama yeye. Sikujiuliza mara mbili, hata sasa nashangaa.
.
.
Kitu pekee nilichokuwa nataka kukiona ni yeye akidondoka na kuwa mfu. Nikamtifua shingo yake …” Brian akaeleza akiwa mbali kifikra. Ni kama vile alikuwa anshuhudia anachokisema. “… nilimtifua kana kwamba plau inavyotafuna ardhi hata akalegea na kudondoka chini … akawa mfu.”
.
.
Wisconsin akamwekea mkono begani na kumminya kidogo, akasema, “Wewe ni shujaa, Brian.” macho yake yalikuwa yanamaanisha anachokisema. “Kecie hakukosea kukuchagua wewe. Aliona kipi kipo ndani yako.”
.
.
Mama Brian akamkumbatia mwanae kwa mara nyingine kisha akambusu mara mbili kwenye paji la uso. “Najivunia kuwa nawe, Brian.” akamtazama mwanaye kwa macho yanayolenga machozi. Wisconsin naye akamfariji na kisha kumwambia, “Inabidi niende huko kwenye hiyo nyumba.”
.
.
“Kufanya nini?” Mama Brian akatahamaki. Akajigeuza vema amtazame Wisconsin.
.
.
“Inabidi niende, kuna kitu nataka kutazama,” akasema Wisconsin kisha akasimama asiseme kitu gani champeleka huko. Akafungua mlango na kujiendea zake akimwacha Mama Brian kwenye bumbuwazi. Mwanamke huyo aliona kwenda huko ni kujitakia maswaibu kama yale ya Brian. Aliogopa.
.
.
Basi sasa tangu Wisconsin alipoyoyoma, akawa anahesabu masaa na dakika. Akawa anatazama saa yake mara kwa mara na hata njia kuangaza kama bwana huyo anarejea. Mpaka kufikia majira ya saa mbili usiku, hakuonekana. Mama Brian akapata shaka sana, hata Brian alitia doa imani yake.
.
.
“Atakuwa salama kweli?” Mama akamuuliza Brian. Alishika tama macho yake yakiwa yamejawa na ndita za woga. Brian akamjibu, “Anajua kujitazama. Haina haja ya kuhofia sana.”
.
.
Punde kidogo mlango ukagongwa, Mama akadamka upesi kwenda kutazama. Hakuwa Wisconsin, bali jirani tu.
.
.
“Habari?”
.
.
“Salama.”
.
.
“Samahani kwa usumbufu, vipi runinga yako yafanya kazi vema?” akauliza jirani. Mwanamama mwenye nywele nyeupe na mashavu mekundu. Kwenye nyonga yake alikuwa amembebelea mtoto mdogo wa kike makadirio ya miaka miwili.
.
.
“Sijajua, acha nitazame,” akasema Mama Brian alafu akaendea runinga yake na kuiwasha. Ilikuwa ajabu runinga hii haikuwa imewashwa mpaka sasa, pengine ni kwasababu hakukuwa na mtu mwenye mpango nayo. Kila mmoja alikuwa anamuwazia Wisconsin. Labda Olivia angelikuwa sebuleni, angeliwasha.
.
.
“Naona kuna matatizo,” akasema Mama Brian. Runinga haikuwa inaonyesha kitu isipokuwa chenga nyeupe tu. Hakujali sana, akaweka rimoti juu ya runinga na kumrudia mgeni wake.
.
.
“Naona kuna matatizo, haionyeshi kitu!”
.
.
“Ni ajabu,” mgeni akasema akitikisa kichwa chake kisha akabinua lips zake nyembamba.
.
.
“Vipi, kuna lolote?” Mama Brian akadadisi.
.
.
“Yah!” Jirani akaitikia kwa uhakika. “Walikuwa wanamwonyesha mtoto mmoja aliyepotelea msituni na kupatikana!”
.
.
“Kweli?” Mama Briana akakodoa macho.
.
.
“Ndio!” akajibu yule jirani. “Ni ajabu. Ni yeye pekee ndiye aliyefanikiwa kurudi baada ya kupotea. Simulizi yake hakika ilikuwa inasisimua! Ila sikufahamu nini kimetokea maana runinga ilizima picha nikadhani ni kwangu tu.”
.
.
“Haukusikia chochote kile?” Mama Brian akauliza. Habari hii ilimvutia. Kwa muda akasahau kuhusu swala la Wisconsin. Hata Brian aliyekuwa ndani naye akasimamisha masikio kuskiza.
.
.
“Sikusikia jambo la maana,” akajibu jirani. “Kabla ya mtoto huyo kuongea, basi runinga ikakata mawasiliano mpaka sasa.”
“Umemtambua mtoto huyo?” Mama Brian akauliza. Jirani akatikisa kichwa. “Hapana. Si wajua Boston ni kubwa!”
.
.
Basi akaendaze, huku nyuma Mama Brian na mwanae wakabakiwa na maswali. Walitamani kumwona mtoto huyo, au kusikia taarifa zake kwani kwa namna moja ama nyingine walikuwa wanazihitaji.
.
.
Brian akasema, “Nadhani kesho naweza kuzipata taarifa hizo vizuri.”
.
.
“Wapi?” Mama akauliza.
.
.
“Shuleni,” Brian akajibu na kuongezea, “Shule ni kubwa, sidhani kama atakosekana mtu mwenye habari hizo kwa undani.” Wazo hilo likajenga hoja kichwani kwa Mama. “Itakuwa vizuri ikiwa hivyo!” akanyanyuka na kwenda jikoni kufanya utaratibu wa chakula. Baada ya muda, chakula kikawa tayari.
.
.
“Brian, unahitaji chakula kwa sasa?”
.
.
“Hapana. Namngoja kwanza bwana Wisconsin.”
.
.
Mama akenda chumbani kumwita Olivia, punde akarejea naye, Olivia alikuwa amelewa usingizi, akampatia chakula, kisha akaketi kitini.
.
.
“Hauli?” Brian akamuuliza. Akatikisa kichwa chake na kusema, “Hapana, Sijisikii. Acha tumngoje Wisconsin kwanza.”
.
.
Kukawa kimya kidogo. Ni Olivia ndiye aliyevunja ukimya kwa kuomba atazamae runinga.
“Haionyeshi, mpenzi!” Mama akamjibu, ila akanyanyuka na kuendea rimoti ili athibitishe maneno yake kwa Olivia. Akawasha runinga. “Ona! Haionye–”
.
.
Hajamalizia, akashangaa picha zaonekania kideoni! “Brian, tazama!” Mama akapayuka. “Inaonyesha hivi sasa!”
.
.
Brian akauliza, “Ni chaneli gani ilirusha ile habari?” Mama naye hakuwa anajua. Wakapata kibarua cha kukagua chaneli zote kwa wepesi. Hawakuona kitu. Chaneli zote zilikuwa zaonyesha mambo mengine. Ila kuna moja bado ilikuwa giza.
.
.
“Ebu ngoja!” Brian akamtaka Mama yake asubiri kwanza hapo penye giza. “Hamna kitu!” Mama akasema.
.
.
“Hapo huwa ni chaneli gani?” Brian akauliza. Mama akapandisha mabega. “Sijui! Nitajuaje na haionyeshi?” Olivia akasema, “Ven 24! … inaitwa Ven 24.”
.
.
“Umejuaje?” Mama akauliza.
.
.
“Kwasababu ndiyo chaneli inayofuata baada ya kutoka Kids Date,” Olivia akajibu akiwa anatafuna.
.
.
“Najua zilipo studio zao,” Brian akasema, “Kesho nitaenda huko kuwauliza. Nadhani tutapata jambo.”
.
.
“Ila Brian,” Mama akatilia shaka. “Ni saa tatu sasa yaelekea na nusu, vipi kuhusu Wisconsin?” Kabla Brian hajajibu, Mama akaamka na kuuendea mlango, akafungua na kuchungulia nje. Hakukuwa na mtu, barabara ilikuwa nyeupe. Akafa matumaini.
.
.
“Inabidi tufanye jambo, Brian,” Mama akashauri.
.
.
“Niende kumfuatilia?” Brian akauliza. Mama akabanwa na
kigugumizi.
.
.
“Sidhani kama ni wazo jema. Pengine tuwataarifu polisi.”
.
.
“Unadhani kweli hilo ni wazo jema?” Brian akauliza na kuongezea, “Kumbuka ni mauaji!”
Mama akakosa la kusema. Hakujua nini afanye. Bahati ndani ya muda mfupi wakasikia mlango unagongwa na mara Wisconsin akaingia ndani. Wakalipuka kwa furaha wakimkaribisha kwa hamu tele ya kutaka kujua nini hicho kimemkalisha muda mrefu hivyo mpaka wakapata hofu kubwa.
Kabla Wisconsin hajasema jambo, akaomba aletewa chai ya moto ajipashe mwili. Akanywa mafundo matatu ya chai hiyo na akiwa ametuama kwa fikra kisha akasema akimtazama Brian, “Brewster ameenda. Ulifanya jema sana kumuua akiwa katika mwili wake wa ulimwengu mfu. Endapo angekufa akiwa kwenye mwili wake wa kawaida basi mtihani ungekuwa mkubwa kwenye ulimwengu wa kiroho. Bado angalikuwa hai.”
“Lakini kwanini ukakawia hivyo?” Brian akauliza. Wisconsin akamjibu, “Kwasababu kulikuwa kuna mambo mengi ya kutazama.” kisha akamuuliza, “Unamjua vema bwana mwenye nyumba ile?”
“Dkt Hamill?”
“Ndio. Unamjua vizuri mtu huyo?” Wisconsin akauliza.
“Siwezi kusema namjua sana, sikupata muda mrefu wa kukaa naye,” Brian akajibu. Wisconsin akamuuliza, “Kwa muda huo ukamfahamu ni mtu wa aina gani?”
“Ni mtu mkarimu … pia mpweke,” Brian akajibu. Wisconsin akanyamaza kwa sekunde tatu, bado akimtazama Brian, kisha akamuuliza, “Una uhakika?”
Brian akatikisa kichwa. “Ndio, nina uhakika. Alinifanyia sana ukarimu. Siwezi kumsahau.”
“Sawa,” Wisconsin akasema na asiseme tena lingine. Brian akauliza, “Vipi kuna lolote?” Wisconsin akamtazama na kutikisa kichwa. “Hamna kitu. Tutaongea zaidi kesho, nahitaji kupumzika hivi sasa.”
“Ngoja basi ule,” Mama Brian akashauri. “Hapana,” Wisconsin akajibu. “Sijiskii njaa, nitakula kesho.” alafu akaenda zake.
Akiwa anaenda, Brian akagundua Wisconsin alikuwa na alama ya damu kwenye nguo yake. Akataka kuuliza lakini akaona ni stara kunyamaza. Wisconsin hakuwa kwenye hali ya kuongea, pengine kesho atafunguka zaidi.
“Vipi kuhusu yule mtoto wa kwenye runinga?” Mama akauliza. “Unadhani kuna haja ya kumwambia?”
“Ndio,” Brian akajibu na kuongeza, “lakini si kwa sasa. Unamwona hayupo kwenye mandhari hayo. Kesho nikitoka shule, nitateta naye vizuri.”
Basi Mama na Olivia nao wakaaga wanaenda kulala, Brian akabakia mwenyewe sebuleni akitazama runinga. Hakuwa mtazamaji mzuri wa runinga ila aliguswa tu kutazama kwa muda huo akidhani pengine anaweza kuona jambo kuhusu yule binti aliyekuwa anahojiwa.
Akaweka chaneli hiyo na kutazama, kulikuwa bado ni kiza. Si sauti wala picha yoyote ambayo ilikuwa inaonekana ama kusikika. Akatazama kwa sekunde kadhaa kisha akasimama na kuisogelea runinga. Akaendelea kutazama kwa makini. Baada ya muda kidogo, akahisi amesikia sauti ya kitu.
Akatazama kushoto na kulia kwake, hakukuwa na kitu. Alipotulia ndipo akajua ya kuwa sauti hiyo inatokea kwenye runinga. Ilikuwa ni sauti ya watu wakiruruma kwa chinichini. Brian akatazama runinga kwa macho ya ndita. Bado hakukuwa na picha, na sauti hii ilikuwa inaendelea kusikika. Ni ya nini?
Brian akaongeza sauti asikie lakini ajabu sauti hiyo haikuwa inaongezeka, ilibakia vilevile japo iliongezwa! Brian akalazimika kuegesha sikio lake kwenye spika za runinga. Akatulia tuli akisikiza kwa umakini…
“ … ruruma rurururuma … zizizissiiizii … vitiviikiviiizz … shishshishizz … trrriikk … chiiichiiib …” sauti ilinguruma pasipo kueleweka. Ilikuwa ni sauti nzito ya kiume. Brian alijitahidi sana kuisikiza aone kama atapata kitu lakini hakuambulia jambo. Akiwa anataka kuachana na sauti hiyo, mara akasikia sauti ya kike! Akatulia tena na kuskiza kwa umakini …
“tiiipttiiiiifff … reeegghaaatt … katkatgushik … chat,chat,chat … sssshhhhhh…” sauti ya kike ilinong’ona na kuendelea kunong’ona. Brian akajitahidi kuiskiza ili aone kama ataitambua sauti hiyo lakini hakufanikiwa. Ilikuwa ni ngeni kabisa.
Baada ya muda kidogo sauti hiyo ikakoma na kukawa kimya. Brian akatazama runinga kama kuna picha. Hakuona kitu. Akarudisha tena sikio lake kwenye spika ya runinga na kuskiza. Hakusikia kitu. Akakaa kwa kama dakika tatu kungoja kama kuna sauti ama picha itaonekana, hakuona wala kusikia kitu. Basi akaona ni kheri akazima runinga akalale.
Akaminya kitufe chekundu cha rimoti na kisha akaweka rimoti juu ya runinga, akageuka na kwenda zake azime taa kisha aende kulala. Alipofikia ‘switch’ kabla hajazima, akasikia sauti tena. Akageuka na kutazama runinga kwa hofu. Hakuona jambo ila sauti iliendelea kusikika.
Akiwa hapohapo ameduwaa, sauti ile ya runinga ikaendelea kuongezeka zaidi na zaidi mpaka kufikia kikomo chake cha mwisho na kuwa kelele kali! Haraka Brian akawahi rimoti na kujitahidi kupunguza mpaka kuwa sauti ndogo kabisa, kisha akatahamaki. Mbona nilizima runinga hii?
Akaiwasha tena na kuizima wa uhakiki. Akaiwasha tena kwa mara ya pili na kuizima kwa uhakiki zaidi alafu akaweka rimoti juu ya runinga na kuiendea ‘switch’ azime taa ya sebuleni.
Akazima taa, kukiwa kimya na salama. Kabla hajaelekea chumbani akaitazama tena runinga. Ilikuwa kimya na nyeusi. Hakukuwa na kiashiria chochote cha shaka. Basi akaelekea chumbani mwake akapumzike.
Akiwa amepiga hatua tano koridoni ambapo kiza kilikuwa kimetawala kwa taa kuzimwa, mara akaona mwanga hafifu ukimulika ukuta. Akasimama na kutazama akijiuliza mwanga huo unatoka wapi.
Alipotazama vema akagundua kuwa unatokea sebuleni. Haukuwa mwanga wa taa, bali runinga! Moyo wake ukakita fundo. Nani amewasha runinga na hakumwacha mtu sebuleni? Akajiuliza aende kutazama ama aachane nayo aende zake chumbani ajifungie na komeo?
Akapiga hatua mbili kusogelea mlango wake, akaona mwanga ule wa runinga ukiwa unachezacheza kuonyesha kwamba kuna kitu kinachorushwa kwenye kideo, kioo cha runinga kinaonyesha matangazo ya picha! Hapa akasita na kujiuliza, moyo wake ukiwa unaelekea kuchanganyia mwendo.
Aende kutazama ama aelekee chumbani mwake afunge mlango na kujifunika shuka gubigubi?
Akadaka komeo la mlango wa chumba chake. Akaminya komeo mlango ukafunguka. Kabla hajaingia, akasikia sauti ya runinga! Akatuliza vema masikio yake kuhakikisha. Ni kweli, ni sauti ya runinga. Kwahiyo sasa haikuwa picha pekee, bali pia na sauti yake!
Sauti hii Brian alipoisikiliza vema akagundua ni ya mahojiano kati ya mtangazaji na binti mdogo wa kike. Ilikuwa ya mahojiano yale ambayo waliyakosa sababu ya mtandao wa chaneli kuzimika. Basi akaona ni stara kukakata shauri akasikize, au angalau achungulie kinachoendelea.
Akarudishia mlango wake wa chumbani kisha taratibu akaanza kusonga kwenda sebuleni. Kwa mwendo wake wa majeraha, taratibu taratibu.
Alipofika kwenye kingo ya korido, akarefusha shingo yake kuchungulia. Kwenye runinga akamwona mtangazaji na binti mdogo wa kike akihojiwa. Uso wa mtangazaji aliuona, ila sura ya yule binti hakuiona kwani alikuwa ameipatia mgongo kamera. Kilichokuwa kinaonekana ni nguo na nywele zake alizobana mafungu mawili.
Mbali na runinga, Brian akatazama kukagua sebule nzima kama kuna mtu aliyewasha na kutazama runinga. Hakuona mtu. Sebule ilikuwa tupu na pweke, basi akahamaishia macho yake runingani kuendelea kutazama. Wakati huo moyo wake bado haujatulia. Hata kichwa chake kinamgonga kuashiria mambo hayako vile yanavyotakiwa kuwa.
“ … Ni nani alikuwa anakuitia msituni?” Mtangazaji akauliza. “ … ulimwona kwa sura?”
Binti yule runingani akatikisa kichwa na kusema, “Nilimwona.”
“Yupoje?” Mtangazaji akauliza. “Unaweza kumwelezea kwa umbo na sura yake?”
Kabla binti huyo hajajibu, Brian akashtushwa na hodi mlangoni! Moyo wake ukapiga bampa na kuanza kwenda kasi maradufu. Alihisi hofu sana. Miguu yake ilianza kutetemeka mpaka kugongana.
Hodi ikapigwa tena, na mara hii anayegonga akasema, “Heey!”
Ilikuwa ni sauti ya kike. Brian akajaribu kuwaza ni ya nani, upesi akili yake ikamkumbuka yule jirani. Ni yeye ndiye alikuja akagonga mlango muda ule alafu akasema heey!
Ina maana amekuja tena? Brian akawaza. Muda huu?
“Tafadhali,” sauti ikasema mlangoni. “…Naweza kuja kuangalia hicho kipindi?”
Brian akatoa macho kwa kuduwaa lakini pia kwa woga. Akasonga hatua kadhaa kulifuata dirisha kisha akatupa macho yake nje kutazama mlangoni. Hapo akamwona jirani yao akiwa pia na mtoto wake ambaye ananesanesa kumbembeleza.
Sehemu Ya 9
Asubuhi ya saa moja na nusu …
Brian akajiuliza zaidi. Akahisi mpaka kichwa chake kinamgonga kwa kuparamiwa na mawazo mengi. Ni namna gani haya mambo yanawezekana? Akaendea dirisha lilikuwepo karibu na runinga akatazama nje kwa jirani yake, akaona ni giza totoro. Sasa ameamkaje pasipo kuwasha taa?
Hodi ikagongwa tena, mara hii sauti ikasema, “Brian, nifungulie niingie!” ilikuwa si ombi bali amri! Brian akaogopa kwenda kufungua, badala yake akaenda mbali na mlango. Akiwa amekaa karibu na korido, akatazama mlangoni. Kulikuwa ni kimya. Aliwaza ni nini kitafuata. Runinga bado ilikuwa inaonyesha lakini hakuwa anaizingatia hivi sasa kama afanyavyo kule mlangoni.
Kukawa kimya kwa kama dakika nne. Brian akawaza pengine kumekuwa shwari, labda mgeni yule atakuwa ameenda zake. Akiwa hapo akijiwazia mema, akasikia mtu akiita jina lake. Haraka akageuza uso wake kutazama kule kwenye runinga. Ilikuwa ni sauti ya kike. Alipoangaza kideoni akaona sura ya mwanamke ambaye alihisi anamfahamu.
Mwanamke huyo alikuwa amevalia sare ya watumishi wa kike kanisani. Gauni jeusi na kiremba chake cheusi. Uso wake ulikuwa mweupe, wenye kutuama kihisia.
Nimemwonea wapi huyu mwanamke? Brian akajiuliza. Yule mwanamke kideoni akakunja sura yake na kutisha, akasema akimnyooshea Brian kidole, “Umeniua. Nami nitakuua!”
Brian ndipo akamkumbuka sasa mwanamke huyu. Alikuwa ni yule Dada aliyeambatana na polisi kule korongoni kanisani. Anasemaje nimemuua? Brian akajiuliza.
“Sijakuua mimi,” akasema kujitetea. Hakuwaza kama anaongea na runinga. “Sihusiki na kifo chako, sijakuua mimi!”
Yule Dada ndani ya runinga akaropoka, “Umeniua!” sauti yake ilikuwa kali na uso wake aliufuma kwa hasira. Alitoa macho na kubinua mdomo wake kana kwamba pakacha. “Nami nitakuua, Brian. Nitakufinyanga mkononi mwangu na kusagasaga mifupa yako kuwa chengachenga. Nitakuua, Brian!”
Punde Brian akahisi kuna mtu nyuma yake. Mwili wake ukapigwa ganzi ya baridi. Akapepesa macho yake akigeuka taratibu kutazama nyuma ya mgongo wake. Mara mkono wa mtu ukamtua begani na kisha sauti ya kiume ikasema, “Brian, bado hujalala?”
Kukurupuka kutazama, akakutana na Wisconsin. Akashusha pumzi ya hofu na mkono wake wa kuume akauweka kifuani kupooza mapigo yake ya moyo.
“Ni wewe!”
“Ndio, ni mimi. Mbona hujalala mpaka saa hii? Ulikuwa unaongea na nani?”
Brian akatazama runinga, ilikuwa kimya na imezima, akastaajabu akiinyooshea kidole, “Kuna mtu … kuna mtu alikuwapo ndani ya runinga!”
“Ulikuwa unatazama runinga mpaka sasa?”
“Hapana! Kuna mtu alikuwepo ndani ya runinga akiongea na mimi!”
Wisconsin akarusha macho kwenye runinga. Hakuona kitu. Akayarudisha kwa Brian. “Una uhakika?”
“Ndio. Kuna mtu alikuwepo kwenye runinga!” Brian akasihi akionyeshea kidole runingani.
“Ni nani?” Wisconsin akauliza. “Alikuwa anasema nini?”
“Alikuwa ni yule Dada aliyekuwa na polisi kule korongoni kanisani! …” Brian akajibu. “ … anadai mimi nimemuua. Anasema naye pia ataniua!”
Wisconsin akakunja ndita za kushangazwa asiseme jambo. Akakagua sebule na kisha akatupa macho yake nje ya dirisha. Hakuona kitu. Akamtaka Brian aende kupumzika.
“Siku ya leo ilikuwa ndefu sana kwako. Umefanya mambo mengi na mazito lakini hujapata muda wa kupumzika. Nenda kalale, Brian. Kapumzishe mwili wako.”
Brian akaendea chumba chake akichechemea. Kweli alikuwa amechoka. Macho yake yalikuwa mekundu na uso wake ukiwa umeelemewa kwa uchovu. Alijitupa kitandani, akasikia sauti ya mlango wa chumba alalacho Wisconsin kikiwa kinafungwa.
Akatazama chumba chake akitafuta usingizi. Muda si mrefu, usingizi ukambeba na kumfanya asijitambue kwa muda. Akalala fofofo akikoroma.
Asubuhi ya saa mbili akaamshwa na sauti fulani ya kipaza sauti. Akajibandua kitandani na kujinyoosha. Mwili wake ulikuwa umejawa na maumivu karibia kila sehemu. Wakati anajinyoosha alijikuta akilalamika kwa maumivu huku akikunja sura kana kwamba amelamba ndimu.
Akasonga dirishani na kuangaza nje. Mwanga wa jua ulikuwa safi, watu walikuwa wanakatiza hapa na pale. Miongoni mwao alikuwa ni mwanaume mzee aliyebebea kipaza sauti akitangaza. Huyu ndiye aliyefanya Brian akaamka.
Brian akatega sikio amsikie ni nini anasema. Alipofanya hivyo akagundua mtu huyo alikuwa akitangaza kuhusu msiba wa mmoja wa wafanyakazi wa muda mrefu wa ofisi ya mtaa wao. Naye si mwingine bali bwana Brewster.
Kwa mujibu wa mtangazaji, Bwana Brewster amekutwa akiwa amefariki nyumbani kwake kwa kile wanachoamini kuwa ni mshtuko wa moyo. Hivyo basi kwakuwa mzee huyo aliitumikia serikali kwa karibu maisha yake yote, basi serikali itasimamia kila kitu msibani. Watu tu wanaomba wafike kumpa heshima zake za mwisho kwenye ardhi ya makaburi.
Bwana huyo akatokomea akitangaza. Akamwacha Brian akiwa na maswali juu ya tangazo hilo. Amekutwa ndani? Mosi. Amekufa kwa mshtuko wa moyo? Pili. Akajiuliza mwenyewe asiwe na majibu. Akatoka hapo dirishani na kwenda sebuleni. Akamkuta Wisconsin, Olivia na Mama wakiwa wamekaa wanapata kifungua kinywa. Baada ya salamu, akawauliza, “Mmesikia tangazo hilo?”
“Lipi?” Mama akauliza.
“La Brewster?” Wisconsin naye akatupa swali lake akimtazama Brian kwa macho ya nje ya kikombe cha chai.
“Ndio la Brewster!” Brian akajibu. Wisconsin akamwambia,
“Ndio, tumesikia. Nadhani itabidi tuhudhurie msiba huo. Nimeshamweleza mama yako hapa.”
“Kwanini?”
“Kwani huwa hamna desturi ya kuhudhuria misiba?”
“Tunayo, ila si kwa mtu kama Brewster!”
“Hastahili kuzikwa? … Brian, kaa chini.”
Brian akaketi akimtazama Wisconsin.
“Umelisikia hilo tangazo, si ndio? Na kwasababu umesikia tofauti na unavyojua ndiyo maana ukakimbilia hapa kuja kutuambia, sio? … sasa kama umesikia usilolijua hapo tu kwenye tangazo, utayasikia mangapi msibani?”
Kabla Brian hajajibu, Wisconsin akanywa fundo moja kubwa la chai na kukiweka kikombe mezani kikiwa kitupu. Akasema, “Tutaenda huko asubuhi. Liweke hilo kwenye ratiba yako, sawa?”
Brian akatikisa kichwa asiseme jambo. Mama akamuuliza, “Nikupatie chai?” napo akatikisa kichwa. “Hapana, niko sawa.”
“Leo hutaenda shule, sio?” Wisconsin akamuuliza.
“Sitaenda,” akajibu na kuongezea, “Nimeshachelewa.”
Wisconsin akasafisha koo lake na kusema, “Mama yako amenambia kilichojiri jana wakati sikuwapo. Ulisema unajua kile kituo cha habari kilipo?”
“Ndio, najua.”
“Basi waweza jiandaa tukaenda huko?”
“Sasa hivi?”
“Ndio, au una kazi ya kufanya?”
Brian akatikisa kichwa.
Basi baada ya nusu saa wakawa tayari wamejiandaa. Wakachukua gari la Mama kuelekea kule kwenye kile kituo ambacho walifanya mahojiano na yule binti aliyepotea na kisha kupatikana. Kwakuwa Brian alikuwa na majeraha, Wisconsin akashikilia usukani.
Mama akawasihi, “Tafadhalini kuweni makini.”
“Usijali,” Wisconsin akamtoa hofu. “Tutafanya hilo kadiri tuwezavyo.” kisha akawasha gari na kutimka.
Wakatembea kwa muda wa takribani lisaa limoja na dakika kumi na saba, ndipo wakafika mbele ya studio ya chombo hicho cha habari. Wakaegesha gari kando na kusonga ofisini.
“Naweza kuwasaidia?” aliuliza mwanadada wa mapokezi. Alikuwa amevalia sare, shati jeupe na kizibao cheusi chenye chapa ya chombo chao cha habari kifuani.
“Tunahitaji kuonana na mwandishi fulani wa habari,” akasema Wisconsin. Brian akadakia, “Yule aliyemfanyia mahojiano mtoto aliyepotea.”
Mdada yule wa mapokezi akawatazama na kuwauliza, “nyie ni wakina nani?” wakati anauliza, akasogeza mkono wake kufuata simu yake ya mezani. Uso wake ulionyesha mashaka.
“Sisi ni ndugu zake na yule mtoto,” Brian akawahi kujibu.
“Nani yake?” Dada wa mapokezi akauliza. Brian akamgusa Wisconsin na kusema, “huyu ni mjomba wake,” kisha akajionyeshea kidole na yeye, “mimi ni binamu yake.”
“Kwani hamjui anapokaa?”
“Tunapajua, ila tumekuja hapa kwa ajili ya yule mtangazaji na si mtoto,” akajibu Wisconsin.
Dada yule akawatazama kwa sekunde chache. Mkono wake ulikuwa tayari umeshikilia simu ya mezani. Akauliza,
“Mnamtakia nini bwana huyo?”
Brian akamjibu, “Kuna mambo tunataka kumwambia zaidi ambayo pengine hayafahamu.”
Dada yule baada ya kuwatazama tena kidogo, akatoa mkono wake kwenye simu na kushusha pumzi ndefu. Akawaomba wakina Brian waketi kwenye kiti kwa muda mchache. Brian na Wisconsin wakatii, wakaendea sofa lililokuwapo hapo, wakaketi kungoja.
Yule dada akaongea na simu kwa dakika moja kisha akarejesha simu mezani na kuendelea na kazi yake. Baada ya dakika kama tatu, simu ikaita, akapokea na kuongea nayo kwa kama dakika moja na nusu kisha akawaita wakina Brian.
“Mtu mnayemhitaji, hayupo kwa sasa. Tulitarajia atakuja kazini lakini imeshindikana. Mnaweza kwenda mkarejea siku nyingine.”
Dada aliposema hayo, akaendelea na kazi yake ya kushika makaratasi. Brian na Wisconsin wakatazamana kwa maulizo kisha Brian akauliza, “Samahani, unaweza kutuambia alipo? Tunaweza kumfuata maana tuna usafiri.”
Basi baada ya kumbembeleza huyo dada, akakubali na kuwapatia anwani ya makazi ya huyo mtangazaji. Wakamshukuru na kwenda zao kufuata chombo kilichowaleta, wakatimka kuelekea katikati ya mji wa Boston. Walipotembea kwa takribani robo saa, wakawa wamewasili mbele ya jengo la ghorofa ambapo hapo waliegesha gari lao na kuanza safari ya kwenda kwenye chumba walichoelekezwa.
Hili lilikuwa ni miongoni mwa maghorofa ya muda mrefu hapa Boston. Yalikuwa ni maghorofa mapacha yaliyopakana, ila hili walilopo wakina Brian lilikuwa ni refu zaidi.
Wakasonga na ngazi mpaka kwenye sakafu ya tano, hapo wakaendea upande wao wa kushoto na kukomea kwenye mlango uliopachikwa nambari 455. Wakagonga mara tatu.
Kimya.
Wakagonga tena na tena, bado kimya. Brian akachungulia kwenye tundu la komeo kama ataona ufunguo, haukuwepo. Akakagua chumba hicho kwa kupitia kitundu hicho, hakumwona mtu. Vitu vilikuwa vuruguvurugu.
Na kwakuwa kitundu ni kidogo, hakuona vema chumba kizima. Alitamani atazame zaidi. Akiwa anachungulia akagundua kuwa dirisha, kule upande wa mbali ukutani, lilikuwa wazi. Akaona ni fursa nzuri ya kutazama chumba hicho.
“Tuzunguke kwa nyuma,” akamwambia Wisconsin.
“Kufanya nini?”
“Dirisha lipo wazi. Twenda tukatazamie chumba huko!”
Wakiwa hapo wanateta, kuna jirani mmoja, mwanamke mzee, alikuwa anawatazama tangu mwanzo. Bibi huyo, akatokea kuwahisi vibaya. Alidhani huenda wakawa wezi kwa namna walivyokuwa wanahangaika mlangoni pale.
Na alivyowaona wakina Brian wakielekea upande wa nyuma ya jengo, akapata mashaka zaidi. Alitazama kando na kando amwambie mtu yeyote juu ya mashaka yake lakini hakukuwapo na mtu. Chumba kizima alikuwa mwenyewe.
“Unaona,” Brian akasema wakiwa wanatupa macho ndani ya chumba. Kitanda kilikuwa kimevurugwa, kuna vikombe chini na sahani iliyopasuka. Walipotazama vema, wakagundua hata mashuka yale yalikuwa yamechanika.
“Kuna nini kimetokea humu ndani?” akauliza Wisconsin kwa kuduwaa kisha akasema “inaoyesha mwenyeji hajatoka humu ndani, umeona viatu vyake …” akaonyeshea kidole pembeni ya mlango, hapo kulikuwa na viatu, kimoja kimesimama wakati kingine kikiwa kimelala.
Brian akauliza, “Vipi kama ana viatu vingine?” Wisconsin akamwonyeshea stendi ya viatu na kumwambia, “basi vile angekuwa kavirejeshea mahala pake.”
Punde kidogo, Brian akaropoka, “Ona kule!” alikuwa amenyooshea mlango wa bafu. Mlango huo ulikuwa ni wa kioo kinachohakisi kwa uhafifu. Kwa chini yake, ilionekana kitu kama damu.
Wisconsin akasema, “yatupasa tuingie ndani. Ukute amekufa, hakuna mtu anayejua!”
Basi kwa kupitia dirisha, wakazama ndani. Kabla hawajapekuapekua, wakanyookea moja kwa moja bafuni kutazama damu ile inatokea wapi. Huko wakakuta mwili wa mtangazaji wanayemtafuta ukiwa upo chini umevuja damu lukuki toka kichwani.
Bafu zima limejawa na damu. Mkononi mwa mwanaume huyo alikuwa ameshikilia sabuni ya kuogea akiwa uchi wa mnyama.
“Amedondoka!” akasema Brian akiwa ametumbua macho. Wisconsin akatikisa kichwa, “Hapana, ameuawa!” Kisha wakatoka ndani ya bafu na kutazama mule chumbani, “Kama angekuwa ameanguka huko bafuni, kwanini shuka limechanwa na vyombo vikapasuliwa? … tazama!” Wisconsin akaonyeshea mlangoni mwa bafuni. “Hata viatu vyake vya kuogea, hakuvaa!”
Brian akauliza, “Sasa nani atakuwa amemuua?”
“Mtu mwenye matumizi naye,” akajibu Wisconsin na kuongezea, “mtu ambaye hataki awe hai.”
“Nani huyo?”
“Brian,” Wisconsin akaita na kumtazama kijana huyo, akamuuliza, “Leo umeona tangazo la watoto kupotea?”
“Hapana!” Brian akatikisa kichwa.
“Basi huyo anayepoteza watoto, atakuwa alikuwa hapa usiku.” kitendo cha Wisconsin kumaliza kuongea kauli hiyo, dirisha likacheza baada ya upepo kupuliza ghafla. Wote wakalitazama.
Kabla hawajafanya kitu, mara dirisha likajifunga na kujitia ‘lock’. ilikuwa ni ajabu kwani hakukuwa na mtu aliyefanya hivyo. Dirisha lilijibana vema kana limesogezwa na mtu. Na kama haitoshi, pazia nalo ambalo lilikuwa wazi, likasonga na kujifunika.
Ndani kukawa na giza!
Brian akamshika mkono Wisconsin wakiwa wamestaajabu. Ndani ya muda mfupi, wakasikia sauti ya maji yakiwa yanamiminika huko bafuni kisha ikafuatiwa na sauti ya mtu akiwa anapiga mluzi.
Moyo wa Brian ukaanza kwenda mbio. Wisconsin naye akatetemeshwa na wakisikiacho. Haraka wakaendea mlango na kujaribu kuufungua, haukufunguka. Wakatazama kuutafuta ufunguo, mara ufunguo ukarushwa tokea bafuni.
Haraka Brian akauchukua na kuchokonolea mlango, bado mlango haukufunguka! Brian akapayuka, “Si wenyewe!” huku akimtazama Wisconsin kwa macho ya hofu.
Kidogo tena, ufunguo ukarushwa tokea chini ya mlango wa bafuni. Brian kabla hajauokota, akamtazama kwanza Wisconsin kana kwamba anahitaji ruhusa alafu haraka akaukwapua ufunguo ule na kuchokonolea mlango.
Bado haukufunguka.
Akiwa anahangaika, ufunguo mwingine ukarushwa, wa tatu sasa kwa idadi, lakini nao haukufungua mlango. Sasa wakawa hawana matumaini na funguo zile zirushwazo.
Maandishi yakaandikwa kwenye kioo cha mlango wa bafuni. Kwakuwa kulikuwa na unyevu wa maji, yakaonekana vema japo yaliandikwa kwa ndani. Maandishi hayo yalisomeka,
“Hakuna Ufunguo Wa Kuwatoa Mkiwa Hai.”
Walipoyasoma, mkono ukayafuta na mara mlango ukaanza kufunguka taratibu. Brian na Wisconsin wakaanza kusonga mbali kusogelea dirishani. Mlango ukakoma kufunguka, na ghafla humo ndani akatoka kiumbe ambacho hawakukitambua. Kilikuwa ni cheusi, chenye mwili mpana na mrefu.
Kikamjia Wisconsin na kumkaba kwanguvu. Kikamnyanyua juu na kumtupia ukutani ambapo alijibamiza na kudondoka chini. Kichwa kikamgonga na punde akazirai. Kiumbe kile kikamgeukia Brian!
Brian akatoa macho na kuhisi anakosa pumzi.
Haraka akanyakwa koo na kunyanyuliwa juu, kisha kama Wisconsin alivyofanywa, naye akatupwa kana kwamba unyonya. Akabamiza ukutani na kudondoka chini! Mbaya akakita kiuno chake kwenye kingo ya kitanda. Akalalama kwa maumivu makali aliyoyapata!
Yule kiumbe, ambaye bado hakumtambua, akamjongea tena upesi alafu kama mpshi akagawanyika na kumvaa Brian puani na mdomoni. Brian akaanza kukohoa kana kwamba anakata roho. Akatoa macho akikohoa. Mpaka mishipa ya damu ikamsimama kichwani akipambana kudaka shingo yake.
Alikuwa anaelekea kufa!
Ni kheri muda kidogo mlango ukabamizwa na punde ukafunguliwa kwa kuvunjwa! Wakaingia ndani wanaume wawili waliovalia sare za polisi, hamaki wakawaona Brian na Wisconsin wakiwa kwenye hali mbaya. Haraka, katika namna ya ajabu, Brian akajikuta anapata ahueni na lile fukuto lililokuwa linamkaba na kuminya viungo vyake vya hewa likamwacha akiwa anapambania pumzi kana kwamba mwana mroho aliyeona chakula baada ya miaka kenda.
Polisi wakapiga simu kwa watoa huduma za afya za dharura, baada ya muda mfupi wakawasili na kuwapatia huduma Wisconsin na Brian. Maiti iliyokuwepo ndani ikachukuliwa na kusafirishwa kwenda hospitali kwa matunzo.
Wisconsin aliporejea kwenye fahamu zake na Brian pia kupata unafuu wa kumwezesha kuongea, wakahojiwa na polisi.
“Tulimkuta akiwa amekufa,” alisema Brian, “Inaonekana alikufa tangu usiku wa kuamkia leo hii, na ajabu ni kwamba muuaji bado alikuwepo ndani ya eneo.” wakati akizungumza, polisi alitega sikio lake vema akimtazama Brian kwa umakini.
Polisi huyu alikuwa ndiye yule ambaye alimfanyia mahojiano Mama Brian baada ya lile tukio la mapolisi wawili kuuawa mbele ya nyumba yake na mtu asiyejulikana. Kwa jina polisi huyu aitwa Afisa Randall.
Akauliza, “Mnaweza kumtambua muuaji huyo?” Brian akatikisa kichwa na kujibu, “hapana. Hakuwa anaonekana usoni. Alikuwa ni kiumbe cha ajabu hakika!”
Afisa Randall akashusha pumzi na kutikisa kichwa chake. “Umesema unaitwa Brian, sio?”
“Ndio.”
“Brian,” afisa Randall akaita na kusema, “Hatufanyi maigizo hapa bwana Brian. Hii ni kesi kubwa. Kesi ya mauaji. Tafadhali nipatie taarifa zenye mantiki.”
Wisconsin akadakia kwa kusema, “Anachosema ni ukweli mtupu.” Sasa afisa Randall akamtazama Wisconsin aliyekuwa amekaa pembeni ya Brian.
“Tuliukuta mwili wa marehemu ukiwa bafuni, umelala mfu. Mkononi mwake kulikuwa na sabuni kavu na kwenye mlango wa bafu kukiwa na viatu vya kuogea ambavyo hakuvitumia. Chumba chake kilikuwa shaghalabaghala. Alipambania roho yake chumbani kabla hajapelekwa kuuawa huko bafuni!”
Afisa Randall akauliza, “na ninyi mliingiaje ndani kwake ingali palifungwa?”
“Kwakupitia dirishani,” Brian akawahi kujibu. “dirisha lilikuwa wazi. Baada ya kuchungulia kwenye tundu la mlango tulibaini hilo na kuamua kutumia njia hiyo kuzama ndani.”
“Kutokana na hicho mlichokifanya, nikiwaita ninyi ni wezi ama wauaji nitakuwa nimekosea? Vipi kama ni ninyi ndiyo mliomuua na kisha mkatengeneza mazingira?”
“Hatujamuua. Hatuna sababu ya kumuua!” Brian akajitetea.
Afisa Randall akabinua mdomo wake na kuuliza, “mlivyoona kuna dalili za hatari, kwanini hamkutoa taarifa polisi badala ya kuvunja na kuzama ndani mwa watu pasipo ruhusa?”
Swali hili likawa gumu. Afisa Randall akawatazama na kisha akasema akitazama kushoto kwake kwa mbali, “mnamwona yule bibi? … ndiye ambaye alitoa taarifa juu yenu baada ya kuwahisi vibaya … mnadhani alikosea?”
“Hapana,” Wisconsin akasema na kujitetea, “Hatukuwa na namna ya karibu ya kuwasiliana na polisi kwa-”
“Vipi kuhusu majirani?” Afisa Randall akamkatisha. Na asisubirie majibu akanyanyuka na kuwataka Wisconsin na Brian wazame ndani ya gari waende kituo cha polisi kwani wana kesi ya kujibu. Tena kesi ya mauaji.
Wakiwa wameduwazwa, wakazamishwa ndani ya chombo na kutimka.
Baada ya masaa matatu ..
Ngo ngo ngo ngo!
“Nakujaa!” Mama Brian akapayuka. Alikuwa jikoni akifuta vyombo alivyotoka kuviosha akiwa pamoja na Olivia. Kwa ishara ya kichwa, akamonyeshea Olivia njia na kumwambia, “nenda katazame ni nani.”
Olivia akaenda zake. Baada ya sekunde chache, akarudi na kumwambia mama, “Ni polisi.”
“Polisi?” Mama Brian akauliza kana kwamba hakusikia, Olivia akamjibu kwa kutikisa kichwa. Akajifuta maji akiwaza nini kitakuwa kimetokea. Taratibu akaenda sebuleni na uso kwa uso akakutana na Afisa Randall. Sura ya afisa huyo aliikumbuka vema.
“Karibu.”
“Ahsante.”
Mama Brian akaketi na kisha akamtazama afisa kwa macho ya maulizo. Kunani?
Baada ya maongezi mafupi, wakajikuta hapa …
“Walisema wanaenda kwenye kituo fulani cha habari kuonana na mmoja wa watangazaji,” Mama Brian akasema akiwa na taharuki usoni mwake. Afisa Randall akamuuliza, “Mtangazaji gani na kwasababu gani?”
Mama Brian akaeleza sababu aijuayo yeye ya kwamba walihitaji maelezo zaidi juu ya yule mtoto aliyepotea na kuonekana tena. Habari hizo zikamsisimua Afisa. “Wakakueleza nini juu ya hilo?” akauliza.
“Hamna kitu,” Mama Brian akajibu. “Tangu walipotoka hapa sijapata kuwaona mpaka sasa.”
Afisa akamtaka mwanamke huyo ajiandae waongozane wote kwenda kwenye kituo hicho cha habari ambapo ndipo alipodai Brian na Wisconsin walimuaga kuendea. Basi baada ya muda mfupi, Mama huyo akawa tayari kuongozana na afisa.
“Nakuja muda si mrefu, sawa?” akamwambia Olivia kisha akambusu kwenye paji lake la uso kumuaga.
**
“Unadhani tutafungwa?” akauliza Brian. Alikuwa amejikunyata ndani ya chumba cha mahabusu, pembeni yake akiwa amekalia Wisconsin. Ndani ya chumba hicho kulikuwa na watu wanne kwa idadi. Kila mmoja alionekana ana lake.
“Kama hawatatuamini, basi tutafungwa,” akasema Wisconsin. “Unajua Brian, kuna dunia za aina mbili, ule ambapo upo kitabuni na ule ambao upo fikirani. Ule ambao upo mwangani na ule wa gizani. Polisi na mahakama wanatambua ulimwengu mmoja tu, ule wa kitabuni, waasadiki wanachokiona na kukigusa.
Wapo kwenye mwanga, hivyo hawataki kuamini kama kuna giza. Lakini mwanga utakujaje pasipo ya giza? Ni giza ndiyo inafanya kuwapo kwa mwanga. Na mwanga ufanya kuwepo kwa giza.”
“Unajaribu kumaanisha nini?” Brian akauliza. Wisconsin akamtazama kijana huyo, kabla hajasema kitu, wakasikia sauti za vishindo, wakatazama nje ya mahabusu. Punde wakamwona polisi ambaye alifungua lango na kuwataka watoke na kuongozana naye.
**
Baada ya lisaa limoja na nusu.
Gari lilikuwa njiani kuelekea nyumbani, ndani yake alikuwapo Mama Brian, Wisconsin na Brian. Mama alikuwa ameshikilia usukani, Wisconsin akiwa ameketi kiti cha kando na dereva na Brian amekalia nyuma peke yake.
Ukimya haukudumu muda mrefu, Wisconsin akauliza, “Yule binti alisemaje kule polisi? Mbona imekuwa rahisi kututoa mule?”
Mama Brian akajibu akitazama mbele waelekeapo, “alisema yale yote ambayo yalimwondolea mashaka afisa Randall kuwa ninyi hamhusiki na yale mauaji.”
“Yapi hayo?” Wisconsin akaongezea swali.
“Ni hivi,” Mama Brian akaanza kueleza, “Tangu binti yule aliyekuwa amepotea kupatikana, mtangazaji yule alianza kumfuatilia akitaka taarifa zake. Alipompata na kukubali kufanya kipindi, akapokea vitisho toka kwa mtu asiyejulikana kwa njia za barua, na isitoshe mtu huyo akamwambia mpaka na muda ataokuja kumuua.
Akapuuzia na kuendelea na kazi yake, japo alifikisha mashtaka yake hayo kwa ofisi za uongozi. Ajabu ni kwamba, aliuawa kama ambavyo aliambiwa, muda na siku ileile.”
“Mmejuaje kama ni muda uleule?” Wisconsin akauliza.
“Kwa mujibu wa chunguzi za marehemu, mwili wake ulipoteza moto kwa makadirio ya masaa sita nyuma kabla ya kupambazuka.”
“Vipi kuhusu barua hizo?” akauliza Brian. “Wameshindwa kujua zilitumwa toka anwani gani?”
Mama akanyamaza kidogo na kisha akasema, “wamegundua zimetokea wapi. Japo mwandishi hakufahamika, ila mtindo wa bahasha ulionyesha zilipotokea.”
Wisconsin akauliza upesi, “Ni wapi huko?”
“Kanisani,” Mama akajibu.
“Kanisani?” wakaduwaa. Mama akatikisa kichwa na kusema. “Ndio, kanisani. Hata kwetu ilikuwa ngumu kuamini, ila ndivyo ushahidi ulivyokuwa unasema. Uzuri barua zote ambazo bwana yule mtangazaji alizopokea, alizikabidhi ofisini kwa hiyo yule dada aliziwasilisha na zote zikasomwa pale.”
“Sasa polisi wanafanyaje?” Brian akauliza.
“Wanalifuatlia hivi sasa,” Mama akajibu. “Kesho tutarudi tena kituoni nadhani tutakuwa tumepata majibu toka huko.”
**
“Ni afisa wa polisi,” alisema Dada Magdalena punde baada ya kuingia kwenye chumba cha padri Alfonso. Mwanaume huyo akakunja uso wake kuonyesha mashaka, alafu akasema, “mruhusu aingie.”
Kabla Dada Magdalena hajaenda, akamuuliza, “Una uhakika?”
“Usijali, hamna shida,” Padri akamtoa hofu. Basi Dada Magdalena akaenda zake na punde Afisa Randall akaingia na kuketi kitini. Mkononi mwake alikuwa na bahasha rangi ya kaki. Wakasalimiana na Padri na kueleza haja iliyomleta hapo.
“Samahani sana kwa ujio wangu wa ghafla,” akasema huku akifungua bahasha alokuja nayo. “Nimelazimika kuja hapa kwa mara nyingine kwasababu zisizozuilika.” akatoa barua zile mfukoni mwa bahasha alafu akaziweka mezani na kumtazama Padri Alfonso usoni. Akamuuliza, “Unazijua hizo barua?”
Padri Alfonso akaziteka kwa mkono wake na kuzikagua. Hakuwa na miwani. Akafungua droo na kuitoa, akaivesha usoni na kuendelea kukagua. Muda kidogo akabinua mdomo wake na kumtazama afisa Randall, “hapana, sizitambui,” akajibu na kuuliza, “Ni wapi umezitoa?”
“Kabla hujaanza kuniuliza, inabidi umalize maswali yangu kwanza,” Afisa akamtanabaisha na kisha akamuuliza, “Umeona chapa kwenye kona ya bahasha?”
“Ndio nimeona la–”
“Ni ya nani?” Afisa akamkatisha kidoomo. Alikuwa anamtazama machoni asitake kupoteza hata sekunde moja mbali.
“Ni-ni ya kanisa,” akasema Padri Alfonso, “Ila si–”
“Imefikaje hapo kwenye bahasha?”
“Sitambui!” Padri Alfonso akatahamaki. “Kama ilivyo kwako, nami sitambui!”
Afisa Randall akamtazama kwa sekunde chache kisha akamtaka awasilishe bahasha za kanisa zilizopo ofisini. Padri Alfonso akatii amri. Akanyanyuka na kuendea kabati kisha akatoa ‘package’ ya bahasha mpya na kumpatia Afisa. Afisa akasema,
“Nahitaji pia na zile ambazo zimeshatumika.”
Kidogo Padri Alfonso akasita, ila hakuwa na budi kutoa. Akainamisha mgongo wake na kumpatia kifurushi hicho Afisa.
Kwa muda kidogo afisa Randall akakagua hivyo vifurushi alafu akamwambia Padri Alfonso, “Bila shaka huwa unatunza kumbukumbu ya barua zako.”
“Ndio,” Padri akajibu akitikisa kichwa. “Huwa nafanya hivyo.”
Afisa akamwambia, “naomba na hizo rekodi kama hutojali.” hapa Padri Alfonso akasita tena. Wakatazamana na Afisa kwa sekunde mbili kabla hajafungua droo ya mezani na kumtolea rekodi za barua. Afisa akaendelea kukagua.
Akatumia kama dakika tano, kisha akaweka vitu kando na kumuuliza Padri Alfonso, “Kuna barua ambayo huwa unaandika na kutuma pasipo kuweka rekodi?”
Padri akatikisa kichwa. “Hapana, ni kinyume na utaratibu wa matumizi ya mali za kanisa.”
“Vema,” Afisa akatikisa kichwa na kuuliza tena, “Kuna mtu yeyote ambaye huandika barua mbali na wewe?”
“Ndio,” akajibu Padri. “Ila afanyavy hivyo basi lazima niwe na taarifa kama kiongozi.”
“Na rekodi hutunzwa?”
“Ndio. Ni lazima itunzwe.”
“Vema. Sasa mbona kuna barua tatu ambazo zimetoka pasipo rekodi?” Afisa akauliza akimkazia macho Padri Alfonso. Padri akawaka, “Barua gani hizo?”
Ndipo Afisa Randall akamwambia kwa mujibu wa kifurushi kipya cha bahasha, huwa ndani kunakuwa na bahasha sitini kwa mkupuo, lakini kifurushi kile ambacho kimetumika, kwa mahesabu, bahasha ishirini na tatu zimeshatoka, ila kwenye rekodi, ni bahasha ishirini na tatu tu ndizo zenye maelezo ya kubeba na kutuma barua. Sasa swali likaja,
“Hizo bahasha tatu zimeenda wapi?” afisa Randall akauliza, Padri Alfonso akakosa cha kujibu. Akadaka vile vifurushi vya bahasha pamoja pia na rekodi zake akaanza kuvikagua upya kuhakikisha kile ambacho afisa Randall amekisema.
Afisa akampatia muda huo. Akahangaika kwa takribani dakika kumi, hamna cha tofauti. Bahasha tatu hazikujulikana zimeenda wapi. Jasho likamtoka.
“Afisa, huenda kuna mtu ambaye atakuwa ametumia bahasha hizo,” akajitetea.
“Ila ulisema lazima kuwe na rekodi,” Afisa akamkumbushia na kisha kuongezea, “Na kama kulitokea tukio la wizi basi ungekuwa umetoa taarifa polisi tukalifahamu.”
Padri akakosa la kusema. Akatoa leso yake na kujifuta jasho. Afisa akamtazama na kumwambia, “Naomba kukagua eneo.”
“Eneo gani, afisa?”
“Ulalapo, kanisani … na pia kule korongoni.”
“Korongoni? … si mlishapakagua?”
“Nitakapakagua tena leo hii.”
“Sawa,” akasema Padri Alfonso na kisha akamwita Dada Magdalena. “Utaongozana na afisa hapa kwenye ukaguzi” akaagiza, ila Afisa akapinga na kusema, “Tutakuwa wote. Naomba tuongozane pamoja, giza linakaribia.” Padri Alfonso akatazama na Dada Magdalena pasipo kusema jambo.
Majira yalikuwa ni ya saa kumi na moja. Jua lilianza kusinyaa na kupoteza nguvu yake. Ndege waoga walishaanza kurejesha mbawa zao kwenye viota.
Basi Padri Alfonso, kwa kufuata maagizo, akaambatana na Afisa kwenda kanisani. Wakakagua na kuona kila kitu ni chema. Baada ya hapo, wakaenda chumbani mwa Padri Alfonso, napo wakakagua na kuona kila kitu ni chema. Sasa kukawa kumebakia kule korongoni.
“Kutakuwa na giza sasa, utaona kweli?” Padri Alfonso akauliza. “Nimekuja na kurunzi, usijali.” Afisa Randall akamjibu na kisha wakaeleka kwenye gari alilokuja nalo, huko wakamkuta afisa mwingine wa polisi, kwa jina Williamson, akampatia Afisa Randall kurunzi kubwa na kumuuliza, “Vipi twende wote?”
“Hapana, sitachukua muda mrefu,” Afisa Randall akajibu alafu akiongozana na Padri wakaelekea na kuzama korongoni. Kiza kilikuwa kimeshaanza kujijenga humo kutokana na uwingi wa miti. Afisa Randall akatazama huku na huko akirusha kurunzi.
Wakatembea kwa takribani dakika sita, wakawa wamezama kabisa kwenye moyo wa korongo. Hakukuwa na kitu ambacho Afisa Randall alikiona. Akasema, “Turudi.”
Wakiwa wanarudi, baada ya kutembea kwa dakika moja na nusu, afisa akamulika kitu fulani kwenye kingo ya korongo. Kitu hicho kilikuwa kinang’aa mithili ya kioo. Akakisogelea kwa ukaribu akitazame.
Akagundua ni bangili. Akafukuafukua kwa kutumia mkono wake, akaja kugundua bangili hiyo ilikuwa pamoja na kiatu kidogo cha kike. Akapata hamu ya kufukua zaidi. Akatumia mkono wake, kwakuwa udongo ulikuwa mlaini basi haikuwa tabu.
Akafukua zaidi na zaidi, mwishowe akakutana na mkono wa mtoto mdogo. Akastaajabu. Akamtazamia Padri na kumtaka watoke korongoni humo.
“Sihusiki na hicho kitu!” Padri akajitetea wakiwa wanatembea kutoka korongoni. “Sitambui kimefikaje huko. Kanisa halihusiki!”
Afisa hakusikiliza, akaendelea kutembea zake. Walipofika kwenye gari, akaudumbukiza mkono ule kwenye mfuko mwepesi wa nailoni na kuuhifadhi. Kisha akamwambia Padri Alfonso, “Nakuhitaji kesho asubuhi na mapema kituoni.” kisha wakawasha gari na kwenda zao.
Padri Alfonso akang’ata meno yake akitazama gari hilo likiishia. Muda si mrefu Dada Magdalena akaungana naye kutazama mapolisi hao wakiyoyoma, akauliza, “Sasa tunafanyaje?”
Padri Alfonso akawa kimya. Akavuta na kushusha pumzi ndefu pasipo kutia neno. Dada Magdalena akamuliza, “Kwanini haukummalizia kulekule korongoni?”
Padri akamtazama na kumrudishia swali, “huoni ingekuwa hatari? … kummalizia kule korongoni kungetuweka wazi kuwa sisi ndiyo tumemuua polisi.”
“Sasa tunafanyaje na ameondoka na vitu vile?” Dada Magdalena akauliza akiwa na shaka. Padri Alfonso akatabasamu, “tunafanyaje? Yani unauliza tunafanyaje? Kwani hujui huwa tunafanyaje?”
Dada Magdalena naye akatabasamu.
Hawakutia tena neno lingine.
Basi afisa Randall akaenda kuonana na familia ya wakina Brian na kuwapa mrejesho wa kilichotokea, nao akawaambia wafike kituo cha polisi kesho asubuhi na mapema, alafu akaenda zake kupumzika.
Afisa Williamson alimshushia nyumbani na kutokomea kwenda kulaza usafiri wa polisi. Randall alikuwa amechoka sana kutokana na kazi za siku nzima. Baada ya kuingia nyumbani kwake, akala na kutulia kidogo sebuleni pamoja na mkewe, alafu muda si mrefu akaenda kupumzika kwa kujimwaga kitandani.
Hata hakuoga. Na muda si muda, akasombwa na usingizi kwa mkupuo. Hakusikia hata mkewe alipozima kila kitu na kuja kulala. Alikuwa usingizini haswa akikoroma na kuachama kinywa.
Kwa mujibu wa saa yake ya sebuleni, mshale ukasonga na kujongea kwenye kituo cha nane usiku. Ulipofika hapo, Afisa Randall akajikuta anaamka toka usingizini asijue nini kimemwamsha kwani bado alikuwa na usingizi mzito.
Akatazama kushoto kwake, akamwona mkewe akiwa amejilalia. Taa ilikuwa imezimwa na hali ilikuwa imetulia tuli kabisa. Hakusikia sauti ya kingine chochote kile zaidi ya pumzi ya mkewe ambaye aliyekuwa anahema kwa uzito.
Akarudisha kichwa chake kitandani na kufumba macho aendelee kulala, usingizi haukuja. Akajitahidi kuyafumba macho kwanguvu, lakini bado hakukuwa na kitu. Macho yaligoma kudaka usingizi abadani,
Muda si mrefu, akasikia harufu fulani ambayo ilimfanya afungue macho na kutazamatazama chumbani. Ni kama kitu kinaungua ila kinanukia. Akanusanusa kama paka jikoni apate kutambua kitu hicho ni nini lakini hakufanikiwa.
Na kadiri muda ulivyokuwa unasonga, akajikuta anahisi harufu hiyo zaidi na zaidi. Akamuita mkewe, “Hey, hey.” akimsukuma bega kistaarabu, ndo’ kwanza mwanamke akageukia kando na kuendelea kulala.
Akataka kuendelea kumwamsha ila akasita. Acha apumzike, akajisemea, kisha akaweka shuka kando na kushuka toka kitandani. Akasikia dirisha linatetemeka, haraka akatazama. Ulikuwa ni upepo. Akapuuzia na kuuendea mlango, akafungua na kutoka chumbani.
Ila punde akarejea na kutwaa bunduki yake kwa dharura ya kiusalama. Akaikoki vema, ndaniye kulikuwa na risasi tatu. Zinatosha kabisa. Akaanza kufuata harufu kwa kudaka korido aende sebuleni na kisha jikoni.
Alipofika sebuleni, akawasha taa. Akatazama kwa kurusha macho yake huku na huko, hakuona jambo. Basi akaelekea kule jikoni. Napo akawasha taa. Akakaguakagua, hakukuwa na kitu. Sasa harufu inatoka wapi?
Dirisha la jikoni likatetemeka, akarusha macho yake kutazama. Ulikuwa ni upepo. Pazia lilichezacheza na mwishowe upepo ulipopita, likatulia. Afisa Randall akafungua droo zote za jikoni na kutazama ndani kama kuna kitu kimeoza, hakuona kitu. Hapo ndipo pua yake ikamwambia harufu ilikuwa inatokea nje.
Akahisi na kuamini kabisa itakuwa inatokea nje. Basi akaona asijisumbue kwenda huko. Kama haipo ndani, basi hana haja ya kujisumbua. Ila kabla hajajirudisha chumbani, akaona haitachukua nguvu sana kutazama nje kwa kupitia dirisha. Huenda akaona wapi harufu inatokea.
Alipotupa macho yake, upande wa mashariki mwa jiko, bustanini, akaona mbwa wawili wakiwa wakiwa wanatafuna. Kwakuwa alikuwa mbali, hakuona mbwa hao wanatafuna nini, ila walichokuwa wanakula kilikuwa kinatoka kwenye mfuko wa nailoni. Si kwamba aliuuona, bali alisikia sauti yake.
Akatazama kwa umakini aone ni nini kile ambacho mbwa hula, hakuweza kuona. Akajiuliza na kustaajabu, ni hicho ndicho hutoa harufu aliyoisikia mpaka kule chumbani?
Dirisha la sebuleni likatikisika. Akatupa macho yake upesi kutazama, hakuona kitu. Ulikuwa ni upepo. Pazia lilicheza na kisha kutulia. Aliporudisha macho yake kule nje, hakuona tena wale mbwa! Wameenda wapi? Akarusha macho yake kutazama na kuwatafuta, hakuwaona.
Akiwa hapo anabung’aa, akasikia sauti za mbwa hao wakiwa wananguruma na kugombana. Walibweka na kunguruma kwa fujo kana kwamba wanagombea kitu, sauti zao zikawa kero na bughudha.
Afisa Randall alipotaka kuachana nazo, zikaendelea pasipo kukoma. Hapo akaona hana budi kuwafukuza mbwa hao kabla watoto wake hawajaamka. Akafungua mlango, akiwa ameshikilia bunduki yake vema mkono wa kuume, akatoka na kurusha macho yake kuwatafuta wale mbwa.
Hakuwaona. Akasonga hatua nane mbele na kisha akatazama tena, hakuwaona! Sasa kulikuwa kimya, ni sauti ya upepo tu wa taratibu ndiyo ambao ulikuwa unasikika.
Wale mbwa wameenda wapi?
Basi kwakuwa aliwakosa na tayari ameshatoka nje, akaona ni kheri akatazame pale bustanini kuona kitu gani ambacho wale mbwa walikuwa wanakula.
Akasonga na kutazama, hakukuta kitu. Ule mfuko haukuwepo, na mbali na hilo, hata alama za miguu ya mbwa, haikuwapo ardhini! Akiwa hapo, bado anaperuzi, kwa nyuma yake mlango aliotokea ukarudi taratibu na kujifunga iiiiiiiiiiiipp .. kisha, tas-tas! Sauti ya komeo ikaita na kumshtua!
Haraka akatoka pale alipo na kukimbilia mlangoni, akagonga na kusema, “Hey, nipo nje! Hey nipo nje!” mlango haukufunguka. Akagonga tena na tena akiita, mlango haukufunguliwa. Akajaribu kuuvuta pasipo mafanikio, mlango ulikuwa umefungwa!
Mlango huu wa jikoni ulikuwa umesanifiwa kwa chuma kizito na kioo kigumu kinachohakisi ndani kwa uhafifu. Na kwakuwa jikoni taa ilikuwa inawaka, kioo hiki kilionekana cheupe kana kwamba mwezi angani.
Basi Afisa alipoona juhudi zake za kugonga mlango hazikuzaa matunda, akatengeneza mduara kiooni kwa kutumia bapa za viganja vyake ili apate kutazama ndani kama kuna mtu ama mlango umejifungwa kwa makosa.
Alipofanya hivyo, akaona kuna mtu ndani, lakini hakuweza kumtambua mtu huyo kwani kioo kile cha mlango hakikuwa chepesi kuonyesha hivyo mtu huyo alikuwa anaonekana kana kwamba kivuli tu.
Randall akabamiza tena mlango na kuita. Akastaajabu, mbona mtu yule hakuwa anamfungulia? Hapa akapata shaka. Huenda ni jambazi! Basi haraka akatoka hapo mlangoni na kwenda kwenye madirisha ya sebuleni, akatupa macho yake ndani.
Hakumwona mtu. Ila kabla hajatoka hapo akiwa amelenga kwenda kwenye mlango wa sebule kujaribu kufungua, akaona kitu fulani koridoni. Kilikuwa ni kitu cheusi kirefu chenye umbo la binadamu, ila hakina sura. Afisa akadhani ni macho yake. Punde taa ya sebuleni ikazima!
Akashtuka.
Ikabakia taa moja tu ya kule jikoni ambayo mwanga wake ukawa unajimwayamwaya kwa uhafifu mpaka huku sebuleni. Hapo ndipo Afisa Randall akaona kile kitu ambacho kipo koridoni, kikiwa na umbo kama la binadamu, kikiwa kinawaka macho mithili ya paka. Moyo wake ukapata mshtuko sana. Akakodoa na kuachama akiwa haelewi kile anachokiona. Alitamani awe ndotoni, ila hapana, ilikuwa ni uhalisia!
Kabla hajavuta hata pumzi tatu, katika ule mwanga ambao ulikuwa unatokea jikoni kufika sebuleni, akaona kivuli cha mtu. Alikuwa ni mwanamke amevalia gauni. Mwanamke huyo alikuwa anacheza mienendo ya bluzi akinyanyua pindo la gauni lake na kusonga kusonga kushoto, kulia.
Akayarudisha macho yake kule koridoni, ajabu hakumwona tena yule kiumbe aliyekuwa anawaka macho kama taa. Akiwa anaangaza ajue yupo wapi, akastaajabu ameshikwa bega na mkono wa baridi kana kwamba barafu. Alipotazama, uso kwa uso akakutana ni kiumbe yule mwenye macho ya taa. Kiumbe mweusi na mrefu!
Akahisi moyo wake umeongeza makasia. Akapatwa na baridi kavu mwilini wake. Alijawa na kihoro haswa, upesi akanyanyua bunduki yake na kutupa risasi zote tatu kwa mkupuo, mara kiumbe yule akapotea!
Afisa akiwa amekodoa, anahema kama aliyekimbizwa, punde kidogo akaguswa tena begani na mkono wa baridi zaidi. Alipogeuka kutazama, akakutana na mwanamke aliyevalia gauni jeusi. Alikuwa amefunga kiremba kichwani kilichoziba mpaka uso wake.
Afisa akajaribu tena kufyatua risasi, hazikuwapo, ziliisha. Basi akawehuka na kuanza kukimbia akipiga makelele kuomba msaada.
**
Saa tatu asubuhi …
Kulikuwa na magari matatu ya polisi na nyumba ya afisa Randall ilikuwa imezungushiwa utepe wa rangi ya manjano na nyeusi kukataza watu wasiohusika kukatiza hapo.
Mbali na hivyo, watu kadhaa, haswa majirani, walikuwa wametoka nje ya makazi yao wakitazama eneo la tukio kwa macho ya maulizo na nyuso za mashaka. Kulikuwa na zogo fulani midomoni mwao.
Muda si mrefu gari ya wagonjwa ikawasili eneoni na kujitengenezea vema. Kutoka ndani ya nyumba, ikatolewa miili mitatu ambayo imefunikwa gubigubi, ikatiwa ndani ya gari la wagonjwa na kisha gari hilo kutimka.
Baadae ikaja kuwekwa bayana ya kuwa afisa Randall alikuwa amefariki, pia mke na mtoto wake mdogo aitwae Bestie. Na kama haitoshi, baadae taarifa zaidi zikaja juu ya kifo cha afisa Williamson. Alikutwa amekakamaa ndani ya chumba chake mwili wake ukiwa mweusi kabisa kana kwamba mtu aliyekitwa na shoti kubwa ya umeme.
Vifo vikawekwa bayana kwenye vyombo vya habari na karibia Boston nzima ikajuzwa. Misiba miwili iliyotokea ndani ya usiku mmoja. Na yote ikiwa imefanana mtindo, yaani muuaji hakuwa anajulikana.
Ila hakuwa anajulikana kweli?
“Padri Alfonso atakuwa ameshamuua,” alisema Brian aliyekuwa ameketi nyuma ya gari hili liendalo. Kwa mbele alikuwa ameketi Wisconsin na Mama ambaye alikuwa ameshikilia usukani.
Katika majira haya ya asubuhi, walikuwa wanaelekea msibani. Msiba wa Brewster. Siku hiyo ndiyo ilikuwa siku ya mazishi yake kwa mujibu wa taarifa. Jana yake hawakupata muda wa kwenda msibani kutokana na kutingwa na shughuli zile za hapa na pale polisi.
“Mbaya zaidi amewaua wote,” akasema Mama. “Ameona awamalize kabisa kufuta ushahidi.”
Kidogo Wisconsin akasema, “ebu twendee kule kwenye kituo cha habari!” Mama akamtazama na kisha akarejesha uso wake haraka barabarani akiuliza, “kufanya nini huko?”
“Nahisi yule dada atakuwa mashakani,” Wisconsin akaeleza. “Kama wale polisi wameuawa wote, basi huenda pia akamuwinda na yule mwanamke ammalize!”
Basi Mama akaongeza mwendokasi akielekezea chombo kule alipoambiwa, muda mchache, kama dakika kumi na tatu, wakawa wamewasili. Wakashuka na kwenda ndani ya ofisi. Pale kwenye ofisi ya mapokezi wakamkuta mwanamke mwingine mwembamba sana mwenye nywele nyingi nyeusi.
Wakamsalimu na kumweleza shida yao, “Tumemkuta Karen?” Mama Brian akauliza pasipo kuonyesha shaka usoni. Yule mwanamapokezi akawatazama kidogo alafu akatabasamu na kutikisa kichwa. “Hapana, hayupo!”
“Atakuja leo?”
“Yah! Atakuja. Ninyi ni wakina nani?”
“Wageni wake tu, tulikuwa na shida naye. Unaweza kuwasiliana naye kumwambia twamngoja?”
“Nishajaribu hilo, nimeongea naye mara moja, lakini baada ya muda sikumpata,” akasema yule dada na kuongezea, “Nimeshampigia mara tano, hajapokea. Mara ya mwisho simu yake haikupatikana kabisa!”
“Unajua unapokaa?” akauliza Mama Brian sasa akiwa ametoa macho.
Sehemu Ya 10
Gari lilipiga breki kali na kisha kukata kona kwa fujo. Mama Brian alikuwa amechanganyikiwa? Aliendesha gari upesi sana na hata wale abiria aliowabeba hawakumkataza wala kumwonya.
Aliyavuka magari mengine kwa haraka, akiwa anabadilisha gia na kukanyagia pedeli ya mafuta, akaadhibu barabara kwa ustadi. Akatembea mithili ya kishada. Uso wake ulikuwa umetambaliwa na mashaka na mikono yake ilikuwa imeshikilia usukani kwanguvu.
Kitu kimoja walichokiamini ni kuwa mwanamke huyo anaweza kuwa mzima, au basi kama sivyo, atakuwa yupo hatarini kwa muda huo, kwani kwa makadirio ya muda ambao aliongea na mwenzake, ilikuwa ni asubuhi hii hii, muda mchache nyuma.
Lakini kwanini hakuuawa usiku? Sababu wauaji walikuwa wakiwamaliza maafisa wa polisi kama ilivyoonyesha wa mwisho kuuawa, afisa Williamson, kwa mujibu wa makadirio ya maelezo ya daktari, alikata moto majira ya alfajiri.
Punde gari lilipokamta breki, likiwa limetumia dakika nane tu kufika hapo, Wisconsin na Brian wakawa wa kwanza kushuka, nyuma wakifuatiwa na Mama yao. Wakagonga mlango, ulipokawia kufunguliwa, Wisconsin akausukuma kwanguvu akitumia bega lake pana. Mlango ukafunguka wakazama ndani.
Kutazama sebuleni hakukuwa na mtu, ila punde kidogo, Karen akatokea akiwa amefungia taulo lake jeupe kifuani. Mwili wake ulikuwa umejawa na maji na macho yake yakiwa yamebebeba mashaka.
Mama Brian akatahamaki kumwona, akaita, “Karen!” na kisha akamkimbilia na kumjulia hali. Karen akasema yu sawa, hakukumbana na tatizo lolote. Ndipo Mama Brian na wenziwe wakaketi na kumweleza kwanini walikuwa wanahofia mpaka kukimbia kuja hapo.
“Kuwa makini sana,” Wisconsin akamhusia. “Huenda muuaji akakufuata na wewe pia.”
Karen, akiwa aliyejawa na woga na mkanganyiko, akatikisa kichwa chake kupokea taarifa hiyo. Akaenda ndani na kujivesha nguo kisha akawaomba wageni wake hao wa dharura wampeleke kazini kwani hana usafiri.
**
“Madam, tunaomba uegeshe upande wako wa kulia, huko kuna nafasi zaidi!” alisema mwanaume aliyevalia sare ya suti nyeusi na mikononi mwake akiwa amevalia glovu nyeupe. Alikuwa hapa maalum kwa ajili ya kazi ya kuwalekeza wageni, aidha wenye vyombo vya usafiri ama lah, waliofika hapa kwenye mazishi.
“Nashukuru.” Mama Brian akakunja kona kufuata maelekezo. Alipoegesha gari na kulizima, wakashuka na kuelekea kwenye viti kadhaa ambavyo viliwekwa kwenye uwanja wa makaburi. Wakaketi na kuchambua eneo.
Hapo kulikuwa na watu takribani thelathini na tatu na magari kumi. Jeneza la Brewster lilikuwa limeshawekwa karibu kabisa na shimo lake na mbele kabisa, kwenye mpangilio wa viti, walikuwa wameketi watu wa karibu wa Brewster, haswa wafanyakazi wenziwe kwani hakuwa na marafiki.
Miongoni mwao, Padri Alfonso na watumishi wawili wa kike waliovalia sare zao kama ilivyo ada wakati wowote.
“Brian,” Wisconsin akaita kwa kunong’oneza. “Hakikisha macho yako yanamtazama Padri Alfonso muda wote, sawa?” Kabla Brian hajajibu, Padri Alfonso akageuka na kuwatazama kwa kuwakazia macho, na kisha akarejesha uso wake mbele.
Brian akauliza, “Atakuwa amesikia?” Kabla Wisconsin hajajibu, wakamwona Padri Alfonso akitikisa kichwa. Wakashtuka na kutazamana kisha hawakuongea tena.
Basi tangu hapo, Brian akawa anamtazama Padri Alfonso kwa woga. Kweli hakubandua macho yake. Hata alipoyafumba, akayafumbua upesi na kuendelea kukodoa.
Muda kidogo Wisconsin akampatia kikaratasi kidogo chenye ujumbe. Akaikichukua na kukisoma.
“Tutawasiliana kwa maandishi,” ujumbe ulisomeka vivyo. Akamtazama Wisconsin na kumtikisia kichwa kama ishara. Wisconsin akamwandikia pia Mama ujumbe kuwa watakuwa wanasiliana kwa maandishi, naye Mama akaelewa.
Muda ukasonga zaidi. Ilipopita lisaa limoja, shughuli za mazishi zikaanza rasmi baada ya ujio wa mwakilishi mkubwa wa serikali. Jeneza likafunguliwa, na watu wakaanza zoezi la kumuaga Brewster kwa mara ya mwisho kabla hajamezwa na udongo.
‘Utaenda kuaga?’ Wisconsin akaandika ujumbe wake kwa peni na kumpatia Brian.
‘Hapana, sitaenda,’ Brian akajibu na kurejesha karatasi.
‘Kwanini?’
‘Naogopa.’
‘Umekuwa ukimtazama Padri Alfonso?’
Kabla Brian hajaandika kujibu, akarusha tena macho yake kumtafuta Padri Alfonso. Hakumwona. Akaangaza kushoto na kulia, hakumwona. Akastaajabu atakuwa ameenda wapi, mara yake ya mwisho kumwona alikuwa amesimama kandokando na jeneza.
Alipomkosa, akarejesha macho yake kwenye karatasi apate kumwandikia Wisconsin ujumbe. Ajabu alipotazama karatasi hiyo, akaikuta tayari ina maandishi. Haukuwa mwandiko wa Wisconsin!
‘Unanitafuta?’ Maandishi yalisomeka hivyo. Brian akahofia sana. Akarusha tena macho yake kuangaza, hakuona kitu. Aliporejesha tena macho yake kwenye karatasi akaukuta ujumbe mwingine, ‘Nipo nyumbani kwenu.’
Hapa sasa ndiyo akatamani kupiga kelele. Haraka akamrejeshea Wisconsin kile kikaratasi kisha akamshtua Mama yake kumtaka waende nyumbani haraka iwezekanavyo!
“Yupo nyumbani!” Brian alisema akiwa amekunja ndita, macho yamejawa na woga. Nyumbani alikuwa amebakia Olivia pekee.
Basi wakatoka upesi na kwenda kwenye gari. Mama akatia ufunguo na kuwasha chombo, ila kabla hawajaondoka, akamwona Padri Alfonso kwa mbali akiwa amesimama na watu watatu wanateta!
Akauliza akistaajabu, “si yule?” wote wakatazama. Kweli alikuwa ndiye. Wakiwa kwenye buwazo hilo, Padri Alfonso akawapatia mkono watu wawili aliokuwa amesimama nao, kisha akaanza kutembea kulifuata gari walilopo wakina Brian.
“Mama, twende!” Brian akasema akimpigapiga mama yake begani, lakini Wisconsin akasema, “Hapana.” wote wakamtazama kwa nyuso za kushangaa.
“Ngoja tuone atafanya nini mbele za watu!”
Basi punde Padri Alfonso akawafikia na kutabasamu. Akawasalimu na kuwakaribisha kwa ukarimu.
“Kuna tatizo lolote?” akauliza.
Mama Brian akawahi kutikisa kichwa na kusema, “Hamna!”
“Una uhakika?” Padri Alfonso akauliza.
“Ndio, hamna!” Mama akasihi. “Nashukuru, padri.”
Padri akamtazama na kumuuliza kwa mara nyingine, “Una uhakika?” sasa hivi macho yake alikuwa ameyakodoa. Mama Brian akasihi baridi na moyo wake waenda mbio.
Ghafla Padri akatabasamu na kusema, “Msijali.” kisha akaenda zake.
Wakamtazama Padri akiishia na kisha Mama akaondoa chombo hapo msibani kurudi zao nyumbani. Walipomfika wakamkuta Olivia akiwa ameketi sebuleni anatazama runinga akila.
“Uko sawa, Olivia?” Mama akauliza. Olivia akatikisa kichwa chake na kumjibu kiufupi, “Ndio.” kisha akaendelea kutazama runinga kana kwamba hamna mtu.
Baadae , baada ya kupumzika, ikiwa ni majirani ya jioni, Wisconsin akamwita Brian na kumtaka watoke kidogo kwani ana maongezi naye. Wakitumia usafiri wa Mama, wakaenda kwenye moja ya bustani inayopatikana katikati mwa mji wa Boston, hapo wakatulia kwenye mojawapo ya viti vinavyopatikana kwenye maeneo hayo, alafu Wisconsin akasema,
“Niambie machache unayoyajua kuhusu Hamill, Dkt. Hamill.”
Brian akamtazama kwanza Wisconsin kabla hajasema jambo. Kwa kiasi fulani alikuwa ameshangazwa na hilo swali. Aliwatazama watoto waliokuwa wanacheza bustanini alafu baada ya muda kidogo, akasema, “Sina mengi ya kusema juu yake. Alikuwa ni mmoja wa watu wazuri ninaowajua, mwenye upendo na haja ya kusaidia wengine. Japo maisha yake yaligubikwa na upweke.”
Wisconsin akaingiza mkono wake ndani ya mfuko wa koti, humo akatoa kiko chake na kibiriti, akawasha na kuanza kuvuta. Akavuta mapafu manne alafu akasema sasa kwa kinywa chake kikavu, “Hakuna kitu chochote alichowahi kukwambia juu ya familia yake?”
“Kidogo,” Brian akajibu. “Mke na watoto wake walifariki na kumwacha mkiwa.”
“Nini kiliwaua?” Wisconsin akauliza. “Alikwambia nini kimewaua?”
Brian akatikisa kichwa. “Hapana,” akasema. “Hakuwahi kunambia, ila …” Wisconsin akamtazama kwa jicho la udadisi. “Aliniachia nyaraka zake tatu nizipitie. Zilikuwa zinahusu maisha yake, lakini sikupata muda wa kuzimaliza kusoma.”
“Ziko wapi sasa?” Wisconsin akadadisi.
“Zilipeperushwa na upepo wa ajabu tukiwa safarini kuja kule kwako,” Brian akaeleza. Kidogo Wisconsin akatulia, akavuta tena kiko chake akiwaza alafu akamtazama Brian na kumwambia, “pengine ungesoma na kuzimaliza nyaraka hizo ungekuwa umebadilisha mawazo juu ya Dkt Hamill.”
Kauli hiyo ikamtia Brian hamasa ya kutaka kujua zaidi. “Kwanini unasema hivyo?” akauliza.
Wisconsin akakuna kidevu chake na kusema, “Dkt Hamill aliua familia yake. Kwa mkono wake, alimmaliza mkewe na watoto akitumia kisu kirefu chenye ncha kali.”
“Kwanini afanye hivyo?” Brian akastaajabu.
“Labda kabla hatujajua kwanini alifanya hivyo, inabidi kwanza ujue kuwa Dkt Hamill alikuwa na familia ya watoto watatu, wawili walikuwa wa kiume na mmoja akiwa wa kike. Alifanikiwa kuwapata watoto hao akiwa kwenye enzi za ujana wake.
Pengine aliwapenda sana, mimi na wewe hatufahamu maana hatukuwapo. Ila tulilo na uhakika nalo ni kuwa alikuja kuwaua pamoja pia na mkewe. Nililikuta hilo kwenye ‘diary’ yake.”
Wisconsin akazamisha mkono ndani ya koti lake na kutoa kijitabu kidogo chenye jalada gumu jeusi, akampatia Brian.
Brian akakikagua na huku Wisconsin akiendelea kunena. “Sijajua kwanini aliua familia yake, kutakuwa na sababu kubwa nadhani. Lakini kwenye karatasi ambayo alikuwa ameeleza ya kuwa amehusika na kuua familia yake, alikuwa ameweka hapo mkufu wenye kidani cha kito cha kijani, kito cha duara.”
Wisconsin akazamisha tena mkono wake ndani ya koti lake na kutoa mkufu huo. Akautazama kwa muda kidogo alafu akamkabidhi Brian.
“Shida si kwamba amewaua familia yake. Tunaweza tukapuuzia juu ya hilo, ila tatizo ni kwamba, makaburi ya wanawe sikuyaona isipokuwa lile la mkewe tu. Ukifungua kwenye diary yake, utaona ameelekeza juu ya wapi alipomzika mkewe, lakini kuwahusu watoto wake, hamna anayejua. Hajaeleza wapi walipo.”
“Unadhani watakuwa wapi?” Brian akauliza. Mkononi alikuwa amebebelea kijitabu na mkufu.
“Sijajua wapo wapi,” akajibu Wisconsin, “Ila nahisi watakuwa wazima.”
“Kwanini unahisi hivyo?” Brian akauliza. “Dkt Hamill ameandika hilo kwenye diary yake?”
“Hapana, hajaandika. Lakini pia hajaandika watoto hao wapo wapi. Kwanini amzike mkewe ndani ya eneo la nyumba, na watoto wasijulikane kawapeleka wapi?”
Brian hakuwa na majibu. Wisconsin akavuta kiko chake na kutia neno, “Ni ajabu, maana hata hilo amelifanya kuwa siri ndani ya siri. Siri ambayo hata yeye hakutaka kuiandika ikajulikana kwa watu.”
“Sasa tutafanyaje kujua hilo?” Brian akauliza.
“Hatuna namna, Brian!” Wisconsin akatikisa kichwa. “Kwa sasa tuna kazi nyingi za kufanya, visa huwa haviishi ndani ya mji. Nilitaka tu kukuweka bayana juu ya hilo ila hatutadiriki kuhangaika nalo. Tumalize kwanza hili kumi lilipo mikononi mwetu.”
Basi baada ya maongezi hayo, Wisconsin akabadili mada na kumwambia Brian ya kwamba tangu Brewster alipofariki, hakuna mtoto yeyote aliyepotea ndani ya mji wa Boston. Hiyo ni ishara kuwa Helo atakuwa amedhoofu kwa mtu huyo kufa. Na endapo watafanikiwa kummaliza na Padri Alfonso, basi kazi itakuwa imekwisha. Atakachokifanya, yeye Brian, ni kwenda kule kwenye ulimwengu wa wafu, akamkabili na kummaliza Helo.
“Lakini tutammalizaje Alfonso?” Brian akauliza. “Anaonekana ni mwenye nguvu, pengine kumzidi Brewster!”
“Ni kweli,” akajibu Wisconsin, “lakini lazima kutakuwa na njia. Mpaka kufikia kesho nitakuwa nimejua cha kufanya. Twende sasa, tumekaa sana hapa.”
**
“Afadhali mmekuja!” Alisema Mama akiwa amekodoa macho. Akawafungulia mlango Wisconsin na Brian kuingia ndani. Wakamwona Karen, dada wa mapokezi, akiwa amejaa kwenye kiti cha pekee, uso wake umeshikwa na wasiwasi.
“Karen amefika hapa muda si mrefu,” Mama akasema kwa pupa, “ameniletea ujumbe mzito sana. Naomba mumsikize.”
Baada ya kusema hivyo, Karen akaanza kujieleza na hakuchukua muda mrefu macho yake yakaanza kumimina machozi. Sauti yake ilikuwa nyembamba inayotetemeka.
“ … amekuja kunifuata. Nimekuta jumbe zake kwenye dawati la kazini akiniambia ni mimi ndiye nitafuata kufa.” Karen akiwa anatumia mkono wake unaotetemeka, akawapatia Brian na Wisconsin karatasi mbili. Wakazisoma na zote zikiwa na jumbe moja, “ NI WEWE NDIYE UTAFUATA.” karatasi zote zikiwa zimefanana na zile zile ambazo yule mtangazaji wa awali alikuwa anazipata.
Lakini,
“Msichana yule aliyefanyiwa mahojiano, yupo wapi?” Wisconsin akauliza maana walikuwa wametingwa sana na hoja za yule mtangazaji na yale yanayotokea mpaka kusahau kabisa kuwa kuna yule binti ambaye naye anaweza kuwa muhimu kwao.
“Sijui,” Karen akajibu. “Mimi ni mdada wa mapokezi tu, siyajui mengi kuhusu mengine.”
“Umewaambia utawala juu ya tishio lako? Umewataarifu polisi?” Wisconsin akaongezea swali.
“Sijamtaarifu yeyote yule,” Karen akajibu. “Hamna atakayeniamini. Najua, hamna atayesadiki maneno yangu. Ni nyie tu!”
Wisconsin akamtazama Mama Brian. Hawakutia neno. Basi Karen akakaribishwa kwenye nyumba ile kulala mpaka hapo atakapohisi kuwa yu salama. Lakini je hilo litamwokoa dhidi ya ahadi ya muuaji?
Mshale wa saa ulipokomea kwenye majira ya saa nane usiku, Brian aligutuka toka usingizi. Hakujua ni nini kilimwamsha, ila alijikuta akihisi upepo wa baridi. Kando yake alikuwa amelala Wisconsin ambaye alimpisha Karen alale kwenye chumba chake.
Brian akaangaza kushoto na kulia, kisha akaamka na kusimamia miguu yake. Akajongea dirisha na kutazama nje. Kulikuwa kimya, kumetulia haswa. Akiwa hapo, akasikia mlango unafunguliwa. Haraka akageuka na kutazama mlango wa chumba chao. Haukuwa huo!
Akasonga na kufungua mlango na kuchungulia kwenye korido kuona ni mlango gani utakuwa umefunguliwa. Macho yakiwa sahihi, akaona mlango wa chumba kile alichokuwa amelala Karen ndicho kipo wazi. Akajawa na shaka.
Akasonga hatua taratibutaratibu akisogelea hicho chumba. Alipofunga mlangoni, akarusha macho yake ndani. Kama macho yake yalikuwa sahihi, alimwona Olivia akiwa kandokando ya kitanda. Mkononi mwake alikuwa ameshikilia kisu kirefu.
Akajikuta akisema, “Olivia!” kwa kunong’oneza. Hamaki, Olivia akageuka na kumtazama. Macho yake yalikuwa yanang’aa kana kwamba taa.
Brian hajakaa sawa, Olivia akakimbia upesi na kumvamia mpaka chini. Binti huyo akawa anataka kumchoma kisu. Brian akapambana kwa kuudaka mkono wenye kisu akitumia nguvu zote asijeruhiwe.
Ajabu Olivia alikuwa ni mwenye nguvu sana, hata Brian hakuwa anaweza kufua dafu, ncha ya kisu ilikuwa inajongea taratibu kufuata kifua chake. Aling’ata meno akikazana kujitetea, alipoona juhudi zake zinaelekea ukingoni na huku akiwa anashindwa, akajikakamua kwa mwili wake wote kumtupia Olivia kando amweke chini, kisha akadaka mkono wa Olivia wenye kisu, akaubondea ukutani kwanguvu mara tatu , kisu kikadondoka chini!
“Nitakuua, Brian!” Olivia akang’aka. Sauti yake ilikuwa inatetemeka kana kwamba inatoka kwenye ‘tape recorder’. Macho yake yalikuwa mekundu na mdomo wake umekauka kuwa mweusi.
“Olivia, nini kimekutokea?” Brian akauliza. Alimtazama Olivia kwa huruma na mshangao. Katika namna ya ajabu akaanza kudhoofu. Kadiri alivyotazama macho ya Olivia akawa anajihisi kupoteza nguvu mwilini. Mwishowe Olivia akamtupia pembeni na kuteka tena kisu, akamfuata.
“Acha Olivia!” Brian akasihi. “Usifanye hivyo tafadhali!”
Olivia hakusikia, akaendelea kutembaa kumfuata. Brian akiwa chini, akawa anajivuta kusonga mbali na Olivia.
“Tafadhali, Olivia! Wewe ni msichana mzuri, usifanye hivyo,” Brian akaendelea kunena. Olivia asijali, akamsongea na kisha akainama kutaka kumchoma kisu Brian. Alikuwa na nguvu maradufu. Na ubaya ni kwamba Brian alikuwa anaishiwa na nguvu mwilini kila alipomtazama Olivia machoni.
Olivia akacheka. Ila punde akanyong’onyea, akapoteza nguvu zote na kufunga macho yake, alafu akadondokea chini. Brian hakuelewa nini kimetokea.
Alipotazama koridoni, akamwona Wisconsin akiwa amesimama. Mara upesi Wisconsin akamkimbilia na kumuuliza, “Brian, upo sawa?” kabla Brian hajajibu, akamtazama Olivia aliyekuwa pembeni. Alikuwa amelala kama mtu asiye na ufahamu.
“Nipo sawa,” akajibu, alafu akanyanyuka na kusimama. “Nini kimetokea?” Wisconsin akauliza.
**
“Alikuwa amebadilika,” alisema Brian aliyekuwa anatazama dari akiwa amejilaza kitandani. Pembeni yake alikuwa amelala Wisconsin naye akiwa anatazama dari huku akimsikiza Brian kwa umakini. Bado ni usiku, muda mchache baada ya Brian kutoka kupambana na Olivia.
“Macho yake yalikuwa yanawaka. Alikuwa ni mwenye nguvu ajabu. Sijui ni nini kilimtokea.”
Kukawa kimya kidogo kabla ya Wisconsin kuuliza, “Nini kilikuamsha, Brian?”
“Sifahamu,” Brian akajibu. “Nilijikuta nikiwa macho. Baada ya muda mfupi ndiyo nikasikia mlango ukifunguliwa. Nilipoenda kutazama, nikamkuta Olivia akiwa chumbani mwa Karen.”
Wisconsin akamtazama Brian na kumwambia, “Olivia atakuwa alitumwa kutekeleza ujumbe wa Padri Alfonso. Ametumia mwili wake kutekelezea kazi.”
Brian akauliza, “Vipi? Kutakuwa na matatizo juu ya hilo?”
“Sijajua,” Wisconsin akajibu kisha akakaa kimya kwa kama sekunde tatu, alafu akasema, “Sikujua kama kazi hii itakuwa kubwa kiasi hiki. Ni kazi pevu sana. Mategemeo yangu ya kuimaliza ndani ya siku tatu yameshindikana, na hata sasa sijui itakwisha lini. Inabidi nifanye namna Brian.”
“Namna ipi hiyo?” Brian akauliza. Naye akamtazama Wisconsin kwa macho ya udadisi.
Wisconsin akavuta pumzi ndefu alafu kisha akakaa kimya. Macho yake yalikuwa yanaonyesha yu mbali kimawazo.
**
“Amesema hatotaka mtu amsumbue, tumpe muda,” alisema Brian. Walikuwa wameketi mezani wakipata kifungua kinywa. Wote walikuwapo hapo isipokuwa Wisconsin pekee.
“Atakuwa humo mpaka muda gani?” Mama akauliza. Brian akapandisha mabega yake pasipo kusema jambo. Akamtazama Olivia, alafu akamuuliza, “Upo sawa, Olivia?”
Olivia akatikisa kichwa akitafuna. Brian akawaza yale yaliyotokea jana. Ilikuwa ni ajabu hakuna mwingine aliyekuwa anajua chochote isipokuwa Brian na Wisconsin pekee.
Alipomaliza kula, Brian akajiandaa na kwenda shule. Huko akakaa mpaka majira ya mchana wa saa nane ambapo kengele iligonga kuashiria muda umekwisha. Akiwa anatoka, mara akasikia sauti ya kike inamwita, alikuwa ni Wayde.
“Habari, Brian!”
“Njema. Unaendeleaje?”
“Kawaida. Vipi ulipata chochote kumhusu Silvia?”
Brian akatikisa kichwa.
“Brian!” Wayde akaita kisha akauliza, “unajua ni namna gani nilivyo mpweke, Brian? Nimekupoteza wewe, nimempoteza na Silvia, unadhani maisha yangu yapoje?” Wayde alizungumza akiwa na macho mekundu yanayokaribia kumwaga chozi. “Maisha yangu yamekuwa magumu sana, Brian. Nahisi kuchanganyikiwa. Tafadhali … kama kuna jambo naweza kufanya kujisaidia na maisha yangu, nieleze, Brian.”
Wayde akamkumbatia Brian kwanguvu kisha akalia. Brian akamsihi anyamaze na kisha akarejea naye darasani kuteta mambo kadhaa.
“Wayde, ni hatari sana. Mambo haya si kama vile ambavyo unaweza ukawa unawaza. Ni makubwa, na naweza kukushauri tuachane nayo kwa usalama wako, na familia yako.”
“Hapana, Brian!” Wayde akatikisa kichwa. “Nawezaje kuacha haya yapite? Unadhani sihisi kinachoendelea?”
“Unahisi nini, Wayde?” Brian akauliza akimtazama mlengwa. Mara Wayde akasimama na kumwambia, “Twende!”
Wakatoka nje ya darasa kwenda kulikuta gari la Wayde, wakajipaki na msichana huyo kutimka. Brian hakuwa anajua wapi wanaelekea, pia alikuwa na hofu ya kukutwa na baba yake Wayde ambaye ashampiga marufuku ya kuonana na binti yake.
“Wayde, naona hili litakuwa na hatari kwangu.”
“Usijali, baba yangu hayupo,” Wayde akamtoa hofu. Wakaenda na usafiri huo mpaka nyumbani kwa wakina Wayde, nyumba kubwa ya ghorofa mbili. Sakafu ya chini ilikuwa ni ya watoto, ya pili ya wazazi na ile ya tatu ikikaliwa na maktaba.
Wayde akampandisha Brian mpaka juu kabisa kwenye maktaba kisha akamwambia, “Keti hapa.” alafu yeye akarudi chini na muda si mrefu akarejea na funguo, akamwambia Brian, “Nifuate huku.”
Wakaendea chumba fulani ndani ya maktaba. “Chumba hiki ni siri kukiingia. Baba yangu amekuwa akizama humu mara kadhaa tu na kujifungia. Pale nilipopata muda wa kusoma baadhi ya vitabu ambavyo vipo katika maktaba nikaja gundua kuwa upotevu wa watoto ndani ya mji wa Boston ni kitu ambacho kilitarajiwa kwa maana ni adhabu anayotupatia bwana Helo.”
Wayde aliposema hayo, akamtazama Brian na kumuuliza, “Ninachokisema ni uongo?”
Brian akatikisa kichwa. “La hasha.”
“Lakini kwanini hukunambia Brian?” Wayde akauliza. “Ulikuwa unayajua yote hayo, sio?” Brian hakusema jambo. “Ulikuwa unayajua yote hayo na ukaamua kunificha, kwanini Brian?”
Wayde akafungua chumba wakazama ndani, humo kulikuwa na vitabu vingine vya ziada tofauti na vile ambavyo vipo kwenye ukumbi mwingine. Akampatia Brian baadhi ya vitabu na barua kadhaa takribani sita, kisha akamwambia, “visome, nawe uniambie ni nini umeona, Brian.”
Brian akachukua muda kuvipitia. Macho yake yalikuwa mepesi kwakuwa alikuwa mzoefu wa kupenda kusoma. Baada ya muda wa dakika arobaini na tano tu, akawa amaemaliza. Akamuuliza Wayde, “Ina maana baba yako ana mahusiano na seneta yule aliyemuua na kumchoma Helo?”
“Ndio,” Wayde akajibu. “Ni babu yake kabisa mzaa mama.”
“Ajabu!” Brian akatahamaki, kisha akauliza, “Kama ni hivyo, kwanini Helo hajamuua baba yako kulipiza kisasi kabla ya kuamua kuitesa Boston nzima?”
Wayde akanyamaza kidogo, alafu akashusha pumzi na kumuuliza Brian, “Nikikuonyesha kitu, je itakuwa siri baina yangu na wewe?”
“Ndio, naahidi hilo,” Brian akajibu. Basi Wayde akaingiza tena mkono wake mfukoni na kutoa ufunguo wa ziada. Ufunguo mdogo wa shaba. Akafungua mlango mwingine ndani ya chumba hicho cha siri, humo Brian akaona jambo lililomshangaza.
Maiti za watu watatu!
“Wayde, ni nini hicho?” Brian akastaajabu. Wayde akamjibu huku akimtazama, “ni watoto wa Helo!”
**
Brian aliyekuwa amepigwa na tahamaki, akajikaza kisabuni kutazama maiti zile. Hakuwa anazifahamu, na hapo ndipo akagundua ya kuwa, Brewster na Alfonso hawakuwa watoto wa Helo, kitu ambacho alikuwa anakiwaza muda wote huo.
“Nahisi hii ndiyo sababu familia yetu imekuwa salama dhidi ya Helo,” alisema Wayde huku akijongea zile maiti. Zilikuwa zimehifadhiwa kwenye kioo baada ya kukaushwa. Kama maiti hizi zingekuwa zimefungua macho basi ungeweza dhani bado ni watu waliohai.
Wayde akampatia Brian karatasi fulani na kumwambia, “Nadhani unatakiwa kuliona na hili.” Brian akaitazama karatasi aliyopewa. Ilikuwa ni barua ya kale ambayo baba yake Wayde alitumiwa na mwanamke aliyejitambulisha kwa jina la Magreth Woodland. Katika barua hiyo, huyo mwanamke alikuwa anamweleza baba yake Wayde, seneta wa Massachusetts, namna gani anavyompenda lakini pia akiwa hatarini kutokana na mapenzi yake kwake.
Ya kuwa mume wake anaonekana kuyajua mahusiano yao, amemuuliza mara kadhaa akakanusha, inawapasa wawe makini kuanzia muda huo kwa usalama wao kwani asingependa kumharibia picha ya kisiasa ya mwanaume huyo kwani ni mtu mkubwa kwenye siasa za Marekani. Kipindi hicho bado baba yake na Wayde hakuwa seneta, bali mwenye mipango ya kuwa.
Brian akamuuliza Wayde, “Magreth ni nani?” Kabla Wayde hajajibu, akampatia tena Brian barua ya pili, hii ilikuwa fupi tofati na ile ya kwanza, pia ilikuwa imetokea kwa Magreth Woodland akimshukuru baba yake Wayde kwa kumletea zawadi ya mkufu wa thamani.
Wayde akasema, “Nadhani unaweza ukawa unamjua mwanamke huyo.” Brian akatikisa kichwa. “Simfahamu. Wewe unamjua?”
Wayde akaendea kabati dogo lililokuwepo ndani ya chumba hicho akatoa picha aina ya ‘passport’ na kumkabidhi Brian.
“Bado haujamjua?” Wayde akauliza akimtazama Brian aliyekuwa anaikodolea macho picha ile. Punde akasema, “Hii sura si ngeni.”
“Umewahi kuiona wapi?” Wayde akauliza. Kidogo, Brian akapata kumbukumbu. “Niliiona kwenye ofisi ya mkuu wa – ni mke wa Dkt Hamill!”
Wayde akatikisa kichwa. “Ndio, ni yeye.”
“Baba yako alikuwa anatembea na mke wa Dkt Hamill?” Brian akauliza kana kwamba haamini alichopata kuelewa.
“Ndio,” Wayde akajibu. “Kipindi hiko kabla sijazaliwa, miaka mingi iliyopita.” Wayde akaketi kwenye kiti na kuendelea kusema, “Inaelekea baba alikuwa anampenda sana Magreth, hata leo hii hakutoa picha wala barua zake kwenye hifadhi. Najiuliza sana yu wapi huyu mwanamke?”
“Amekufa,” Brian akamjibu na kuongezea, “Dkt Hamill alimuua mkewe. Ameandika hivyo kwenye diary.”
“Kweli?” Wayde akatahamaki.
“Ndio,” Brian akajibu. “Nadhani ni kwasababu ya mahusiano ambayo Magreth alikuwa nayo na baba yako, na huo mkufu ambao Magreth anauongelea kutoka kwa baba yako, itakuwa ndiyo kitu kilichomfanya Dkt Hamill akahakiki mahusiano baina yao. Hata kwenye diary ya Dkt Hamill, mkufu huo ameuweka kwenye karatasi inayokiri kuwa amemuua kwa kumchoma kisu.”
Wayde akashangazwa sana na hizo habari, lakini Brian hakuwa amemaliza kueleza. Akasema pia kuwa Dkt Hamill aliua watoto wake watatu, wote kwa kuwachoma kisu. Hapa kila mmoja akawa na maswali. Hakuna aliyekuwa anajua kwanini Dkt Hamill alifanya tukio hilo la kinyama.
“Naomba niende, Wayde,” akasema Brian. “Tuonane kesho, nadhani nitakuwa na cha kukuambia zaidi.”
“Sawa, acha nikusindikize.” Wayde akafunga kila kitu na kutoka Brian mpaka kwenye usafiri wake, akampeleka kijana huyo nyumbani kwao.
**
“Una uhakika?” Wisconsin aliuliza akiwa anamtazama Brian kwa kukodoa.
“Ndio, kila kitu nimekiona na kuhakikisha,” Brian akajieleza. Wisconsin akatulia kidogo akiwaza. Akanyanyua kikombe cha chai na kunywa mafundo matatu kisha akasafisha koo lake.
“Kwanini Dkt Hamill aliwaua wanae?” Brian akauliza. Bado Wisconsin alikuwa amenyamaza kimya, anatazama huku na kule akiwaza. Baada ya sekunde kadhaa, akasema akinyanyuka, “Twende kwenye nyumba ya Dkt Hamill.”
**
Baada ya dakika kumi na mbili …
“Ndiyo hapa,” akasema Wisconsin. Walikuwa tayari wapo ndani ya nyumba ya marehemu Dkt Hamill upande wa nyuma. Hapo walikuwa wamesimama kwenye kaburi la Magreth Woodland, mke wa Dkt Hamill. Mikononi mwao walikuwa wamebebelea chepeo za chuma na mikono yao imefunikwa na glovu nyeusi.
Wakaanza kuchimba na kuchimba. Wakanyoosha migongo yao, wakakung’uta jasho, na kuendelea kuchimba. Haikuwa kazi nyepesi maana udongo ulikuwa mgumu wenye kujawa na kokoto. Waliweka vituo mara tatu kabla hawajafika chini kabisa. Ajabu hawakukuta kitu, si mabaki wala kitu chochote bali udongo mwekundu tu. Wisconsin akasema, “Dkt Hamill hakuwa amemzika mkewe ndani kama alivyoeleza kwenye diary.”
Brian akauliza, “Sasa atakuwa amemzika wapi?”
Wisconsin akanyamaza kidogo akiweka sawa mambo yake kichwani, alafu akasema, “Ndiyo maana Dkt Hamill aliwapoteza watoto wake, sasa napata maana.” Akamtazama Brian usoni na kusema, “Dkt Hamill atakuwa alienda kumtupia au kumfukia mkewe kule msituni. Na kwasababu hiyo basi, mkewe akaanza kutumika na Helo mpaka pale alipowatoa sadaka watoto wake watatu kumtumikia Helo.”
“Umeyajuaje hayo?” Brian akamuuliza.
“Ni Magreth pekee ndiye aliyeuawa,” Wisconsin akasema akitikisa kichwa. “Na ndiyo maana kaburi lake lipo, au ndiyo maana Dkt Hamill akadanganya kuwapo kwa kaburi lake. Ila kuhusu wanawe, hao hawajauawa, bali walipotea. Hakuna namna nyingine ya kumtuliza Helo isipokuwa kwa sadaka tu, naye Hello aliwatoa sadaka wanawe.”
“Ina maana Brewster na Alfonso si watoto wa Helo,” akasema Brian, “bali ni watoto wa Dkt Hamill?”
Wisconsin akatikisa kichwa. “Ndio. Ni watoto wa Dkt Hamill aliowatoa sadaka.”
“Mbona hawapo vivyo kwenye picha ya familia niliyoiona?” Brian akauliza.
“Brian,” Wisconsin akaita. “Unadhani baada ya Hamill kusema kuwa wanawe wamepotea, wangekuja kuonekana wakiwa na sura zilezile?”
Brian akashusha pumzi. Wisconsin akamsihi watoke ndani ya shimo waende zao nyumbani. Wakiwa njiani kuelekea huko, Brian akamuuliza Wisconsin, “Umepata kile kitu ulichokuwa unasema unakifanyia kazi?”
“Ndio,” akajibu Wisconsin. “Lakini nadhani tutafuata njia mbadala. Binti wa Seneta ammetupatia njia nzuri zaidi.”
“Ipi hiyo?” Brian akauliza. Wisconsin akasimama na kumtazama Brian kisha akamwambia,
“Tutatumia ile miili ya watoto wa Helo. Itatusaidia sana kumaliza kazi moja kwa moja. Mosi, kummaliza Helo, na vibaraka wake. Lakini pili, kuacha pia roho za hao watoto wa Helo nazo zikaenda zake.”
“Unadhani itawezekana?” Brian akauliza.
“Kwa asilimia zote, muhimu kupata tu msaada toka kwa Wayde juu ya miili ile.”
Baada ya maongezi hayo, wakaendelea na safari yao mpaka nyumbani. Hawakumwambia mtu kitu. Walijipumzisha wakiwa wamepanga kesho yake kufanya kila kitu, kuonana na Wayde na kufanya taratibu ya kuhodhi miili ile kwa matumizi.
Ukiwa ni usiku wa kuelekea saa nne, Brian akiwa ameketi sebuleni anatazama runinga, Olivia akamjongea na kumwambia, “Kuna kitu chako nimekiokota.” kisha akaingiza mkono kwenye gauni lake na kutoa mkufu ule wenye kito cha kijani.
“Umeitoa wapi?” Brian akahamaki.
“Nimeiokota,” Olivia akajibu. “Umeiokota wapi? Mbona nakumbuka niliiweka mahali salama?”
“Mimi nimeiokota chini ya kitanda chako,” Olivia akaeleza. Brian akateka mkufu ule na kuutazama akiukagua.
“Brian,” Olivia akaita. “Huo mkufu umeutoa wapi?”
Brian akatabasamu. Akauweka mkufu huo mfukoni mwake na kujibu, “Ni wangu. Kuna mtu tu amenipa.”
“Nani huyo?”
“Rafiki yangu.”
“We ni mwongo,” Olivia akasema akimtazama Brian machoni. Uso wake haukuonyesha masikhara hata kidogo. Brian kidogo akapata shaka.
“Unadhani ni wa nani?” Brian akauliza. Olivia hakumjibu, akabaki akimtazama kwa macho yake ya ukali. Brian akajitengenezea vema kwenye kiti na kuuliza, “Olivia, upo sawa?” Bado Olivia hakujibu, aliendelea kumtazama Brian akikaza macho.
“Olivia,” Brian akaita. “Olivia! … hey, msichana!” akamchezeachezea Olivia mashavu. Olivia asijibu lolote, akaachana na Brian na kuketi kitini akitazama runinga. Brian akabakia na maswali kichwani kwamba nini shida.
Akanyanyuka na kwenda chumbani kuuhifadhi mkufu ule mahali salama tena, alipoufungia na kupaficha, kisha akarudi sebuleni. Hakumkuta Olivia. Runinga ilikuwa inawaka yenyewe sebule ikiwa pweke.
Akatazama jikoni, hakukuwa na mtu. Akaketi na kutazama kidogo runinga kabla hajamezwa na mawazo lukuki aliyokuwa nayo kichwani. Aliwaza siku yake nzima, namna alivyokutana na Wayde na kuona vitu ambavyo hakuwa anavitarajia. Pia alivyoongozana na Wisconsin kwenda kule kwa Dkt Hamill kuchimba kaburi.
Alioona ilikuwa ni siku ndefu, ila zaidi ya hapo, ni siku muhimu sana kwenye zoezi lao la kuhitimisha yale yanayotukia pale Boston. Lakini kama kuna kitu kilimshangaza na kumtia huruma, ni yale mahusiano ya mke wa Dkt Hamill. Aliwaza ni namna gani Dkt Hamill alivyokuwa anajisikia mpaka kumuua mkewe. Hakika lilimuumiza sana. Alijikuta akitikisa kichwa chake na kusonya.
Muda ukazidi kwenda akiwa hapo. Ikiwa inaelekea kuwa majira ya saa saba usiku, akaona ni kheri akapumzike sasa kitandani kwakuwa kesho yampasa kuamka asubuhi na mapema.
Akazima kila kitu na kuendea chumba chake kujilaza. Ila hakuwa amechoka kabisa, alishangazwa kwanini. Bado alijihisi mwenye nguvu na macho yake ni makavu. Hakuwa anahisi usingizi hata kidogo. Alifumba macho yake akigeukia huku na huko lakini hakulala. Alibaki akimtazama Wisconsin akiwa amesombwa na usingizi, anaunguruma kwa utamu.
Akajigeuza kutazama dari, pia dirisha na mara mlangoni, bado usingizi haukuja. Nao muda ukaendelea kusonga mpaka kufikia saa tisa, kimya, alikuwa ameshageukia kila pande anayoijua, akaweka kila mtindo anaoujua, usingizi haukuja.
Akiwa sasa amechoka kujaribu, na anawaza aidha aamke na kutumikia udadisi wake kusoma kitabu cha Wisconsin, akasikia sauti ya kitu huko nje. Alihofia kwanza kisha alipotulia ndipo akajua ya kwamba ni sauti ya mlango. Hapa akili yake ikampeleka moja kwa moja kwenye tukio la usiku wa kuamkia jana. Ina maana lile jaribio la kuuawa kwa Karen litakuwa linajirudia?
Haraka akatoka kitandani na kuufuata mlango. Aakafungua taratibu na kuchungulia koridoni. Macho yake yakaona mlango wa chumba cha Olivia ukiwa wazi, kabla hajajiuliza, akaona tena mlango wa chumba alalacho Karen ukiwa unafunguka na kuwa wazi.
Akabaki akishangaa. Nani anafungua milango hiyo? Macho yalimtoka akiwa anatazama kwa umakini nini kinaelekea kutokea. Kukawa kimya. Hakuona kitu wala mtu. Zikapita kama sekunde sita.
Kidogo, milango ile iliyofunguka ikaanza kucheza, ikaenda mbele na kurudi nyuma. Ilianza kucheza taratibu lakini kadiri na muda ulivyokuwa unaenda kasi yake ikawa inaongezeka. Brian akashagaa ni nani anayeisukuma milango hiyo.
Kidogo tena, kule sebuleni mapazia ya dirishani yakaanza kupepea. Hakukuwa na upepo wowote ule. Lilikuwa ni jambo la kushangaza kwa Brian. Alikunja sura yake akijiuliza ni nini kinachotokea. Ghafla vitu vyote vikakoma ndani ya sekunde kana kwamba vimekatazwa mara moja! Brian akaendelea kushangaa.
Kwa macho yake akauona mkono wa mtoto ukichomoza toka mlangoni ukiwa umebebelea kisu. Ukatokea pia na mkono mwingine, wa pili, ambao ulinyooshea kidole kwenye mlango wa chumba cha Karen. Mara kidole hicho kikafanya ishara ya kukataza kwa kwenda kushoto na kulia alafu kikamnyookea Brian!
Brian akatahamaki. Kufumba na kufumbua, akatoka Olivia akiwa aonekana kama kivuli. Macho yake yalikuwa yanawaka kama gololi iliyomulikwa kurunzi. Mkono wake wa kuume ulikuwa umebebelea kisu na ule wa kushoto ukiwa mtupu.
Akamnyooshea kidole Brian, alafu akatikisa kichwa chake mara tatu kisha akaanza kusonga taratibu kumfuata kijana huyo. Brian akarejea upesi ndani ya chumba chake na kufunga mlango kwa komeo, alafu akatulia hapo kusikiza nini kitatukia.
Kukawa kimya. Hakusikia sauti ya kitu chochote isipokuwa moyo wake uliokuwa unapiga kwa kasi. Alimtazama Wisconcosin akamwona bado amelala, hana habari, akaona ni kheri akamwamsha na kumjuza yanayoendelea.
“Bwana Wisconsin!” Brian akaita. “Amka uone kinachojiri!”
Hola! Wisconsin alikuwa amelewa usingizi. Hakuwa anasikia lolote isipokuwa utamu wa usingizi. Brian akamsukuma na kumvutavuta. “Amka!” akapaza sauti. “Amka, Wisconsin!” Alistaajabu ni usingizi wa aina gani uliokumba bwana huyo. Hakuwa anasikia wala kuelewa.
Kidogo, Brian akaanza kusikia mlango ukigongwa – tih!-tih!-tih! – na sauti ya kike ikaimba kwa kutetema, “Brian, toka tucheze. Hakika utafurahi. Brian … Brian, toka tucheze.”
Brian akaendelea kumshtua Wisconsin pasipo mafanikio. Akatazama kushoto na kulia kwake kama atapata dhana ya kujitetea. Akanyanyuka na kufuata mahali aliporundika nguo zake, akafukua na kutoa gongo la bati, akalishika vema kujihami.
Kimya. Hakusikia tena ile nyimbo ikiimbwa wala mlango kugongwa. Kulikuwa ni kimya, akisikia pumzi yake ikihema kwa upesi.
Akasonga taratibu kuufuata mlango wake na kutulia hapo kidogo. Akaweka sikio lake mlangoni kuskiza. Hakusikia kitu. Kidogo kabla hajatoa sikio hapo, akasikia sauti ikimnong’oneza, “toka tucheze, Brian. Au niende kucheza na Karen, na kisha mama yako?” baada ya kusema hivyo sauti hiyo ikachekea kooni.
Haraka Brian akafungua mlango na kutazama nje kwa tahadhari ya gongo lake. Alitazama kushoto na kulia. Mikono yake yote ilikuwa imeshikilia gongo lake kwanguvu. Hakuona kitu. Akiwa anasonga kuelekea kwenye milango ile miwili ambayo ipo wazi, akawa anatupa macho yake aliyoyakodoa.
Kumbe Olivia alikuwa darini. Alikuwa amejishikiza katika namna ya ajabu akimtazama Brian anayetembea kwa hatua za pole. Brian aliposonga akiwa amebakiza hatua chache kuufikia mlango wa Karen, Olivia akaanguka toka darini na kumvamia, akamdondosha chini!
Akamchoma Brian kisu cha ubavuni. Brian akapiga kelele kali za maumivu. Akatupa kiwiko chake kwanguvu kikamkita Olivia usoni, Olivia akadondokea kando. Brian akajivuta mbali na Olivia kisha akatazama jeraha lake. Lilikuwa linamwaga damu. Alikuwa anasikia maumivu makali sana.
Olivia akalamba damu kwenye kisu kisha akatabasamu na kusema kwa sauti yake ya ajabu, “ni tamu mno, Brian. Nataka tena!” akanyanyuka na kuanza kumfuata Brian kwa kasi. Akaruka juu akitaka kumkita, upesi Brian akamzaba kichwa kwa gongo lake. Alimzaba kwanguvu mno mpaka damu kuruka. Olivia akatupiwa ukutani na kudondoka chini akiwa amelala kifudifudi, akatulia tuli.
Brian akamtazama kwa mashaka. Akanyanyuka akiwa ameuweka mkono wake wa kushoto kwenye jeraha kuzuia damu zisitoke zaidi. Akahema akimtazama kile kiumbe. Amekufa ama amezirai? Akajiuliza.
Kidogo, akasikia sauti ya Olivia akigugumia, mara akaanza kulia. Alikuwa akilia akivuta makamasi na kubanwa na kwikwi. Sauti yake ya kulia ilikuwa ndogo ila kwakuwa usiku sauti husafiri kiwepesi, Brian aliisikia vema.
Olivia akalia kwa takribani sekunde tano kisha sauti yake iliyobanwa na kilio ikauliza, “Nimekukosea nini Brian kuniadhibu kiasi hiki?” Mara hii sauti ilikuwa ni ya Olivia tunayemjua. Sauti ndogo ya kike ya msichana asiye na makosa. Sauti inayotia huruma.
Basi Brian akashikwa na kigugumizi, akaita na kuuliza, “Olivia, ni wewe?” Olivia akaendelea kulia asijibu. “Olivia, tafadhali niambie, ni wewe?”
“Nimeumia sana, Brian!” Olivia akalalamika kwa sauti yake ya kike. “Siuhisi uso wangu kabisa. Wote umejawa damu.”
“Nisamehe, Olivia,” Brian akasema akisonga. “Sikudhamiria kukuumiza, nilidhani ni mtu mwingine amekuingia.”
Olivia akaendelea kulia na kugugumia, akivuta makamasi na kuguna.
“Nisamehe, Olivia,” Brian akaendelea kuomba akisonga karibu. Moyo wake ulikuwa wa baridi kwa majuto. Alipomkaribia Olivia, akainama na kumshika bega. Upesi Olivia akaamka na kumzaba Brian kofi kali, Brian akadondokea chini! Kabla hajaamka, Olivia akawa tayari amekaa juu yake, akacheka na kusema kwa sauti yake ya awali, sauti ya ajabu, “We ni mpumbavu, Brian!” kisha akanyanyua mkono wake wenye kisu kumkita, ila ghafla akaganda. Akatazama kushoto na kulia kwake akinusanusa. Mara akanyanyuka na kwenda zake chumbani mwa Brian.
Brian akamtazama akiishilia humo. Macho yake yalikuwa hayaoni vizuri kwasababu ya kofi alilozabwa. Nacho kichwa kilikuwa kinamgonga haswa upande wa kulia alipoadhibiwa.
Olivia alielekea mahali ambapo Brian alikuwa amerundika nguo zake. Hapo kwa chini kulikuwa kuna kaki ‘container’ kadogo ka chuma kalichondoka na kukaa wazi. Kumbe Brian wakati anachukua lile gongo lake, alidondosha kifaa hicho pasipo kujua.
Sehemu Ya 11
Olivia akainama na kutwaa mkufu ule alafu akaubania kiganjani mwake na kusema, “Mama.”
Akaubusu mkufu ule na kisha akarejea kule koridoni. Hakumkuta Brian. Kugeuka nyuma, akapigwa kwanguvu na gongo, akadondoka chini akiwa amepoteza fahamu. Brian akatokea nyuma yake na kumtazama. Akampokonya kisu na kumgeuza akimkagua.
Akamwona mkononi akiwa na ule mkufu. Akauchukua na kuuweka ndani ya mfuko wake kisha akambeba na kumrejesha chumbani. Akamfunga kamba mikono na miguu kisha akamlaza kitandani. Alipomaliza, akaendea ‘first aid kit’ na kujipa huduma ya kwanza. Akajimiminia dawa ya kukata damu na kuua wadudu alafu akajifunga bandeji.
Akarudi chumbani na kujaribu kumwamsha Wisconsin. Bwana huyo akaamka. Brian akamweleza yaliyotokea. Wisconsin akastaajabu. Alah! Yote yametokea akiwa amelala! Akaamka na kwenda kumtazama Olivia kisha akarejea kwa Brian.
“Utakuwa upo sawa kweli?” akamuuliza.
“Ndio,” Brian akamtoa shaka. “Nipo sawa, asubuhi nitaenda hospitali.”
**
Asubuhi ya saa mbili, Brian akiwa kitandani mwa hospitali.
Mama aliongea kidogo na daktari kisha akaja kukutana na Brian. Akatabasamu na kusema, “Pole sana, mwanangu.” akamshika Brian nywele akitabasamu.
“Daktari amesemaje?” Brian akauliza.
“Amesema tunaweza kwenda. Jeraha halijasababisha maafa makubwa. Kuna dawa za kutumia … na pia amehasa upumzike ili urudi upesi kwenye hali yako.”
Brian akaigiza kutabasamu alafu akauliza, “Wisconsin bado yupo?” Mama akatikisa kichwa. “Hapana, ametoka kidogo. Ila alisema atarejea muda si mrefu.”
Alipomalizia hiyo kauli yake, Brian akamwona Wisconsin akiwa amesimama dirishani. Alikuwa tayari amesharejea. Mama akaenda kuongea naye na muda mfupi, Wisconsin akaingia ndani kukutana na Brian.
“Unaendeleaje, mshindi?”
“Niko sawa. Nadhani nastahili tu kurudi nyumbani.” Wisconsin akatabasamu. “Mama yako anaona uendelee kubaki hapa mpaka upone kabisa.”
“Haitawezekana,” Brian akatikisa kichwa, Wisconsin akaangua kicheko. “Mimi siwezi kulala humu hospitali, unajua Wisconsin. Tuna mambo mengi ya kufanya. Inabidi umwambie Mama hilo.”
“Usijali,” Wisconsin akamtoa hofu. “Kila kitu kitakuwa sawa, Brian. Unajua nini?”
Brian akamtazama Wisconsin kwa kuitikia.
“Kama ingekuwa ni kufa, basi ungeshakufa Brian. Tena muda sana. Mungu yupo upande wako.” akamshika Brian mkono na kumtazama machoni. “Utashinda hata na hili.”
Brian naye akamshika mkono na kumwambia, “Tutashinda wote.” Wisconsin akatabasamu pasipo kutia neno. Brian akamuuliza, “Kuna lolote ambalo umegundua?”
Wisconsin akakuna pua yake na kushusha pumzi ndefu kisha akajitengenezea pale kitandani alipokuwa amekaa. Akaita, “Brian.” Brian akaitikia kwa kuguna. “Olivia ndiye yule mtoto wa mwisho wa Dkt Hamill.”
Habari hizi hazikumshangaza sana Brian. Ni kama vile alikuwa anazitarajia. Matukio ya Olivia, na zaidi juu ya ule mkufu yalimtia mashaka. Akauliza, “Sasa tunafanyaje? Kutakuwa na shida yoyote?”
“Ndio, shida ipo tena kubwa,” Wisconsin akajibu na kuongeza, “Olivia, Brewster pamoja na Alfonso, wote ni mali ya Helo. Wote walitolewa sadaka kumtumikia mdhalimu huyo. Nadhani utakuwa ushajua ni shida kiasi gani.”
“Hatuwezi kulibadili hilo?” Brian akauliza. Wisconsin akabinua mdomo wake na kusema, “Haiwezekani, Brian. Pumzi yake, maisha yake ni mali ya Helo. Wapo hapa duniani kutimiza maagizo hayo. Laiti Helo angelikuwa hajaamka, basi wangelikuwa sawa. Wangeweza kuendelea na maisha yao pasipo bughudhi ya watu.”
Brian akatazama pembeni kwa mafikirio, alafu akaurudisha uso wake kwa Wisconsin na kuuliza, “Ina maana hamna kabisa namna?” kabla hajajibiwa, akaongeza, “Olivia ni msichana mzuri sana. Natamani angelikuwa kwenye ulimwengu wetu.”
Wisconsin akamshika mkono na kumminya kidogo. “Najua, Brian. Hata mimi natamani ikawa hivyo … ila tutafanya kadiri ya uwezo wetu.” Brian akanyamaza. Kuna jambo alikuwa anawaza kichwani. Wisconsin akamtazama na kumwambia, “Inabidi unyanyuke hapa tukaonane na yule binti. Sawa?”
**
Saa nane mchana, nje ya uzio wa shule …
Wanafunzi walikuwa wanatoka kwenda majumbani. Kandokando ya geti, alikuwa amesimama Brian pamoja na Wisconsin. Walikuwa wanatazamia wanafunzi wapungue ili wazame ndani.
Baada ya muda kidogo, wakaingia na kabla hawajaenda mbali wakaliona gari la Wayde likiwa linasonga kwenda zake. Brian akalipungia mkono na kwenda moja kwa moja kulifuata.
Wakaingia ndani ya gari, Wayde akaendesha kuacha nyuma shule. Alipotembea kwa dakika kadhaa, akaegesha gari kando na kumtaka Brian amwelezee kinachoendelea.
“Huyu ni Wisconsin, yeye ni mtaalamu wa yale mambo tuliyokuwa tunayazungumzia. Anahitaji kuona vile vitu ulivyonionyesha jana.”
Wayde akamtazama Wisconsin na kumsalimu, kisha akarejesha uso wake kwa Brian na kumwambia, “sidhani kama itawezekana, Brian.”
“Kwanini?”
“Leo baba anarejea tokea Carolina. Hapa tuongeapo, yupo safarini kurudi. Ni hatari!” Wayde alizungumza akiwa amekodoa macho. Wisconsin akaingilia maongezi,
“Kama kuna nafasi, basi ni hii! Yatupasa kufanya kila jambo ambalo lipo ndani ya uwezo wetu. Tukishindwa leo, basi tutakuwa tumeshindwa milele. Kitakuwa ni kiama cha Boston.”
Brian akamtazama Wayde. Wakatazamana kwa kama sekunde tatu kisha Wayde akashusha pumzi ndefu na kutazama mbele akiwa ameshika usukani. Akakuna kichwa chake kwanguvu. Akatulia kwa muda kidogo na kusema, “Sawa.”
Alafu akawatazama wageni wake na kuwaambia, “ila sitaweza kwenda nanyi wote.”
“Sawa,” Wisconsin akaitikia. “Nenda na Brian!” bado Wayde akawa anasita. Alilaza kichwa chake kwenye kiti akiwaza, mwisho wa siku akasema yampasa aende mwenyewe.
“Ni hatari kwenda na yeyote. Mama yu nyumbani pamoja na wageni wengine. Endapo nikirudi na yeyote, basi italeta shida. Naomba niende mwenyewe.”
Brian akamtazama Wisconsin.
“Sawa,” Wisconsin akajibu na kuongeza, “Basi itabidi twende kwanza nyumbani.”
Wakaelekea nyumbani kwa wakina Brian, Wisconsin akampatia Wayde kitabu chake cha maarifa na kumwelekeza cha kufanya pindi atakapokuwa karibu na maiti zile zilizotiwa komeoni. Alipomaliza na Wayde kujiridhisha kuwa ameyashika maelekezo hayo, akaenda zake.
Wakamtazama msichana huyo akiishia.
“Unadhani ataweza?” Brian akauliza wakiwa wanatazama barabara.
“Ataweza,” Wisconsin akamjibu. “Anaonekana ni msichana mwerevu sana, pia mwenye kujiamini … nadhani ataweza.”
Brian hakuongeza neno. Aliendelea kuangalia barabara. Wisconsin akamtazama na kumwambia, “inaonekana anakupenda sana.”
“Kwanini?” Brian akamuuliza akimtazama. Wisconsin akatabasamu na kumshika bega, “Ameyafanya haya kwakuwa anakupenda. Si kingine.”
**
Saa kumi jioni …
Baada ya kutazama mazingira na kuyaona yapo salama, Wayde alizama ndani ya chumba cha wazazi wake na kuiba ufunguo, kisha akanyata kutoka, na upesi akakimbia kupandisha kule juu ilipo maktaba. Akafungua mlango wa kwanza, akazama ukumbini, akaufungua tena ule wa pili, wa siri, akazama ndani, kisha akaelekea ile miili ya wafu.
Hapo akaitazama, akavuta na kushusha pumzi ndefu kisha akayafumba macho yake na kunyamaza kwa sekunde tano. Akivuta hewa na kushusha. Kabla hajafungua mdomo wake kunena, akasikia honi huko nje! Akashtuka na kukurupuka.
Akatoka ndani ya chumba kile upesi na kurudi kule maktaba kutazama kupitia dirishani. Akaona gari la baba yake likiingia ndani. Kwa uhakiki zaidi, akangoja mpaka amwone akishuka. Kweli akamwona. Baba yake alikuwa amerudi.
Sasa afanyaje? Aache kufanya ile kazi arejee chumbani ama? Akahisi kichwa kinamuuma. Alipotaka kuondoka, akakumbuka yale maneno ya Wisconsin, ni leo ama milele! Hapo akajihisi kukanganyikiwa. Kwa muda akawa amesimama kana kwamba kuku mwenye homa.
Haraka akakurupuka na kwenda kule kwenye kile chumba, akajifungia ndani na kuendea ile miili iliyokufa. Hapo akafumba macho yake na kutulia. Akazivuta pumzi ndefu na kuzishusha, kisha baada ya muda akaanza kunena maneno kwa kunong’oneza.
Alipoyasema maneno hayo, akaweka kiganja chake kwenye kioo. Kabla hajaendelea kusema tena, akasikia sauti ya mlango wa maktaba ukifunguliwa. Moyo ukampasuka. Akasikia vishindo vya miguu, na mara mlango wa chumba alimo ukafunguliwa. Uso kwa uso na baba yake!
“Wayde,” baba akaita akiwa ametoa macho. Akatazama kushoto na kulia ndani ya chumba alafu akarejesha macho yake kwa Wayde. Sasa yakiwa yamejawa na hasira. Akauliza, “unafanya nini huku, Wayde?”
Wayde angejibu nini? Hakuwa na cha kusema. Alijihisi mdhaivu. Mwili unamtetemeka haswa. Alihofu ni nini ambacho baba yake atamfanya. Akasema kwa kutia huruma, “nisamehe, baba. Sitarudia tena kutazama vitu vyako!”
Kabla baba hajasema jambo, akakagua kwanza chumba chake. Kwa macho yake kana kwamba kamera akabaini ya kuwa Wayde alikuwa amepachika kiganja chake kwenye kioo kilichokuwa kimehifadhi zile maiti.
“Wayde, umeanza lini kuja huku?” Akauliza.
“Ni leo tu,” Wayde akajitetea akiapa. “Sijawahi kuja humu siku nyingine isipokuwa hii!”
Baba akamtazama, kisha akaufunga mlango kwa funguo.
“Kuna yeyote ambaye umemwambia kilichomo humu?” Baba akauliza. Wayde akatikisa kichwa upesi, “hapana! Hamna anayejua. Hata mama hajui!”
“Una uhakika?” Baba akauliza. Ungemtazama vema kwenye paji lake la uso alikuwa anachuruzwa na jasho.
“Ndio, nina uhakika, baba! Sijamwambia mtu!”
“Niambie ukweli mwanangu, nani aliyekutuma?” Baba akauliza akimsongea Wayde karibu. Wayde akaogopa maradufu. Akaanza kusonga kurudi nyuma akihofia uhai wake. Hakuwahi kumwogopa baba yake hata siku moja, ila siku hii ilikuwa tofauti. Kila kitu kilikuwa tofauti. Kila baba yake alipokuwa anamtazama, alihisi mapigo yake ya moyo yameamia masikioni kwa namna yanavyokita.
Na zaidi alipokuwa anamsogelea ndiyo akahisi kabisa anaelekea kufa. Kama angeliweza kupotea kimazingara hapo, basi angelishapotea.
Baba akamdaka koo. Akamtazama kwa macho yanayoogofya akisema, “Umeenda mbali ya mipaka, Wayde. Sina budi kukumaliza!” Akamminya koo kwanguvu, Wayde akiwa anapapatika, akapapasa meza aloegemea, mara mkono wake wa kuume ukadaka ‘vase’ nzito rangi ya zambarau.
Hakujiuliza mara mbili akampachika nayo baba yake kichwani, paah!! Baba akalalamika akimimina damu. Akatazama kiganja chake, kilikuwa kimelowa damu. Akamtazama Wayde kwa hasira pomoni, ila hakukaa vema, akabamizwa tena na vase ya pili. Sasa akawa mlegevu, mtepetevu, akadondoka chini na kutulia tuli.
Wayde akashika mdomo wake na kukodoa macho. “Mungu wangu, nimefanya nini hiki?” Alihisi ameua. Aliinama na kumgeuza baba yake, kisha akaweka mkono wake kifuani kuhisi mapigo ya moyo. Alipohisi yapo sawa, angalau akahema.
“Ahsante, Mungu!”
Baba alikuwa anahema kwa mbali. Kichwa chake kilikuwa kinavuja damu taratibu toka kwenye majeraha. Macho yake hakuwa ameyafumba, bali yanayorembua. Alikuwa anamtazama Wayde akimwona kwa mbali, akimwona kimaruweruwe.
Mwili wake haukuwa na nguvu ya kupambana tena. Kichwa kilikuwa kinamgonga akijihisi mzigo.
“Samahani, baba. Inabidi nifanye hivi kwa ajili ya Boston!”
Jicho la kulia la baba yake likadondosha chozi. Akamfuta kwa kiganja chake na kisha akakiendea kile kioo kinachotunza wafu. Kabla hajaanza kunena, akamtazama baba yake alafu akanong’ona, “Samahani, baba.”
**
Saa kumi na mbili na robo …
Wisconsin alitazama saa yake ya mkononi alafu akaminya lips zake. Brian akamtazama na kumuuliza, “ni muda mrefu, sio?” Wisconsin akashusha pumzi ndefu na kusema, “kutakuwa kuna kitu, si bure. Si zoezi la kuchukua muda wote huo!”
Brian akashika tama, “ilinipasa niende naye, tumempa mzigo mku–” akakatishwa na sauti ya gari huko nje. Upesi wakatoka kuelekea huko. Alikuwa ni Wayde!
Alishuka kwenye gari upesi na kumkimbilia Brian akiwa analia. “Pole, Wayde.” Brian akambembeleza. “Usijali, yatakuwa sawa.”
Wayde akalia kwa kama sekunde sita, alipojibandua toka kwenye bega la Brian akajifuta machozi kwa kutumia mikono ya sweta alilovaa, kisha akasema, “nimefanikisha!”
“Kweli?” Brian akatahamaki. Wayde akatikisa kichwa, “kweli Brian.”
“Hongera sana!” Wisconsin akampongeza, “sasa twende ndani haraka!” Wakazama ndani na upesi wakaelekea chumbani kwa Brian kuchukua kile kitabu cha Wisconsin. Ajabu walipofika, hawakukiona!
“Kilikuwa hapa!” Alisema Wisconsin akiangaza kwenye kabati dogo linalopakana na kitanda. Akafungua droo zote, hamna kitabu!
“Atakuwa kachuku–” Wisconsin alisema na kusita. Haraka akanyanyuka na kwenda chumba cha Olivia, huko wakakuta kamba zikiwa kitandani, hamna mtu.
“Tumtafute Olivia!” Wisconsin akasihi akiwa aliyechanganyikiwa. Kidogo, wakasikia mlango ukibamizwa. Wakatazamana. Upesi wakatoka chumbani kuelekea huko. Walipofika, wakamwona Olivia kwa mbali akiwa anakimbia! Mkononi alikuwa amebebelea kitabu.
“Yule kule!” Wisconsin akapayuka. Basi haraka Brian akaanza kutupa miguu yake kwa fujo kumkimbiza Olivia. Kasi ya Wisconsin na Wayde ilikuwa hafifu kwake. Alikuwa anakimbia mno karibia visigino viguse kisogoni!
Akawa anamkaribia Olivia zaidi na zaidi, na huku akiwa amewaacha wenziwe huko nyuma wasionekane kabisa. Kidogo, Olivia akazama msituni na kuanza kupotelea humo. Naye Brian alipopiga kwanja, akazama mitini. Huyo! Huyo! Akimkimbiza Olivia anayepepea kama kishada.
Akaruka viunzi, matawi na vichaka, akaendelea kukimbia! Akazidi kumsogelea Olivia zaidi na zaidi ya zaidi. Kwa makadirio isingepita sekunde nne angekuwa ameshamtia Olivia mkononi, ila ghafla, mguu wake ukadakwa na mzizi wa mti, akachumpa na kudondoka chini kama kifurushi!
Akaguguma kwa maumivu akishika tumbo. Kutazama mbele, Olivia akasimama na kumcheka, alafu akaendelea kukimbia akiyoyomea msituni! Brian akapoteza matumaini.
Olivia akakimbia kwa takribani dakika moja, akatokezea barabarani, upesi akivuka, aendelee kuzama msituni, akasombwa na gari kwanguvu! Tiih!! Akarushwa na kudondokea mbali, puh! Kisha akatulia tuli kama kiroba cha mchanga. Kitabu kilirushwa mbali kabisa na yeye. Kikiwa huko kikawa kimejifungua kwa shurba.
Kwenye gari akashuka Wayde na Wisconsin.
“Yu wapi, Brian?” Wayde akaangaza. Haraka Wisconsin akafuata kitabu chake na kukitia kwapani. Wakatazama kushoto na kulia kumtafuta Brian, punde Wisconsin akamwona akiwa anajikongoja.
“Yule kule!” Akajikuta akiropoka. Wayde akamkimbilia na kumkumbatia kwanguvu. “Upo sawa?” Brian akatikisa kichwa kuitikia.
“Mmepata kitabu?” Akauliza.
“Ndiyo, tumekipata!” Wayde akamjibu kwa tabasamu. Wakajikongoja kufuata gari waondoke zao, lakini kabla hawajaingia, Brian akatumbua macho na kusema, “Ona, anaamka!”
Wisconsin na Wayde walipotazama wakamwona Olivia akisimama. Viungo vyake vilikuwa vimevunjikavunjika, amejawa na damu mwili mzima. Hata sijui aliwezaje kusimama katika namna ile. Ilikuwa ni ajabu. Akiwa amegeukia mbele, akageuza shingo yake nyuma kuwatazama wakina Brian, alafu akapunga mkono wake na kutabasamu.
“Ingia ndani ya gari!” Wisconsin akahadharisha. “Fanya upesi! Upesi!” Wakazama garini na kufunga milango. Wayde akawasha gari na kulirejesha nyuma kwa kasi, Olivia akaanza kulikimbiza!
Alikimbia akipindapinda ila mwendo wake ukiwa ni wa kasi mno! Wayde kutengenezea gari wageukie walipotokea, Olivia akawa ameshafika, akarukia darini mwa gari na kung’ang’ania huko.
Wisconsin akamsihi dereva, “Endesha! Endesha!” Gari likatimuliwa kwa fujo. Likashika lami na kukaa humo vema, likaenda kwa kasi, kwa mrama!
Wayde alilipeleka kushoto na kulia, kushoto na kulia. Bado Olivia alikuwa darini. Akalichochea kwa usawa, kisha akaminya breki kali, hapo Olivia akatupiwa kwa mbele kama mzigo, ila ajabu mikono yake ikawa imebaki imeng’ang’ania dari!
Wayde hakupoa, akaminya mafuta na kumsigina kiumbe huyo. Kama haitoshi, akarudisha tena gari nyuma na kumkanyaga, kisha akapeleka tena mbele na kumkanyaga. Olivia akawa chapati!
Wakatoka zao msituni.
**
“Ni lazima usiku huu uwe wetu!” Alisema Wisconsin. Alifungua kitabu upesi Brian na Wayde wakiwa kando, na mara kidogo Mama Brian akaungana nao akitokea chumbani.
“Karen yupo wapi?” Brian akauliza.
“Hajarudi tokea kazini,” Mama akamjibu akiketi. Wisconsin akawaagiza walete mshuma na wafunge madirisha na milango yote. Maagizo yake yakatiiwa upesi basi akaanza kusoma kile alichokuwa anakitazama kwenye kitabu.
**
Bado kulikuwa kimya ndani ya chumba. Hakuwa amepata msaada wowote tangu mwanaye, Wayde, amwache hapo chini. Macho yake yaliyokuwa yanarembua yalikuwa yanatazama kile kioo kilichohodhi miili ya wafu. Hakuwa anayatoa macho hapo. Hata alipoyafumba, akayafumbulia papo hapo
Ni kana kwamba kuna kitu alikuwa anangoja.
Akiwa anaendelea kutazama, mara akaanza kuona kioo hicho kikichipua ufa! Akakoroma akitaka kusema jambo lakini hakuwa anaweza. Kioo kikaendelea kuchipua ufa zaidi na zaidi. Na mmoja wa mwili uliokuwemo ndani ukaanza kujigusa. Ukachezesha kidole!
Ukafuatiwa na mwingine, ukachezesha jicho!
**
Baba yake Wayde akatamani kunyanyuka azuie anachokiona, ila hakuwa anaweza. Hata kusogeza tu mwili wake ulikuwa ni mtihani, angewezaje kunyanyuka? Akabaki akigugumia, macho yakimtoka machozi zaidi na zaidi kutengeneza mto. Ni punde, kioo kikavunjika na wale walio wafu wakawa wazima!
Wakasimama kwa miguu yao. Wakatazama kwa macho yao! Ajabu ni kwamba viumbe hivi havikuwa vikipumua, wala mapigo yao ya moyo hayakuwa yanaita. Miili yao ilikuwa ya baridi na macho yao yalitingwa na mboni zenye rangi ya maziwa yaliyoharibika.
Wakamtazama yule mzee pale chini, wasiwe na habari naye, wakajiendea isijulikane wapi wanaelekea.
**
Wakiwa wameshikana mikono, kwa pamoja wakamalizia kusoma kifungu cha mwisho ambacho Wisconsin alielekezea. Wakiwa wanasoma kifungu hicho, mshumaa ukaanza kufifia, mapazia yakapeperuka kwa upepo, na milango ikaanza kucheza yenyewe.
Hawakukoma, wakamaliza kusoma kabisa, kisha Wisconsin akamchanja Brian kidole gumba na kuchuruzia damu kwenye ukurasa ule waliokuwa wameusoma. Ajabu pakaanza kufuka moshi mweusi karatasi likijifinya kuwa jivu.
Moshi huo Brian alipoutazama kwa sekunde kadhaa, akahisi anapoteza akili yake. Akahisi anapotelea moshini. Hata mwili wake ukaanza kupungukiwa nguvu. Alijishangaa kichwa chake kikidondoka kwa uzito na kujikuta chini!
Akiwa anapata fahamu, akasikia sauti za wadudu, na ngozi yake ikahisi kukalia majani. Akafungua kope zake nzito na kuangaza. Alikuwa kizani, na zaidi alikuwa msituni!
Akanyanyuka upesi na kutupa macho yake huku na kule. Akavuta pumzi ndefu na kujikuna kwa kuwashwa na majani, kisha akaanza kusonga kufuata mwanga anaouona kwa mbali.
Alipotembea kwa dakika tatu, akahisi kuna mtu nyuma yake, upesi akageuka kuangaza. Hakuona mtu! Ni miti ilikuwa imesimama tuli, miti meusi!
Akavuta pumzi ndefu na kusonga na safari. Akatembea tena kwa takribani dakika mbili, akahisi mtu akikatiza kwa mara nyingine! Alipogeuka na kuangaza, hakuona mtu. Akaokota gongo la kuminyia mkononi kwa tahadhari.
Kisha akaendelea kutembea.
**
“Atakuwa sawa?” Mama aliuliza akimtazama Wisconsin. Mikono yake ilikuwa imemshika Brian ambaye alikuwa amelazwa kwenye kochi akiwa hana fahamu.
“Usijali,” Wisconsin akamtoa mashaka. “Atakuwa sawa tu. Yeye ni mpambanaji, najua atashinda vita hii.”
Mama akamtazama mwanaye na kutikisa kichwa kwa huruma. Alitamani amwamshe na kumkumbatia, ila alikuwa ulimwengu mwingine. Alikuwa yupo kwenye ulimwengu wa wafu.
Mama Brian akauliza, “na vipi kama akiuawa huko?” Wisconsin akamtazama kwa imani na kumwambia, “Halitatokea hilo.”
“Vipi kama likitokea?” Mama akasisitiza. “Kama akiuawa huko na huku itakuwaje? … atakufa pia?”
Wisconsin akatikisa kichwa kuafiki, “ndio, atakufa pia. Hatoamka katika usingizi wake huu.”
Mama akajawa na hofu. Akaketi na kumlaza mwanaye mapajani mwake. Mwanaye wa pekee. Naye Wayde akaweka kiganja chake kwenye paji la uso la Brian na kusema, “Tafadhali, kuwa salama.”
Kidogo mshumaa ukazimika na ndani kukawa totoro.
“Nini kinatokea?” Mama akapaza sauti. Wisconsin akafanya jitihada za kuwasha mshumaa, ulipowaka, wakamwona mtu akiwa amesimama mlangoni. Mtu mpana mweusi. Wote wakashtuka!
Wasipate muda wa kujiuliza, mtu huyo akamvamia Wisconsin, akamkaba na kumnyanyua juu, kisha akamtupia kwanguvu ukutani!! Alafu, kwa kasi kali ya shingo yake, akamgeukia Mama yake Brian na kumnyooshea kidole chake kirefu. Akasema, “Wewe na mwanao, wote mtakufa!”
Akamnyaka Mama Brian, ila kabla hajafanya kitu, Wayde akamrukia mgongoni na kujaribu kumng’ata shingoni. Haraka akamdaka binti huyo na kumtupia kwenye meza ya runinga. Meza na runinga yake vikavunjikavunjika! Wayde akalalama sana kwa maumivu.
Bwana yule, mweusi kwa rangi, uso wake ukiwa haujulikani ni wa nani, akamgeukia sana Mama Brian aliyekuwa amemkumbatia mwanaye, akamtazama kwa kupindisha shingo, kisha akayarudia maneno yake, “wewe na mwanao, wote mtakufa” akamnyaka Mama Brian na kumnyanyua juu kama unyoya, alafu naye akamtupia mbali, akajibamiza na kudondoka chini akiwa hoi bin taabani.
Sasa dubwana likawa limebaki na mwili wa Brian pekee. Brian ambaye yupo hapo kimwili tu. Akamtazama na kumnyanyua juu akiwa amemkaba, akasema, “sasa na mwisho wako umefika!”
Akanyanyua mkono wake wa kushoto juu, ukachomoza kucha ndefu kama koleo, akamzamishia nazo Brian tumboni, Mama akapiga kelele kwa maumivu ya mwanaye! Mwili wa Brian ukaanza kumimina damu lukuki na yule Dubwana akafurahi haswa.
Akautupia mwili huo kochini alafu akanyonya vidole vyake vyenye makombo ya damu kisha akajilamba kana kwamba ametoka kula chakula kitamu.
“Tafadhali, mwache mwanangu!” Mama akalia. “Kaa mbali na mwanangu wewe shetani!”
Dubwana lile likaangua kicheko na kusema, “nishamwacha ajifie. Bado wewe!”
Likaanza kupiga hatua zake nzito kumfuata Mama Brian, alipomkaribia akamdaka shingo yake na kumnyanyua juu alafu akamkandamizia ukutani. Mama Brian akapapatika kutetea uhai wake. Miguu yake ikaogelea hewani akiwa anaelekea kufa.
Ila kheri, na ni ghafla tu, hilo dubwana likaanza kupoteza nguvu zake kwa upesi! Likastajaabu. Likamwachia Mama Brian akadondoka chini na yeye akaangaza huku na huko akitafuta kinachomtafuna.
Kule kingoni, dirishani, akamwona Wisconsin akiwa amefungua pazia sehemu ndogo na mkononi mwake ameshikilia kitabu anasoma. Basi dubwana hilo likakasirika likinguruma, haraka likaanza kusonga kumfuata Wisconsin akammalize mara moja!
Akiwa amebakiza hatua moja kumkabili mtu wake, Wayde akamrukia na kumganda mgongoni. Kabla hajamwondoa binti huyo, akastaajabu akichomwa na vioo usoni, tena mara nyingi asizoweza kuhesabu. Kumbe Wayde alikuwa ameteka baadhi ya vipande vya runinga. Na japo naye vilikuwa vinamkata kiganjani, hakuwa anajali!
Alimtofoatofoa yule dubwana na kumfanya alalamike kwa kunguruma. Macho yake ambayo hayakuwa yanaonekana, yakavuja damu akihangaika huku na kule kumtoa Wayde mgongoni. Mithili ya chombo kilichokumbwa na dhoruba, akawa anapepesuka, anajigonga na kutaka kuanguka.
Alipofanikiwa kumtia Wayde mkononi, akamvuta kwanguvu kisha akamminya shingo yake akitaka kumvunja na kummaliza moja kwa moja, ila hakuwa na nguvu hizo tena. Sasa alijihisi mdhaifu kuliko hata mara ya kwanza. Magoti yalishindwa kumbeba kabisa akaangukia chini kama mtu anayesujudu.
Mikono yake ikamwachia Wayde, ambaye naye alidondoka akiwa amechoka, amejeruhiwa. Haraka Wisconsin akaenda kumjulia hali binti huyo, na asipoteze muda, akamwagiza aweke presha kwenye jeraha la Brian ingali yeye akienda kutafuta huduma ya kwanza.
Kidogo akarejea akiwa na mkoba wa huduma hiyo, akatoa bandeji na dawa, upesi akamtia dawa Brian na kumfunga kisha akamwendea Mama. “Upo sawa?”
Mama akatikisa kichwa kuafiki. Wisconsin akamnyanyua ampeleke kumlaza kochini, lakini kabla hajasonga, akamwona dubwana lile likiwa limeamka! Tayari alishakusanya nguvu zake kama hapo awali!
“Mungu wangu!” Mama Brian akanong’ona. Upesi Wisconsin akapaza sauti, “Wayde, zima mshumaa!” Haraka Wayde akapuliza mshumaa na kuzimika.
Kidogo Wisconsin, akauwasha tena, na mara hii ulipowaka, mlangoni wakawa wamesimama watu watatu! Kutokana na mwanga hafifu, hawakuwa wanaonekana vema ila Wisconsim aliwatambua. Ni wale watoto wafu wa Helo.
Basi akasema maneno ya ajabu, na mara wale wafu wakamvamia dubwana yule na kumteketeza wakihodhi haki yao kama watoto wa Hernandez Lorenzo. Haki ambayo watoto hawa wa kuasili; Alfonso, Brewster na Olivia waliiteka kwa muda!
**
“Brian, amka! Brian, Brian, amka!” Sauti hiyo ya kike ilikuwa inanong’ona kwenye masikio ya Brian. Hakuwa anajitambua yupo wapi. Alikuwa gizani. Tangu, dubwana lile lilipomkita tumboni kule kwenye ulimwengu wa waliohai, alipoteza nguvu na fahamu.
Sasa anaanza kurejea kwenye hali yake. Bado akiwa kwenye ulimwengu wa kiza! Ule wa waliokufa. Na mtu yule aliyekuwa anamhisi yupo nyuma yake, ameshamteka! Mguu wake wa kuume umedakwa na anaburuzwa.
Akafungua macho yake na kuangaza, alikuwa hajui anapelekwa wapi. Alichokiona ni mwanaume jabali akimburuza kana kwamba kiroba.
Akaangaza kushoto na kulia kwake, bahati akajigongoa kwenye jiwe. Akalibeba jiwe hilo pasipo kulalamika kwa maumivu. Alivumilia. Alipoweka vema mkononi akalirusha kumbamiza yule aliyemshika, naye akageuka na kumtazama.
Alikuwa ni Helo!
Alimdaka Brian kwanguvu, na mara kule kwenye ulimwengu wa waliohai, mwili wa Brian ukaanza kuchuruza damu puani!
Puh! Brian akatupwa chini. Kabla hajakaa sawa, akazabwa teke kali la kichwa. Akahisi kupoteza fahamu. Akiwa ameshajua ameshakwisha, hajui tena alipo, akasikia tena sauti ya kike ikimwambia, “amka! Brian, amka!”
Akafungua macho yake kuangaza, akaona akiwa ameshakaribia kwenye makazi yale yaliyokuwa na mwanga hafifu aliouona kwa mbali. Akajikakamua. Kidogo, bwana yule akamshtukia. Akamwapua na kumbeba kuzama naye ndani. Akiwa amebebwa, Brian akasikia sauti za funguo mfukoni mwa Helo.
Walipofika kwenye chumba fulani, Brian akatupiwa humo na kisha Helo akasimama akimuuliza ni nini amekuja kufanya huko kwenye ardhi ya wafu.
“Kwanini waja huku na hutaki kusikia?” Na akahitimisha, “.. yanipasa nikuue ile uje kutuama huku kabisa maana unapapenda!”
Akamsogelea Brian amnyake, ila ghafla akasikia sauti za watu wakiwa wanagongagonga mlango. Akanguruma kuguna na kutoka humo ndani kwenda huko aliposikia sauti. Ilikuwa ni kwenye chumba ambacho amewafungia mateka wake. Mateka wa kiroho anaowatumikisha. Humo ndani alikuwapo pia na Kecie.
Akafoka, “mnataka nini? Kufa mara ya pili!”
Wote wakatulia. Akajipapasa mfukoni, hakuhisi ufunguo. Akastaajabu! Upesi akakimbilia kule alipomwacha Brian, kufika hakukuta mtu. Akaangaza akishangaa.
Kidogo, akahisi vishindo vya watu. Alipotoka ndani, koridoni akakuta roho zile ambazo alikuwa amezifungia. Zilikuwa tayari huru!
Akafoka, “kabla sijawaangamiza, rejeeni zizini!” Uso wake ulikuwa umeghafirika kwa hasira. Kecie akamjongea na kumwambia, “hauwezi kutufanya chochote hivi sasa, Helo. Hauna nguvu hiyo tena!”
Helo akatazama mikono yake akiwa amekodoa. Akajaribu kumkamata Kecie, akashindwa, mkono ulivuka kama kivuli. Akastaajabu na kuhofia.
Kecie akamwambia, “muda wako umekwisha, Helo. Ni wakati wako wa kuangamia.”
Mara, “hapana!” Sauti ya kiume ikasikika. Kutoka nyuma ya wakina Kecie akatokea Brian aliyesonga mbele kabisa. Mkononi alikuwa ameshikilia funguo, ni yeye ndiye aliyewafungua huru wakina Kecie.
Akamtazama Helo na kumwambia, “familia yako iko hapa. Nadhani hauna haja tena ya kuusumbua ulimwengu wa walio hai.”
Helo alipotazama nyuma akawaona watoto wake watatu. Akawakimbilia na kuwakumbatia kwanguvu macho yake yakiwa yanalenga machozi.
Kecie naye akamshukuru Brian kisha akamuaga kwa kumfumba macho na kumwambia”rudi sasa duniani. Umemaliza kazi yako Brian.”
**
Brian akakohoa.
“Ameamka!” Mama akalipuka kwa furaha. Akamkumbatia mwanaye kwanguvu na kumbusu kwenye paji la uso. Wayde naye akamkumbatia na kisha Wisconsin. Walikuwa wamemaliza na kufaulu mtihani!
Walijawa na furaha tele. Punde Karen akajiunga nao, wakafanya tafrija fupi. Kesho yake Wayde akarejea kwao na kupewa taarifa kuwa baba yake alikuwa hospitalini akiendelea vema
.
Alipomweleza baba yake kilichotukia akiwa kitandani amelazwa, baba yake akamshika mkono kwanguvu na kumwambia, “umefanya kile ambacho sisi tulishindwa.” Kisha akatabasamu na kumbusu, “hauna haja ya kuomba msamaha. Najivunia kuwa nawe.”
.
MWISHO

