KWA MAPENZI HAYA LAZIMA TU NIMSALITI
ONYO: Wakubwa tu, kuanzia Miaka 18, ndio wasome hii Hadithi
SEHEMU YA 31
“Mke wangu nahisi kuvurugwa, Joshua hajanitumia pesa ya mzigo uliopita pia nimemtumia mzigo mwingine, mbaya zaidi hapatikani”
“Labda ni changamoto tu za mawasiliano, Joshua mbona hana shida yoyote”
“Lakini ni zaidi ya mwezi unakatika ananizungusha tu, hapatikani wasap wala facebook, amepotea kabisa”
“Usijali, tusubiri kwanza”
Siku zilikatika Joshua hakupatikana. Nilikumbuka siku moja Docra aliniambia niwe makini na Joshua, kwa mbali nilianza kuhisi kutapeliwa. Mke wangu aliniambia nikatoe taarifa polisi, nilielekea kituoni waliniambia watawasiliana na polisi wa marekani lakini siku zilikatika na hakuna cha maana ambacho kilifanyika. Niliona nikizubaa haki yangu itapotea, nilifunga safari kuelekea marekani ili nikajue tatizo ni nini, nilibeba leseni yangu ya biashara na document zingine ambazo zilionyesha kuwa mimi ni mmiliki wa duka la mchele lililopo marekani.
*****
Kimya kimya nilifika New York katika mtaa ambao nilifungua duka, ajabu ni kwamba pale dukani nilimkuta mfanyabiashara mwingine ambaye alifungua duka la nguo. Nilimuuliza imekuwaje awe yeye badala ya Joshua? aliniambia kuwa hamjui Joshua wala hamtambui. Nilielekea nyumbani kwa Joshua, huko nako nilikuta mambo yamebadilika, badala ya kumkuta Joshua nilikutana na mwanamke flani hivi kibonge ambaye sikumtambua, nilimuuliza kuhusu Joshua alinijibu hamjui. Nilimuuliza kama hamjui sasa hiyo nyumba ni ya nani? alinijibu hiyo ni nyumba ya kupanga. Alinielekeza nyumbani kwa mmiliki wa nyumba, nilimfuata nilimuuliza kuhusu Joshua alinijibu kuwa alimfukuza kutokana na utapeli. Uzuri ni kwamba jamaa alikuwa anaongea Kiswahili, tulielewana vizuri kabisa.
“Kwani unamtaka Joshua wa nini?” Aliniuliza
“Ni rafiki yangu, mimi na yeye wote watanzania ila yeye alitangulia kuja kuishi huku. Nilimuachia biashara yangu aiendeshe, sasa nashangaa nikimtafuta kwenye simu hapatikani”
“Aaah kumbe wewe ndiye ulikuwa mmiliki wa mchele na unga wa Tanzania?”
“Ndiyo ni mimi”
“Pole sana, ushaingia cha kike. Yule mtu ni zaidi ya jambazi, ana matukio mabaya sana, kwanza anatafutwa na polisi, mimi nilimfukuza kwenye nyumba yangu kwa sababu alitaka kuiuza nyumba yangu. Nadhani hata biashara yako ameiuza kisha amekula pesa ndio maana amekimbia. Sijui yupo wapi, ila marafiki zake wakubwa ni wafanyabiashara wa madawa ya kulevya”
Hadi kufikia hapo nilivurugwa sio kitoto, na ukicheki mimi sio mtaalamu wa mitaa ya New York, sikujua niingilie wapi nitokee wapi, na sikujua nitalala wapi. Uzuri wa yule jamaa mwenye nyumba ni mkarimu sana, nilimueleza kuwa Joshua kanitapeli biashara ambayo ndiyo muhimili mkuu wa maisha yangu, nilimwambia kuwa lazima nimtafute anipe pesa zangu, jamaa alinikabidhi chumba cha kulala na hakunitoza pesa yoyote. Siku ya kwanza nilipumzika, siku ya pili niliingia mtaani kumsaka Joshua, sikuwa pekeyangu bali nilikuwa na jamaa aliyenipa chumba. Yeye ndiye alinipitisha na kunionyesha vijiwe maarufu vya Joshua, pia alinionyesha jumba ambalo Joshua alikuwa akifanya kazi ya uuzaji wa madawa ya kulevya. Aliniambia kuwa jumba hilo ni hoteli ya kawaida tu, ukiingia huwezi kujua kama kuna biashara mbaya. Tulizama ndani ya jumba hilo lakini hatukumuona Joshua, alinipitisha mitaa yote lakini hatukuambulia kitu.
Siku ya iliyofuata mwenyeji wangu alielekea kazini kwake, mimi niliingia mtaani kumsaka Joshua, nilipita vijiweni lakini nilimkosa, hatimaye nilifika katika ile hoteli. Ndani ya hoteli nilikuta watu wengi wakitazama warembo ambao walikuwa wakinengua mbele ya steji, mimi nilitulia tu nikiwa naangaza macho huku na huko. Sasa katika kutazama mara nilimuona Joshua akiwa amepiga suti nyeusi, hakuwa pekeyake bali alikuwa na kundi la watu ambao walivaa mavazi meusi. Sikutaka kuzubaa nilimkimbilia kisha nilimshika shati.
“Joshua vipi? Mbona sikuelewi? simu zangu hupokei, pale dukanı haupo, tatizo nini ndugu yangu?” Nilimuambia kwa upole lakini mwenzangu hata hakunielewa, kwanza alinishangaa sana.
“We ni nani?” Aliniuliza kwa kufoka, hata marafiki zake walinishangaa.
“Hunijui mimi Joshua? Ebu acha utani wako…Nimekuja kwaajili ya kujua kuhusu biashara yangu ya mchele na unga”
“Usinisumbue, sikufahamu”Alinijibu kisha aligeuka, yeye na wenzake walipiga mwendo kuelekea nje ya hoteli.
Sikutaka kukubali, niliwafuata huko huko nje lakini kilichonikuta nashindwa hata kusimulia. Joshua alinitwanga ngumi ya tumbo na pua, marafiki zake walinilamba miteke na m itama, dakika moja m bele tayari nililowana damu, walizama kwenye garı kisha walirudi kinyumenyume wakitaka kunikanyaga; niliokolewa na yule mwenyeji wangu ambaye sikujua alitokea wapi, alinibeba kwenye gari lake alinirudisha nyumbani kwake. Kwanza alinipa pole alafu pili aliniambia kuwa niachane na Joshua hasije akaniua. Nilimwambia siwezi kuachana nae kwa sababu Joshua alikula pesa zangu zaidi ya million 500.
“Duh! Million 500? Pesa nyingi sana ila sijui hata nikuambiaje, Joshua hafai, marafiki zake wote wanamiliki silaha, yeye mwenyewe ana bastola, pia kuua ni jadi yao” Jamaa alizidi kunitaadharisha lakini sikutaka kumwelewa hata kidogo. Hata ungekuwa wewe sidhani kama ungekubali kuziacha million 500 kirahisi.
Niliuguza majeraha yangu hadi nilipona, siku ya tatu nilielekea tena pale pale hotelini, ajabu ni kwamba wahudumu wa hoteli walinifukuza waliniambia siruhusiwi kukaa kwenye hoteli yao hadi niwe na kitambulisho cha uraia wa marekani. Nilishangaa sana, hata hivyo sikubisha kwa sababu hoteli sio ya bibi wala shangazi yangu, nilijidai kama naondoka vile lakini nilijificha sehemu flani hivi nikimsubiria Joshua. Hazikupita sekunde nyingi nilimuona akitoka nje akiwa na watu wake, nilimfuata kisha nilimuambia kuhusu pesa zangu, alinitolea bastola kisha aliwaamuru watu wake wanikamate, walinibeba walinifunga plasta mdomoni na kitambaa usoni kisha walinipakiza kwenye gari yao, sikujua napelekwa wapi, kila nikipiga kelele nilitulizwa kwa kofi zito. Baada ya kufunguliwa kitambaa nilishtuka nipo kwenye chumba ambacho sikukitambua, chumba kilijaa madawa ya kulevya, bunduki kama zote, picha za kutisha, kila sehemu ilikuwa ya hovyo hovyo. Hawakutaka kuchukua maelezo kutoka kwangu, nilishushiwa kipigo cha kufa mtu, kuna muda niliiona dunia ikizunguka kutoka Tukuyu kwenda Uyole. Joshua akiwa anacheka aliniambia kuwa nisimfuatilie na kuhusu pesa sitopata hata 100.
SEHEMU YA 32
“Nipige niue pesa zangu utanipa” Nilimuambia nikiwa navuja udenda wa kipigo
“Sasa Derick ndugu yangu kwa nguvu zipi ulizonazo ambazo zinaweza kunidai mimi pesa? Mimi mwenzio ni muuaji, au we unadhani huku naishi kindezindezi kama kule kwenu? Alafu ulidhani utanitumikisha kwa muda gani niwe nakuuzia mchele alafu wewe upate mafaida tu? shenzi…narudia tena, leo nakuacha kwa sababu wewe bado ni ndugu yangu, angekuwa mtu mwingine ningemuua. Ondoka rudi bongo, ukinisumbua tena sitokuacha” “Joshua kukuamini kote kule unataka kunitapeli? Hujui kuwa nilitoa mzigo wote nilikupa wewe? Naomba angalau hata tugawane nusu nusu kuliko huo mchezo ambao unataka kunifanyia”
“We mshenzi nimekupa nafasi ya uhai lakini hunielewi, sasa leo utakuwa agent wetu wa madawa au nakuua kabisa!”
Alichukua unga wa madawa ya kulevya alinilambisha mdomoni na puani, baada ya muda nilianza kupiga chafya, alinizimisha na mtama mkali, kilichofuata hapo hata sikukijua. Yalipita masaa mengi sikujua kilichoendelea duniani, nilikuja kushtuka nipo nyumbani kwa mwenyeji wangu; tena ilikuwa ni asubuhi ya siku ya pili, usoni nilifungwa bandeji kama zote.
“Pole sana, pia shukuru Mungu amekulinda na kifo”
“Kwani hapa nimefikaje? Na mbona nimeumia hivi?”
“Sijui ni msamaria mwema gani ambaye alikuokoa kwenye kifo, inaonekana alikupeleka hospitali kisha alikuleta hapa kwangu, nilikukuta nje ya mlango wangu asubuhi hii. Mi naona hii ishu achana nayo tu, kubali kuwa umetapeliwa”
“Mi siwezi kukubali kumuachia pesa zangu, kama kuniua aniue” “Duh! Sasa kama ni hivyo ni heri uende polisi kuliko kupambana pekeyako”
“Kituo cha polisi kipo wapi?”
“Kwanza huyu Joshua hata mimi nina hasira nae, ebu twende wote, bora akafungwe tu”
Tulielekea kituo cha polisi, mwenyeji wangu ndiye alikuwa muongeaji mkuu, aliwaeleza polisi kuhusu Joshua na matendo yake mabovu, nilieleza namna nilivyotapeliwa pesa na biashara yangu, niliwaonyesha hati ya biashara kisha niliwasimulia jinsi alivyonipiga na kunilisha madawa ya kulevya. Kitu kilichonipa matumaini ni kusikia kwamba hata polisi walikuwa wanamtafuta Joshua kwa sababu alitapeli watu wengi. Tulizama kwenye gari ya polisi kisha tulielekea hotelini lakini tulikuta pamefungwa. Tuliwapeleka kule kwenye jumba lao chafu lenye silaha tulikuta wakivuta bangi. Walikuwa watano, watatu walikimbia, mmoja alipigwa bastola alikufa hapo hapo lakini Joshua alikamatwa.
Nilifurahi sana kuona Joshua kakamatwa, mimi sikutaka Joshua afungwe; nilitaka anilipe pesa zangu. Alipewa sharti moja tu, alipe pesa au afungwe jela. Hata hivyo kwa kiburi na dharau alisema ni heri afungwe ila pesa hatolipa hata 100. Kwa mara ya kwanza nilishuhudia namna polisi wanavyojua kumtesa mtu, Joshua alipigwa hadi nilimuonea huruma lakini alikataa kuwa pesa halipi hata senti.
“Wewe utaozea jela. Kwanza tapeli, mwizi, muuza madawa, mvuta bangi…Sidhani kama kuna muda wa kusikiliza kesi yako, kesho utapelekwa mahakamani.” Alizungumza polisi mmoja
“Hata sasa nipelekeni, tena kwenye hayo makosa mmesahau koÅŸa moja, mimi ni muuaji. bora mmenileta jela la sivyo mngekuta huyu muuza mchele nishamuua. Pumbavu zenu”
“Unalitukana jeshi la polisi?”
“Sio polisi tu, hata jeshi la wanajeshi na serikali wote mbwa nyie”
Mara nilisikia “pah pah pa” virungu vilitua juu ya kichwa na miguu ya Joshua, alipigwa hadi alishindwa kutembea, alibebwa alienda kutupwa ndani ya nondo, mimi na mwenyeji wangu tuliambiwa tuondoke kisha turudi siku ya pili kwaajili ya kusikiliza kesi yetu. Pia waliniambia nisijali pesa zangu zitalipwa zote na Joshua atapelekwa mahakamani. Tuliondoka tulirudi nyumbani tukiwa na furaha ya ushindi.
Siku iliyofuata tulirudi kituo cha polisi kwaajili ya kusikiliza kesi yangu. Nakumbuka tulifika pale kituoni mida ya saa mbili asubuhi, hadi inafika saa 10 jioni bado tulikalishwa nje ya kituo, polisi walikuwa wanazunguka zunguka tu. Baada ya muda tulimuona Joshua akipandishwa kwenye difenda, tulijua hiyo ndo safari ya mahakamani, waliondoka nae na hatukujua walimpeleka wapi. Polisi mmoja alinifuata aliniambia nimpe nyaraka zote za kesi pamoja na leseni ya umiliki wa biashara; nilimkabidhi kila kitu, aliniambia niondoke kisha nirudi siku iliyofuata nikiwa pekeyangu. Nilishangaa kuambiwa nirudi nikiwa pekeyangu, hata hivyo nilipotezea.
Tulielekea nyumbani, mwenyeji wangu alinipa matumaini kuwa nisiwe na wasiwasi nitashinda tu. Uzuri ni kwamba tayari nilizoea mitaa ya New York, pia sikuwa mwoga kama mara ya kwanza. Kes ho ya ke nilirudi kituoni nikiwa pekeyangu kama nilivyoambiwa, nilikaribishwa katika ofisi flani hivi ambayo humo ndani nilimkuta Joshua akiwa na polisi watatu. Muda wote Joshua alikuwa anatabasam tu, mimi nilitulia nikisubiri maelekezo. Eti niliambiwa kwamba kesi imeisha, Joshua hana hatia yoyote.
SEHEMU YA 33
“KeÅŸi yangu imeishaje? Joshua kanitapeli pesa na biashara yangu yote, ameuza duka langu, amenipiga na amenilisha madawa ya kulevya” Niliwaambia polisi
“Una ushahidi?”
“Ndiyo, hata yule mwenyeji wangu anajua, pia nyaraka zangu za biashara ambazo niliwapa zimeonyesha kila kitu”
“Hizo nyaraka ulimpa nani? sisi hatujaona nyaraka zozote, ondoka kabla hatujakufungulia kesi ya usumbufu, kwanza umeingiaje kwenye taifa letu bila kibali maalumu? Isije ikawa wewe ndiye muharifu, hii nchi haturuhusu ngozi nyeusi ambazo hazina vitambulisho”
Waliniondoa kwa nguvu hadi nilishangaa, nilijua tayari nimechezewa mchezo mwingine, mwanzoni nilidhani nchi za wenzetu zina haki sawa; kumbe bora hata nchi zetu maskini za Africa kuliko mataifa makubwa ya ulaya na america, wana ubaguzi mkubwa sana, pia wao ndio wanaongoza kwa rushwa na uonevu. Sikutaka kukubali, nilirudi nyumbani nikitaka nikamchukue mwenyeji wangu aje kunisaidia. Ajabu ni kwamba nilivyofika kwake alinikabidhi begi langu kisha aliniambia niondoke nyumbani kwake, alinifukuza kama mbwa mwizi. Hakunipa hata nafasi ya kujitetea, aliniambia kuwa mimi ni jambazi toka Tanzania, alinitimua mbio.
Nilikosa muelekeo, nilijikuta naingia kwenye shida na matatizo ambayo sikuyatarajia. Nilimueleza mke wangu kuhusu changamoto hizo aliniambia nibadili kituo cha polisi, ni kweli nilielekea kwenye kituo kingine; baada ya kufika huko niliambiwa niende na document za biashara yangu, na ukicheki document zote nilitapeliwa na wale polisi wa kituo cha kwanza. Nilifunga safari hadi kwenye kituo cha kwanza, sikutaka kuwabuguzi wala kuwakera, sikutaka kuwasumbua wala kuwalalamikia, niliwaambia tu wanipe nyaraka zangu niondoke. Mi hata sijui niliwakosea nini; walinichukua waliniweka ndani ya nondo, na kila nilivyowauliza kosa langu nini walinipiga mateke.
“Na usipotuonyesha kibali cha kuishi marekani kesho tunakupeleka jela” Polisi mmoja aliniambia akiwa ananitazama usoni kwa macho makali.
*****
Siku iliyofuata kijana wa watu pasipo kosa lolote nilibebwa nilipelekwa mahakamani, walitaka kunihukumu kwa makosa ambayo sikuyatambua. Kesi yangu ilikosa ushahidi hivyo basi nilitakiwa nisomewe mashtaka na kuukumiwa moja kwa moja. Nilifikishwa kizimbani ambako kulikuwa na watuhumiwa wengi, hata wasikilizaji wa kesi walikuwa wengi. Wenzangu walihukumiwa hatimaye ilifuata zamu yangu, nilisomewa mashataka kama ifuatavyo;
“Ndugu Derick Mwakasungura mwenye kesi no. 186904, unatuhumiwa kwa makosa matatu; kuingia nchini bila kibali maalumu, kuwatukana polisi pamoja na utumiaji na uuzaji wa madawa ya kulevya, je unakubaliana na mashtaka hayo?” Wakili alinisomea kesi
“Hapana, mimi kibali ninacho, pia sijawahi kuwatukana polisi. Kuhusu madawa ya kulevya hata rangi yake siijui, nilitumia lini? niliuza lini? Nilimuuzia nani?”
“Ebu tuonyeshe kibali chako ambacho kinaonyesha kuwa una ruhusa ya kuishi ndani ya nchi hii, pia tunaomba utoe mifuko ya suruali yako nje tuone kama hakuna madawa ya kulevya”
Kwakuwa nilijiamini sikuwa na shaka, nilizamisha mkono mfukoni nikitaka kutoa kitambulisho, ajabu ni kwamba badala ya kutoa kitambulisho orijino nilikuta kitambulisho feki ambacho kilionyesha jina la mtu mwingine alafu picha ni yangu. Kila mtu alishangaa, hata muheshimiwa hakimu alikodoa macho. Balaa lingine lilikuwa pale ambapo nilitoa mifuko ya suruali nje, huwezi amini mifuko yangu ilijaa kete za madawa ya kulevya, bangi na unga wa madawa. Ndani ya mahakama kukasikika “Aaaaaah” watu wote walinishangaa! Moja kwa moja nilikamatwa na hatia, hakukuwa na swalia mtume wala swalia nabii!
“Mheshimiwa hakimu na watu wote ambao mnatazama tukio hili, nadhani kila mmoja amejionea namna ambavyo mtuhumiwa alitaka kukataa makosa yake lakini amekutwa na hatia za makosa yale yale. Pia sidhani kama kesi hii inahitaji ushahidi mwingi, kuna yeyote ana kipingamizi?”
“Hakunaaaaaa” Walijibu wasikilizaji.
“Narudia tena, kuna mtu mwenye kipingamizi kuwa Derick hausiki na vitu hivyo?”
“Ndiyooooo! Derick hana kosa lolote” llikuwa ni sauti kali na kubwa kutoka mlangoni, watu wote tuligeuza macho tulitazama mlangoni, hakika sikuamini hata kidogo! Nilijikuta natabasam kwa amani, nilicheka kwa raha kisha nilitoa machozi ya furaha. Hata polisi, mawakili, hakimu na wasikilizaji wa kesi wote walishindwa kuelewa kilichoendelea! Kwa macho yangu mawili nilimshuhudia mpendwa wangu wa nguvu akiingia ndani ya mahakama akiwa amevalia suti maridadi, mpendwa huyo sio mwingine bali ni Docra. Sikujua kama Docra ana ushahidi ila kitendo cha kumuona tu kilinifanya nijione mfungwa huru mwenye maisha ya furaha kuliko watu wote duniani. Docra alitembea kwa madoido, skonkwido ambazo alizivaa zilitoa mlio wa “ko ko ko”, na ukicheki mtoto alifungasha, kuna baadhi ya watu walisahau kila kitu walibaki wanatazama nyuma kwenye mkia ambao ulicheza ku s h oto kulia, yaani ni mwendo wa “hamsini hamsini, myaa”. Alipita hadi m bele mahali ambapo mashahidi huwa wanasimama, alisogea kwenye maiki kisha alitulia akisubiria achokozwe.
SEHEMU YA 34
“Binti unaweza kutueleza kipingamizi au ushahidi ulionao juu ya mtuhumiwa Derick?” Wakili aliuliza
“Ndiyo. Kwanza naomba mniambie ni nani alijua kuwa ndani ya mfuko wa Derick kulikuwa na madawa ya kulevya? Sote tunajua kuwa Derick alilala rumande ndani ya kituo cha polisi, sasa kama alilala kituoni; hayo madawa yaliwekwa lini? Yaliwekwa na nani? na kwa kawaida huwezi kuingia kituoni bila kukaguliwa, na kama mlimkagua alafu mlikuta madawa ilikuwaje hadi muyaache mfukoni? ….Pili, kila mtu anajua kuwa marekani ni nchi kubwa sana, sifa kuu ya nchi hii ni ubora wa majeshi yake yaliyopo mipakani. Mnataka kusema majeshi yaliyopo mipakani yanaruhusu watu wenye viza/vitambulisho feki kuingia nchini? Kwamba Derick alipitishwa kinyemela na majeshi yenu?…Tatu nataka kujua; juzi Derick alikuja kituoni kwenu akishtaki kuibiwa pesa zake na umiliki wa biashara zake, aliwakabidhi mtuhumiwa aitwaye Joshua, pia aliwapatia hati za biashara zake, naomba kujua Joshua yupo wapi? leseni za biashara za Derick zipo wapi?.” Mahakama nzima ilibaki kimyaa! Polisi walivurugwa, mawakili walichanganyikiwa, hakimu alibaki ngorongondiii! Docra aliongea kwa kujiamini utadhani mwanasheria kumbe hana sheria yoyote! Hakuna polisi wala wakili aliyethubutu kujibu maswali ya Docra, mimi niliburudika kwa raha jamani hadi nashindwa kuelezea, kuna muda nilitamani nipae nikamkumbatie Docra pale pale kizimbani lakini ndio hivyo nilikuwa chini ya ulinzi mkali. Hata hivyo polisi hawakosagi sababu, yule wakili alitabasam kwa dharau kisha alimtazama Docra;
“Binti umekuja kulichafua jeshi la polisi? Unatuhusisha sisi kwenye makosa ya mtuhumiwa? Una ushahidi gani wa kuthibitisha maelezo yako?”
“Naomba na wewe utoe mifuko ya suruali yako nje, bila shaka tutakuta umechukua kitambulisho cha Derick…Muheshimiwa hakimu, naomba wakili wako atoe mifuko ya suruali yake nje, tena aitolee hapa hapa”
Hakimu alimuamuru wakili afanye hivyo lakini yule wakili hakutoa mifuko yake. Uzuri wa Docra ni kwamba huwa haogopi, alimfuata wakili kisha alimshika mkono alimpitisha mbele ya hakimu. Walinzi wa hakimu ndio ambao walimkagua wakili, huwezi amini walimkuta kaficha kitambulisho changu orijino. Minong’ono ilitapakaa kila sehemu, watu walipiga kelele wakisema “Wakili afungweee…afungweee”. Docra hakuishia kwa wakili tu, aliwaumbua na polisi wote ambao walishirikiana na Joshua kuniibia pesa na umiliki wa biashara yangu. Baada ya tukio hilo hakimu aliamuru Joshua aka mat we, pia ilibidi nirudishwe rumande nikisubiri hukumu ya Joshua. Docra alichezwa na machale, alishauri mimi nisilale mahabusu wasije wakaniua kwa roho mbaya zao, hata hakimu alikubaliana na mawazi ya Docra, niliachiwa huru lakini nilitakiwa kuripoti siku iliyofuata.
Docra alinichukua alinipeleka nyumbani kwao, kumbe wabaya wetu walikuwa wanatuchora tu. Tulifika nyumbani kwa Docra tulimkuta baba yake ambaye alifurahi kuniona, kwanza alinipongeza kwa kutokumsumbua binti yake, pili alinipa pole kwa yote yaliyonikuta, aliniambia nisiwe na shaka kila kitu kitakaa sawa. Licha ya kuokolewa na Docra, licha ya kunikaribisha kwao lakini sikupata muda wa kuongea na Docra, muda wote alikuwa akikaa chumbani kwake, usiku alipika chakula aliweka mezani; tulikula pamoja. Baada ya chakula Docra alielekea chumbani kwake kulala, mimi nilionyeshwa chumba changu nilienda kulala. Mida ya saa saba usiku tulivamiwa na watu wa Joshua, kulikuwa na vita nzito ya bunduki, watu hao walitanguzana na polisi wala rushwa, hata hivyo walikutana na ulinzi mkali kutoka kwa walinzi waliokuwa ndani ya nyumba ya kina Docra, pia baba yake Docra aliita kikosi cha jeshi ambacho kilikuja kusaidia, majambazi wote walikamatwa akiwemo na Joshua.
Siku ya pili kesi ilikuwa raisi tu, baba yake Docra ndiye alisimamia mchongo mzima, kwakuwa yeye ni mtu mkubwa alimueleza hakimu namna alivyokamata waharifu/majambazi na polisi wala rushwa ambao lengo lao lilikuwa kuniua mimi na Docra. Siku hiyo Joshua alikula kipondo hadi alikubali kukiri makosa yake, aliulizwa kuhusu pesa zangu alisema kuwa aligawana na polisi. Walipewa masaa matatu kunirudishia pesa, sikuamini hata kidogo! Pesa zangu zilirudi, hati na nyaraka zangu za biashara zilirudi, watuhumiwa wote walihukumiwa vifungo vya miaka 30 kila mmoja.
Baada ya kukabidhiwa mali zangu tulirudi nyumbani kwa kina Docra, niliwashukuru sana kwa msaada wao, nilitaka niwape pesa ila walikataa kata kata. Sikutaka kukaa sana nchi za watu, pia sikutamani tena kuendelea na biashara hiyo ya mbali ambayo ilijaa utapeli. Hata hivyo Docra aliniambia nisiache kufanya biashara hiyo, alinishauri nibadili eneo pia aliniambia yeye na baba yake watanisaidia kusimamia biashara katika ishu zote za ulinzi. Kutokana na ushawishi wa Docra sikukataa, nilikubali kwa silimia 1000. Alinisaidia kutafuta eneo, tuliweka kila kitu sawa kisha niliwaambia watu wangu wanitumie mzigo. Ilibidi nisiondoke kwanza, Docra nae japo alitakiwa aende chuo lakini alidanganya kuwa bado anaumwa ili anisaidie kwenye ishu zangu za biashara. Baada ya siku 28 tulipokea mzigo kisha tuliujaza ndani ya duka. Hata hivyo nilipata wasiwasi kuhusu kutafuta wateja wapya;
“Usijali, nitakuletea wateja wako wote” Docra aliniambia “Utawaletaje?”
“We subiri hata usiwe na shaka, tena safari hii biashara yako itakuwa kubwa kupita ile ya kwanza”
Siku hiyo hiyo aliandaa matangazo ambayo yalionyesha kuwa duka la mchele wa Tanzania limefunguliwa. Aliweka namba na anuani ya duka langu, mtaa ambao lilipatikana, alinifungulia akaunti mbali mbali za mitandao ya kijamii ili niwafikie wateja zaidi. Pia aliniambia kwamba wamarekani wengi hawapendi kutembea kufuata huduma, kwa kutumia pesa zake alininunulia kigari kidogo ambacho kazi yake kubwa ilikuwa ni kusambaza mchele na unga kwa wateja wa majumbani ambao walihitaji kupelekewa (delivery). Tulipita mitaani tulibandika matangazo kuhusu kupatikana kwa mchele, tulienda hadi mtaa wa The Bronx ambako nilifungua duka langu la kwanza; huko nako tulisambaza matangazo ya mchele na unga. Baada ya wiki moja nilitamani nijenge nyumba marekani niwe naishi huko huko, nilipata wateja wa zamani, wasasa na wa baadae. Hapa namaanisha niliwarudisha wateja wangu ambao niliwapoteza, nilipata wateja wapya na nilipata wale ambao waliweka oda kwa muda unaokuja.
Tulitafuta wafanyakazi wachache ambao walifahamika kisheria, wao ndio walikaa kwenye duka langu. Kabla hatujaondoka tuliagiza mzigo mwingine kisha tuliacha maagizo kwa wafanyakazi ambao walisimamiwa na baba yake Docra, tuliwaambia kuwa wao ndio watapokea mzigo huo.
Wakati hayo yote yanaendelea mke wangu alikuwa akipata taarifa lakini sikumuambia nani kanisaidia hadi nimepata haki zangu. Kuna siku nilimuuliza Docra itakuwaje kuhusu chuo? Aliniambia kwamba alisimamisha masomo yake ili ashughulikie matatizo yangu. Pia nilimuuliza alijuaje ishu zangu za kutapeliwa biashara na pesa?
“Hivi unajua kuwa yule rafiki yako Joshua alinitongoza?”
SEHEMU YA 35
“Alikutongoza?” nilishangaa
“Yeah. Aliiba namba yangu kutoka kwenye simu yako, alinitongoza nilimkatalia, aliniambia kwamba nikikataa atakufanyia kitu kibaya. Baada ya kutoka hospitali alinitumia meseji kwamba amekukamata ili akupe kesi ya uuzaji wa madawa ya kulevya, pasipo baba na mama kujua nilienda kusimamisha masomo kisha nilikuja huku marekani. Hata hivyo baba yangu ana watu wake pale chuoni, aliambiwa kwamba nimesimamisha masomo; alinifukuza nyumbani aliniambia nirudi chuoni lakini sikurudi, nilitoroka nilienda kulala katika ofisi za ubalozi wa Tanzania uliopo hapa marekani. Nikiwa ubalozini sikukaa ndani, nilianza upelelezi kuhusu ishu yako; nilifika hadi nyumbani kwa Joshua nilikuta kafukuzwa na mwenye nyumba, watu walinionyesha hoteli ambayo alikuwa akipatikana, hapo ndipo nilianza kumfuatilia. Siku moja nikiwa hotelini kwa Joshua niliwaona walikubeba walikuweka kwenye gari yao kisha walikupeleka kwenye camp yao, siku hiyo walitaka wakuingize kwenye biashara ya madawa au wakuue kabisa; hata hivyo nilipiga kelele za kuita polisi, wote walikimbizana walikuacha ndani ya camp. Nilikuchukua nilikupeleka hospitali, baada ya matibabu nilikurudisha nyumbani kwa mwenyeji wako, nilikuweka mlangoni kwake”
“Aaaah kumbe wewe ndiye ulinisaidia? Jamaa aliniambia kuwa nimeokolewa na msamaria mwema, kumbe ni wewe? Dah! Asante sana Docra”
“Ndo hivyo. Hata ile siku mnaelekea kituo cha polisi mimi nilikuwa nawafuatilia, yule mwenyeji wako alipewa rushwa na ndio maana alikufukuza. Niliona wakati unanyang’anywa document zako, nina video inaonyesha namna ulivyokuwa unaudhuria kituo cha polisi. Hivi unajua kuwa mimi nililala rumande siku moja?”
“Ebu acha utani”
“Ndiyo niliamua kujipa kesi ya uongo kisha niliwaambia wanifunze adabu nilale maabusu siku moja, kwanza walikataa, ilibidi niwahonge pesa, niliwaonga kisha nilizama ndani. Lengo langu lilikuwa ni kufuatilia kama wanakutesa au hawakutesi, ndipo nilishuhudia wakikubadilishia kitambusho chako cha kusafiria. Siku uliyopelekwa mahakamani na mimi niliomba kutolewa”
“Ila wewe Docra mi sijui hata nikulipe nini, kabisa ulikaa maabusu ili uniokoe? Mungu akubariki sana, natamani hata hii biashara yangu iwe ya mimi na wewe.”
Nilimuomba tumiliki biashara yangu lakini alikataa. Urafiki wetu ulianza kurudi tena, taratibu tulizoeana na tulishibana kuliko zamani. Nilisahau kurudi nyumbani, mimi na yeye tulikuwa tunashinda dukani kwangu tukiwauzia watu mchele na unga. Baba yake aliamua kutuacha tu, hakuwa na wasiwasi wowote juu yangu. Miezi miwili ilipita nikiwa nchi za watu, nilisahau kurudi kwetu.
Siku moja nilipigiwa simu na mtoto wangu aliniambia kuwa mama yake alipata ajali ya garı kaumia vibaya kakimbizwa hospitali. Ilibidi nijiandae kwa safari ya ghafla, Docra hakuwa nyuma aliniambia kuwa atanisindikiza. Siku ya pili tulimuaga baba yake Docra tuliondoka tulirudi Tanzania, moja kwa moja hadi Mbeya. Tukiwa njiani kuelekea hospitali kwa bahati mbaya niligongwa na gari nilizimia hapo hapo.
Docra ndiye alinikimbiza kwenye hospitali ile ile ambayo mke wangu alilazwa, iligundulika kwamba mimi na mke wangu wote tulipungukiwa damu, Docra alijitolea damu kwa ajili ya sisi wote wawili. Docra ndiye alimlea mtoto wetu Monica kwa kipindi ambacho mimi na mke wangu tulikuwa wagonjwa. Docra ndiye alishughulikia gharama zote za matibabu ya mimi na mke wangu. Mke wangu alikuwa hajui lolote kuhusu Docra, ila kwa jinsi ambavyo alituuguza alijikuta akimpenda kwa kası ya ajabu. Sio hivyo tu balı mwanangu Monica alipendwa sana na Docra; ilifikia hatua walipendana na walikuwa kama mtu na mdogo wake.
Tuliruhusiwa kutoka hospitali tulirudi nyumbani tukiwa na magongo, Docra ndiye alikuwa muuguzi wetu, mpishi wetu, na ndiye alihusika katika harakati zote za kusimamia biashara zangu.
Muda mwingi yeye na Monica walielekea shopping kisha walituletea zawadi za kutosha, m ke wangu alinunuliwa vitenge, magauni na vimini. Mimi nilipewa makoti, masweta, suti kama zote. Licha ya kulala nyumbani kwangu lakini hata siku moja hakuonyesha wivu kwa m ke wangu, hakuonyesha tabia mbaya nyumbani kwangu, na hakuna siku hata moja ambayo alionyesha kunitamani kimapenzi m bele ya m ke wangu. Hata usiku wa manane akinikuta natoka chooni hakunisumbua kwa namna yoyote, na anaweza akakaa na mimi hadi saa sita za usiku tukitazama movie lakini hakunisumbua hata kidogo. Alikaa nyumbani kwangu kwa wiki 3 kisha alituaga kuwa anaondoka mara baada ya kuhakikisha tumepona kwa asilimia 100.
“Asante kwa moyo mzuri ulionao, asante kwa msaada ulioutoa kwa familia yangu, sina cha kukulipa. Mimi na mume wangu tumepona kupitia wewe, Mungu akubariki sana” M ke wangu alitoa shukrani
“Asanteni, mimi pia nimefurahi kuishi nanyi kwa amani”
M ke wangu ndiye alimpeleka Docra hadi stendi kuu, waliagana na kila mmoja alirudi kwake. Maisha yaliendelea, niliendelea kuwasiliana na Docra. Siku moja usiku niliota kwamba katika maisha yangu ni Docra pekee ndiye alionyesha kunisaidia kwa vitu vingi lakini mimi sikumsaidia kwa lolote, mbaya zaidi nilikuwa nikimshukuru kwa maneno matupu kitu ambacho ni sahihi lakini sio sahihi sana. Wahenga walisema tenda wema nenda zako lakini amini amini nakuambia kwamba kuna mtu anaweza akakutendea wema alafu ukaona hasara kumuacha pasipo kumlipa wema wake. Kusema asante pekee hakutoshi kumshukuru mtu aliyekupa msaada mkubwa kama ambao nilipewa na Docra. Japo hakutaka nimuhusishe kwenye biashara zangu lakini niliona haiwezekani, nilipanga nikampe zawadi ya mifuko ya unga na mchele ili aanze biashara yake huko huko dar.
SEHEMU YA 36
Nilifunga safari hadi kwenye mashine zangu, niliwaambia waniandalie mzigo wa kutosha kwenye gari moja, vijana wangu waliniandalia. Nilisafirisha ule mzigo kuelekea Dar, nikiwa huko nilimpa taarifa Docra kwamba nimefika; nilimuomba tukutane sehemu ili nimsalimie. Wala hakukataa, tulikutana katika mgahawa flani hivi uliopo posta. Siku hiyo alikuwa amependeza hadi nilijikuta nameza mate ya uvumilivu, kichwani mwangu sikusahau kiapo changu na mke wangu, pia sikusahau yule jamaa aliyekufa kwa kuvunja kiapo. Baada ya salamu nilitiririka kama ifuatavyo;
“Docra” Nilimuita
“Abee”
“Siwezi sema huu ndio mwisho wa wewe kunisaidia mimi, ikitokea nimepata tatizo usisite kunisaidia. Leo nimekuja ku kupa asante ya msaada wote ulionipa katika maisha yangu na ya familia yangu, asante sana Docra”
“Usijali” Alijibu akiwa anatazama pembeni, hakunitazama usoni hata mara moja.
“Docra nisamehe kwa matatizo ambayo nilikusababishia na makosa yangu yote nisamehe! Kwa namna ambavyo nilikukosea sikudhani kama kuna siku utarudi kuwa msaada wa maisha yangu, sikutegemea kama una roho nyepesi kiasi hicho, asante sana Docra”
“Nimekuelewa”
“Leo nimekuletea zawadi. Unaiona ile gari? Ule mzigo wote pamoja na ile kenta nakupa wewe. Mzigo ule ni unga na mchele, naomba fungua duka lako hapa Dar, japo hukuwa na wazo la kufanya biashara hii lakini ipokee tu kwa sababu hiyo ndiyo zawadi ambayo naweza kukupa. Pia kule Mbeya nina mashamba mengi ya mpunga, nitakupa ekari 10 ambazo utazitumia kwa kuanzia. Nitakupa trekta moja ambalo litakusaidia katika ulimaji wa mashamba hayo, pia nitakuwa karibu na wewe kuhakikisha biashara yako inakuwa kubwa, kukiwa na shida utaniambia tu..Docra naomba uipokee zawadi yangu, sina kingine cha kukupa zaidi ya zawadi hiyo, nimeshindwa kukupa pesa kwa sababu umekuwa ukizikataa muda wote”
Baada ya kumueleza hivyo hakunijibu kitu, zilipita dakika nyingi pasipo kuongea chochote. Alafu sasa badala ya kunijibu alianza kulia, nilisogea karibu yake nilimbembeleza nikimuuliza kwanini alilia lakini hakunijibu. Alisimama akitaka kuondoka lakini sikumruhusu, nilimvuta kwenye kiti kisha nilimtuliza kifuani ili hasiendelee kulia. Ajabu ni kwamba akiwa kifuani kwangu aliacha kulia, alifuta machozi kisha alitulia kama sio yule ambaye alikuwa analia. Kwa mara nyingine nilimuomba akubali zawadi ambayo nilimpa, alijitoa kifuani kwangu; kwa mara ya kwanza alinitazama usoni kisha aliniambia maneno yafuatayo;
“Asante kwa zawadi yako ila siitaki.” “Kwanini?” “Sihitaji chochote kutoka kwako zaidi ya penzi lako tu, kama utashindwa kuwa mpenzi wangu basi usihangaike kunipa zawadi yoyote wala usihesabu kama utakuwa umenishukuru kwa msaada ambao nimekupa. Mimi mwenyewe najua kuwa nimekufanyia mambo mengi, unajua kuwa nimefanya haya yote kwa sababu nakupenda, sasa kwanini nikubali biashara na gari wakati mimi nataka mapenzi? Siwezi. Na kwa ufupi naomba ujue kuwa hadi sasa umeshindwa kunipa shukrani kwa msaada ambao nimekupa, hata hivyo sio lazima unishukuru, na sitokuchukia kwa sababu msaada nilikupa mimi mwenyewe pasipo kulazimishwa na mtu. Mimi sijui kwanini amri 10 ziliandika nisimtamani mwanaume haÅŸiye mume wangu, ila nachojua ni kwamba Mungu ameniletea mwanaume ambaye ni mume wa mtu. Kwaheri Derick” Aliongea akisimama
“Sasa unaelekea wapi?”
“Kwa sasa naelekea kwenye ile hoteli ambayo ilisababisha unipe maumivu, naenda kuchukua chumba kile kile ambacho kilinipa maumivu, kama unanipenda na kama unataka kunishukuru basi utanikuta katika chumba kile, nitakuwa pale kwa saa moja tu. Baada ya hapo nitapotea kabisa”
Baada ya maneno hayo Docra aliondoka, nilimuona akielekea kwenye ile hoteli. Nilitulia kwenye meza nikiwaza nifanye nini, nikamsaliti mke wangu ambaye nilimuahidi kwa kiapo kuwa sitomsaliti? Nikifa je? Si watanizika mimi jamani. Mawazo yalinifanya nipitiwe na usingizi wa stress, machoni nilivuja machozi ya kiume, nilikuja kushtuka dakika 30 ziliondoka; ilibaki nusu saa Docra aondoke hotelini. Haraka haraka nilizama kwenye gari kisha nilielekea kanisani, nilipita mbele ya madhabau nilipiga magoti nilisali nikisema “Eeeh Mungu wangu niliapa kuwa sitomsaliti mke wangu. Wewe mwenyewe umeona namna ambavyo nimejitahidi kuzuia usaliti usifanyike, hata hivyo majaribu uliyonipa ni makubwa kwangu, iliandikwa tutafanya dhambi kisha tutatubu na tutapata msamaha. Japo usaliti haupo katika amri zako 10 lakini ni dhambi kubwa kwa sababu tayari nimeoa. Japo sikuapa kwa jina lako lakini kiapo changu ulikisikia. Sijui nini kitatokea baada ya tukio hili, nahitaji msamaha wako; na kama ni adhabu basi nipo tayari kuipokea. Eeh Mungu wangu niliapa kuwa nikisaliti nife hapo hapo, naomba nikifa basi nipumzishe mahala salama! amen”.
INAENDELEA