JINSI UKIMYA ULIVYONIPA NDOA
Simulizi Ya Kweli
PART 1
Shalom naitwa Bite ni binti shushani, nimemuomba Mama aandike ushuhuda wangu kwa ufupi ili angalau watu wajifunze
Baada ya Mimi kuzaliwa Baba yangu na Mama yangu waliachana. Nakumbuka waliachana kwa ugomvi mkubwa na ni ghafla tu Baba alikuja akasema hamtaki tena Mama aondoke. Mama alijitahidi sana kuomba msaada, kumuomba Baba msamaha na kumbembeleza lakini ilishindikana, Baba alisisitiza kuwa hamtaki Mama na anataka aondoke. Basi ikabidi Mimi na Mama tuondoke na twende nyumbani kwa Bibi mzaa Mama tukakaa huko.
Baba yangu alikuwa hatumi matunzo wala huduma yoyote kwangu hivyo tuliishi maisha ya shida sana. Ikafikia kipindi tukasikia Baba ameoa mwanamke mwingine na ana Mtoto tayari. Mama aliumia sana lakini hakuwa na jinsi ikabidi akubali.
Basi nikaendelea kuishi na Mama na Bibi huku nikisoma kwa shida. Nilipomaliza darasa la Saba Baba alikuja kunifwata na kusema anaomba akakae na Mimi ili anipeleke shule ya secondary na nitakuwa narudi kwa Mama kipindi cha likizo tu. Basi Mama alikubali na Bibi alifurahi kwani alitamani sana mjukuu wake niweze kusoma ili nije kumsaidia Mama yangu baadae.
Nikaenda nyumbani kwa Baba nikaanza kuishi pale pamoja na Mama wa kambo na Watoto wake. Huyu Mama wa kambo aliolewa na Baba akiwa tayari na Watoto wake wawili wakike ambao ni wakubwa kidogo kwangu, lakini ambao Baba yao ni mwingine, halafu kwa Baba yangu huyu amezaa watoto wawili wa kiume, hivyo kwa Baba nina wadogo zangu wawili wa kiume.
Baba yangu alikuwa ananipenda sana na aliniambia usijali ukiwa na tatizo lolote niambie mwanangu hapa ni kwenu kuwa huru. Baba yangu alikuwa anafanya kazi mkoa mwingine hivyo maranyingi alikuwa anarudi mara moja moja kutusalimia, hivyo tulibaki na Mama tu. Maisha yalikuwa magumu sana pale nyumbani huyu Mama alionyesha wazi kunichukia na kunibagua waziwazi. Muda wote alikuwa ananifokea, kunisema na kunipiga pia.
Kulikuwa na Mdada wa kazi lakini asubuhi kabla ya kwenda shule nilikuwa natakiwa kudeki nyumba, kufua au kuosha vyombo ndio niende shule na hata kama nimechelewa ni lazima kazi ziishe ndio niende shule. Mara kibao amekuwa akininyima chakula usiku, utakuta nimemaliza mikazi ya usiku nataka kula nakuta chakula kimeisha au hakipo kimefichwa, kakipeleka chumbani. Hivyo nilikuwa nalala sana na njaa.
Lakini Baba akirudi anabadilika anakuwa mwema mwenye upendo sana sana. Na alikuwa haniruhusu kukaa kuongea na Baba yangu, kila Baba akitaka kuongea na Mimi anakuja na anaweza akanitumia kitu mradi tu nisiongee na Baba yangu. Hivyo Baba anakuja na kuondoka bila kuongea nae.
Baba yangu alikuwa anatuma hela za viatu, begi na madaftari lakini sinunuliwi wananunuliwa Watoto wake tu. Baba anatuma pesa ninunuliwe nguo lakini wapi sinunuliwi ila wanae wote wanapata nguo mpya kila baada ya muda.
Alikuwa kitu kidogo tu atanipiga, anaweza amka akanipiga bila sababu tu. Na Watoto wake walikuwa waongo kuna muda wananisingizia Mimi maneno ya uongo kwa Mama yao, na Mama yao bila kunisikiliza anaanza kunipiga na kunipa maneno ya kashfa.
Tusi lake kubwa kwangu huyu Mama lilikuwa lilikuwa Wewe ni mbwa tu kama Mama yako, na utaishia kuzalishwa na kuachwa. Imagine hayo maneno alikuwa ananiambia Mimi nikiwa mdogo. Na anasema kwa sauti ujue kabisaaa hapa hauna chako, hizi mali ni za wanangu pambana ukatafute maisha yako kaa ujipange uondoke. Nikawa simjibu kitu.
Niwe mkweli nilikuwa naumia sana sana sana na sikuwa na namna ya kufanya
PART 2
Sio siri maisha yalikuwa magumu sana pale, sikuwa na raha wala furaha hata kidogo. Huyu Mama alininyanyasa sana na kunibagua mnoo mnoo. Na alionyesha chuki yake kwangu na ubaguzi wazi kabisa bila kuficha.
Huyu Mama wa kambo alikuwa Mlokole hivyo kuna kanisa tulikuwa tunaenda kusali pamoja. Hapo kanisani Huyu Mama alikuwa ni kiongozi wa wamama, alikuwa ni mmoja wa viongozi wa wamama hapo kanisani na Walimuamini sana sana. Siku zote akiwa kanisani ni Mtu mwema sana lakini akirudi nyumbani aisee ni simba anae rarua. Kanisani ni muombaji mzuri anaomba mpaka anagalagala chini lakini nyumbani anakuwa shetani, haombi, wala hasomi neno ni matusi tu, atatukana na kufoka siku nzima.
Sijawahi kuwa na Amani pale nyumbani, amani nilikuwa naipata angalau nikiwa kanisani. Nikifika kanisani muda ule wa kuimba, kuomba ndio ninapata amani baada ya hapo Nikirudi nyumbani ni mateso, matusi, kupigwa nilikuwa naumia sana.
Huyu Mama sijui kwanini ila alikuwa hapendi kuniona naenda shule au nasoma, akiona nimejiandaa kwenda shule atapambana anipe mikazi ili nichelewe, lakini pia usiku nikiamka kusoma utashangaa anawasha radio sauti kali anaweka nyimbo za kuabudu anaanza kuabudu, basi najikuta nashindwa kusoma naenda kulala, na akiona nimeingia chumbani kulala anazima radio anaenda kulala na Yeye. Hili jambo liliniumiza ikabidi nimshirikishe Mwalimu wangu wa Darasa, mwalimu akasema tumia muda wa mapumziko kusoma, lakini pia ukitoka Darasani usiwahi kurudi nyumbani kaa usome mpaka jioni ndio urudi nyumbani.
Mama yangu mzazi baada ya kuachana na Baba aliumia sana moyo ikapelekea akapata tatizo la akili. Kuna muda alikuwa ananyamaza tu kimya haongei, hacheki hata ukimuita haitiki anakuwa yuko mbali sana kimawazo, ni kama mtu aliyekuwa na stress nyingi. Japo kuna muda anarudi kuwa sawa kabisaaa. Sasa Kutokana na hilo nikawa naogopa kumueleza Mama mateso ninayokutana nayo hapa nyumbani kuepuka kumuumizwa tena moyo.
Niliendelea na masomo kwa shida sana, mpaka nikafika kidato cha nne. Nakumbuka Baba yangu alikuwa so excited na Mimi kumaliza kidato cha nne, alinipigia simu kwa furaha sana na akatuma pesa ninunuliwe vifaa vya kufanyia mtihani. Alimuagiza yule Mama aninunulie hivyo vitu na kunipa hela ya chakula kipindi cha mitihani. Cha lakini ile hela sikupewa. Yule Mama alikasirika sana na alinichukia sana. Basi nikajiandaa hivyo hivyo kwenda kufanya mtihani, mwalimu wangu ndio alinipa Pen, penseli, rula, compass ili vinisaidie kufanya mtihani. Na kipindi chote cha mitihani nilikuwa nawahi kuondoka asubuhi na nachelewa kurudi nyumbani nabaki shule kujisomea. Ulikuwa Wakati mgumu ila sikuwa na jinsi.
Baada ya kumaliza mitihani, Baba yangu alirudi na zawadi nyingi ikiwemo nguo nzuri na viatu. Baba alininunulia gauni zuri akasema jumapili hii nataka twende kanisani tukatoe sadaka ya shukurani, Wewe ni Mtoto wangu wa kwanza na umemaliza kidato cha nne lazima nimshukuru Mungu, na Mimi nilifurahi sana nikaanza kujiandaa kwa ajili ya ibada ya jumapili.
Usiku nilinyoosha ile gauni yangu na kuandaa na viatu, nikaziweka chumbani tayari kwa kuvaa kesho. Lakini cha kushangaza nilipoamka asubuhi ile nguo haikuwepo, ilikuwa haionekani. Nikaanza kulia naitaka nguo yangu. Baba alishangaa sana nguo inapoteaje humu ndani na hakuna mwizi aliye ingia. Basi Baba ikabidi awe mkali, akasema kwa usalama wenu naomba Nguo na viatu vya mwanangu vipatikane. Basi tukaanza kutafuta, baadae Baba akaingia chumbani kwa wale Dada zangu Watoto wa yule Mama akaikuta nguo yangu ikiwa imechanwachanwa na mikasi, ikawa na matobo matobo kote, kiufupi iliharibiwa. Na viatu pia vilikuwa vimekatwa katwa zile kamba vikawa havifai. Baba aliumia sana alifoka sana na aliwachapa baadae wakasema sio wao ni Mama yao ndio aliyechana. Weeeh ukahamia kwa Mama, kwanini uchane nguo ya Mtoto. Mama kwa hasira akamwambia Baba una ubaguzi, unamnunuliaje Mtoto mmoja Nguo wakati unao wengi. Weeeh akawa akasema watoto wengi wapi, huyu ndio binti yangu pekee Mtoto wangu wa kwanza, unanizuiaje nisimnunulie nguo, akasema kuanzia leo sitamnunulia Mtu kitu chochote mnawezaje kuharibu Nguo ya mwanangu niliyo nunua kwa hela yangu. Mimi nilibaki nalia tu, Baba akasema mwanangu usijali tutatoa sadaka ya shukurani siku nyingine Leo tuahirishe maana siku yangu imeharibika. Basi nikajiandaa nikaenda Ibadani hivyo hivyo kwa unyonge.
ðŸ˜ðŸ˜ðŸ˜ðŸ˜
PART 3
Wakati nasubiri matokeo ya kidato cha nne, nilimuomba Baba niende kwa Mama kukaa , lakini alikataa. Alisema kutokana na misukosuko ya pale nyumbani ukienda kwa Mama yako wanaweza wakakuzuia usirudi. Akasema ukienda unaweza usirudi, alisema nikiwaambia ndugu wa Mama maisha yangu pale nyumbani wangeweza kataa na kunizuia kurudi kwa Baba yangu. Hivyo Baba aliomba nikae pale na akanisihi sana nisiwaambie ndugu zangu yale niliyokuwa nafanyiwa. Basi ikabidi niwe mpole. Sikwenda kwa Mama nikabaki pale pale wakati nasubiri matokeo.
Baadae Baba pia alihamishiwa kikazi hapa hapa mjini hivyo akawa anaishi pale pale nyumbani, angalau amani ilikuwepo japo si sana.
Sikutaka kukaa nyumbani muda wote ikabidi nijiunge na kwaya ya kanisani. Hivyo nilikuwa angalau ibada za katikati ya wiki naenda, mikesha na mazoezi nikawa nahudhuria, hiyo ilinisaidia sana na kunifanya niwe na amani. Nilichangamka nikapata na marafiki pale kanisani ambao kwakweli walinifanya nijisikie vizuri sana. Japo huyu Mama hakufurahi Mimi kujiunga na kwaya kanisani, na akawa akiniona nimesimama mbele Ibadani jumapili alikuwa anachukia na kununa haswaa. Yani unamuona kabisa kakunja sura.
Akaanza kupeleka maneno mabaya kanisani, akaanza kunisema vibaya kwa wanakwaya wenzangu, baadhi yao nikashangaa wakaanza kunichukia. Yani wananichukia bila sababu yoyote ya msingi. Nikaanza kunyimwa nafasi za kuimba au kuongoza japo kwangu haikuwa shida sana.
Baadae akaanza kupeleka maneno kwa Mchungaji, ikawa kila siku kesi, mara Leo hili kesho hili na akamwambia Mchungaji anisimamishe kuimba kwaya kwasababu ya tabia zangu mbaya. Basi Mchungaji baada ya kuona maneno ni mengi akanisimamisha, akasema Bite nikuombe upumzike kidogo maana kesi zimekuwa nyingi. Niliumia sana ila sikuwa na jinsi ðŸ˜ðŸ˜
Matokeo ya kidato cha nne yalitoka, na nilifanya vizuri tu nikapata Div 2, Baba yangu alifurahi sana sana akanipa zawadi nyingi sana. Yule Mama alichukia mnoo na hakunipongeza hata kidogo. Nilimuomba Baba alipeleke shule ya Boarding japo yule Mama alikataa akasema hapana Boarding huyu ataharibika tabia, abaki hapa hapa. Ila Baba hakumsikiliza akanitafutia shule ya Boarding nikaenda. Namshukuru Mungu nilipata shule nzuri na nikaanza kujiandaa kwenda.
Nilienda kwa Mama na Bibi kuwaaga walifurahi sana nikawaahidi nikimaliza tu Form Six nitahamia pale ili tuishi wote. Basi nikawaaga nikaenda zangu shule.
Maisha ya shule yalikuwa mazuri sana, nilikuwa nasoma naelewa, lakini ghafla hali ikabadilika. Nikaanza kuwa naumwa umwa sana, kila wakati napelekwa hospital. Hasa kipindi cha mitihani, utashangaa asubuhi nataka kufanya mtihani naanza kuumwa. Hii ilipelekea kuto kufanya vizuri kwenye masomo. Kwani mitihani mingi nilikuwa nafanya nikiwa mgonjwa sana, na cha ajabu mitihani ikiisha nakuwa mzima kabisa.
Lakini kitu kingine cha ajabu kikaanza kunitokea, ghafla tu nikaanza kuchukiwa na watu bila sababu. Nikawa nashangaa baadhi ya walimu wananichukia, matron nae ananichukia. Wanafunzi wenzangu nao hawanipendi kabisa. Baadhi wakawa wanasema ninanuka, mchafu, mara Mimi mbaya na sura mbaya, yani maneno yakawa mengi. Nikaanza kusingiziwa viti visivyo eleweka, unashangaa kitu kinapotea naambiwa Mimi nimeiba, sio siri hii hali iliniumiza sana sana, nikawa sina raha ya shule.
Nilikata tamaa kabisa nikasema niende wapi maana ninayokutana nayo shule ndio ninayokutana nayo nyumbani, chuki chuki chuki.
Nakumbuka mpaka namaliza form six sikuwa na raha kabisaaa, kwanza kipindi cha mitihani nilipata homa kali ya ajabu sana iliyopelekea kushindwa kufanya vizuri baadhi ya mitihani. Na mpaka narudi nyumbani nilikuwa mgonjwa kabisa. Nikamuomba Baba niende kukaa kwa Mama angalau kipindi nasubiri majibu, Baba alikataa akasema nikienda kwa Mama nisimtafute tena. Basi ikabidi nikae pale.
Lakini nilishangaa Baba yangu nae alinichukia sana tofauti na zamani, alikuwa hanipendi, hata nikimsalimia haitiki, sikuelewa ni kwanini. Iliniumiza sana kila Mtu ananichukia.
Matokeo japo sikuwa nimefanya vizuri nilipata Div 4. Baba alikasirika sana, akasema yani nimetupa hela zote hizo unaenda kuniletea 4 kweli. Nililia sana sikuelewa nifanyaje. Nilihisi kabisa maisha yangu hayako sawa, kuna kitu hakiko sawa ila sikuwa na namna ya kufanya.
Baba alikataa kunipeleka Chuo, alisema asije tupa hela zake. Basi nikakaa tu nyumbani sifanyi chochote. Baadae Baba yangu mdogo akaja nikaongea nae, akanilipia chuo cha ufundi nikaenda kujifunza ufundi cherehani, akasema Wewe ushakuwa mkubwa huwezi kaa tu hapo nenda kajifunze baadae ujiajiri nitakununulia cherehani ukimaliza.
Basi nikaanza kujifunza ufundi cherehani, nilipomaliza Baba mdogo alinitafutia kazi, nikapata kazi kwenye kampuni ya ushonaji, tulikuwa tunashona Uniforms za wanafunzi wa shule mbalimbali. Baba mdogo alinishauri kuwa nipambane pale nihame, nipange hata chumba kimoja nikae ila nisikae pale, kwani alikuwa anaona manyanyaso yangu.
Baadae nikapata hela nikaamua nikapange, japo ilikuwa ngumu kwa Baba kukubali ila Baba mdogo alisimama kidete kunitetea, akasema anahama kwaajili ya kazi ila weekends atakuwa anakuja. Basi Baba akakubali, nikaenda kupanga, japo Nilikuwa narudi mara moja moja kuwasalimia lakini pia kanisani nilikuwa naenda kwani nilirudi tena kwenye kwaya.
Nikaanza maisha ya kujitegemea
PART 4
Nilianza maisha ya kuishi mwenyewe, yalikuwa ni maisha magumu kidogo japo baadae nikazoea, nikaanza kupata amani ya moyo.
Nilikuwa naenda kwa Baba japo bado yule Mama alikuwa anaonyesha kuto kunipenda. Ila nilikuwa naenda kwani Baba mdogo alinisisitizia kuwa niwe naenda.
Nikawa nikifika pale hanichangamkii hata kidogo, kuna muda anawaambia wasinipe chakula, nikifika chakula kinafichwa wanasema nikale kwangu, ila sikuona shida kwani chakula sio issue kwangu. Mimi nilikuwa naenda pale kwasababu ni kwetu na kuto kuenda ningeonekana nina dharau.
Lakini pia sijui Baba aliambiwa nini kuhusu Mimi kwani aliendelea kunichukia, nikimsalimia haitiki, Nikimpigia simu anapokea kwa ukali. Nilitamani kujua kosa langu ni lipi kwa Baba ili angalau niombe msamaha, kwani nilikuwa naumia kwa namna tunavyoishi. Ukizingatia Mama yangu hayuko vizuri kiafya, sio Mtu wa kumshirikisha jambo akalipokea vizuri na kukushauri. Huwa ukimwambia jambo baya anapanic na anaanza kuumwa hapo hapo. Hivyo nilitamani sana Baba awe mshauri wangu ila ndio hivyo haikuwezekana.
Niliendelea na maisha, nikawa naweza kujitegemea na nikaanza rasmi kuwahudumia Mama yangu na Bibi yangu. Nilikuwa napambana kila mwezi nawafanyia shopping ya vyakula, nawawekea na Umeme, na uzuri pale nje Bibi amelima mboga hivyo akipata tu unga na mchele inatosha mboga wanachuma nje wanakula. Maisha yakaanza kuwa mazuri ya amani na nikaona Mama yangu anaanza kubadilika na kuwa Mtu wa furaha.
Katika pitapita zangu nilipata mchumba, huyu kijana niseme hakuwa ameokoka japo ni mkristo na alikuwa ni mfanyabiashara ana duka la vifaa vya simu na anafanya huduma za miamala ya simu. Kwakweli tulipendana, alikuwa ananihudumia kwa kila kitu, na akaniomba tuoane. Alisisitiza sana Bite nataka kukuoa naomba nije kwenu. Mwanzoni nilisita, ila kwakuwa alisisitiza basi nikaamua kukubali. Nikaamua kwenda kwa Baba, nikamuelezea, Baba alilipokea vizuri ila akasema kabla ya mambo yote nimlete huyo kijana kwanza nyumbani amuone halafu ndio taratibu zingine zifwate.
Basi ikapangwa weekend moja tukaenda Mimi na huyo mchumba wangu mpaka nyumbani kwa Baba. Na siku hiyo walikuwepo wotee Mama, Baba, wale dada zangu na wadogo zangu. Kikapikwa chakula tukala. Ila Mama alinifwata akaniuliza unaharakia nini kuolewa? Si usubiri Dada zako waolewe Ndio Wewe uolewe? Sikumjibu kitu nikakaa kimya kwani swala la kuolewa ni Neema na kila mtu anaolewa kwa wakati wake, siwezi kukaa kusubiri mwingine aolewe halafu Mimi ndio niolewe hapana.
Basi Baba akasema sawa, nimekubali, akamuuliza unampango wa kuoa lini, kijana akasema mwakani tutafunga ndoa, ila mwaka huu December nitakuja kutoa Mahari, halafu mwakani mapema tuoane. Baba akasema sawa karibu sana, nimekupokea na uwe huru kuja wakati wowote.
Lakini kuna kitu kilitokea, wakati tunatoka Mama akamuomba mchumba wangu namba, akasema tunaomba namba yako na Wewe uchukue ya kwangu na ya Baba. Kijana akasema sawa akampa. Basi tukaondoka.
Tukaendelea na mahusiano, tukawa na amani tele. Akawa ananiambia Mama yako kanipigia Leo kunisalimia, nikawa nashangaa imekuwaje ila sikuonyesha chochote, sikutaka ajue kitu chochote. Nikamwambia hongera japo Mimi Mama hajawahi kunipigia wala kunitafuta.
Baada ya kama miezi miwili mahusiano yangu yakaanza kuyumba, mwanaume akabadilika kabisa. Ukimpigia simu hapokei, message hajibu, ukimuomba tuonane hataki na hata ukienda ofisini kwake anakwambia niko busy siwezi kuongea na wewe. Kiukweli niliumia moyo ukizingatia nilikuwa nampenda sana, sasa nikawa sijui ni nini kimembadilisha.
Kuna siku mdogo wangu wa kiume akanipigia akasema sister vipi kuna shida? Nikamwambia hapana kwani vipi? Akasema mbona mchumba wako anakuja sana hapa nyumbani, na anakuwa anaongea na Mama sana na kina Dada. Nikamwambia hata sijui mdogo wangu na wala hajaniambia. Akasema amekuja kama mara mbili na ni kama kuna kikao kirefu hivi na baadae anaondoka. Nikamwambia poa Dogo ngoja nifwatilie akasema sawa fwatilia. Nikampigia simu mchumba wangu hapokei, nilitaka kujua alikwenda kwetu kufanya nini, ila hakupokea na sikumpata.
Basi tulikaa kama miezi miwili hatuna mawasiliano na hatuonani, nikimtafuta simpati. Siku moja jioni nikaamua kwenda ofisini kwake, nikasema leo namsubiri mpaka amalize kazi ili nionane nae, natamani kujua kama kuna kitu nimemkosea basi nimuombe msamaha yaishe ili tuendelee, maana bado nampenda sana.
Basi nikatoka zangu kazini jioni huyo mpaka dukani kwake, ilikuwa mida ya saa moja hivi usiku alikuwa bado hajafunga. Nimeshuka zangu kwenye Daladala huyo nikaanza kutembea, ile nakaribia kwa mbali nikaangalia dukani nikamuona Dada yangu Joy Mtoto wa Mama yangu wa kambo akiwa hapo dukani kwa mchumba wangu. Ikabidi nisimame nianze kuangalia nini kinaendelea. Nilikaa pale kwa muda, ila nikashangaa Joy haondoki, yuko pale pale wanapiga story na kucheka. Nikajipa moyo nikasema ngoja nisubiri labda alileta simu itengenezwe, ngoja nisubiri.
Lakini haikuwa hivyo, alikaa mpaka wanafunga duka, na walipofunga nikaona wamepanda pikipiki, maana huyu kijana alikuwa na pikipiki. Akampakia Dada yangu hao wakaondoka. Kwa namna walivyokuwa ilionyesha kabisa hawa ni wapenzi, yani bila ubishi. Maana wakati wanatembea walikuwa wameshikana viuno, ishara ya kwamba ni wapenzi.
Niseme tu, niliishiwa nguvu, mwili ulikufa ganzi, nikakaa chini. Nikaanza kulia, nikasema inamaana Dada yangu kaamua kunichukulia Bwana wangu kweli ðŸ˜ðŸ˜ðŸ˜
Basi nikarudi zangu nyumbani ila nilikuwa so down, moyo uliniuma sana sana.
Niliendelea kumpigia simu mwanaume bila mafanikio, hapokei simu zangu wala hajibu message. Ila kuna siku moja usiku saa nne alinitumia message mbaya sana na akaniblock. Aliandika hivi
BITE NISEME TU MAPENZI YANGU KWAKO YAMEKWISHA, SIKUTAKI NA WALA SIKUPENDI TENA. SASA NIKO KWENYE MAHUSIANO NA MTU MWINGINE, NAOMBA FUTA NAMBA YANGU, USINITAFUTE TENA
IT’S OVER BETWEEN US
Nyie Nyie Nyie acheni ðŸ˜ðŸ˜ðŸ˜ðŸ˜, yani kaniacha kirahisi tu hivyo ðŸ˜ðŸ˜ðŸ˜ðŸ˜
PART 5
Baada ya kunitumia ule ujumbe niliumia sana sana sana, japo sikukubali, sio siri nilimpenda huyu kaka na sikuwa najua naanzaje kuishi bila Yeye. Nilikuwa naona kabisaaa siwezi. Basi nikaanza kujaribu kumpigia simu kumuomba anisamehe lakini sikumpata. Nilituma message nyingi kumwambia namna ninavyompenda na vile ambavyo siwezi kuishi bila Yeye lakini hakunijibu hata moja. Nilikuwa natumia namba za simu za watu tofauti tofauti kumpigia akipokea akasikia sauti yangu tu ana kata. Kuna siku akanitumia message ya matusi makubwa mnoo kiufupi tangu siku ile sikurudia tena tena kumtafuta. Alinitukana lakini aliongea neno moja gumu sana, akasema Wewe ni Malaya una laana kama Mama yako, hauwezi kuolewa wala kudumu kwenye ndoa, siwezi kuwa na Mwanamke mwenye laana hiyo achana na mimi.
Aisee niliacha kulia nikapandwa na hasira, nikajiuliza mara mbilimbili hivi ni Mimi huyu ndio natukanwa hivi au. Hapo hapo nikafuta namba na nikaanza kumchukia kuanzia hapo. Aisee niseme utakavyo, nitukane utakavyo lakini sio Mama yangu, uwii haiwezekani haiwezekani.
Basi nikaanza kuishi maisha yangu, nikawa busy tu na kazi, nikaamua kumuachia Mungu. Na nikajua tu aliyemwambia maneno hayo ni Joyce na Mama yake, maana ndio watu ambao siku zote wamekuwa wakinitukania Mama yangu. Nikaamua kuachana nao.
Kuna siku Baba alinipigia simu akaniuliza vipi Bite yule mchumba wako mmefikia wapi, nikamwambia tumeshaachana. Baba akasema afadhali mwanangu bora mmeachana, nikamuuliza kwanini Baba? Baba akasema nimeshangaa naletewa taarifa eti mchumba wa Bite kampa mimba Joyce nikajiuliza imekuwaje, mchumba wa Bite kumpa mimba Joy imekuwaje.
Baba akasema bora umeachana nae mwanangu, na Joy nimeshamfukuza nimemwambia aende kwa huyo mwanaume pale nisimuone sitaki ujinga. Nikamwambia Baba sio siri nimeumia Moyo sana ila namuachia Mungu. Joyce ameniumiza na sijui ila sitakaa nimtazame usoni.
Baba akaniambia pole mwanangu achana nae endelea na maisha yako yule sio muoaji angekupotezea muda tu. Nikamwambia sawa Baba.
Hiyo habari ilinichoma sana yani. Yani Joyce kutembea na mchumba wangu na mpaka mimba wamepeana na sasa wanaishi wote, sawa. Nikajikuta naanza upya kulia, nililia sana sana. Baadae nikaamua kunyamaza na kuendelea na maisha yangu. Nikawa niko busy na kazi japo moyoni nina maumivu makali sana.
Nikaamua niwe busy na kanisa, nikawa naenda kanisani, naimba Praise angalau ikawa inanikeep busy. Namshukuru Mungu baadae nilipona kabisa na nikawa vizuri kabisa.
Joyce alijifungua lakini yule jamaa baadae wakaachana, jamaa akapata mwanamke mwingine, hivyo Joyce akarudi pale pale nyumbani na mwanae. Nikajiapiza kuwa sitakuja kwenda pale nyumbani tenaa. Baba nitawasiliana nae kwa simu tu au nitamfwata ofisini basi lakini Mimi tena kurudi pale hapana.
Ikapita kama miaka mitatu, nikawa nimepata kazi sehemu nyingine na mshahara ni mzuri tu. Kipindi hicho nimeshasahau yaliyotokea nyuma, nikawa nipo na amani tele.
Pale kanisani akatokea kijana mmoja kunipenda. Huyu kijana alikuwa ni mgeni hapa kanisani, ni mwenyeji wa Shinyanga ila alikuja Dar kikazi, alikuwa ameajiriwa na Bank moja kama Afisa Mikopo (Loan Officer). Alikuwa ni mkaka mzuri, msafi very smart. Huyu kaka akaonyesha kunipenda. Na kuna siku akaomba namba yangu ya simu na hapo hapo tukaanza kuwasiliana. Basi tukawa tunachat, tunaongea, kuna siku akaniomba kunitoa outing, nikakubali, tukaenda kwenye ile Hotel inayozunguka ile pale Posta. Ilikuwa mara yangu ya kwanza kufika pale.
Huyu kaka aliongea maneno mengi jamani, mazuri, akasema ananipenda, Mimi naonekana nafaa kuwa mkewe. Sio siri nilisisimka sikutegemea kusikia haya ninayo yasikia.
Akaniambia naomba ukubali tuanze mahusiano na tuanze process ili tufunge Ndoa, nina kufahamu, nimekufwatilia muda mrefu kidogo nikaona wewe ni binti wa tofauti sana. Nimekupenda na naomba unikubalie tuwe wote.
Weeeh hebu niambie kwa maneno hayo matamu ungekataa 😀😀. Nikajichekesha chekesha pale ila moyoni jibu lilikuwa Ndio hata Leo tuoane 🤣🤣.
Tukaanza mahusiano, mawasiliano ya mara kwa mara, zile za Baby umekula, Baby I miss you, Baby pokea simu, Good night my love ndio zilikuwa zetu. Kiufupi tulizama haswaa, nikaanza kumpenda na Mimi
INAENDELEA………….
1 Comment
Ni nzuri sana uvumilivi ni kila kitu watesi midomo mmmmm. Utukufu kwa Mungu awezae kutenda makuu