HATIMAYE NIMEOLEWA, NGUVU ZA GIZA SIO MCHEZO
Kulikuwa na mwanamke mmoja aliyenipigia simu na kujitambulisha kwa heshima. Aliniambia kwamba alikuwa ameona ushuhuda wa dada Agatha ambaye nilimwombea na baadaye akapata mume na kuolewa nchini Marekani.
Lakini hali yake ilikuwa tofauti kidogo. Yeye ni binti ambaye kwa muda mrefu amekuwa akivutwa na wanaume, lakini wengi wao wamekuwa ni waume za watu. Mara nyingi wamekuwa wakimwomba awazalie watoto kisha wamuahidi kumtunza pamoja na mtoto huyo. Lakini yeye, akiwa na msimamo, amekuwa akikataa kwa kuwa hiyo siyo ndoto wala njia aliyoitamani katika maisha yake.
Pia, vijana wa rika lake wakijitokeza, huwa wanamweleza kuwa wanataka kuwa naye kimapenzi, lakini si kwa ndoa halali wanataka kufanya naye mambo ya ndoa bila kufuata taratibu sahihi. Hilo pia huwa analikataa.
Aliniambia kuwa hajui kwa nini haya yote yanamtokea na hajui afanye nini ili apate ndoa ya heshima na baraka.
Nikaanza kumweleza kwamba hiyo ni dalili kuwa adui amefunga milango ya ndoa katika maisha yake. Kusudi lake ni kumchanganya hadi akubali ndoa isiyo sahihi, ambayo itakuja na majuto.
Tulipoanza kuomba pamoja, pepo wa mizimu kutoka kwao wakaanza kufichuka. Walikiri kwamba wamefunga baraka zake za ndoa na kwamba hawataki avae shela ya harusi maana baraka zake zimefichwa ndani ya ndoa halali.
Baada ya kumaliza maombi na kuhakikisha amefunguka kiroho, nikamwelekeza akatafute gauni la harusi (shela), alivae kisha turudi tena kwenye maombi akiwa amelivaa.
Akalipokea kwa mshangao na kuniuliza, “Mchungaji, nifanye hivyo wakati hata sijapata mume wa kunioa?”
Nikamwambia, “Hilo ni tendo la imani. Fanya hivyo, na Mungu atatenda jambo kabla ya miezi mitatu kupita.”
Kwa kweli, hata mimi nilikuwa nazungumza kwa uongozi wa Roho, maana ya kibinadamu sikuwa na majibu ya kina ya kwa nini alivae shela kabla ya kuwa na mume. Lakini nilitii sauti ya kiroho.
Alitii, akaazima gauni la harusi, akalivaa, kisha tukaingia tena maombi ya baraka na kutangaza maneno ya unabii juu ya maisha yake.
Haikupita hata wiki mbili, wakajitokeza wanaume watatu tofauti, kila mmoja akiwa tayari kwenda kujitambulisha kwa wazazi wake, kulipa mahari, na kufunga ndoa kanisani.
Tukaendelea tena kwa maombi ili tujue kati yao ni nani aliyepangiwa na Mungu kuwa mume wake.
Leo hii, binti huyo ameolewa kwa ndoa halali na amejaaliwa watoto wawili. Mungu ametimiza.
Ninachotaka uelewe ni kwamba: mara nyingi ni vigumu sana kumwelewa Mungu bila kujifunza kutulia na kunyenyekea chini ya uongozi wake. Lakini ukitii na kuwa na imani, utaona mkono wake ukitenda mambo makubwa.
Utukufu wote ni kwa Mungu ambaye anaweza kufanya mambo yote. Alisema: “Niite nami nitakuitika, nami nitakuonyesha mambo makubwa na magumu usiyoyajua” Yeremia 33:3.
Sasa, ikiwa unasoma ushuhuda huu na unahitaji kazi, ndoa, biashara, kibali katika huduma, au umefikia hatua hujui la kufanya akili ya kibinadamu haioni mlango wa kutokea basi karibu tumwite Mungu pamoja.
Je, kuna jambo gumu la kumshinda Mungu?
Kama unaamini kwamba Mungu anaenda kufanya jambo kubwa na lenye ushuhuda katika maisha yako kuanzia sasa, sema Amina kwa imani, na itakuwa hivyo.
Na kila kizuizi ambacho adui ameweka katika njia zako cha kuzuia, kuharibu, au kuchelewesha mafanikio yako – kikavunjike na kuteketezwa kwa moto wa Roho Mtakatifu, kuanzia sasa!