TULICHOMFANYA YULE MCHAWI HATAKUJA KUSAHAU KAMWE
SEHEMU YA 16
Nilifungua ule mlango ulokuwa umefungwa kwa komeo nikatoka nje na kuanza kukimbia kama mwendawazimu.Niliingia kwenye shamba la jirani na hapo kwao Monica lililokuwa na mahindi madogo saizi ya magoti kisha nikalala chini!.Nilishindwa kuelewa mpaka muda huo binti Monica atakuwa yupo wapi maana mlango haukufunguliwa na yeye ndani hakuwepo!.Sasa nilinyamaza kimya ili kuona ni kitu gani kilikuwa kinaendelea.
Baada ya kama dakika 20 hivi,nikawa nasikia sauti ya Monica ikiniita kuashiria kunitafuta,mimi niliendelea kukaa kimya huku nikichukua tahadhari na nilidhani uenda asiwe Monica nikaingia chaka!.Kwa mbali niliona ule mlango wa ile nyumba unagunguliwa mtu akaingia ndani kisha akatoka tena akawa anaita.Baada ya kujiridhisha kwamba alikuwa Monica ndiye aliyeniita,niliamua kusimama na kujipangusa mchanga uliokuwa umenijaa kwenye tumbo na magoti na hii ilikuwa ni baada ya mimi kulala chini!,mpaka wakati huo nilikuwa kama nilivyozaliwa maana nilipokurupuka sikukumbuka hata nguo nimeziweka sehemu gani!
Monica “Uko wapi?”
Monica alijifanya kuniuliza niko wapi kana kwamba alikuwa hanioni,ila nilichoamini mimi ni kwamba alikuwa akiniona tu vizuri!.Niliondoka kuelekea ule uelekeo alokuwa amesimama Monica.
Monica “ulikuwa wapi?”
Mimi “Nilikuwa pale”
Monica “Sasa huku nje umefata nini!?”
Mimi “Wewe ulienda wapi?”
Monica “Mimi mbona nilikuwepo?”
Mimi “Ulikuwepo wakati nimekutafuta sikuoni!?”
Monica “Kuna mjinga mmoja nilikuwa namshikisha adabu”
Mimi “Mjinga gani?”
Monica “Hukusikia napigana na mtu”
Mimi “Mimi sijasikia,nilichosikia ni kishindo kikubwa nyuma huko nageuka nakuangalia na wewe hauonekani,ndiyo nikatoka kukimbia”
Monica “Nilikwambia umughaka nitakulinda usiku na mchana,kuna mjinga alikuja kutaka kunijaribu,nimepambana nae alitaka kunishinda nikamuita mama”
Mimi “Kwahiyo mama yupo ndani!”
Monica “Mama amemchukua amempeleka wakamtengeneze vizuri!”
Basi baada ya kuniambia maneno yale ilibidi tuingie ndani,kiukweli nilikuwa nina hofu sana na nilijilaumu kwanini nimeingia kwenye mahusiano na yule binti,kibaya zaidi siku zilivyokuwa zikienda ndivyo na mimi nilikuwa siambiliki wa kuelezeka kwa yule binti!,ilifikia pointi ambayo nisipokuwa nikimuona nilikuwa ninapata mawazo sana.
Mida hiyo ilikuwa yapata saa 9 usiku na tangia hapo sikupata usingizi tena,ilipofika mida ya saa 10 kuelekea saa 11 ambapo niliona kabisa kama kuna miale ya mapambazuko,nilimwambia anisindikize kurudi nyumbani.
Monica “Mbona unawahi hivyo?”
Mimi “Nadhani unamjua Ema alivyo muongo,na najua kama aliamka kwenda chooni akakuta sipo sijui itakuwaje,lazima tu amwambie Ba’mdogo”
Monica “Yule hawezi kuamka mpaka wewe ufike”
Mimi “Wewe yule humjui vizuri!”
Monica “Basi tufanye kidogo halafu ndiyo uende”
Kiukweli sikuwa kabisa na hamu tena ya mizagamuano ila kwakuwa alitaka sikuwa na namna,ikabidi tulianzishe tena!.Fimbo ziliendelea mpaka sasa nikawa nasikia majogoo yanawika huko nje kuashiria kumepambazuka!.Nilivaa zangu nguo na yeye pia akavaa na safari ya kunisindikiza kwetu ikachukua nafasi.Monica hakutaka kabisa kuniacha njiani,alihakikisha mpaka naingia ndani ndipo na yeye anarudi kwao.
Ilikuwa ni kama kuonekana kwao ni mbali lakini nilipokuwa nikitembea na yeye sikuwahi kuona wala kuhisi umbali wowote,hebu fikiria umbali wa zaidi ya kilometa 6 lakini ndani ya dakika kama 10 mnajikuta shafika!,haya yalikuwa ni maajabu ya binti wa kisukuma Monica.Basi baada ya kuhakikisha nimefungua mlango na kuingia ndani na yeye aliondoka kurudi kwao.
Nilisukuma mlango nikaingia ndani nikakuta Ema bado amelala,sasa sikufahamu aliamka wakati mimi sipo ama la!.Kwakuwa kulikuwa kumepambazuka sikutaka kujiegesha maana niliona ningepitiwa na usingizi,nilijifanya namuamsha jamaa ili nione!.sasa baada ya kumpiga piga na mkono,jamaa alishituka sana!.
Mimi “nimekushitua?”
Ema “Maanangu nilikuwa naota”
Mimi “Ooh,jana ulichoka sana nini!”
Ema “Yaani sijawahi kulala usingizi mtamu kama wa leo”
Mimi “Kumekucha kijana jiandae uende skonga”
Ema “Leo sidhani kama nitaenda”
Mimi “Shida nini?”
Ema “Nahisi kuchoka tu”
Sasa jamaa alikuwa ananieleza huku akiendelea kupiga miayo ya kufa mtu!.Nilipoendelea endelea kumdodosa ndipo nikagundua tangu ule usiku nilipotola hakuwa ameamka hata kidogo!.
Basi kulipopambazuka zaidi nilielekea lamboni kuchota maji ya kuoga na kurejea nyumbani,basi baada ya kumaliza kila kitu niliingia ndani kumsalimia Headmaster na mkewe na kisha mimi kuelekea kwa mzee masumbuko kuchukua miwa ya kwenda kuuza.Sasa wakati unatoka hapo kwa mzee masumbuko ili uikamate njia ya kuelekea Senta,kulikuwa kama na makutano ya njia,njia moja ndiyo njia ambayo ilikuwa inatoka kwenye uwanja unapofanyikia mnada na ukipandisha nayo inakupeleka moja kwa moja kwa kina Monica kule Masairo,njia nyingine ni njia ambayo ilikuwa inakupeleka mpaka lamboni ambako unatokea mpaka shuleni,na njia nyingine ndiyo njia ambayo nilikuwa naipita mimi kuelekea senta kila ninapotoka kuchukua miwa!.
Sasa wakati naikamata njia ambayo ilinipaswa kupita kwa mbele kuna kina mama walikuwa wakija wakiwa wawili,mmoja wapo nikama nilimuona kwenye zile ngoma pale kwao Monica ule usiku!,sasa walizungumza kisukuma halafu wakawa wananitazama sana,nikama walikuwa wananiteta!,waliponipita nilihisi kabisa wanaendelea kunitazama,sasa nilipofika kwa mbele nikautua ule mzigo wa miwa nikajifanya kama naufunga kwa kukaza,nikawaangalia kwa kuibia ndipo nikaona wananitazama na nikama wakawa wanazungumza kwa kubishana!,walipoona nawaangalia wakaondoka huku wakionekana kama kunishangaa!.
Sasa nikabaki namuangalia yule mama ambaye nilimuona ule usiku nikabaki kushangaa tu,kiukweli ukikutana naye hivi kwa mara moja na ukiambiwa mambo anayoyafanya huwezi kabisa kuamini!.Nilijitwisha zangu zigo la miwa na kuondoka huku nikishindwa kuelewa kwanini wale kina mama walikuwa wakiniangalia kwa makini sana!.
Siku hiyo biashara ya miwa ilikuwa mbaya sana,kiukweli tangu asubuhi hadi jioni niliuza pingili tatu tu za muwa,basi kwakuwa nilijua biashara siku zote haifanani sikutaka kujipa presha kabisa,nilipanga Headmaster akiniuliza nitamaambia ukweli ya kwamba biashara imekuwa ndivyo sivyo,basi ilipofika jioni nilienda kupeleka miwa kwa yule mama aliyekuwa akinifadhia na mimi kuondoka kueleke nyumbani,wakati wote nilikuwaga naondoka hapo senta mida ya saa 12 jioni na kufika nyumbani mida ya saa 1 kuelekea saa 2.
Sasa nilipotembea kwa umbali mrefu,huku nikiwa naendelea kuitafakari siku,mara ghafla mbele yangu akatokea yule mzee Makono ambaye pia alikuwa mmoja aa wale watu waliokuwa wakicheza ngoma ule usiku,nilishangaa sana kwasababu eneo nililokutana nae,ndilo aneo ambalo siku ile nilikutana nae na akanitaka nikamsalimie Headmaster,safari hii nilishituka sana mpaka akashangaa!.
Mzee makono “Unishituka nini wewe!”
Mimi “Mzee shikamoo”
Mzee makono “Kwahiyo hujashituka jana leo ujifanye kushituka!”
Kiukweli nilishangaa sana na ghafla uoga mkuu ukaniingia,nilishindwa hata kukimbia nikabaki nimepigwa na bumbuwazi,sasa nilibaki kushangaa kwasababu iliwezekana vipi jana kuniona na wakati Monica aliniambia sababu ya yeye kunipaka ile dawa ni kusudi nisionekane na wacheza ngoma kama adui na wahisi mimi ni mmoja wao!,pili nikajiuliza yeye mzee makono alinionaje?,Sasa wakati naendelea kutafakari nisijue cha kufanya,akaendelea kuniambia kwamba
Mzee makono “wewe na kale kakondefu mmeshirikiana kunitesea mwanangu!,si ndiyo?”
Akaendelea “Nataka leo unitambue mimi ni nani!”
Sikutaka kabisa kumjibu yule mzee nikawa nimebaki kimya kwa bumbuwazi,basi baada ya kuniambia maneno hayo akasonya kwa kufyonza kisha akaondoka!,kiukweli ongea ya yule mzee alionekana kabisa amechukizwa sana na alikuwa na hasira mno!.
Sikufahamu kwa haraka haraka ni kitu gani kilikuwa kimemkasirisha na ni nani aliyekuwa amemtesa mwanaye!.
Basi kutokana na uoga niliyokuwa nao,nikaanza kukimbia ili kuwahi nyumbani,safari hii nilipofika pale kwenye miembe nilipita kwa spidi kali mno kama kipanga na sikutaka hata kugeuka nyuma!.
Sasa nilipofika karibu na nyumbani nilimkuta Monica akiwa amesimama anaongea na Ema.
Ema “Haya huyo hapo ongea nae”
Baada ya kusema hivyo Ema akawa anaelekea ndani!.
Mimi “Kwani kuna nin?”
Monica “Tuondoke hapa”
Mimi “Nakupenda umughaka,nakuomba tuondoke,utajua huko huko”
Basi Monica akanishika Mkono tukaongozana kuelekea nisipopafahamu.Mpaka muda huo hata ndani sikufika kabisa.
Mimi “Tunaenda wapi?”
Monica “Nilikwambia nitakulinda kwa gharama yeyote,huyo mjinga anajifanya
mjanja muache”.
SEHEMU YA 17
Wakati tunaondoka Monica alikuwa amechukia sana na haikuwa kawaida yake,niliwaza sana itakuwaje maana niliona Ema ameondoka kwa hasira kuelekea nyumbani baada ya mimi kufika pale!.Basi nilikuwa mpole huku binti wa watu akiniongoza kuelekea nisikokufahamu.
Mimi “Tunaelekea wapi?”
Monica “Wewe twende acha hayo maswali yako”.
Mimi “Lakini si tunawahi kurudi?”
Baada ya kuona maswali yamekuwa mengi,Monica alisimama akawa ananisukuma sukuma kwa mkono akiniambia “Hivi lini utafunguka hayo macho yako?,hivi wewe unajiona upo kawaida?”
Monica “Huku nimekuja kwa ajili yako,kama unataka hurudi kwenu wewe rudi lakini kitakachokukuta utajua mwenyewe!”
Mimi “kwani kuna nini Moni?”
Monica “Yaani unataka kuwa tahira kama huyo ndugu yako”
Aliendelea “Nishakwambia kila kitu tangu jana kwamba nitakulinda usiku na mchana lakini unajitoa ufahamu!”
Monica “Kama unanipenda na unaniamini twende,lakini kama huniamini rudi kwenu,njia hiyooo nyeupe”.
Monica alikuwa mkali sana baada ya kuona kama namchosha kwa maswali ambayo yeye aliamini kabisa majibu yake uenda nikawa nayafahamu,sikuwa na namna ikabidi nijifanye kondoo niongozane nae kusikofahamika.
Mimi “Mbona jamaa alikuwa amekasirika?”
Monica “Achana nae mjinga yule,itakula kwake”
Monica “Mimi leo nimemueleza ukweli kwamba wewe ni mpenzi wangu”
Mimi ” Siulisema lakini iwe siri Moni?”
Monica “Nimefika pale kwa mambo mengine kabisa,sasa yeye akaanza kuleta mambo yake ya niache kumsumbua,mimi nikamwambia sijaja hapa kwa sababu hiyo,kilichonileta sicho unachofikiria,na kama ni mapenzi kwasasa mpenzi wangu ni umughaka siyo wewe”
Aliendelea “Basi ndiyo kama ulivyotukuta,alipokuona akasema niongee na wewe na kwa hasira akaondoka,sasa mimi ulitaka nifanyeje?”.
Mimi “Ninavyo mjua yule,hatutaongea mwaka mzima”.
Monica “Nimekwambia achana nae,utakipata”.
Basi tulitembea kwa muda mrefu kidogo huku tukiendelea kupiga stori za hapa na pale,yule binti Monica kiukweli mpaka wakati huo nilikuwa nampenda sana toka ndani ya moyo wangu!,na alikuwaga jasiri sana asiyeogopa chochote!.Sasa kwakuwa alikuwa amenihakikishia ulinzi kama mpenzi wake,sikuwa na hofu kama angeweza kunifanyia jambo lolote!.
Baada ya safari ya dakika kadhaa,tuliiacha njia na kuingia kwenye shamba moja kubwa la mihogo,tulitembea mle kwenye lile shamba kwa takribani dakika 2 tukawa tumefika kwenye mji mmoja ambao ulikuwa umezungukwa na mashamba ya mihogo,sasa baada ya kufika pale ghafla nikawaona wanawake watatu ambao kwa haraka haraka sikuweza kuwatambua kwakuwa walikuwa kwa mbali kidogo!.Monica aliniambia nisubiri hapo pembeni na yeye akawa amewafuata wale kinamama na kuanza kuzungumza nao kisukuma.
Sasa ghafla nikaona wale kina mama wananikimbilia na walipofika wakawa wamenishika kwa kunitaka nifanye haraka nisogee walipokuwepo wao.Basi wakamwambia Monica kwa kisukuma kwamba aingie ndani na alete jamvi ili nikalie.Sasa wale kina mama nikawa nimewatambua baada ya kuwa nimewaona kwa karibu,mmoja alikuwa mama yake Monica,na wale wawili walikuwa wale kina mama ambao nilionana nao njiani wakati natoka kuchukua miwa kwa mzee masumbuko ile Asubuhi,kumbuka hao wote akiwamo na mama yake Monica walikuwa ni miongoni mwa watu waliokuwa wakicheza ngoma ule usiku pale kwao Monica.
Sikuelewa kwa nini Monica alinipeleka pale na sikufahamu ni kitu gani kilikuwa kikiendelea!.Baada ya lile jamvi kuletwa na kuwekwa chini,mama yake Monica akaniambia nisimame na nivue nguo zangu zote nibaki kama nilivyozaliwa!.Basi ikabidi nifanye kama alivyoniambia.
Sasa baada ya kumaliza kuvua nguo,akaniambia nikae pale katikati ya jamvi;Mama mmoja kati ya wale niliokutana nao ile asubuhi nikaona anachukua maji kwenye chungu akawa anakunywa kwa kupiga fundo kisha ananitemea,alinitemea yale maji mwili mzima mpaka yalipomalizika kwenye kile chungu!.Baada ya hilo zoezi la kutemewa maji walinizunguka wote wale kina mama akiwemo mama Monica wakaanza kunipaka vitu ambavyo sikuelewa ilikuwa ni kitu gani,harufu yake haikuwa nzuri kiukweli na nilibaki kushangaa tu!.
Waliendelea kunipaka kwa haraka na walipomaliza,mama mmoja akaniambia nisimame.Sasa baada ya kusimama yule,yule yule mama ambaye ndiye alikuwa akinitemea yale maji,niliona mkononi ameshika kitu kama usinga wa mnyama na akaanza kuchovya ule usinga kwenye chungu kiingine kilichokuwa pembeni akawa kama ananichapa na ule usinga uliojaa yale maji aliyokuwa akichovya kwenye kile chungu.
Wakati anaendelea kunitandika na ule usinga alikuwa akinuia kwa kisukuma.
Sasa baada ya lile zoezi la kuchapwa na usinga,mama yake Monica alimwambia binti yake aingie ndani awashe kibatari alete,baada ya kuletwa kile kibatari kukawa angalau na mwanga pale nje,sasa mama yake Monica akanisogeza kwa pembeni kulipokuwa na jiwe lilikuwa lichongwa kama kigoda akaniambia nikae.(Lile jiwe nadhani ni yale mawe ambayo huwa wanasagia nafaka kama mtama,udaga, na ulezi,lilikuwa ni jiwe fulani ambalo lilikuwa limekaa kama bakuri).
Basi baada ya kukaa hapo akaanza kunichanja kwa kisu kilichokuwa kikali mithili ya wembe,amenipiga chale za kutosha karibia mwili mzima.Baada ya kumaliza lile zoezi nikatakiwa nikae kwanza uchi ili niendelee kukauka kisha ndipo nikatakiwa kuvaa nguo.Sasa baada ya kuwa nimemaliza kuvaa nguo ndipo mama yake na Monica na wale kina mama wakaanza kuzungumza na mimi,kile kitendo kilikuwa ni kitendo cha haraka sana ambacho hakikuchukua hata saa nzima!.
Mama Monica “Mkwe wangu hujambo mwanangu”
Mimi “Sijambo mama,shikamoo”
Mama Monica “Maraba mwanangu”
Mama Monica “Baba huu ulimwengu una watu wabaya sana,lazima tukulinde mwanangu”.
Basi mimi nikawa nimetulia tu sikusema jambo lolote,mama yake Monica akaanza kuongea na mwanaye kisukuma na nadhani alimwambia aniambie kilichokuwa kinaendelea!.
Monica “Umughaka dhumuni la mimi kukuleta huku kama nilivyokwambia ni kukulinda mpenzi wangu,sitaki baya lolote likukute kwasababu nakupenda na wewe ndiye mama yangu anataka unioe!”
Aliendelea “Unakumbuka kile kishindo cha jana kilichofanya mpaka ukakimbia?”
Mimi “Ndiyo,nakumbuka!”
Monica “Basi yule mtu alikuwa ametumwa na baba yake ili waje kukuchukua,ndipo nikamuwahi kupambana nae kabla hajaleta madhara,sasa aliponizidi nguvu nilimuita mama yangu akaja kunisaidia na akawa ameondoka naye”
Aliendelea “Sasa lile jambo limeleta shida kwa huyo mshirika mwenzao na mama na kuna vita inaendelea”
Kiukweli nilikuwa nimekodoa macho huku nikiendelea kusikiliza kinaga ubaga ile stori ya Monica ambayo nilikuwa hata siifahamu.
Monica “Kuna mzee mmoja ambaye naye jana alikuwa akicheza ngoma na hutoweza kumfahamu,sasa yule mzee kumbe wakati wakiwa kule miembeni alimuagiza mwanaye aje akuchukue akupeleke kwake wakakufanyie michezo yao”.
Aliendelea kusema “Sasa baada ya yule mzee kuona mwanaye amedhibitiwa alikasirika sana na mama anasema walikaa kikao wakamtaka atoe sadaka kwa kufanya lile jambo kwa mshirika mwenzie”.
Monica “Sasa yule mzee alisema kwa wenzie kwamba anataka aisambaratishe nyumba ya mwalimu na lazima awapeleke mbele ya kamati iliyomuagiza sadaka nyinyi nyoote ingawaje alitumwa mtu mmoja tu kama fidia”
Sasa baada ya kusema yale maneno nilishituka sana na ndipo akili yangu ikafunguka kwa haraka sana!,kwa haraka nikamuwaza uenda atakuwa ni mzee makono kwasababu ndiye niliyekutana naye akawa amenipa vitisho vingi kuhusu tulichomfanyia mwanaye!,pia nikajua uenda atakuwa ndiye maana usiku nae alikuwa miongoni mwa wacheza ngoma pale kwao Monica!.
Mimi “Kuna mzee mmoja anaitwa Makono,je mama mnamfahamu?”
Baada ya kuuliza vile lile swali wakashituka sana na mama yake Monica akaniambia “Unamjua mzee Makono?”
Mimi “Ndiyo mama”
Mama yake Monica “Ndiyo huyo huyo anataka kukutoa sadaka mwanangu,sitakubali!”
Basi wakaanza kuzungumza kwa kisukuma huku wakionekana kusikitika!.
Mimi “wakati natoka senta nimekutana naye jioni akanitisha sana kuhusu mwanae”
Mama Monica “Ndiyo maana tumekuleta hapa maanangu tukutengeneze vizuri,huyo makono ni mtoto mdogo sana kwetu,nitamshughulikia”.
Basi kwakuwa hali haikuwa nzuri siku hiyo kutokana na Makono na genge lake kupanga kwenda kufanya uhalifu wa kichawi pale nyumbani,mama yake Monica na wale kina mama wakaniambia leo sipaswi kabisa kukanyaga pale nyumbani na nitalala hapo kwa hao kina mama mpaka asubuhi!.
Mimi “Je sitaonekana”
Mama Monica “Baba hapa ni kiboko,hakuna wa kukanyaga hapa”
Aliendelea “Tumekupika na hakuna wa kukusogelea na hata wakija hakuna wa kukuona,ondoa shaka mwanangu”
Mama Monica “Huyu huyu makono tuliyemfundisha kazi anataka kuniulia mwanangu na mkwe wangu?,atanijua mimi ni nani,nitamuaibisha mpaka atajuta”
SEHEMU YA 19
Kiukweli nilikuwa nimechukia sana namna nilivyodharirishwa pale shuleni mbele ya wanafunzi!,sikutaka kuonekana mkorofi na mkaidi,nilifanya kila nilichoambiwa ili mambo mengine yapite!,niliona angalau Ba’mdogo aniadhibu kuliko taarifa za kulala nje ningemfikia baba yangu hakika angeniua kwa kipigo na shule angeweza kuacha kunisomesha nikawa mchunga ng’ombe!.Japo nilifanya kosa la kulala nje bila taarifa lakini nilidhani ile adhabu ya kudharirishwa haikufaa hata kidogo na ilijaa uonevu mkubwa!.
Basi nilianza kutembea kutoka hapo Senta kuelekea nyumbani huku kile kichwa cha cherehani nikiwa nimejitwisha kichwani,kiukweli nilichukia sana lakini niliamua kujikaza mtoto wa kiumwe,niliamini hayo ni mambo ya kawaida tu na yangepita!.Kile kichwa cha cherehani hakikuwa chepesi kama nilivyodhani na ilipelekea nikawa nafika sehemu najitua kichwani nashikiria kwa mikono miwili lakini bado haikusaidia,kwahiyo nilichokifanya ilikuwa nakiweka begani angalau nikawa naona kuna unafuu!
Nilifika nyumbani nikiwa nimechoka sana na kwakweli kuanzia siku hiyo,mimi na Ema tulikuwa kama Paka na Panya,sikutaka kabisa jamaa aniambie chochote wala kunisogelea kwasababu nilimuona ni mnafiki!,mara kibao tu yeye nilikuwa nikimtunzia siri zake lakini jamaa yeye za kwangu hakutaka kabisa kuziweka moyoni.Kitendo cha kumwambia Ba’mdogo nilikuwa natembea na binti Monica tena mbele ya wanafunzi kilifanya nikamchukia sana jamaa!,na nilichoamua ni kwamba kama mbwai na iwe mbwai!.
Haikupita muda Maza mdogo naye akawa ametoka senta,kama kawaida yeye alikuwa akitoka senta alikuwa anaingia kuoga na kusubiri kula,wa kupika sana sana nilikuwaga mimi maana Ema nae alikuwa anajifanya kusoma kila alipokuwa akitoka shule,sasa nilikuwaga najiongeza tu kuingia jikoni kupika ili kuepuka matusi ya Ba’mdogo.
Siku hiyo nilikuwa nimechoka sana na nilikuwa nanuka jasho kwasababu ya zile kazi kuanzia asubuhi hadi ile usiku lakini sikuweza kuyasogelea maji kwasababu niliambiwa na Monica na akanionya nisiguse maji!.
Siku hiyo nililala kwa uchovu sana,namshukuru Mungu palipo pambazuka niliamka nikajiandaa kuondoka zangu senta,sasa nilichofanya nikupiga mswaki tu na kubadili nguo,sikutaka kabisa hata kunawa uso,nilipomaliza niliingia ndani kuwasalimia Headmaster na mkewe!.
Maza mdogo “Wewe unaenda halafu hicho kichwa cha cherehani nani atakipeleka?”
Nikawa kimya kwa muda huku nikiwa natafakari nini cha kujibu!.
Headmaster “Kwani kichwa cha cherehani sikuhizi unakileta nyumbani?”
Maza mdogo “Juzi sinilikwambia wanasema yule mama Mayala aliwahi kuibiwa kichwa cha cherehani pale kibandani kwake,unadhani chanzo cha Mama Mayala kuacha kushona ni nini?”
Headmaster “Sasa kwanini usiwe unamuomba mama Rebecca unakiacha pale nyumbani kwake kuliko kupata kazi ya kukileta huku!”.
Maza mdogo “Ngoja nitajaribu kuongea nae!”.
Headmaster “Wewe nenda uwahi kwenye shughuli zako bhana!”
Maza mdogo “Sasa nani atanisaidia kukipeleka senta”
Headmaster “Utakamata hapo mwananfunzi akusaidie”
Sasa mimi sikutaka kabisa kuonekana uenda nilichukia kukibeba kile kichwa,niliamua kujikaza na kumwambia ningekifata baada ya kupeleka miwa senta.
Mimi “Haina shida mama ngoja nikachukue miwa nipeleke senta halafu narudi kukichukua”.
Maza mdogo “Sawa,uwahi sasa”
Sasa nilidhani uenda Headmaster alivyokuwa amemshauri ya kwamba angekamata pale shuleni mwanafunzi amsaidie kubeba kile kichwa na kukipeleka Senta angekubaliana nae lakini haikuwa hivyo,kitendo cha kuniambia niwahi kurudi kukibeba ilionyesha kabisa alifurahishwa na mimi kwenda senta na kurudi kukibeba!.Basi sikuwa na hiyana mtoto wa kiume nikaondoka zangu kuelekea kwenye mashamba ya mzee Masumbuko kwa ajili kufata miwa kama kawaida,ingawaje miwa iliyokuwepo haikuisha ila niliona ni heri nikakusanya ikawa mingi ili inipunguzie safari ya kila siku kuamka asubuhi na mapema kisa kuwahi miwa!.
Nilipofikisha ile miwa pale senta niliibwaga chini nikaondoka zangu kurejea nyumbani kwa kukimbia ili kuwahi kurudi!,sasa kuna sehemu nilifika nikamuona dogo mmoja akiwa kwa mbele kabeba kile kichwa cha cherehani huku Maza mdogo akiwa nyuma yake,nilipowafikia nilimwambia dogo anipe kile kichwa nimsaidie na yeye arudi shule!.
Nilijifanya kuchangamka na kutabasamu kiunafiki lakini kiuweli nilikuwa nimechukia sana,nikawa najiuliza kama alikuwa anajua angempatia mwanafunzi amsaidie kubeba kwanini alitaka nirudi tena?,kama kawaida yangu sikutaka maneno na mtu nikaamua kufunga bakuli langu ili mwanaharamu apite.Wakati huo kiukweli nilikuwa nimeanza kupoteza nuru ya muonekano wangu kwasababu ya kushinda kule senta wakati mwingine sili kabisa mchana na chakula nilikuwa nakutana nacho usiku tu!,mara nyingi nikiwa pale senta nilikuwa nashindia sana miwa!.
Tulifanikiwa kufika senta na nikakipeleka kile kichwa kwenye kibanda alichokuwa akishonea na mimi kwenda mpaka kwa yule mama ambaye nilikuwa nikilaza ile miwa,niliichukua nikaenda kuinganisha na ile niliyokuwa nimekuja nayo na kuanza kuuza!.Namshukuru Mungu siku hiyo niliuza sana ile miwa,japo haikuisha lakini mpaka kufika mida ya saa 10 alasiri ikawa imepungua kwa kiasi kikubwa!
Sasa nikiwa naendelea kuuza miwa yangu pale,kwa mbali nikamuona yule binti Mwise akiwa na binti mmoja wakiwa wamevaa sketi za shule na tisheti za kawaida wakiwa wanakuja hapo senta, sikufahamu kilichokuwa kimewaleta uenda walifata mahitaji kama watu wengine!.
Yule binti kiukweli ndiye alikuwa binti wa kwanza kwa hapo kijijini kuumiza na kuutesa moyo wangu,nilikuwa nampenda na kumtamani sana kutokana na shepu yake nzuri!,ila baada ya kuanza kutembea na Monica kiukweli upendo na matamanio yangu kwake yakaanza kupungua kwa kasi ya ajabu!.Walipofika karibu waliingia kwenye duka moja wakanunua kilichowaleta kisha wakatoka wakawa wanaelekea kwenye vibanda na maduka ya mbele ambako huko pia ndiko mama mdogo anakofanyia shughuli zake,sasa baada ya kugeuka na kutazama uelekeo niliokuwepo mimi,nikampiga mkono kwa ishara ya kwamba aje!.
Mwise “Narudi!”
Kwakuwa aliniambia anarudi nikasema ngoja nisubiri.Safari hii sikutaka kabisa kuwa na kimuhe muhe kwasababu sikuweza kujificha na ile biashara yangu na yeye alifahamu kabisa nilikuwa muuza miwa!,niliamini kama ni kumpata basi ningempata tu na kama ni kumkosa basi ningemkosa vilevile!.
Haukupita muda wakawa wanarudi na huyo mwenzie,sasa alipofika pale kwenye eneo langu la biashara akaanza kama kuonyesha nyodo na dharau.
Mwise “Nionjeshe muwa rafiki yangu!”
Mimi “Kwahiyo mimi leo nimekuwa rafiki yako?”
Mwise “Jamani!,kwani kuna ubaya wewe kuwa rafiki yangu?”
Basi nikamkatia pingili mbili za muwa yeye pamoja na mwenzie!,basi wakawa wanazungumza na huyo rafiki yake maneno ya kisukuma huku wakicheka kwa kicheko cha kichini chini!,kiukweli walikuwa wanikiteta kwa kisukuma na ishu kubwa walikuwa wakizungumzia zile stiki nilizokuwa nimelambwa na Headmaster mbele ya wanafunzi!,wao walidhani siwaelewi lakini hata kama sikuelewa kisukuma vizuri mtu alikuwa akiteta inafahamika kabisa!.
Walipomaliza kukwangua kwangua miwa kwa kisu akawa ameniambia wanaondoka kuwahi kurudi nyumbani,nikawa nimemuomba anivumilie angalau kwa dakika mbili nizungumze nae!,sasa yule mwenzake akawa amemwambia atamkuta mbele!.
Mwise “Sasa na wewe unaniacha nyanoko”
Mwenzie “Utanikuta mbele bhana”
Mwise “Mmh!,niambie mi nina haraka”
Mwise “Kwahiyo Mwise Ombi langu vipi lakini?”
Mwise “Ombi gani tena jamani”
Mimi “Kwani mara ya mwisho mimi na wewe tuliongea nini?”.
Mwise “Siulianimbia unanipenda,nashukuru kwa kunipenda”
Mimi “Usinifanyie hivyo Mwise”
Mwise “Wewe si unaye mwanamke wako”
Mimi “Mwanamke gani tena jamani!?”
Mwise “Wewe ema kaniambia habari zako nyingi tu!,kumbe ulikuwa tu unataka unilale uniache”
Mimi “Daaah!,hebu achana na mambo ya Ema Mwise,Ema anashida kubwa na wewe yule unamfahamu akili yake”.
Mwise “Mimi nachelewa bhana,kesho!”
Basi yule binti alianza kukimbia kumfuata mwenzie aliyekuwa akimsubiria.Niliamini kabisa kwa kilichotekea pale shule ukichanganya na uongo wa Ema,haikuwa rahisi mimi kumpata tena yule binti.Niliamua kujipa moyo ya kwamba mademu mabaya siku zote ndiyo yanayoringa lakini kuna muda bado nilikuwa nikifikiria kiuno cha yule binti na kuwaza kinavyo chakatwa na wanaume wengine,kiukweli nilikuwa naumia sana!.
Sikuwa na namna ilibidi niwe tu mpole ili maisha yasonge!.
Baada ya kukamilisha siku ya uuzaji wa miwa niliamua kurudi nyumbani na namshukuru Mungu safari hii sikurudi na kichwa cha cherehani kwasababu maza mdogo alipata pa kukiweka hapo senta.
Sasa nilifika nyumbani mida ya saa 1 usiku,nilielekea lamboni ile usiku kuchota maji ili nije nioge kwasababu nilikuwa sijaoga tangu jana yake!,sasa nilipotoka bafuni kuoga,nikawa nimeingia ndani kwa ajili ya kupaka mafuta!,sasa wakati napaka mafuta nikasikia kuna mtu ananipiga piga mgongoni kwa mkono akiashiria nigeuke!,sasa ile nimegeuka nikawa nimekutana na Monica uso kwa uso!.
Kiukweli nilishituka sana ila akanifanyia ishara ya kidole mdomoni akinitaka nisipige kelele wala kuongea!.
Mimi “Monica kuna nini mbona huko humu”
Monica “Vaa nguo tuondoke”
Mimi “Tuondoke twende wapi tena!?”
Monica “wewe vaa twende”
Mimi “Tunarudi lakini?,maana mwenzio jana jana nimepigwa kwasababu yako”
Monica “Hatuendi mbali tutakuwa nje hapo”
Basi baada ya kuvaa nguo,Monica akawa amenishika mkono na ghafla tukawa nje ya nyumba kwa pembeni kidogo.
Monica “Tusogee pale kwenye lile jiwe!”
Baada ya kufika pale kwenye lile jiwe akanitaka tukae pale na kuna watu tuwasubiri walikuwa wanakuja!.
SEHEMU YA 20
Basi wakati tukiwa tumekaa pale kwenye lile jiwe,ghafla wakawa wametokea wale kina mama wawili ambao juzi yake tu nilitoka kwao kupigwa chale!.Walifika pale kwa ghafla sana na wakanitaka nisimame!.Baada ya kusimama, mama mmoja wapo akaniambia nivue nguo ili nipakwe dawa,sikutaka kabisa kupoteza muda nikaanza kuvua nguo na wakaanza kunipaka dawa kwa haraka sana!.Walipomaliza wakawa wamekaa kimya kwa muda kidogo.
Mimi “Kwani kuna nini?”
Monica “Shiiiiiiiiiiii,nyamaza”
Monica alinifanyia ishara ya kidole mdomoni kwamba ninyamaze na aliniambia kwa sauti ndogo sana.Sasa baada ya muda kidogo kupita mama mmoja akamwambia Monica kwa kisukuma aniambie kila kitu!.
Monica “Mpenzi wangu umughaka,unaniamini?”
Mimi “Ndiyo,nakuamini”
Monica “Sasa hawa mama zangu wadogo siunawakumbuka?”
Mimi “Ndiyo,Hawa si ndiyo wale wa juzi?”
Monica “kumbe una kumbukumbu,sasa ni hivi!,mama yangu kawatuma kuja kukusaidia maana kuna kikao kilikuwa kinaendelea kwa yule mzee mshenzi(Makono)na washirika wenzie ya kwamba leo unapaswa ufe!”
Mimi “Kwanini nife Monica!?”.
Kiukweli nikaanza kupaniki na amani ikaanza kunitoweka!.
Monica “Yule mzee nilikueleza alipewa adhabu ya kutoa kafara kwasababu alivunja mashariti ya kumtuma yule mwanaye pale nyumbani kwetu akifahamu kabisa mama yangu ni mmoja wapo,sasa hasira zake amehamishia kwangu na kwako,hivyo ndiyo maana nilikwambia nitakulinda usiku na mchana mpenzi wangu!”
Mimi “Kwahiyo tutakaa hapa mpaka asubuhi hawezi kutuona?”
Monica “Hapa tunamsubiri mama afike kwanza atupe maelekezo”
Mimi “Sawa”
Tulikaa pale kwenye yale mawe mimi na Monica wakati huo wale kina mama wakiwa wamesimama!.Haukupita muda ghafla mama yake Monica akawa amefika pale tulipokuwepo.Monica alisimama akamuinamia mama yake kwa heshima na unyenyekevu ikiwemo pia wale kina mama.
Mama Monica “Mwanangu hujambo?”
Mimi “Sijambo mama,shikamoo”
Mama Monica “Marhaba mkwe wangu”
Mama Monica “Sasa hebu shika hii”
Alinipatia kitu kama kibuyu kidogo sana ambacho sikuelewa ndani kulikuwa na kitu gani!.
Mama Monica “Nenda ndani utakiweka pembeni ya mlango chumbani unapolala,sawa?”
Mimi “Sawa mama”
Mama Monica “Ukishaweka hurudi hapa,fanya haraka”.
Niliondoka kuelekea ndani ambako nilipofika sikumkuta mtu nje!,basi niliingia ndani nikakiweka kile kibuyu kisha nikatoka nje!,sasa nadhani baada ya kuurudishia ule mlango Headmaster alisikia.
Headmaster “Wewe leo huli?”
Mimi “Nakuja kula baba”
Maza mdogo “Njoo uchukue hili bakuli ukaongeze mboga umughaka”
Basi niliamua kwenda sebuleni na nikawakuta wakiwa wanakula!.Nilichukua lile bakuli nikaingia jikoni kupakua mboga kisha nikarudi sebuleni kula haraka ili niondoke niende kwa mama yake Monica aliyekuwa ameniambia niwahi kurudi!.
Maza mdogo “Uliondoka saa ngapi leo!,nimewahi kufunga ili tuongozane sikukuona”
Mimi “Mimi niliwahi mama baada ya kuona giza limeanza”
Headmaster “Kwani ulikuwa wapi?,mbona mwenzio anasema hukuwepo?”
Mimi “Nilikuwa hapo nje baba”
Headmaster “Mbona tumekuita na hukuitika?”
Mimi sikutaka kujibu kitu nikaamua kukaa kimya ili kuepeusha mambo mengi!.
Headmaster “Biashara inakwendaje?”
Mimi “Leo angalau kidogo nimeuza uza”
Kiukweli wakati huo nilikuwa naona kama wananichelewesha kuondoka kwenda nje,baada ya kupiga matonge kadhaa ya ugali nikaamka nikasema nimeshiba!.
Headmaster “Leo ulikula wapi bhana”
Mimi “Sijala sehemu baba nahisi kushiba”.
Headmaster “Hivi mchana huwa unakula wapi?”
Mimi “Huwa nashindia miwa tu pale kijiweni”.
Headmaster “Aya bhana”
Niliamka nikanawa kisha nikatoka nje kujifanya kama najikoholesha pale kisha nikafungua mlango na kutoka nje ya nyumba.Nilitembea kwa haraka kuelekea nilipokuwa nimewaacha kina Monica,nilipofika nilimkuta Monica akiwa peke yake,wale kina mama pamoja na mama yake Monica sikuwaona.
Monica “Ila wewe nae kuna muda unakera sana”
Mimi “Sasa nakera nini Moni!”.
Monica “Mama alikwambia uende uwahi kurudi wewe umefika ukaamua kukaa!”
Mimi “Haikuwa rahisi Moni kama unavyodhani”
Monica “Hebu tuachane na hayo,shika hii hapa ulambe na hii uweke mfukoni.”
Monica alinipatia kitu kama unga ulokuwa mweusi kama mkaa nikalamba kisha akanipatia kitu kilichokuwa kimefungwa kwa kitambaa kidogo cheusi akanitaka niweke mfukoni.
Mimi “Mama anarudi?”
Monica “Arudi huku kufanya nini?,wao ndiyo wameondoka hivyo!”.
Monica “Naomba unisikilize kwa makini umughaka”
Aliendelea “Utakachokiona leo usipige kelele na ikawe siri yako,mimi nipo na wewe na nikizidiwa nitamuita mama atatusaidia”
Mimi “Sawa”
Monica “Twende”
Basi tuliondoka kuelekea ndani ya nyumba yetu nikiwa nimeongozana na Monica,sasa nilipofungua geti kuingia ndani ghafla sikumuona,nikabaki kushangaa tu na kujiuliza atakuwa ameleekea wapi kusiko julikana,sasa kwakuwa nilifahamu alikuwa na uwezo mkubwa niliamini ametoka mara moja na angerudi!.Nilipoingia hapo uwani nilimkuta Ema anafua soksi zake za shule na kufuta futa viatu vyake!,kwakuwa sikuwa na stori nae nikaingia zangu ndani!.
Nilipoingia tu chumbani Ghafla nikamuona Monica akiwa amesimama kwenye ile kona ambayo niliweka kile kibuyu!,alinifanyia ishara ya kunyamaza!.Sasa jamaa alipomaliza shughuli zake aliingia ndani akaanza kusoma,mimi niliamua kujilaza kitandani wakati huo namuona Monica huku Ema yeye akiwa haoni kitu chochote!.Sasa baada ya kupiga buku kwa dakika kama ishirini niliona anarudisha madaftari kwenye mfuko kisha akazima ile taa akapanda kitandani kuja kulala!.
Baada ya jamaa kulala,Monica alinisogelea kitandani akanishika mkono akanisogeza kwenye ile pembe aliyokuwepo yeye akanitaka nikae kimya!.
Tulisimama kwa muda mrefu kidogo ndipo nikasikia kuna vishindo hapo uani kama miguu ya watu!,na kwa vishindo vile yaelekea walikuwa watu zaidi ya wawili.Monica akaniambia nitulie tuli kwani hakuna ambaye angetufanya chochote.Kiukweli nilikuwa nina jiamini kupita maelezo kwa wakati huo!.
Haukupita muda nikaona mlango unasukumwa,waliingia watu wanaume wawili waliokuwa uchi ambao sikuwa nikiwafahamu,basi Monica akanitaka nitulie kabisa!,wale jamaa wakaenda mpaka pale kitandani wakawa kama wanashangaa!,basi mmoja akatoka nje,haukupita muda akawa ameingia na mzee mmoja ambae nilimfahamu alikuwa yule mzee makono!.
Yule mzee alisogea mpaka pale kitandani kisha nikaona anaangalia kwa kushangaa na yeye pia!.
Jamaa “Ndiye huyu?”
Makono ” Siye huyu”
Makono “Mchukueni huyu tuondoke”
Basi nikaona wale jamaa wanamuamsha Ema akaamka,Ema aliamka akiwa kama mlevi aliyepoteza kumbukumbu kabisa!.Walimtoa nje Ema na ndipo Monica akaniambia tutoke nje na nihakikishe kile kibuyu kidogo alichonipatia mama yake nakibeba!,basi tulipotoka nje tukakutana na grupu la watu wengine kama watano akiwemo Headmaster ambao walikuwa kama wamewelewa pombe na hawakuelewa kitu chochote!.
Wale jamaa wawili mmoja alikaa mbele na mwingine nyuma huku wa mbele akitoa ishara kwamba waondoke,sasa yule wa nyuma alikuwa akiwapiga wale watu akiwemo Headmaster na walisimama wakatoka nje!.Sikumuona tena mzee makono hapo nje kwa wakati huo na sikufahamu alikuwa amekwenda wapi!.
Monica “Twende”
Mimi “Tunaenda wapi?”
Monica “wewe twende”
Basi tukaanza kuwafatilia wale watu wakiwa wanapelekwa kusiko julikana!.
INAENDELEA…….