NILIYOYAONA NYUMBANI KWA RAFIKI YANGU KIPINDI NASOMA
Niliwahi kwenda kutembea nyumbani kwa rafiki yangu kipindi nikiwa shule ya msingi. Tulikuwa tumemaliza vipindi vya mchana na kwa vile hakukuwa na kazi nyingi shuleni siku hiyo rafiki yangu alinialika kwao. Nilipofika nilivutiwa sana kwao kulikuwa pazuri pamepangwa vizuri na kulikuwa na bustani yenye maua ya kuvutia. Ilikuwa mara yangu ya kwanza kufika huko na nilihisi furaha ya kipekee.
Tulicheza, tukacheka, na tukapiga stori za kitoto mpaka jioni ilipokaribia. Ghafla nikiwa nipo kwao kabla sijaludi nyumbani mvua kubwa ilinyesha kabla sijajitayarisha kurudi nyumbani. Rafiki yangu na familia yake walinikaribisha nikae hadi mvua iishe pia nilale pale na kuniambia watawasiliana na wazazi wangu kua nipo kwao.
Nilipokuwa ndani nikaanza kuona mambo ya ajabu. Vitu vidogo vilianza kusogea vyenyewe taa zilikuwa zinawaka na kuzima bila kuguswa na mara kwa mara nilihisi kama kuna mtu ananitazama kutoka nyuma ya pazia.
Nilipojaribu kumuuliza rafiki yangu kuhusu hali hiyo, alitabasamu kwa aibu na kuniambia, “Usijali, umezoea sana kwao tu, huku ni kawaida.” Lakini usiku huo sikulala nilikaa macho karibu usiku mzima nikihisi sauti za ajabu na hatua zisizoonekana.
Usiku ulizidi kusonga huku mvua ikiendelea kunyesha kwa nguvu. Nilikuwa nimelazwa kwenye godoro karibu na kitanda cha rafiki yangu, lakini usingizi haukuja. Nilikuwa macho nikitazama dari nikisikiliza kila sauti kwa makini. Mara kwa mara nilihisi upepo wa baridi ukipita licha ya madirisha kufungwa. Ilikuwa kama kuna kitu kilikuwa kikitembea ndani ya ile nyumba kimyakimya.
Karibu na saa sita za usiku nilisikia mlango wa stoo ukifunguka polepole kwa mlio wa kukereketa. Nilijaribu kumwamsha rafiki yangu lakini alikuwa amelala fofofo. Nikanyanyuka kwa tahadhari nikasogea taratibu mpaka sebuleni.
Mlango wa stoo ulikuwa wazi kidogo na ndani yake kulikuwa na giza nene lisilopenywa hata na mwanga wa taa ya korido Yani kiufuupi usingeweza kuona chochote kile kwenye hicho chumba cha stoo.
Ghafla kitu cheusi kilionekana kikining’inia juu ya dirisha la stoo. Kilikuwa kama kivuli cha mtu lakini hakikuwa na uso. Kiliyumba yumba polepole kana kwamba kinavuta pumzi nzito halafu ghafla kikaingia ndani ya stoo na mlango ukajifunga kwa kishindo.
Nilihisi miguu ikinikataa. Nilirudi chumbani kwa haraka huku moyo ukidunda kwa nguvu. Niliingia chini ya blanketi na kujifunika mwili mzima, nikitetemeka. Nilijua kabisa sikuwa nimeota. Kulikuwa na kitu kisicho cha kawaida ndani ya ile nyumba.
Asubuhi ilipofika mvua ilikuwa imekoma. Nilijifanya niko sawa na nikamwambia rafiki yangu kuwa natakiwa kurudi nyumbani haraka. Nilipotoka nje na kuvuta pumzi ya hewa safi, nilihisi kama nimeondoka mahali pa giza zito na siku hiyo nilijiambia kamwe sitarudi tena kulala kwao.
Lakini hadi leo, bado huwa najiuliza kile kivuli kilikuwa nini? Na je, familia ya rafiki yangu wanajua kuwa wanaishi na kitu kisichoonekana?
Mimi kwakweli niliacha kutamani maisha ya watu wengine kuanzia kipindi kile Yani naogopa sana watu wenye maisha ya kifahari na haujui kuhusu mali zao.