𝐍𝐈𝐋𝐈𝐌𝐓𝐄𝐒𝐀 𝐌𝐓𝐎𝐓𝐎 𝐖𝐀 𝐊𝐀𝐌𝐁𝐎 𝐁𝐈𝐋𝐀 𝐊𝐔𝐉𝐔𝐀 𝐍𝐈 𝐌𝐖𝐀𝐍𝐀𝐍𝐆𝐔 𝐍𝐈𝐋𝐈𝐘𝐄𝐌𝐓𝐔𝐏𝐀𝐆𝐀 𝐌𝐒𝐈𝐓𝐔𝐍𝐈 𝐊𝐈𝐏𝐈𝐍𝐃𝐈 𝐂𝐇𝐀 𝐍𝐘𝐔𝐌𝐀
Episode 21
Baada ya kumaliza kunywa maji, Kareem akamtazama mke wake na kumwambia;
“Ni kwa sababu wewe ni mke wangu vinginevyo nisingekubali kwamba Majaliwa sio mwanangu. Ni kweli kabisa Majaliwa sio mwanangu wa damu ila nilimuokota msituni akiwa mtoto mchanga. Mpaka sasa najiuliza inawezakana vipi niliweza kukuoa mwanamke mwenye roho ngumu kama wewe? Mwanamke mwenye
roho ya kikatili isiyo na utu ndani yake? Hivi ulipata ujasiri gani wa kuweza kumtelekeza pale msituni mwanao uliyemzaa kwa uchungu? I swear, kama ningejua ulishawahi kufanya tukio la kinyama kiasi kile basi nisingekuoa Radhia. Nina mashaka sana na historia ninayoijua mimi kuhusu maisha yako. Ni wazi kabisa ulinidanganya Radhia. Naamini kabisa mpaka sasa sina chochote ninachokijua kuhusu wewe na huenda hata jina lako umenidanganya.” Kareem aliongea maneno hayo kisha akapiga hatua kichovu akakaa kitandani.
Mwili mzima ulinyong’onyea kwa uchovu wa ghafla kufuatia kile kilichokuwa kinaendelea. Mawazo yalikuwa mengi sana kichwani kwake baada ya kugundua ukweli kwamba Radhia ndo mama mzazi wa
Majaliwa. Radhia alitambaa kwa chini kwa magoti mpaka akamfikia Kareem pale kitandani. Alipomfikia akamshika miguu kisha akamwambia;
“Mume wangu, Ni kweli ile historia niliyokuambia kuhusu mimi haina ukweli wowote. Kitu pekee
unachokijua kuhusu mimi ni jina langu tu ila mengine yote ya nyuma hauyajui. Naomba unisamehe sana kwa kukudanganya mume wangu. Nilifanya hivyo kwa sababu ya kutafuta afueni ya maisha. Huko nyuma nilipitia kipindi kigumu sana katika maisha kiasi kwamba nilikosa tumaini la kuishi. Nilipoteza wazazi wangu nikiwa mdogo hivyo nikalelewa na Bibi yangu. Bibi nae alikuja kufariki nikiwa na umri wa miaka 16 naelekea 17. Tangu kipindi hiko maisha yangu yalikuwa magumu sana kwa kuwa sikurithi chochote zaidi ya jina la ukoo. Kula na kuvaa yangu ilikuwa ya shida sana lakini baadae nikaja kupata ahueni baada ya kupata mchumba. Ni kijana ambaye alijitoa sana kwa ajili yangu. Alinipambania sana kwa kila kitu kama mke wake na alionesha upendo wa dhati kwangu. Maisha yangu mimi yalikuwa mikononi mwake yeye kwa kuwa nilimtegemea kwa kila kitu. Mambo yakaja kubadilika baada ya kunasa ujauzito. Yule kijana akanibadilikia kabisa na kunikana na mimba yangu. Tangu hapo akakata mawasiliano na mimi hivyo akanitelekeza na mimba yangu. Maisha yangu yakawa magumu mara mbili zaidi ya awali. Nilitanga tanga sana na tumbo langu katika suala zima la kutafuta chakula. Ule msemo “Kila mtoto anakuja na baraka zake” Kwangu ulikuwa tofauti kabisa kwani hali ya maisha ilikuwa mbaya zaidi tangu nilipomzaa mwanangu. Sikuwa na uhakika wa kula hivyo hata mwanangu akawa anakosa maziwa ya kutosha. Nilizurura sana na mwanangu kuomba msaada lakini sikupata ule msaada wa kudumu. Hata yule mwanaume niliyezaa nae nilimfuata kwa mara nyingine kuomba msaada wake lakini alinifukuza na tayari alikuwa na mahusiano mengine. Sina uhakika wa kula, mwanangu hapati maziwa ya kutosha, unadhani ningefanya nini mimi? Akili iliyonijia kichwani mwangu ni kuja mjini kutafuta maisha. Niliamua kumtelekeza mwanangu msituni kwenye eneo ambalo nilijua sauti yake ya kilio ingeweza kumpa msaada kwa wapita njia. Nilikuwa na imani kwamba huenda mwanangu atapata familia nzuri ya kumlea na kumtunza. Sikuwa tayari kuona mwanangu anadhoofika na kunifia mikononi mwangu kwa kukosa chakula. Hivyo ndivyo ilivyokuwa mume wangu. Huo ndo ukweli wa maisha halisi niliyopitia. Naomba unisamehe kwa kukudanganya hapo awali. Nilikudanganya wewe, nikamdanganya pia kaka Vonso. Huo uongo ndo umebadilisha maisha yangu mpaka kufikia muda huu maana kama ningesema ukweli basi kaka Vonso asingenisaidia na kunipokea nyumbani kwake mwanamke katili kama mimi.” Radhia alimaliza kumsimulia Kareem ukweli wa mambo yalivyokuwa.
Ni simulizi ambayo ilimpa huzuni Kareem kwa kiasi fulani ingawa bado aliona Radhia hakuwa sahihi kwa uamuzi wake.
“Pole sana mke wangu kwa kupitia magumu lakini bado maamuzi yako hayakuwa sahihi kabisa. Hata muumba wako hakufurahishwa kabisa na uamuzi wako wa kumtelekeza mtoto mchanga ambaye bado alikuwa anakuhitaji mama yake. Hivi unahisi kabisa kama ungebaki na mwanao basi mngekufa kwa njaa? Unaamini kabisa uamuzi wako ndo umewanusuru katika kifo? Kwamba Mwenyezi Mungu aliamua
kubadilisha tarehe zenu za vifo baada ya wewe kuchukua uamuzi wa kumtelekeza mtoto pale msituni? Najua unajua kwamba jibu ni hapana, Hata kama ungebaki Songea na mwanao au ungekuja nae huku Dar es salaam bado mngekuwa hai mpaka sasa. Hakuna kiumbe hai kinachokufa kabla ya siku yake mke wangu. Siri ya kifo anayejua ni Mwenyezi Mungu pekee. Yeye ndo aliyekupa kizazi, akakusimamia ukazaa na yeye ndo angewapa chakula. Kitu usichokijua ni kwamba ulikuwa kwenye kipimo cha imani lakini imani yako ikawa ndogo sana. Mimi kama mume wako na pia kama mwanadamu siwezi kukuadhibu maana tayari Mungu ameshaanza kukuadhibu hapa hapa duniani. Siku zote ulikuwa unamtesa Maja ukijua ni mtoto wa mwanamke mwenzako kumbe ni mtoto wako mwenyewe. Hebu niambie sasa, Unajisikiaje baada ya kujua yule mtoto uliyempitisha kwenye tanuri la moto ni mwanao? Unajisikiaje baada kujua yule mtoto uliyemfanyia kampeni za kumuharibia maisha yake ya kesho ni mwanao? Unadhani yule mtoto atakubali kukuita Mama? Ulimtupa msituni, haikutosha ukaja kumtesa na kumjengea chuki tangu akiwa mdogo mpaka sasa amekua. Vipi utawezaje kufuta makovu ya vidonda vyote ulivyomsababishia kwenye moyo wake? Je unadhani unastahili kuitwa mama kwa sauti yake?”
Maswali yalikuwa magumu sana kwa Radhia kiasi kwamba akabaki amejiinamia huku akilia kwa uchungu.
Episode 22
[SIKU ILIYOFUATA]
Asubuhi ya siku hiyo familia nzima iliketi mezani kwa ajili ya kupata chakula cha asubuhi kwa pamoja. Siku hiyo ilikuwa tofauti kabisa kwa Radhia kwani alionesha upendo mkubwa sana kwa Majaliwa. Picha linaanza Radhia alimpakulia Majaliwa nyama za kutosha huku akimtazama kwa macho ya upendo. Macho ya Radhia hayakuacha kabisa kumtazama Majaliwa kila alipotafuna chakula. Radhia aliweza kuiona taswira ya Tony kwenye uso Majaliwa hivyo akajikuta anazidi kuamini kwamba Majaliwa ndo yule Bahati wake aliyezaa na Tony dereva wa bodaboda. Kadri Radhia alivyozidi kumtazama Majaliwa ndivyo nafsi yake ilivyozidi kumuuma na kujikuta anadondosha machozi. Ni Kareem tu ndo hakustaajabu chozi la Radhia lakini Majaliwa, Fetty na Jemima walishangaa kuona Mama mwenye nyuma anatokwa na machozi. Majaliwa ndo alishangaa zaidi maana yale machozi ni kama vile yalikuwa yanamuhusu yeye. Kuna mabadiliko fulani ya upendo aliyaona kwa mama yake wa kambo tangu jana mpaka kufikia muda ule walipokuwa kwenye
meza ya chakula. Dogo alijiuliza ni kipi kimemsibu mama yake wa kambo, mbona ghafla sana ameanza kumpenda? Au ni kwa sababu anaenda chuo kikuu kusomea udaktari ndo maana ameanza kujipendekeza? Majaliwa alijiuliza hayo maswali lakini hakuwa na uhakika na jibu lake. Wakati wanaendelea kupata chakula, Ghafla nyumba ikaanza kupokea wageni. Mgeni kwanza kufika alikuwa Bibi yake Majaliwa ambaye ni mama mzazi wa Kareem. Ni Bibi ambaye alimlea Majaliwa tangu akiwa mtoto mchanga. Bibi huyo ndo
alimnyonyesha maziwa ya kopo huku akijua ni mjukuu wake kabisa. Zilipita dakika mbili tu tangu Bibi aingie,
Vonso na mkewe pia wakafika pale ndani. Ulikuwa ugeni wa ghafla kwenye macho ya Majaliwa lakini kwa Kareem na Radhia ule ugeni waliutarajia.
“Maja! Kuna kikao cha dharura muda huu kwahiyo hutakiwi kutoka.” Kareem alimwambia Majaliwa maneno hayo baada ya ujio wa wale wageni. Majaliwa alishangazwa na ile taarifa maana hakutarajia kabisa. Kwa namna alivyokuwa anamheshimu
Baba yake ikabidi tu atii amri bila kuhoji chochote. Watu wote pale ndani wakakusanyika sebuleni isipokuwa yule dada wa kazi ambaye alienda jikoni kufanya shughuli zake. Kila mmoja akaketi kwenye sofa kwa ajili ya kikao cha dharura. Kikao kilichoitishwa na Kareem huku wahudhuriaji wakiwa hawajui ajenda kuu ya kikao hiko. Ni Kareem na Radhia tu ndo walikuwa wanafahamu kile kinachotakiwa kuzungumzwa. “Jamani, Nadhani imekuwa ghafla sana kukutana mahali hapa na nafikiri kila mmoja anajiuliza kwanini yupo hapa muda huu. Kipekee kabisa niwashukuru kwa kuweza kufika licha ya kwamba kikao kimekuwa cha kushtukiza. Dhumuni kubwa la kikao hiki ni kuwaomba msamaha nyie wote kama familia yangu kwa kosa la kuwadanganya kwa miaka takribani 22. Nahitaji sana msamaha wako
Mama yangu kipenzi, Mke wangu, Braza Vonso, shemeji yangu hapo na mwanangu Majaliwa. Huyu ndo mtu ambaye nimemkosea sana maana nimemuweka gizani kwa muda mrefu.
Siku ya leo nitaweka wazi kila kitu ili kila mtu aweze kujua ukweli.” Kareem alizungumza maneno hayo na kuwafanya watu wabaki na mishangao.
Shauku zilikuwa kubwa sana kwa kila mtu kujua kosa alilotendewa na Kareem. Kila mtu alitaka kujua huo ukweli uliofichwa kwa miaka mingi ni upi? Kimya kikatawala kwa muda huku wakimsubiri Kareem azungumze kile anachotaka kuzungumza. Kareem akavuta glasi ya maji kisha akayanywa kwa mkupuo. Alipomaliza kunywa akashusha glasi mezani kisha akaanza kuelezea kile kilichomsukuma kuitisha kile kikao. Ni hadithi ya miaka takribani 22 iliyopita ndo ilianza kusikika kutoka kwenye kinywa cha Kareem. Hadithi yenyewe ilikuwa kama ifuatavyo; Ilikuwa yapata majira ya saa 11 alfajiri. Ni siku ambayo Kareem alikuwa akiendesha gari kubwa la mizigo akitokea mkoani Ruvuma katika wilaya ya Songea na kuelekea Dar es salaam. Kioindi hiko Kareem alikuwa dereva wa kampuni ya magari yanayosafirisha mizigo mikoani na nje ya nchi. Kareem alikuwa mwenzake ambaye ndo msaidizi wake wa kazi. Wakati safari inaendelea, Ghafla Kareem akajikuta anasimamisha gari katikati ya pori baada ya kubanwa na haja ndogo. Baada ya kusimamisha gari akateremka na kusogea pembezoni mwa barabara kwa ajili ya kujisaidia. Wakati anajisaidia, Ghafla akasikia sauti ya mtoto mchanga ikitokea kwenye kichaka kidogo kilichokuwa mbele yake. Kareem alishtuka kwa marefu na mapana baada ya kusikia sauti hiyo. Alihisi huenda ni mauzauza tu ndo yanasikika pale kichakani maana sio rahisi kabisa mtoto kuwepo kwenye yale mazingira. Mwanaume akafunga chap zipu ya suruali na kuanza kuondoka lakini ghafla akasimama wima baada ya nafsi yake kusita. Alihisi huenda ni kweli kuna mtoto mchanga ametupwa kichakani hivyo akamuita mwenzake na kumtaka ateremke kwenye gari. Yule mwenzake ambaye alifahamika kwa jina la Steve akateremka kwenye gari kisha wakaongozana huku wakitembea kwa tahadhari mpaka pale ilipokuwa inasikika sauti ya mtoto. La haula! Mtoto mchanga aliweza kuonekana kwenye macho yao akiwa peke yake amelazwa chini na kufunikwa kwa vizuri.
“Oya Kareem! Huu mtego tuondoke mwanangu.
“Hapana kaka! Hatuwezi kumuacha hapa huyu mtoto. Ni lazima tumsaidie haraka iwezekanavyo vinginevyo atakufa huyu mtoto.
“Sasa tumsaidiaje Kareem wakati sisi sio Mama yake? Au utamnyonyesha nini ukimchukua? Vipi akitufia kwenye gari itakuaje? Hebu tuwahishe mzigo mjini kaka achana na kesi zisizokuwa na ulazima maana tunaweza kuonekana tumemuiba ujue.
“Hapana Steve, Hiki kiumbe kinahitaji msaada kaka na sisi ndo watu pekee wa kumsaidia. Ni wazi kabisa huyu mtoto ametelekezwa na Mama yake kwahiyo hatuwezi kumuacha hapa…” Hayo yalikuwa mazungumzo kati ya Kareem na Steve mara baada ya kumkuta mtoto mchanga kichakani. Baada ya mazungumzo hayo, Kareem aliamua kumchukua yule mtoto ingawa Steve hakufurahia. Awamu hii Steve ndo akakamata usukani huku Kareem akimbembeleza yule mtoto wakati safari inaendelea. Baada ya mwendo wa nusu saa wakafika sehemu fulani kwenye makazi ya watu, Kareem akamtaka Steve asimamishe gari. Steve akasimama gari kisha Kareem akateremka na kwenda kwenye duka moja la jumla akanunua maziwa ya kopo ya watoto pamoja na chuchu ya kunyoyea. Baada ya kununua vitu hivyo akarudi tena kwenye gari kisha
akamtengenezea chakula yule mtoto ambaye alionekana kuwa na njaa sana. Kwa bahati nzuri yule mtoto alinyonya maziwa na safari ikaendelea kuchanja mbuga. Kareem akageuka kuwa mlezi wa yule mtoto huku Steve akishikilia usukani wa gari. Waliendelea na safari kuelekea jijini Dar es salaam kupitia mkoani Morogoro. Hatimaye wakafanikiwa kufika salama ndani ya jiji la Dar es salaam.
“Oya mzee, Tushafika tayari mjini. Huyo mtoto unampeleka wapi sasa na muda huu tunatakiwa kufikisha mzigo ofisini.” Steve alimuuliza Kareem.
Kareem alikatazama kale katoto na kujikuta anakaonea huruma. Ni kama vile macho ya yule mtoto yalimwambia Kareem tafadhali usiniache nahitaji msaada wako Babaa. Kareem akambusu yule mtoto kwenye paji la uso kisha akasema; “Huyu mtoto ni wangu kuanzia sasa. Kwa gharama yoyote ile nitahakikisha anakua na kuishi kama watoto wengine. Naamini kabisa hii ni zawadi kutoka kwa Mungu.”
Episode 23
Kareem alimaliza kusimulia hadithi ya miaka 22 iliyopita alipokuwa anafanya kazi kwenye kampuni ya magari ya kusafirisha mizigo. Hadithi hiyo ilimfanya kila mtu ashtuke na wote wakaanza kumtazama Majaliwa licha ya kwamba jina lake halikutajwa. Hata Majaliwa mwenyewe alihisi muhusika wa ile hadithi ni yeye. Muda huo Radhia yeye alikuwa anatokwa na machozi tu maana alijua yeye ndo mama aliyemtelekeza mtoto msituni. Baada ya kumaliza kusimulia hadithi Kareem akamtazama mama yake mzazi kisha akamwambia; “Mama eeh, Yule mtoto mchanga niliyekuleteaga umlee miaka ishirini iliyopita sio mwanangu wa kumzaa. Naomba unisamehe sana mama yangu kwa kukudanganya, nilifanya vile kwa kuwa nilitaka umlee yule mtoto kama ulivyonilea mimi mwanao. Nisamehe sana mama yangu kwa kukudanganya.” Maneno ya Kareem yakazidi kuwaacha watu kwenye mshangao. Hakuna mtu aliyepata nguvu ya kuinua mdomo na kuuliza swali kwa wakati huo. Huyo Majaliwa alijikuta anatokwa na jasho mithili ya mtu anayekimbia mbio za marathon. Kareem alimtazama Majaliwa kisha akamwambia;
“Maja mwanangu, Huyo mtoto ninayemzungumzia hapa ni wewe kijana wangu. Maja eeh, Naomba unisamehe sana kwa kushindwa kukueleza ukweli kwa miaka mingi. Mimi unayenitambua kama Baba yako mzazi sio Baba yako niliyekuzaa bali nilikuokota msituni ukiwa mtoto mchanga. Sikutaka kukuambia ukweli kwa sababu sikutaka ujione yatima kwenye hii dunia. Leo nimeamua kukuambia ukweli kwa sababu siku ya jana nilifanikiwa kumpata mama yako mzazi aliyekutelekeza wewe msituni. Majaliwa mwanangu, Huyu mwanamke (akimnyooshea kidole Radhia) unayemtambua kama mama yako wa kambo ndo Mama yako mzazi aliyekuweka tumboni kwa miezi 9 na kukuzaa wewe. Yeye ndo Mama yako mzazi na yeye ndo anamjua Baba yako halisi.”
Aisee, Kila mtu pale ndani hakuamini masikio yake kwa kile alichokisikia kutoka kwenye kinywa cha Kareem. Majaliwa yeye alihisi kama anaota njozi mbaya sana hivyo akatamani kushtuka usingizi ili asiendelee kuota. Suala la kuambiwa Kareem sio Baba yake mzazi huku Radhia ndo Mama yake mzazi lilikuwa zito sana moyoni mwake. Kwa namna alivyoganda, Ni kama vile dunia ilikuwa inazunguka kichwani mwake.
Vonso na mkewe wakabaki na maswali kwenye vichwa vyao, Inawezekana vipi Radhia ndo awe
Mama mzazi wa Majaliwa wakati wao ndo walimpokea Radhia kwa mara ya kwanza kabisa alipofika mjini na katika historia ya maisha yake aliyowasimulia haikuwa na kipengele kwamba alishawahi kuzaa mtoto hapo awali. Alichosemaga Radhia ni kwamba alikimbia kijijini kwa sababu alilazimishwa kuolewa na mtu asiyempenda. Lakini pia miaka ishirini hiyo hiyo iliyopita ndo
walimpokeaga Radhia nyumbani
kwao alitokea kijijini. Vonso alihisi akili yake imekosa akili kufuatia ile ajenda iliyokuwa inaendelea. Kilio cha
kwikwi kilisikika pale ndani kikitoka kwa Radhia ambaye alikuwa anamtazama Majaliwa. Kadri alivyokuwa anamtazama ndivyo alivyozidi kulia. Vonso akashindwa kuvumilia hivyo akamtaka Radhia atolee ufafanuzi juu ya kauli ya mume wake. Inawezekana vipi yeye ndo awe mama mzazi wa Majaliwa wakati hakuwahi kumwambia chochote kwamba alishawahi kuzaa? Radhia alifuta machozi kisha akajikaza na kuanza kuzungumza;
“Kaka Vonso eeh, Naomba unisamehe
sana kaka yangu. Ile historia niliyokusimuliaga siku ya kwanza kabisa tulipokutana haikuwa na ukweli wowote. Ule ulikuwa uongo, nilizungumza kwa sababu ya kutaka kupata msaada. Wewe, mkeo pamoja
na mume wangu Kareem
niliwadanganya kuhusu historia yangu ya maisha. Moyo wangu umekuwa na siri nzito sana inayonitesa kwa miaka mingi sana nilipokuwa msichana. Leo nataka kuwaelezea historia ya kweli ya maisha yangu. Jina langu halisi ni………….” Radhia alianza kusimulia historia ya kweli juu ya mambo yalivyokuwa kwenye maisha yake mpaka kufikia hatua ya kumtupa mtoto na kwenda mjini. Alielezea ukweli wote bila kuongeza wala kupunguza neno. Mpaka kufikia nukta ya mwisho kabisa ya simulizi, Kila mtu akabaki kimya pale ndani. Walihisi kuchoka kana kwamba walitoka kufanya kazi ngumu ya shambani au kusaidia fundi ujenzi.
Mke wa Vonso alimgusa mume wake kisha akamwambia kwa sauti ya chini; “Mume wangu, Si unakumbuka siku ya kwanza kabisa tulipomkaribisha Radhia ndani ya nyumba yetu? Si unakumbuka nilikuambia kwamba Radhia anaonekana kama mama anayenyonyesha ila ukanibishia? “Yeah! Nakumbuka vyema mke wangu. Ama kweli nyie wanawake mnajuana sana.” Vonso alimjibu mkewe.
Taratibu kabisa Radhia akapiga magoti chini kisha akaanza kutembea kumfuata Majaliwa huku machozi yakimtiririka kwa wingi. Alipomfikia Majaliwa aliyeketi kwenye kiti akamshika magoti kisha akamwambia;
“Am Sorry Mwanangu! Ile siku nilipokuacha msituni nilitamka hayo maneno na leo nimekutana na tena wewe basi narudia tena kutamka haya maneno. Am Sorry! Am so sorry Mwanangu! Naomba unisamehe kwa maovu na ukatili wote niliokutendea mwanangu. Najua ni vigumu sana kwako kuweza kunikubali na kunipenda kama mama yako kutokana na manyanyaso
niliyokufanyia hapa ndani tangu ukiwa mtoto mpaka kufikia hatua ya utu uzima. Nipo tayari kutumikia adhabu yoyote kutoka kwako lakini naomba tu unitazame mimi kama Mama yako niliyekuzaa. Wewe ni Bahati wangu na mimi ndo Mama yako mwanangu.
Nakupenda sana mwanangu na naomba unisamehe mimi mama yako.” Radhia alizungumza maneno hayo kwa uchungu mkubwa sana huku machozi yake yakiogesha miguu ya Majaliwa.
Huwezi kuamini, Majaliwa aliinua mikono ya mama yake taratibu kisha akaitoa kwenye mwili wake. Baada ya kufanya hivyo akainuka kwenye sofa kisha akaanza kutembea taratibu kabisa akielekea chumbani kwake huku machozi yakimtiririka kwa uchungu.
Episode 24
Huo ndo ukawa mwisho wa kikao.
Mpaka kufikia majira ya saa 3 usiku, Majaliwa hakutoka chumbani wala hakula chakula tangu ile asubuhi alipokunywa chai. Kijana alikuwa na msongo mzito wa mawazo kuliko kawaida. Majira yale ya saa 3, Kareem aliamua kwenda kuzungumza na Majaliwa baada ya kuhisi tayari ameshapata afueni na utulivu kwenye akili. Kareem alizama ndani ya chumba cha Majaliwa akiwa na glasi mbili za maziwa mkononi. Alipofika alimkuta Majaliwa amejilaza kitandani huku miguu ikining’inia chini. Kareem akaenda kuketi pale pale kitandani kisha akamgusa kijana wake aliyekuwa na Earphones masikio akisikiliza muziki. Majaliwa alipomuona Baba yake akainuka kisha wakawa wanatazamana. Kareem alimpatia Majaliwa glasi moja ya maziwa huku yeye akibakiwa na nyingine. Licha ya kwamba Majaliwa hakuwa na hamu ya kula chochote lakini kwa namna alivyokuwa anamheshimu Baba yake ilibidi tu apokee glasi na kuanza kunywa Yale maziwa. Majaliwa alikunywa yale maziwa huku akiwa hana nguvu ya kumtazama Baba yake. Roho yake ilimuuma sana baada ya kujua kwamba Kareem sio Baba yake mzazi. Kimya kilitawala pale chumbani huku kila mmoja akifakamia glasi ya maziwa. Ndani ya dakika tu, kila mmoja alikuwa tayari ameshamaliza kunywa yale maziwa.
“Maja!
“Naam, Babaa!
“Vipi umeyaonaje maziwa?
“Yapo vizuri sana.
“Well! Unajua nini mwanangu,
Haijalishi upo kwenye wakati mgumu kiasi gani ila usiache kula. Ukila na kushiba basi akili yako ndo inakuwa na uwezo mkubwa wa kuchanganua jambo. Hili suala linaloendelea linazungumzika vizuri sana maana lipo ndani ya familia hii hii. Hakuna kitu kitakachobadilika kwenye maisha yako mwanangu. Wewe bado utaendelea kuwa mtoto wa hii familia na nafasi yako itabaki vile vile. Jambo la kushukuru upande wako ni kwamba umekutana na Mama yako mzazi na umeshaijua sura yake.” Kareem alizungumza maneno hayo huku mkono wake ukiwa begani kwa Majaliwa aliyeelekeza macho yake chini.
Majaliwa alijipangusa uso kwa mikono yake yote miwili kisha akainua macho na kumtazama Baba yake;
“Mzee wangu, Sijui hata nitumie neno gani ili niweze kukushukuru kwa kila kitu ulichokifanya kwenye maisha yangu. Natamani kusema ahsante lakini nahisi kama haitoshi kukuambia hivyo Baba yangu. Thamani uliyonayo kwangu, Baada ya Mwenyezi Mungu basi wewe ndo unafuata Baba yangu. Kwa namna ulivyonilea na kunipa upendo ni ngumu sana kwangu kuamini kama wewe sio Baba yangu uliyenizaa. Hii siku ni ngumu sana Baba yangu baada ya kujua kwamba wewe sio Baba yangu. Ni bora
ungekufa na hii siri kuliko kuifichua Baba. Mimi nakupenda wewe Baba yangu. Sitaki kujua kama nina Baba mwingine zaidi yako wewe. Ngoja nikuambie kitu Mzee wangu, Kile kikao cha asubuhi mimi sijasikiliza ajenda iliyozungumzwa, sijahudhuria kikao wala sitambui kama kulikuwa na kikao. Kile kikao hakiwezi kubadilisha chochote kwenye akili na moyo wangu. Wewe ndo Baba yangu na wewe ndo Mama yangu. Sihitaji hata kujua sura ya mwanaume aliyenizaa inafananaje. Mimi siitwi Bahati, Naitwa Majaliwa Kareem na
Kareem mwenyewe ndo wewe Baba.” Majaliwa alizungumza maneno hayo kwa uchungu mkubwa sana huku akibubujikwa na machozi.
Hata Kareem nae alishindwa kuzuia machozi kwenye mboni zake baada ya kuhisi maumivu aliyokuwa nayo Majaliwa. Kareem alitoa kitambaa kwenye mfuko wake wa suruali kisha akamfuta machozi Majaliwa. Baada ya kumaliza kumfuata machozi akamwambia;
“Maja mwanangu! Kama nilivyokuambia hakuna kitu kitakachobadilisha mahusiano yetu. Mimi bado ni Baba yako na wewe ni mwanangu. Hata ikitokea leo hii nikifa basi jina lako utalikuta kwenye waraka wa urithi. Wewe ni mwanangu Maja wala sijakuondoa kwenye orodha. Nafikiri huu ni wakati wako wa kufurahia maisha na kuwa huru zaidi kwa sababu ule uadui wako na mama yako umekwisha. Kwa sasa mama yako anajutia maovu yote aliyokutendea. Naomba umsamehe na umtazame kwa jicho jipya kama mama yako mzazi.
“Babaa eeh, Yule mwanamke atabaki kuwa mama yangu kwa sababu ni mke wako wewe Baba yangu lakini sio kwa sababu amenizaa mimi. Yule mwanamke ni mama yangu lakini hawezi kuwa mama yangu mzazi. Hilo jicho la kumtazama kama Mama yangu mzazi tayari alishalitoboa na sasa nimekuwa kipofu kwake. Ningeweza kumtazama kama mama yangu licha ya kwamba alinitelekeza lakini kwa mateso na manyanyaso aliyonipatia hayawezi kusameheka kirahisi. Yeye ndo alifanya niione dunia chungu mpaka nikajuta kuzaliwa. Kumbukumbu zote mbaya nilizonazo kwenye kichwa changu zimebeba taswira yake yeye. Hata kama alijua mimi sio mwanae lakini kwanini anitese? Sheria gani inasema mtoto wa kambo anapaswa kuteswa na kunyanyaswa? Baba eeh, Mimi nitaendelea kumtazama mke wako kama mama yangu lakini yeye sio mama yangu mzazi.”
Wakati mazungumzo hayo ya Baba na mwana yakiendelea chumbani kwa Majaliwa, Radhia alisimama mlangoni akisikiza mazungumzo hayo kwa siri. Kila neno alilolisikia kutoka kwenye kinywa cha Majaliwa lilimuumiza sana moyo na kumfanya azidi kulia kwa uchungu. Kwa namna alivyomtesaga Majaliwa na kufikia hatua ya kutaka kumuua akaona ni kweli kabisa hastahili kuwa mama mzazi wa yule mtoto.
****
Asubuhi na mapema ya siku iliyofuata, Majaliwa alikuwa wa kwanza kuamka na alionekana begi mgongoni. Kijana alipata wazo la kwenda kumalizia likizo yake kuishi kwenye chumba chake hosteli. Hakuhitaji kumuaga mtu yoyote asubuhi hiyo kwa kuwa tayari alishamuaga Baba yake tangu jana usiku. Hakuwa na mzigo wowote zaidi ya begi lake la mgongoni tu. Katika ya mlango mkubwa wa kutokea nje ya nyumba, Mwanamama Radhia alionekana akiwa amepiga magoti huku akitokwa na machozi. Ni pale pale mlangoni ambako Majaliwa alitakiwa kupita ili aondoke. Kumbe ile ratiba ya Majaliwa kuondoka, Radhia tayari alishaambiwa na mume wake. Majaliwa alisimama kwa mshangao baada ya kuona njia yake imezuiliwa na mama yake. Muda ule ule Kareem nae akafika akiwa na taulo lake kiunoni. Alitulia na kutazama picha linalotaka kuendelea kati ya mama na mwana.
“Bahati mwanangu, Msamaha wako ni muhimu sana kwa maisha yangu ya hapa duniani pamoja na mbinguni. Haijalishi nimekuwa mbaya kwako kiasi gani lakini hakuna kitu kinachoweza kubadilisha ukweli kwamba wewe ni mwanangu. Naomba unisamehe sana mwanangu kwa mabaya yote niliyokutendea.” Radhia alizungumza maneno hayo huku akitokwa na machozi ya kiutuuzima.
Pale pale Majaliwa nae akajikuta anatokwa na machozi kila alipomtazama mama yake. Matukio ya maisha yake ya nyuma tangu akiwa utotoni ndo yalikuwa yanamtoa machozi kila alipoyakumbuka. Majaliwa alikaza roho kiume kisha akamjibu mama yake;
“Mwanao alikuwa anaitwa Bahati na ulishamtupa msituni. Mimi hapa naitwa Majaliwa, Ni yule mtoto uliyemnyanyasa na kumfanya aione dunia chungu. Mpaka hapa nilipofikia sidhani kama nahitaji mama mwenye roho mbaya kama yako. Ulininyima chakula, ulinipiga, ulinifanyisha kazi bila mipaka na mbaya zaidi ukanizuia nisisome. Kama uliweza kuninyima haki yangu kama mtoto, Unawezaje kudai haki ya kuwa Mama? Hivi ni Mama gani anayeweza kumfanyia mwanae vitu kama hivyo? Hata kama ulijua mimi sio mwanao lakini kwanini unitese? Nilikukosea nini mimi? Mbona nilikuwa nakuheshimu sana mama yangu? Mbona nilikuwa natimiza wajibu wangu kama mtoto? Kiukweli kabisa sina hisia zozote za upendo kwako na wala sijawahi kukupenda. Wewe ni mbaya sana mama yangu.” Majaliwa aliongea kwa uchungu sana huku machozi yakizidi kumtiririka.
“Majaliwa Mwanangu, Mimi ni binadamu mwenye mapungufu wala sikuumbwa na ukamilifu. Licha ya roho mbaya niliyokuwa nayo lakini kumbuka kwamba tumbo langu mimi ndo lilikubeba wewe na kukuhifadhi kwa miezi 9. Baba yako alinitaka nitoe mimba yako lakini licha ya mimi kuwa na roho mbaya lakini sikuwa tayari kukuua mwanangu. Nilitekezwa na Baba yako na nikakubali kuteseka na dunia ilimradi tu uwe na afya njema ukiwa tumboni ili uje kuiona hii dunia. Msoto wa maisha niliopitia wakati upo tumboni mwangu ni mzito kuliko msoto niliokusababishia hapa ndani. Kiukweli kabisa niliteseka sana kwa ajili yako lakini sikuacha kukupenda mwanangu. Hata ule uamuzi wa kukuacha msituni ni kwa sababu nilijua utapata msaada na kwenda kulelewa kwenye maisha bora. Maisha yangu mimi yalishakuwa magumu kiasi kwamba nilikuwa nakosa hata chakula hivyo hata maziwa yakawa hayatoki vizuri. Kiukweli kabisa sikuwa tayari kuona njaa inakuua mwanangu kwa kukosa maziwa. Majaliwa eeh, Mimi ndo mama yako mzazi mwanangu.” Maneno ya mama yalikuwa mazito kiasi kwamba Majaliwa akaishiwa nguvu. Lile begi alilovaa mgongoni likadondoka chini kwa kishindo. Ni machozi tu ndo yalikuwa yametawala kwenye uso wa Majaliwa na mama yake ambao walikuwa wanatazamana kwa huzuni. Hata Kareem nae akajikuta anatokwa na machozi kutokana na kile kilichokuwa kinaendelea. Kareem akafungua kinywa chake na kusema; “Mke wangu, Tazama Mungu alivyokuwa wa ajabu. Ulimtelekeza mwanao kisa maisha magumu, Mungu akakupa maisha mazuri kisha akakuletea tena mwanao yule yule ili umlee kwenye hayo maisha mazuri. Lakini sasa, tamaa, uchoyo na ubinafsi ukakufanya ushindwe kutekeleza wajibu wako ipaswavyo. Siku zote nilikuwa nakuambia mke wangu, Mwanangu ni mwanao lakini hukuweza kuizingatia hiyo kauli. Nakukumbusha tena mke wangu, Mwanangu ni mwanao wewe na mwanao ni mwanangu mimi haijalishi
ulizaa na nani au nilizaa na nani.” Kareem alimwambia mke wake maneno hayo kisha akamgeukia Majaliwa na kumwambia;
“Maja mwanangu, Wewe ni msomi hivyo unaelewa kwamba hakuna mwanadamu aliyekamilika na siku zote tunajifunza kutokana na makosa. Ukiona mtu mzima anapiga magoti na kumlilia mtoto basi ujue jambo limeshagusa kwenye moyo. Mimi pia kama Baba yako naungana na Mama yako kumuombea msamaha kwako. Msamehe sana mama yako maana hata wewe ulimtesa sana kipindi ulipokuwa tumboni lakini hakuwahi kukuchukia wala kukukana. Ni wazi kabisa mama yako aliteseka na kudharaulika kwa sababu yako. Lakini pia Mama yako alikupenda sana ila ni hofu na changamoto za maisha ndo zilimfanya akuache msituni. Msamehe sana Mama yako mwanangu ili tudumishe amani katika familia yetu. Wewe ndo mtoto wa kwanza katika familia hii.” Baada ya Kareem kumaliza kuzungumza, Majaliwa alianza kutembea taratibu kabisa kumsogelea mama yake pale chini alipokuwa amepiga magoti.
Alipomfikia tu nae akadondoka chini kwa magoti kisha akamkumbatia kwa nguvu. Wote kwa pamoja walikumbatiana huku machozi ya huzuni na furaha yakiwatiririka mashavuni. Ni dhahiri kabisa hisia zilizokuwemo kwenye mioyo yao zilikuwa nzito kiasi kwamba mioyo ilishindwa kuhimili.
“Na…. Na…. Nakupenda sana Mama yangu. Dhambi zote ulizoandikiwa kwa sababu yangu naomba Mwenyezi Mungu akufutie Mama yangu. Nimekusamehe Mama yangu na nakupenda sana. Nakupenda sana
Mama yangu.”
Aisee, Majaliwa alizungumza maneno hayo na kufanya wazidi kukumbatia kwa nguvu huku machozi yakizidi kuwatiririka kwa pamoja. Vita ya Mama na mwana ikamalizika kwa staili hiyo huku Kareem akitabasamu kwa furaha.
Episode 25
[MIAKA MITATU BAADAE]
Hatimaye kijana Majaliwa alifanikiwa kuhitimu shahada yake ya chuo kikuu na tayari alishaanza rasmi kuishi kwenye ndoto zake. Yule Majaliwa Kareem alikuwa anatambulika kama Dokta Kareem ndani ya Hospitali ya taifa, Muhimbili. Licha ya kuwa mwajiriwa katika hospitali ya taifa, Muhimbili lakini pia alikuwa anafanya kazi za muda wa ziada (part-time) kwenye hospitali mbalimbali za watu binafsi. Hiyo ni kutokana na madaktari wenye taaluma kama yake kuwa wachache nchini. Ndani ya miaka miwili tu tangu alipoajiriwa alijikuta anatengeneza pesa nyingi kuliko umri wake. Alinunua kiwanja na kujijengea nyumba ya kisasa ya kuishi. Lakini pia alinunua uwanja kwa ajili ya kumjengea nyumba mama yake huku akimzawadia Baba yake gari la kutembelea. Kwa hakika Majaliwa aliwafanya wazazi wake (Kareem & Radhia) kutembea vifua mbele. Wazazi hao walijivunia sana mtoto wao Majaliwa. Kareem hakuwahi kabisa kujutia ule uamuzi wake wa kumuokota mtoto na kwenda kumlea kama mwanae. Majaliwa ndo mtoto wao pekee aliyebarikiwa upeo mkubwa katika masomo na kuwa msaada katika familia. Kwa kuwa umri ulikuwa mkubwa, Majaliwa aliona wakati sahihi wa kuondoka nyumbani kwa wazazi na kwenda kuanzisha kaya yake umefika. Ni wakati ambao Majaliwa alitaka kuoa na kwenda kuishi na mke wake ndani ya nyumba
yake. Jasmine ndo mwanamke pekee aliyefanikiwa kuziteka hisia za Majaliwa tangu walipokutana chuoni kwa mara ya kwanza. Wawili hao walidumu kwenye mahusiano kwa kipindi cha miaka nne. Penzi lao lilishaota mizizi ya uaminifu na kuchipua maua ya upendo. Jasmine alisomea kozi ya Unesi na aliajiriwa kwenye hospitali fulani ya mtu binafsi ila mshahara wake ulikuwa wa wastani kabisa. Ni Jasmine Anthony, Mrembo wa dini ya kiikristo aliyekuwa tayari kuslimu kwa sababu ya mapenzi. Ilikuwa vigumu sana kwa Jasmine kuishi bila Majaliwa na Majaliwa kuishi bila Jasmine. Kwa kipindi chote walichokuwa kwenye mahusiano walifanya mambo mengi sana yaliyodumisha upendo wao.
Barua ya posa kutoka kwa Majaliwa ilifika salama kwenye mikono ya wazazi wa Jasmine na iliweza kupokelewa na kukubaliwa. Ilikuwa rahisi sana barua ya Majaliwa kukubaliwa kwa sababu tayari alikuwa anajulikana kwa wakwe zake na alikuwa anawasaidia kwenye mambo mengi sana ya kifedha. Wazazi wa Jasmine walikuwa na furaha sana kuona mtoto wao anaenda kuolewa na Daktari kutoka hospitali kubwa nchini hivyo umaskini kwao ni mwiko. Wakati mchakato wa kupeleka barua ya posa ukifanyika, Tayari Jasmine alikuwa na ujauzito wa miezi minne. Wazo la ndoa lilipigwa kalenda kwa kuwa sheria za dini ya kiislamu zinamzuia mwanamke mjamzito kuolewa. Endapo mwanamke ataolewa na mimba yake basi kama mtoto aliyetumboni akiwa wa kiume basi tafsiri yake ni kwamba yeye na Baba yake watakuwa wamemuoa mama. Na kama mtoto wa tumboni ni wa kike basi na yeye pia atakuwa ameolewa na Baba yake. Ndoa ya Majaliwa na Jasmine ikapangwa kufanyika baada ya Jasmine kujifungua mtoto. Kwa kipindi chote cha kusubiri wawili hao wakawa wanaishi pamoja maadam barua ya posa pamoja na mahari tayari ilishatolewa. Kila mmoja alikuwa anajulikana kwa wazazi wa mwenzake ila ni wazazi wao tu ndo hawakuwahi kukutana. Wazazi wa Jasmine walikuwa wanaishi mkoani
Ruvuma katika wilaya ya Songea huku Majaliwa wazazi wake wakiishi pale Dar es salaam.
****
“Dear, Vipi umemkumbusha mzee kuhusu ile safari?
“Yeah! Nimemkumbusha na tayari wameshajiandaa kesho kutwa wanakuja.
“Basi sawa ni vyema waje mapema maana tayari nimeshapata mwezi mmoja wa likizo. Hiyo kesho kutwa akifika, siku inayofuata nitaenda kumtafutia VISA ili tuwahi kuondoka.” Hayo ni mazungumzo kati ya
Majaliwa na mpenzi wake Jasmine.
Ni mazungumzo yaliyohusu safari ya India kwa ajili ya matibabu ya Baba yake Jasmine. Mzee alikuwa na matatizo ya miguu baada ya kupataga ajali ya pikipiki miaka michache iliyopita. Mguu mmoja uliharibika kabisa hivyo ukakatwa, mwingine uliobaki ndo ulikuwa unamsumbua miaka nenda miaka rudi hivyo ulihitaji matibabu makubwa nchini India. Kwenye ule mguu uliokatwa tayari kulikuwa na mguu wa bandia ambao alinunuliwa na Binti yake Jasmine punde tu baada ya kuajiriwa. Jasmine ndo alikuwa mtoto wa pekee katika familia na changamoto zote za maisha ya wazazi wake zilikuwa chini yake. Siku mbili baadae, Wazazi wa Jasmine wote wawili walitia maguu ndani ya jiji la Dar es salaam wakitokea Songea. Majaliwa na Jasmine waliwapokea wazazi hao kwa furaha sana na kuwakaribisha nyumbani kwao. Huwezi kuamini, Baba mzazi wa Jasmine ni Tony, Yule mwanaume aliyempaga mimba
Radhia na kumtelekeza. Kwa tafsiri nyepesi ni kwamba Majaliwa na Jasmine walikuwa watoto wa Baba mmoja ambaye ni Tony. Lakini pia mama mzazi wa Jasmine ni Kidawa, Yule mwanamke aliyekuwaga na mahusiano na Tony wakati Radhia akiwa mjamzito. Ni yule mwanamke aliyemshinikizaga Tony amfukuze Radhia nyumbani kwake. Mwaka ule ule Tony na Kidawa walipeana mimba na wakabahatika kupata mtoto wa kike ambaye ni Jasmine. Mpaka kufikia muda huo, umri ulikuwa umesogea kidogo hivyo Tony hakuwa na ule muonekano wa ujanani. Kwa sasa alikuwa M’baba mtu mzima anayefukuzia miaka 50. Changamoto kubwa aliyokuwa nayo kwa wakati ni matatizo ya miguu yaliyotokana na ajali mbaya aliyoipata wakati anaendesha pikipiki. Tony alikuwa na mguu mmoja wa bandia huku mguu mwingine ukihitaji matibabu makubwa ya nje ya nchi. Hata ujio wake ndani ya jiji la Dar es salaam ni kwa lengo la kusafiri na mkwe wake Majaliwa kuelekea India kwenye matibabu. Tangu Tony alipopata ajali hakuwa na uwezo wa kutafuta pesa hivyo msaada wake mkubwa ilikuwa kwa Binti yake Jasmine. Huo ndo ulikuwa uhalisia wa maisha ulivyokuwa mpaka kufikia muda huo. Hatima ya penzi ama ndoa ya
Jasmine na Majaliwa ilikuwa ndani ya bomu zito la machozi linalokaribia kulipuka. Maajabu ya dunia kuzunguka yaliwakutanisha ndugu wawili waliozaliwa na Baba mmoja na kuwazamisha kwenye mahusiano ya kimapenzi bila wenyewe kujua.
Unadhani nini kitafuata? Je itakuaje siku Majaliwa na Jasmine wakijua wao ni ndugu wa Baba mmoja? Nini hatima ya maisha yao ikiwa tayari wanatarajia kupata mtoto?
INAENDELEA………..