𝐍𝐈𝐋𝐈𝐌𝐓𝐄𝐒𝐀 𝐌𝐓𝐎𝐓𝐎 𝐖𝐀 𝐊𝐀𝐌𝐁𝐎 𝐁𝐈𝐋𝐀 𝐊𝐔𝐉𝐔𝐀 𝐍𝐈 𝐌𝐖𝐀𝐍𝐀𝐍𝐆𝐔 𝐍𝐈𝐋𝐈𝐘𝐄𝐌𝐓𝐔𝐏𝐀𝐆𝐀 𝐌𝐒𝐈𝐓𝐔𝐍𝐈 𝐊𝐈𝐏𝐈𝐍𝐃𝐈 𝐂𝐇𝐀 𝐍𝐘𝐔𝐌𝐀
Episode 11
Hakukuwa na muda wa kusubiri tena, siku iliyofuata Radhia na Kareem wakakutana kwa ajili ya
mazungumzo. Makutano yalifanyika majira ya saa 7 mchana nyumbani kwa Kareem na walikuwa wawili tu. Picha linaanza Radhia alistaajabu baada ya kuingia kwenye mjengo mkali. Ukweli ni kwamba hakutegemea kabisa kama Kareem anamiliki nyumba kubwa na ya kisasa inayogharimu zaidi ya milioni 100 za kitanzania. Umri wa Kareem ulikuwa haufanani kabisa na mali alizokuwa nazo. Ukiachana na kazi ya kusafirisha mizigo nje ya nchi, wazazi wake walikuwa na pesa na hakuwahi kabisa kujua njaa inaumaje tangu akiwa mtoto. Radhia hakuamini kabisa kama yeye ndo atakuwa mama mjengo pale ndani endapo atakubali kuolewa na Kareem. Nyumba ilikuwa imekamilika kila kitu na kulikuwa na fenicha zote zinazohitajika ndani. Ni mke tu wa kutunza nyumba ndo alikosekana pale ndani. Ndani ya chumba cha sebule, Radhia na Kareem kila mmoja aliketi kwenye sofa lake huku kimya kidogo kikitawala. Kwenye meza iliyokuwa mbele ya Radhia kulikuwa na sahani ya chipsi mayai, kuku mzima aliyekaushwa pamoja na glasi ya maziwa. Ni chakula ambacho Kareem alimuandalia mgeni wake Radhia. Radhia alijikuta ananogewa sana na kila kitu alichokutana nacho pale ndani. Ule utamu wa ule msosi alioandaliwa ndo ukamfanya anogewe kabisa na yale maisha. Mwanadada alimtazama Kareem mara mbili mbili huku akimtafakari kwa kina zaidi. Muda huo Kareem nae alikuwa bize na sahani ya chakula. Mwanaume hakutaka kuzungumza
wakati wa kula hivyo alisubiri wamalize kwanza kula kisha ndo waanze mazungumzo. Takribani dakika 20 ziliwatosha kumaliza chakula. Hapo sasa Kareem akafungua mdomo wake na kumsemesha mtoto wa kike;
“Radhia! Ni matumaini yangu kwamba ombi langu kuja kwako tayari limefika. Ni ukweli usiopingika kwamba nakupenda na kukuhitaji katika maisha yangu yote. Sihitaji kukuchezea bali nataka kukuoa kabisa kabla sijaugusa mwili wako. Naomba ukubali kuishi na mimi hapa ndani tuzae watoto na nife ufe tuzikane. Nakuahidi Radhia,
Nitakupenda mpaka pumzi yangu ya mwisho endapo utakubali kuolewa na mimi.” Kareem alizungumza maneno hayo na kuzidi kuuteka moyo wa Radhia.
“Kareem!
“Naam,
“Naomba nikuulize swali. “Wala usijali, kuwa huru niulize Radhia.
“Hivi ulishawahi kuoa hapo awali? “Hapana sijawahi kuoa ila ukweli ni kwamba nina mtoto tayari.” Radhia akashtuka kidogo baada ya kusikia Kareem ana mtoto tayari.
“Una mtoto?
“Yeah! Nina mtoto wa kiume anaitwa Majaliwa. Kwa sasa ana umri wa miaka tano.
“Sasa kwanini hujamuoa mama wa mtoto wako?
“Ni kwa sababu sio kila mwanamke anastahili kuolewa Radhia. Ndoa sio kitu anachostahili kila mwanamke kwa sababu wengi hawajui kabisa misingi yake.
“Mmh! Misingi yake kama ipi sasa?
“Msingi mkuu ni heshima tu. Mwanamke anayestahili kuolewa ni yule anayejua kujiheshimu mwenyewe na kuheshimu watu wengine akiwemo mume wake.
“Mmh! Kwahiyo unavyoona wewe mimi nina heshima eti? “Yeah! Naiona heshima kwako Radhia. Kwanza kabisa unajua kujiheshimu mwenyewe maana muonekano wako kimavazi unatosha kuthibitisha hilo. Mwanaume anayejitambua hawezi kumuoa mwanamke anayejitukanisha hadharani kwa kuvaa nusu uchi. “Nimekuelewa Kareem! Kwahiyo mwanao yupo kwa mama yake? “Hapana! Yupo kwa Bibi yake ambaye ni mama yangu mimi mzazi. Kwa sasa nataka kumchukua ili nianze kuishi nae mwenyewe.
“Vizuri sana! Ila naomba nikuulize swali lingine Kareem. Kwa mfano na mimi nikikuambia kwamba nina mtoto, Je bado utaendela na msimamo wako wa kutaka kunioa? “Yeah! Nitakuoa na kukupenda wewe pamoja na mwanao bila mipaka wala masharti. Kama utaridhia kuwa mke wangu basi mwanao atakuwa mwanangu na mwanangu atakuwa mwanao. Na kitu ambacho unapaswa kukifahamu Radhia, Kama utakubali kuolewa na mimi basi tambua kwamba umekubali kuwa mama wa Majaliwa pamoja na ndugu zake utakaowazaa wewe. Na kama unahisi kabisa hutoweza kumtazama Majaliwa kama mwanao basi usikubali kuolewa na mimi. Furaha yangu mimi ni pamoja na kumuona mwanangu anapata malezi bora na upendo kutoka kwa mama. Kwahiyo basi, Nenda ukafikirie vizuri kabla hujanipa jibu la ombi langu.”
Baada ya mazungumzo hayo, kimya kidogo kikatawala. Radhia akaanza kuyatafakari vizuri maneno ya Kareem kisha akautazama vyema ule mjengo na vitu vilivyomo ndani yake. Hapo sasa akajikuta anakumbuka kibanda alichokuwa anaishi kule Songea. Alikumbuka tabu zote alizopitia mpaka akapata wazo la kumtupa mtoto na kwenda mjini kutafuta maisha. Radhia akajiuliza, kama alikuja mjini kutafuta maisha sasa anataka maisha gani tena zaidi ya yale yaliyojisogeza mbele yake? Kwanini akatae fursa wakati akiolewa na Kareem na kumzalia mtoto basi ile nyumba itakuwa urithi wa mwanae. Lakini pia akawaza kwanini amkatae Kareem wakati ni kijana mwenye mvuto kwenye macho ya kila
mwanamke anayemtazama? Radhia
aliamini sasa ile ni bahati kubwa sana upande wake hivyo hatakiwi kuipoteza. Hata lile wazo la kutumia siku kadhaa za kufikiri kabla ya kutoa jibu akaliona linaweza kumkosesha ile bahati. Alihofia huenda Kareem atabadilisha uamuzi wa kumuoa au anaweza kukutana na mwanamke mwingine akavutiwa nae. Kwa kuzingatia ule msemo wa “Chelewa chelewa ukute mwana si wako” Radhia akaamua kutoa jibu pale pale; “Kareem! Nimekubali kuolewa na wewe! Nimekubali kuwa mama wa watoto wako Kareem! Nimekubali kuishi na wewe na kujenga familia.
Kuanzia sasa na kuendelea,
Nakupenda sana Kareem.”
Hivyo ndivyo Radhia alivyomjibu Kareem akiridhia ombi la Kareem bila shuruti. Kareem alifurahi sana kusikia maneno hayo hivyo akamshika Radhia viganja vya mkono kisha akambusu kwa upendo na kumwambia;
“Radhia, Ahsante sana kwa kuridhia ombi langu. Kwa sasa sina muda wa kupoteza nataka tuanze kabisa maandalizi ya ndoa yetu. Kama nilivyokuambia hapo awali, sihitaji kukuchezea bali nataka kukuoa kabisa uwe mke wangu wa halali.” Hivyo ndivyo mambo yalivyokuwa kati ya Kareem na Radhia. Hatimaye Radhia alikubali kuolewa na Kareem ili aanze maisha mapya kabisa. Hakukuwa na muda wa kupoteza hivyo ndoa ikapita salama, Radhia akawa mke wa Kareem na Kareem akawa mume halali wa Radhia. Vonso na mkewe ndo walikuwa kama wazazi wa Radhia hivyo suala walilimaliza kule kule mjini maana Radhia alisema
hakuna mtu anayemtazama kama
ndugu yake kule kijiji alikotoka ingawa alishadanganyaga kwamba kuna Baba yake mdogo. Kareem aliweza kumchukua mwanae
Majaliwa na kuanza kuishi nae ndani ya nyumba yake baada ya kufanikiwa kumtafutia mama wa kumpa malezi. Mpaka kufikia muda huo, Majaliwa alikuwa na umri wa miaka mitano hivyo akapelekwa shule ya chekechea kuanza safari ya kuitafuta elimu ya kidunia. Lakini pia Kareem alimwandikisha mwanae Madrassa kwa ajili ya kuipata elimu akhera itakayomuwezesha kumjua Mola wake. Upendo na amani ulitawala sana ndani ya familia ya Kareem. Majaliwa alimpenda na kumheshimu
Radhia kama mama yake huku Radhia nae akionesha kumpenda sana Majaliwa kama mwanae wa kumzaa.
Episode 12
Maisha yaliendelea huku siku nazo zikizidi kusonga. Mwezi mmoja ukakatika huku amani na furaha zikitawala ndani ya nyumba. Kareem tayari alishafungua duka kubwa la urembo na vipodozi mjini Mwenge. Ni biashara ambayo ilimpa faida kubwa na kuzidi kuboresha kipato chake kadri siku zilivyokuwa zinasonga. Wakati Kareem anaenda kwenye biashara zake kila siku, Radhia alibaki nyumbani kama mama wa familia. Kila siku asubuhi alikuwa
anamtengenezea Breakfast Majaliwa, Anamuogesha na kumvalisha sare kisha anamsindikiza shule. Hayo yote Radhia aliyafanya kwa upendo mkubwa sana kwa Majaliwa katika siku za mwanzo za ndoa yake.
Sababu nyingine iliyokuwa inamfanya Radhia ampende Majaliwa alikuwa anamfanya amkumbuke mwanae aliyemtelekeza msituni miaka iliyopita. Radhia aliamini kama mwanae Bahati yupo hai basi umri wake unafanana kabisa na umri wa Majaliwa. Huo ndo uhalisia wa maisha yalivyokuwa mara baada ya Radhia kuolewa na Kareem.
****
Siku zote wanasema milima haikutani ila binadamu hukutana, Huwezi kuamini baada baada ya kutengana kwa takribani miaka tano, hatimaye marafiki wawili wakafanikiwa kukutana tena. Si wengine bali ni Radhia pamoja na Landina.
Walikutana mjini Kariakoo kwenye duka moja la nguo ambapo kila mmoja alikwenda kufanya shopping siku hiyo. Wakati Landina anatoka ndani ya duka, Radhia nae ndo alikuwa anaingia. Landina aliongozana na mwanaume mmoja huku Radhia akiwa pamoja na mwanae Majaliwa. Kwa hakika ilikuwa sapraizi kubwa sana kwa Radhia na Landina maana hawakutegemea kabisa kama wangekutana ndani ya jiji kubwa kama lile. Kwa kuwa Landina alikuwa na haraka hawakuweza kabisa kupata muda wa kuzungumza badala yake wakapeana namba za simu na kuahidiana watatafutana baadae. Baada ya kupeana namba za simu, Landina akaondoka huku Radhia akiingia ndani ya duka kununua nguo. Baada ya siku ile waliweza kuwasiliana kwa njia ya simu kisha walikubaliana kukutana. Radhia ndo alikuwa wa kwanza kumkaribisha Landina nyumbani kwake ili akapajue na wapate muda wa kutosha wa kuzungumza. Hakukuwa na muda wa kupoteza, Siku iliyofuata Landina akaenda nyumbani kwa Radhia. Alipofika tu akashtuka kukaribishwa ndani ya jengo kubwa. Katika fikra zake alihisi huenda rafiki yake ni mdada wa kazi pale ndani lakini alizama ndani ya nyumba akashtuka kukuta picha ya ndoa ukutani ikimuonesha Radhia pamoja na mume wake Kareem.
“Radhia rafiki yangu! Unajua nashindwa kuamini mpaka sasa. Kwahiyo wewe ndo mama mjengo hapa ndani?
“Hahahah! Ndo maana yake Landina. Tayari nimeolewa na hapa ndo nyumbani kwangu na mume wangu.
Hatujapanga bali ni kwetu kabisa.
“Wow! Hongera sana rafiki yangu. Kiukweli Mungu amekufungulia milango na kubadilisha maisha yako kwa ujumla. Kwa sasa umenawiri kweli kweli shoga yangu. Vipi mwanao yupo wapi shoga yangu maana ile jana nilimtazama tu juu juu. “Kaenda shule akitoka anaunganisha Madrassa kwahiyo anarudi jioni.
“Ooh! Kumbee… Ila hongera sana Radhia rafiki yangu kwa kuweza kuzishinda changamoto na hatimaye umepata faraja. Najua haikuwa rahisi kwako kuweza kumlea mwanao kwenye yale mazingira niliyokuacha kule kijijini. Mimi nilipofika huku mjini nilikutana na changamoto nyingi sana za maisha na nilishaibiwa simu na kupoteza kabisa namba yako. Ila kiukweli kwa sasa nimefurahi sana kuweza kukutana na wewe na kilichonifurahisha zaidi ni maisha uliyonayo sasa hivi. Kwa hakika bahati imeshuka upande wako Radhia. Unajua kwa dunia ya sasa sio rahisi mwanaume kukubali kumuoa mwanamke mwenye mtoto. Hilo ni jambo la kumshukuru Mungu shoga yangu.
“Ni kweli kabisa Landina lakini mimi sina mtoto kwa sasa. Yule mwanangu alishafariki miezi michache tu tangu nijifungue. Baada ya hapo ndo nikaamua kuja huku mjini kutafuta maisha na ndipo nikakutana na huyu mume wangu.
“Ooh! Pole sana rafiki yangu kwa msiba mzito. Unajua yule mtoto nilivyomuona tu ile jana nikamfananisha na Tony. Yaani nilimuona Tony mtupu kwahiyo nikajua ndo yule mwanao niliyemuacha tumboni.
“Hapana! Itakuwa ulimtazama kwa haraka haraka tu. Yule ni mtoto wa mume wangu alizaa na mwanamke mwingine huko nyuma. Mimi ni mama mlezi kwake.
“Mmh! Kweli nilimtazama juu juu. Kwahiyo shemeji ana mtoto wa nje ya ndoa?
“Yeah! Ndo huyo tu mmoja. “Sawa! Ila nataka kukushauri kitu Radhia rafiki yangu.
“Kitu gani hiko?
“Hakikisha unamzalia shemeji haraka iwezekanavyo ili uwe na haki ya kupata fungu kupitia mwanao endapo shemeji atafariki. Unajua kwa sasa ikitokea shemeji anafariki basi mali zitakuwa chini ya huyo mtoto wa nje ya ndoa na msimamizi wake atakuwa mama yake mzazi. Wewe utaondoka hapa ndani mikono mitupu shoga yangu. Nakukumbusha rafiki yangu, mtoto wa kambo sio mwanao
kwahiyo usije ukajisahau. Siku ikifika huyo mtoto atazipeleka hizi mali kwa mwanamke mwenzako. Yangu ni hayo tu shoga yangu usiseme sikukuambia.”
Episode 13
Kwa kiasi fulani maneno ya Landina yalibadilisha mtazamo wa Radhia juu ya mtoto Majaliwa. Sasa akaanza kuamini kwamba huenda Majaliwa akaja kuwa adui yake huko mbeleni kwenye suala zima la mali za Kareem. Hapo sasa akaona kuna kila sababu ya kumzalia Kareem mtoto ili aweze kupata fungu la urithi kupitia mwanae. Miezi miwili baadae Radhia akapata ujauzito wa Kareem na kufanya ndoa iendelee kujichimbia mizizi. Wakati Kareem akitamani mkewe ajifungue mtoto wa kike, Radhia yeye alitamani mtoto wa kiume. Alitamani mtoto kiume kwa kuamini kwamba ataziba pengo la mwanae Bahati aliyemtelekeza msituni. Bado zile kumbukumbu za kumtelekeza mwanae zilikuwa zinamtesa sana akilini mwake. Lakini pia alitamani mtoto wa kiume kwa kuwa angekuwa na nguvu ya kupigania mali dhidi ya kaka yake Majaliwa. Radhia hakutaka kabisa mwanae aje kuwa chini ya kivuli cha Majaliwa ambaye ni mtoto wa nje ya ndoa. Kuna chuki fulani zilianza kujijenga kwenye roho ya Radhia dhidi ya Majaliwa. Ule upendo ukaanza kupungua siku hadi siku. Miezi 9 ilipofika, Radhia akafanikiwa kujifungua salama mtoto wa kike.
Mwenyezi Mungu aliamua kumpa
Radhia kile anachostahili sio kile anachokitaka. Baada ya Radhia kujifungua, Yale mapenzi yake kwa mtoto Majaliwa yakafutika kabisa. Hakumtazama tena Majaliwa kama mwanae hivyo akaanza kumnyanyasa kimya kimya bila Kareem kujua. Muda huo Majaliwa alishafikisha miaka 6 na tayari alishaanza darasa la kwanza licha ya kutofikisha umri wa miaka 7. Kilichomfanya aanze darasa la kwanza ni kwa kuwa alikuwa na akili nyingi sana hivyo akapokelewa bila wasiwasi. Maisha aliyopitia mtoto Majaliwa chini ya mama wa kambo yalikuwa mazito kuliko umri wake. Radhia alimnyanyasa sana Majaliwa na kumnyima haki zake za msingi kama mtoto. Mara nyinyi alimtembezea kichapo kikali na kumnyima chakula pindi alipofanya makosa ya kitoto. Majaliwa akawa anamuogopa sana mama yake mlezi na kumuona kama Simba. Hakuwa kabisa na amani wala furaha mbele ya mama yake mlezi. Kareem alianza kuona mabadiliko makubwa sana ya kimwili kwa mwanae hivyo akajua kuna kitu hakipo sawa pale ndani. Alishangaa sana kuona mwanae anapungua mwili kila siku ilihali ndani nyumba kuna vyakula vya kila aina. Lakini pia alishangaa kuona
Majaliwa ameacha kabisa kumdekea mama yake wa kambo. Manyanyaso kwa mtoto Majaliwa yaliendelea kadri siku, wiki, miezi na miaka ilivyozidi kukatika. Mpaka Majaliwa anafika darasa la nne bado aliendelea kupitia malezi ya mateso kutoka kwa mama yake wa kambo, Radhia. Mpaka kufikia muda huo Majaliwa alifikisha miaka kumi huku mdogo wake akiwa na miaka takribani minne. Radhia alimfanyisha Majaliwa kazi za ndani bila kuzingatia umri wake. Tangu alipofikisha miaka saba hakuwahi kabisa kumfulia nguo za kushindia wala sare za shule. Mara nyinyi Majaliwa alikuwa anachelewa kwenda shuleni kutokana na kazi za nyumbani asubuhi. Kule shuleni akawa anachapwa fimbo kila siku kwa kosa la kuchelewa. Mara nyinyi sana Majaliwa alionekana kuwa mnyonge na kukosa furaha maana shuleni fimbo na nyumbani fimbo pamoja na kazi zisizokuwa na kikomo. Majaliwa alikuwa hapati muda wa kucheza na watoto wenzake mara baada ya kurudi nyumbani akitokea shuleni. Hata muda wa kupumzika alikuwa hapati maana vyombo vichafu vinakuwa vikimsubiria. Lakini pia hata zile adhabu za kunyimwa chakula bado zilikuwa zinaendelea pindi anapofanya makosa. Kwa kiasi kikubwa matukio hayo yalikuwa yanamuharibia taaluma mtoto Majaliwa. Ufaulu wake ukawa wa wastani kabisa tofauti na watoto wengine. Yote yaliyokuwa yanaendelea pale ndani, Kareem alikuwa hatambui kabisa maana hakuwa mtu wa kushinda nyumbani. Kila siku alikuwa anatoka asubuhi na mapema sana na kuwahi kwenye biashara zake. Mpaka kufikia muda huo alifanikiwa kufungua ofisi nyingine ya biashara na alinunua gari dogo la kuendea kwenye biashara zake. Alikuwa na muda mchache sana wa kukaa na familia hivyo malezi yote ya watoto yalikuwa chini ya mke wake Radhia. Muda wake wa kurudi nyumbani ulikuwa usiku wa saa 3 au 4. Lakini sasa, Yale mabadiliko ya kimwili na kiakili aliyoyaona kwa mwanae Majaliwa yalimfanya ahisi kuna kitu hakipo sawa pale ndani. Siku hiyo Kareem akaamua kumuuliza mwanae maswali machache maana alikuwa hapatagi kabisa muda wa kukaa na mwanae.
“Maja mwanangu, Vipi shule unaenda kila siku?
“Ndio Baba!
“Unakula na kushiba kila siku?
“Ndi…. ndi…. ndio Baba!
“Mama yako huwa anakupiga?”
Kareem alipouliza hilo swali Majaliwa akakaa kimya bila kujibu chochote. “Mbona hujibu mwanangu, Niambie mimi Baba yako usiogope. Niambie mwanangu, Mama huwa anakupiga?” Kareem alimuuliza mwanae kwa mara ya pili.
Majaliwa alitingisha kichwa kwa ishara ya kukataa akimaanisha kwamba hapigwi na mama yake wa kambo.
“Sikiliza wewe Ngedere mtoto,
Ukithubutu kumwambia Baba yako kwamba nakutesa basi nitakukata kabisa hayo masikio. Umesikia wewe mpumbavu?
“Ndi….. Ndi……. Ndio Mamaa!
“Pumbavu! Nilikuambia kama Baba yako hayupo uniite nani?
“Bo….. Bo….. Boss!
“Sasa ole wako uniite tena Mama kama Baba yako hayupo. Mimi ni mama yake Fetty sio Majaliwa. Baba yako hajakuambia tu ukweli ila mama yako ameenda uarabuni kudanga sio kufanya kazi. Narudia tena kukuambia wewe Kima, Ole wako umwambie Baba yako kwamba nakutesa. Akikuuliza chochote mwambie kwamba nakupenda, nakufulia, unakula vizuri na unaenda shuleni kila siku.” Hiyo ni kumbukumbu ya Majaliwa akikumbuka namna alivyopewa vitisho na Mama yake wa kambo ili asithubutu kumwambia ukweli Baba yake. Majaliwa alitii amri ya mama yake kwa kuwa alikuwa anamuogopa kuliko Simba. Na mpaka kufikia muda huo, Majaliwa alikuwa anajua Mama yake mzazi alimuacha akiwa mdogo na kwenda uarabuni kufanya kazi. Bwana mdogo hakuwahi kabisa kuijua sura ya mama yake mzazi hivyo ilimuuma sana. Malezi ya
Majaliwa yalianzia kwenye mikono ya Bibi yake (Mama Kareem) tangu akiwa mtoto mchanga mpaka kufikia umri wa miaka tano. Baada ya hapo
Kareem akaamua kumchukua mwanae na kuanza kumlea chini ya malezi ya mama wa kambo. Ingawa Kareem alimchukua Majaliwa kutoka kwenye mikono ya Bibi yake lakini Bibi yeye bado alikuwa anatamani kuendelea kumlea mjukuu wake. Ukweli ni kwamba alikuwa anampenda mjukuu wake kwa kuwa ni damu ya mwanae Kareem. Na kwa taarifa iliyokuwa mezani kuhusu mama mzazi wa Majaliwa ni kwamba aligombana na Kareem kisha akam’bwagia mtoto na kutimkia uarabuni kutafuta Rial (Pesa). Hakuna ndugu wala rafiki yeyote aliyekuwa anamjua Mama mzazi wa Majaliwa zaidi ya Kareem mwenyewe.
Episode 14
Matukio yote yaliyokuwa yanaendelea ndani ya nyumba kati ya Majaliwa na Mama yake wa kambo, Kareem hakuweza kabisa kuyatambua mpaka Majaliwa alipofika darasa la saba. Matokeo ya mtihani ya Mock, Darasa la saba yalikuwa mabaya sana kwa mtoto Majaliwa kiasi kwamba Kareem alipata mshangao.
Alishangaa sana kuona mwanae amefeli hivyo ilitoa ishara mbaya sana kwa baadae ya mwanae. Yale matokeo ndo yalimwamsha Kareem katika suala zima la kufuatilia maendeleo ya mwanae ili kubaini chanzo cha kufeli. Kuna kitu alihisi hakipo sawa kuanzia nyumbani mpaka shuleni ndo maana mwanae amefeli mtihani. Alichokifanya Kareem ni kwenda kimya kimya kwenye shule anayosoma mwanae ili kuonana na kuzungumza na walimu. Majira ya saa 5 asubuhi, Kareem alifunga ofisi yake na kwenda kwenye shule anayosoma mwanae. “Ooh! Umesema wewe ni mzazi wa Majaliwa Kareem?
“Yes, Ndo mimi Baba yake mzazi. “Okay! Karibu sana Mr Kareem. Mimi naitwa Madam Joan, Ni mwalimu wa darasa analosoma mwanao. Karibu sana mzazi, unaweza kuongea kile kilichokuleta hapa shuleni.
“Ahsante sana mwalimu, Kubwa zaidi lililonileta hapa ni kuhusu mwanangu tu. Haya matokeo aliyoyapata kwenye mtihani wake wa Mock yamenishtua sana kiasi kwamba nimepata wazo la kuja kujua mienendo yake kwa ujumla anapokuwa kwenye mazingira ya shule. Nyie walimu ndo wazazi wa wanetu wanapokuwa huku shuleni kwahiyo mnatambua kila kitu kinachopelekea hawa watoto kufeli au kufaulu.
“Ni kweli kabisa hujakosea Mr Kareem. Sisi walimu ndo tunajua kwanini mtoto huyu anafeli na yule amefaulu. Lakini pia jukumu la mtoto kufeli au kufaulu linafanywa na mzazi kulingana na mazingira
anayomjengea mwanae. Unajua huyu Majaliwa ni mtoto mwenye upeo mkubwa sana darasani lakini nidhamu yake ndo inaharibu taaluma yake kila siku. Mwanao amekuwa na mahudhurio mabaya sana shuleni yani ni mtoro na amekuwa mchelewaji kwa hizo siku chache anazokuja shuleni. Sisi walimu tumejaribu sana kumnyoosha lakini jitihada zetu hazijafanikiwa mpaka leo hii. Hata nyie wazazi wa Majaliwa tulishawaita hapa shuleni na tukajadili kuhusu mwenendo wa mtoto wenu lakini cha kushangaza bado mtoto hajaacha utoro na uchelewaji.” Kauli ya mwalimu ilimfanya Kareem ashtuke kidogo. Alishtuka sana kusikia kwamba mwanae ni mtoro sana na mchelewaji wa shule. Hilo lilikuwa suala geni sana masikioni mwake. Lakini pia alishtuka sana kusikia kwamba wao kama wazazi wa Majaliwa walishawahi kuitwa pale shuleni, wakafika na kujadili kuhusu mienendo ya Majaliwa. Hilo pia lilikuwa geni kwenye masikio yake. “Mwalimu! Unajua hizi taarifa zote unazonipa ni ngeni kabisa masikioni mwangu. Kiukweli sijawahi kujua kama mwanangu ni mtoro wa shule wala sijawahi kujua kama ni mchelewaji. Lakini pia sijawahi kupata taarifa yoyote ya kuhitajika shuleni kwenye kikao cha kumjadili mwanangu. Au labda unazungumzia Majaliwa mwingine mwalimu? “Hapana! Majaliwa Kareem ndo ninayemzungumzia hapa maana yeye ndo Majaliwa pekee kwenye darasa langu. Lakini pia mzazi aliyefika kwenye kikao ni mtu aliyejitambulisha kama Mama yake Majaliwa na hata Majaliwa mwenyewe alithibitisha kwamba ni mama yake. Alafu sio mara moja tu, ni mara mbili hivi huyo mama alishafika hapa tukakaa nae kikao.
“Dah! Hapo umeniacha njia panda mwalimu maana mimi sifahamu chochote nikiwa kama Baba mzazi na naishi na mwanangu pamoja. Mwalimu, naomba kwanza niitie Majaliwa ili nimuulize huyo mama aliyemleta kwenye kikao ni yupi? Ni mke wangu mimi au amemkodisha mtaani? Kama ni mke wangu, kwanini sikuambiwa chochote?”
Mwalimu wa darasa alitoka nje ya ofisi kisha akamuagiza mwanafunzi fulani akamuite Majaliwa Kareem. Baada ya dakika mbili Majaliwa akafika ofisini na kumkuta mwalimu wa darasa pamoja na Baba yake. Alishtuka sana kumuona Baba yake pale shuleni hivyo akajua yajayo hayafurahishi kabisa. Mwalimu wa darasa alimuuliza Majaliwa, “Majaliwa! Unamjua huyu?
“Ndio namjua.
“Nani huyu?
“Baba!
“Ndo unayeishi nae nyumbani kwenu?
“Ndio!
“Okay! Unakumbuka nilishawahi kukuagiza uje na mzazi wako hapa shuleni?
“Ndio nakumbuka mwalimu.
“Enhee, Yule uliyemleta ni nani?
“Yule ni Mama yangu.
“Mama yako unayeishi nae nyumbani kwenu? “Ndio mwalimu.
“Haya sasa Mr Kareem nadhani umeupata ukweli kutoka kwa mwanao mwenyewe.”
Mpaka kufikia hapo Kareem akapata uhakika juu ya kauli alizozungumza mwalimu hapo awali. Mwanaume akabaki na maswali kichwani, kwanini mke wake hakumwambia chochote kuhusiana na suala la wao kuhitajika shuleni? Kwanini aliamua kumficha wakati yeye ndo Baba mzazi wa Majaliwa na yeye ndo Baba wa familia.
“Maja!
“Naam Baba,
“Kwanini hukuniambia?
“Nisamehe baba, Nilimfikishia taarifa mama akaniambia nisikuambie yeye atakuja shuleni kuonana na mwalimu. “Kwahiyo Mama yako ndo anafuga ujinga unaoufanya si ndio?” Kareem alimuuliza Majaliwa kwa hasira.
Majaliwa hakujibu chochote badala yake akawa anatokwa na machozi. “Maja, Kwahiyo siku zote najua mwanangu unakuja shule kumbe hauji? Naomba unipe sababu ya msingi inayokufanya uwe mtoro na mchelewaji wa shule.”
Swali la Kareem likazidi kumtoa machozi Majaliwa kisha akasema “Nisamehe sana baba, Natamani sana kuja shule kila siku bila kuchelewa, Natamani sana kusoma na kufaulu mitihani kama wanafunzi wenzangu lakini tatizo Mama.”
Episode 15
Baada ya Majaliwa kumtaja Mama yake kama kikwazo cha yeye kwenda shule, Kareem alishtuka sana maana alijua mke wake Radhia ndo anayezungumziwa pale.
“Mama yako amefanyaje Maja? Hebu niambie mwanangu, Kivipi tatizo ni mama yako?” Kareem alimuuliza mwanae huku akiwa na shauku kubwa ya kutaka kujua jambo lililojificha. Alihisi kabisa kuna jambo linafanyika nyuma ya mgongo wake bila kujua. Lakini sasa Majaliwa hakuweza kabisa kufungua mdomo wake na kuzungumza namna mama yake alivyokuwa tatizo kwenye safari yake ya masomo. Kadri Kareem alivyomtaka mwanae amwambie
ukweli ndivyo machozi yalivyotiririka kwenye mashavu ya Majaliwa. Kareem akajua kabisa kuna jambo zito lipo kwenye moyo wa mwanae ndo maana anashindwa kuongea. “Madam, Kwa leo naomba unipe ruhusa niondoke na mwanangu nikazungumze nae nyumbani maana nahisi kabisa kuna kitu kibaya kinaendelea kwenye kifamilia. “Sawa Mr Kareem, Ni ruksa unaweza kumchukua mwanao ila nakuomba tu usitumie hasira ukampiga maana anaonekana hana hatia yeyote maskini.
“Ondoa shaka kabisa Madam siwezi kumpiga mwanangu bila sababu ya msingi. Huyu mtoto nampenda kuliko kitu chochote na siku zote napambana ili kuhakikisha anapata haki zake zote za msingi. Maja mwanangu, Nenda kachuku daftari zako tuondoke nyumbani.”
Majaliwa alielekea darasani kuchukua begi lake la daftari kisha akaongozana na Baba yake mpaka kwenye gari kisha wakaondoka pale shuleni. Safari ilikuwa kuelekea nyumbani kwao lakini kabla hawajafika, Kareem akasimamisha gari na kupaki pembezoni mwa barabara. “Maja,
“Naam Baba.
“Nakupenda sana mwanangu. Nakupenda sana kuliko hata ninavyoipenda nafsi yangu. Siku zote napambana kwa ajili ya kuhakikisha nyie wanangu mnakuwa na furaha kwenye hii dunia. Wewe na mdogo wako ndo mnanipa mimi nguvu ya kutafuta pesa ili niwatengenezee maisha bora wanangu. Maisha bora kwenu yanaanzia shuleni ndo maana nimekupeleka shule ukasome mwanangu. Kila siku natoka asubuhi na mapema naenda kazini huku nikijua huku nyuma unaamka na kwenda shule. Kumbe mwanangu huendagi shule? Naomba uniambie mwanangu, Kipi kinakuzuia kwenda shule mwanangu? Ni kitu gani mama yako anakufanyia mpaka ushindwe kwenda shule? Niambie mimi Baba yako usiogope chochote mwanangu.” Kareem aliongea maneno hayo na kumfanya Majaliwa aanze kutokwa na machozi kwa mara nyingine.
“Baba eeh, Mimi hapa naogopa. “Unaogopa nini mwanangu?
“Namuogopa mama, Kama
nikikuambia atanifanya kitu kibaya.” Kauli ya Majaliwa ilimshtua sana
Kareem na kuzidi kumvuruga akili. “Maja mwanangu! Hakuna mtu yeyote anayeweza kukufanya kitu kibaya wakati bado nipo hai. Niambie mwanangu, Kitu gani mama yako anakufanyiaga ninapotoka kwenda kazini. Niambie mwanangu mimi ndo Baba yako.
“Baba eeh, Kila siku asubuhi lazima nifanye usafi wa nyumba nzima na kuosha vyombo kabla sijaenda shule. Kazi zinakuwa nyingi sana kiasi kwamba natumia muda mwingi hivyo nashindwa kwenda shule na nikienda huwa nachelewa. Yule Mama’angu hataki mimi nisome na aliniambia sitakiwi kufaulu kwa sababu hakuna pesa za kunisomesha. Baba eeh, Mwanao mimi napigwa sana na kumnyima chakula kila ninapofanya makosa pale ndani. Mama kaniambia atanifanya kitu kibaya kama nikikuambia wewe ukweli.” Majaliwa alizungumza maneno hayo huku akiendelea kutokwa na machozi. Maneno ya Majaliwa yalimfanya mtu mzima Kareem adondoshe machozi ya uchungu. Hakuamini kabisa masikioni kusikia mwanae ananyimwa chakula anachokitafuta kwa jasho lake. Hakuamini pia masikio yake kusikia mwanae ananyanyasika kwenye nyumba aliyoijenga kwa jasho lako.
“Kwahiyo mwanangu hayo mambo mama yako ameanza kukufanyia lini? “Ni miaka yote Baba mimi nateseka pale ndani. Hata leo nimeondoka nyumbani na kuja shule bila kufanya usafi wa nyumba kwahiyo adhabu yangu ni kutokula chakula cha mchana na kipigo kinanihusu nikifika nyumbani. Ila Baba naomba tu usimwambie Mama kama mimi nimekuambia. Mimi nitavumilia tu Baba kwa kuwa sina sehemu yoyote ya kwenda kuishi. Natamani sana na mimi ningekuwa karibu na mama yangu mzazi naamini ningepata upendo kama watoto wengine.” Maneno ya Majaliwa yalizidi kumuumiza kichwa Kareem na kumliza kabisa. Kareem alipangusa machozi kwenye mashavu yake kisha akafuta machozi mwanae na kumkumbatia kwa upendo. “Maja mwanangu, Nisamehe sana Baba yako kwa kushindwa kukutunza na kukulinda. Haya ni makosa yangu mwanangu nimeshindwa kufuatilia mienendo yako kwa ukaribu zaidi. Ni makosa yangu mimi kwa kuwa bize na utafutaji wa pesa kuliko kukuzingatia mwanangu. Ni makosa yangu pia kuamini kwa asilimia mia kwamba mama wa kambo ni mama. Nisamehe sana mwanangu ila nikuhakikishie tu kwamba haya makosa hayatojirudia tena. Kuanzia leo usinitazame mimi kama Baba tu bali nitazame kama mama yako pia. Kama nilivyokuambiaga mama yako alikuacha mikononi mwangu ukiwa bado mchanga kisha akatokomea uarabuni kwa tamaa za pesa. Hili limekwisha mwanangu, kuanzia leo furaha yako itarejea upya. Utasoma vizuri, utakula na kulala bila kipengele chochote.” Kareem alimwambia mwanae maneno hayo kisha akawasha gari na kuanza safari kuelekea nyumbani kwake.
INAENDELEA…………..