KIBURI CHANGU KIMENIPONZA
Wanandoa, niandikapo meseji hii nalia. Nawaomba msifanye makosa kama yangu. Kama mmegombana hakikisheni mnapatana kabla jua halijachwa. Msimpe Ibilisi nafasi.
Kilichotokea ni kwamba asubuhi ya siku ya tukio, tulikuwa tunakunywa chai na mke wangu mezani. Nikamuomba anipakie mkate wangu siagi lakini namna alivyokuwa anapaka sikupenda na nikajikuta nimemfokea kwa sauti ya juu.
“Weeee acha kunivimbia mimi unampandishia nani sauti ? Kama unaona napaka vibaya si upake mwenyewe?” Alinijibu kwa hasira.
(Niliinuka nikifyonza) “Haya kunywa hiyo chai yako sili na huo mkate wako sio lazima”
“Utajiju”. Alinijibu nami nikaondoka zangu kwenda kazini.
Niliporudi nilimkuta kakaa sebuleni ila kiburi changu kikaniambia usimsemeshe, mkomeshe hadi aje kukuanza yeye kukusemesha. Niliingia chumbani, nikaoga na kupanda kitandani.
Kuna sauti ikawa inaniambia msemeshe Irene lakini kiburi changu kinaniambia atapata bichwa.
Mara nikamsikia anakuja chumbani nikajifanya kama nimeshalala. Alilala muda mfupi na akaanza kuhangaika kugeuka geuka. Sikutaka kugeuka niliamua kumfundisha adabu. Baadae akaanza kunipigapiga mgongoni kama anayeniita lakini nikajifanya nimelala..
Basi baada ya muda mfupi akatulia na mimi nikawa nimepitiwa usingizi.
Asubuhi nikaamka na nikataka kumsalimu ila kiburi changu kikanizuia. Nikaingia bafuni nikaoga na kuvaa huku namtupia jicho la wizi. Kilichonishangaza nikagundua ni muda mrefu Irene amelala style hiyo hiyo bila kugeuka wala kujitikisa. Nikaangusha kopo la mafuta makusudi huku namtazama kwenye kioo kama atatikisika. Hakustuka. Nikaamua kumsogelea, “Irene” namuita lakini haamki. “Irene!!” Namgeuza na kumkumbatia na ndipo nagundua mwili wa baridiii. Irene amekufa!?! Naweka kichwa changu kifuani mwake nathibitisha kweli hakuna mapigo ya moyo. Irene alikuwa na shida ya Pumu kumbe yawezekana wakati ananiita alikuwa anahitaji msaada.
Jamani laiti ningemsikiliza Irene asingekufa.Najuta mimi kiburi changu kimenipotezea mke.
Nawashauri wanandoa wote chagua hekima kuliko hasira. Mwenzi wako sio mpinzani wako. Kuanzia leo usikubali kulala mkiwa mmegombana hakikisha mmeyaongea kabisa. Ona mimi nimempoteza Irene wangu kwa uzembe wangu mwenyewe.
1 Comment
Inatufunfisha vizr