MWANAUME WA NDOTO ZANGU
SEHEMU YA 91
Nakumbuka iIikuwa ni siku ya x-mass, kama kawaida mapema alfajiri alinipigia simu aliniambia nijiandae tuende kanisani pamoja. Nilimkubalia ila nilijiandaa haraka haraka kisha nilitangulia kanisani ili kumkomesha. Alinipitia nyumbani lakini hakunikuta, alinipigia simu sikupokea, alinikuta kanisani nikiwa nimekaa benchi la mbele. Sikumtazama usoni wala sikumchekea nyani nisije nikavuna mabua. Hata baada ya misa kuisha nilikuwa mtu wa kwanza kutoka, nilizama kwenye gari yangu nilirudi nyumbani.
Alinifuata hadi nyumbani akiwa na hasira, alinifokea kwanini nilimtoroka muda wa kwenda na kurudi kanisani? Nami sikutaka kujishusha sana, nikiwa na uso mkavu nilimuambia anisamehe kisha nilichukua vyombo vichafu nilivitoa nje kisha nilianza kuviosha. Alinifuata, aliniuliza nina matatizo gani mbona nimebadilika sana? Nilimjibu sina tatizo na wala sijabadilika.
“Sikuhizi hunichangamkii kama zamani, huonyeshi kama una hamu ya kuwa karibu na mimi. Kama kuna kitu nimekukosea naomba nisamehe”
“Hujanikosea chochote, kuwa na amani tu ndugu yangu” Niliongea kwa kujisikia nikiwa natembea tembea, mara niliingia ndani, mara nilitoka nje, yaani sikutulia hata kidogo.
“Gensuda” “Nakusikiliza”
“Nadhani unajua kuwa leo ni sikukuu, naomba baadae twende club ila nakuahidi sitokunywa bia, tunaenda kufurahi tu”
“Huna haja ya kuniahidi, we kama unataka kulewa nenda kalewe. Alafu kuhusu kwenda club siwezi kufanya hivyo siku kama ya leo, sitoenda”
“Eeh kwanini?”
“Leo nashangilia kuzaliwa kwa mtoto yesu, siwezi kwenda kwenye mambo ya anasa.
Nitashinda hapa hapa nyumbani na mama yangu”
Alinishangaa sana, alintazama kwa macho ya kiulizo alishindwa kunielewa nimekuaje. Kwa hasira aligeuka nyuma, alizama kwenye gari yake kisha aliondoka kwa kasi ya ajabu!
Nilitabasam kisha nilicheka kwa madoido, ndo akome kuringa! Ye si alinichukulia mimi punguani, haiwezekani anionyeshe mapenzi alafu aseme hanipendi, na nitamkera zaidi.
Alafu sio kwamba sikuwa na hamu ya kwenda club, nilitamani sana ila tu kiburi kilinikaa kichwani. Usiku alinipigia aliniomba tena nimpeleke Club lakini niliendelea kukataa, aliniambia kama mimi siendi na yeye haendi, alikata simu kisha tulinuniana. Siku iliyofuata nilijua ataendelea kunisumbua lakini hakunitumia meseji wala hakunipigia, mikausho ilizidi kupamba moto.
Wiki moja ilikatika tukiwa tumevimbiana. Hata jumapili iliyofuata hakutaka kuniomba tuende kanisani pamoja, badala yake aliamua kuongozana tena na Ex wake. Hapo kwa Ex sasa alinishtua, aliniogopesha sana, niliogopa hasije akanikomoa kwa kurudiana nae. Sio kanisani tu bali hata club walienda pamoja, walitembea pamoja, na za ndaani kabisa zilisikika zikisema tayari wamerudiana. Hapo sasa tumbo langu lilipata joto, nilianza kulia hovyo hovyo. Lakini licha ya skendo hizo sikumtafuta Genson kumuuliza wala
sikumsumbua. Nilikubaliana na matokeo, niliheshimu chaguo lake.
SEHEMU YA 92
Taarifa za Genson kurudiana na Ex wake zilimfikia Ex wangu Nasri. Nae hakutaka kupoteza muda, alinifuata dukani kwangu kisha alinipa pole. Alinisisitiza kuwa mimi nimeumbwa kwaajili yake, aliomba nimsamehe makosa yake yote kisha turudiane kwa kishindo kikubwa. Alikuwa tayari kunikabidhi mali zake zote mbele ya wanasheria endapo nitakubali kurudiana nae. Alinipigia magoti, alitoa machozi, alihuzunika kwa lugha zote lakini sikuwa tayari kurudiana nae; hakuniingia moyoni hata kidogo, mimi bado nilimuwaza Genson pekee, hisia zangu zilikuwa kwa Genso wangu hata kama hanipendi.
“Gensu achana na Genso, yule jamaa anakupotezea muda. Hivi unajua kuwa siku ya
mwaka mpya atamvisha pete ya uchumba Ex wake?”
“Ninii? Kwamba Genson anataka kumuoa Oliver?”
“Habari ndio hiyo, na nasikia wameshaanza kuandaa kadi na ukumbi… We endelea na ubishi wako, nakuambia turudiane lakini hunielewi!!
Unataka hadi wakuue kwa presha si ndio?….
Sawa naondoka, ila utanikumbuka”
Aliondoka aliniacha nikiwa nimezubaa kama chizi vile, niliwaza taarifa ya Genson kutaka kumvisha pete Oliver; kiukweli sikutaka kuiamini taarifa hiyo, nilihisi ni uzushi wa Nasri ili nirudiane nae. Nilijaribu kumpigia Genson ili nimuulize lakini hakupokea simu zangu, nilimtumia meseji hakujibu. Nilifunga safari hadi hospitali kazini kwake lakini sikumkuta, niliambiwa kuwa amepewa likizo ya maandalizi ya ndoa yake!! nusura nidondoke kwa mshtuko.
Haraka haraka nilirudi kwenye gari yangu kisha
nilielekea nyumbani kwake nako sikumkuta, nilimkuta mama yake tu ambaye aliniambia Genson kaelekea shopping kununua vitu kwaajili ya ndoa yake. Walizidi kunipagawisha, nilitaka kuruka uchizi, niliwaza hivi kweli Genson kaniacha mimi kisha kamchagua Oliver msaliti na mpenda pesa? Ama kweli mapenzi kizunguzungu, mapenzi upofu, mapenzi hayaeleweki, wanaume wote mbwa tu dadeq.
Nilirudi nyumbani nilifikia kitandani, kilichofuata hapo ni kilio tu. Siku ya kwanza nilishinda chumbani nikilia, nililia hadi sauti ilikatika. Siku ya pili sauti yangu ilirudi lakini niliendelea kulia hadi ilikata tena. Siku ya tatu sikulia, ila bado nilijifungia chumbani, nilikula tu ilimradi nisife ila sikuona ladha yoyote ya chakula.
Na hatimaye ilifika siku ya mwaka mpya. Siku hiyo nilibaki nyumbani pekeyangu, mama alialikwa kwenye sherehe za watu mtaa wa pili. Nikiwa nyumbani mida ya saa 12 jioni nilisikia mlango ukigongwa, nilihisi atakuwa ni Genson
kaja kuniona, haraka haraka nilienda kufungua mlango nilishtuka kukutana na Oliver Ex wa Genso. Alipendeza vibaya mno, alisuka vizuriii, uso wake ulijaa tabasam murua!!
“Mambo Gensu, nimekuletea kadi yako hii ya mualiko. Tafadhari baadae usikose, jambo la msingi hakikisha unapendeza sana, pendeza kuliko kawaida. Tukio litaanza saa 1 na nusu usiku, nakukumbusha usikose, kwaheri” Aliondoka mara baada ya kuniachia kadi.
Haraka haraka nilifungua kadi niliitazama, nilikuta imepambwa kwa maua mazuri na makopakopa. Ilikuwa na maandishi machache tu ambayo yalisomeka hivi; “Mpendwa Gensuda, leo hii tarehe 1 mida ya saa 1;30 usiku; familia ya Genson inakukaribisha katika tukio maalumu la kumvisha pete ya uchumba mpenzi wake ambaye wanapendana sana. Ni mpenzi ambaye amemchagua kuishi nae katika maisha ya ndoa, hivyo basi usikose kuja, ujio wako ndio ukamilifu wa shughuli hiyo; PLEASE USIKOSE”
SEHEMU YA 93
Sura yangu tayari ilibadilika, nilianza kulia tena. Nilijua wananisisitiza niende ili wakaniumize vizuri zaidi, ili wakaitoe roho yangu. Niliona bora nijitoe roho mapema kuliko kwenda kuhimili maumivu ya ukumbini. Shetani mtoa roho alinitawala kichwani. Niliwaza kujiua, fasta nilitupa ile karatasi kisha nirudi ndani nilichukua pesa nilielekea dukani; nilinunua sumu ya panya kisha nilirudi nyumbani ili ninywe nife.
Nilifika chumbani nilijifungua mlango, niliandaa sumu yangu vizuri kwaajili ya kunywa. Lakini kabla sijanywa mara simu yangu iliita; nilitazama nilikuta mpigaji ni Genson, licha ya kumchukia lakini nilijikuta nimepokea.
Alionekana kuwa na furaha sana, aliniambia kuwa nisikose kwenda ukumbini kwa sababu ameniandalia zawadi kubwa ambayo sikuwai kuipata tangu nizaliwe. Baada ya kumaliza kuongea alinipiga busu ambalo lilifanya nidondoshe sumu yangu. Nilihisi mwili wangu
wote umekufa ganzi, nilijiona kama napaa vile, aisee huyu mwanaume kama kunikamata tu alijua kunikamata!!
Kwa mara ya mwisho alinisisitiza nisikose kisha alikata simu. Sijui hata nilipata wapi nguvu za kusimama kisha nilielekea bafuni, haraka haraka nilijiandaa kwa kuvaa pamba kali.
Nilipiga gauni ndefu ambalo liliniachia umbo zuri, nilinoga kweli kweli. Licha ya kwamba sikusuka lakini nywele zangu nilizibana vizuri, maandalizi yalikuwa marefu kwelikweli. Nilikuja kushtuka tayari ilitimia saa 1 na nusu usiku, fasta nilitoka nje nilizama kwenye gari nilielekea ukumbini.
**** UKUMBINI;
Yaani ile naingia tu zilisikika shangwe na vigelegele, dj aliwasha muziki kisha aliweka song la GIDI GIDI GIDI GA GA GAAAA!! Nilihisi raha utadhani mimi ndo navishwa pete kumbe
wala!! Nilitembea kwa madoido, kamati ya mapokezi ilinionyesha sehemu ya kukaa.
Nilikaa pamoja na dada na mama yake Genson, pia nilishtuka kumuona mama yangu mzazi akiwa anatabasam kama sio yeye vile; walinisifia waliniambia nimependeza sana. Pia mama yake Genson alinipongeza kwa kuvaa kiheshma kuliko wanawake wengine ambao walivaa utupu utupu. Nilitabasam kwa furaha lakini roho iliniuma sana, laiti angejua jinsi navyompenda mwanae nadhani hasingeruhusu amvishe pete Ex wake.
Hadi muda huo sikumuona Genson wala Oliver, sikujua wapo wapi. Dakika zilikatika, saa mbili ilifika, ratiba ziliendelea, watu walikunywa bia, wengine waligonga soda, vyakula pia viliandaliwa. Ilikuwa ni party Party kweli.
Hatimaye saa tatu ilifika, watu hawakuonekana, hata hivyo niliona bora wachelewe tu mana niliogopa kuumia roho.
Mida ya saa tatu na dakika 10 Dj alitangaza
watu wote tusimame ili tuupokee ugeni rasmi ambao ulikuwa unasubiriwa. Tulisimamishwa na ngoma la UTU NA UTULIVU, kila mtu macho yalikuwa nyuma, na hatimaye ugeni mzito uliingia ukiwa umeongozwa na VVIP mwenyewe ambaye ni Genson, alipiga suti moja hatari sana. Pembeni aliongozana na Oliver pamoja na machawa wa kutoshaa, hadi kufikia hapo nilikata kauli, nilikosa matumaini, Jasiri niliumaliza mwendo.
SEHEMU YA 94
Wageni rasmi walikaa katika viti vya mbele. Genson na Oliver walikaa pamoja. Mc alisogeza maiki mdomoni kisha alitangaza kwamba muda wa mtu kuvishwa pete umewadia, alituomba watazamaji tuwe watulivu kisha alimsimamisha Genson alimuomba apite mbele kwaajili ya kukamilisha lengo kuu. Taratibu Genson akiwa anatabasam alisimama kisha alipita mbele,
aliutazama Umma.
“Kwanza nianze na Sallam, wakubwa zangu shikamoni!”
“Marhaabaaaaa!”
“Wadogo zangu hamjamboo?” “Hatujambooo”
“Na vijana wenzangu mambo vipi?” “Powaaaaa”
“Heshma kuu kwa mama yangu mzazi kokote aliko, yeye ndiye alinisisitiza nioe ili nimtafutie wajukuu. Lakini pia aliniambia nisiharakishe kuoa kwa kuokota mwanamke yeyote yule, alinishauri nichunguze tabia za wanawake kisha nichague aliye bora. Ni muda mrefu nimekuwa nikimtafuta, hata baada ya kumpata mama yangu alinipongeza aliniambia nimeweza kuchagua kinachonifaa katika maisha ya ndoa, na kinachoifaa familia yetu Jamani
natangaza kwenu kwamba mwezi huu nataka
kuoaaa”
“Oyoooooooooo oa babaaaa ule mzigoooooo upate watotoooo” watu walishadadiaa, palinoga sana ila tu mimi sikuwa na amani hata kidogo, tumbo la kuhara lilinivuruga vibaya mno.
“Leo hii nimewaalika hapa kwa sababu nataka niwaonyeshe mwanamke anayenipenda kwa muda mrefu, ninayempenda toka long time, ambaye nimemchagua mimi mwenyewe bila kushinikizwa na mtu yeyote, nitamtambulisha mbele yenu kisha nitamvisha pete ya uchumba… Jamani mko tayariiii?”
“Tuko tayari babaaaaaaa”
“Bila kupoteza muda, mwanamke nitakayemtaja muda huu, ambaye nitamuita hapa mbele, huyo ndiye nimemchagua awe wangu milele….
Mnaniruhusu nimtaje?”
“Mtaje baba mambo kunoga leoooo uwiiiiiiiiiii” Kwa jinsi ambavyo watu walipiga kelele za
furaha nilihisi nataka kuzimia, nilijua tu Genson anataka kumtaja Oliver wake. Nilipiga mahesabu itakuwaje endapo akimtaja, si naweza kufa kwa presha jamani mmh!!!!!…
Ghafla nilisimama, niliona sitoweza kuvumilia mitikisiko ya pwani, niliona bora tu nijiepushe na kifo cha kushtukiza!! Haraka haraka nilipiga mwendo kuelekea nje lakini kwa bahati mbaya mlangoni nilikutana na mlinzi;
“We dada unaenda wapi tena mida kama hii?”
“Sahamani kaka, nahisi kutita naomba nitoke nje”
“Ndugu mteja, kutita kwa sasa haiwezekani. Tafadhari rudi kwenye siti yako ili umshuhudie mke mteule wa Dokta Genso”
“Hivi we kaka hunionei huruma? Unataka nife kwa presha si ndio?”
“Rudi pale, niliambiwa muda wa pete nisiruhusu mtu kutoka nnje”
“Sawa bwana, nikifa mtanizika… ” Niliongea kwa sauti ya kukata tamaa, taratibu niligeuka tena kisha nilirudi kwenye siti.
Muda huo Genson alikuwa akipokea boksi la zawadi kutoka kwa kamati ya zawadi, boksi lilimeremeta kinoma. Baada ya makabidhiano wanakamati waliondoka, boksi lilibaki kwa muhusika. Sikutaka tena kutazama mbele, japo nilikuwa makini kusikiliza lakini niliamua kulala juu ya meza ili nisishuhudie kitu chochote. Kuna muda niliinuka nilimtazama Oliver, nilimuona akitabasam na kujishaua vibaya mno, alijikuta kinoma!! Nilimuonea sana wivu ila ndo hivyo yeye ndiye alichaguliwa, ni ridhki yake, sisi wengine tutaendaga kuolewa mbinguni au motoni na malaika au mashetani.
“Nafikiri kila kitu sasa kimekaa poa, zawadi ninayo mkononi… Natamani nimtaje mke wangu mtarajiwa ila naogopaaa”
“Jamani wewe usiogopeee, mtajeeee”
“Naogopa ndugu zanguuuu” Genso aliongea kwa kujishaua, hakujua kuwa alizidi kunirusha roho yangu
“Dokta Genso usiogopeee, mtaje mkeo tumjueeeee”
“Hii dunia ina wanawake jamani, lakini huyu wangu amewazidi wengi”
“Wacha weeeeee”
“Humu ukumbini kuna watoto wakali lakini huyu wangu amewazidi wengi”
“Usiseme hivyoooooooo”
“Wanawake wenye heshma wapo kila kona lakini huyu wangu amewazidi wotee”
“Uwiiii jamani mtajeeeeee”
“Binti aitwaye GENSUDA PINSLOTO MWAKONYO, wewe ndiye nimekuchagua, naomba popote ulipo simama kisha uje mbele”
Yaani laiti kama isingekuwa wifi yangu,
SEHEMU YA 95
ningedondoka na kuzimia. Mapigo ya moyo wangu yalikuwa yakipiga kwa kiwango kikubwa, mgandamizo wa damu ulikuwa mkubwa, presha ilipanda kwa kiwango kikubwa sana kiasi kwamba nilitamani kuruka kichaa.
Sikutegemea kama Genson angelitaja jina langu, sikutegemea kama ningekuwa chaguo lake, yaani sikutarajia kabisa.
Nilishindwa kusimama, nilibaki natemeka tu, watu walikuwa wanacheka kwa furaha, Genson alitabasam kwa raha, baadhi ya wanawake na mabinti wenzangu akiwemo Oliver walinifuata kisha walinizunguka walianza kuniimbia nyimbo, Dj nae aliachia song la mahaba!! Ukumbini palinogaaaaa!!!!
Sio wanawake tu, hata wanaume walimsindikiza Genson ambaye alinifuata nilipo kisha alininyanyua, alinishika mkono alinipeleka mbele. Kabla hajaongea chochote alinikumbatia kisha alinipiga bonge la dendraaaa!! Kwa mara ya kwanza tangu nizaliwe nilipokea denda tamu
kutoka kwa my boo my honey my sukari gulu!!
Nilivishwa pete, nilipewa maiki nilishukuru, Genson nae alishukuru, na mwisho maiki ilipelekwa kwa Oliver ambaye aliongea maneno yafuatayo ambayo yalisisimua watu wengi ndani ya ukumbi.
“” Mimi binafsi nilidhani nampenda sana Genson kuliko wanawake wengine, lakini baada ya kukutana na Gensuda niligundua kuwa kuna mwanamke mwenzangu ana upendo wa kweli kiliko mimi mwenye upendo wa tamaa. Katika wanawake wawili ambao wanamgombania mwanaume mmoja, mwanamke mmoja huwa ana vigezo vya kumpata mwanaume huyo ila ubaya ni kwamba wenye vigezo wengi huwa wanakata tamaa mapema, alafu sisi tusio na vigezo huwa tunapambana kwa vurugu zote ili tu kuziba ridhki za wenye haki. Sasa baada ya kugundua kuwa Gensuda ana haki kuliko mimi, niliamua kutengeneza urafiki na Genson ili kuona kama Gensuda atavunjika moyo au la,
pia nilitumia urafiki huo kumshawishi Genson hasimpoteze mwanamke bora kama Gensuda. Mimi Oliver nawakilisha wanawake wote wenye tamaa ya kuolewa na wanaume wenye mali, ni haki yetu kutamani ila ubaya wetu ni kwamba huwa hatumfuati mwanaume bali tunafuata mali zake. Sasa ikitokea siku mwanaume huyo anayumba kiuchumi huwa tunashindwa kumvumilia, tunamsaliti au tunamkimbia. Na Mwisho naomba niombe msamaha kwa Gensuda, nilimliza sana kiasi kwamba ilifikia hatua nilikuwa namuonea huruma. Gensu naomba nikuondoe hofu, huyu mumeo hanitaki kimapenzi hata kidogo, yaani tangu tulivyoachana miaka hiyo hatamani hata kuuona mwili wangu. Sijazini nae na wala hafikirii kukusaliti. Nami nakuhakikishia kuwa kwa sasa nimepata mchumba wangu mwingine, hivyo basi sitokusumbua tena kwenye mapenzi yako… Niwatakie maandalizi mema ya ndoa yenu” Oliver alimaliza, watu walishangilia,
zawadi zilitolewa, vyakula vililiwa, muziki ulichezwa, na hatimaye tafrija ilikwisha nikiwa nimetunukiwa pete ya uchumba.
Baada ya tukio kumalizika watu walianza kutawanyika, mimi na mchumba wangu tulikaa kwenye gari moja. Safari za kurudi nyumbani zilianza, msafara ulikuwa mkubwa kweli kweli, ndani ya magari watu waliimba nyimbo, miziki ilipigwa utafikiri nishaolewa kumbe ni pete tu.
Binafsi niliamini kinachofuata hapo ni kupelekwa hotelini kwenda kutumika, niliwaza lazma jamaa atakuwa amenipania sana mana kitambo sana nilikuwa nikimtega, nami nilitabasam kisha nilijiweka tayari kwaajili ya mpambano utakaopigwa chumbani. Niliona kuchelewa, nilitamani sana penzi lake.
INAENDELEA