MWANAUME WA NDOTO ZANGU
SEHEMU YA 76
Licha ya kumtega kwa mavazi na mikao ya kihasara lakini ubaya ni kwamba Genson hakuonyesha kushtuka, hakunishangaa, hakunitamani wala hakudata na mwili wangu! Jamaa alikuwa wa kawaida tu as if hakuona chochote cha kushangaza.
Aliweka zawadi juu ya godoro kisha alinitazama
kidogo alafu alitabasam. Nilijua atakaa kwenye godoro lakini alivuta kiti alikaa. Moyoni nilijiuliza huyu mwanaume ni wa wapi? Ni kabila gani huyu? Mbona hategeki?
“Gensuda” aliniita “Abee” niliitika taratibu
“Ulijua kuwa nitaingia chumbani kwako, sasa kwanini umevaa hovyo hovyo? Ni kwamba siku hizi umeanza kukosa heshma au?”
“Aah samahani Genson, tangu nilivyolala jana sikuamka kabisa na ndio maana bado nimevaa nguo hizi”
“Sawa. Basi ngoja nikupishe ubadili nguo kisha utaniita ukiwa tayari”
Aisee kama kupatikana tu nilipatikana. Kumbe hapa duniani kuna wanaume wa ajabu eeh!! Mi nilidhani angeniambia nibadilishe mbele yake lakini jamaa alitoka nje ili hasinione. Sikuwa na namna, kwa hasira nilienda kuoga kabisa,
nilipiga mswaki kisha nilirudi nilianza kujipara! Nilitaka kumkomoa kimavazi, pia nilitaka kumchelewesha hasiondoke haraka. Nilivaa gauni refu kisha nilifunga mkanda kiunoni. Ule mkanda wa kiunoni ulisababisha juu na chini kutengane, chini kulibinuka alafu juu kulilala, nilifanana na umbo namba 8. Nilizichana nywele zangu ndefu, nilijifunga mtandio kisha nilijipulizia pafyumu.
Safari hii sikutaka kuonyesha tabia mbaya, niliamua kumfuata huko huko sebuleni kwake; nilikaa pembeni yake. Mama angu hakutaka kutubughuzi, aliondoka alienda kwenye vicoba. Ndani ya mjengo tulibaki wawili tu, mimi na yeye, moyoni niliapa kwamba afe kipa afe beki siku hiyo ni lazma nimpate.
“Haya nichambe tena” nilimtania
“Sasa umependeza, yani hadi nimekutamani” “Mh mwongo wewe, sikuamini hata kidogo…” “Kweli, sasa husichoamini ni kipi?”
“Siamini tu, hata sijui siamini nini”
“Ah ah ah tuachane na hayo, unaumwa nini? Ni homa gani hiyo ambayo imefanya usiende kazini?” aliniuliza swali ambalo sikujua nilijibu vipi. Kiukweli sikuwa naumwa homa yoyote labda homa ya mapenzi tu, hata hivyo niliogopa kumchana makavu kuwa nampenda hasije akaniona najirahisisha kwake. Niliwaza nimdanganye naumwa nini? Nilikumbuka kuwa nina changamoto za uzazi.
“Mbona huniambii unaumwa nini? Au ulikuwa unanidanganya?”
“Sikudanganyi, si unakumbuka kipindi kile Nasri ananichamba kuwa sizai?”
“Nakumbuka, kwani unataka kuzaa?”
“Ndiyo nataka, kuna changamoto za uzazi zinanisumbua kiasi kwamba nimekuwa nashindwa kushika ujauzito!! Na nishazunguka hospitali zote lakini sijapona”
“Kama hospitali tumeshindwa kukutibu basi ngoja nikupeleke kwenye tiba mbadala, kuna jamaa yangu mzee wa mitishamba anahusika na mambo hayo.. Twende nikupeleke”
Na ndiyo maana Genson alifanya nimpende sana, ni kwa sababu alipenda kunijali na kunipambania katika shida na raha. Tulitoka nje tukiwa tumeshikana mikono, yaani ukituangalia unaweza sema sisi ni wapenzi kumbe jamaa hata kunitongoza kwenyewe hakunitongoza, na hakuonyesha dalili zozote kwamba kuna siku atanitongoza.
Tulizama kwenye gari yake kisha tulielekea kwa mtaalamu wa tiba asili. Njiani aliniambia namna anavyopenda wanawake wachakarikaji, wavumilivu, wasio wasaliti, wanaojitambua, wenye hekma na heshma. Aliniambia kuwa hapo zamani kabla hajaajiriwa alikuwa na mpenzi ambaye waliachana kisa pesa. Mpenzi wake alimsaliti kwa jamaa mwenye pesa. Na hayo yote yalitokea kwa sababu yeye na mpenzi
SEHEMU YA 77
wake wote hawakuwa na kazi, licha ya kukosa kazi lakini yeye pekee ndiye alikuwa anategemewa kwa kila kitu kwenye penzi lao. Aliombwa kila kitu hadi vocha jambo ambalo lilipelekea penzi kuwa gumu.
“Mh pole sana… Kumbe nawe ushasalitiwa”
Nilimpa pole
“Ndo hivyo, tangu siku hiyo nawachukia sana wanawake wasio na pesa.”
“Mh ina maana wewe huwezi kumpenda mwanamke maskini?”
“Naweza, ila ili niwe nae kimahusiano itabidi nimbadilishe kwanza aweze kujitegemea, anivutie kimafanikio na kimaendeleo kisha mambo mengine yafuate”
“Ooh hapo sasa nimekuelewa Genson” Nilijibu nikiwa natabasam, nilimuelewa vizuri sana.
Binafsi nilihisi ananipenda ila alitaka nifanikiwe kwanza ili nisije nikawa mzigo mkubwa kwake. Kutoka moyoni nilipanga kufanya mambo
makubwa kibiashara na kimaisha ili tu kumvutia anitongoze.
Tulifika kwa mtaalam wa tiba asili, nilipewa tiba nyingi ambazo nilitakiwa ninywe kwa mwezi mzima kisha ningekuwa na uwezo wa kushika ujauzito. Tiba hizo zilikuwa maalumu kwa kusafisha mfumo wa uzazi, mirija, hedhi na mengineyo. Licha ya kwamba nilikuwa nina pesa za kulipia dawa lakini Genson alilipa, kitendo hicho kilizidi kunihakikishia kuwa ananipenda sana.
Alinirudisha nyumbani kisha nae alielekea kazini kwake. Siku iliyofuata nilielekea kazini kupiga kazi kwaajili ya mafanikio. Nikiwa kazini kwanza nilijiuliza mafanikio ni nini?. Kupitia makala mbali mbali waliandika kwamba mafanikio yana maana nyingi. Kwanza, Mafanikio ni hali ya mtu kutimiza au kufanikisha kusudi au sababu ya kuwepo kwake duniani. Pia, Mafanikio ni ukamilishaji wa malengo yanayoipatia nchi, jamii au mtu binafsi ustawi, afya njema au
hadhi. Mafanikio pia hujulikana kama ufanisi, maendeleo au neema. Sio hivyo tu bali mitandao iliandika kwamba kila mtu anahitaji mafanikio, hakuna mtu atayekupa mafanikio ila mtu au watu wanaweza kukusaidia ufanikiwe.
“Kumbe kila anayehitaji kufanikiwa anatakiwa apambane yeye mwenyewe. Kumbe ndio maana kwenye ndoa wanaume wanafanikiwa alafu wanawake wengi hatufanikiwi kwa sababu tunadhani mwanaume ndiye atatupatia mafanikio. Pia hapa wameandika mafanikio ni matokeo ya kazi fulani, ina maana watu wasio na kazi hawawezi kufanikiwa. Wasio na malengo au mipango nao hawawezi kufanikiwa. Wanawake tegemezi hawawezi kufanikiwa.
Kumbe ndio maana Genson anataka nipambane nifanikiwe kwa kutimiza malengo yangu…
Kwanza inabidi nijiulize malengo yangu ni yapi?…. Kujenga nyumba yangu, kununua gari yangu, kuweza kumudu mahitaji yangu muhimu pamoja na kusaidia wenzangu wasiojiweza….
Kwahiyo nikitimiza hayo yote Genson atanipenda si ndiyo?… Ndiyoo bwanaaa” Nilitafakari kiasi kwamba nilibaki natabasam tuuu!!
Nilitengeneza malengo ya muda mfupi na muda mrefu. Kitu cha kwanza kununua kilikuwa ni Uwanja wangu binafsi, Genson alinipongeza kwa kumiliki ardhi. Kitu cha pili kununua ni gari yangu ndogo, nzuri, ya kutembelea. Nakumbuka baada ya kununua gari mitaa iliniheshimu sana, wale waliokuwa wananitamani walinipenda kabisa, idadi ya wanaume waliokuwa wananitongoza iliongezeka kwa kiwango kikubwa. Sio hivyo tu bali watu wengi waliyatamani maisha yangu, walitamani kuwa kama Mimi. Genson ndiye alikuwa mwalimu wa kunifundisha kuendesha gari, muda wote alinipongeza kwa kupiga hatua kubwa za kimaisha.
Jambo la tatu ambalo nilifanya ni kununua bajaji mbili kisha niliwapa vijana wawili wasio
na ajira, walinifanyia kazi kwa mmkataba maalumu. Bajaji ziliniongezea kipato lakini pia ziliwapa ridhki vijana wenzangu ambao niliwaajiri. Pia mara chache nilikusanya michango kutoka kwa marafiki zangu kisha tulipeleka misaada kwa watu wenye uhitaji, ilifikia hatua walinichagua kuwa mwenyekiti wao wa kikundi cha kutoa misaada, nilijisikia fahari, Genson aliniambia kuwa hata kama bado sijatimiza malengo mengi lakini nimefanikiwa.
Kitendo cha kuambiwa nimefanikiwa kilifanya nijione wamotooo!! Nilihisi raha vibaya mno. Ila sasa licha ya mapambano yote hayo lakini Jamaa hakunitongoza. Nikajiuliza au ni domo zege ananiogopa? Sasa kama ananiogopa si aseme nimsaidie. Na ukicheki nilitimiza zaidi ya mwaka mzima pasipo kukutana kimwili na mwanaume yeyote alafu jamaa alikuwa ananiacha tu badala ya kunitongoza ili anizagamue, kiukweli alinikera sana. Niliamua kufanya jambo, siku hiyo tukiwa matembezini
nilimfungukia. “Genson”
“Naam mwanamke wa Nguvu”
“Ah ah ah sasa jamani mi nina Nguvu gani, kujenga kwenyewe tu bado sijajenga.
Nimepanga nijenge mwakani”
“Hata husipojenga lakini kwa ulipofikia wanawake wengi wameshindwa. Kwa sasa wewe hauna shida za kifedha, na hata ukisema umpende mwanaume nadhani utampenda kimapenzi sio kitamaa! Hivyo ndivyo inavyotakiwa”
“Asante my G, but unajua nini?” “Eeh niambie”
“Ni muda mrefu umepita tangu nimalize kutumia zile dawa za asili za uzazi, mtaalamu aliniambia nikimaliza kutumia dawa hizi nitakuwa na uwezo wa kushika ujauzito.
Kiukweli natamani sana nijue kama nina uwezo
huo, natamani nijue haraka ili kama bado sijapona nipate tiba nyingine”
“Ok, unamaanisha kwamba inabidi ufanye mapenzi si ndiyo?”
“Ndiyo, nataka kufanya tendo ili nijue kama nina uwezo wa kushika mimba”
SEHEMU YA 78
“Umeongea jambo zuri, nakuunga mkono. Bila shaka umeshampata mwanaume wa kufanya nae… Nenda ufanye nae ujue kama umepona”
“Mh bado bwana sijampata, Na ndio maana nimekuambia wewe”
“Sasa unaniambia Mimi nitakusaidia nini? Kwani mi ni mwanaume wako?” Alinijibu kwa kunikazia sauti, ni kama alipaniki vile.
“Wewe sio mwanaume wangu, mi nimekuambia tu jamani…. Nisamehe basi kama nimekukosea “
“Okay!!”
“Vipi umenisamehe Genson?”
“Sawa, turudi nyumbani mi nishachoka kutembea. Nataka nikalale”
Ngoma ilikuwa ngumu. Jamaa kila nikimleta kati alijitoa ufahamu, alifanya kama hanielewi vile. Sasa sijui ni kweli hakunielewa au alikuwa ananifanyia makusudi. Kuna muda nilihisi ananipenda kweli lakini kuna muda niliona kama hanipendi, mana kwa jinsi wanaume walivyo na tamaa haiwezekani awe karibu na mimi kwa zaidi ya mwaka mmoja pasipo kunitongoza.
“Huyu atakuwa hanipendi tu, anadanganya yupo singo kumbe ana mwanamke wake Anataka
kusema na yeye ana mwaka mzima hajaseksi?? Mmh yaani mwanaume hasisekc mwaka mzima? Wanaume wa kizazi hiki cha kina Manshyne? Thubutuuuu…. Huyu ana mtu ambaye wanafanyaga mambo yao Sasa
hapa itabidi nipate uhakika kama ana mtu au hana. Na itabidi nijue kama ananipenda au hanipendi. Kwanza natakiwa nitafute mwanaume feki aigize kama mpenzi wangu, mwanaume huyo nitapita nae mbele ya Genson ili nimrushe roho. Kama kweli ananipenda najua ataumia na atapata wivu. Pia akiona nina mwanaume lazima nae atamfukua huyo mwanamke wake anayemficha…. Subiri tuone” Niliwaza nikiwa natabasam, niliona mpango wangu umekaa sawa.
*****
Siku iliyofuata bila kupoteza muda nilitafuta mwanaume wa bandia, nilimlipa pesa ndogo tu (Tsh elfu 10) kwa siku moja tu. Mwanaume huyo nilimwambia aigize ana homa kisha nilimpeleka hospitali kwa Genson. Tukiwa maeneo ya hospitali kazi yetu ilikuwa ni kujizungusha tu, mkononi nilibeba maua
mekundu.
Muda mwingi tulikatiza karibu na ofisi ya Genson ili akitoka atuone, baada ya mizunguko mirefu hatimaye Genson alitoka nje kisha alibahatika kutuona. Mimi pia nilimuona ila nilijidai kama sijamuona vile. Kitu nilichofanya ni kumrusha roho, kwa mahaba mazito nilimkumbatia mwanaume feki kisha nilimpa maua. Nilijua Genson ataganda ili atutazame vizuri lakini jamaa hakuwa na muda wa kupoteza, alitutazama mara moja tu kisha alisepa zake. Pale pale nilinuna, nilimsukuma jamaa feki kisha nilimwambia aondoke zake apite kushoto nami nipite kulia, nilienda kusimama mlangoni nilimsubiri Genson arudi ili nione ataniambia nini. Baada ya dakika 20 Genson alirudi alinikuta nje la lango la kuingilia ndani hospitali.
“Vipi mbona umeganda hapa? Mshamaliza kubebika?” Aliniuliza, moyoni nilifurahi kugundua kuwa alituona
“Kubebika? Kubebikaje? Na nani?”
“We si nilikuona ulikuwa na mchumba wako mkikumbatiana mkipeana maua, au haukuwa wewe?”
“Mh jamani yule sio mchumba wangu, ni rafiki yangu tu… Nilimleta hapa hospital ila kashaondoka”
“Hayo mengine utajua wewe. Nachojua mimi ni kwamba ulitaka kutuonyesha walimwengu kuwa una mpenzi, hongera sana, tushamuona….
Kwaheri, nipo bize na kazi” Aliondoka alielekea ofisini kwake, nilibaki nimeganda kama mstimu wa umeme, pozi lolote lilinikwisha, taratibu kinyonge niligeuka nyuma nilizama kwenye gari yangu nilirudi nyumbani.
Zilipita siku mbili sikuonana na Genson, meseji zangu hakujibu na nikimpigia hakupokea. Alizidi kunichanganya, nilijiuliza sasa kama hanipendi kwanini aninunie? Kwanini akasirike baada ya kuniona na mwanaume feki?…. Kutokana na
hofu nilifunga safari nilimfuata kazini kwake lakini hakuwa na muda wa kukutana au kuongea na mimi; muda wote alikuwa bize na wagonjwa. Nilijipa matumaini akipata muda atanitafuta lakini masaa yalipita hakunitafuta.
SEHEMU YA 79
Siku iliyofuata nikiwa kazini nilishtushwa na ugeni mzito, ugeni ambao sikuutarajia hata kidogo. Nilitembelewa na Nasri ambaye alikuja na baskel, sio kawaida yake kutembelea baskeli, Na sikujua gari yake ipo wapi. Pia hata mavazi yake hayakuwa ya kawaida, Mara nyingi alizoea kuvaa suti lakini siku hiyo alivaa kinjunga na singlendi. Ni muda mrefu hatukuonana, na sikuwaza kama kuna siku nyingine tungeweza kuonana.
Nilitulia nikimtazama, nilijiuliza kaja kufanya nini?. Kuna muda nilihisi labda kaja kutoa au kuweka pesa lakini mkononi hakuwa na simu
wala fedha, alikuwa mpole, alisimama pembeni alisubiri wateja wengine wote waondoke kisha alisogea dukani.
“Dah kitambo sana yani, mzima lakini Gensuda wangu?”
“Mi ni Gensuda wako?” Nilimuuliza kwa hasira
“Eeh jamani unafanya utadhani hunijui.. Hongera sana Kwa Biashara nzuri”
“Asante, unahitaji huduma gani? Unatoa au unaweka fedha”
“Duh! Mi sijafuata hayo mambo ya kutoa na kuweka, nimekufuata wewe….. Unajua mini Gensu, najuta sana kukupoteza. Nilikuchezea sana nikiamini hutokuwa na uwezo wa kuniacha. Nilikukandamiza wewe wa muhimu kisha nilimpa cheo Rahabu ambaye leo hii anafanya nione ndoa chungu. Mimi na Rahabu kila siku tunagombana, anarudi saa nane za usiku akidanganya kuwa alikuwa bize na kazi. Rahabu amefanya niuze gari yangu ili nikuze mtaji wa
biashara yake ambayo sijawai kuona faida yake. Zamani nilikudanganya kuwa nina madeni, kumbe pesa nilikuwa nampa Rahabu. Lakini leo hii Rahabu amenisababishia madeni ya ukweli ukweli kiasi kwamba kila mwezi sipati mshahara wowote, imefikia hatua nafikiria kurudi kwenye kuuza mkaa… Na itabidi nifanye hivyo ili niwe kama zamani. Lakini hayo yote yametokea kwa sababu ya roho mbaya yangu kwako, naomba nisamehe Gensu”
“Haya nimekusameh. Alafu unaziba nafasi ya wateja, unaweza kuondoka.
“Mh usinifanyie hivyo, kumbuka nilikowatoa wewe na mama yako. Hata kama kuna mabaya nilikutendea lakini kumbuka mazuri yangu”
“Jamani kwani we unatakaje? Si nimekuambia nimekusamehe au?”
“Shida yangu sio msamaha tu, mi bado nakupenda Gensu. Nakuhitaji kwenye maisha yangu, Na nakuahidi ukirudi kila kitu utakitawala
SEHEMU YA 80
wewe. Nipo tayari kuachana na Rahabu kwaajili yako “
“Ah ah ah shenzi kweli. Kwanza Mimi sijawahi kukupenda wewe, ni uongo na ulaghai wako tu vilifanya niishi pale kwako. Pia ni kwakuwa kipindi kile sikuwa na akili nzuri ya kufanya maamuzi. Ni kwa sababu nilikuonea huruma kutokana na misaada ambayo ulitupatia. Ni kwa sababu Mimi na mama yangu hatukuwa na pa kukimbilia… Lakini leo hii nina kila kitu ambacho nimekitafuta kwa jasho langu, kama nyumba tunayo, gari ninayo, Biashara kubwa ninayo, pesa ninazo, Na kubwa zaidi mpenzi ninaye; muda si mrefu atanioa”
“Mpenzi yupi?… Wewe una mpenzi gani?.. Sikiliza nikuambie, Mimi najua unampenda Genson, Na unaamini yule ndiye mwanaume wako sahihi. Unadhani kwamba ipo siku atakuoa, hawezi kukuoa kwa sababu hakupendi”
“Nini?”
“Sio kila mtu anayekusaidia anakutaka kingono au kimapenzi, Genson sio kama mimi, yule jamaa alikusaidia kiwema tu lakini ana mwanamke wake. Wanapendana sana. Na ndio maana hadi leo hii hakutongozi wala hajakuambia jambo lolote kuhusu mapenzi, jamaa hakutaki… Na hivi ninavyokumbia Genson yupo mgahawani na mpenzi wake wanakula chakula na vinywaji, wanapendana sana…”
“We nini! Unasemaje?” Nilichanganyikiwa, pia nilivurugwa kusikia Genson ana mpenzi wake ambaye wanapendana sana. Kwanza nilihisi labda ananidanganya kwakuwa nimekataa kurudiana nae.
Nilimbishia nilimwambia ananidanganya. Aliniambia nifunge duka kisha nimfuate anipeleke mgahawani aliko Genson na mpenzi wake. Haraka haraka nilifunga duka kisha
tulianza safari, yeye alitembeza kibaskeli chake; mimi nilikuwa nikimbia njia nzima. Baada ya kupiga kona nyingi hatimaye tulitokea mgahawani (cafeteria), wateja walizagaa kwenye kila meza; mimi macho yangu yalikuwa yakimtafuta Genson lakini sikumuona.
Nasri aliniambia nitazame pembeni yangu chini ya mti, niligeuza macho haraka haraka! Ni kweli nilimuona Genson akiwa amekaa meza moja pamoja na binti mrembo wa wastani. Binti huyo ndiye alionekana kuongea sana kuliko Genson ambaye alikuwa anasikiliza kwa umakini. Kuna muda nilimuona binti huyo akiukumbatia mkono wa Genson, aliubusu kisha aliukumbatia kifuani kwakwe, aliubana kimahaba!! Weuwee!
Niliweweseka kiasi cha kutaka kuweuka!! Mizuka ilinipanda! Hasira zilinishika na wivu ulinitawala!!
INAENDELEA