MWANAUME WA NDOTO ZANGU
SEHEMU YA 66
“Nini?… Wewe umejuaje?”
“Nimefuatilia nimegundua hivyo. Licha ya kwamba mumeo alimfukuza Rahabu pale kwenu lakini bado walikuwa wanaendelea kimahusiano. Alimpangia chumba, alimnunulia gari na mwisho walitengeneza kesi za uongo ili achukue vitu alivyokupa (nyumba, gari na biashara) alafu ampe Rahabu.”
“Kumbe ndio maana mali zangu zote anazo Rahabu? Sasa kwanini hukuniambia mapema?”
“Sikutaka kuwagombanisha, hata leo nakuambia lakini sitaki ukamuambie chochote. We kaa kimya tu ila uwe makini na ndoa yako.
Yale yote anayofanya Rahabu anaambiwa na mumeo. Kwa sasa hakupendi wewe, anampenda Rahabu”
Nilishindwa kuongea kitu, nilipata uchungu na hasira kali lakini Genson alinituliza aliniambia niwe mpole. Alinichukua alinipeleka out, tulizunguka mitaani, alininunulia zawadi mbalimbali, tulifurahi pamoja na usiku tulirudi
nyumbani kwake.
Licha ya kwamba usiku huo alitakiwa kwenda kazini kwenye zamu ya usiku lakini aliniambia hatoenda kwaajili yangu. Kiukweli nilifarijika mno, nilihisi kama niko kwenye dunia nyingine. Ndo kwanza ilikuwa siku yangu ya pili lakini niliingia jikoni, sikupika pekeyangu; nilipika pamoja na Genson ambaye muda wote alikuwa karibu yangu. Uzuri wa mimi ni kwamba nikipataga mtu anayenithamini sana, huwa ni mwepesi sana kumsahau mtu aliyekuwa hanithamini. Hivyo basi kwa wakati huo nilimsahau kabisa mume wangu!! akili, muda na fikra zangu zote niliziamishia kwa Genson ambaye alionyesha kunipa kipaumbele katika nyazfa zote. Genson alifanya nione tofauti ya sisi wanawake na wanaume.
Sasa wakati tunaendelea kupika mara simu yangu iliita. Nilijua ni mama mzazi anataka kunisalimia, lakini baada ya kutazama nilikuta ni mume wangu; kwa jeuri kubwa sikupokea.
Alipiga zaidi ya mara 5 na zote sikupokea. Alinitumia meseji aliniambia nirudi nyumbani haraka, sikumjibu. Alinitumia meseji nyingine alinituhumu kuwa nipo kwa mchepuko hivyo basi nirudi haraka nyumbani, sikumjibu. Kwanza nilikasirika, sikutamani kabisa kurudi nyumbani. Yeye si aliamua kunisusa!! Kama alinisusa basi na asuse!! Eeeh asuseee!!
“Gensuda” Genson aliniita
“A-abee” niliitika kwa adabu na heshma zote
“Naona mumeo anakupigia alafu hupokei simu, unataka akuhisi vibaya si ndio? Ebu rudi nyumbani, hata kama anakutesa lakini hupaswi kumuonyesha tabia mbaya. Wewe endelea kuwa mwanamke bora, malipo yako yatapatikana hapa hapa duniani”
“Hapana mi sitaki kurudi nyumbani”
“Sasa kwanini hutaki kurudi kwenu?… Kwani hapa ni kwako?” aliniuliza swali ambalo lilinishtua
SEHEMU YA 67
“Sio kwangu”
“Mimi nimekusaidia tu, na sikupaswa kabisa kufanya hivi kwa sababu wewe ni mke wa mtu. Ebu fikiria endapo mumeo akigundua kuwa mimi ndiye nimekusaidia, unataka aseme kuwa mimi ni mchepuko wako??… Ebu rudi kwenu kabla hujanisababishia matatizo”
“Sawa Genson nimekuelewa, pia nisamehe kama nimekukosea”
“Hujanikosea”
“Naomba nirudishe nyumbani”
Tuliacha kupika tulielekea sebuleni, niliwaaga wenyeji kuwa naondoka; aisee walisikitika sana, hasa hasa dada wa Genson hakupenda hata kidogo, alinuna kisa mimi kuondoka.
Nilimuahidi kuwa nitarudi siku nyingine, alifurahi baada ya kusikia hivyo. Mimi na Genson tulitoka nje, tulizama kwenye gari yake kisha alinirudisha nyumbani kwa mume wangu.
Kutokana na mimi kuwa mke wa mtu ilibidi anishushie njiani karibu na nyumbani kisha nitembee kwa miguu. Genson alisimamisha gari, alianza yeye alitoka nje kisha alikuja upande wangu alinifungulia mlango. Baada ya kushuka tulisimama nje ya gari tukitazamana kwaajili ya kuagana. Tulitazamana tukiwa tunatabasam, yeye alinitazama kwa macho ya kawaida tu lakini mimi sikujua namtazama kwa macho gani, nilikuwa mbali kweli kifikra na kihisia. Aliniaga kwa maneno kisha aligeuka akitaka kurudi kwenye gari yake lakini nilimdaka nilimgeuza!!
“Mbona unaondoka hivi hivi Genson”
“Mh! Hivi hivi kivipi?… Kwani kuna kitu ambacho bado sijakufanyia?”
“Ndiyo”
“Kipi? Au unataka pesa ya matumizi?”
“Hapana…. Au basi! Usiku mwema” niliongea kwa upole nikiwa nimenuna. Halafu hata sikujua nimenuna kwa ajili gani, yaani nilinuna tu,
nilimnunia Genson ambaye hakuwa na kosa lolote.
Mwenzangu bado aliganda akinitazama, mimi niligeuka nikitaka kurudi nyumbani. Sasa ile nageuka tu mara nilipigwa mwanga wa tochi kubwa kiasi kwamba niliogopa, nilirudi nyuma nilijibana kwenye kifua cha Genson ambaye aliniacha nitulie kifuani kwake. Sote tulitazama mbele ili tumuone huyo anayetupiga tochi usoni. Baada ya sekunde chache alizima tochi, nilipepesa macho ili nimuone vizuri, weuwee!
Nilishtuka baada ya kugundua kuwa ni mume wangu.
“Kaeni hivyo hivyo…. Hivyo hivyo… Endelea kulala kwenye kifua chake… Shenzi kabisa, nilijua tu una mchepuko… Haya utaniambia nini sasa” alinikoromea akiwa ananikaribia, kutokana na woga ilibidi nikae mbali na Genson
“Sio mchepuko wangu, ni rafiki yangu”
“Rafiki yako, rafiki yako umelala nae, Rafiki yako
mnatazamana kimahaba, rafiki yako anakufungulia mlango wa gari… We mwanamke kumbe ni malaya kiasi hicho? Unatoka nje ya ndoa kwani kipi hukipati kwangu, ina maana mimi sina nguvu za kiume si ndiyo? Sikufikishi kileleni au vipi?….. We kahaba si naongea na wewee” alirusha kofi akitaka kunipiga lakini Genson alizuia, aliushika mkono wa mume wangu ili hasinipige.
“Mwanaume mzima unataka ushindane na mke wako. Hata kama amekukosea si ungeenda kumpigia nyumbani kwako. Pia mimi sio mchepuko wake, nilimsaidia tu kutokana na shida anazopitia. Hakulala na mimi, alilala nyumbani kwa wazazi wangu. Alafu kama ulimfukuza kwako, ulitaka akalale wapi? Ulitaka tusimsaidie? Unadhani sisi wote tuna roho mbaya kama wewe?” Genson aliongea
“Ooh kwahiyo leo hii mimi Nasri nafundishwa na mchepuko wa mke wangu. Wewe nyau unaongea kama nani? Kwani wewe una
mamlaka gani juu ya huyu mwanamke? Wewe ndiye ulinilipia mahari?… Yaani umelala nae alafu unanivimbia mimi? Eti ulimsaidia, nani kasema nahitaji kusaidiwa kumlea mke wangu?… Pia mimi kumfukuza mke wangu hasilale nyumbani kwangu, wewe inakuhusu nini….. Alafu kumbe wewe ndiye huwa unampa mke wangu pesa za matumizi. Mimi simuachii pesa ili ajifunze maisha, wewe unampa ili aniletee kiburi. Kama unajiona una pesa kwanini usiende kusaidia maskini wengine? Kwani anayehitaji msaada ni mke wangu pekee?….
Sikiliza kaka, mke wa mtu sumu! Nitakufanyia kitu kibaya sana, nitakutoa roho”
“Jaribu alafu tuone nani atatolewa roho. Yaani umtese mkeo alafu tuwe tunakuangalia tu, eti tuogope kumsaidia mkeo kwakuwa wewe ndiye umemuoa. Sikiliza nikuambie, kama hutompa pesa, sisi tunaojua thamani yake tutampa. Na ikitokea humpi mapenzi mazuri, sisi wenye mapenzi yetu tutampa. Ukishindwa
kumuhudumia, sisi tutamuhudumia. Na hata kama ukimuacha, tutamchukua”
SEHEMU YA 68
“Fala wewe, kumbe ndo lengo lako eeeh… Kwa taarifa yako simuachi ng’o”
Mume wangu alinishika mkono alinivuta tulielekea nyumbani, Genson nae alizama kwenye gari yake alirudi nyumbani kwake. Nilijua nikifika nyumbani nitapigwa sana lakini hakunipiga wala hakunisema vibaya, aliniuliza kama nishamsaliti nilimwambia sijamsaliti pia nilimuondoa hofu kuhusu Genson, nilimueleza kuwa sikulala kwake bali nililala na dada yake.
Siku hiyo mume wangu alikuwa mpole kweli kweli, aliniandalia chakula, tulioga pamoja, na hata kitandani tulilala tukiwa tumekumbatiana. Asubuhi aliniamsha mapema tulisaidiana kufanya usafi, aliniachia pesa nyingi za matumizi kisha aliniaga alienda kazini.
Siku 3 za mwazo alionyesha utofauti mkubwa, alimuheshimu mama, aliniheshimu mimi na alitujari kwa kila kitu. Binafsi niliamini amebadilika, nilifurahi sana kuona amekuwa bora kama zamani. Siku ya nne ilibidi alale kwangu lakini alilala kwa Rahabu. Siku ya tano kwa Rahabu, na siku zote zilizofuata alikuwa analala kwa Rahabu.
Mambo mengine yote aliyatekeleza lakini unyumba hakunipatia na hakuwa analala na mimi, alikuwa analala na Rahabu. Mwezi mmoja ulikatika mume wangu hakulala kwangu. Na hata akirudi mchana au asubuhi hakuonyesha kunitamani kimapenzi. Nilivumilia sana lakini mwisho nilimuuliza kwanini halali kwangu, alinijibu kuwa ananipumzisha kwakuwa amenitumia sana. Aliniambia kuwa ni zamu ya Rahabu kutumika kwkuwa bado kinda. Sio hivyo tu lakini pia aliniambia haoni umuhimu wa kusex na mimi kwakuwa hata tukifanya itakuwa kazi bure, mtu mwenyewe sizai. Kauli hiyo
iliniuma sana.
Siku hiyo nilijifungia chumbani niliwaza mateso nayopitia, mwanaume hataki kulala na mimi, pesa za matumizi ni hadi tugombane, kila siku matatizo hayaishi, niliona bora niombe TALAKA. Kwanza nilimpigia rafiki yangu Genson, nilimueleza kuhusu wazo langu, aliniambia kama mawazo yangu ni sahihi basi nifanye kilicho sahihi.
Jioni nilimpigia simu mume wangu nilimuambia nina maongezi nae. Alifika nyumbani kisha nilimuomba Talaka, alishangaa, alicheka sana, alikataa kutoa na alisema hata iweje hawezi kunipa talaka.
“Sikiliza mke wangu, najua unaona kama sikupendi kisa tu nalala kwa Rahabu. Mimi kulala na Rahabu haimaanishi sikupendi, ila nafanya vile ili nawewe upumzike… Ebu fikiria nimekutumia kwa miaka mingapi? Hadi hamu inaisha, na ndio maana nakuacha kwanza ili
siku nikipata hisia juu yako tufanye unachokitaka. Siwezi kukupa talaka mwanamke mvumilivu kama wewe, hata Rahabu mwenyewe hawezi kukufikia hata robo! Wewe ni mwanamke bora ambaye anahitajika na kila mwanaume. Na ndio maana yule boya wako anakushauri tuachane ili akurithi… Usije ukamsikiliza, yule hatokuoa, anataka akuchezee tu. Mwisho wa siku naweza nikakuacha alafu usiolewe tena “
“Nani kasema nataka kuolewa na Genson?…
Mimi sijashauriwa na Genson, nimeamua mwenyewe kwa sababu hii ndoa imenishinda”
“Haiwezi kukushinda, wasiwasi wako tu. Kwanza wiki hii yote nitalala na wewe Nina
hamu sana na wewe, nitakupa mapenzi mubashara”
Kabla sijaongea chochote alinirukia alinibeba alinipeleka chumbani, alijilazimisha kutaka kufanya mapenzi na mimi ili tu nimuone kama
SEHEMU YA 69
ananithamini. Kiukweli alinitoka moyoni, sikumpenda tena, nilikuwa namchukia sana, na niliona kama ananicheleweshea mahusiano yangu mengine ambayo yangenipa raha za dunia.
Tukiwa kitandani alihangaika kunjfanyia mautundu na maujuzi lakini sikusisimka, sikuweweseka, sikufurukuta wala sikutetemeka kwa raha zozote. Sikuwa na hisia nae tena.
Hata muda ambao alianza kazi nilipata maumivu tu, sikuinjoy, niliona kama ananibaka tu. Niliamua kumuacha afanye ili amalize shida zake kisha aniache!!
Na hata baada ya kumaliza kufanya nilimtazama usoni kisha nilimuomba Talaka yangu. Nilimueleza kabisa kuwa simpendi.
Alichanganyikiwa, alivurugwa, hakutegemea kama ningefikia hatua hiyo. Aliniomba msamaha kwa mabaya yote aliyonifanyia, aliahidi kunirudishia mali zangu zote ambazo ziliuzwa lakini nilikataa. Nilimwambia kuwa
sitaki mali zake bali nataka uhuru wa maisha yangu, nilihitaji talaka tu lakini aligoma kunipa. Kwa hasira alishuka chini alivaa nguo zake kisha aliondoka.
Sikujali wala nini, tayari nilichafukwa kuanzia kwenye ubongo hadi kwenye miguu!! Kitu pekee ambacho nilikihitaji ni kupewa talaka tu. Nami niliingia bafuni nilioga; nilivaa nguo zangu kisha nilitoka nje, sikujua naelekea wapi ila nilijikuta nimefika msikitini. Niliwakuta masheikh na maostadhi wakiswali. Niliwasubiri na baada ya swala tulikaa nje ya msikiti kwenye mkeka; niliwaeleza mkasa mzima kuhusu ndoa yangu, walisikitika sana. Pia niliwaeleza kuhusu kuomba talaka lakini mume wangu kakataa.
Uzuri ni kwamba mume wangu alikuwa anafahamika. Aliitwa pale pale msikitini, alishtuka kunikuta. Tuliweka kikao, alisomewa mashtaka yake. Baadhi ya mashtaka aliyakubali ila mengine aliyakataa. Mfano kunisaliti, kunizunguka kwa kuninyang’anya mali zangu
kumpa mke mwenzangu hiyo alikubali. Lakini kunipiga na kunilaza njaa hiyo alikataa.
Sikutaka tuweke mjadala mkubwa, mbele ya masheikh nilisisitiza kwamba simpendi tena. Iwe alinikosea au hakunikosea niliomba talaka yangu pale pale msikitini. Viongozi wa dini walinielewa vizuri tu lakini mume wangu hakuwa tayari. Aliniomba msamaha, aliahidi kuwa atatulia. Nae alisisitiza kuwa hawezi kutoa talaka yoyote hata nikienda kwa viongozi wote wa dini, hata nikitumia msaafu, aliwafokea masheikh kisha kwa hasira na dharau aliondoka pale msikitini.
Matendo ambayo aliyaonyesha mbele ya viongozi yalithibitisha kwamba ni mwanaume wa hovyo mwenye tabia mbaya. Masheikh walinipa pole na waliniahidi kwamba watanisaidia kupata haki zangu za msingi kulingana na sheria za dini. Nilirudi nilimkuta kanishikia kiboko, aliniambia talaka hanipi ila nisiingie ndani. Nilicheka kwa dharau kisha
SEHEMU YA 70
niliondoka kwa madoido, ilikuwa ni kama amempiga teke chura. Yaani pale pale niligeuka nyuma, nilitoka nje nilichukua boda nilimwambia anipeleke nyumbani kwa my best friend Genson.
Nilifika nilimkuta akijiandaa kwenda kazini, nae baada ya kuniona alihairisha safari; eti aliniambia tuingie jikoni tupike! Ah ah ah nilicheka kwa raha na furaha. Jamani kupendwa raha hasikuambie mtu. Hata kama alikuwa rafiki yangu lakini alijua kunikosha jamani!
Aliufanya moyo wangu usuuzike.
Alafu muda huo ndani ya mjengo tulikuwa wawili tu, mimi na yeye. Mama na dada yake walielekea kwenye sherehe. Lakini kabla hatujaelekea jikoni mara ghafla mlango ulifunguliwa kwa kasi, aliingia mume wangu bila hodi. Mkononi alishika kiboko kirefu. Moja kwa moja alinivamia alianza kunipiga kila sehemu ya mwili wangu. Nilijua Genson atakuja kunisaidia lakini hakuja kunisaidia, bali alikuwa anarekodi
tukio zima kwa kupitia simu yake.
Mume wangu sio kunipiga na kunitukana tu, bali alinidhalilisha kabisa. Alinifokea kuwa mimi sio mtamu, nina maji mengi machafu, sijui kuoga kama Rahabu, nina magonjwa mengi kiasi kwamba siwezi kushika mimba, na mwisho aliniambia kuwa ataendelea kunitesa.
Pia aliniambia kuwa mimi ni kama dada wa kazi wa nyumba yake alafu Rahabu ndiye mke mkubwa na mke sahihi. Hayo yote Genson aliyarekodi kwenye simu yake kisha alitulia pembeni akiendelea kututazama tu. Mume wangu aliendelea kunipiga, uso wangu ulivimba, ulichubuka na damu zilimwagika. Baada ya kunipiga alinivuta alinitoa nje, alinikalisha kwenye gari yake kisha tuliondoka.
Tulifika nyumbani, mama yangu alishindwa kunitazama mara mbili; kutokana na uchungu alishikilia tumbo lake akihisi maumivu makubwa. Nasri alitufokea kama watoto wadogo, alituambia tuache kulia la sivyo
atatuchalaza fimbo sisi sote yaani mimi na mama. Kutokana na woga ilibidi tuache kulia, mimi aliniambia niingie jikoni nimpikie haraka. Sikuwa na namna, nisingeweza kushindana nae kwa ngumi au maneno, niliingia jikoni nilianza kupika nikiwa nalia kwa kwikwi. Baada ya kupika niliandaa vyakula mezani, nilitaka nisile lakini alinilazimisha alisema wote tunapaswa kula kwa pamoja. Nilirudi mezani nilikaa pembeni ya mama, japo hatukuona ladha ya chakula lakini tulikula hivyo hivyo.
Sasa tukiwa tunaendelea kula mara ghafla mlango ulifunguliwa kwa kasi, aliingia polisi wa kwanza alitunyoshea bastola. Sote tuliacha kula, tulipigwa na butwaa. Yule polisi alinitazama usoni kisha alitikisa kichwa kulia kushoto akionyesha kusikitika. Kabla hatujakaa sawa waliingia polisi wengine wawili wakiwa wameongozana na rafiki yangu kipenzi Genson.
INAENDELEA